Apr 11, 2017
KITABU; Mambo 15 Ya Kujifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha THE POWER OF NOW.
Hiki
ni kitabu kilichoandikwa na ECKHART TOLLE ambacho kinalenga kukutoa kwenye utumwa wa kufikiri na utumwa wa
kuendelea kuteseka kwenye maisha yako, kwa sababu ya kutokujua au kukosa
maarifa sahihi ya kuyatumia sasa.
Watu
wanashindwa sana katika maisha kwa sababu tu hawako makini na yale
wanayoyafanya sasa, wanajikuta ni watu ambao wapo wapo tu, hawafanyi jitihada
yoyote kubwa ya kujifikirisha kufanya mipango yao sasa.
Hebu tuangalie mambo ya msingi tunayoweza kujifunza kupitia kitabu hiki;-
1.
Matatizo mengi ya binadamu chanzo kikubwa yanaanzia kwenye ufahamu na sio sehemu
nyingine yoyote. Ukichunguza utagundua matatizo mengi sana yamesababishwa na
matokeo ya kutokutumia ufahamu kwa usahihi.
2.
Hakuna kitu ambacho kinaweza kukutokea katika maisha yako bila ya wewe kuamua
kuanza sasa. Nguvu kubwa ya mafanikio
inaanzia hapo ulipo kwa kukubali kuchukua hatua mara moja. Huwezi kuwa na
maisha mazuri kesho, kama kwa sasa hufanyi kitu cha maana, msingi mkubwa wa
mafanikio yako unajengwa sana leo. Hivyo wekeza sana leo, upate mafanikio
makubwa kesho.
3.
Uhalisia wa maisha yako unatengenezwa sasa, unapofikiria kwamba kesho utakuwa
na maisha mazuri, maisha hayo hayawezi kuja kama sasa unafanya upuuzi mwingi,
lazima ujue nguvu ya mafanikio yako inatengenezwa sasa. Hata hayo maisha bora
unayoyataka yatakuja kwa kutenda vilivyo bora kwanza sasa.
4. Kila
wakati unatakiwa ujiulize kama hautaweza kufanya mambo yako sasa, utayafanya
lini? Je, unafikiria kwamba utakuwa na muda wa kutosha hapo baadae? Maisha yako
yanatengenezwa sasa na sio kesho, kesho unayoisubiri sana inaweza isifike kwako
na ukashindwa kutenda, chukua hatua mapema.
5.
Kama kuna kitu unakifanya, acha kuweka nguvu zako nyingi kwenye matokeo, badala
yake weka nguvu zako nyingi kwenye hatua unazochukua. Ukiweka nguvu zako nyingi
kwenye matokeo na ukashindwa kuyapata matokeo mapema, itakufanya ushindwe
kufurahia hata kile unachokifanya.
6.
Njia rahisi ya kumjua mtu vizuri ni kutazama ile thamani anayoitoa. Kama unaona
mtu huyo anatoa mawazo mabovu au thamani anayoitoa ipo duni, basi elewa
kinachoingia ndani yake ni kibovu pia.
Mara
nyingi vile vitu tunavyovitoa nje, ni ishara ya sisi jinsi tulivyo ndani yetu.
Sasa jiulize mwenyewe kila siku unatumia jitihada gani, kuwekeza ndani yako na
kuwa bora kila iitwapo leo?
7. Popote
ulipo weka mawazo yako hapo. Chochote unachokifanya pia weka mawazo yako hapo.
Weka nguvu yako ya mawazo kwa kile unachokifanya. Epuka mara moja tabia ya
kufanya kitu hiki halafu mawazo mengine yapo kule. Hutaweza kufanya kwa usanifu
kama mawazo yako yamegawanyika sana, zaidi utajipotezea muda wako bure.
8.
Kuna malengo makubwa ya aina mbili katika maisha yako. kwanza, kuna lengo la
nje na pili kuna lengo la ndani. Haya ni malengo makubwa yanayoongoza maisha
karibu ya watu wote duniani.
Malengo
ya nje ni yale malengo yanayotokana na kuchukua hatua zitakazokuwezesha kufikia
malengo yako uliyojiwekea. Hatua hizi ni rahisi kuziona sana.
Malengo
ya ndani ni yale malengo yanakufanya uchukue hatua ndogo ndogo na za sasa
kuweza kutimiza malengo yako. Kama hutaweza kufanikiwa katika malengo haya ni
ngumu kufanikiwa.
Kwa
hiyo ni lazima ufanikiwe kwanza katika malengo ya ndani, malengo ambayo
unafanya kila siku au sasa, ili ujenge msingi mkubwa wa kufanikiwa kwa kesho au
kwa malengo yako uliyojiwekea.
Watu
wengi wanajisahau katika hili na kujikuta ni watu wa kuwaza malengo makubwa na
kusahau malengo madogo madogo ambayo yangeweza kuwasaidia. Fanikisha malengo
madogo kwanza ya ndani na utafanikiwa.
9. Kuwaza
tu kile unachokifanya peke yake bila kupeleka mawazo sehemu nyingine inakufanya
kufanya jambo hilo kwa usahihi, lakini pia inakutengenezea nguvu nyingi zaidi
za kufanikisha jambo hilo. Hiyo iko hivyo kwa sababu, mawazo yote ya nje
yanayoweza kukukwamisha yanakuwa yanapungua sana, hivyo nguvu zako unajikuta
zinaelekea sana kwa kile unachokifanya na kuleta matokeo sahihi. Hii ndiyo
faida ya NGUVU ZA UZINGATIVU.
10.
Huwezi kuona uzuri au thamani ya kile ulichonacho mpaka mawazo yako kwa muda
mwingi uyaweke kwenye hicho kitu ulichonacho. Kwa mfano, huwezi kuona uzuri wa
kazi yako mpaka mawazo yako yawe kwenye hiyo kazi yako. Pia huwezi kuona uzuri
wa mume au mke wako kama kila siku unakazana tu kuwaangalia watu wengine.
Mara
nyingi ni rahisi tu kuona uzuri kwa mambo yasiyo ya kwetu kwa sababu akili zetu
tunakuwa tumezielekeza huko sana na kusahau kabisa ya kwetu. Siri kubwa ya
kuona thamani ya kile ulichonacho ni kuweka mawazo kwenye kitu hicho
ulichonacho. Kama kuna kitu unataka kuona thamani yake ni rahisi tu, weka
juhudi na mawazo yako hapo.
11. Kila
wakati jifunze kuwa msikilizaji mzuri. Kama kuna kitu mtu anazungumza hebu
msikilize vizuri. Acha kufikiri vitu vingine kama kuna mazungumzo yanaendelea
ya mtu mwingine. Hutaweza kujua mtu huyo anayezungumza ana maanisha nini? zaidi
utaanza tena kuuliza kwa sababu ya kutokusikiliza kwako.
12.
Unatakiwa uwe na utulivu mkubwa sana ndani yako wa kifikira ndio uwe na utulivu
wa nje. Kama ndani yako hauna utulivu mkubwa hata kwa nje utaonekana
haujatulia. Jitahidi sana kutuliza fikra zako ili kupata utulivu pia wa nje
utakaokusaidia kufanikiwa.
13.
Upendo wa kweli katika maisha hauchagui. Kama lilivyojua ambavyo halina ubaguzi
wowote pia upendo wa kweli katika maisha hauchagui. Upendo huu wa kweli una
mulika popote bila kuchagua. Hili ndilo pendo ambalo analo Mungu wetu. Ni
upendo ambao hauna ubaguzi wowote.
14.
Mbinu mojawapo bora ya kuondokana na mawazo hasi ni kuweka mawazo yako katika
eneo moja. Ikiwa utakuwa una uwezo wa kuweka mawazo yako eneo moja na kwa muda
mrefu basi utafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuondokana na mawazo mengi
sana hasi ambayo yangekuzuia kwa namna fulani kufanikiwa.
15. Kama hali yako ya nje ni
mbovu na huipendi, anza kubadilisha hali ya ndani yako sasa. Mabadiliko yote,
yanaanzia ndani mwako kwanza na sio sehemu nyingine yoyote ile. Anza
kubadilisha hali hiyo sasa.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 628 929 816, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.