Apr 7, 2017
Dalili Zinazoonyesha Kwamba Hutaweza Kutimiza Ndoto Zako.
Najua kuna wakati unakuwa unajiwekea malengo yako
vizuri tu, lakini unakuwa unashangaa kwa nini pamoja na kujiwekea malengo hayo
bado tu ndoto zako fulani hazitimii?
Naamini umeshawahi kukutana na kitu kama hiki na
kimekuwa kikikusumbua sana na kushindwa kujua ni nini ambacho huwa kinatokea
hadi kuna ndoto zako nyingine hazitimii.
Kupitia makala haya nataka nikupe jibu litakalokusaidia
kujua dalili zinazoonyesha kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako. Kama una dalili hizo ujue kabisa ndoto zako
haziwezi kufanikiwa hata ufanyaje.
Hebu sasa twende pamoja kwenye somo letu tujifunze dalili
zinazoonyesha kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako.
1. Kusubiri
wengine wakubali ndoto yako.
Kati ya kosa kubwa ambalo hutakiwi kulifanya wakati
unajiwekea ndoto zako ni kule wewe kuendelea kusubiri wengine wakusifie au
wakubali kwamba eti ndoto yako ni nzuri na itatimia. Huhitaji kitu cha namna
hiyo hata mara moja.
Unachotakiwa kufanya ni kwa wewe kufanya tu. Acha
kusubiri mtu fulani akwambie ndoto yako inawezekana. Taarifa ya kujimbia kwamba
utafakisha hili au lile unatakiwa ujiambie wewe kwanza.
Kwa hiyo dalili ya kwanza na ya wazi kabisa ambayo
itasaidia kutuonyesha kwamba ndoto yako haiwezi kutimia ni kule wewe kusubiria
wengine wakwambie ndoto yako inawezekana. Kama unasubiria uambiwe hivyo,
unajichelewesha hutaweza kufanikisha kitu.
Acha kusubiri sana, tekeleza ndoto yako mara moja. |
2. Kutoipa
ndoto yako vipaumbele.
Ni rahisi sana kusema kwamba nina ndoto ya kufanya
kitu fulani au nataka kufanikisha jambo hili mwaka huu. Hata hivyo ukiwaangalia
watu wengi wanaosema hivyo, ndoto zao hizo hawazipi sana vipaumbele.
Utakuta ni watu wa kusema tu, lakini hawachukui
hata zile hatua ndogo ndogo za kufikia ndoto zao. Kiuhalisa, kama ndoto yako
hauipi vipaumbele, yaani huchukui hatua hata ndogo ndogo, hutaweza kufanikisha
ndoto yako hiyo, zaidi utajidanganya.
3. Kutoipa
ndoto yako hali ya uzingativu.
Kama unataka kujua ndoto yako itafanikiwa au haitafanikiwa
angalia jinsi unavyoipa nguvu ya uzingativu. Je, unaizingatia ndoto yako kila
wakati? Ndoto hiyo inakunyima usingizi? Kama hakuna uzingativu hauwezi
kuifanikisha.
Wale wanaoshindwa katika ndoto zao, wengi
wanashindwa kuzizingatia ndoto zao, yaani wanashindwa kuwa na ile tunasema ‘focus’, kuweka mawazo ya aina moja
kuelekea kwenye ndoto zao.
4. Kutokuwa
na mahusiano na watu sahihi.
Ndoto yako haiwezi kutumia kama upo kwenye
mazingira mengi na watu ambao sio sahihi kwako. Inatakiwa ujue watu
wanaokuzunguka ni akina nani? Je, watu hao wana msaada katika kutimiza ndoto
zangu au hapana.
Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya
jambo kama hili la kutokuwa na mahusiano sahihi. Wengi ni watu ambao wana mahusiano
mabovu sana, hali ambayo huweza kupelekea mipango yao hiyo isiweze hata
kutimia.
Hizo ndizo dalili muhimu ambazo zinaweza kuonyesha
kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako. Kama una dalili hizo na unataka ndoto zako
zitimie, hakikisha;-
Kwanza, unafanya kile unachokiamini kuelekea kwenye
ndoto zako bila kusubiri mtu mwingine akwambie jambo hili linawezekana. Jiamini
kwamba unaweza kutimiza ndoto zako na uiamini pia ndoto yako.
Pili, hakikisha unaipa ndoto yako vipaumbele. Jua
kitu cha kufanya kila siku kitakachokusogeza kwenye ndoto yako. Usiache siku ikapita
bila kufanya kitu cha kukupeleka kwenye ndoto zako.
Tatu, hakikisha unajenga tabia ya uzingativu kwenye
ndoto yako. Mawazo na akili zako kila wakati unatakiwa uzielekeze kwenye ndoto
zako na kila kitu kitatimia kwako.
Mwisho, Jenga mahusiano sahihi na watu
watakaokusaidia kutimiza ndoto zako. Hapa kwa kifupi tengeneza ‘timu’ itakayokusaidia kufanikiwa.
Endelea kujifunza kupitia
dirayamafanikio.blogspot.com kila siku na washirikishe wengine pia waweze
kujifunza kupitia mtandao huu.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio
makubwa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Mshauri wa
mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano;
+255 628 929 816, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.