Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, February 29, 2016

Mbinu Za Kukabiliana Na Ushindani Katika Biashara.

No comments :
Mara nyingi wote tunajua wakati mwingine ili kuendesha biashara hadi ikakuletea mafanikio makubwa, inahitaji uvumilivu na kujituma sana hasa kutokana na changamoto nyingi zinazojitokeza kila siku kwenye biashara tunazozifanya.

Bila shaka utakubaliana nami moja ya changamoto kubwa zinazojitokeza katika kuendesha biashara iwe ndogo au kubwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya kutosha, mfumko wa bei, ushindani wa kibiashara na changamoto nyinginezo, ambapo usipokuwa makini unaweza ukakwama.

Leo katika makala haya tutaangalia moja ya changamoto hizo kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi sana. Changamoto hii si nyingine ni changamoto ya upinzani au ushindani unaojitokeza kwa kasi katika biashara kila kukicha.

Naamini hakuna asiyejua kwamba, kwa sasa ushindani kibiashara uko juu. Kila siku kumekuwa na biashara nyingi zinazoanzishwa. Na imekuwa si kitu cha ajabu kujikuta watu ishirini mkifanya biashara ya aina moja na kwenye mtaa mmoja.

Kutokana na ushindani mkubwa, wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanikiwa na wengine kukwama kwa sababu ya kushindwa na nguvu ya ushindani. Lakini kwa kusoma makala haya, itakusaidia kujua mbinu za kukabiliana na ushindani kwenye biashara yako. Karibu sana kujifunza.

1. Toa bidhaa bora.

Ili uweze kumudu kukabiliana na washindani wako vizuri, njia bora ya kukabiliana nao ni kutoa bidhaa bora. Hakikisha wateja wako wanaridhika kabisa na kile unacho wahudumia. Isije ikatokea au ukasikia eti wateja wako wanalalamika kwa kukosa bidhaa bora. Kama itatokea hivyo, jirekebishe na toa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Kwa mfano wewe una duka la kuuza vifaa vya umeme. Jitahidi dukani kwako uwauzie wateja wako vifaa hivyo 'orijino' na sio 'feki'. Hiyo itakupa sifa kwanza na pia itakusaidia kuwashinda kirahisi wale wanaotoa bidhaa zisizofaa ambazo zikitumika kwa muda mfupi zimekufa. Kumbuka hili, kila wakati, kila siku,  kutoa bidhaa bora ni njia nzuri ya kuwashinda washindani wako.

KUWA MBUNIFU
 2. Angalia udhaifu wa washindani wako.

Hata kama washindani wako unaona wana bidhaa bora sana pengine hata kuliko wewe hilo lisikutishe sana. Kitu cha kufanya wewe, boresha bidhaa zako na  kisha nenda hatua ya ziada kwa kujifunza udhaifu wao. Ukishagundua udhaifu wao ni nini, utumie udhaifu huo kukusaidia kukufanikisha.

Tuchukulie kwa mfano wote mna mgahawa na mnatoa huduma ya chakula. Halafu ukaja kugundua jirani yako na ambaye ni mshindani wako, kwanza hawakaribishi wateja vizuri na pia  wateja wanalalamika chakula ni kidogo. Kitu cha kufanya wewe, ni kuhakikisha unawakaribisha wateja wako vizuri sana na ikiwezekana kutoa chakula kingi kidogo ili kufanya wateja wako wasilalamike kama yeye. Kwa kufanya hivyo utaweza kujipatia  wateja wengi hata waliokuwa kwa mshindani wako.

3. Kuwa mbunifu.

Mpaka hapo umeshajifunza ili kuwashinda washindani wako ni lazima utoe bidhaa bora na kuangalia udhaifu wao. Lakini hiyo haitoshi, pia unalazimika kuwa mbunifu zaidi kwa wateja wako. Ni muhimu kujua wanataka nini kwa wakati, ni kitu gani ambacho ukiongeza watavutika au ni huduma ipi ambayo wataitaka zaidi ambayo kwa sasa huna. Huo ni ubunifu unaotakiwa ili kukabiliana na ushindani hasa kwa kipindi cha sasa.

Kwa biashara yoyote inayoendeshwa kwa ubunifu ni rahisi kushinda ushindani na kusonga mbele. Lakini kama unaendesha biashara kimazoea kufanikiwa itakuwa ngumu. Tafuta kitu ambacho huna, kiongeze kwenye biashara yako. Kama una biashara ya saluni na ukagundua pengine ukiweka televisheni huku ukionyesha baadhi ya mipira ya ulaya itavuta wateja, basi fanya hivyo ili upate wateja  kutosha. Kama nilivyosema ubunifu katika biashara yoyote unalipa sana na pia ni njia sahihi ya kukabiliana na ushindani.

4.  Toa punguzo la bei.

Biashara yako inaweza ikawa ina mvuto mkubwa sana ikiwa kuna wakati fulani kunakuwa kuna punguzo maalumu la bei. Punguzo hili unaweza ukalifanya katika kipindi maalumu mfano cha sikukuu au ukaamua kushusha bei bidhaa fulani fulani hivi ili kuweza kuwavuta wateja na kuushinda upinzani.

Kwa mfano unaweza ukawa unafanya biashara ya kuuza simu. Ni vyema kwa baadhi ya simu ukashusha bei na kuwatangazia wateja wako ofa hiyo ambayo uwe na uhakika wataipenda. Kwa kutoa ofa hizo siku hadi siku zitaifanya biashara yako ing'ae na kuzidi kwenda juu na kuushinda upinzani.

 5. Toa huduma bora kwa wateja wako.

Tatizo kubwa walilonalo wafanyabiashara wengi hasa wadogo ni kule kushindwa kutoa huduma bora. Wamekuwa ni wafanyabiashara wa kufanya biashara, bora liende na kusahau kutoa huduma bora. Kwa vyovyote vile unaposhindwa kutoa huduma bora unajiwekea mazingira ya kushindwa kukabiliana na ushindani. Huduma bora inahitajika sana ili kuifanye biashara yako iende na wakati na kuwashinda washindani wako.

Katika kutoa huduma bora jifunze kuwafurahia wateja wako, jifunze kuwasikiliza na pia jifunze kuomba msamaha kama kuna kosa linaweza likawa limetokea la kibiashara. Hiyo ni mifano michache ya kutoa huduma bora lakini lilokubwa kwako ni kuhakikisha kwa namna yoyote ile unatoa huduma bora kwa mteja wako itakayomfanya afurahie huduma hiyo na kesho kurudi kwako tena. Bila kufanya hivyo, utapoteza wateja na watakimbilia kule zinakotolewa huduma bora.

6. Toa matangazo ya biashara yako.

Kwa kawaida hakuna biashara ambayo inaweza ikajiendesha kwa mafanikio makubwa na kushinda ushindani bila kuwa na matangazo. Biashara yako inategemea sana matangazo kuliko unavyofikiri. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu biashara yako inatakiwa kujulikana kila eneo ilina kuwavutia wateja wengi.

Tunapozungumzia matangazo kama huna mtaji wa kutosha si lazima yawe ya redioni au kwenye televisheni. Unaweza ukatengeneza vipeperushi kwa gharama ya kawaida au unaweza ukatumia wateja wako hao hao kuitangaza biashara yako na kupanua soko kwa kiasi kikubwa na kuwashinda wapinzani wako.

Kwa  kufanya mambo haya, yatakusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ushindani mkubwa unaojitokeza katika biashara yako.

Tunakutakia kila la kheri katika biashara yako na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.

Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,

Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
No comments :

Post a Comment