Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, February 22, 2016

Sababu Zinazoweza Kufanya Biashara Yako Ikafa, Hata Kama Ina Mtaji Mkubwa.

No comments :
Mara nyingi wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mara kwanza huamini sana mtaji ndio kila kitu. Kwa imani hiyo, hujikuta mara baada ya kuingia kwenye biashara wanakuwa hawaweki nguvu nyingi katika maeneo mengine muhimu ili kuboresha biashara zao. Na matokeo yake hupelekea biashara hizo kuanza kufa huku zikiwa zina mtaji mkubwa kabisa.
Kinaweza kuonekana ni kitu cha kushangaza lakini huo ndio ukweli. Unajua ni kwa nini ? Ni kwa sababu waliaminishwa toka siku nyingi kwamba ukiwa na mtaji mkubwa basi, kila kitu kimekwisha. Lakini, leo katika makala yetu tutaangalia sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa.  
Kwa kupitia makala haya itakuonyesha na kukupa ukweli wa wazi  kwamba, mtaji mkubwa peke yake sio ‘gerentii’ ya kukufanya wewe ukafanikiwa kibiashara.  Yapo mambo mengine ya ziada ambayo unatakiwa kuyazingatia na kuyatilia mkazo kila siku, ili biashara yako iweze kukupa yale matunda unayoyataka.
Kumbuka haijalishi biashara yako ina mtaji kiasi gani, lakini elewa ukweli huu inaweza ikafa usipozingatia mambo haya ya msingi. Sasa nataka twende pamoja kujifunza na kujua mambo au sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa vipi.  Karibu sana tujifunze pamoja.
1. Kukosa usimamizi imara.
Kama unaona unataka kuanzisha biashara yako, halafu ukagundua huna usimamizi imara ni bora ukaachana na hiyo biashara. Na kama ungekuja kwangu leo na kunieleza hali hiyo ilivyo,  ningekushauri hivi ‘ Chukua pesa hizo kisha nenda mjini, katafute sehemu wanakochoma nyama nzuri kula pesa yote usibakize hata  Shilingi mia moja.’
Sikutanii. Kwa nini nakwambia hivyo, kufanya biashara yako huku ukiwa huna usimamizi wa kutosha ni sawa na kupoteza pesa hizo. Tena unazipoteza bila kufaidi hata tone. Hapa unaona hata kama ungekuwa na mtaji mkubwa vipi, kama huna usimamizi ni lazima biashara hiyo itakufa tu, hakuna ubishi.

KUKOSA USIMAMIZI BORA, NI SUMU YA BIASHARA.
2. Kukosa elimu ya biashara.
Najua umeshawahi kusikia sana fulani alipata mkopo wa  benki milioni sitini, lakini biashara zake zimekufa. Unajua chanzo chake kimojawapo ni nini? Ni kukosa elimu ya biashara. Wengi wanapokosa elimu hii huwekeza kiholela sana matokeo yake kupoteza pesa nyingi bila sababu ikiwa pamoja na mtaji.
Kwa hiyo ili kufanikiwa kibiashara ni lazima wewe kuwa na elimu ya kutosha kibiashara. Pengine unataka kujiuliza nitaipata wapi sasa? Sikiliza huhitaji gharama kubwa sana kuipata. Unaweza kujifunza kupitia semina, huwezi hilo unaweza kujifunza kupitia mitandao ya kuhamasisha au ukanunua vitabu vinavyohusu biashara ukajifunza polepole. Lakini kikubwa usiikose elimu hii, vinginevyo utapoteza mengi ikiwa pamoja na biashara yako.
3. Matumizi mabaya pesa.
Sio kwa sababu biashara yako ina mtaji mkubwa na inaingiza pesa nyingi kwa siku, basi na matumizi yako yanakuwa yako juu bila sababu. Kama unafanya hivyo kwenye biashara yako nikupe tu uhakika huu, huwezi kufika mbali. Ni lazima uwe na mpangilio mzuri wa matumizi yako ya pesa ili kuifanya biashara yako ikazidi kuendelea.
Acha kujidanganya kwa kuendelea kutumia pesa vibaya, utazipoteza zote mpaka utashanga. Kikubwa unajua jinsi huo mtaji ulivyoupata. Kama ni hivyo kwa nini uutumie hovyo? Kuwa makini na pesa zako. Tofauti na hapo biashara yako itakufa tu hata kama sio leo, lakini lazima itakufa.
4. Kukosa ubunifu.
Ili uweze kukabiliana na ushindani, ubunifu ni muhimu sana katika biashara yako. Bila kuwa mbunifu huwezi kufanikiwa katika hiyo biashara kutokana na mazingira ya ushindani mkubwa tulionao kwa sasa. Kwa hiyo ni lazima kuwa mbunifu na kuifanya biashara yako ikaonekana ya tofauti na kukupa wateja wa kutosha.
Wengi wanaoshindwa kwenye biashara ni wale walioingia kwa kiburi cha mtaji mkubwa na kusahau ubunifu. Haijalishi unafanya biashara ndogo au kubwa weka ubunifu. Kila wakati tafuta ni kitu gani biashara yako inakosa, kisha kiboreshe zaidi. Jitahidi sana kuweka ubunifu ili kuifanya biashara yako iwe hai siku zote, vinginevyo utaiua.  
5. Kukosa nidhamu.
Kama unaendesha biashara yako na ukakosa nidhamu ya kuiendesha biashara hiyo, elewa kabisa utakuwa na mchango mkubwa sana wa kuiua. Nidhamu ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote na sio biashara tu peke yake. Jaribu kuangalia watu wote wenye nidhamu ya kazi mafanikio yao yakoje? Bila shaka ni makubwa.
Biashara nyingi sana zinazokufa huku zikiwa na mtaji mkubwa mara nyingi hukosa nidhamu. Tuchukulie una duka la reja reja, huwezi kufanikiwa ikiwa unafungua na kufunga unavyotaka. Ni lazima uwe una nidhamu ya muda, nidhamu ya kuwajali wateja au nidhamu ya kauli nzuri. Kwa kukosa nidhamu hizi biashara itakufa tu hata iwe kubwa vipi.
 6. Kukosa wateja.
Kati ya kiungo muhimu sana kwenye biashara yako ni wateja. Bila wateja hakuna biashara inayoweza kufanyika. Sasa kama utakuwa huna wateja hiyo inamaanisha biashara yako kwa vyovyote vile itaenda kufa hata ufanye nini. Maana hao ndio wawezeshaji wakubwa kwenye biashara yako kuendelea.
Sasa huwa zipo sababu zinazopelekea biashara hii ikakosa wateja na nyingine ikawa na watej wengi. Hivyo ni vyema ukazijua sababu hizo ili zikusaidie kuweza kujenga biashara ya uhakika na yenye mafanikio makubwa.
7. Kukosa vipaumbele.
Biashara yoyote iwe inanza au inaendelea ni lazima iwe na vipaumbele vya msingi ambavyo vinatakiwa vifuatwe kila siku. Kama kipaumbele chako kimojawapo ni kutaka kukuza mtaji ni vyema ukawa makini kuhakikisha hilo linatimia na kutekelezeka kwa haraka sana.
Lakini kama pia vipaumbele vyako ni kuhakikisha unadumisha mahusianao mazuri na wateja wako, pia ni bora ukatekeleza. Unapokosa vipaumbele hata vile unavyoviona ni vidogo ni rahisi sana kwa biashara yako kuweza kufa na kushindwa kuendelea hata kama ina mtaji wa kutosha. Kwa sababu hapa tunasema biashara inakuwa inakosa dira maalumu.
8. Kukosa mgawanyo wa majukumu.
Pia biashara inaweza ikafa hata kama ina mtaji wake mkubwa, ikiwa itakosa mgawanyo wa majukumu.  Ni lazima biashara iwe na mgawanyo wa majukumu ili iweze kusonga mbele. Kama unaona unafanya biashara huku kila kitu umeshikilia wewe na hakuna wa kukusidia elewa upo kwenye hali mbaya.
Ni lazima utafute watu wa kukusaidia hata kama pale haupo mambo yaweze kwenda sawa kabisa. Siri mojawapo kubwa ya kufikiwa mafanikio makubwa kwenye biashara yako ni kutengeneza mgawanyo mzuri wa majukumu kwa wasaidizi wako. Kushindwa kufanya hivyo ni lazima utaua biashara yako.

Kama nilivyoanza kwa kusema zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa. Kwa leo naomba niishie hapo. Tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine nzuri ya biashara. Kumbuka kuchukua hatua. KILA LA KHERI.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,

No comments :

Post a Comment