Jan 14, 2018
HEKIMA ZA MAISHA NA MAFANIKIO; Anayekata Poli, Moshi Utaonyesha Tu.
Ni wakati
mwema na siku njema ambayo tunakutana tena katika jamvi letu pana la kuweza
kujifunza hekima za maisha na mafanikio. Hapa kama ambavyo nimekua nikukueleza
tunakuwa tunajifunza misemo ambayo inabadilisha maisha yetu.
Misemo
hii ni ipi kama wewe ni mgeni hapa, hii ni misemo ambayo ilitolewa na babu zetu
enzi hizo ambazo wewe hukuwepo lakini ina maana sana katika kujifunza kwetu,
ndio maana tunaiita hekima za maisha na
mafanikio.
Kwa upande
wangu kama upo mbali nakualika, sogea karibu jamvini, sogea na kalamu yako ili
tuweze kujifunza hekima za maisha na mafanikio kama ilivyo ada yetu kwa siku
kama ya leo. Karibu sana tujifunze pamoja;-
1. Anayekata poli, moshi utaonyesha tu.
Kwa kawaida
kama mtu yuko polini na amekazana kukata msitu au poli, haina haja ya kusema
sana kwamba mtu huyo anafanya kitu gani, hata kama hujaambiwa yaani uko mbali
utakachosikia ni sauti ya shoka na moshi unaofuka baada ya miti kuchomwa.
Kupitia
hekima hii ya mafanikio inatupa fundisho kwamba; kama kuna kazi inafanyika
hauna haja ya kuiongelea sana kazi yako hiyo, mafanikio yenyewe yataonekana tu
kwa nje bila ya wasiwasi. Hio ni sawa na kupiga kazi kimya kimya lakini matokeo
tutayaona.
Kwa mantiki
hiyo iko hivi, kama kuna kazi unaifanya, ifanye tena kwa nguvu zote, usitake
kuwaonyesha watu kwamba ni matokeo yapi yatatokea, hayo matokeo yatatoka tu
hata kama usiposema kwani tunaambiwa mkata poli moshi utaonyesha tu na hakuna
ubishi.
Mtu anaweza
asione unachofanya, hilo lisikusumbue wala kukuumiza akili, wewe piga kazi,
fanya unachofanya kwa uhakika, unaweza ukawa kwenye hatua za kama kupanda mbegu
tu hakuna kinachoonekana, lakini matokeo yatakuja.
Itafika
muda au wakati watu wataanza kuona moshi, na hapo ndio watagundua alaa kumbe
kulikuwa kuna mtu yupo msituni anakata poli. Na kwa bahat nzuri moshi huo
utaonekana mpaka mbali, hivyo piga kazi usife moyo, moshi utaonekana tu wa
mafanikio yako.
2. Yule anaemulika nyoka usiku na tochi,
huanzia miguuni mwake.
Ni kawaida
sana usiku unapaoambiwa kwamba kuna nyoka hapo hatua ya kwanza ambayo unachukua
kama una tochi ni kuanza kumulika miguuni mwako. Hilo wewe unaweza kulifanya
hivyo na mwingine anaweza kulifanya hivyo pia.
Hekima
hii ina maana gani kwetu, ni kwamba, ni vyema kabla hujatatua changamoto za
wengine au kabla hujaangalia matatizo ya wengine walionayo na kuanza kuwalaumu pengine
ni bora ukaanza kujiangalia kwanza wewe, je, uko sawa.
Ni rahisi
kuwakosoa wengine kumbe wewe ndio umeisha kabisa na ndio unatakiwa kukosolewa
wa kwanza. Hili ni onyo linalotutaka kushugulika kwanza na sisi na kujijua
vizuri na kisha kutoa msaada kwa wengine.
Unaweza
ukawa unamulika nyoka mbele na matokeo yake ukang’atwa wewe na ndivyo ilivyo
kwenye maisha unaweza ukawa unashugulika na wengine na kujisau wewe. Kitu cha
kwanza cha kuelewa hapa usijisahau anza kushughulika na wewe kwanza.
Unapogundua
umemaliza kushughulika na wewe, kisha wafate wengine kuwapa unachotaka kuwapa
ndio maana tunaambiwa yule anayemulika nyoka huanzia miguuni mwake na si vinginevyo, lazima uanzie pale ulipo.
Mpaka
hapo kwenye hekima za maisha na mafanikio sina la ziada, tukutane wiki lijalo
na wakati kama huu tena, tchaooo.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO
YAIMARIKE,
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713
048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.