Jan 31, 2017
Kilimo Cha Maharage Ya Njano.
Kilimo cha maharage ni rahisi na
kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio
mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani
kwako na kuchukua mzigo.
Ekari moja ya maharage ya njano kwa
maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo
unalolimia.
Shamba la maharage kama unalima kwa
kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja
tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi
minne.
Upandaji wa Maharage
1.Mbegu.
Upandaji wa maharage unatakiwa
ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya
kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage
yasiharibikie shambani.
Maji mengi yaliyotuama na ukame
siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.
Kuna aina nyingi za maharage ambazo
zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder)
ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa
wakulima ambazo huhimili
baadhi ya magonjwa na wadudu.
Inashauriwa kupanda maharage katika
umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea
kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza
kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.
Kama mbegu moja moja katika kila
shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na
idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo
idadi yake ni nusu ya
maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 =
ekari 2.471.
2.Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka
kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage
huhitaji madini ya ‘phosphorous’
na ‘potassium’ ambayo hupatikana
kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo
na mabaki ya mimea.
Ni muhimu kufahamu udongo ambao
unatarajia kupanda mimea yako ili
kutathmini viwango vya madini
yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.
Zaidi ya yote ni vizuri kutumia
mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza
kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai
(nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen.
Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye
udongo.
3.Magugu.
Inashauriwa kupalilia mimea kabla
haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga
mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza
kusababisha magonjwa kwa mmea.
Inashauriwa kupanda mimea kwa
kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza
kushambulia
mimea.
4.Wadudu na magonjwa.
Maharage hushambuliwa na wadudu na
magonjwa. Miongoni mwa njia
za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu
ni kuhakikisha kuwa mimea
ipo katika hali nzuri (imepaliliwa,
nafasi ya kutosha na haijaharibika).
Pia kubadilisha aina ya mimea
inayopandwa kwenye shamba moja mara
kwa mara husaidia kupunguza uwezekano
wa wadudu kuongezeka.
Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi
(African Ballworm) huweza
kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au
vitunguu saumu.
Maji ya muarobaini ni dawa nzuri
sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa
binadamu.
5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe
kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda.
Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka
kinapokuwa kimefikiwa.
Kwa mfano asilimia 80 ya maharage
yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine
kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.
Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na
kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea
na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.
Baada ya kukauka hadi kufikia
angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye
chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea
kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha
kuyafunika tena.
6. Kilimo mchanganyiko.
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda
maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani
husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye
kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.
Maharage yanaweza yakapandwa katikati
ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa
kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous)
kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata
virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi
weupe.
Jan 30, 2017
Mambo Ya Lazima Kuwa Nayo Katika Safari Ya Mafanikio.
Katika safari yoyote ya mafanikio huwa ipo
misingi na mambo ya lazima ambayo ni lazima uyajue ili kufanikiwa. Kwa kuyajua
mambo hayo yatakupa dira na mwelekeo mzuri wa kufikia mafanikio makubwa.
Ni kweli unaweza ukawa una malengo mazuri
uliyojiwekea, lakini bila kuyajua mambo hayo na kuyafanyia kazi itakuwa ni
ngumu sana kufikia mafanikio yako. Watu wengi wenye mafanikio wanayajua mambo
haya na kuyafanyia kazi mara kwa mara. Je, unajua ni mambo gani ambayo ni ya
lazima sana katika safari yako ya mafanikio?
1. Hamasa.
Ili uweze kufanikiwa ni lazima kwanza uwe na
hamasa kubwa ya kufikia mafanikio hayo. Wengi huwa wanashindwa kufanikiwa kwa
sababu ya kukosa hamasa. Unapokuwa unashindwa kuwa na hamasa inakuwa ni ngumu
kufikia mafanikio yoyote kwa sababu karibu kila kitu utakifanya kizembe au
kivivu ilimradi ukikamilishe.
Kitu kinachokufanya uongeze juhudi kwa kile
unachokifanya sasa ni kwa sababu una hamasa ya kutaka kufanikiwa. Kushindwa kwako
kutaanza mara moja ikiwa utaanza kukosa hamasa hiyo. Huu ni ukweli ambao ni
lazima uujue ili kuweza kufanikiwa, vinginevyo hakuna utakachoweza
kukifanikisha. Kila kitu kitakuwa kigumu kwako.
2.
Uzingativu.
Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani lakini
ikiwa ndani yako utakosa uzingativu, kuyafikia mafanikio hayo itabaki kuwa
ndoto za mchana. Watu wote ambao huwa wanafanikiwa katika mambo yao ni watu wa
kuzingatia sana. Huwa ni watu ambao hawana papara, wakianzisha jambo
hulifatilia mpaka kulifanikisha.
Mara nyingi unapoweka nguvu ya uzingativu
katika jambo moja, huwa zinaleta matokeo makubwa na kuyashangaza. Hakuna
kinachoshindikana katika nguvu hizi za uzingativu zinapotumika. Hiki ni kitu ambacho
unatakiwa kukiweka kwenye akili yako na kukifanyia kazi. Na hili ni jambo la
lazima sana katika safari yako ya mafanikio, bila hivyo huwezi kufanikiwa.
3.
Kujiamini.
Msingi mkubwa wa mafanikio upo kwenye
kujiamini. Ikiwa wewe utakuwa mtu ambaye unajitilia shaka na hujiamini katika
mambo yako ukweli wa mambo uko wazi hata ufanyaje huwezi kufanikiwa. Kama
unabisha hebu angalia mambo ambayo hukuwahi kufanikiwa, utagundua mengi
hukuweza kujiamini sana.
Kwa hiyo mpaka hapo utagundua kwamba kujiamini
ni jambo la lazima sana katika safari ya mafanikio yako. Mafanikio yoyote yale
yanahitaji kwanza wewe uanze kujiamini binafsi kuwa utafanikiwa. Kwa kadri
unavyozidi kujiamini sana katika maisha yako, ndivyo ambavyo utajikuta
ukifanikisha mengi.
4.
Kufanya kazi kwa bidii.
Ni kweli unaweza ukawa una hamasa kubwa, una
nguvu ya uzingativu na unajiamini vya kutosha, lakini kama hufanyi kazi kwa
bidii huwezi kufanikiwa. Kazi ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote
unayoyahitaji. Ili uweze kufanikiwa ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa
bidii zote. Hapo ndipo utaanza kuyaona mafanikio yako.
Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watu wa
kujituma sana. Bila kufanya kazi kwa bidii, elewa kabisa mipango na malengo
yako mengi yataishia njiani. Kwa hiyo kama ni kazi weka juhudi zako zote mpaka
ikuletee mafanikio. Kwa sababu unakuwa umeweka nguvu zako nyingi, hata ikitokea
umeshindwa hutajilaumu sana.
Kwa mambo hayo manne ni silaha kubwa sana ya
mafanikio kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufikia mafanikio makubwa. Kitu kikubwa
naomba ufanyie kazi mambo hayo ili yaweze kubadili maisha yako na ya wengine
wanaokuzunguka. Kila kitu kinawezekana ukiamua, hivyo amua sasa upate
kufanikiwa.
Nikutakie kila la kheri katika safari yako ya
mafanikio . Kumbuka tupo pamoja.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI
NGWANGWALU,
Jan 27, 2017
Kama Unaogopa Kufanya Kitu Hiki, Sahau Kuhusu Mafanikio Katika Maisha Yako Yote.
Fikiria kila
unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe katika maisha yako,
halafu uone ukweli huu kama kweli nawe ni mmoja kati ya watu
wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na pengine tu wewe
hujijui. Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini mara kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa
kufanya jambo ambalo lingeweza kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio
mkubwa? Hili ndilo tatizo walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya
mabadiliko kwa namna moja au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao
wenyewe kuna wakati huwa wanaogopa pia.
Kimaumbile, kila
binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya mabadiliko inapozidi kuwa kubwa
na kukuzuia kufanya mambo ya maana kwako, hofu hii sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia
wewe kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya mabadiliko
Fulani katika maisha yako, lakini
umekuwa ukijikuta ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani?
Ni mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na hofu
nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati mwingine bila
sababu ya msingi.
Wengi wetu kutokana na
kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa sababu ambazo hata hazina mashiko
zinazosababisha wao washindwe kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta
mtu anakwambia hawezi kufanya biashara
ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu
ambayo amekuwa akiitoa kwa muda mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana
mtaji tu. Kama uko hivi una hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza
kuvifanyana , tambua kuwa kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako
anayekuzuia kufanikiwa. Na unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa
ili ufanikiwe, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote.
Tatizo kubwa
utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa kufanya mabadiliko ni
lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo
ya kutaka kufanikiwa leoleo hata kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa
wana hofu hii kubwa ya mabadiliko ndani mwao, unaweza kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli huu ulio
wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini subira ndani mwao,
bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao unaanza leo biashara na wiki
ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa.
Hivi ndivyo walivyo
watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini katika miujiza, sio katika wao
wenyewe kutenda na kuona matokeo. Hebu jaribu
kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu wanaofikiria
sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya karibu sana na hawataki
shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila kitu kimalizike leo. Sijui kesho
watafanya kitu gani? Ukimwambia mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya
miaka 10 kutoka sasa kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu
zimuume. Anataka leo hata kama ni kwa miujiza.
Ndiyo maana wengi kati
ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka
malengo siyo sehemu ya maisha yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira,
mtu anayeamini kwamba maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni
kulalamika na kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila
kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya kazi,
wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine waliobaki
wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni kwa kufanya
uhalifu wa aina yoyote.
Ni watu ambao wanataka
kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza kuiamuru iwape wakitakacho na
wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi tu, watu hawa kwao mabadiliko ni
kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe
kwako, unatakiwa kubadilisha fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio
yanahitaji mabadiliko makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa
kujitoa hasa. Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe,
chukua hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka.
Nakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila mara
kwa kupata maarifa bora yatakayoweza kuboresha yako, kwa pamoja tunaweza.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035/dirayamafanikio@gmail.com
Jan 26, 2017
Kama Unayatafuta Mafanikio Kwa Njia Hii, Huwezi Kuyapata.
Kuna
wakati mwingine binadamu tunakuwa ni viumbe wa ajabu sana kutokana na kutotaka
usumbufu hata kwa yale mambo tunayoyahitaji. Inapotokea tunataka kitu cha aina
fulani tunakuwa ni watu ambao tumejiweka katika kundi fulani ambalo hatutaki
kuweka juhudi sana yaani kwa lugha rahisi tunakuwa kama tunajihuhurumia hivi na
kuona kama tutaumia kwa kutafuta vitu hivyo.
Kutokana
na hali hiyo hupelekea wengi wetu kuanza kutafuta njia za kupata mafanikio ya
haraka na upesi. Kumbe kwa kufuata njia hizo ndiyo tunakuwa tunajidanganya na
kupotea kabisa ukizingatia katika maisha hakuna njia ya mkato kuweza kufikia
mafanikio. Mafanikio yote yanakuja hatua kwa hatua. Na kama unaona njia hiyo
ipo tayari unakuwa unapotea.
Utambue
kuwa kila kitu kwenye maisha kinapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa na
maarifa. Hakuna lelemama katika kutafuta mafanikio. Mafanikio ni mfumo wenye
hatua zake ambazo ni lazima zifuatwe. Sasa anapokuja mtu anakwambia kwamba ipo
njia hii hapa ya mkato kuyapata mafanikio, mmmh huyo ni vyema ukamuogopa sana
kwa kuwa atakuwa anakupoteza huku ukiwa unajiona.
Ni
vigumu sana kuweza kufanikiwa kama utategemea njia za mkato na bila kuweka
juhudi yoyote ile kubwa. Kama utayapata mafanikio hayo kwa njia hiyo ni wazi tu
yatakuwa ya muda. Hiyo yote inaonyesha hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio
yako. Kitu kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuweka juhudi zako kubwa mpaka
kufanikiwa na siyo vinginevyo.
Hebu
jaribu kuangalia watu wote wale ambao wamewahi kushinda bahati nasibu. Watu
hawa wengi wao ukija kuwafatilia maisha yao
baada ya miaka michache mbele utakuja kugundua ni watu ambao pesa hizo
hawana tena na wafelisika. Kufilisika kwao kumekuja kutokana na walizipata pesa
hizo nyingi kwa ghafla na kwa njia ambayo ni ya mkato na sasa zimewakambia.
Kama
nilivyosema mafanikio yanakuja hatua kwa hatua. Kuna kujifunza kwingi sana
inapotokea umeanzia chini kabisa. Mara nyingi
hiyo inakuwa inakujengea misuli ya kukua kidogo kidogo na mwisho wa siku
unajikuta upo kwenye kilele cha mafanikio makubwa. Endesha maisha yako kwa
kujiamini na kujua maisha yako ni lazima ufanikiwe hata bila kutegemea njia za
mkato ambazo nyingi huwa zina mashimo mengi na isitoshe hazina uhakika wa kufika.
Hiki
ni kitu ambacho unatakiwa ukiweke kwenye ubongo wako kuwa unahitaji ujasiri,
kujitoa na kuwekeza nguvu zako nyingi kwa kile unachokifanya na siyo kupita
njia ya mkato kama unavyofikiri. Kumbuka, ni lazima kujituma kwa bidii tena
wakati mwingine katika magumu na vizuizi vya kila aina bila kukata tamaa. Kila
kitu kitawezekana na utafika kule unakohitaji kufika katika maisha yako ikiwa
utazingatia ukweli huo ninao kwambia sasa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya maisha yako na endelea
kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani
Ngwangwalu,
Jan 25, 2017
Imani Tatu Unazotakiwa Kuwa Nazo Ili Kukufanikisha.
Najua
hapo ulipo una mipango au malengo ya aina fulani uliyojiwekea na unahitaji
mipango hiyo itimie. Lakini ili kuyafikia hayo malengo yako, mara nyingi huwa
hayawezi kutimia mpaka ndani yako ujenge imani tatu muhimu. Hizi ni imani
muhimu sana kwa mabadiliko yoyote unayoyataka maishani mwako.
Bila
kuwa na imani hizo si malengo peke yake ambayo hayataweza kutimia hata pia mabadiliko yoyote hayawezi kutokea
kama huna imani hizo tatu. Kwa sababu hiyo, hili ndilo lengo la makala haya,
ikusaidie kujua aina za imani unazotakiwa kuwa nazo ili kukufanikisha kwa kile
unachokihitaji.
Hizi
ni imani ambazo unatakiwa kuwa nazo wewe kila siku. Huwezi kufanikiwa sana kama
huna au hujajifunza kujenga imani hizi
tatu muhimu kwenye maisha yako.
Bila
kupoteza muda fuatana nasi katika makala haya kujifunza pamoja imani tatu
unazotakiwa kuwa nazo ili kukufanikisha;-.
1. Lazima uamini maisha yako
yanakwenda kubadilika.
Ili
uweze kuleta matokeo chanya na kukipata kile unachokitaka ni lazima uamini
maisha yako ni lazima yatabadilika. Imani hii ni muhimu sana kwa kwa mabadiliko
yoyote unayotaka kuyachukua kwenye maisha yako.
Kama
hutakuwa na imani hii itakuwa ngumu sana kuweza kufanikiwa. Hata uwe katika
wakati mgumu vipi, lakini ni lazima kwako kutambua maisha yako ni lazima
yabadilike.
Kwa
kuendelea kuamini hivyo itakupelekea kuchukua hatua ambazo zitakusaidia kufikia
ndoto zako. Kama una kitu au hali unayotaka
kuibadili, amini kabisa unakwenda kuibadili hali hiyo au maisha hayo.
2. Lazima uamini wewe ndiye
utakayebadii maisha yako.
Hakuna
mtu mwingine mwenye uwezo wa kubadili maisha yako zaidi yako. Kama unaisubiri
serikali ibadili maisha yako utachelewa, kama unasubiri ajira utachelewa,
unatakiwa kuchukua hatua mara moja.
Hakuna
mwenye uwezo wa kubadili`maisha yako zaidi ya wewe. Upo ulazima wa wewe kuamini
kwamba ndie utakayebadili maisha ako na familia yako na siyo mtu mwngine.
Iwe
unakabiliwa na changamioto ya mtaji ni lazima ujue wewe ndiye unatakiwa ubadili
hali hiyo. Ikiwa unakabiliwa na changamoto ya hali ngumu ya maisha pia wewe ndiye
mwenye uwezo wa kuibadili.
3. Lazima uamini unao uwezo wa
kubadili maisha yako.
Pamoja
na kwamba umeamini maisha yako yatabadilika na ni wewe ndiye utakayebadili hali
hiyo, pia upo ulazima wa kuamini hali
hiyo inawezekana kwako kabisa kubadilika.
Acha
kujikatisha tamaa kwa namna yoyote ile. Kila kitu kinaweza kubadilika katika
maisha yako na kufikia mafanikio makubwa. Hata hali ya maisha yako nayo pia ina
uwezo wa kubadilika.
Kwa
kifupi hizo ndizo imani tatu muhimu unazotakiwa kuwa nazo ili kufanikishha jambo
lolote lile katika maisha yako.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI
NGWANGWALU,
Jan 24, 2017
Jinsi Ya Kutengeneza Karanga Za Mayai.
Kama ilivyo ada yangu kukueleza
masomo ya kijasiliamali nakusihi uambatane nami mwanzo mpaka mwisho, maana
maana halisi ujasirimali husishwa na utengenezaji wa vitu vipya au kuviboresha
vya zamani.
Hata hivyo ushindwe wewe kuchukua
hatua ya kuweza kufanyia kazi masomo haya ambayo nimekuwa nikifundisha, kwani
wakati unalaumu masuala ya umaskini mimi nitakuwa nimeshanawa mikono.
Nilishafundisha namna ya kutengeneza Tomato souce, chill souce.
Hivyo leo tuangalie utengenezaji wa
karanga za mayai. Karanga za mayai zimekuwa zikipendwa na watu wengi sana
nikiwemo mimi mwenyewe. Pamoja na utengenezaji wa bidhaa hii wapo ambao
wamekuwa wakijmtengeza bidhaa hizo kama sehemu ya kujipatia kipato.
Hivyo ungana nami twende sawa kwa
kuangalia mahitaji ya awali kabla ya kuanza kukaanga karanga za mayai.
1. Sukari kiasi
2. Unga wa ngano kilo 1 moja na
nusu.
3. Karanga kilo 1
4. Mayai 3
5. Mafuta ya kupikia kiasi kulingana
na mchanganyiko wako.
Namna ya kutengeneza
a. Pasua mayai ,changanya mayai
na sukari kisha koroga katika chumba kimoja.
b. Hatua ya pili chukua unga wa
ngano kisha changanya na mchanganyiko namba (a) yaani mchanganyiko wa
mayai na sukari.
c. Weka mafuta katika sufuria
kisha injika motoni. Lakini hakikisha moto hauwi mkali sana. Ukiwa mkali
sana utasababisha karanga kuungua sana na kupoteza radha.
d. Koroga mchanganyiko huo
taratibu ili kuondoa kugandamana kwa mchanganyiko huo wa karanga pamoja na unga
wa ngano. Fanya hivyo kila baada ya dakika kadhaa.
e. Ukiona zimeanza kubadilika
rangi onja kwa kujiridhisha kama kweli zimeiva.
f. Zikisha iva ziepue kisha
weka katika chombo kisafi ili zipoe. Baada ya dakika kadhaa zivunge katika
vifungashio kwa ajili ya biashara.
Muhimu. Hakuna kitu chenye thamani
katika biashara kama kufunga bidhaa katika vifungashio vizuri vyenye kuvutia
lakini vifungashio pekee havitoshi hakikisha bidhaa yenyewe ni bora.
Asante tukutane siku nyingine hapa hapa
tukijadili masuala ya biashara na maisha kwa ujumla. Nakutakia siku njema na
mafanikio mema.
Ndimi Afisa Mipango Benson Chonya,
Jan 23, 2017
Upi Ni Uhusiano Wa Kimazingira Na Mafanikio?
Kuna mahusiano makubwa kati ya mafanikio yako na mazingira
yanayokuzunguka. Lakini mafanikio hayo huwa hayaji kwa bahati mbaya, au
huwa hayaji kama ajali. Bali huja kwa kuyatazama mazingira hayo, kama
sehemu ya mafanikio yako. Huenda nikawa nimekuacha kidogo ipo hivi, maana
halisi ya neno mazingira ni mjumuisho wa kila kitu ambacho humzunguka
mwanadamu.
Hivyo Moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa ikisababisha
maisha ya wengi kuwa katika hali ya ya kawaida ni kutokana na vile ambavyo
wameamua kuyachukulia mazingira katika hali ya kawaida pia. Lakini ukweli ni
kwamba ili uweze kuwa mtu mwenye mafanikio amini ya kwamba wewe si mtu wa
kawaida na mazingira uliyonayo ni ufunguo wa mlango wa mafanikio yako.
Kuwa mtu wa kawaida kumekufanya ushindwe kufikia kusudio lako.
Swali linakuja tena kwanini uwe mtu wa kawaida kama kweli unataka mafanikio ya
kweli? Bila shaka majibu yake yasikufanye kuwa ni mtu wa kawaida.
Mafanikio makubwa huja kwa mtu ambaye yupo tayari kwa ajili ya mafanikio hayo.
Pamoja na changamoto nyingi ambazo zipo katika dunia hii,
changamoto hizo zisikufanye ushindwe kufanikiwa. Kabla ilivyo ada yangu
kukueleza bayana ya kwamba "kukata tamaa ni kosa la jinai" hii ni kwa
mujibu wa sheria za mafanikio.
Huenda bado ukawa huamini kama ipo siku utafanikiwa, ila
nataka kukutia moyo kwa kukwambia ya kwamba mafanikio yako yapo upande wako,
endapo utaamua leo kuweza kuyatawala mazingira yako vizuri.
Sheria ya mafanikio na uhusiano wa mazingira inatuambia ya
kwamba watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wametawaliwa na mazingira.
Mazingira hayo hayo umewafanya watu wengine wamefanikiwa na wengine bado
hawajafanikiwa. Sasa swali linakuja mazingira haya ya nini kwani?
Tuendelee kidogo kwa kuyazungumza mazingira haya. Mazingira haya
endapo utayatazama kwa macho mawili utagundua ya kwamba yametawaliwa na wingi
wa changamoto nyingi kuliko fursa. Na endapo utayatazama mazingira hayohayo kwa
jicho la tatu utagundua yametawaliwa na fursa nyingi kuliko changamoto.
Unashangaa wala usishangae huo ndio ukweli. Swali la kujiuliza
unatumiaje mazingira uliyonayo kama fursa ili uweze kufanikiwa? Usinipe
majibu. Lakini Ukichunguza kwa umakini utagundua ya kwamba watu wengi
tumekuwa tukiyachukulia mazingira ambayo tunaishi katika misingi ya ukawaida na
ndo maana tumekuwa siku sote sisi ni wa kawaida.
Lakini nataka nikuase kwa kusema ya kwamba maisha hayo ambayo
unatamani kuwa, ni lazima uweze kuyatazama mazingira katika sura ya fursa
na si changamoto kama ulivyokuwa ukifanya awali. Hata kama mazingira
iliyopo yana changamoto gani, Changamoto hizi unatakiwa kuzikabili kwa kufanya
kitu tofauti . Maana kuna usemi ambao unasema ya kwamba changamoto ni
fursa.
Mazingira yanayokuzunguka isiwe kigezo cha wewe kuwa maskini
kwani wewe si mtu kawaida, hivyo yafanye mazingira hayo kama kigezo cha
wewe kufanikiwa. Siri ya mafanikio yako ipo katika mazingira yako.
Nikuache na ujumbe usemao" Mazingira yangu mafanikio yangu
"
Ndimi: Afisa Mipango Benson Chonya,
Jan 20, 2017
Hatua Nne Za Kujifunza Kutokana Na Makosa.
Mara
nyingi tumekuwa tukisema ili ufanikiwe ni muhimu sana kujifunza kutokana na
makosa. Tumekuwa tukiongea sana kuhusu juu ya hilo mara kwa mara na
kukusisitizia juu ya umuhimu wake.
Pamoja
na msisitizo huo wa kujifunza kutokana na makosa ambao tumekuwa tukikupa, leo
tumeona vyema tukuongezee kitu cha cha ziada katika huko kujifunza kutokana na
makosa.
Kitu
hiki si kingine bali hatua ambazo unatakiwa uchukue ili uweze kujifunza kwa
makosa kiuhakika. Kwa kujifunza hatua hizi itakusaidia wewe kuvuka hapo ulipo na kwenda ng’ambo nyingine
kimafanikio.
Ili
kunielewa vizuri katika hili hebu twende pamoja tuangazie nukta kadhaa zitakazo
tusaidia kuzielewa hatua nne za kujifunza kupitia makosa tunayoyafanya kila siku
kwenye maisha yetu.
Hatua 1. Andika makosa yako.
Unapojikuta
upo katika kitu kipya unachofanya, tambua makosa yapo na ni lazima utafanya. Kitu
cha kwanza cha kufanya ili uweze kujifunza vizuri kutokana na makosa yako,
andika makosa yako. Hakuna mkato katika hili, andika makosa yako ili ikusaidie
wapi pa kuanzia pale unapotaka kujirekebisha.
Fanyia kazi makosa yako mapema. |
Hatua 2. Jifunze kutokana na makosa ya
wengine.
Usisubiri
sana kujifunza kutokana na makosa yako, angalia pia wengine wanafanya makosa
gani, pia yachukue makosa hayo na ya andike mapema ili yasije yakajirudia na
kwako pia. Unapoandika makosa ya wengine
mnaofanya kitu kinachofanana inakusaidia na wewe kuwa makini sana.
Hatua 3. Andaa orodha ya makosa ya
kuyafanyia kazi.
Katika
hatua ya kwanza na ya pili utakuwa umefanya zoezi la kuandika makosa yako. Hapa
katika hatua hii andaa sasa makosa ambayo unataka kuyafanyia kazi lakini ambayo
yametoka kwenye orodha uliyoandika kwenye hatua mbili zilizotangulia, kisha
chukua hatua.
Hatua 4. Hakikisha usiridhike mapema.
Hata
mara baada ya kurekebisha makosa yako, usibweteke na kuridhika na kujiona wewe
ni wewe. Endelea kujifunza kutokana na makosa mengine tena na tena na kurudia
hatua hizo, hiyo itakufanya uzidi kuwa bora sana siku hadi siku.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,
Jan 19, 2017
Jiwekee Mkakati Huu,…Ili Ujihakikishie Mafanikio Yako.
Katika
utoto wake hakuna kitu ambacho alipenda sana kijana huyu kama kuona ndoto yake
inatimia. Aliandika vizuri ndoto yake kwenye daftari lake na kisha kila wakati
aliipitia ndoto hiyo.
Shauku
ya kuona ndoto yake ikitimia alizidi kutokea karibu kila siku. Alitamani kuiona
ndoto yake ikitimia mapema sana kwa kadri iwezekanavyo. Kwa kifupi, alikosa
raha hasa alipoona kwa nini ndoto yake haitimii?
Hata
hivyo pamoja na kuwa na hamasa kubwa ya kuona ndoto yake inatimia ,kijana huyu
alikuja kugundua kuna kitu kimoja kinamzuia kufanikiwa. Kitu hicho hakikuwa
kingine bali ni shule.
Akiwa
na miaka 22 akiwa elimu ya juu aliamua kuachana na shule na kwenda kutimiza
ndoto yake aliyokuwa akiifikiri. Lakini hata hivyo kazi haikuwa nyepesi sana
kama alivyofikiri.
Jiwekee mpango wa muda mrefu ukusaidie kufikia ndoto zako. |
Ingawa
kijana huyu alikuwa hana pesa, maskini, hivyo ilimlazima kuanza kuimba kwenye
kumbi za starehe, ‘bar’ na ilimlazima
wakati mwingine hata kulala vibarazani, lakini alidhamiria kutimiza ndoto yake.
Hali
ya kuendelea kuimba huku akiwa katika wakati mgumu aliendelea nayo hivyo hivyo,
lakini kuna wakati mambo yalizidi kuwa magumu sana hadi hali iiyopelekea mpenzi
wake mpendwa kuachana naye.
Kitendo
cha kuweza kuachana na mpenzi wake kilimuuma sana, aliona maisha ndio yamefikia
mwisho, hivyo uamuzi pekee aliamua kuuchukua ni kujiua. Maisha yalikuwa hayana
maana tena kwake.
Kabla
hajachukua uamuzi huo aliamua kwenda hospitali kupima kama akili zake kweli
ziko sawa, baada ya majibu na kugundulika kwamba yuko sawa, alikaaa chini na
kujiuliza ni nini hasa kinachonifanya nijiue?
Alikuja
kugundua huo ungekuwa ni ujinga wa kutupwa. Aliapa na kuamua kwa vyovyote vile
itakavyokuwa, hata dunia nzima imtenge ni lazima aitimize ndoto yake. Alikubali
kufanya kazi usiku na mchana mpaka kieleweke.
Tokea
afanye uamuzi huo, ilimchukua miaka mingine miwili hadi pale angalau alipoanza
kuona matunda ya kazi yake. Hapo ndipo alipoanza kukubalika na muziki wake
kuanza kufahamika.
Kitu
kilichomsaidia ni kule kujitoa kwake na kukubali kuchukua mpango wa muda mrefu
kuliko kuota ndoto za kufanikiwa mara moja ambazo zingemuangusha.
Huyu
tunaye mzungumzia hapa si mwingine bali ni Bill
Joel, moja kati ya wanamziki maarufu duniani. Leo hii angekuchukua maamuzi
ya kujiua mara baada ya kuachwa na kushindwa usingeweza kumsikia tena.
Hapa
tunajifunza kuna wakati ili kuweza kufanikiwa unahitajika kujiwekea mikakati ya
muda mrefu yaani ‘long term plan’. Bila
kufanya hivyo ni rahisi sana kushindwa hata pale ambapo hukutakiwi kushindwa.
Kwa
lugha nyingine namaanisha ile habari ya kutaka kufanikiwa ndani ya muda mfupi,
unatakiwa ujifunze ‘kuizika’ mapema
ili ujipe muda mzuri wa kutengeneza mafanikio yako kwa uhakika.
Kile
kinachonekana leo kama hakitoi mafanikio kwako makubwa, kitafanikiwa na kukupa
mafanikio makubwa endapo utakipa muda na kuendelea kuweka juhudi kila siku na
kujifunza.
Maisha
yapo kama majira ya mwaka, kuna wakati wa baridi, wakati wa joto au wakati wa
upepo. Hivyo unatakiwa kujifunza kukabiliana na nyakati zote hizo ili zikusaidie
kuweza kufanikiwa.
Lakini
ikiwa ni mtu wa kulia na kuona mambo hayawezekanai kwa sababu umeshindwa au kwa
sababu dunia imemekukata utakua ni mtu wa kushindwa sana.
Kila
wakati jiandae kuwa kuwa shujaa kwa kile unachookifanya. Achana na habari ya
kulialia. Ukiweka msingi na mikakati wa kuwa na malengo ya muda mrefu. Hakuna kitakachokuzuia
kufanikiwa.
Endelea
kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama
makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja
tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE
UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA
KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni
wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,
Subscribe to:
Posts
(
Atom
)