Sep 10, 2015
Siri Kubwa Iliyofichika Katika Mafanikio Ni Hii Hapa.
Ninakumbuka
ni miaka mingi sasa imepita wakati nikiwa darasa la tatu nilikuwa nikisumbuana
sana na wazazi wangu kwa sababu ya shule. Kilikuwa ni kipindi ambacho nilitokea
kuichukia shule na nilikuwa nipo tayari kwa lolote kuacha shule. Kwa kipindi
hicho kwangu shule ilikuwa siyo sehemu ya kujifunza kama watoto wenzangu
walivyoifurahia, kwangu ilikuwa ni mateso.
Karibu
kila siku nilikuwa niliamshwa kwamba muda wa shule umefika. Na hata kama
ikitokea kweli siku hiyo nilienda ilikuwa ni kwa kujikongoja sana. Sababu hasa
zilizonifanya nichukie shule kwa wakati ule zilikuwa ni nyingi, lakini chache
nilizokuwa nazo ni pamoja na baridi iliyokuwepo hasa nyakati za asubuhi, pia
utamu wa usingizi na hiyo haitoshi nilikuwa nimechoshwa na umbali wa mahala
shule ilipo. Zilikuwa ni sababu za kitoto kweli ingawa kwangu wakati ule
zilikuwa za maana sana.
Nimekuwekea
mfano huo sio kukufurahisha tu, bali kuna kitu ambacho ninataka tujifunze
pamoja kutokana na maisha yetu ya kila siku. Mara nyingi wengi wetu huwa hatupo
tayari kuvumilia mpaka mwisho kuelekea kwenye ndoto zetu. Wengi tunajikuta
tunakuwa tuna sababu nyingi za kitoto kama nilizokuwa nazo mimi ambazo moja kwa
moja zinatuzuia kwenye mafanikio.
Jaribu
kujiuliza, ni mara ngapi umekuwa mtu wa visingizio na kuacha ndoto zako
zikiyeyuka kutokana na sababu nyingi zisizo na maana ambazo umekuwa
ukizishikilia? Ni mara ngapi ambapo umekuwa ukikosa hamasa na uvumilivu kwa kile
unachokifanya na kuachia ndoto zako zikipita kirahisi eti kwa sababu ndogo tu
kuwa huwezi hiki ama kile? Bila shaka umekuwa na sababu kama hizi nyingi tu, tena zisizo na msaada
kwako.
Ni
kweli miongoni mwetu wapo watu ambao ni rahisi kujisikia na hatimaye kuamua
kutokufanya mambo fulani kama nilivyokuwa mimi kutokana na sababu ndogondogo. Hawa ni watu wa kutokujisikia
kufanya kitu hata kama kina manufaa na faida kwao kubwa. Kufanya kwao
kunategemea sana na kujisikia. Kwa mfano leo hii kama ameamka amechoka basi,
kazi nyingi zitalala ama hataweza kwenda kazini kabisa kwa kisingizio hiki na kile. Kama ni kweli
umeamua kufanya hivyo, hiyo yote ni sawa kwako kwa sababu maisha ni yako na
kama ni mafanikio ni yako pia.
Unaweza
ukawa unaona uvivu kufanya jambo fulani au ukahisi huwezi kabisa, lakini kitu
peke unachotakiwa kufanya ili ufanikiwe ni kulianza jambo hilo au kitu hicho
haijalishi unajisikiaje au unawaza nini kwenye kwenye kichwa chako. Mafanikio
yote unayoyataka huwa yanaanza kwa kuanza, hapo ndipo ilipo siri ya wewe kuweza
kusongambele. hakuna mafanikio yanayoanza kwa sababu hata siku moja, jaribu kuchunguza hilo utagundua uhalisia wake.
Inawezekana
ukawa upo kwenye maisha magumu, huna mtaji na unaona kabisa haiwezekani kufanya
kitu, lakini uwezo wa kubadilisha maisha yako unao kwa kuanza hivyohivyo. Acha
kufanya kosa la kusubiri mambo yako yote yawe sawa ndiyo uanze utakuwa tayari
umechelewa. Huna haja tena ya kusubiri kitu anza kutekeleza ndoto zako mara
moja.
Kila
mtu anauwezo mkubwa wa kufanikiwa na kufika kule anakotaka kufika ikiwa
atatambua umuhimu wa kuanzia pale alipo. Kama umeamua kuanzisha mradi fulani,
usiwaze sana kuanzisha mradi wa mamilioni mengi anza na kile kidogo
ulichonacho na kisha ondoa sababu zako ulizonazo hata kama ni nzuri vipi.
Jenga
tabia ya kuthamini kile unachokifanya na kisha ukifanye kwa nguvu zote bila
kujali ni kidogo kiasi gani kifanye kwa ubora wa juu zaidi. Mafanikio yako
utaanza kuyaona kwa kadri utakavyozidi kufanya. Hiyo kumbuka mafanikio yako
yatakuja tu, hata kama unachofanya ni kidogo vipi. Kitu cha msingi kithamini na
anzia hapo hapo, acha visingizio, wajibika na maisha yako na hapo utakuwa umegusa siri kubwa ya mafanikio
yako.
Kwa
makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza
kila siku na kuboresha maisha yako. Pia usiache kuwashirikisha wengine kuweza
kujifunza kupitia mtandao huu.
Ni
wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.