google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Oct 30, 2015

Kama Kila Unachokifanya Kimeshindwa Kukupa Mafanikio, Fanya Kitu Hiki.

No comments :
Inawezekana  umefanya mambo mengi ya kukupa mafanikio, lakini kila ukiangalia umekuwa ukiona kama juhudi zako zimekwenda bure. Karibu kila kitu unachojaribu kukifanya unaona kimeshindikana. Kila ukiangalia hakuna mafanikio  makubwa uliyoyapata.
Ninajua unaweza ukawa unapitia katika hali hii ambayo kwako inakuwa ni ngumu na inakutesa. Kama ni hivyo huna haja ya kukata tamaa sana. Kila kitu kinaweza kubadilika. Ikiwa kama kila unachokifanya kimeshindwa kukupa mafanikio, kitu pekee cha kufanya hapo siyo kukata tamaa kama unavyofikiri, bali ni KUFANYA KAZI KWA BIDII TENA. Hiki ndicho kitu unachotakiwa kukifanya.
Unaweza ukasema ‘ooh mbona mimi najituma sana na nimekuwa nikifanya hivyo siku zote.’ Hilo linaweza kuwa ni sawa kwako, lakini ongeza juhudi zaidi na zaidi kwa namna tofauti mpaka ‘kieleweke’. Hakuna mbadala mwinginwe wa kitu cha kufanya zaidi ya kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii kuliko mwanzo. Kama ulikuwa ukifanya kazi kwa saa 8, unaweza ukaongeza masaa mengine tena ya ziada, hata kama ni mawili.
Hiyo ndiyo siri kubwa inyoweza kukutoa hapo ulipo na kukupa maisha mengine ya kimafanikio. Acha kujihurumia, acha kufikiria kwamba unajitesa. Wewe fanya kazi kwa bidii. Zipo faida na mambo mengi unayoweza kuyapata ikiwa utaongeza juhudi za makusudi tena kwa kila unachofanya.

FANYA KAZI KWA BIDII ZOTE.
Kwanza, itakusaidia sana kukuondolea wasiwasi kwenye maisha yako. Kwa nini hiyo iko hivyo ni kwa sababu. Kila juhudi na uwezo wako wote utakuwa umeweka sehemu moja. Hivyo, hutajilaumu sana kwa matokeo utakayoyapata hata kama siyo ya kuridhisha.
Pili, kufanya kazi kwa bidii kutakusaidia kutatua matatizo mengi. Kama kulikuwa kuna matatizo fulani madogo yalikuwa yanakusumbua itakuwa ni rahisi kwako kuweza kuyapatia majibu yanayotakiwa.
Tatu, kufanya kazi kwa bdii kutakupunguzia msongo wa mawazo. Hiyo yote ni kwa sababu akili yako haitaweza kupata muda wa kufikiria mambo ya ajabu ajabu kwa sabau ya kuchoka. Baada ya kazi kwako itakuwa ni kupumzisha mwili kwa kulala.
Kama nilivyoanza makala haya, kama kila kitu unachokifanya kimeshindikana ongeza juhudi ya kufanya kazi kwa bidii zote kama mtumwa, matokeo mazuri utayapata na mafanikio yatakuwa kwa upande wako.
Nakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote na kumbuka endelea kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,



Oct 27, 2015

Usiruhusu Mambo Haya Matatu Yakakuzuia Kufanikiwa.

No comments :
Yapo mambo mengi ambayo mara nyingi yanakuwa yanamzuia binadamu kufikia mfanikio yake. Mambo hayo yapo ambayo tunakuwa tunayajua na tunaweza kuyatawala, lakini mengine tunakuwa hatuyajui, hivyo inakuwa ngumu kuyatawala. Hivyo kwa vyovyote vile kila mtu hukutana na vizuizi fulani katika safari yake  ya kufikia mafanikio.
Kwa kuwepo kwa vizuizi hivi, hapa ndipo utofauti wa maisha huanza kujitokeza. Wapo ambao huwa ni rahisi kushindwa kutokana na vizuizi. Wapo pia ambao huwa ni ving’ang’anizi mpaka kufikia mafanikio yao. Wale ambao hushindwa , kuna wakati hushindwa kwa vizuizi ambavyo naweza kusema wangeweza kuvishinda kama wangekuwa makini kidogo.
Hapa ndipo kipo kiini cha makala haya kilipo. Jaribu kukumbuka kidogo hivi, ni mara ngapi umekuwa umekuwa ukizuiliwa na mambo madogo madogo kufanikiwa? Bila shaka ni mara nyingi. Kuna wakati ulishindwa kutimiza ndoto zako kwa sababu pengine ya visingizio tena visivyo na maana. Utakuta ni sababu ndogo ndogo ambazo umekuwa ukijitengenezea.
Lakini leo ninachotaka kukwambiani hiki, kama unataka kufanikiwa usiruhusu kabisa mambo haya madogo matatu yakakuzuia kufanikiwa:-
1. Kukosolewa.
Acha kushindwa kufikia mafanikio yako kwa sababu ya kugopa kukosolewa. Makosa unayoyafanya yachukulie yawe fundisho kwako la kuweza kukusogeza mbele kufikia mafanikio unayoyahitaji. Acha kusikiliza maneno ya watu wanaozidi kukukwambia kuwa eti huwezi kufanikiwa tena. Hilo sio kweli kwani hakuna mtu anayejua uwezo wako halisi.
Wapo wengi ambao hushindwa kutimiza malengo yao kwa sababu ya kuogopa kukosolewa. Kama kuna jambo unataka kulifanya wewe lifanye. Kama kuna mtu anayekukosoa mwache aendelee kukosoa lakini safari yako izidi kusonga mbele. Hakikisha usizuiliwe na kosa hili dogo na kukufanya ukashindwa kufikia mafanikio yako.

ONDOA HOFU ILI KUFIKIA MAFANIKIO YAKO
2. Wasiwasi/woga.
Wengi ni watu wa wasiwasi ama woga sana na hata wao kuna wakati wanashindwa kuelewa wasiwasi huo hutokea wapi hasa. Utakuta ni watu wa wasiwasi kwa mambo madodogo madogo na ya kawaida kabisa. Kwa mfano akitaka kufanya jambo hili au lile anakuwa na wasiwasi mwingi sana nafsini mwake. Hili ni jambo ambalo kiukweli huwakwamisha wengi kufanikiwa.
Sasa kwa kuwa na wasiwasi huo ambao unakuwa unaujenga kila siku, inasababisha mipango na malengo yako mengi kushindwa kutumia. Wasiwasi ni kitu ambacho kinawafanya watu wengi kushindwa sana kutimiza malengo yao. Hiyo yote ni kwa sababu unapokuwa una woga unasababisha kushindwa kujaribu mambo mengi ya kukufanikisha.
3. Maumivu.
Inawezekana unashindwa kuendeea mbele zaidi ya hapo ulipo kwa sababu ya maumivu uliyonayo moyoni mwako. Maumivu hayo inawezekana uliumizwa baada ya jambo ulilokuwa ukilifanya kushindwa kukuletea mafanikio makubwa au kukupa hasara ya kutosha. Na ikafika mahali ukashindwa kujuani nini cha kufanya.
Haya ni maumivu ambayo kwa namna moja nyingine tunakutana nayo katika maisha. Ni maumivu ambayo hutufanya tushindwe kusonga mbele kila tukikumbuka makosa hayo. Kama upo au ulishapitia hali hii, najua unaelewa ni kitu gani ninacho kiongea hapa. Ili kufanikiwa, usiruhusu maumivu haya yakakufanya ukashindwa kufikia mafanikio yako hata siku moja.
Kumbuka, kwa kuwa na wasiwasi sana juu ya maisha yako, kuogopa kukosolewa na kushikilia sana na maumivu ni mambo madogo ambayo yanaweza kukuzuia  wewe kufikia mafanikio makubwa. Acha kuruhusu hali hii ijitokeze kwako. Kuwa shujaa wa maisha yako.
Dira ya mafanikio inakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote. Na kumbuka endelea kujifunza kila siku bila kuchoka.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,

Oct 26, 2015

Jinsi Unavyoweza Kufanya Jambo Ambalo Hujisikii Kulifanya.

No comments :
Maisha yanakuwa na maana na mazuri kwetu kama tunafanya yale mambo ambayo tunayapenda na kuyatamani. Inapotokea unakuwa unafanya jambo ambalo hulipendi au hujisikii mara nyingi mambo yanakuwa magumu sana. Ni kitu ambacho huwa kinatokea, unakuta tu, hujisikii kufanya jambo fulani ambalo pengine ni muhimu kwako.
Je, inapokutokea unataka kufanya kitu halafu ukawa hujisikii hapo unakuwa unafanyaje? Je, unakuwa unaacha na kuendelea na mambo mengine au kuna hatua unakuwa unachukua? Yapo mambo mengi unayoweza ukawa unajifikiria, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, zipo njia unazoweza kuzitumia kufanya jambo ambalo hujisikii kulifanya.
Zifuatazo Ni Njia Ambazo Unaweza Kuzitumia Kufanya Jambo Ambalo Hujisikii Kulifanya.
1. Anza kwa kidogo.
Kama ni jambo ambalo hujisikii kulifanya anza nalo kwa kidogo. Kama wewe ni mwandishi unataka kuandika kitu na unahisi hujisikii, anza na sentensi moja kwanza, hiyo itakupa nguvu ya kuendelea zaidi. Na katika maeneo mengine ya maisha yako unaweza ukatumia mbinu hiyohiyo, kwa kuanza na hatua ndogo katika kila jambo.

ACHA KUKATA TAMAA, ANZA KUFANYA MARA MOJA.
2. Usiruhusu akili yako kuogopa sana.
Kuna wakati ni rahisi kujisikia huwezi kufanya jambo fulani kwa sababu ya woga ambao unakuwa umeujenga kwenye akili yako. Mara nyingi akili inapokuwa na woga wa aina fulani inakuwa siyo rahisi kufanya jambo lolote hata iweje. Ili kufanikiwa katika hili, kwa vyovyote vile usiruhusu akili yako ikawa na woga wa kupitiliza, kwa mfano woga wa kuweza pengine hutaweza kufanikiwa.
3. Jipe muda wa kujifunza.
Inawezekana unashindwa jambo hilo kwa sababu hujalijua vizuri zaidi. Kama ni hivyo jipe muda wa kujifunza na kulielewa jambo hilo kwa undani. Hii itakusaidia kuanza kulifanya huku ukiwa na hamasa kubwa ambayo itakusaidia wewe binafsi kuweza kulifanya jambo lako na kuweza kusonga mbele kimafanikio.
4. Acha kuahirisha.
Pamoja na kuwa upo ugumu fulani wa kutokujisikia kulifanya jambo hilo, dawa pekee ya kuweza kulifanya ni jifunze kutoweza kuliahirisha jambo hilo. Lianze hivyohivyo hata kama ni kwa kidogo, hata kama huku ukiwa unahisi kama mwili  hautaki, lakini kikubwa usiahirishe. Kwa kadri utakavyozidi kufanya bila kuahirisha utajikuta unazidi kuongeza hamasa ya kulifanya zaidi na zaidi.
Kwa kifupi, hizo ndizo njia ambo unaweza ukazitumia kufanya lile jambo ambalo kwako hujisikii kulifanya.
Tunakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote. Na kumbuka endelea kujifunza kila siku bila kuchoka.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,

Oct 22, 2015

Kama Hujui, Hawa Ndiyo Watoto Wenye Akili Nyingi zaidi.

No comments :
Hivi karibuni kumekuwa na maneno hata mijadala kuhusu watoto wanaozaliwa kwa njia ya upasuaji. Kuna madai na maneno kwamba, watoto wanaozaliwa kwa upasuaji wanakuwa na akili kubwa sana ukilinganisha na wenzao wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.
Wataalamu wa sayansi ya utabibu hivi sasa wanakiri kwamba, watoto wanaozaliwa kwa njia ya upasuaji, wanakuwa salama kiakili kuliko wale wanaozaliwa kupitia njia ya kawaida.
Karibu watoto watatu kati ya kila kumi, wanaozaliwa kwa njia ya kawaida, huwa wanapata tatizo la kuvuja damu ubongoni, ambalo husababishwa na mchakato mzima wa kujifungua kwa mama.
Hivi sasa bila shaka, unaweza ukajua ni kwa nini watu wanaamini kwamba, watoto wanaozaliwa kwa upasuaji wanakuwa na akili kuliko wale wanaozaliwa kwa njia ya kawaida. Kama ulikuwa hujasikia, inabidi ujue kwamba, imani hiyo imeingia na inakua haraka.
Kuna kipindi ambapo wataalamu wa chuo cha utabibu cha North Carolina, waliwahi kusema kwamba, watoto wanaozaliwa kwa upasuaji, wanakuwa na akili salama zaidi.

Waliweza kukiri pia kwamba, kuna uwezekano kuwa, uzaliwaji kwa njia ya kawaida, huathiri kwa kiasi fulani ubongo wa mtoto. Kwa wale watatu katika kumi athari huwa kubwa zaidi.
Kwa wanaozaliwa kwa njia upasuaji, hakuna hata mmoja anayeweza kupata athari ya kwenye ubongo. Ndiyo maana wale wanaozaliwa kwa njia hii, inatabiriwa kwamba, wanaweza kuwa na akili kubwa au salama.
Hata hivyo, watafiti hawa wanasema, ugunduzi huu hauna maana ya kuwataka akina mama kung’ang’ania kujifungua kwa njia ya upasuajii ili kuwafanya watoto wao kuwa na akili nzuri na salama.
Mtoto anapozaliwa kupitia kwa njia ya kawaida, huwa anatoka damu kidogo ubongoni, lakini wataalamu wanajipa moyo kwamba, huenda hiyo ni njia ya maumbile katika suala zima la kujifungua.
Hivi karibuni ndipo ambapo imebainika kwamba, katika harakati za kujifungua kwa njia ya kawaida, kichwa cha mtoto huwa kinabanwa na ubongo kupata msukomsuko.
Jambo kama hili halitokei kwenye kujifungua kwa njia ya upasuaji, kwani hapo hakibanwi na chochote.
Dk. Honor Wolfe, wa chuo hicho anakiri kwamba, watoto wanazaliwa kwa njia ya upasuaji wana uhakika wa kuwa na ubongo usio na kasoro, ukilinganisha na wale wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.
Maana yake ni kwamba, kujifungua kwa njia ya upasuaji inaweza ikaanza kuwa ‘fasheni’ kwa siku za karibuni.
Ni wazi akina mama wengi wangependa kuona wanazaa watoto ambao wako salama kiakili kadri inavyowezekana.
Kuna watu wanaosema kwamba, utafiti huo hauna jipya , kwani binadamu amekuwa akizaliwa kwa njia ya kwaida kwa miaka nenda rudi.
Kama ni hatari, basi ilitakiwa iwepo, kwani upasuaji ni njia inayotumika kama kuzaa kwa kawaida kumeshindikana.
Lakini, bado ukweli upo kwamba, huenda wengi watu tumeathirika kiakili wakati wa kuzaliwa. Kama tumeathirika kiakili wakati wa kuzaliwa haina maana kwamba, ni lazima liwe jambo la awaida.
Kama kila watu kumi unaokutana nao, watatu walivuja damu ubongoni wakati wa kuzaliwa , hatuwezi kusema ni jambo la lazima au kimaumbile.
Jarida la Radiology linaonesha kwamba, watoto wanaozaliwa Marekani kila mwaka, kwa mfano kati ya milioni 4, milioni 1.1 huzaliwa kwa upasuaji.
Idadi hiyo imeongezeka hivi karibuni kwa kadri wazai wanavyoamini kuhusu utafiti huu. kwa afrika kujifungua kwa upasuaji hakuko kwa kiwango kikubwa.
Nilichotaka kusema hapa ni kwamba ni kweli wale watoto wanaozaliwa kwa upasuaji wanakuwa na akili kubwa au iliyo na usalama zaidi.
Tunakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,         
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu;  0713 048 035,                               
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com

Oct 21, 2015

Mbinu Tano Za Kukuza Biashara Yako.

No comments :
Kwa mapenzi yake Mungu naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nami bila hiana nakukaribisha tena katika siku nyingine ili uchote maarifa sahihi ya kuweza kukusaidia kubadili maisha yako. Ni maarifa hayahaya yatakayokusaidia kuboresha maisha yako kila siku na kwa nyakati tofauti.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia namna unavyoweza kukuza biashara yako na kufikia viwango vya juu. Ikumbukwe kukuza biashara ni hitaji ambalo karibu kila mjasiriamali analitamani kulitimiza. Kama ni hivyo basi, unawezaje kukuza biashara yako? Hapa nimekuwekea mbinu muhimu za kukusaidia kukuza biashara yako hadi kufikia mafanikio makubwa.
1. Toa thamani.
Ili biashara yako iweze kuwa kubwa sana na inayokupa faida, haihitaji mtaji mkubwa sana kama unavyofikiri, inachohitaji ni thamani unayoitoa. Je, thamani unayoitoa inaendana na ile ambayo wateja wako wanaitaka? Kama kweli unatoa thamani halisi, kwa vyovyote vile lazima biashara yako ikue. Haijalishi mtaji ulionao, toa thamani bora utapata matokeo mazuri.
SOMA; Sababu Tano Kwanini Unatakiwa Kumiliki Biashara Yako Sasa?

THAMANI UNAYOTOA ITAKUPA MAFANIKIO MAKUBWA.
2. Kuwa na mahusiano mazuri na wateja wako.
Unaweza ukawa unatoa thamani inayotakiwa, lakini kama huna mahusiano mazuri na wateja biashara yako haitaweza kukua kwa kiwango kikubwa. Wateja ndio kila kitu kwenye biashara yako. Jitahidi hata kama kuna mteja amekukera mwonyeshe kumjali. Kwani hiyo itakujengea jina na kupelekea kuwa na wateja wengi wanaohitaji huduma yako.
3. Kuwa na usimamizi mzuri.
Wapo watu ambao huamua kuanzisha biashara na kuwaachia wengine wasimamie. Linaweza likawa jambo zuri, lakini linahitaji umakini kwa wasimamizi utakaowaweka. Kama watasimamia vibaya uwe na uhakika tayari umeua biashara yako. Hivyo, iwe unasimamia wewe au wengine, inabidi utambue usimamizi mzuri ni kitu ambacho kinahitajika sana ili kukuza biashara.
4. Tengeneza timu sahihi yakukusaidia.
Haiwezekani kila kitu ukafanya wewe kwenye biashara yako. Inabidi ifike mahali ambapo unatakiwa utengeneze timu bora itakayokusaidia kufikia malengo yako. Kipo kipindi ambacho unaweza ukawa unaumwa, au una dharura fulani. Je, katika hiki kipindi unafanyaje? Hapa ndipo unatakiwa uwe na timu au watu wa kukusaidia kukuza biashara yako pale ambapo dharua zinaweza zikajitokeza kwako, ili mambo yaende mbele bila kusimama.
5. Ongeza ukubwa soko lako.
Kama ulikuwa ni mtu wa kuuza bidhaa zako ndani ya mtaa mmoja, ni vyema ukaongeza ukubwa wa soko lako kwa kadri siku zinavyokwenda. Tafuta soko lingine, nje ya eneo ulipo. Utamudu hili lakini ikiwa utawaridhisha wateja wako wa kwanza ambao watakusaidia kukutangazia biashara yako, hali itakayopelekea biashara yako kuzidi kukua siku hadi siku.
Hizo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza ukazitumia ili kuboresha biashara yako na kufikia mafanikio makubwa. Je, una mbinu nyingine ambazo unafikiri zinaweza kutusaidia kukuza biashara na kufikia mafanikio makubwa? Unaweza ukatushirikisha hapo chini kwenye maoni, tukajifunza pamoja.
Dira ya mafanikio inakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote. Na kumbuka endelea kujifunza kila siku bila kuchoka.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,




Oct 20, 2015

Kama Unataka Kutimiza Ndoto Zako, Acha Kufanya Makosa Haya.

No comments :
Kila mmoja ana ndoto zake katika maisha, kila mmoja ana njia yake ambayo anaiamini inaweza kumsaidia katika kutimiza ndoto zake za maisha. Ndoto ni kama malengo ambayo kila mmoja anakuwa amejiwekea katika safari yake ya maisha. Mafanikio ni pale unapokuwa umeweza kutimiza ndoto zako. Kuna ambao walishindwa kutimiza ndoto zao labda kutokana na kutoelewa mambo machache ambayo walioweza kutimiza mipango yao waliweza kuyaelewa.

Je unaweza kuiweka ndoto yako kuwa hai? Kuweka ndoto hako hai na kuiishi ni kuepuka kufanya makosa ambayo wengi waliokata tamaa walishindwa. Je ni makosa gani ambayo wengine hushindwa na kupelekea ndoto zao kuzimika?

1.Wasiwasi.
Wapo ambao ndoto zao zimezimika kwani wamekuwa na wasiwasi sana. Unaweza ukawa unajiuliza "Je nitafanikisha kweli?". Wasiwasi hauna nguvu yoyote katika kupelekea mambo yaende sawa bali huaribu mambo kwenda sawa. Wasiwasi hukatisha tamaa, na kupelekea mtu kuona kuwa hawezi kutimiza malengo yake. Una wasiwasi wa nini? Unapoona una wasiwasi chekelea na uuambie wasiwasi wako kuwa "Nitazidi kuwa imara". 

Woga ni kitu ambacho kinatenganisha watu waliofanikiwa na waliofeli kufanikiwa. Kumbuka maana ya kufanikiwa simaanishi pesa na umaarufu bali hali ya kuweza kutimiza malengo yako uliyopanga ni mafanikio pia. 

Hivyo badala ya kuruhusu wasiwasi ukutawale, endelea kuweka msimamo na kushikilia malengo yako.
kweli
MIPANGO MIZURI YA MALENGO NI MUHIMU KUJIWEKEA.
2. Usikubali vikwazo vikutawale.
Kwa kifupi ni kuwa lazima utakutana na vikwazo, vikwazo ni jambo la kawaida katika maisha, vikwazo vipo kwa lengo la kutuimarisha. Na kama kungekuwa hamna vikwazo tusingeimarika kwani kujisahau kungeongezeka. Vikwazo vinatakiwa uvitazame kama vile ni ngazi, vinakusaidia kupanda hali fulani na tunapaswa kujifunza na kuwa imara zaidi katika hali za vikwazo. 

Ukifuatilia watu walioweza kuishi katika ndoto zao kila mmoja atakuambia ni lini alipopata kikwazo kikuu ambacho hatasahau, wengine walikataliwa kuwa hawawezi, wengine walikosa hata uwezo wa kutimiza ndoto zao, lakini wote hao ambao wamefanikiwa japokuwa walikutana na vikwazo hivyo, watakuambia kuwa HAWAKUKATA TAMAA. 

Hawakuruhusu vikwazo viwatawale na kuwarudisha nyuma. Walizidi kuimarika na kusonga mbele na kuzidi kushikilia nia yao.

3. Kubaliana na hali uliyonayo.
Hali uliyonayo hivi sasa inabadilika. Maisha hubadilika na hayabaki sawa milele. Hali zinapita, utazidi kukutana na watu mbalimbali, utazidi kujifunza vitu mbalimbali na maisha hayataacha kukundisha. Wapo ambao wamekata tamaa kutokana na hali waliyonao hivi sasa haiwezi kuwafikisha pale wanapodhamiria lakini wanasahau kuwa mambo hubadilika. Jambo dogo linaweza kubadilisha maisha yako yote na hukutegemea. Maisha ni maajabu. 

Kubali hali ya sasa na maisha yako ya wakati huu, shukuru kwa uhai ulio nao, marafiki wanaokuelewa, na tafuta kitu cha kushukuru nacho badala ya kujiumiza kwa mawazo na lawama. 

Kubali wakati huu wa sasa, shukuru kwa kila jambo, huku ukifanya juhudi kuhakikisha unaendeleza malengo yako. Hata kwa madogo shukuru.

4. Kushikilia yaliyopita.
Kosa lingine ambalo wengi hukosea na mwishowe kushindwa kutimiza malengo yao ni kushikilia wakati uliopita. Bado wanaishi kwa kuwaza makosa waliyoyafanya, mazuri waliyopoteza n.k. Wakati uliopita ulishapita, wakati uliopo ndio wakati ambao unakupa nafasi wewe kujirekebisha na kuishi vyema. Wakati ujao nao unategemea wakati huu wa sasa kutabirika. Kama wakati huu wa sasa unautumia vyema na kuweka malengo utasonga mbele. 

Kumbuka hakuna kiasi cha majuto ya wakati uliopita kinachoweza kubadili yaliyopita na hakuna kiasi cha wasiwasi kuhusu wakati ujao ambacho kinaweza kuubadili wakati ujao bali wakati huu wa sasa ndio pekee kwetu sisi. Jifunze kwa yaliyopita na zidi kusonga mbele.

 5. Kusahau kujitunza.
Wengine husahau hata kutunza miili yao, kula kwa afya, mazoezi, na kuhakikisha wana afya ya mwili, akili na roho. 
Huwezi kufurahia matimizo ya ndoto zako kama una afya mbaya, kama umezungukwa na tatizo. Usikubali kupoteza uhai, kuharibu afya yako, au kufanya ambacho kinaashiria huwezi kujitunza na kujithamini. Unapaswa kujijali na kutambua kuwa nawe unastahidi kujijali badala ya kujali ndoto/malengo yako tu.

TAFUTA MSAADA IKIWEZEKANA
6. Kusubiri msaada ukusaidie.
Wapo ambao wanaamini bila kusaidiwa hawawezi kutimiza ndoto zako. 
Labda nitoe mfano mzuri, unaweza siku moja ukakutana na mtu na kutokana na kujitambua kwako ukaweza kuweka urafiki mzuri na mtu yule. Kumbe mtu yule anafahamiana na fulani ambaye naye kuna kitu ulichokuwa unahitaji sana kusaidiwa na anakuunganisha na mwishowe unajikuta umepata mtu wa kukusaidia kutimiza ndoto zako. 

Sio kwamba hali ya kusaidiwa haitokei bali hutokea, kumbuka Mungu hana mikono kwamba itashuka mikono mawinguni na kukupa unachotaka bali ulimwengu ukitaka kukupa kitu fulani au huduma fulani hutumia wanadamu wenzio kukufunza na kukusaidia. Badala ya kutegemea msaada bali endelea kuishi vyema, heshimu kila mmoja awe wa chini yako au wa juu yako. Ishi na watu vyema na ishi katika haki. Haimaanishi ukifanya hivi itakusaidia moja kwa moja bali itasaidia njia yako ya kutimiza ndoto zako kwa kukuweka katika amani na watu. 

Wengine husubiria mpaka wawe na pesa kutimiza malengo yao, wakati wakiwa hawana uwezo wa kutimiza malengo yao wanaacha ndoto zao. Kiukweli unaweza pia kila siku ukafanya jambo moja ambalo linahusiana na ndoto zako, hata kama ni dogo lakini siku yako imepita vyema kwa kuiishi katika ndoto yako.

7. Kujisikia vibaya watu wakikusema vibaya.
Fahamu kuwa watakuhukumu (watahukumu kwa mabaya au kwa mema), kwani wanadamu wengine hupenda kuhukumu watu na kuwazungumzia watu, lakini ukipoteza raha yako kuwaza watakuhukumu vipi utakuwa mtumwa. Sio vibaya kusikiliza watu wanavyokuhukumu, lakini ni vibaya pale mtu anapokuhukumu vibaya na wewe kumchukia, mpende na jifunze uimara kupitia yeye, kwani changamoto hiyo ipo kwa ajili ya kukuweka imara na kuzidi kuongeza upendo kwa wanaokusema vibaya.
Shukuru kwa kila jambo na jiamini. 

8. Kushikilia mambo hasi.
Ni vigumu kuwaza mambo chanya au hasi kwa pamoja, bali unaweza kuwaza au kushikilia moja. Kumbuka mawazo na fikra zako huumba. Pale unapoona unawaza mambo katika upande chanya basi badili mtazamo wako na jaribu kuwaza katika upande wa hasi.

Wengi wanawaza kuwa "ni vigumu kufanya hivi", "Ukifanya hivi utashindwa", "Wewe huwezi", "Unajidanganya" n.k. Mawazo haya hayajengi bali huzidi kukupa hofu. Unapowaza mambo chanya hupelekea mambo chanya kutokea na unapowaza mambo hasi hupelekea hasi kutokea. Kila njia moja ina umuhimu na kila njia inakupeleka katika upande tofauti.

Badala kuwaza mabaya na kushikilia imani duni weka msimamo wako katika njia sahihi. Usikubali kuwaza mabaya wakati wote. Usikubali hofu, wasiwasi, hukumu, maneno, mawazo mabaya yakutawale. 

Unapoweka akili katika mawazo hasi unaipa nafasi ya kukuonyesha njia.

9. Kujilinganisha na wengine.
Kujilinganisha hupelekea "wivu" na "tamaa". Usikubali kujilinganisha na watu wengine, usikubali kuweka tamaa ya kutamani maisha au hali ya mwingine. Sheherekea mafanikio ya mwenzio lakini sio utamani na kutaka kuwa kama yeye, bali jifunze kupitia kwake na wewe uwe kama wewe. Kila mmoja ana safari yake ya maisha, ndio maana uhai ukajigawanya katika personality mbalimbali.
Hata wewe ukijiangalia kuna anayetamani kuwa kama wewe, kuna ambaye hajafika ulipofika wewe, kuwa wewe kama wewe huku ukifurahia mafanikio ya wenzio na sio ushindani, wivu, tamaa n.k.
10. Kutaka Watu Wakukubali Kwa Ndoto Zako.
Usifanye kitu ili watu wakuone mjanja au watu wakusifie bali weka malengo yako kwa nia ya kujiendeleza wewe na kuendeleza wanaokuzunguka. Ukitaka watu wakukubali ukitimiza ndoto zako utakuwa unaishi kama mfungwa. Jikubali kwanza wewe na hakikisha unaishi katika ndoto yako wewe kama wew
Fahamu unataka nini, weka nia kwa unacholenga, na tumia ulichonacho na kila nafasi uliyonayo kufika unapopanga.

Makala  hii imeandikwa na Apolinary Protas wa JITAMBUE SASA . Unaweza kujifunza zaidi kuhusu maisha na mafanikio, kwa kutembelea blog yake www.jitambuesasa.blogspot.com. Kwa mawasiliano zaidi wasiliana naye kwa email jitambuesasa@gmail.com

Oct 19, 2015

Mambo 6 Ambayo Watu Wasio Na Mafanikio Wanayafanya Kila Wakati.

No comments :
Kitu kikubwa kinachotofautisha watu wenye mafanikio na wale wasio na mafanikio ni fikra, tabia na yale mambo ambayo wanayafanya kila siku. Watu wenye mafanikio yapo mambo ambayo wanayafanya kila wakati na ambayo huwapelekea kufanikiwa kwao. Na watu wasio na mafanikio yapo mambo pia ambayo wanayang’ang’ania kuyafanya na yanapelekea kushindwa kwao.
Kwa hiyo kama katika maisha yako hujafikia viwango fulani vya mafanikio unayoyahitaji, tambua kabisa kuna mambo ambayo umekuwa ukiyang’ang’ania sana na yamekufikisha hapo ulipo. Hivyo, kama unataka kufanikiwa na kutoka hapo ulipo huna haja ya kujilaumu sana, ni kitendo cha kuamua na kuchukua hatua ya kuachana na mambo yanakurudisha nyuma.
Kwa haraka haraka naomba nikutajie mambo ambayo  wasio na mafanikio wanayafanya kila wakati.
1. Kulalamika.
Watu wasio na mafanikio mara nyingi ni watu wa kulalamika sana. Utakuta wanalalamikia hiki mara kile na mwisho hujikuta wakishindwa kuchukua hatua na kubaki kama walivyo. Hili jambo ambalo hulifanya karibu kila siku kwa kulalamikia hata mambo madogo ambayo wanauwezo wa kuyabadili. Na kwa kulalamikia huko sana, hujikuta wakishindwa kufanikiwa.

ACHA KUWAZA HASI KILA WAKATI

2. Kuwaza hasi.
Fikra na mitazamo ya watu wasio na mafanikio mara nyingi zipo hasi sana. Karibia kila kitu wanakiona kwa mtazamo hasi. Hata suala la mafanikio kwao wanakuwa wanaona ni suala la wengine sio lao. Kwa mitazamo hiyo huwafanya wazidi kuona kila kitu hakiwezekani ikiwa pamoja na mafanikio yao. Kwa kuendelea kujenga fikra hasi, hivyo ndivyo ambavyo hujikuta maisha yao wakiyabomoa bila kujijua.
 3. Kupoteza muda.
Kati ya kitu ambacho hakina thamani sana kwa watu wasio na mafanikio ni muda. Matumizi yao ya muda ni mabovu utafikiri wao wana saa 48 kwa siku. Na kutokana na sababu hii ya kupoteza muda hovyo, maisha yao hubaki kuwa ya hovyo. Kwa sababu hakuna wanachokuwa wanakizalisha katika muda mwafaka. Muda mwingi wanakuwa wanapoteza katika mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana.
4. Kupuuza.
Siku zote watu wasio na mafanikio maisha yao ni ya kupuuza mambo mengi ambayo kama wangeyafatilia yangewaletea mafanikio makubwa. Ni watu ambao wanapuuza kwa kudharau sana biashara ndogo ingawa hawana. Hiyo haitoshi wanapoteza pesa kwa matumizi yasiyo ya msingi kwa kuona si kitu. Utakuta haya ndiyo maisha yao kwa sehemu kubwa wanaishi kwa kupuuza mambo madogomadogo ambayo baadae yanawarudisha nyuma kimafanikio.
5. Kujenga uadui.
Pia hiki ni kitu ambacho watu wasio na mafanikio wanacho. Mara nyingi ni watu wa kujenga uadui na watu waliofanikiwa. Maisha yao yanakuwa yamejaa roho mbaya ambazo hazitaki kuona wengine wakifanikiwa. Kwa ubinafsi huo wanaoutengeneza mara kwa mara, huwafanya washindwe kujifunza kutoka kwa watu walio na mafanikio. Na matokeo yake hujikuta maisha yao yakizidi kuwa magumu.
6. Kuficha ukweli wa mambo.
Siyo rahisi kwa watu wasio na mafanikio kuweka wazi ukweli wa maisha yao, hata inapotokea pale wanapohitaji msaada wa kweli. Hawa ni watu ambao ni wasiri sana na hujifanya wana mafanikio kumbe hawana. Na Hili ndilo kosa kubwa wanalolifanya ambalo linawatesa na kuwafanya wakose msaada wa kile wanachokitaka katika maisha yao ya kila siku.
Kwa vyovyote vile, maisha uliyonayo sasa, yanatupa picha nzima ya kile unachokifanya mara kwa mara. Ikiwa maisha yako ni ya mafanikio, endelea kung’ang’ania mambo yaliyokupa hayo mafanikio. Lakini, ikiwa maisha yako ni ya kushindwa inabidi ubadili mwelekeo haraka sana na kuacha kushikilia mambo yanayokurudisha nyuma. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo ambayo watu wasio na mafanikio huyafanya sana katika maisha yao.
Tunakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika. Kumbuka TUPO PAMOJA.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,

Oct 16, 2015

Hizi Ndizo Athari Mbovu Za Malezi Kwa Watoto Wetu.

No comments :
Tumekuwa tukishangaa au kama siyo kushangaa, kukerwa na kuachiwa maswali na tabia hii. Inasemekana wasichana wa mijini wanadanganyika kirahisi sana zaidi kwa magari. Utakuta msichana anakubali kuwa na uhusiano na mwanamume kwa sababu amegundua kwamba, ana gari.
Lakini, wengine wanajua kabisa kwamba, gari siyo la huyo mwanamume, lakini hujikuta wakikubali kuwa na uhusiano naye kwa sababu ya gari tu. Ndiyo maana madereva wengi, hasa wale wa teksi wanajisifu kwamba, wanawake wanawapapatikia sana. Kuna ukweli wa aina fulani.
Lakini, je wasichana ni  wote ambao wanawapaptikia madereva au watu wenye magari? Ndilo swali gumu sana kwenye suala hili. Kila kitu kinachohusu uhusiano wa kimapenzi, tunajifunza kutoka kwa wazazi au walezi wetu, labda asilimia 10 tu ndiyo tunajifunza nje ya nyumbani.
Siyo suala la gari peke yake, bali ni suala la karibu kila kitu. Je watoto wetu tunawajengea dhana gani kuhusu kila kitu kwenye maisha? Halafu tunawaambia kitu gani kuhusu kupenda? Siku zote na tulio wengi, tunawaambia watoto wetu uongo mwingi sana.
Uongo huo unatokana na sababu nyingi. Kwanza, nasi tulidanganywa na wazazi wetu. Pili hatujiamini. Tatu, hatuna uhakika sisi ni akina nani na nne, tunadhani uongo huo utawasaidia watoto kuwapa moyo.

Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba, wasichana wanaobabaikia magari ni wale ambao wamelelewa  kwenye malezi ya uongo mtupu.
Unaweza kudhani wale waliotoka kwenye familia maskini ndiyo ambao wanababaikia magari, hapana. Msichana anaweza kutoka kwenye familia maskini na asibabaikie utajiri wala mali ya mtu. Wako wengi wa aina hiyo.
Kama nyumbani, wazazi wanasifu wenye magari, wanaonesha kwamba, ukiwa na gari ndiyo unakuwa na maana, kwamba, gari ni kiwango cha juu cha mafanikio, unatarajia kitu gani kutoka kwa watoto? Kuna wakati wazazi wanasema, ‘ameshafika mbali siyo mwenzio, yule ana akili bwana. Ana magari mawili na nyumba tatu’
Wakati mwingine inatosha mara moja tu jambo kusemwa na mzazi na mtoto kuamini, kwamba, mwenye gari au magari na nyumba, ndiye aliyekamilika, ndiye mwenye akili.
Kumbuka, mtoto anaingiza akilini mwake maarifa kutoka kwa watu anaowaamini na anaokutana nao maishani. Kwenye suala la uhusiano, wazazi ndiyo wanaoaminika zaidi.
Kwa sababu ya umaskini wetu tulio wengi, gari na nyumba ndiyo tunayoyachukulia kuwa ni malengo ya juu kabisa kuyapata. Kwa hiyo mtoto anakuwa ana akili ya aina hiyo , kigezo chake kuhusiana na mtu kitakuwa ni gari na nyumba au mali kwa ujumla.
Kwake, binadamu, mwenye maana na anayefaa ni yule anayemudu kumiliki vitu hivyo, hii siyo kwa wasichana peke yake, bali hata wanaume, kama mtoto wa kiume alioneshwa thamani ya mtu inatoka kwenye gari, nyumba, na mali, naye bila shaka atakuwa anababaikia vitu hivyo.
Linapokuja suala la uhusiano, anajitahidi kumwonesha msichana kwamba, anavyo vitu hivyo au anao uwezo wa kuvimiliki. Anafanya hivyo, kwa sababu, aliambiwa thamani yake inakuwepo pale anapokuwa na vitu hivyo.
Wazazi wengi wameegemeza thamani zao kwenye vitu, badala ya wao wenyewe. Bila hiari yao wanawafundisha watoto watoto wao kujali na kuthamini vitu, badala ya utu wao. Kwa kadri mfumo wa maisha ulivyokuwa ukiendelea, ukilinganisha na zamani, utagundua binadamu alijitoa thamani na kuiweka kwenye vitu, hasa mali.
Bahati mbaya, wale watoto wa wazazi ambao wana maisha ya kati, ndiyo ambao wanasumbuliwa sana na mali. Kwa nini? Wazazi hao hawajui kama wako juu au chini kimapato.
Katika kujitafuta hufanya mambo na kutoa kauli zenye kuonesha kwamba, maisha ni mali, basi. Wazazi walio chini kabisa, wanaweza nao kuwaathiri vibaya watoto kwa kuzungumza na kutenda kwa njia ambayo watoto wataamini kwamba, umaskini huondoa kabisa thamani ya mtu.
Wale wa juu kabisa, wanaweza wasifikirie kuwa gari au nyumba ni mambo ya maana sana, hata kama wamefundishwa kuhusu mali. Wao watafikiria mali kwa mkabala mkubwa zaidi.
Labda watafikiria kuhusu ndege ya kutembelea, boti ya kifahari na mengine. Lakini, yote ni ileile, kuamini mali ni kubwa kuliko thamani ya binadamu. Mali ambayo unaitengeneza na kuitafuta mwenyewe iwe kubwa kuliko wewe.
Wazazi ambao wanakuchukulia mali kwa ujumla, kama kitu cha kawaida sana, ambacho uwe nacho au usiwe nacho, maana ya maisha haibadiliki, na thamani yako haiondoki, hawa ndiyo ambao watoto wao tunawapenda.
Nikisema tunawapenda, nina maana kwamba, ni watu ambao kwao, kila binadamu ana thamani bila kujali anamiliki au hamiliki kitu gani. Wazazi ni wepesi sana kusema, ‘hawa watoto wetu nao, wakiona mwanamume ana gari, basi wanamkubali tu, bila hata kuchunguza’
Lakini, nyumbani akina mama kauli zao ni hizi; ‘ukiwa na gari na wewe mbele ya watu unasimama ati’ halafu wanatarajia mtoto anayesikia kauli hizo aje ajue kuwa ana thamani kuliko gari. Hizo ni ndoto za mchana.
Ni wazazi hawahawa ambao hawaishi kusema, ‘umefanya kazi miaka yote, hata nyumba wala gari huna, una akili kweli wewe?’ watoto wanasikia, wanaamini kwamba, asiyemiliki nyumba au gari hana akili. Halafu leo watoto wetu wakiyumbishwa na vitu hivi hadi wanakuwa kama vichaa, tunashangaa.
Nakutakia siku njema iwe ya ushindi kwako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.






Oct 15, 2015

Kama Na Wewe Utazidi Kung’ang’ania Fikra Hizi, Umaskini Ni Halali Yako.

No comments :
Katika hali ya kawaida, fikra ulizonazo ndizo zinazoamua maisha yako yaweje. Kama unafikiria chanya ni wazi maisha yako yatakuwa ya mafanikio, lakini kama pia utakuwa na fikra hasi nalo hilo halina ubishi ni lazima utaishia kwenye umaskini tena wa kutupwa. Je, wewe binafsi huwa una mawazo gani? Yakukufanikisha au kukwamisha?
Wengi  wanakwamishwa sana na mawazo yao badala ya kuwasaidia. Utakuta ni watu wa kulalamikia sana watu wengine lakini ukija kuchunguza kinachowatesa ni mawazo yao na si kingine. Mara nyingi huwa nashangaa sana hasa pale ninapokutana na watu wengi wakiwa na fikra  kama za kutaka kusaidiwa sana katika maisha yao. Bila shaka umeshawi kuliona hili, tena nina uhakika sana tu.
Hizi ni moja kati ya fikra au mawazo mabovu yanayowarudisha watu wengi nyuma sana kimafanikio. Wengi wanafikra hizi sana za kutaka kusaidiwa badala ya kusaidia. Kila mmoja anakuwa anajitahidi sana kufikiria namna atakavyoweza kusaidiwa na ndugu yake, serikali, mfadhili au tajiri fulani. Ni jambo la ajabu sana kuona watanzania wengi wanafikra kama hizi.
Tangu tukiwa wadogo tumefundishwa kwamba, maana ya ndugu ni kusaidiwa naye, siyo kumsaidia. Tunakuja kujua kuhusu kumsaidia ndugu, pale tunapokuwa watu wazima na kuwa na uwezo ambao unawafanya hao ndugu kutujia kutuomba msaada. Lakini muda wote huwa tunajua kwamba, wajibu wetu ni kusaidiwa.

Kwa hali hiyo, tumejengewa dhana kwamba, serikali inawajibu wa kutusaidia na ndugu na jamaa zetu wapo kwa ajili ya kutusaidia. Hivyo tunasahau kwamba, ni wajibu wetu kusaidia kuliko kusaidiwa.
Kuna msemo maarufu sana duniani ambao uliwahi tolewa na Rais wa zamani wa marekani kwamba, kabla hujauliza nchi yako imekufanyia nini, jiulize wewe umeifanyia kitu gani nchi yako. Msemo huu una mantiki kubwa sana ndani. Lakini pia kabla hujadai ndugu yako akusaidie, jiulize wewe umewahi kumsaidia nani maishani mwako? Kwa kawaida, wasiosaidia wala kujisaidia, ndiyo wanaodai sana kusaidiwa.
Ni jambo la kusikitisha kwamba, kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo watu wengi wanazidi kuamini kwamba, wajibu wao ni kusaidiwa na kamwe kusaidia hakuwahusu. Kwa hali hiyo, mtu anakwepa kulipa kodi, halafu analaumu barabara haihudumiwi, hakuna dawa hospitalini au hakuna huduma za jamii kwa ujumla.
Kuna watu ambao kazi yao kubwa ni kuwalaumu ndugu zao kwamba, hawataki kuwasaidia, kuilaumu serikali kwamba, haiwajali, bila kujiuliza ni nani aliwaambia kuna kudai haki bila wajibu.
Inabidi kila mmoja atimize wajibu wake, ili kuomba haki kwake liwe ni suala lenye mashiko. Kuomba haki bila kutimiza wajibu ni aina ya ukichaa. Wajibu wa kila mmoja wetu ni kuuliza yeye amesaidia wapi, amemsaidia nani, na amesaidia nini, na siyo amesaidiwa na nani, lini na wapi.
Siyo suala la mzaha kwamba, wengi wanazidi kuwa wataalamu wa kuomba, wataalamu wa kusubiri kusaidiwa wafanyiwe, bila wao kujiuliza mchango wao kwenye kutenda ambayo yatawasaidia wengine hata serikali pia. Kuna haja ya kubadilika kwani tunaelekea kuchelewa. Na ndio maana kama unandelea kung’ang’ania fikra hizi, mafanikio kwako yatakuwa ni ndoto za mchana.
Tuanze kujifunza na kuwafundisha watoto wetu kwamba, wajibu wao ni kusaidia na siyo kusaidiwa. Ni lazima tuwafundishe kwamba, wasione aibu kusaidiwa, lakini wasiishi kwamba, kusaidiwa ndiyo wajibu wao.
Ni lazima tuanze kujifunza kuwajibika badala ya kudai haki kwanza. Kwa kujifunza kuwajibika, tunajikuta tukisaidia badala kuishi kwa kusubiri kusaidiwa.
Nakutakia mafanikio mema na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.