google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jun 29, 2015

Kama Unataka Kuishi Maisha Ya Furaha Na Mafanikio? Hakikisha Unafanya Uchaguzi Huu Katika Maisha Yako.

No comments :
Maisha uliyonayo yanaweza yakawa mazuri sana ama mabaya kutokana na aina ya uchaguzi unaofanya juu ya maisha yako kila siku. Mara nyingi uchaguzi tunaofanya katika maisha yetu ndiyo huwa unaamua zaidi maisha yetu yaweje. Kama uchaguzi unaofanya ni mbaya, ni wazi maisha yako yatakuwa mabaya na kama uchaguzi wako ni mzuri basi maisha yako yatakuwa mazuri hivyohivyo hakuna atakayezuia hilo.
Kwa kuwa uchaguzi wowote tunaofanya katika maisha yetu unakuwa una athari ni vizuri tukawa makini kidogo na uchaguzi wa mambo tunayofanya kila siku. Nikiwa na maana kuwa inatakiwa tujue kama kuna jambo tunalifanya ni muhimu kutambua lina athari zipi kwetu. Kama tumeamua kufanya kitu fulani tuanze kwa kutafakari matokeo yake kwanza. Hivyo ndivo tunavyotakiwa kufanya ili kuwa na uchaguzi sahihi katika maisha yetu.
Kwa uchaguzi sahihi tutazidi kufanya maisha yetu kuwa bora siku hadi siku. Ikumbukwe pia kila kunapokucha tunanya aina nyingi sana za chaguzi ambazo zinaamua hatima ya maisha yetu. Mara nyingi huwa ni watu wa kuchagua mavazi, nguo za kuvaa, njia na mambo mengineyo mengi. Sasa ikiwa tunachagua mambo haya, kwanini tusiwe na uchaguzi juu ya maisha yetu? Je, unajua ni aina gani ya uchaguzi sahihi tunaotakiwa kuufanya katika maisha yetu ili kufanikiwa zaidi?
 1. Chagua kuishi sasa.
Hii ndiyo siri ya wewe kuweza kufurahia maisha yako. Hautaweza kufurahia maisha yako na kuyaona katika uzuri wake halisi ikiwa unaishi kwa fikra sana za siku ziliyopita ama siku za nyuma zaidi. Kwa kuishi kwako sasa, kuishi kwa kutokuwa na hofu sana juu ya kesho yako, hapo utakuwa unafanya uchaguzi sahihi utakao weza kubadilisha maisha yako na kuwa ya furaha na yenye mafanikio kwako pia.

2. Chagua kuishi maisha yasiyokuumiza.
Acha kuishi maisha ya kuumiza utaumia sana. Ili kufanikwa kwa hili, jifunze kutokuyachukulia mambo kwa ujumla ili usiweze kuumia zaidi. Ikiwa mtu atakwambia wewe ni mbaya, hufai hiyo yote inaweza ikawa sawa kulingana na mtazamo wake. Hapo lakini wewe usije ukachukulia huo ndiyo ukweli na kuanza kuumia na kujiona kweli hufai. Fuata ukweli ulio ndani yako kuhusu wewe na siyo vinginevyo.
 3. Chagua kuishi maisha ya ukarimu.
Haijalishi mtu amekufanyia nini katika maisha yako kitu kikubwa cha kujifunza nikuwa mkarimu kwa wetu wengine. Unapokuwa mkarimu unakuwa unaishi maisha ya utulivu ambayo mara nyingi yanakuwa hayana msuguano zaidina wengine katika maisha yako. Kwa kuishi maisha hayo yatakusaidia kukupa furaha na nguvu ya kufanikiwa. Hivi ndivyo unavyotakiwa kuishi na kuwa hivyo.

4. Chagua kuishi kwa kufanya mambo yako kwa uchache.
Ikiwa utajifunza kumudu tabia hii basi utaweza kuishi maisha safi ya furaha ambayo wewe mwenyewe utakuwa ni wazi unayafurahia kwa vyovyote vile iwavyo. Jifunze katika maisha yako kuongea kidogo na kuwa msikilizaji sana. Jifunze pia kula chakula kiasi ili kukujengea afya bora zaidi. Mambo mengi jaribu kuyafanya kwa kiasi hiyo itakuwa ni siri mojawapo ya kuweza kukupeleka kwenye mafanikio.
 5. Chagua kufanya mambo mapya.
Hautaweza kufanikiwa kama utakuwa unafanya mambo yaleyale siku zote. Ili kuweza kufanikiwa unalazimika kuchagua kufanya mambo mapya ambayo hujayazoea. Katika kufanya mambo mapya ni lazima kujitoa mhanga na kukabiliana na kila aina ya changamoto ili kuweza kufanikiwa, vinginevyo itakuwa ni ngumu sana kuweza kumudu kuleta mafanikio tunayoyataka katika maisha yetu.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Jun 27, 2015

Kilimo Bora Cha Bilinganya.

No comments :

Bilinganya  imo  katika   jamii   ya  mimea   inayohusisha   nyanya,  pilipili,  viazi  mviringo  na  nyanya  mshumaa.    Mboga  hii  ina   viini lishe  muhimu   kama  vile    madini  aina   ya  chokaa  na  chuma,  Vitamini  A,  B   na   C,  wanga,   protini  na  maji.    Mboga   hii    hutumika   kutengeneza  supu  au   kama  kiungo   katika  vyakula  mbalimbali.

Vilevile    huweza    kuhifadhiwa   kwa  kukatakata   vipande  na  kuwekwa  kwenye  makopo.


MAZINGIRA:
Zao    hili huhitaji   hali  ya  joto  la wastani,   udongo   wenye  kina  kirefu  na   rutuba   ya  kutosha  na  usiotuamisha   maji.  Kwa  kawaida   bilinganya   hulimwa  zaidi  ya  msimu  mmoja,    lakini    katika  nchi  za    Kitropiki  (joto)   zao   hili  hulimwa  kwa  msimu   mmoja.

 AINA:
Aina   za      bilinganya   zinazolimwa   kwa  wingi    katika   nchi  za  ukanda   wa   joto  ni  kama   zifuatazo;-
·        Black  Beauty:
Aina   hii   huzaa   sana,    matunda    yake  meusi,   makubwa,   na  ya  mviringo

·        Florida   Market.
Matunda    ya   Florida   Market  yana  umbo   la  yai.    Aina    hii    pia  huzaa   sana,    lakini   hushambuliwa  kwa   urahisi  na  ugonjwa  wa  mnyauko   bakiteria  (Bacterial   wilt)

·        Florida    High    Bush.
Matunda   yake  ni   makubwa  yenye    umbo   la   yai   na  rangi  ya  kijani  kibichi   iliyochanganyika   na  nyeusi.

·        Newyork Spineless.
Matunda       ya  Newyork     Spineless    ni  ya   mviringo,   makubwa  na  yana   rangi  ya  ya  zambarau.

·        Peredeniya.
Aina   hii   huzaa   sana,  matunda    yake  ni   makubwa  kiasi   na  yana   umbo  la  yai.

Aina   zingine    za  bilinganya   ni  matale,    Kopek  na   Rosita. Aina   hizi  huvumilia    sana  mashambulizi    ya  ugonjwa   wa  mnyauko   bacteria.


 KUOTESHA   MBEGU:
Mbegu    huoteshwa     kwanza   kwenye    kitalu  na  baadaye   miche   huhamishiwa     shambani.    Kabla    ya  kusia   mbegu,  tengeneza     tuta  lenye  upana  wa  mita  moja     na  urefu   wowote. Weka    mbolea  za   asili  kama    vile  samadi    au   takataka  zilizooza  vizuri,  kiasi  cha  ndoo    moja  au   mbili  katika    eneo  la  mita  mraba  moja.   Sia  mbegu  kiasi  cha   gramu  mbili  mpaka  tatu  (nusu   kijiko  cha  chai   chenye   ujazo   wa  gramu   tano)   katika  eneo   hilo.


Gramu  500  za  mbegu   zinatosha   kupandikiza  katika  eneo  la  hekta  moja.    Nafasi   kati  ya   mstari   na  mstari   iwe   sentimeta  10  hadi  15  na  kina  kiwe  sentimita   1.5.    Baada    ya  kusia  mbegu   fukia  na  tandaza   nyasi   kavu  na  kisha    mwagilia  maji. Endelea    kumwagilia   kitalu   kila  siku,    asubuhi  na  jioni,  hadi   mbegu  zitakapoota.    Mbegu   huota   baada  ya  siku   ya   10   hadi   12.

KUHAMISHA     MICHE:
Miche    huwa  tayari   kwa  kupandikizwa  shambani    baada  ya  wiki   sita  hadi   nane.    Wakati  huu   huwa na  urefu   wa  sentimita    15   mpaka   20   (sawa  na   urefu   wa  kalamu   ya  risasi).

Mwezi  mmoja   kabla  kupanda miche,  rutubisha   udongo   kwa  kuweka   mbolea  za  asili    zilizooza   vizuri.      Mbolea    hizi   ni  kama   samadi,  mbolea   vunde  na  mbolea    ya  kuku.

Weka    kiasi  cha   tani   10  hadi  20  kwa  hekta.    Kiasi   hiki  ni  sawa  na   kuweka  ndoo     moja  hadi  mbili    zenye ujazo   wa  lita  20  katika  eneo  la  mita  mraba  moja.    Mbolea   ya  mchanganyiko    aina  ya  N.P.K   yenye  uwiano    wa   20:10:10    huwekwa   kwenye  shimo    wakati  wa  kupandikiza  mche.  Kiasi    kinachohitajika    ni  gramu  tatu  hadi   tano   (sawa   na  nusu   kijiko  mpaka   kijiko  kimoja   kidogo   cha  chai)   kwa  kila  shimo.

Nafasi    ya  kupandikiza    hutegemea   aina   ya  bilinganya.   Aina   ndogo  hupandikizwa     katika  nafasi   ya  sentimita   80  mpaka   100 kutoka   mstari hadi   mstari  na  sentimita   50   mpaka   60  kutoka  mche  hadi  mche.  Aina    kubwa   hupandikizwa  katika  nafasi  nafasi    ya  sentimita  80   mpaka   100  kutoka  mstari  hadi  mstari na    sentimita    80   mpaka  90 kutoka  mche  hadi  mche.     Kazi    ya  kuhamisha    miche   ifanyike   kwa   uangalifu  mkubwa    ili  kuepuka   kuikata  mizizi.


KUTUNZA  SHAMBA:
·         Kuweka   matandazo.
Mara   baada  ya  kupandikiza  miche,    tandaza   nyasi   kavu.   Matandazo  husaidia    kuhifadhi   unyevu,  huzuia   magugu   yasiote  na   huongeza   rutuba   ya  udongo.

·        Palizi.
Hakikisha    shamba    ni  safi   wakati  wote  ili  kuzuia   ushindani    wa  chakula,   maji  na   mwanga  kati  ya  mimea  na  magugu.   Usafi  wa   shamba   pia  huondoa    maficho  ya  wadudu   waharibifu   na  huzuia  kuenea   kwa   magonjwa.

·        Mbolea.
Mbolea    ya  kukuzia  aina  ya   S/A   huwekwa    wiki  tatu  baada  ya   mmea   kuanza    kutoa  maua.   Kiasi   cha  gramu   tatu  hadi   tano  kuwekwa    kuzungukia    kila  mche.   Mbolea    iwekwe    katika  umbali   wa  sentimita   tano  mpaka   15   kutoka    kwenye  shina,   hutegemea  ukubwa   wa  mche.    Hakikisha   mbolea  haigusi  mmea.

·        Kukata  kilele.
Wiki  mbili  baada   ya  kupandikiza     miche,    kata  sehemu  ya   juu  ya  mmea (kilele)  kama   umepanda  aina   ndefu  ya  bilinganya.  Hii    itasaidia    kupata   matawi   matatu  hadi  manne   na  mmea    kutengeneza   kupata  matawi  matatu  hadi  manne  na   mmmea   kutengeneza  umbile  la   kichaka.    Matawi    yakizidi   manne  yaondolewe    ili kupata    mazao  mengi   na  bora.

·        Kumwagilia.
Zao    la  bilinganya     hustawi   vizuri   likipata   maji  ya  kutosha.  Umwagiliaji     ufanyike    kila  siku    asubuhi  na  jioni  kutegemea  hali    ya  hewa.

Kuzuia    Wadudu    Waharibifu   na  Magonjwa.
Wadudu    Waharibifu:

·        Vivyatomvu      wa  Bilinganya   (Eggplant   Lacebugs)
Wadudu    hawa    hushambulia   zaidi    sehemu  ya   chini  ya  jani.    Hufyonza  utomvu   wa majani   na  kusababisha   majani    kuwa   na   mabaka   meupe  au  njano.     Mashambulizi     yakizidi   majani    huanguka  chini.    Vinyatomvu    wanaweza    kuzuiwa  kwa    kunyunyizia     moja  ya  dawa   zifuatazo;-
Deltamethrin   (Decis), Dimethoate  (Sapa  Dimethoate)   Fenvalerate (Sumicidin),  Lambda  -  Cyhalothrin (Karate).

·        Vidukari   au  wadudu   mafuta  (Cotton    Aphids)
Hawa  ni    wadudu     wadogo     wenye     rangi    nyeusi.   Hushambulia    majani  machanga  na    kuyasababisha     kudumaa   na  kukunjamana.    Zuia   wadudu   hawa     kwa   kutumia    mojawapo     ya  dawa   zifuatazo;-
Dimocron  50%  E.C,   Lambda  - Cyhalothrin  (Karate) Dichlorvos  (Nogos).

·        Utiriri   wa  Mimea  (Red    Spider   Mites).
Ni   vidudu   vidogo    vyenye    rangi   nyekundu   iliyoiva. Hushambulia     majani  kwa   kufyonza    utomvu.  Majani   yaliyoshambuliwa    huonyesha    utando    kama   wa  buibui.    Mashambulizi   yakizidi    mea   hudumaa,  majani   hukauka    na   hatimaye   hufa.

Utiriri     unazuiwa    kwa    kutumia     dawa  zifuatazo;-   Acrex,  Karathane 25%   W.P,  Dimethoate,   Ekalux,  Kelthane.

·        Minyoo    Fundo   (Root    knotnematodes).
Wadudu     hawa   hushambulia  mizizi.    Hutoa  kinyesi    ambacho  ni  sumu  kwa    mmea.    Sumu  hii    husababisha  mizizi    kuwa  na  nundu  kama    ya  mizizi  ya  maharagwe.   Mashambulizi   yakizidi    mmea   hudumaa,  hunyauka    na  hatimaye  hufa.


Njia   ya  kuzuia  wadudu   hawa  ni  kubadilisha  mazao   kwa  mfano  baada  ya  kuvuna   zao  hili,  zao  linalofuata   lisiwe  la  jamii  moja   na   bilinganya   kama  vile  nyanya,  pilipili  na   viazi  mviringo.  Pia   dawa  aina    ya   Carbofuran   (Furadan)   inaweza    kutumika.

Magonjwa:
·        Mnyauko  Bakteria  ( Bacterial  Wilt).
Ugonjwa      huu  husababishwa    na   backteria.   Mmea    ulioshambuliwa   hunyauka   ghafla    hasa  wakati    wa  jua  kali.
Mnyauko   bacteria    unaweza    kuziuwa  kwa   kubadilisha  mazao    shambani.   Endapo    ardhi  itashambuliwa      na   ugonjwa    huu   zao   la   bilinganya   lisipandwe    katika  eneo   hilo   kwa  muda    wa  miaka   mitatu  hadi  mitano.

Njia   nyingine    ni  kupanda    aina  za   bilinganya   kama  vile  Matale,  Kopek  na   Rosita   ambazo   huvumilia  mashambulizi  ya  ugonjwa   huu.

·        Phomopsis  Vexans:
Ugonjwa     huu     husababishwa    na   bacteria   na  kushambulia    majani,   shina    na   matunda.

·        Verticillium   Wilt.
Huenezwa     na  maji   na    husababisha    mmea   kudumaa,    majani   kukunjamana  na   kuanguka.

Magonjwa   ya   Phomopsis   vexans   na    Verticillium   Wilt  yanaweza  kuzuiwa  kwa   kung’oa    ma  kuchoma    moto    mimea     iliyoshambuliwa,   kubadilisha  mazao,  na  kuweka    shamba   katika  hali    ya  usafi   wakati  wote.


KUVUNA:
Bilinganya     huanza    kutoa    matunda    yaliyokomaa  baada   ya  miezi  miwili   hadi  mitatu   tangu    kupandikiza.    Uvunaji    huendelea   kwa   muda     wa  zaidi  ya   miezi  minne    na  hauna  budi   ufanyike    mapema   mara  matunda    yanapokomaa.   Matunda   yaliyokomaa    sana  hayafai      kulimwa   kwa  sababu   huwa  na  kambakamba    na  mbegu  zilizokomaa.
Vuna    mara  mbili   au   tatu   kwa  wiki,   kwa  kutumia   kisu   kikali  ili    usiumize     matunda.

 MAVUNO:
Kwa  kawaida     zao   hili     huzaa    sana   iwapo   limetunzwa    vizuri.    Shamba     lililotunzwa    vizuri    linaweza    kutoa   mavuno   tani  50  hadi   60   kwa  hekta.    Hata  hivyo    mavuno   mengi     hutegemea    aina  ya    bilinganya,  umwagiliaji    na  rutuba  ya   udongo.

§  MAKALA HII IMEANDALIWA NA SAID MALOGO, MTAALAMU WA MASUALA YA KILIMO.

MAWASILIANO 0782 396 729

Jun 26, 2015

Hizi Ndizo Athari Za Kuwa Na Maumivu Makali Kihisia.

No comments :
Nakumbuka ni hivi karibuni ambapo  ilikuwa ni majira ya jioni na nilirudi nyumbani tofauti na kawaida yangu. Siku hiyo niliamua kupitia jikoni kama kituo change cha kwanza. Nilipoingia jikoni nilimwona binti ambaye huwa tunakaa naye  akiwa  ameinamia kwenye beseni la kuoshea vyombo hapo jikoni.

Nilimsemesha na aligeuka kuniangalia bila kunijibu chochote. Mikono yake alikuwa ameiweka ndani ya beseni kama kuficha kitu lakini hata nilipomwangalia nilihisi kama alikuwa analia hivi. Nilipomsogelea na kutazama mikono yake, nilipatwa na mshtuko sana. Alikuwa ameshika kisu na mkono wake wa kushoto ulikuwa ukitoka damu. Ilionesha alikuwa amejikata.

Nilipomuuliza ni kwa nini anafanya vile huku nikiwa nimetundikiwa, alinitazama tu huku machozi yakimtoka. Siyo siri niliogopa sana. Baada ya tukio lile niliamua kumuulizia daktari kwa ufafanuzi zaidi alionipa  ndipo nilipojua hasa kuhusu jambo lile ambalo lilipelekea binti yule kuweza kujiumiza.


Ilinibidi kwa kweli, nimpeleke hospitali na tatizo nililokuja kuambiwa na daktri ni tatizizo  linalotokana hasa na mtu kukata tamaa, kuchangiwa na kuamua kujiadhibu kwa kujiumiza. Bila shaka tunajua kwamba, kukata tamaa kunapozidi na mtu anapohisi kuwa maisha hayana maana, anaweza kujiuwa.

Nilijifunza yote  hayo kutokana na tatizo alilokuwa nalo binti yangu huyu. Kujiumiza huku kunaweza kuwa ni kwa kujikata mikono, miguu au sehemu nyingine ya mwili. Wakati mwingine inaweza kuwa kwa kuvuta nywele , ung’ata kucha kwa nguvu, kujipiga au kujichubua au kukwaruza hata kidond ambacho hata kilikuwa karibu kupona.


 Ingawa siyo tatizo kubwa , kwani inakadiriwa  ni mtu mmoja tu kila mia moja anakabiliwa nalo, bado hii ni idadi kubwa ya kutosha. Ina maana kwaba kwa hapa nchini kiasi cha watu 440,000 wanakabiliwa na tatizo hilo.

Pamoja na ukubwa wa tatizo hilo kwa bahati mbaya hakuna mtaalamu ambaye hadi sasa amewahi kusema  kwa hakika tatizo hilo linatokana na nini hasa. Lakini angalau inafahamika kwamba ni juhudi ya anayejiadhibu kutaka kujihisi ahueni ya kimaisha angalau kwa muda fulani.

Bila shaka tumewahi kushuhudia au kusikia kuhusu watu wanaojikwangua, wanaojiumiza, wanaojibamiza ukutani, wanaopanda mitini na kujiangusha ili wavunjike kwa kuamini kuwa wanapata ahueni kwa kufanya hivyo. Kama tumewahi kushudia au kusikia, hii yote ni sehemu ya tatizo hili.

Mara nyingi kujiadhibu huku hufanywa kwa siri sana na wahusika. Kwa hiyo wakati mwingine inakuwa vigumu kuona kuwa anajiadhibu,  bali tunaweza kuona matokeo yake. Mtu anaweza kuona kidonda kipya kwenye mwili wa mtu au kuona nywele zimevurugwavurugwa ghafla tu ama dalili nyinginezo.

Kwa bahati mbaya, hawa watu wanaojiumiza wenyewe, ni mara nyingi huwa hawajui ni kwanini wanajiumiza, hujiumiza kwa sababu huhisi wakifanya hivyo watapata nafuu. Lakini nafuu ya nini, huwa ni swali gumu kupatiwa majibu.

Bado hata hivyo, ukweli unabaki kwamba, wanafanya hivyo kwa sababu wana maumivi kihisia. Kwa hali hiyo, kama inatokea mtu anagundua kwamba, jamaa yake ameingia mahali ambapo anajiumiza mwenyewe kwa njia yoyote, inabidi ajaribu kumsaidia akijua ni tatizo la kihisia.

Nimeshawahi kusikia kuhusu watu amao wamepelekwa kwa waganga wa asili kwa sababu ya tatizo hili. Kufika huko wakaambiwa wana wana jini anatafuta damu na kuanza kutibiwa kwa kutaka kumtoa jini huyo, hali ambayo iliwazidishia maumivu kihisia hadi wakaamua kujiua. Kumbe ambacho hawakujua  kujiumiza huko siyo majini wala nini bali hizo ndizo athari za kuwa na maumivu makali ya kihisia.

Tatizo la mtu kujiumiza mwenyewe kwa lengo la kupata nafuu, halihusiani na kulongwa au nguvu nyingine za giza. Ni tatizo ambalo kisaikolojia linaelezeka kabisa. Ingekuwa halijanipata, ningeweza kusema, huenda lina nguvu za giza ndani yake kama wengi wanavyofikiri. Lakini nimelishuhudia moja kwa moja na nalijua vizuri.

Tunakutakia kila la kheri, endelea kujifunza kila siku bila kuchoka kwa kupitia mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO lakini hakikisha unawashirikisha wengine ili kuweza kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,



Jun 25, 2015

Sababu 10 Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.

No comments :
Mara nyingi huwa inakadiriwa kuwa biashara nyingi mpya zinazoanzishwa, huwa zinajikuta  zinakufa kabla hazijafikia miaka mitano na chache huwa ndio zinazoendelea baada ya hapo. Kufa huku kwa biashara hizi huwa hakuji kwa bahati mbaya, bali huwa kunatokana na sababu kadhaa ambazo pengine huwa zinatokana na wajasiriamali wenyewe au nje ya wajasiriamali. Ni muhimu kujua sababu zinazopelekea biashara nyingi zife kabla hazijafikisha miaka mitano, ili kama upo kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ama upo kwenye biashara usije ukafanya makosa hayo na kujikuta umeua biashara yako.

Hizi Ndizo Sababu 10  Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.

1. Usimamizi mbovu.
Hili ndilo kosa kubwa huwa linafanyika kwa biashara nyingi na matokeo yake ni kuwa ni biashara za kawaida ambazo hazina mafanikio makubwa sana na mwisho wa siku kufa kabisa. Kunapokosekana usimamizi mzuri na wa kutosha, mara nyingi biashara huanza kujiendea kiholela ama kwa mazoea ya kawaida tu, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara. Ni muhimu kwa biashara ikawa na usimamizi mzuri na mipango iliyotulia ili iweze kuleta faida na mafanikio makubwa, vinginevyo itakufa.



2. Kukosekana kwa ung’ang’anizi.
Mara nyingi huwa inachukua muda mrefu kidogo kwa biashara mpya, kuweza kukuletea faida kama ulivyokuwa umepanga. Katika kipindi hiki huwa ni kipindi kigumu kwa wajasiriamali wengi, kwani ni kipindi ambacho biashara huwa inajiendesha kwa faida kidogo sana na uvumilivu wa hali ya juu huwa unahitajika. Hapa ndipo, biashara nyingi mpya huwa zinakufa ama kushindwa kuleta mafanikio makubwa, kutokana na kukosekana kwa ung’ang’anizi ambacho huwa ni kitu muhimu sana.


3. Kuweka biashara  katika eneo lisilo sahihi.
Hii ni moja ya sababu muhimu sana ambayo mara nyingi huwa inapelekea biashara nyingi mpya kufa. Unapoweka biashara yako katika eneo lisilo sahihi, mara nyingi kitakachotokea utaanza kukosa wateja na utajikuta unabaki kulaumu kuwa biashara hiyo hailipi au haifai kumbe eneo uliloweka ndilo sio sahihi. Ili kuepuka hili, ni muhimu sana kuiweka biashara yako katika eneo lililosahihi ambapo una uhakika unaweza kupata wateja, ambao watasaidia kuifanya biashara yako kuwa hai.

4. Biashara inakuwa haitatui matatizo mengi ya watu.
Lengo kuu la biashara sio kupata faida pekee, bali ni pamoja na kutatua matatizo ya watu. Kwa jinsi biashara inavyozidi kutatua matatizo mengi ya watu ndivyo inavyozidi kupata wateja wengi na faida kuwa kubwa zaidi. Hakuna biashara yoyote duniani ambayo imeendelea bila kutatua matatizo muhimu ya watu. Kama unataka kufanikiwa na kupiga hatua kwa biashara unayofanya,  ni lazima biashara yako itatue matatizo ya watu kwa sehemu kubwa.

5. Kushindwa kujifunza kutokana na makosa.
Ni ukweli usifiochika wajasiriamali walio wengi huwa ni watu wa kufanya makosa katika biashara zao. Lakini, pamoja na makosa hayo kitu pekee ambacho huwa kinawafanya wananyanyuka na kusonga mbele ni kile kitendo cha kuchukua hatua ya kujifunza na kujirekebisha kutokana na makosa hayo. Tatizo walilionalo wajasiriamali wapya, huwa ni wazito kujifunza kutokana na makosa na kujikuta ni watu wa kurudia makosa yale yale yanayopelekea kuua biashara zao.

6.Kukabiliwa na ushindani mkubwa.
Biashara nyingi mpya huwa zinashindwa kufanya vizuri sokoni kutokana na kukutana na ushindani wa hali ya juu. Kunapokuwa kuna ushindani wa kisoko, halafu wewe ukiwa kama mjasiriamali ukashindwa kusoma nyakati za jinsi gani unaweza kukabiliana hali hiyo, uwe na uhakika biashara yako haiwezi kufanikiwa sana, zaidi baada ya muda itaanza kupotea polepole na mwisho ni kufa kabisa.

7. Kutokuwa na mtaji wa kutosha.
Kutokuwa na mtaji wa kutosha katika biashara, hii pia huwa ni sababu mojawapo inayopelekea biashara nyingi mpya kufa mapema. Mtaji huwa unahusika sana hasa pale unapohitaji kuongeza pengine bidhaa ili kuweza kukabiliana na soko na wakati huohuo unakuwa hauna pesa ya kutosha. Inapotekea hali hii ya kukosa mtaji wa kutosha kwa biashara unayoifanya, hapo ndipo huwa mwanzo wa kushindwa kwenye ushindani na biashara huanzia kuyumbia hapo na baadae kupelekea kufa, kama jitahidi nyingine za ziada zisipofanyika.

8. Kunafanya biashara na watu ambao sio sahihi.
Ili biashara yako iweze kuleta mafanikio makubwa unayotaka, ni muhimu kwako kuwa na timu sahihi utakayoshirikiana nayo kukuletea mafanikio. Kwa kawaida huwa hakuna mafanikio makubwa ya mtu mmoja, ni vizuri ukashirikina na timu uliyonayo katika biashara yako ili kuleta mafanikio makubwa. Inapokosekana timu ya uhakika katika biashara, hii ndiyo huwa sababu mojawapo inayosabbisha biashara nyingi mpya kufa. 

9. Mipangilio mibaya ya bei.
Mara nyingi biashara nyingi zinazoanza huwa zinamipangilio sio mizuri ya bei kitu ambacho husababisha kuwachanganya wateja. Hili huwa linatokea pengine kutokana na kupanga bei ya bidhaa, pasipo kujali ama kuangalia ubora wa bidhaa husika, hali ambayo husababisha wateja kuingiwa na shaka na kuanza kuhama kidogo kidogo, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara kuweza kuendelea.

10. Kukosa ushauri mzuri wa Kibiashara.
Mjasiriamali unapokosa ushauri mzuri ambao ungewezakukusaidia kuifanya biashara yako ikawa hai, kinachotokea hapo ni kuua biashara. Biashara nyingi huwa zinakufa kwa sababu ya kupokea ushauri wa kila aina na kuufanyia kazi hata kwa watu ambao sio wazoefu sana wa biashara husika. Kama unataka biashara yako iweze kusonga mbele na kuleta matunda acha kupokea ushauri wa kila aina, vinginevyo utaua biashara yako.

Mwisho, zipo sababu nyingi zinazopolekea biashara nyingi mpya kutoweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa na kupelekea nyingi kuweza kufa hata kabla ya kufikisha miaka mitano. Kwa kuanzia, hizo ndizo baadhi ya sababu zinazofanya biashara nyingi kuweza kufa na kushindwa kusonga mbele kabisa. Ni muhimu kuweza kujifunza na kuchukua hatua zitakazotusaidia kuepuka makosa hayo na kuweza kufanikiwa.

Nakutakia ushindi katika biashara yako iwe ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa zaidi, yatakayoboresha maisha yako kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,




Jun 24, 2015

Nguzo Tatu Muhimu Za Mafanikio Ambazo Ni Lazima Uwe Nazo.

1 comment :
Umefika sasa wakati wa kila mmoja wetu kutambua kuwa ana uwezo mkubwa wa kutumia vipaji vilivyo ndani mwake kuweza kumletea mafanikio makubwa  maishani. Hii  nikiwa na maana kuwa inakulazimu kuweza kujua kuwa hiki kipindi tulichonacho sasa ni kipindi cha maarifa ambayo kwa sehemu kubwa yanahusisha vipaji na ubunifu mkubwa zaidi ili kuweza kufanikiwa.

Katika kipindi hiki mtu anayefanya chochote kwa sababu yoyote hawezi kufika popote. Watakaoweza kumudu mashindano ya dunia hii ya sasa, ambayo imefanywa kuwa ndogo zaidi, ni wale tu walio na maaarifa maaalum na kwa sababu maalum na siyo tu maarifa. Ninasema hivi sio kwa kukutisha na pia si maanishi uwe na elimu ya chuo kikuu ndiyo uwe na maarifa haya, unaweza kuyapata hata kama hukwenda shule.

Kwa kulijua hilo kuwa tupo kwenye dunia ya ushindani ambayo inatulazimisha kuwa na maarifa, vipaji na ubunifu ni muhimu kwetu kujipanga ili kuhakikisha mambo hayo yote matatu tunayo ili kuweza kujihakikishia kufanikiwa, kwani mambo hayo ni nguzo muhimu sana kwetu sisi na kizazi kijacho ili kujenga taifa imara lililofanikiwa.


Pamoja na umuhimu wa maarifa, ubunifu na vipaji katika suala zima la mafanikio yetu, lakini kwa bahati mbaya wazazi wengi hapa nchini hawajui au hawajali sana kuhusu vipaji. Hii hupelekea wazazi wengi kuweza kukandamiza vipaji vingi vya watoto wao bila kujua kuwa wanaua vipaji hivi vya watoto.

 
Kuna wazazi ambao huwakataza watoto wao wasiimbe kwa maelezo kwamba, kuimba ni ibilisi. Kuna wazazi wengine huweza kuwavunja nguvu  watoto wanacheza mpira, kuchora na shughuli nyingine za kisanii kwa maelezo kwamba mambo hayo huwapotezea muda wa masomo. Wasichokifahamu wazazi hao ni kwamba, huenda  hivyo wanavyofanya watoto ndivyo vipaji vyao, yaani ndiyo makusudi ya wao kuletwa hapa duniani.

Kwa watu wengi ikiwemo wazazi kama ambavyo nawaongelea hapa wanapenda au wanataka watoto wao wawe ama wafanye yale ambayo wao wazazi ndiyo wanayoyapenda bila kujali upendeleo na uwezo wa watoto. Hali hiyo ndiyo ambayo inawafanya wasomi wengi wa nchi hii kwa wasomi wa sifa na pato, badala ya kuwa wasomi wa ubunifu kwa faida ya jamii.


Kuna wasomi ambao hawakujua tangu awali kwa nini wanasoma kile walichokisoma, kwa sababu hata uchaguzi wa wasome kitu gani, ulifanywa na wazi wao, wakati mwingine, kwa kuwalazimisha. Kuna vijana wengi wenye vipaji vikubwa ambao wameshindwa kuvitumia kabisa au kuvitumia vizuri, kwa sababu vilikandamizwa utotoni.

Kama tulivyosema, umefika muda sasa ambapo wazi wanapaswa kama siyo kulazimishwa na mazingira, kujua kwa makusudi vipaji vya watoto wao ili waweze kuwasaidia kujenga kesho yenye mkabala thabiti zaidi wa kimafanikio.

Mtoto anapoonesha kipaji fulani, sisi wazazi tusikikandamize kwa sababu, hatukitaki. Anapoonyesha kipaji tumpe moyo  ili aweze kukiendeleza kwa faida yake na ya kwa wengine. Kukandamiza vipaji vya watoto na kujaribu kuwaingizia kile ambacho hakiko ndani mwao kwa hakika ni kuwaumiza bure tu.

Ifike mahali na sisi tukubali kwamba, hata sisi huenda vipaji vyetu huenda vilikandamizwa au hatukuoneshwa kwa namna nzuri ya kuvibaini na ndiyo maana pengine wengi wetu hatufurahii shughuli tunazizifanya maishani mwetu. Kwa nini nasi tulee watoto ambao watakuwa na utapiamulo wa ufahamu na matumizi ya vipaji.


Pia tutambue kuwa, tupo kwenye kipindi cha zama za maarifa ni jukumu lako kutumia nguzo tatu hizo muhimu kuweza kutufanikisha nikiwa na maana Maarifa, ubunifu na vipaji tulivyo navyo ili kufikia mafanikio makubwa. Vitu hivi vikikaa pamoja na kufanyiwa kazi vinaleta matokeo makubwa na ya kushangaza. Kwani hizo ndizo nguzo tatu muhimu za mafanikio kwako na kizazi kijacho unazotakiwa kuzijua.

Tunakutakia kila la kheri, endelea kujifunza kila siku bila kuchoka kwa kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO lakini hakikisha unawashirikisha wengine ili kuweza kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Jun 23, 2015

Hii Ndiyo Siri Ya Mafanikio Iliyojificha Kwenye Kushindwa Kwako.

No comments :
Kama kushindwa ingekuwa ndiyo mwisho wa safari ya mafanikio basi leo hii kusingekuwa na mtu ambaye angekuwa amefanikiwa. Kwa bahati nzuri sana dunia imejaa watu wengi ambao kabla ya kufanikiwa kwao walishashindwa sana. Watu hawa hawakuweza kukata tama pale waliposhindwa ila walichukulia kushindwa kwao kama fundisho na kuzidi kusonga mbele.

Ukifatilia hili utagundua kuwa watu wote wenye mafanikio makubwa  hao ndio walikuwa washindwaji  sana katika kile walichokuwa wakikifanya. Kwa maana hiyo hakuna mtu ambaye amefanikiwa sana hakuwahi kushindwa kwa namna yoyote ile. Unaweza kuthibitisha juu ya hili kwa kuangalia maisha ya Thomas Edson. Katika maisha yake alikosea karibu mara 999 kabla hajaja na ugunduzi rasmi wa balbu(glopu).

Kwa makosa aliyokuwa akiyafanya Thomas Edson aliyachukulia kama fundisho na kuamua kusonga mbele. Pengine leo hii dunia ingekuwa giza kama sio ubishi wa Edson kung’ang’ania ugunduzi wake huo wa taa mpaka ukafanikiwa. Ipo siri kubwa sana katika kukosea kwetu ambayo wengi wetu hawajui. Wengi hujikuta wanakatishwa tamaa sana na makosa yao na kurudishwa nyuma.


Kwa vyovyote vile iwavyo pale inapotokea umekosea usitoke mikono mitupu, jifunze kitu. Kwa kujifunza itakusaidia kuweza kuendelea zaidi kwa ujasiri na mafanikio makubwa. Ni mara ngapi umekuwa ukikosea na kukata tamaa, bila shaka ni mara nyingi. Kukosea kwako mara mbili, tatu, au nne kusikukatishe tamaa, wapo waliokosea zaidi ya mara elfu moja lakini walijirekebisha na kusonga mbele.

Nimekuandikia makala hii kukutia moyo kuwa mafanikio katika maisha yako yapo na yanakusubiri hata kama umeshindwa mara ngapi. Unachotakiwa kufanya ni kuwa mvumilivu kwa muda ili kuyafikia. Kama nilivyoanza katika makala hii, watu wengi wenye mafanikio walianza kwa kushindwa kwanza kisha wakafanikiwa. Hicho ndicho kitu unachotakiwa kukifanya kwa sasa badala ya kujilaumu.

Ni muhimu kujua kuwa kushindwa ama kukosea ni hatua nayo mojawapo katika safari ya mafanikio ingawa hatua hiyo huja kwa kuumiza. Tukubali kujifunza pale tunapokosea kisha baada ya hapo tusonge mbele na kuachana na tabia ya kulalamika. Kama unafikiri makosa na kushindwa kumekurudisha nyuma sana, angalia maisha ya watu hawa na kisha jifunze kitu na kuwasha moto wa mafanikio ndani yako.

1. Soichiro Honda, huyu ndiye mwanzilishi wa kampunni kubwa  ya kutengeneza pikipiki aina ya Honda. Maisha yake kimafanikio yalianzia pale ambapo alienda kuomba kazi katika kampuni ya utengenezaji wa magari aina ya Toyota na kukataliwa sana kuwa alikuwa hafai na hawezi kitu chochote akatafute kazi nyingine na sehemu nyingine.

Kwa Honda hilo halikumkatisha tamaa, aliamini anaweza na anao uwezo mkubwa ndani yake utakaomsaidia, ndipo akaamua kuanzisha kampuni yake ya Honda ambayo baadaye ikaja kuwa kampuni kubwa ya magari duniani inayoshindana na kampuni ile ya Toyota ambayo walimkataa mwanzo. Ikiwa kuna kitu cha kujifunza hapa kupitia maisha ya Honda kamwe USIKATE TAMAA kwa kile unachoamini kuwa kitakufanikisha.


 
2. Stephen king's, huyu ni mwandishi maarufu wa vitabu lakini wengi hawajui alikotokea zaidi ya kuishia kusoma vitabu vyake tu. Stephen King’s ni mwandishi pekee ambaye kitabu chake cha kwanza kilikataliwa sana na kampuni nyingi za uchapishaji alikotaka kwenda kuchapisha kwa kuambiwa kuwa hakifai. Hata hivyo  hakukata tamaa mpaka alipotimiza lengo lake.Kwa hiyo unakuja kuona kwa vyovyote hata ukataliwevipi, unao uwezo wa kubadili matokeo na kufanikiwa ikiwa unajiamini.

3. Oprah Winfrey's, katika maisha yake ya sasa huyu ni moja kati ya wanawake wenye pesa nyingi sana duniani, mhamasishaji wa mafanikio na mwendeshaji wa vipindi vya TV. Kwa kazi hiyo ya utangazaji imempa pesa nyingi sana kiasi kwamba naweza kusema ni moja kati ya wanawake matajiri duniani na mwenye umaarufu mkubwa sana. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo, Oprah Winfrey kabla hajafika hapo kituo kimojawapo cha kwanza walichomwajiri walimfukuza kazi kwa madai kuwa hafai. Hilo yeye halikuwa pigo alikaa chini na kuongeza juhudi hatimaye kufika juu kwenye kilele cha mafanikio makubwa.

4. Bill gates, huyu ni mwanzilishi wa kampuni inajulikana sana duniani ya Microsoft ni mmoja kati ya wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa sana dunia. Pamoja na hayo, lakini je? unajua kwamba wazo lake la kutengeneza kompyuta ambayo ingekuwa inatumia ‘mouse’ lilikataliwa kabisa katika kampuni alikolipeleka wazo hilo kwa mara ya kwanza?. Lakini yeye hakujikatia tamaa na wazo lake aliweza kuliendeleza na kumpa mafanikio makubwa.  Sasa ndiyo huyu Bill Gates unayemjua sasa alikotoka na kwa sasa ndiye tajiri wa kwanza duniani.


Nini cha kujifunza kupitia maisha ya watu hawa.

1. Kukataliwa au kuambiwa huwezi kitu isiwe sababu ya wewe kushindwa na kuamua kuachana na ndoto zako. Jiamini na kisha songa mbele, utafanikiwa sana tena sana.

2. Kushindwa katika kile unachokifanya sio tatizo hata kidogo, kikubwa jifunze kupitia kushindwa kwako huko. Jiulize ni wapi ulipokosea, jirekebishe na zidi kuendelea mbele kukamilisha ndoto zako.

3. Kujiamini wewe kwanza, kuwa unaweza na hakuna kitu cha kukuzuia, huo ndiyo ufunguo halisi wa kukufikisha kwenye njia ya mafanikio.

4. Watu wanaokukatalia wewe kuwa huwezi, ni wazi hawajui kitu kukuhusu wewe kwamba ni mtu mafanikio.

5. Kama ukishindwa kitu leo, haimanishi umeshindwa milele. Unaweza ukajipanga upya na kufikia mafanikio makubwa zaidi ya mwanzo.

Kumbuka, unaweza kufanikisha malengo yako yote unayotaka ikiwa utaamua na kuishi kwa vitendo na hakuna wa kukuzuia. Suala la kufanikiwa katika maisha yako siyo la bahati kama unavyofikiri. Inapotokea umeshindwa jipe moyo na kusonga mbele kwani katikati ya kushindwa ipo siri kubwa ya mafanikio yako ambayo unatakiwa kitumia na kufanikiwa zaidi na zaidi.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio iwe ya ushindi. Na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,