google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 31, 2017

Kilimo Cha Maharage Ya Njano.

2 comments :
Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.

Ekari moja ya maharage ya njano kwa maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo unalolimia.

Shamba la maharage kama unalima kwa kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi minne. 

 Upandaji wa Maharage 

1.Mbegu. 

Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.

Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.

Kuna aina nyingi za maharage ambazo zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder) ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa wakulima ambazo huhimili 
baadhi ya magonjwa na wadudu. 



 Inashauriwa kupanda maharage katika umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.

Kama mbegu moja moja katika kila shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo idadi yake ni nusu ya 
maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 = ekari 2.471. 

2.Mbolea.

Mimea huhitaji virutubisho kutoka kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage huhitaji madini ya ‘phosphorous’ na ‘potassium’ ambayo hupatikana kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo na mabaki ya mimea.

Ni muhimu kufahamu udongo ambao unatarajia kupanda mimea yako ili 
kutathmini viwango vya madini yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza. 

Zaidi ya yote ni vizuri kutumia mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye udongo. 

3.Magugu. 

Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea.

Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza kushambulia 
mimea. 

4.Wadudu na magonjwa. 

Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia 
za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea 
ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika). 

Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara 
kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka. 
Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza 
kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu.

Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu. 

5.Kukomaa na Kuvuna.

Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda. Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa.

Kwa mfano asilimia 80 ya maharage yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.

Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.

Baada ya kukauka hadi kufikia angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena. 

6. Kilimo mchanganyiko. 

Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.

Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi weupe.






Jan 30, 2017

Mambo Ya Lazima Kuwa Nayo Katika Safari Ya Mafanikio.

No comments :
Katika safari yoyote ya mafanikio huwa ipo misingi na mambo ya lazima ambayo ni lazima uyajue ili kufanikiwa. Kwa kuyajua mambo hayo yatakupa dira na mwelekeo mzuri wa kufikia mafanikio makubwa.
Ni kweli unaweza ukawa una malengo mazuri uliyojiwekea, lakini bila kuyajua mambo hayo na kuyafanyia kazi itakuwa ni ngumu sana kufikia mafanikio yako. Watu wengi wenye mafanikio wanayajua mambo haya na kuyafanyia kazi mara kwa mara. Je, unajua ni mambo gani ambayo ni ya lazima sana katika safari yako ya mafanikio?
 1. Hamasa.
Ili uweze kufanikiwa ni lazima kwanza uwe na hamasa kubwa ya kufikia mafanikio hayo. Wengi huwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa hamasa. Unapokuwa unashindwa kuwa na hamasa inakuwa ni ngumu kufikia mafanikio yoyote kwa sababu karibu kila kitu utakifanya kizembe au kivivu ilimradi ukikamilishe.
Kitu kinachokufanya uongeze juhudi kwa kile unachokifanya sasa ni kwa sababu una hamasa ya kutaka kufanikiwa. Kushindwa kwako kutaanza mara moja ikiwa utaanza kukosa hamasa hiyo. Huu ni ukweli ambao ni lazima uujue ili kuweza kufanikiwa, vinginevyo hakuna utakachoweza kukifanikisha. Kila kitu kitakuwa kigumu kwako.

2. Uzingativu.
Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani lakini ikiwa ndani yako utakosa uzingativu, kuyafikia mafanikio hayo itabaki kuwa ndoto za mchana. Watu wote ambao huwa wanafanikiwa katika mambo yao ni watu wa kuzingatia sana. Huwa ni watu ambao hawana papara, wakianzisha jambo hulifatilia mpaka kulifanikisha.
Mara nyingi unapoweka nguvu ya uzingativu katika jambo moja, huwa zinaleta matokeo makubwa na kuyashangaza. Hakuna kinachoshindikana katika nguvu hizi za uzingativu zinapotumika. Hiki ni kitu ambacho unatakiwa kukiweka kwenye akili yako na kukifanyia kazi. Na hili ni jambo la lazima sana katika safari yako ya mafanikio, bila hivyo huwezi kufanikiwa.
3. Kujiamini.
Msingi mkubwa wa mafanikio upo kwenye kujiamini. Ikiwa wewe utakuwa mtu ambaye unajitilia shaka na hujiamini katika mambo yako ukweli wa mambo uko wazi hata ufanyaje huwezi kufanikiwa. Kama unabisha hebu angalia mambo ambayo hukuwahi kufanikiwa, utagundua mengi hukuweza kujiamini sana.
Kwa hiyo mpaka hapo utagundua kwamba kujiamini ni jambo la lazima sana katika safari ya mafanikio yako. Mafanikio yoyote yale yanahitaji kwanza wewe uanze kujiamini binafsi kuwa utafanikiwa. Kwa kadri unavyozidi kujiamini sana katika maisha yako, ndivyo ambavyo utajikuta ukifanikisha mengi.
4. Kufanya kazi kwa bidii.
Ni kweli unaweza ukawa una hamasa kubwa, una nguvu ya uzingativu na unajiamini vya kutosha, lakini kama hufanyi kazi kwa bidii huwezi kufanikiwa. Kazi ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote unayoyahitaji. Ili uweze kufanikiwa ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa bidii zote. Hapo ndipo utaanza kuyaona mafanikio yako.
Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watu wa kujituma sana. Bila kufanya kazi kwa bidii, elewa kabisa mipango na malengo yako mengi yataishia njiani. Kwa hiyo kama ni kazi weka juhudi zako zote mpaka ikuletee mafanikio. Kwa sababu unakuwa umeweka nguvu zako nyingi, hata ikitokea umeshindwa hutajilaumu sana. 
Kwa mambo hayo manne ni silaha kubwa sana ya mafanikio kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufikia mafanikio makubwa. Kitu kikubwa naomba ufanyie kazi mambo hayo ili yaweze kubadili maisha yako na ya wengine wanaokuzunguka. Kila kitu kinawezekana ukiamua, hivyo amua sasa upate kufanikiwa.
Nikutakie kila la kheri katika safari yako ya mafanikio . Kumbuka tupo pamoja.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

Jan 27, 2017

Kama Unaogopa Kufanya Kitu Hiki, Sahau Kuhusu Mafanikio Katika Maisha Yako Yote.

No comments :
Fikiria kila unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe katika maisha yako, halafu  uone ukweli huu  kama kweli nawe ni mmoja kati ya watu wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na pengine tu wewe hujijui. Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini  mara kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa kufanya jambo ambalo lingeweza kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio mkubwa? Hili ndilo tatizo walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya mabadiliko kwa namna moja au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao wenyewe kuna wakati huwa wanaogopa pia.

Kimaumbile, kila binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya mabadiliko inapozidi kuwa kubwa na kukuzuia kufanya mambo ya maana kwako, hofu hii  sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia wewe kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya mabadiliko Fulani  katika maisha yako, lakini umekuwa ukijikuta ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani? Ni mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na hofu nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati mwingine bila sababu ya msingi.

Wengi wetu kutokana na kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa sababu ambazo hata hazina mashiko zinazosababisha wao washindwe kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta mtu anakwambia  hawezi kufanya biashara ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu ambayo amekuwa akiitoa kwa muda mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana mtaji tu. Kama uko hivi una hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza kuvifanyana , tambua kuwa kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako anayekuzuia kufanikiwa. Na unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa ili ufanikiwe, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote.


Tatizo kubwa utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa kufanya mabadiliko ni lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo ya kutaka kufanikiwa leoleo hata kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa wana hofu hii kubwa ya mabadiliko ndani mwao, unaweza  kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli huu ulio wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini subira ndani mwao, bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao unaanza leo biashara na wiki ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa.

Hivi ndivyo walivyo watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini katika miujiza, sio katika wao wenyewe kutenda na kuona matokeo.  Hebu jaribu kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu wanaofikiria sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya karibu sana na hawataki shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila kitu kimalizike leo. Sijui kesho watafanya kitu gani? Ukimwambia mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya miaka 10 kutoka sasa kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu zimuume. Anataka leo hata kama ni kwa miujiza.

Ndiyo maana wengi kati ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka malengo siyo sehemu ya maisha yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira, mtu anayeamini kwamba maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni kulalamika na kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya kazi, wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine waliobaki wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni kwa kufanya uhalifu wa aina yoyote.

Ni watu ambao wanataka kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza kuiamuru iwape wakitakacho na wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi tu, watu hawa kwao mabadiliko ni kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe kwako, unatakiwa kubadilisha fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio yanahitaji mabadiliko makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa kujitoa hasa. Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe, chukua hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila mara kwa kupata maarifa bora yatakayoweza kuboresha yako, kwa pamoja tunaweza.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,






Jan 26, 2017

Kama Unayatafuta Mafanikio Kwa Njia Hii, Huwezi Kuyapata.

No comments :
Kuna wakati mwingine binadamu tunakuwa ni viumbe wa ajabu sana kutokana na kutotaka usumbufu hata kwa yale mambo tunayoyahitaji. Inapotokea tunataka kitu cha aina fulani tunakuwa ni watu ambao tumejiweka katika kundi fulani ambalo hatutaki kuweka juhudi sana yaani kwa lugha rahisi tunakuwa kama tunajihuhurumia hivi na kuona kama tutaumia kwa kutafuta vitu hivyo.
Kutokana na hali hiyo hupelekea wengi wetu kuanza kutafuta njia za kupata mafanikio ya haraka na upesi. Kumbe kwa kufuata njia hizo ndiyo tunakuwa tunajidanganya na kupotea kabisa ukizingatia katika maisha hakuna njia ya mkato kuweza kufikia mafanikio. Mafanikio yote yanakuja hatua kwa hatua. Na kama unaona njia hiyo ipo tayari unakuwa unapotea.
Utambue kuwa kila kitu kwenye maisha kinapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa na maarifa. Hakuna lelemama katika kutafuta mafanikio. Mafanikio ni mfumo wenye hatua zake ambazo ni lazima zifuatwe. Sasa anapokuja mtu anakwambia kwamba ipo njia hii hapa ya mkato kuyapata mafanikio, mmmh huyo ni vyema ukamuogopa sana kwa kuwa atakuwa anakupoteza huku ukiwa unajiona.
Ni vigumu sana kuweza kufanikiwa kama utategemea njia za mkato na bila kuweka juhudi yoyote ile kubwa. Kama utayapata mafanikio hayo kwa njia hiyo ni wazi tu yatakuwa ya muda. Hiyo yote inaonyesha hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio yako. Kitu kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuweka juhudi zako kubwa mpaka kufanikiwa na siyo vinginevyo.

Hebu jaribu kuangalia watu wote wale ambao wamewahi kushinda bahati nasibu. Watu hawa wengi wao ukija kuwafatilia maisha yao  baada ya miaka michache mbele utakuja kugundua ni watu ambao pesa hizo hawana tena na wafelisika. Kufilisika kwao kumekuja kutokana na walizipata pesa hizo nyingi kwa ghafla na kwa njia ambayo ni ya mkato na sasa zimewakambia.
Kama nilivyosema mafanikio yanakuja hatua kwa hatua. Kuna kujifunza kwingi sana inapotokea umeanzia chini kabisa. Mara nyingi  hiyo inakuwa inakujengea misuli ya kukua kidogo kidogo na mwisho wa siku unajikuta upo kwenye kilele cha mafanikio makubwa. Endesha maisha yako kwa kujiamini na kujua maisha yako ni lazima ufanikiwe hata bila kutegemea njia za mkato ambazo nyingi huwa zina mashimo mengi na isitoshe hazina uhakika wa kufika.
Hiki ni kitu ambacho unatakiwa ukiweke kwenye ubongo wako kuwa unahitaji ujasiri, kujitoa na kuwekeza nguvu zako nyingi kwa kile unachokifanya na siyo kupita njia ya mkato kama unavyofikiri. Kumbuka, ni lazima kujituma kwa bidii tena wakati mwingine katika magumu na vizuizi vya kila aina bila kukata tamaa. Kila kitu kitawezekana na utafika kule unakohitaji kufika katika maisha yako ikiwa utazingatia ukweli huo ninao kwambia sasa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya maisha yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,

Jan 25, 2017

Imani Tatu Unazotakiwa Kuwa Nazo Ili Kukufanikisha.

No comments :
Najua hapo ulipo una mipango au malengo ya aina fulani uliyojiwekea na unahitaji mipango hiyo itimie. Lakini ili kuyafikia hayo malengo yako, mara nyingi huwa hayawezi kutimia mpaka ndani yako ujenge imani tatu muhimu. Hizi ni imani muhimu sana kwa mabadiliko yoyote unayoyataka maishani mwako.
Bila kuwa na imani hizo si malengo peke yake ambayo hayataweza kutimia  hata pia mabadiliko yoyote hayawezi kutokea kama huna imani hizo tatu. Kwa sababu hiyo, hili ndilo lengo la makala haya, ikusaidie kujua aina za imani unazotakiwa kuwa nazo ili kukufanikisha kwa kile unachokihitaji.
Hizi ni imani ambazo unatakiwa kuwa nazo wewe kila siku. Huwezi kufanikiwa sana kama huna au hujajifunza kujenga  imani hizi tatu muhimu kwenye maisha yako.
Bila kupoteza muda fuatana nasi katika makala haya kujifunza pamoja imani tatu unazotakiwa kuwa nazo ili kukufanikisha;-.
1. Lazima uamini maisha yako yanakwenda kubadilika.
Ili uweze kuleta matokeo chanya na kukipata kile unachokitaka ni lazima uamini maisha yako ni lazima yatabadilika. Imani hii ni muhimu sana kwa kwa mabadiliko yoyote unayotaka kuyachukua kwenye maisha yako.
Kama hutakuwa na imani hii itakuwa ngumu sana kuweza kufanikiwa. Hata uwe katika wakati mgumu vipi, lakini ni lazima kwako kutambua maisha yako ni lazima yabadilike.
Kwa kuendelea kuamini hivyo itakupelekea kuchukua hatua ambazo zitakusaidia kufikia ndoto zako. Kama una kitu au hali  unayotaka kuibadili, amini kabisa unakwenda kuibadili hali hiyo au maisha hayo.

2. Lazima uamini wewe ndiye utakayebadii maisha yako.
Hakuna mtu mwingine mwenye uwezo wa kubadili maisha yako zaidi yako. Kama unaisubiri serikali ibadili maisha yako utachelewa, kama unasubiri ajira utachelewa, unatakiwa kuchukua hatua mara moja.
Hakuna mwenye uwezo wa kubadili`maisha yako zaidi ya wewe. Upo ulazima wa wewe kuamini kwamba ndie utakayebadili maisha ako na familia yako na siyo mtu mwngine.
Iwe unakabiliwa na changamioto ya mtaji ni lazima ujue wewe ndiye unatakiwa ubadili hali hiyo. Ikiwa unakabiliwa na changamoto ya hali ngumu ya maisha pia wewe ndiye mwenye uwezo wa kuibadili.
3. Lazima uamini unao uwezo wa kubadili maisha yako.
Pamoja na kwamba umeamini maisha yako yatabadilika na ni wewe ndiye utakayebadili hali hiyo, pia upo ulazima wa kuamini  hali hiyo inawezekana kwako kabisa kubadilika.
Acha kujikatisha tamaa kwa namna yoyote ile. Kila kitu kinaweza kubadilika katika maisha yako na kufikia mafanikio makubwa. Hata hali ya maisha yako nayo pia ina uwezo wa kubadilika.
Kwa kifupi hizo ndizo imani tatu muhimu unazotakiwa kuwa nazo ili kufanikishha jambo lolote lile katika maisha yako.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,





Jan 24, 2017

Jinsi Ya Kutengeneza Karanga Za Mayai.

3 comments :
Kama ilivyo ada yangu kukueleza masomo ya kijasiliamali nakusihi uambatane nami mwanzo mpaka mwisho, maana maana halisi ujasirimali husishwa na utengenezaji wa vitu vipya au kuviboresha vya zamani. 

Hata hivyo ushindwe wewe kuchukua hatua ya kuweza kufanyia kazi masomo haya ambayo nimekuwa nikifundisha, kwani wakati unalaumu masuala ya umaskini mimi nitakuwa nimeshanawa mikono.  Nilishafundisha namna ya kutengeneza Tomato souce, chill souce.

Hivyo leo tuangalie utengenezaji wa karanga za mayai. Karanga za mayai zimekuwa zikipendwa na watu wengi sana nikiwemo mimi mwenyewe.  Pamoja na utengenezaji wa bidhaa hii wapo ambao wamekuwa wakijmtengeza bidhaa hizo kama sehemu ya kujipatia kipato. 


Hivyo ungana nami twende sawa kwa kuangalia mahitaji ya awali kabla ya kuanza kukaanga karanga za mayai. 

1. Sukari kiasi
2. Unga wa ngano  kilo 1 moja na nusu. 
3. Karanga kilo 1
4. Mayai 3
5. Mafuta ya kupikia kiasi kulingana na mchanganyiko wako. 

Namna ya kutengeneza 

a.  Pasua mayai ,changanya mayai na sukari kisha koroga katika chumba kimoja. 

b.  Hatua ya pili chukua unga wa ngano kisha changanya na mchanganyiko namba (a)  yaani mchanganyiko wa mayai na sukari. 

c.  Weka mafuta katika sufuria kisha injika motoni.  Lakini hakikisha moto hauwi mkali sana. Ukiwa mkali sana utasababisha karanga kuungua sana na kupoteza radha. 

d.  Koroga mchanganyiko huo taratibu ili kuondoa kugandamana kwa mchanganyiko huo wa karanga pamoja na unga wa ngano.  Fanya hivyo kila baada ya dakika kadhaa. 

e.  Ukiona zimeanza kubadilika rangi onja kwa kujiridhisha kama kweli zimeiva.

f.  Zikisha iva ziepue kisha weka katika chombo kisafi ili zipoe.  Baada ya dakika kadhaa zivunge katika vifungashio kwa ajili ya biashara. 

Muhimu. Hakuna kitu chenye thamani katika biashara kama kufunga bidhaa katika vifungashio vizuri vyenye kuvutia lakini vifungashio pekee havitoshi hakikisha bidhaa yenyewe ni bora. 

Asante tukutane siku nyingine hapa hapa tukijadili masuala ya biashara na maisha kwa ujumla. Nakutakia siku njema na mafanikio mema. 

Ndimi Afisa Mipango Benson Chonya,

Jan 23, 2017

Upi Ni Uhusiano Wa Kimazingira Na Mafanikio?

No comments :
Kuna mahusiano makubwa kati ya mafanikio yako na mazingira yanayokuzunguka. Lakini mafanikio hayo huwa hayaji kwa bahati mbaya,  au huwa hayaji kama ajali.  Bali huja kwa kuyatazama mazingira hayo, kama sehemu ya mafanikio yako.  Huenda nikawa nimekuacha kidogo ipo hivi, maana halisi ya neno mazingira ni mjumuisho wa kila kitu ambacho humzunguka mwanadamu. 

Hivyo Moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa ikisababisha maisha ya wengi kuwa katika hali ya ya kawaida ni kutokana na vile ambavyo wameamua kuyachukulia mazingira katika hali ya kawaida pia. Lakini ukweli ni kwamba ili uweze kuwa mtu mwenye mafanikio amini ya kwamba wewe si mtu wa kawaida na mazingira uliyonayo ni ufunguo wa mlango wa mafanikio yako.

Kuwa mtu wa kawaida kumekufanya ushindwe kufikia kusudio lako. Swali linakuja tena kwanini uwe mtu wa kawaida kama kweli unataka mafanikio ya kweli?  Bila shaka majibu yake yasikufanye kuwa ni mtu wa kawaida. Mafanikio makubwa huja kwa mtu ambaye yupo tayari kwa ajili ya mafanikio hayo.

Pamoja na changamoto nyingi ambazo zipo katika dunia hii, changamoto hizo zisikufanye ushindwe kufanikiwa.  Kabla ilivyo ada yangu kukueleza bayana ya kwamba "kukata tamaa ni kosa la jinai" hii ni kwa mujibu wa sheria za mafanikio.


Huenda bado ukawa huamini kama ipo siku utafanikiwa,  ila nataka kukutia moyo kwa kukwambia ya kwamba mafanikio yako yapo upande wako, endapo utaamua leo kuweza kuyatawala mazingira yako vizuri. 

Sheria ya mafanikio na uhusiano wa mazingira inatuambia ya kwamba watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wametawaliwa na mazingira. Mazingira hayo hayo umewafanya watu wengine wamefanikiwa na wengine bado hawajafanikiwa. Sasa swali linakuja mazingira haya ya nini kwani? 

Tuendelee kidogo kwa kuyazungumza mazingira haya. Mazingira haya endapo utayatazama kwa macho mawili utagundua ya kwamba yametawaliwa na wingi wa changamoto nyingi kuliko fursa. Na endapo utayatazama mazingira hayohayo kwa jicho la tatu utagundua yametawaliwa na fursa nyingi kuliko changamoto.

Unashangaa wala usishangae huo ndio ukweli. Swali la kujiuliza unatumiaje mazingira uliyonayo kama fursa ili uweze kufanikiwa?  Usinipe majibu.  Lakini Ukichunguza kwa umakini utagundua ya kwamba watu wengi tumekuwa tukiyachukulia mazingira ambayo tunaishi katika misingi ya ukawaida na ndo maana tumekuwa siku sote sisi ni wa kawaida. 

Lakini nataka nikuase kwa kusema ya kwamba maisha hayo ambayo unatamani kuwa,  ni lazima uweze kuyatazama mazingira katika sura ya fursa na si changamoto kama ulivyokuwa ukifanya awali.  Hata kama mazingira iliyopo yana changamoto gani, Changamoto hizi unatakiwa kuzikabili kwa kufanya kitu tofauti .  Maana kuna usemi ambao unasema ya kwamba changamoto ni fursa.

Mazingira yanayokuzunguka isiwe kigezo cha wewe kuwa maskini kwani wewe si mtu kawaida,  hivyo yafanye mazingira hayo kama kigezo cha wewe kufanikiwa. Siri ya mafanikio yako ipo katika mazingira yako. 

Nikuache na ujumbe usemao" Mazingira yangu mafanikio yangu "
Ndimi:  Afisa Mipango Benson Chonya,


Jan 20, 2017

Hatua Nne Za Kujifunza Kutokana Na Makosa.

No comments :
Mara nyingi tumekuwa tukisema ili ufanikiwe ni muhimu sana kujifunza kutokana na makosa. Tumekuwa tukiongea sana kuhusu juu ya hilo mara kwa mara na kukusisitizia juu ya umuhimu wake.
Pamoja na msisitizo huo wa kujifunza kutokana na makosa ambao tumekuwa tukikupa, leo tumeona vyema tukuongezee kitu cha cha ziada katika huko kujifunza kutokana na makosa.
Kitu hiki si kingine bali hatua ambazo unatakiwa uchukue ili uweze kujifunza kwa makosa kiuhakika. Kwa kujifunza hatua hizi itakusaidia wewe  kuvuka hapo ulipo na kwenda ng’ambo nyingine kimafanikio.
Ili kunielewa vizuri katika hili hebu twende pamoja tuangazie nukta kadhaa zitakazo tusaidia kuzielewa hatua nne za kujifunza kupitia makosa tunayoyafanya kila siku kwenye maisha yetu.
Hatua 1.  Andika makosa yako.
Unapojikuta upo katika kitu kipya unachofanya, tambua makosa yapo na ni lazima utafanya. Kitu cha kwanza cha kufanya ili uweze kujifunza vizuri kutokana na makosa yako, andika makosa yako. Hakuna mkato katika hili, andika makosa yako ili ikusaidie wapi pa kuanzia pale unapotaka kujirekebisha.

Fanyia kazi makosa yako mapema.
Hatua 2. Jifunze kutokana na makosa ya wengine.
Usisubiri sana kujifunza kutokana na makosa yako, angalia pia wengine wanafanya makosa gani, pia yachukue makosa hayo na ya andike mapema ili yasije yakajirudia na kwako pia.  Unapoandika makosa ya wengine mnaofanya kitu kinachofanana inakusaidia na wewe kuwa makini sana.
Hatua 3. Andaa orodha ya makosa ya kuyafanyia kazi.
Katika hatua ya kwanza na ya pili utakuwa umefanya zoezi la kuandika makosa yako. Hapa katika hatua hii andaa sasa makosa ambayo unataka kuyafanyia kazi lakini ambayo yametoka kwenye orodha uliyoandika kwenye hatua mbili zilizotangulia, kisha chukua hatua.
Hatua 4. Hakikisha usiridhike mapema.
Hata mara baada ya kurekebisha makosa yako, usibweteke na kuridhika na kujiona wewe ni wewe. Endelea kujifunza kutokana na makosa mengine tena na tena na kurudia hatua hizo, hiyo itakufanya uzidi kuwa bora sana siku hadi siku.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

Jan 19, 2017

Jiwekee Mkakati Huu,…Ili Ujihakikishie Mafanikio Yako.

No comments :
Katika utoto wake hakuna kitu ambacho alipenda sana kijana huyu kama kuona ndoto yake inatimia. Aliandika vizuri ndoto yake kwenye daftari lake na kisha kila wakati aliipitia ndoto hiyo.
Shauku ya kuona ndoto yake ikitimia alizidi kutokea karibu kila siku. Alitamani kuiona ndoto yake ikitimia mapema sana kwa kadri iwezekanavyo. Kwa kifupi, alikosa raha hasa alipoona kwa nini ndoto yake haitimii?
Hata hivyo pamoja na kuwa na hamasa kubwa ya kuona ndoto yake inatimia ,kijana huyu alikuja kugundua kuna kitu kimoja kinamzuia kufanikiwa. Kitu hicho hakikuwa kingine bali ni shule.
Akiwa na miaka 22 akiwa elimu ya juu aliamua kuachana na shule na kwenda kutimiza ndoto yake aliyokuwa akiifikiri. Lakini hata hivyo kazi haikuwa nyepesi sana kama alivyofikiri.

Jiwekee mpango wa muda mrefu ukusaidie kufikia ndoto zako.
Ingawa kijana huyu alikuwa hana pesa, maskini, hivyo ilimlazima kuanza kuimba kwenye kumbi za starehe, ‘bar’ na ilimlazima wakati mwingine hata kulala vibarazani, lakini alidhamiria kutimiza ndoto yake.
Hali ya kuendelea kuimba huku akiwa katika wakati mgumu aliendelea nayo hivyo hivyo, lakini kuna wakati mambo yalizidi kuwa magumu sana hadi hali iiyopelekea mpenzi wake mpendwa kuachana naye.
Kitendo cha kuweza kuachana na mpenzi wake kilimuuma sana, aliona maisha ndio yamefikia mwisho, hivyo uamuzi pekee aliamua kuuchukua ni kujiua. Maisha yalikuwa hayana maana tena kwake.
Kabla hajachukua uamuzi huo aliamua kwenda hospitali kupima kama akili zake kweli ziko sawa, baada ya majibu na kugundulika kwamba yuko sawa, alikaaa chini na kujiuliza ni nini hasa kinachonifanya nijiue?
Alikuja kugundua huo ungekuwa ni ujinga wa kutupwa. Aliapa na kuamua kwa vyovyote vile itakavyokuwa, hata dunia nzima imtenge ni lazima aitimize ndoto yake. Alikubali kufanya kazi usiku na mchana mpaka kieleweke.
Tokea afanye uamuzi huo, ilimchukua miaka mingine miwili hadi pale angalau alipoanza kuona matunda ya kazi yake. Hapo ndipo alipoanza kukubalika na muziki wake kuanza kufahamika.
Kitu kilichomsaidia ni kule kujitoa kwake na kukubali kuchukua mpango wa muda mrefu kuliko kuota ndoto za kufanikiwa mara moja ambazo zingemuangusha.
Huyu tunaye mzungumzia hapa si mwingine bali ni Bill Joel, moja kati ya wanamziki maarufu duniani. Leo hii angekuchukua maamuzi ya kujiua mara baada ya kuachwa na kushindwa usingeweza kumsikia tena.
Hapa tunajifunza kuna wakati ili kuweza kufanikiwa unahitajika kujiwekea mikakati ya muda mrefu yaani ‘long term plan’. Bila kufanya hivyo ni rahisi sana kushindwa hata pale ambapo hukutakiwi kushindwa.
Kwa lugha nyingine namaanisha ile habari ya kutaka kufanikiwa ndani ya muda mfupi, unatakiwa ujifunze ‘kuizika’ mapema ili ujipe muda mzuri wa kutengeneza mafanikio yako kwa uhakika.
Kile kinachonekana leo kama hakitoi mafanikio kwako makubwa, kitafanikiwa na kukupa mafanikio makubwa endapo utakipa muda na kuendelea kuweka juhudi kila siku na kujifunza.
Maisha yapo kama majira ya mwaka, kuna wakati wa baridi, wakati wa joto au wakati wa upepo. Hivyo unatakiwa kujifunza kukabiliana na nyakati zote hizo ili zikusaidie kuweza kufanikiwa.
Lakini ikiwa ni mtu wa kulia na kuona mambo hayawezekanai kwa sababu umeshindwa au kwa sababu dunia imemekukata utakua ni mtu wa kushindwa sana.
Kila wakati jiandae kuwa kuwa shujaa kwa kile unachookifanya. Achana na habari ya kulialia. Ukiweka msingi na mikakati wa kuwa na malengo ya muda mrefu. Hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,