google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Apr 27, 2015

Kama Unataka Mafanikio Makubwa, Hakikisha Unabadili Kitu Hiki Haraka Sana.

No comments :
Habari za leo mpenzi msomaji wa DIRA YA MAFANIKIO, nimatumaini yangu ya kuwa umzima na unaendelea vyema katika shughuli nzima ya kuboresha maisha yako. Kama nilivyosema katika makala iliyopita kuwa katika makala ya leo tutajifunza juu ya kubadili fikra zetu ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.
 
Ikumbukwe kuwa fikra ni kitu cha muhimu sana kutuwezesha kufikia mafanikio makubwa tuliyojiwekea. Bila kuwa na fikra sahihi ni vigumu sana kuweza kufikia mafanikio yoyote yale. Hivyo, hiyo inatuhakikishia kuwa kama kweli unataka mafanikio makubwa, kitu cha kwanza unachotakiwa kukibadili kwa haraka ni fikra zako. 

Kumbuka,kufikiri ni kufikiri, wengi ndivyo tunavyamini. Huwa tunachukulia kufikiri kwetu kama jambo ambalo halituhusu kabisa. Inawezekana kabisa hapo ulipo ulishasahau kwamba huwa unafikiri  hadi hivi sasa unaposoma kuhusu kufikiri.
Ni ajabu sana kwa sababu, huku kufikiri ndiko kunakokufanya tuhisi au kutenda kwa namna hii au ile maishani. Kila tunachofanya na mengi kama siyo yote kati ya yale yanayotutokea kwenye maisha yetu yanatokana na kufikiri kwetu.


Katika kutafuta kufanikiwa ni lazima kufikiri kwetu kuwe katika mkabala wa kufanikiwa kwanza. Kama kufikiri kwetu kuko katika mkabala wa kushindwa, tunakuwa sawa na mtu anayeomba watu wasukume gari lake kwenda mbele huku akiwa tayari amewaomba wengine kulisukuma gari hilo kurudi nyuma.


Kama binadamu, tunatofautiana katika mambo yanayoenda vichwani mwetu na mambo hayo ni mengi sana. Wataalamu wamethibitisha kwamba, kwa kutwa moja binadamu anapitiwa na mawazo zaidi ya elfu hamsini. Lakini jambo ambalo hatutofautiani ni ukweli kwamba, kufikiri kwetu huko kwa namna-kufikiri kuzuri na kufikiri kubaya.

Singependa kuzungumzia kufikiri vizuri na kufikiri vibaya kwa sababu, inahitaji maelezo mengi na hata hivyo, haitasaidia sana katika muktadha huu. Bali ninachoweza kusema ni kwamba, kufikiri vizuri ni ile hali ya kuingiza fikani mwetu yale mambo ambayo hayatuumizi kihisia, kiroho na kimwili, wala kuwaumiza wengine kwa njia hiyo.

Kufikiri vizuri ni kuingiza fikirani mwetu yale tu ambayo tunaamini kwamba yatatupa moyo, kutuongezea matumaini na kutujengea uhusiano mzuri na wengine. Yale tu ambayo ndiyo tunayotaka , tunayoyatamani na kupenda yatokee maishani mwetu.


Kufikiri vibaya, kwa kifupi naweza kusema kuwa ni kufanya kinyume na kufikiri vizuri. Pale ambapo kile tunachokiruhusu kuingia fikrani mwetu ni chenye kutuumiza kihisia, kiroho na kimwili au kuwaumiza wenzetu kwa njia hiyohiyo, ndipo tunapaswa kujua kwamba, tunafikiri vibaya. Kufikiri vibaya ni kuingiza mawazoni mwetu yale tusiyoyataka au kuyatamani ama kuyapenda.

Unachopaswa kufanya kama kweli unataka mafanikio maishani mwako ni kujiuliza kuhusu mfumo wako wa kufikiri . je, mawazo yako mara nyingi yanabeba mambo gani? 

Inawezekana kabisa huwa unaamini kwamba wewe ni dhaifu, wewe huwezi kupata cheo, wewe huwezi biashara fulani kama wengine au wewe ni msindikizaji tu. Kama unajiita ‘mlalahoi’ hujitendei haki. Kama unajiita ‘dhaifu’hujitendei haki. Kama unajiita mnyonge hujitendei haki. Kama unajiambia una mkosi ndiyo kabisa na kama unajilaumu kila wakati, tambua kwamba unajifuja kupita kiasi.

Kama unafikiri vibaya inabidi ubadilike na kuanza kufikiri vizuri, yaani kuingiza fikrani mwako yale tu ambayo yatakusaidia katika kufika kule unakotaka bila kujiumiza au kuwaumiza wengine. Kuingiza ffikrani mwako yale tu unayotaka  au kuyatamani, na siyo kuingiza yale usiyoyataka.

Kwamba unaweza kufanya au kupata kile unachokitaka maishani ni jambo lililowazi kabisa, bila kujali kama umesoma au hukusoma, un rangi nyeusi au nyeupe, unatoka kwenye familia maskini au ya kitajiri, unasali au husali. Sifa au vigezo vya kupata kile unachokitaka vinafahamika, lakini kama nilivyosema sifa ya kwanza ni kufikiri.

Wale wote waliofanikiwa, ukiwauliza watakwambia kwamba waliamini kuwa watafanikiwa walifanya juhudi wakijua kuwa iko siku. Kuna wakati rais wa zamani wa marekani Abraham Lincolin( Alikuwa rais mwaka 1860) ambaye alianguka na kushindwa zaidi ya mara ishirini katika mambo mbalimbali ikiwemo katika uchaguzi, kufilisika biashara na hadi kuchaganyikiwa. Lakini aliendelea bila kusema , ‘ninamkosi’ au ‘siwezi’ hadi akaja kuwa kiongozi maarufu duniani.


Kwenye kitabu chake cha Unlimited power, Anthony Robbins anamzungumzia mtu ambaye alipata ajali ya barabarani akaumia sana kiasi ch akuharibika kabisa mwili. Mtu huyu alikuja tena akapata ajali yaa ngege ambapo alipooza kuanzia kiunoni kwenda chini. Bila kujali ulemevu na uharibifu wa sura na mwili, mtu huyu alisema, ‘ninawea na nitafanya’. Aliweza na kuwa miongoni mwa mamilionea wa marekani. Kwa wenzetu wengi, kwa ulemavu wa aina hiyo hunyoosha miguu na kuanza kuomba wakiamini hawawezi tena.

Anthony Robbins mwenyewe hakusoma zaidi ya elimu ya kidato cha sita, lakini kwa kuamini kwamba, inawezekana mtu anapoamua, alifanya maajabu. Kwa kiwango chake hicho cha elimu aliweza kwa muda mfupi tu, kutoka katika hali ya uhohehahe wa kuishi chumba kimoja chenye mende, hadi kuaminika katika kuwafundisha watu kuhusu maisha wakiwemo viongozi wan Nchi.

Sasa hivi Robbins ni bilionea na hakuiba  wala kutumia ujanjaujanja, bali kanuni za kimaumbile katika kujenga uwezo wa binadamu. Kama angeamini kuwa, kwa sababu hakusoma sana asingeweza, ni wazi asingeweza, lakini wa sababu hakujiwekea vizingiti amemudu.

Uwezo wa mawazo yetu unaonekana vizuri kwa mtu na wazi kwa zaidi kwa mtu aitwaye Stephen Hawking, ambaye ni miongoni mwa wanasayansi bora ambao karne iliyopita na karne hii zimeweza kumshuhudia. Kwa nini mtu huyu ni mfano bora wa namna mawazo yalivyo na nguvu?

Akiwa na umri wa miaka 13 aliugua maradhi yanayofahamika kama amyotrophic lateral screrosis u lo gehrig’s, hali ambayo hulemaza mwili. Hawking alilemaa mwili mzima isipokuwa shingo, kichwa na mkono wake wa kushoto. Pia alikuwa hana uwezo wa kuzungumza.

Akiwa kwenye hali hiyo, aliweza kufanya maajabu kwenye eneo la fizikia na kutoa nadharia nyingi ambazo zimesaidia kuibadili dunia katika maeneo mbalimbali. Kwa kuamini kwamba anaweza, kupania na kujua anataka nini, ameshangaza wengi. Kwa sababu bado yu hai, atashangaza wengi zaidi. 

Ukiweza kuyabadili mawazo yako, yanauwezo wa kukupa mafanikio makubwa ukiamua. Kitu unachotakiwa ni kuacha kabisa kujidharau na kujishusha, utafanikiwa.

TUPO PAMOJA KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO,

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,


Apr 25, 2015

Hii Ndiyo Kanuni Rahisi Kwako Unayoweza Kuitumia Kukupa Mafanikio Makubwa.

No comments :
Ni hivi. Ili uweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa unayotaka iwe katika masomo, kupata kazi, kuvuna sana mazao shambani, kupata faida katika biashara au kuwa na uhusiano mzuri na ndoa nzuri, ni lazima kwanza ujue kwamba hayo yote yanawezekana na yanakuhusu wewe moja kwa moja kwa asilimia zote na siyo bahati.
 
Unapotaka mafanikio ambayo huamini kwamba unastahili kuyapata, huwezi kamwe kuyapata hata kama ungefanya nini. Unapotaka kupata ajira, lakini ukajiambia kwamba kuna watu wengi wenye sifa kuliko wewe, ambao watapata kazi hiyo na siyo wewe, ni wazi pia hutapata kazi hiyo unayoitafuta.

Unapoamini kwamba utapata kazi hiyo kwa juujuu, lakini ndani kabisa mawazoni mwako unajua ni jambo gumu litakuwa gumu kweli. Unapoingia kwenye biashara kwa kuamini kwamba hutaweza kufanikiwa kwa sababu haijawahi kutokea ukafanikiwa au kwa sababu wewe una mtaji mdogo, hufahamiki na pengine hukusoma sana kama wengine, ni wazi hutafanikiwa.


Unaposema na kuamini kwamba una mkosi, utaendelea kuwa na mkosi hadi unaingia kaburini. Sisi binadamu ni kile tunachoamini. Kwa nini inakuwa hivyo, kwamba tunapoamini kuwa hatuwezi au tuna mkosi, mambo yanakuwa kama tunavyoamini?

Siyo kuamini tu kwamba mambo yatakwenda vibaya au tuna mkosi, lakini hata tunapoamini kwamba tunaweza, tutamudu, tutashinda, tutafurahi na tutatekeleza, basi ni wazi itakuwa hivyo. Hii ni kanuni ya kimaumbile, na ndiyo kanuni pekee ambayo ukiitumia ni lazima ikupe mafanikio unayoyataka. Kwa mujibu wa kanuni hii kwa vyovyote vile, tunavyofikiri na kuamini ndicho kinachokuwa chetu, iwe ni katika mafanikio au maanguko.

Kwa hiyo, ili kuweza kupata kile unachokihitaji katika maisha na kuenda sawa na kanuni hii ambayo ni rahisi kwako kuitumia na kukupa mafanikio, ni lazima kuweza kutambua umuhimu wa kufikiri vizuri. Kwa kufikiri kwetu vizuri itatusaidia kuweza kumudu na kutenda kwa mkabala wa kimafanikio na kuweza kuvuta mafanikio makubwa kwa upande wetu zaidi.


Kwa kufikiri kwamba hatuwezi au hatustahili, bila wenyewe kujua, tutafanya kwa mkabala wa kutoweza na kutostahili. Kumbuka kuwa upo uhusiano mkubwa sana kati ya fikra zetu, hisia zetu na tabia au matendo yetu. Tunapofikiri kwamba hatuwezi, bila kujua, tutakuwa na tabia zitakazotupeleka mahali ambapo hatutaweza kweli. 

Mwandishi na mwanafalsafa maarufu duniani Shakespeare aliwahi kusema: ‘Hakuna jambo baya au zuri, bali kufikiri kwetu ndiko kunakolifanya jambo kuwa hivyo’. Huu ndiyo ukweli , kwamba, kufikiri vibaya hutudhuru sana , tuwe tunajua au hatujui. Ubaya au uzuri wa mawazo yetu, hasa yale ya kina ni kwamba, kile tunachokifikiri  na kukiamini ndicho kinachotokea au kufanyiwa kazi, hayachagui au kutuhurumia ati kwa sababu hatujui juu ya ukweli huo.

Kwa hiyo, hatua ya awali kabisa ya mafanikio ya binadamu yako kichwani au mawazoni mwake. Kuna familia, koo, hata makabila ambayo yamekuwa na fikra kwamba hayawezi au hayastahili. Mtu kutoka familia, koo au makabila hayo anaweza kuwa na uwezo mkubwa sana katika kutenda, kipaji na ufahamu mkubwa ajabu, lakini akabaki kuwa mbumbumbu ambaye familia , ukoo au kabila lake limefanywa kuaminika kwamba ndilo linalostahili kuweza au kuwa nacho.

Bila kuanza kukagua namna tunavyofikiri, inaweza kuwa kazi bure kujaribu kutafuta au kuzungumzia mafanikio kwa ngazi yoyote, iwe mtu binafsi au taifa. Ni lazima tuanze kwa kujiuliza kile tunachoamini kuhusu mafanikio, yaani kupata kile tukitakacho maishani. Inawezekana kabisa, bila sisi wenyewe kujua tulishawekewa mipaka ya mafanikio tangu wakati tukiwa wadogo. Mipaka kama hii huwekwa vipi?


Inawezekana kabisa wazazi au jamii yote tulimokulia ilikuwa ikisema na kutenda kwa njia ambayo ilituonyesha kwamba tunachoweza sanasana ni kuhangaika na kupata ajira mahali, basi. Pengine ilisema na kutenda kwa njia ambayo ilituonyesha kwamba, ni vigumu kwetu kumiliki gari. Inawezekana kwamba ilisema na kutenda kwa njia ambayo ilituonyesha kwamba hatupaswi kuinuka sana kimaisha kwani sisi kwa ukoo au kabila fulani hatustahili.

Pia kuna wakati tunajikuta tukitamani kusonga mbele katika kutafuta kile tunachokitaka, lakini tunazuiwa na uvivu wa aina fulani tu tusioujua sababu yake, tunazuiwa na kuahirisha kufanya hivyo, bila kujua ni kwa nini. Inawezekana kabisa kwamba hiyo inatokana na malezi, mazingira tulimokulia au uzoefu wetu maishani. 

Kumbuka kuwa kuna vizuizi vingi vilivyowekwa kwenye mawazo yetu katika hatua hizo tulizopitia maishani. Lakini ili uweze kumudu kuondokana na vizuizi hivyo ni muhimu kwako kujua mambo mawili tu, ambayo ni  kuweza kutumia kanuni tuliyoongelea ya kuamini kuwa katika maisha yetu tutaweza, tutamudu, tutashinda na tutatekeleza na jambo la pili ni kubadili mtindo wako mzima wa kufikiri.

Unapoamua kubadili mtindo wako wa kufikiri sio kwamba tu unakuwa unajiondoa kwenye vizuizi vya kutofanikiwa, bali pia unakuwa unajiweka katika nafasi nzuri ya kupata kile unachokihitaji. Je, unawezaje kubadili mfumo wako mzima wa kufikiri na kukuwezesha kukupatia kile unachohitaji ama kufanikiwa kwa ujumla? Kujua hilo hakikisha unafuatilia makala ijayo katika DIRA YA MAFANIKIO bila kukosa, ili kujua mawazo yako jinsi yanavyoweza kufanya kazi na kukupa utajiri. 

Ansante sana kwa kuwa msomaji mzuri wa DIRA YA MAFANIKIO, endelea kuwashirikisha wengine kujifunza zaidi kupitia mtandao huu. Kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kabisa kufika mbali kimafanikio na kuufuta umaskini.

DAIMA TUKO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU,
0713048035,

Apr 24, 2015

Hatua Muhimu Zitakazokuongoza Kufanya Maamuzi Yatakayokupa Mafanikio Makubwa.

No comments :
Ni kitu ambacho kinawezekana kabisa katika maisha yako kuwa unaouwezo mkubwa wa kuwa na maisha yenye mafanikio kama unavyotaka iwe kwako. Ili uweze kufikia mafanikio hayo unayoyataka kwako ni lazima ujifunze kutumia uwezo mkubwa ulionao kuchunguza maamuzi unayoyafanya kila siku juu ya maisha yako. Maamuzi unayofanya, ndio msingi mkuu wa mabadiliko ya maisha yako.

Mara nyingi maamuzi unayofanya kila siku juu ya maisha yako ndiyo yanayotabiri au kukupa picha kamili ya maisha yako yanaekea wapi. Kama unafanya maamuzi mabovu kila wakati na kila mara uwe na uhakika maisha yako ni lazima yatakuwa sio mazuri. Kwa kulijua hilo ni muhimu sana kwako kuwa makini na maamuzi unayofanya kila siku ili uweze kuboresha maisha yako zaidi.

Ni kweli kwamba kuna wakati inaweza ikawa ni ngumu kwako kufanya maamuzi yatakayokupa mafanikio makubwa katika maisha yako, yote hiyo ni kwa sababu pengine ya kutaka kuona matokeo ya haraka zaidi. Kama umeamua kuwekeza ni muhimu sana kwako ukawa mvumilivu na kujipa muda ili kuweza kupata matokeo ya kile unachokitaka. Ukifanya hivyo, ule ugumu wa maamuzi unaouona hautakuwa shida kwako.


Kwa haraka haraka mpaka hapo unaona kuwa maamuzi ni kitu cha msingi sana katika maisha yako kuliko unavyofikiri.  Unapokesea kufanya maamuzi hata kama ni madogo vipi, ndivyo unavyozidi kubomoa maisha yako hata kama hujui. Hivyo basi, ni muhimu kwako kuwa na maamuzi mazuri na sahihi kila siku yatakayoweza kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio makubwa.

Unapokuwa na maamuzi haya sahihi, hii itakusaidia wewe kukuwezesha kustawisha uwezo wako  wa kuchagua maisha yanayofaa kila siku. Katika makala hii ya leo utaweza kujifunza hatua muhimu unazotakiwa kuzichukua katika maamuzi yako ili kuweza kuishi maisha ya mafanikio. Je, unajua ni hatua zipi zitakazokuongoza kuchagua kuishi maisha ya mafanikio?

Hizi Ndizo Hatua Muhimu Zitakazokuongoza Kufanya Maamuzi Yatakayokupa Mafanikio Makubwa.

1. Fikiria matokeo ya maamuzi yako.
Kabla ya kufanya uamuzi wowote ule katika maisha yako, fikiria kwa makini matokeo ya uamuzi wako huo. Ukichunguza matokeo ya uamuzi wa unaotaka kuuchukua hiyo itakusaidia kuwa makini sana na uamuzi wowote unaouchukua kwenye maisha yako. Kwani utakuwa umejua uamuzi huu unaweza kuboresha ama kubomoa maisha yangu kwa kiasi gani.

Pia kabla hujafanya uamuzi wowote ule jiulize hivi, uamuzi wangu huu utakuwa na matokeo gani katika maisha yangu baada ya mwaka mmoja, miaka miwili au hata miaka kumi ijayo. Kama uamuzi huo unaouchukua utaona unaharibu maisha yako kwa sehemu kubwa, ni bora ukaachana nao na ukafanya uamuzi tofauti utakao boresha maisha yako.



2. Chunguza kwa makini maamuzi unayohitaji kufanya.
Ni muhimu sana kuchunguza maamuzi unayotaka kufanya na sio tu kujifanyia maamuzi ambayo wakati mwingine hayawezi kukusaidia zaidi ya kukugharimu. Wengi wetu huwa ni watu wa kuiga maamuzi ya wengine kitu ambacho huweza kuathiri maisha yako moja kwa moja. Ni muhimu kujichunguza maamuzi unayotaka kuyafanya mara kwa mara.

Kwa mfano kama unataka kuwa na maisha mazuri ni lazima kwako kujiliza na kujichunguza ni kipi  ukifanye ambacho kitaweza kukupa hayo maisha unayoyatamani. Haitawezekana kwako kufikia maisha hayo kama tu utakuwa bado mtu wa kuishi maisha yaleyale ya kuendekeza marafiki wa uzembe ama kuendekeza matumizi ya hovyo. Ukiweza kujichunguza kwanza maamuzi unayoyafanya yatakusaidia kusonga mbele.

Kwa kumalizia makala hii, tambua kuwa hizo ndizo hatua muhimu ambazo zinaweza kukuongoza kufanya maamuzi ambayo yatakupa maisha ya mafanikio kwako na sio tu kujifanyia maamuzi ambayo hayawezi kukusaidia. Kumbuka kabla hujafanya maamuzi yoyote ni muhimu kufikiria matokeo ya maamuzi yako na kujichunguza kwa makini maamuzi unayoyataka kufanya yatakusaidia vipi kuboresha maisha yako.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kuwashirikisha wengine kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO ili kuboresha maisha yetu.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,


Apr 18, 2015

Siri Kubwa Ya Mafanikio Unayoitafuta Katika Maisha Yako ipo Hapa…

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako huwa unahitaji kuona ndoto zako zikitimia na kuyafurahia maisha katika uzuri wake. Kuna wakati pia katika maisha yako huwa unatamani kubadili maisha yako kwa sehemu kubwa na kufikia hata kuwa huru kifedha. Pia kuna wakati katika maisha yako huwa unatamani ujue ama utambue siri ya mafanikio kwa ujumla ilipo ili ufanikiwe kwa viwango vya juu kabisa kama unavyotaka. Hata hivyo, umekuwa ukishindwa kutokana na kutokujua siri hii.

Kama hiyo kwako ndiyo nia na shauku yako kubwa ya kutaka kujua siri kubwa ya mafanikio ilipo ili nawe uweze kufanikiwa kama hao wengine wanaliofanikiwa, hujakosea kusoma makala hii upo sahihi kwa asilimia zote. Kupitia makala hii utajua na kuelewa kwa uwazi siri ya mafanikio ilipo ambayo itakufanikisha. Lakini je? Ulishawahi kujiuliza siri hii ipo kwenye mambo gani? Sitaki uumize kichwa sana, ukweli ni huu, siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye mambo haya kama utayatekeleza:- 

1. Penda kile unachokifanya.
Hautaweza kufanikiwa katika maisha yako kama utakuwa unafanya mambo ambayo huyapendi katika maisha yako. Unapofanya jambo ambalo hulipendi kitu kikubwa kinachokutokea kwanza hutaweza kufanya kazi hiyo kwa moyo wote, utakuwa unafanya ilimradi tu, kama vile umelazimishwa na mtu. Lakini, si hivyo tu bali hata utendaji wako utakuwa wa kiholela ambao ndani yake hauna ubunifu wowote ule.

Siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye kufanya kile kitu unachokipenda na si vinginevyo. Asilimia kubwa ya watu wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao wanapenda vitu wanavyovifanya. Kama unataka kubadili hali yako uliyonayo sasa na kufikia mafanikio makubwa, kitu cha kwanza unachotakiwa kukifanya ni kuchagua kile unachokipenda na kukifanya kwa moyo wote, utaona mabadiliko makubwa sana katika maisha yako.


2. Anza kwa  kidogo.
Kwa kila unachonza kukifanya ni muhimu kwako kuanza kufanya kwa kidogo. Hii ina maana gani au inaashiria nini kwako? Unapoanza kufanya kwa kidogo hiyo inakuwa inakupa uzoefu na ukomavu kwa lile jambo ambalo unalifanya na hii itakusadia zaidi hasa pale unapokumbana na changamoto inakuwa ni rahisi sana kwako kuweza kupambana nazo na kuzikabili kwa urahisi zaidi.

Kuanza kwa kidogo hii ni moja ya siri kubwa ambayo inatumiwa na watu wengi wenye mafanikio kuweza kufika mbali.ieleweke kuwa kabla hujaanza kukimbia marathoni ni vizuri kuanza kukimbia mita chache ili kuweza kupata uzoefu zaidi. Hivi pia ndivyo ilivyo katika maisha yetu, unataka kufanikiwa sana na ukawa ambaye hushikiki anza kujenga uzoefu kwa mambo madogo ambayo utayamudu kwanza kwa vizuri.

3. Kuwa na nidhamu binafsi.
Pia huu ndio ukweli usiouweza kuupinga kuwa, mara nyingi siri kubwa ya mafanikio yetu ipo kwenye sisi wenyewe kuwa na nidhamu binafsi. Bila kuwa na nidhamu binafsi kupata mafanikio makubwa katika maisha yako, sahau kabisa na kitu ambacho hakitakuja kuwezekana. Unapokuwa unajiwekea nidhamu binafsi hiyo inakuwa inakujengea nguvu kubwa ya kukusadia kuweza kusonga mbele zaidi.

Kama umekuwa kwa muda mrefu ukihangaika na kutafuta siri gani kubwa iliyojificha ambayo inaweza kukusaidia kuweza kufikia mafanikio makubwa, tambua kuanzia sasa ni nidhamu binafsi. Kama unafikiri natania anza sasa kujiwekea nidhamu binafsi kwenye mambo yako halafu utanipa matokeo yake. Kama kweli upo makini na maisha na unataka kufanikiwa kwa viwango vya juu jifunze juu ya hili, utabadilisha sana maisha yako.

4. Kuwa mwaminifu.
Mafanikio yoyote unayoyatafuta yanakutaka ni lazima uwe mwaminifu. Unapokuwa mwaminifu uwe na uhakika ni lazima utaweza kutimiza chochote kile katika maisha yake hata iweje. Kwa nini uaminifu ni kitu muhimu sana kwako? Unapokuwa mwaminifu hiyo  inakusaidia kukujengea imani na wengine na kukuza ushirikiano kwa sehemu kubwa katika biashara unayoifanya ama kitu chochote.

Pasipo kuwa mwaminifu huwezi  kufanikiwa sana katika biashara yako au tasnia unayoifanya hata iweje. Kila utakapojaribu kutaka kufanikiwa utapata tabu sana. Na ninapozungumzia uaminifu na maaninisha ni lazima  uaminifu uanze kwako wewe na kwa wengine pia. Ni muhimu kujijengea uaminifu katika maisha yako pia wewe binafsi. Unaposhindwa kuwa mwaminifu  kwako pia na kushindwa kutimiza ahadi ulizojiwekea hiyo itakupa tabu sana na utashindwa kutimiza chochote.

5. Kufanya kazi kwa bidii.
Siri kubwa ya mafanikio ipo pia kwenye kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Hakuna mafanikio makubwa uatakayoweza kuyapata kama wewe utakuwa sio mtu wa kuweza kufanya kazi zako kwa bidii, kwa maarifa na kujituma kwa hali ya juu. Ukichunguza kidogo tu, utagundua kuwa watu wengi wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao wamejitoa na kufanya kazi kazi kwa juhudi zao zote bila kuchoka.

Kama unataka kufikia mafanikio makubwa ambayo umekuwa ukiyahitaji na kuishi maisha yoyote yale ya ndoto zako, hilo linawezekana lakini litakuja tu kwa kufanya kazi kwa bidii. Unapofanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa mapema na kuwa king’ang’azi wa ndoto zako uwe na uhakika kwa sehemu kubwa ni lazima mafanikio utayafikia. Hakuna kitu kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa hata kidogo kama utakuwa mchapa kazi.

Kwa kuhitimisha makala hii, elewa kuwa utafanya kila unalofanya katika maisha yako, lakini siri kubwa ya kuweza kutimiza ndoto zako ulizojiwekea ipo katika hayo mambo na hiyo ndiyo siri ya kufikia mafanikio makubwa unayatafuta katika maisha yako, vinginevyo utasumbuka sana katika maisha yako kama utakuwa unaishi kinyume na hayo.

Kwa kujifunza zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Apr 14, 2015

Ukishajiwekea Malengo, Kinachofuata Ni Hiki Hapa…Ili Kutimiza Malengo Yako Kwa Urahisi.

No comments :
Ni ukweli uliowazi, mara nyingi ukishajua unataka kwenda wapi katika safari yako ya mafanikio ina maana kwamba kila kitu kwako ni rahisi. Kama unataka kuwa muuza ndizi maarufu, kuwa dereva mkuu, mpiga kiwi mwenye sifa mjini kote, mwanamziki wa kimataifa, ni rahisi kujua ufanye nini kufika huko unakotaka kwenda.
 
Inakuwa kwako ni rahisi kuweza kuvumilia shida, kusubiri, kutokata tamaa, kujipa moyo na kuwa na matumaini yasiyofifia kwa kuwa unajua unachokitafuta . Unaweza kuuingiza mtaani ndizi zisinunuliwe hata moja, lakini kwa kuwa unajua unachokitafuta, yaani kuwa muuza ndizi maarufu baadaye, kikwazo hicho kimoja hakitakuvunja nguvu. Kwanini? Kwa sababu hapa utakuwa unaangalia picha kubwa, badala ya kapicha kadogo.

Hii ya kuangalia picha kubwa badala ya ndogo, pia ndiyo siri kubwa ya mafanikio mengine maishani. Kuangalia picha kubwa badala ya ndogo ina maana kwamba, unapoingia kwenye matatizo au changamoto, itakusaidia kukabiliana na changamoto hizo kwa urahisi. Kama umeanzisha mgahawa, lakini lengo lake ni kuja kuwa na hotel kubwa ya hadhi, unapopata matatizo, chukulia hayo ni mafunzo unayoyapata kuelekea kwenye hilo jambo kubwa unalolitaka.

Kila unapokuwa unafikiri kuwa kuna jambo kubwa sana ambalo ni lazima uweze kulitimiza na ndilo lengo lako kuu, hutaweza kukatishwa tamaa na matatizo katika hiki kidogo unachoanza nacho. Hata kama utafungua biashara fulani kwa muda, halafu ukaja kuifunguka kutokana na matatizo au changamoto hizo, lililo muhimu kwako ni kujifunza kwa changamoto hizo na kuanza upya mpaka kufikia lengo ulilojiwekea.


Mtu anayejua anaelekea wapi kwenye safari yake haamui kuvunja safari hiyo kwa sababu basi limeharibika. Atasubiri mpaka litengenezwe ili aendelee na safari. Lakini kama hajui hasa anaelekea wapi, lakini yumo kwenye basi liloharibika, likipita lori kuelekea kule alikotokea, anaweza kulidandia, kwani anachotaka yeye ni kuonekana tu yuko safarini, bila kujali anaelekea wapi hasa.


Kwa kawaida tukishachagua tunataka kuwa nani au kufanya nini, tutajiuliza namna tutakavyoanza kuelekea huko. Kwa bahati mbaya, wengi wetu tunataka tunapoamua leo, basi asubuhi inayofuata tuwe tumeshakamilisha kila kitu au kufanikiwa. Kama tumeamua kumiliki duka au kufanya biashara ya mazao au kuja kuwa madaktari, ni lazima tujiulize kama tuna chochote cha kutusaidia kuanza safari ya kuelekea huko. Ukishajua una chochote au tayari  umejiwekea malengo kinachofuata kwako ili kutimiza malengo hayo ni:- 

1. Kwanza, ni lazima uwe na  elimu na maarifa.
Kuna malengo fulani yanahitaji tuwe na elimu fulani, mengine yanahitaji tuwe na uzoefu fulani na mengine yanahitaji muda kwani yana hatua kadhaa ambazo ni lazima tuzipitie kwanza. Kama mtu anapenda sana na ameamua kuwa mpambaji wa maharusi na mpishi wa keki za harusi, itabidi asomee utaalamu huo. 

Kwa mfano kama mtu atakuwa ameamua kwamba, atakuwa anasafirisha vyakula kutoka mikoani na kuvipeleka jijini Dar es salaam, ni lazima ajue vyakula gani na vinatokea maeneo gani ya nchi, vinasafirishwa vipi na msimu upi ambao unafaa kupelekwa jijini Dar es salaam na sababu gani? Kama ni mwanafunzi anataka kuja kuwa mwandishi wa habari, ni lazima tangu awali ajue ni masomo gani anatakiwa kuyazingatia.

Elimu na maarifa siyo lazima viwe vitu vya darasani kama unavyoweza kufikiri. Kama tumegundua jambo au mambo ambayo tunataka kuyafanya maishani, ufahamu kuhusu jambo au mambo hayo ni muhimu sana kwako. Ufahamu huu huweza kupatikana kwa njia mbalimbali na kwa kawaida upo, ni juu yetu kuutafuta.


2. Pili, ni lazima uwe na ushirikiano na wengine.

Kuna shughuli nyingine inabidi tuwe na watu ambao tayari wamo humo kutuelekeza. Inawezekana kabisa tunataka kuwa wafanyabiashara, inabidi muda mwingi kutafuta ushirikiano na wafanyabiashara ili kuweza kutuonyesha mwanga wa kile ambacho tunataka kukifanya.

Ni jambo la kushangaza kugundua kwamba mtu ana kipaji fulani, ana ujuzi fulani ana maarifa fulani, lakini hana uwezo kuonyesha na pengine kuyatumia kwa faida kutokana na ukosefu wa rasilimali. Wakati huohuo inawezekana kwamba kuna watu wenye raslimali ambao wanatafuta mtu au watu wa kipaji chake, lakini hawawaoni.


Kama unataka kufika mbali ni lazima tukubali kushirikiana na wengine kwa njia moja au nyingine. Tukiwa wachoyo kamwe hatutamudu. Wakati mwingine siyo uchoyo, bali hatujui kwamba vipaji, maarifa na uwezo tulionao tunaweza kutafuta watu wa kushirikiana nao na kwa pamoja tukamudu. Tunakaa na kusubiri hao wengine watubaini ili watutembelee katika kufanya nao mambo fulani. Ni sisi ndiyo tunaotakiwa kuwatafuta wengine ili tufanye nao.

Hakikisha unaendelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa maarifa na elimu bora itakayoboresha maisha yako.

TUNAKUTAKIA USHINDI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,




Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo.

No comments :
Je, huwa unaingia kwenye msongo wa mawazo haraka au kirahisi? Kama jibu ni ndiyo, kwa nini usijiulize ni kwa vipi unaingia kwenye kusongeka? Kitu ninachoamini kwa kujiuliza ni kwa nini mtu anasongeka, kunakuwa kuna mengi ya kujifunza, lakini wakati mwingine, mengi ya kushangaza pia.

Kusongeka humfanya mtu kuona kwamba, kila kitu kinakwenda hovyo, kila kitu kiko shaghalaghabala, kila kitu kiko hovyo. Wanaoingia kwenye kusongeka kiakili hujiambia siku zote kwamba, kila kitu hakina maana, yakiwemo maisha yao pia.

Je, kitu cha kujiuliza hapa kama itatokea nikaingia kwenye kusongeka kiakili nitakuwa nazungumza vipi, yaani kwa sauti namna gani? Bila shaka nitakuwa nazungumza kwa sauti ya chini na pia ya kuburuza. Siyo kuzungumza tu, bali hata kusimama au kutembea kwangu kutakuwa ni kwa kujiinamia na kuona kila kitu kwangu kimeharibika.

Hivi ndivyo wengi wanavyojiona wanapokuwa wamesongeka kimawazo, ingawa kuna wakati mwingine huweza hata kuonyesha nyuso za huzuni na simanzi, hiyo yote huweza kutusaidia sisi kubaini na kutambua wazi kinachoendelea kwenye akili zao kuwa wana mawazo mengi au kusongeka sana ndiko kunakowasumbua.



Kama upo kwenye kusongeka na unaendeleza mawazo hayohayo kila mara ambayo yanakupekea wewe kusongeka hiyo inakuwa sawa na wewe kuamua kujichanganya kwenye maisha yako. Na unapoamua kujichanganya mwenyewe kwenye maisha yako, tambua kabisa hakuna utakachoweza kufanikisha, zaidi ya kuharibu maisha yako tu.

Ni vizuri kwako kujua kuwa unaouwezo wa kuweza kubadili kusongeka kwako kimawazo na kuishi huru kabisa. Najua inaweza ikawa kwako sio rahisi kuelewa, lakini ninachotaka kukwambia kuwa unaweza kuondokana na kusongeka kwako, ikiwa tu utaweza kubadili namna ya kuyatazama mambo au matukio katika maisha yako.

Ni kweli kwamba, kusongeka kiakili husababishwa na mambo mbalimbali, lakini sisi huweza kufanya kusongeka huko kushika mizizi kwa namna tunavyokaa, kusimama au hata kwa namna yetu tunavyofikiri na kutafsiri mambo. Tunapokaa au kufikiri kwa namna ya kinyonge, tunafanya mawazo yanayotupitia kuwa ya kinyonge pia.

Kwa kuhakikisha hili zaidi, hebu jaribu kumuuliza au kumchunguza mtu anayetembea huku akiwa ameinama na Yule anayejiinamia kama atakwambia kuwa anafikiria mambo mazuri. Ni wazi kabisa mtu kama huyu ni lazima atakuwa anafikiria mambo mabaya yanayopelekea kusongeka kwake kimawazo.

Kufikiri kwetu kukiwa nako ni kule kunakotutia hofu, mashaka na kutuingiza kwenye kijicho, ni lazima tutajikuta tukianza kusimama au kutembea kwa njia yenye kuonesha kukata tamaa, wanyonge na hata tusiojiweza. Kwa nini tusibadili mambo hayo ili tuweze kuondoka kwenye huzuni kali au kusongeka? Kwa kujiambia mambo yenye kutia huzuni na simanzi tunajiingiza kwenye huzuni bila kujua.

Lakini kumbuka kuwa kwa kujiambia mambo mazuri na yenye kutia moyo ndivyo tunajikuta ambavyo tunaingia mahali ambapo tunayaona au kuyatazama maisha katika mwanga mkubwa zaidi. Na hivi ndivyo tunavyoweza kuondokana na msongo wa mawazo kwa kujiambia mambo mazuri kila mara katika maisha yetu na si vinginevyo.

Kwa kuwa tunaweza kufikiri kwa namna isiyoumiza, tunaweza kwa hali hiyo kujitoa kwenye kusongeka. Kuna wakati mtu mwenye msongo wa mawazo anahitaji tabasamu tu au kujiambia kimoyomoyo kwamba, kila kitu kiko sahihi na kinakwenda kama kilivyotarajiwa. Halafu, ni kweli, ataanza kuhisi tofauti, kuhisi ukamilifu na uwezo zaidi katika maisha yake na kuondokana na kusongeka ambako kunaweza kuwa kunamtesa.

Ninaomba nikutakie mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.

MAKALA HII IMEANDIKWA NA DEVOTA KAUKI WA MANYONI, SINGIDA.

Kama una maoni au ushauri unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa email truesuccess89@gmail.com

Apr 2, 2015

Hivi Ndivyo Nguvu Ya Mawazo Yako Inavyoweza kukuepusha Na Matatizo.

No comments :
Umewahi kupata  hisia ama mawazo fulani kuhusu jambo fulani, lakini usijue hisia hizo zina maana gani na wala zinatokana na nini? Basi hisia hizo ndiyo hasa nguvu ya ufahamu wako au ‘intuition’, kama wataalamu wanavyoita. Nguvu za ufahamu ni nini? Fikiria ufahamu kama mshauri wako aliye karibu nawe akitaka kukusaidia na kukuongoza katika kila jambo.
 
Tatizo kubwa la mshirika wako huyu ni kwamba huwa hazungumzi lugha uliyoizoea wewe. Hii ni kwamba si wakati wote mshirika huyu hutoa kauli na kutoa maelekezo katika lugha uliyoizoea kuisikia na kuielewa kirahisi. Ili kuweza kukuza nguvu za ufahamu wako, unawajibika kuielewa lugha yake na huu ndio mtihani mkubwa katika hilo.

Unaweza vipi kujua namna ufahamu ufanyavyo kazi, au jinsi ya kuilewa lugha yake? Ufahamu unatumia ujumbe katika miundo tofauti wakati wote, kila siku. Wakati mwingine ufahamu huenda ukawa ni hisia hiyo niliyoilezea hapo mwanzo, yaani wakati unajua jambo fulani, lakini huna njia ya kufafanua kile unachofahamu.

Kwa mfano, unaweza ukawa uko barabarani unaendesha gari, na mara gari lingine likakupita kwa kasi. Gari hilo baadaye linapunguza mwendo na kuonekana kukuziba usiendelee vema na safari yako. Unaamua kulipita, lakini unasita ghafla na kuamua kuliacha liendelee kuwa mbele yako, ingawa unaliona kama linakuchelewesha na safari yako uliyonayo.



Muda mfupi baadaye, unalishuhudia gari hilo lililo mbele yako, likigonga gari lilolo mbele yake kwa kushindwa kusimama wakati lilipolikaribia. Unawaza akilini kwamba , kama ungeamua kulipita gari lile, bila shaka wewe ndiye ungekuwa umegongwa saa hizi. Hii yote inadhihirisha uwezo au nguvu kubwa ya ufahamu jinsi inavyoweza kufanya kazi kwako.


Mfano mwingine, tuchukulie unatembea kandokando ya barabara ukiwa unazungumza na mtu. Mazungumzo yenu yanakuwa ni ya wewe kuomba kitu Fulani kwake na kusisitiza. Ghafla mtu unayezungumza naye anabadilika na kuonekana kukasirika. Anaamua kukuacha na kuongeza mwendo.

Ukiwa katika hali ya kushangaa kwanini amekuacha kuna wazo linakujia kuwa umfuate ili uendelee kuzungumza naye, lakini ghafla wazo linakujia usifanye hivyo bila kukupa sababu, ni kwa nini usifanye hivyo. Mita chache baadaye, gari linalokuja kwa kasi linaacha njia na kumgonga Yule jamaa yako uliyekuwa ukizungumza naye aliye mbele yako.

Si hivyo tu, kuna wakati unaweza ukajikuta unataka kusafiri. Mipango ya safari unakuwa umeiweka sawa, kinachokuwa kimebakiwa ni wewe tu kuondoka. Lakini, kitu cha kushangaza unaanza kujihisi mzito, unajivuta mpaka lile gari linakuacha. Muda mfupi tokea uachwe na gari lile unakuja kupigiwa simu kuwa gari lile limepata ajali mbaya sana.

Akili mwako sasa unaanza kujiuliza nini kingetokea kama ningepanda lile gari. Bila shaka utaanza kuwaza ni lazima pengine ningekuwa nimepoteza maisha. Lakini ni nini kilichokuokoa basi hadi ukashindwa kupanda lile gari bila kujijua, wewe mwenyewe unashangaa na unashindwa kupata majibu hasa yaliyokamili kwako. 

Pamoja na kuwa unaweza ukawa hujui kitu kinachokuokoa, lakini ni ukweli kwamba kinachokusaidia ama kukuokoa ni nguvu zako za ufahamu ulizonazo. Nguvu hizi za ufahamu kuna wakati zinaweza kuokoa maisha yako ikiwa utasikiliza kile zinachosema. Watu wengi wamewahi kuokolewa na nguvu za ufahamu wao bila kujijua.

Kuna wakati katika maisha yako kabla ya jambo baya halijaweza kukutokea, nywele za nyuma ya kichwa huwa kama unahisi zinasimama. Hii yote ufahamu wako huwa unataka kukuonyesha kuwa mbele kuna hatari.  Ikiwa unataka kuvuka barabara kwa mfano, basi ujue zinakuonya usivuke, kama unataka kwenda mahali basi ujue zinakuonya usifanye hivyo.

Nguvu hizi za ufahamu pia  huweza kukuokoa pale ulipotaka kwenda mahali na kusita ghafla, halafu huko ambako ungeenda kukatokea ajali ama mtu kupoteza maisha. Hivyo, huwezi kulijua hilo kwa sababu hukwenda huko, lakini kikubwa kinachokuwa kimekuokoa ni uwezo wa nguvu zako hizi. Ni nguvu hizi za ufahamu ambazo hufanya kazi kwa njia ambayo ni ya kushangaza kidogo. 

Ufahamu huu huja kwa sura tofauti. Fikiria ufahamu kama mshirika wako, kuna wakati mshirika huyu atazungumza na wewe kwa hisia tu, kuna wakati atazungumza kwa maneno kupitia mtu mwingine, kuna wakati atakupa ishara, kuna wakati atajaribu kukuzuia kufanya jambo fulani ambalo sio zuri kwako. Uko umuhimu wa kujua namna anavyoweza kuzungumza na wewe.

Kwa mfano, kama nguvu hizi za hisia zitazungumza nawe kupitia hisia, zinaweza kuwa hisia nzito  zinazokutaka ufanye kitu fulani ama uache kitu na kufanya kile kwa nguvu zako zote.

Kuna wakati nguvu za ufahamu zaweza kuzungumza nawe kupitia mtu mwingine. Kwa mfano, unaweza kuwa unafikiria kununua nyumba mpya, lakini huna uhakika ununue eneo gani. Mtu wa kwanza unayezungumza naye anakutajia eneo fulani.
 
Mtu wa pili unayejaribu kuzungumza naye anakutajia eneo hilohilo, wa tatu naye anakutajia eneo hilohilo. Unatazama kwenye gazeti na kukuta makala inayolisifia eneo hilo ambalo marafiki zako walikutajia kuwa ni eneo bora na linalokufaa kwa kuishi. Hadi hapa, ni wazi nguvu za ufahamu wako zitakusaidia kulifikiria eneo hilo na huenda sasa ukaamua kwenda kuliona.

Kuna wakati nguvu za ufahamu wako zitakuongoza kwa kukupa ishara. Zitakuongoza kwa kukupa ishara kwa kuona kitu kinachofanana na kile unachokitafuta. Kwa kuona kitu ambacho kipo sawa na kile unachokitafutia jibu hiyo moja kwa moja ni ishara tosha kwako.

Kuna wakati nguvu za ufahamu wako zitajaribu kukuzuia kuchukua hatua fulani. Huenda unataka kununua nyumba kwenye eneo fulani, lakini unagundua kwamba si ya hadhi unayotaka ama ni ya bei ya juu sana. Hii ni ishara ya kutaka utafute eneo jingine, ama kuwa na subira mpaka utakapopata nyumba kwenye eneo sahihi, ama kufikiria eneo lingine.

Huenda unataka kazi mahali fulani, lakini unakuta hakuna mwelekeo hata wa namna ya kuifatilia kazi hiyo ama wapi pa kuanzia. Hapa huenda nguvu za ufahamu zinakuelekeza utafute kwingine na kutokuendelea kuifatilia kazi hiyo tena uliyoelekeza mawazo yako. Katika matukio yote, ujumbe sio utakuwa wazi kama unavyotaka uwe.

Namna nguvu za ufahamu zinavyozungumza nasi, si siku zote unaeleweka kiurahisi. Lakini ikiwa utaendelea kuupima na kuendelea kutafuta jibu, jibu litakuwa wazi. Hisia zitakuwa nzito. Ishara zitaendelea kurudiwa na kuwa wazi. Ujumbe kutoka kwa watu wengine utarudiwa tena na tena na hatimaye ujumbe utakuwa wazi.

Kuna wakati huenda usielewe ujumbe mpaka miaka kadhaa baadaye. Lakini kuna siku utaonesha maana itakayoonekana katika wakati mwafaka utakapotimia. Kwa kifupi hivyo ndivyo, nguvu ya ufahamu inavyofanya kazi kwako na kukuongoza katika mambo mengi ambayo kuna wakati hata wewe hujui.

Nakutakia mafanikio mema katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

IMANI NGWANGWALU,

Apr 1, 2015

Hawa Ndio Watu 5 Hatari Wanaoweza kuharibu Maisha Yako.

No comments :
Ni ukweli na imedhibitishwa katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya malezi na dini zetu, kwamba huwa tunaambukizwa tabia nzuri au mbaya na wale watu ambao kwa muda mrefu tuko nao na tunawaamini kwa kiasi fulani. Watu hao wanaweza kuwa wazazi, marafiki, wafanyakazi wenzetu, wanafunzi wenzetu, jirani zetu na wengine.
 
Nimeona siyo vibaya kwa hali hiyo, kukushauri kwamba, unapaswa kuwa makini sana na watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa hata kama tunawapenda vipi.  Hili si jambo la mzaha kama unavyoweza kulitazama kijuu-juu. Ni jambo la dhati. Kwa haraka haraka naomba nikutajie watu hawa, wanaoweza kuharibu maisha yako.

1. Watu wanaofikiri, kusema na kutenda hasi.
Hawa ni watu ambao siku zote huwa hawaoni suluhu ya jambo, bali kuona matatizo tu. Ni watu ambao huzingatia zaidi mambo yasiyopendeza na siyo yale yanayopendeza. Mtu anaweza kufanikiwa kupata zabuni ya shilingi milioni 20 na kukosa ile ya milioni 100. Badala ya kushukuru na kuangalia ile zabuni aliyoipata, atazingatia na kuumizwa kichwa na kile alichokikosa. 

Hawa huwa ni watu ambao hata wakifanikiwa kivipi kimapato,bado maisha yao yanakuwa yamezingwa na hofu zisizoisha, kutoridhika na kutamani tena na tena bila ukomo. Kwao kushindwa kupata wakitakacho, bila kujali ni kitu gani, ndilo jambo linalopewa uzito badala ya kile walichokipata.

Lakini kwa bahati mbaya, watu wa aina hii huwa ni vigumu pia kufanikiwa kimapato katika Nyanja waitakayo. Ni kwa sababu, kwao matatizo madogo kuyaongeza chumvi nyingi na kuonekana kuwa makubwa sana. Kwao kushindwa jambo wanakutazama kama msiba mkubwa ajabu. Hukata tamaa haraka kwenye matatizo na hivyo hawapati nafasi ya kujifunza kupitia katika matatizo yao.

Ukiwa karibu na watu wa namna hii, ni wazi utadhani maisha ni tahadhari na mashindano ambayo mshindwa hapaswi kuishi. Lakini hata kama nawe uko hivyo, inabidi ujue kwamba, una safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio kama kweli unayataka. Watu wa aina hii wana nguvu hasi za kuweza kuambukiza maradhi yao kirahisi kwa wengine.

  
2. Watu ambao ni wafujaji wa mali.
Bila shaka umewahi kusikia watu wakisema ‘ponda mali kufa kwaja’. Sina uhakika watu wanaoamini katika usemi huu wana maana gani? Inawezekana ukawa na ukweli kama mtu anaamini kwamba yeye ni huo mwili wake na maisha yake huisha pale mwili wake unapoachana na mawazo au roho yake. Lakini hata kama mtu anaamini hivyo, bado kuna swali la msingi kwamba, maisha ni yeye peke yake?

Kuna wengine wanaoamini hivyo ambao wamesomeshwa kwa fedha za mifuko ambayo waanzilishi wake walishakufa zamani. Ni watu waliohangaika kutafuta, wakapata na kuweka ili wateja waje wawasaidie wengine. Sasa unashindwa kujua inakuaje mtu huyu anayeamini katika kuponda mali kufa kwaja asijiulize mchango wake kwa wengine ambao atawaachia nyuma. 

Hatukuletwa duniani ili kula na kuvaa vizuri na kufanya mapenzi sana, halafu tufe. Tuliletwa kwa kusudi maalumu na kusudi hilo kwa sehemu kubwa ni mchango wetu kwetu na kwa wengine hapa duniani. Elewa tu, unapaswa kuwaepuka watu ambao hawaamini kwamba wanapaswa kuweka akiba ili kufanya mambo ambayo yatawasaidia wengine baadaye. Wengine wao wanaweza kuwa ni familia zao, ndugu au jamaa zao, ama jamii nzima kwa ujumla. Bila shaka huko ndiko kufanikiwa kwa juu kabisa, tunapokuzungumzia kufanikiwa kwa upana wake.

3. Watu wasiojua cha kufanya baadaye.
Kuna watu ambao ukweli ni kwamba hawajui cha kufanya muda ujao. Watu hawa hula chakula tu, kunywa pombe tu, kucheza bao au karata tu, lakini wafanye jambo gani la kuwasaidia wao au wengine inawawia vigumu. Ni afadhali mtu ambaye hana malengo lakini kuna jambo au mambo anafanya, hawa hawana wanachofanya kabisa.

Kazi yao ni kutafuta mtu wa kumlaumu kwa kushindwa kwao kuwajibika. Hata wakipewa shughuli, watashindwa na kurejea kwenye kuishi kama mawe au kuku wa kufugwa bandani. Wanajua sana watu hawa kusingizia serikali au viongozi wa nchi. ‘wanaiba sana, ndiyo maana wengine hatuna cha kufanya’. Ni hodari sana kulaumu ndugu, ama jamaa zao. 

Hawa ni watu ambao kwa kawaida ukiwaendekeza wanakufikisha mahali ambapo unaweza kuamini kwamba maisha yana kasoro na wanaweza kukufanya uamini kwamba hata wewe hutendi mema kufanya shughuli na kuingiza kipato kingi. Dawa ni kuwakwepa kwa mbali na wala usikubali ‘kuwafuga’, watakuharibia sana maisha yako. 

4. Watu wanaoharibu majina ya wengine.
Siyo rahisi kwa mtu kufanikiwa kama ana kijicho, dhidi ya watu waliofanikiwa. Kuna watu ambao ni maadui wa watu wote wanaofanya vizuri. Hutumia kila wanaloweza kuwaharibu ama kuwazuia ili wasiende mbali. Wanaweza kukuza majungu au sifa mbaya kwa watu ambao wanaonyesha kuelekea kwenye mafanikio au hata kufanya njama tu ili waanguke. Badala ya kuwa karibu na hao wanaoelekea kwenye mafanikio ili wajifunze kitu, hutaka kuwaona wameanguka, hivyo muda wao mwingi huupoteza katika kutafuta na kumharibia yule au huyu na sio katika kutafuta mafanikio.

Kufuatana au kuwa karibu na watu hawa ni sawa na kutaka kuambukizwa bure nguvu hizi hasi ambazo zinadhuru sana bila mhusika kujua. Kwa nini tusijaribu kuiga na kujifunza kupitia mafanikio ya wengine katika kutafuta mafanikio yetu, badala ya kuwachukia? Kwa nini tusiamini kwamba wengine wakifanikiwa, nasi bila kujua tumefanikiwa pia? Kama kweli tunataka mafanikio ni lazima tuwaepuke watu hawa wenye kijicho na chuki.

5. Watu wasipenda shida wala usumbufu.
Hawa huwa ni watu ambao idadi yao inazidi kuwa kubwa kila kuchao. Ni watu ambao mara nyingi wakishasoma basi kila kitu huishia hapo na hutamani ama hupenda zaidi kila kitu kiletwe miguuni mwao. Ni watu ambao hawana juhudi wala ubunifu kwa kile wanachokifanya katika maisha yao. Watu hawa huwa ni watu wa jua kucha, jua kuzama siyo zaidi ya hapo. Matokeo yake ni kupata shida katika maisha. Pia hawa ni watu hatari sana kwako unaotakiwa kuwaepuka sana.

Hao ndio watu hatari ambao usipokuwa nao makini wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa sana. 

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila siku.

IMANI NGWANGWALU,


.