google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Aug 31, 2015

Tabia Tatu Muhimu Ambazo Watu Wenye Mafanikio Wanazitumia Kila Siku Kufikia Mafanikio Makubwa.

No comments :
Njia pekee na ya haraka kwa wewe kufikia mafanikio makubwa ni kuhakikisha unajijengea tabia kama walizonazo watu wenye mafanikio makubwa. Watu wenye mafanikio makubwa katika maisha yao wana tabia za aina fulani ambazo wanazifuata kila siku bila kuacha. Ni tabia hizo hizo ambazo zinawasaidia sana kuwafanikisha kwa kile wanachokifanya.
Ili uweze kufanikiwa na hatimaye kufikia viwango angalau vinavyofanana na wao, unalazimika kujifunza kujijengea tabia kama walizonazo. Hiki ndicho kitu cha lazima ambacho unatakiwa kufanya kila wakati. Bila kujijengea tabia hizo, suala la kuwa na mafanikio makubwa sahau katika maisha yako, zaidi  utaishia kuwa kama ulivyo sasa na maisha yako ya kawaida tu.
Usije ukafikiria nasema hivi kwa lengo la kukatisha tamaa au ukaona kwamba na kudharau huwezi kitu, hapana. Ninachotaka ujue hapa  huo ndio ukweli wa wazi ambao ninaotakiwa nikwambia uujue, sitaki kukudanganya kwa chochote, ni lazima kujijengea tabia hizo kwa faida zetu wenyewe na mafanikio yetu.
Na pia tambua kwamba tabia hizo ndizo zilizowasadia na kuwafikisha watu kama akina Bill Gates, Warren Buffet, Brian Tracy na wengineo wengi wenye mafanikio makubwa pale walipo sasa. Maisha ya watu hawa siku zote wanazitenda tabia hizi na kuzifuatilia bila kuacha. Unaweza ukawa ni mmoja watu kama hawa ikiwa utakuwa na tabia kama zao. Je, Unajua ni tabia zipi hasa walizonazo?
1. Kupangilia siku inayofuata mapema.
Unaweza ukafikiri ni kitu cha kitoto lakini huo ndiyo ukweli, watu wenye mafanikio siku zote wamejijengea utaratibu wa kupangilia siku zao mapema ikiwezekana kabla. Nakumbuka wakati ninajijengea tabia hii mwanzoni niliona ni kama kitu kinachopteza muda na wala hakina maana yoyote ile kwangu.
Lakini nilipouzoea utaratibu huu nilikuja kugundua unapopangilia siku yako mapema, mambo yako mengi unakuwa unayafnya kwa urahisi na ufanisi mkubwa.  Hii inakuwa hivi kwa sababu unapopangilia siku kila kitu kinakuwa kwenye utaratibu na ratiba ya utekelezaji. Hivyo inakuwa sio rahisi kupoteza muda kwa namna yoyote ile.
Kwa msingi huo, matokeo chanya utayaona ikiwa utafuata tabia kama hii. Kabla hujalala jizoeze kila siku kupanga mambo yako mapema na kujua kwa siku ya kesho unakwenda kufanya nini?. Kwa kadri siku zinavyosonga utazoea na utaona utaratibu ni wa kawaida. Ni muhimu sana kwako kujifunza tabia hii ya kupangilia siku yako mapema ili kufanikiwa zaidi.

2. Kuweka vipaumbele mapema.
Watu wenye mafanikio mbali na kuipangilia siku nzima ya kesho mapema, lakini  ni watu wenye utaratibu mzuri wa kujiwekea vipaumbele mapema kabla ya siku inayofuata haijaaanza. Wanakuwa ni watu wa kujua kesho wataanza kufanya kazi gani na itafuatia kazi gani tena. Hakuna ajali wala mshituko wa kiutendaji kwao. Kila kitu kimepangwa tayari katika utaratibu ambao ni rahisi kuweza kufuatwa.
Watu hawa wanajua bila vipaumbele hakuna kitakachoweza kufanikiwa zaidi ya kurukia hiki au kile katika kazi na kujikuta ni mtu wa kugusa na kuacha kazi. Kwa sababu hujiwekei vipaumbele unaweza ukawa unashangga siku nzima ya kazi hujafanya kazi ya maana zaidi ya kuruka ruka mara huku mara kule. Hiki ni kitu ambacho kinawatokea wengi.
Hata ukija kuangalia mazingira mengi ya kazi nyingi zinafanywa bila ufanisi kwa sababu ya kukosa vipumbele. Ukijifunza kuweka vipaumbele kazi zako nyingi utaweza kuzisukuma kwa mwendo mkubwa kuliko unavyofikiri. Kwa sababu ndani yako unakuwa na kitu kinachokwambia ni lazima nifanye kitu hiki. Ukichunguza siri kubwa mojawapo ya watu wenye mafanikio umejificha kwenye tabia hii ambayo siyo rahisi kwako kujua.
3. Kukamilisha kazi waliyoianza mpaka mwisho.
Kama unataka usifanikiwe katika maisha yako jiwekee utaratibu wa kuanza kazi nyingine kabla hujamaliza ile ya kwanza. Kwa maisha hayo ukiamua kuyachagua kwako, suala la kuwa na mafanikio litabaki kuwa kwako hadithi. Wapo watu ambao maisha yao yako hivi, ni watu wa mipango mingi hivyo kujikuta wanarukia mpango huu mara ule lakini yote ikiwa inatakiwa umaliziwaji.
Watu wenye mafanikio ni watu wa kulenga kitu kimoja na wanahakikisha kumekamilika na kufuata kingine tena. Hata siku moja hawarukii mambo, ni watulivu ndani ya mioyo yao lakini pia ni watu wa kujizuia kukurupuka. Hii ni moja ya tabia waliyojijengea na inawasidia kufikia mafanikio makubwa katika maisha yao siku zote.
Hitimisho
Ikiwa utaendeleza tabia hizi tatu katika maisha yako, uwe na uhakika ufanisi na utendaji wako wa kazi utaongezeka na kuwa wa kiwango cha juu.
Kwa makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuboresha maisha yako kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,





Aug 24, 2015

Jinsi Unavyoweza Kushinda Tatizo Ulilonalo Na Kuishi Maisha Ya Ushindi Na Furaha.

No comments :
Kila mmoja wetu katika maisha yake huwa anakabiliana na matatizo ya aina fulani, ambayo katika hali ya kawaida huwa siyo rahisi kuyakwepa. Matatizo haya mara nyingi huwa yanajitokeza katika biashara zetu, familia na wakati mwingine ni matatizo ya mtu binafsi ambayo huwa nayo. Wakati mwingine matatizo haya, huwa yanaonekana ni makubwa sana kwetu kama mlima kiasi kwamba tunaanza kufikiri tunashindwa kuyamudu.  

Kutokana na matatizo haya wapo ambao hufikiri na kujiona wanamkosi na wapo ambao hufikiri kuwa wamerithi kwa namna fulani matatizo. Kila mtu huja na mtazamo wake kutokana na matatizo yanayomkabili. Kitu wasichokijua kumbe ndani yao wanauwezo mkubwa wa kushinda matatizo waliyonayo na kuishi kwa ushindi ili mradi tu waitambue siri hiyo na kuweza kuitumia vizuri.
Katika makala hii utajifunza njia, mbinu na mikakati ya kukusaidia kushinda tatizo ulilonalo na kuishi maisha ya ushindi. Utatambua jinsi unavyoweza kuhamasika na kujiamini wewe mwenyewe binafsi kuwa unaweza kutatua tatizo lako na kufanikiwa kusonga mbele bila shida yoyote. Ieleweke kuwa kila tatizo ndani yake huwa lina njia ya kulitatua hata liwe kubwa vipi.
Inaweza isiwe rahisi sana kwako kunielewa lakini, kwa vyovyote vile iwavyo kama una tatizo linalokukabili huo si mwisho wa kufanikiwa kwako. Bali ni dalili tosha ya kukupeleka kwenye mafanikio unayoyataka. Unaweza ukajiuliza kwa nini hiyo iko hivyo? Ni kwa sababu matatizo yanakuwa yanakupa ukomavu ambao hukuwa nao hapo mwanzo ikiwa utajifunza kupitia matatizo hayo.
Unawezaje kushinda matatizo uliyonayo na kuishi maisha ya furaha na ushindi?  
1. Amini inawezekana kulitatua tatizo ulilonalo.
Siku zote ushindi wa mambo yote huwa unaanzia kwenye kuamini. Kuamini ndiyo nguzo kuu ya mafanikio. Unapokuwa na imani inakusaidia kuweza kutatua tatizo ulilonalo hata liwe kubwa vipi. Kitendo cha kuwa na imani kinakupa ujasiri wa kukabiliana na tatizo lako bila woga. Watu wenye imani kubwa mara nyingi huwa ni washindi katika mambo yao.
Hata ukiangalia dini nyingi duniani msingi wake mkubwa umejikita kwenye imani. Watu mbalimbali waliopata matatizo kipindi hicho walitumia imani kama nguzo kuu na kuamini kuwa wanaweza kufanikiwa kutoka katika matatizo waliyonayo na ni kweli waliweza kutoka. Hivyo ili uweze kutoka katika tatizo ulinalo ni muhimu kuwa na imani ya kukusaidia kutoka hapo.

2. Lijue tatizo lako vizuri.
Kuamini tu peke yake hakutoshi, ili kuweza kutoka kwenye tatizo ulinalo ni muhimu pia kulijua tatizo lako vizuri. Kwa nini ninasema ni muhimu kulijua tatizo lako? Unapolijua tatizo lako hiyo inakusaidia kuweza kulikabili vizuri bila woga  na hatimaye kulishinda. Kama tatizo lako hulijui vizuri itakuwa ngumu kulishinda.
Hata unapokwenda kwa daktari kwa ajili ya kutibiwa pamoja na kuwa unajua kuwa unaumwa na umemweleza daktari kuwa pengine kichwa kinauma, lakini daktari huyu atalazimika kukupima kabla ya kukupa dawa. Anachofanya daktari hapa, nikuhakikisha anajua tatizo lako vizuri kabla hajakupa dawa ambazo hazihusiki. Ili utoke kwenye tatizo ulinalo ni muhimu ulijue vizuri ili upate njia sahihi za kulikabili.
3. Acha kuchanganyikiwa na tatizo lako.
Hata kama ikitokea tatizo lako limekuwa kubwa kiasi gani gani kitu cha msingi acha kuchanganyikiwa na tatizo lako. Unaweza ukasema ‘aah hili haliwezekani’, lakini ninachotaka kukwambia inawezekana. Unapokuwa unakuja juu ama unajihisi kuchanganyikiwa mara nyingi kinachokutokea unakuwa hauna uwezo wa kulikabili hilo tatizo na badala yake unalikuza.
Watu wengi huwa wanashindwa kukabili vizuri matatizo yao kutokana na kuhisi kuchanganyikiwa. Linapotokea tatizo kaa chini kwanza tulia kwa muda kisha tambua njia sahihi ya kulikabili. Mara nyingi huwa linaonekana kubwa ni kutokana na jinsi tunavyolipokea. Tuchukulie kweli hata kama ni kubwa hata ukija juu kiasi gani au uhisi kuchanganyikiwa utafanyaje? ndio limeshatokea. Kitu cha msingi tuliza kwanza sana akili yako unapopata tatizo, ili upate njia sahihi za kulitatua.
4. Acha kufikiria sana juu ya tatizo hilo.
Usipoteze muda sana kufikiria juu ya tatizo lako. Si maanishi hapo unakuwa unalipuuza hapana, ila badala ya kulifikiria tatizo hilo sana weka nguvu zako nyingi katika kulitatua tatizo hilo na kulishinda. Kama utaendelea kulifikiria tatizo hilo kwa muda mrefu usishangae kama itatokea hutapata suluhisho la kulitatua.
Weka nguvu nyingi chanya katika kutatua tatizo lako. Ikitokea umeshindwa kwa namna moja au nyingine tafuta msaada wa kukusaidia kutoka kwenye tatizo hilo na acha kung’ang’ania kulifikiria. Inawezekana tatizo linalokusumbua linaweza lisiwe kubwa sana kama unavyolifikiria, zaidi unajiumiza bure kwa kulifikiria sana.
 5. Acha kuzungumzia kushindwa.
Inaweza ikawa inaonekana kweli upo katika hali ngumu ambayo inapelekea kushindwa hiyo ni sawa, lakini acha kuzungumia juu ya kushindwa kwenye tatizo lako. Kwa kadri unavyokuwa unazungumzia kushindwa ndivyo ambavyo unakuwa unakosa ujasiri wa kukabiliana na tatizo ulinalo na mwisho wa siku unajikuta unashindwa kabisa kulitatua.
Kumbuka tatizo lolote ulinalo unaweza kukabiliana nalo. Haijalishi ukubwa uliopo kwenye hilo tatizo, kwa vyovyote vile iwavyo mwisho wake upo. Jipe moyo inawezekana na hakuna marefu yasiyo ya ncha, kama ni hivyo na tatizo lako litaisha hivyohivyo bila wasiwasi.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu sana kwenye mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku na endelea kuwashirikisha wengine kuweza kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,



Aug 21, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuishi Kwa Mafanikio Kazini Kwako.

No comments :
Watu wenye uwezo mkubwa wa kijamii, wanaweza kuishi karibu na kila mtu, na ikiwa unataka kufanikiwa katika fani yako, unatakiwa kuwafanya watu wajisikie vizuri. Jaribu kuchunguza ni kitu gani kinachowaudhi, nini kinawafurahisha na baadae utumie vifaa hivyo wakati unaposhirikana nao kila siku.
Nguzo kuu ya kupendwa ni kuweza kujinasibisha na hali tofauti. Hii haina maana kwamba, unalazimika kuwa mtu ambaye wewe sivyo ulivyo. Kila mmoja wetu ana matatizo yake, anaweza kubadilika na ni mwenye utashi tofauti. Unahitaji kujitambua wewe mwenyewe kiasi cha kutosha na kufahamu ni kwa namna gani tofauti unaweza kujitokeza kwa kundi fulani la watu.
Fani ya saikolojia inayoelekea kwenye suala hili ni Saikolojia ya jamii. Na kwa bahati nzuri tunazo kumbukumbu nyingi sana kutoka kwenye tafiti za kidaktari zinazotueleza namna mawazo, hisia na tabia za watu zinavyotawaliwa na uhalisia, fikara na matarajio ya watu wengine. Tumia utafiti huu kuwa mtu ambaye kila mtu atapenda kufanya nawe kazi.
Lakini waweza kugundua katika nafsi yako  zinazoweza kushirikiana  na kila mtu, ikiwa ni mwangalifu kwa nafsi yako na zile za wengine. Wanasaikolojia ya jamii huwaita watu wanaochunguza hali za kijamii na kujaribu kutafuta vile watakavyoweza kuishi na jamii kulingana na wao walivyo kuwa ni ‘ wafuatiliaji wa juu ya nafsi’.

Wafuatiliaji wa nafsi ni mabingwa wa kutambua kile watu watu walio mbali mbele yao wanachotarajia kwa wakati waliopo. Na watu hawa wana hisia za juu katika ufundi na mbinu za kuvutia, hutazama watu wengine wanavyotumia mbinu fulani, hujizoeza na baadaye kuzitumia wao.
Kwa baadhi ya watu, ujuzi huu wa kufuatilia wengine ndani ya kundi, huja wenyewe, wao ni kama kinyonga wanaoweza kusoma hisia za watu wengine.
Vinyonga hawa hujua nini cha kusema kwa wakubwa wao wa kazi ili kuwafurahisha wakati pengine ng’ombe wa wakubwa hawa nyumbani wanapokufa. Watu wengine ni wafuatiliaji wa nafsi.  Watu hawa hujaribu kubadili ili kuweza kwenda mbele kama wanavyotaka wao.
Watu hawa wanachojua ni hali moja tu ya kujiendesha kama wanaweza kubadilika kwa kufuata hali ilivyo. Hawa ni watu unaoweza kukuta wakifanya mizaha kwenye mkutano muhimu wa kikazi ama kuonekana wasio na mzaha kwenye tafrija ama pikiniki ya kampuni.
Mara nyingi vinyonga huonwa kuwa wapuuzi na hawa wafuatiliaji wa chini wa nafsi, lakini ukweli ni kwamba vinyonga huwa hawapotezi nafasi kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi ns watu wa kila aina.
Ikiwa utaweza kufanya kazi na watu wenye tabia tofauti, si kwamba utapendwa zaidi kwenye nafsi yako ya kazi tu bali utaweza kutimiza malengo yako binafsi.
Watu wanaoweza kujenga urafiki na watu wa aina tofauti kwa wingi, wanakuwa na uwezo kubadilikaa vile wanavyofikiri wao ndivyo walivyo, kwa mujibu wa Profesa Tracy McLaughlin-Volpe, mhadhiri wa Saikolojia kwenye Chuo kikuu cha Vermont.
Tofati na kuwa na marafiki wenye tabia za aina moja, kuwa na marafiki wenye tabia tofauti kunakupa uwezo zaidi za aina moja, kuwa na marafikki wenye tabia tofauti kunakupa uwezo zaidi wa kujijengea picha nzuri zaidi yako, unakuwa una nafsi ya kuweza kubadilika na kuwa tu unayetaka kuwa.
Unahitaji kuwa mtu unayebadilika pale inapobidi, kwa sababu wanasaikolojia wa jamii pia wamegundua kwamba watu hukumbuka kirahisi mabaya kliko mema.
Hivyo, ukimweleza mfanyakazi mwenzako mgeni kwamba mkubwa wenu ni mtanashati , muwazi asiye na mwelekeo, ni wazi mfanyakazi huyo mpya atamchukulia zaidi mkubwa wenu huyo kama mtu asiye na mweleko kabisa,
Kumbukumbu zako mbaya huweza kunasa zaid kwenye akili yako kuliko kumbukumbu nzuri. Ikiwa unataka kupendwa, kubaliana na udhaifu wako na uwa tayari kuubadili. Wale wanaojaribu kwa katia hali zao bora wasikivu, wenye kuweza kujieleza, wanaopenda wengine bila wao wenyewe kujua watafanya mambo mazuri ofisini mwao.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya ujasiriamli na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,




Aug 20, 2015

HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUKABILIANA NA WATU WABAYA KATIKA MAISHA YAKO.

No comments :
Katika maisha yako kwa vyovyote vile huwezi kukosa watu ambao ni lazima wakuone wewe ni mbaya wao, hufai, huna maana wala lolote na pengine wanaokupinga kwa mambo mengi ambayo unayafanya hata kama yana msaada kwao. Unapokutana na watu hawa ambao kwako ni lazima wanakuwa wanakuumiza kwa namna moja au nyingine huwa unajisikiaje?
Inawezekana ukawa unajisikia vibaya sana kiasi cha kutaka kupambana nao, lakini ukija kuangalia hiyo kwako haikusaidii sana. Kitu cha kutambua ni kwamba hawa ndiyo watu wabaya kwako ambao huwezi kuwakwepa, lakini unao. Kama ni hivyo unawezaje kukabiliana na watu hawa ambapo wakati mwingine wanaweza kuwa ni jamaa zako wa karibu?
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukabiliana Na Watu Wabaya Katika Maisha Yako.
1. Weka mikakati ya kuongea nao.
Badala ya kuwapa nafasi ya kukuongelea wewe tu, fanya mpango wa kuweza kuongea nao. Usifanye kosa la kuwakimbia au kuwaongelea na wewe pembeni. Ukifanikiwa kuongea, hiyo itakusaidia kuweza kulewana nao vizuri kwa kujua nini hasa tatizo na kulitafutia majibu yanayotakiwa. Na huo ndiyo unaweza ukawa mwisho wa kukuongelea wewe tena vibaya katika maisha yako.

2. Tafuta marafiki chanya.
Inaweza kabisa kwako ikawa ngumu kuongea nao na kila kitu unaona kama kimeshindikana. Lakini kitu muhimu cha kufanya hapa fanya mpango wa kutafuta marafiki wengine chanya ambao utakuwa nao. Marafiki hawa watakusaidia kuona mambo kwa mtazamo chanya na  kukusahaulisha na wabaya wako ambao pengine wanakuumiza moyo.
3. Tafuta msaada zaidi.
Ni vizuri ukatafuta msaada wa kuweza kukusaidia kupata kile unachohitaji na ukaacha kulaumu kwa nini watu hao wanakusema vibaya. Tafuta ushauri kwa mtu makini ambaye anaweza kukupa ushauri mzuri wa namna gani utakavyokabiliana na wabaya wako. Kwa kubadilishana mawazo na mwingine inaweza kuwa kukupa majibu ya upesi ni nini kifanyike.
4. Acha kusikiliza sana maneno hayo.
Kama unaamini unasemwa kwa tabia ambayo kwako wewe uaona ni sahihi, endelea na tabia yako hiyo bila kusikiliza kitu chochote. Funga masikio na songa mbele kwa kile unachoona ni msaada kwako. Ukisikiliza kila kitu utajikuta ukiumia sana na mwisho hutafanya kitu chochote cha kuweza kukabiliana na tatizo lako la kukabiliana na wabaya wako.
5. Achana nao.
Inaweza ikawa ni uamuzi mgumu kwako, lakini kama mambo yote yameshindikana hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuachana nao. Haina haja ya kushikiria kitu ambacho kinakutesa. Kwa vyovyote vile watu hao hawana msaada kwako ni vyema ukafanya uamuzi mgumu wa kuwatoa kwenye ubongo wako na kuendelea na mambo mengine, vinginevyo utaumiza kichwa kufikiria mambo ambayo huna uwezo nayo.
Zipo namna nyingi ambazo unaweza ukakabiliana na watu wabaya maishani mwako, hizo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kuzitumia kulifanikisha hilo.
Kwa makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza kila siku na kuboresha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,



Aug 19, 2015

Siri 6 Za Mafanikio Ya Mjasiriamali.

No comments :
Ili uweze kufanikiwa ukiwa kama mjasiriamali unahitaji kuzijua siri ama mbinu muhimu za kuweza kukupa mafanikio hayo. Mbinu hizi zitakusaidia kukuongezea maarifa  ambayo yatakupelekea kufanya shughuli zako kwa ufanisi  na kukupa mafanikio unayoyahitaji.
Ni mbinu ambazo ambazo zinatumiwa na wajasirimli wengi wenye mafanikio makubwa duniani kote. Kwa hiyo ni muhimu hata kwako wewe kuweza kuzitimia. Na mbinu au siri hzi zipo za aina mbalimbali ambazo mjasiriamali anatakiwa kuzitumia ili kujipatia uhakika wa mafanikio zaidi.
Zifuatazo Ni Siri 6 Za Mafanikio Ya Mjasiriamali.
1. Kauli nzuri za kumjali mteja.
Moja kati ya sumu kali katika biashara yoyote ile ni kutokumjali mteja. Kwani kwa kauli yako unaweza kumfanya mteja wako akawa ni wa kudumu katika biashara yako au kumfukuza kabisa mteja huyo.
Wengi hufikiri kuwa asipomridhisha mteja mmoja haina tatizo kubwa katika biashara yake. Lakini ukweli ni kwamba mteja huyo mmoja ana nafasi kubwa ya kukutangazia biashara yako, kwa kadri utakavyomhudumia vizuri ndivyo atakavyoshawishi wengine waje kwenye huduma yako.
Acha kutumia kauli za matusi badala yake tumia maneno mazuri, yenye mvuto mbayo yatamfanya mteja wako ashawishike kurudi kwako tena. Kujali mteja siyo lazima uwe mwongeaji sana, bali waweza kutumia maneno machache kama ‘karibu dada, au samahani’ na mengineyo. Hii ndiyo siri mojawapo ya mafanikio kwa mjasiriamali.

2. Uaminifu.
Uaminifu ni moja kati ya nguzo muhimu sana kwa mjasiriamali yoyote Yule. Inabidi mjasiriamali awe mwaminifu kwa wadau wote husika, yaani kwa wateja wake, anakochukulia bidhaa zake, wafanyabiashara wenzake, taasisi za fedha, serikali na washirika wake wote.
Unapokuwa mwaminifu unakuwa unazidi kushirikishwa mambo mengi ya kijasiriamali. Hata mafanikio ya wajasiriamali wengi wenye mafanikio yametokana na uaminfu. Uaminifu ni moja ya kati ya mambo yanayotangaza biashara kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo matunda ya kesho katika ujasiriamali yanatokana na uaminifu unaounyesha kila siku.
3. Kujali muda.
Katika karne hii ya syansi na teknolojia watu wengi huzingatia sana muda ili waweze kukamilisha mipango yao katika muda unaohitajika. Hivyo kitendo cha kumpotezea mtu muda wake unamuuingizia hasara kubwa sana. Pengine hujui muda huo kidogo mtu huyo angeingiza kiasi gani cha pesa.
Kwa hiyo kwa mjasiriamali ni vyema akawa wa kisasa zaidi kwa kuzingatia muda katika shughuli zake za kila siku. Ni muhimu sana kuheshimu ahadi ulizopanga na wateja wako na hata wafanyabiashara wenzako. Muda unachukua nafasi kubwa katika maendeleo binafsi ya mjasiriamali.
4. Utafiti wa bei na masoko.
Moja kati ya mambo yanayoweza kupunguza kasi ya mauzo ya mjasiriamali ni bei ya bidhaa zake kutofautiana kwa kiasi kikubwa na jirani zake. Utakuta bei ni ileile lakini kila mtu amejipangia bei yenye tofauti kubwa na jirani zake. Wengine bila uoga hupanga bei mara mbili au tatu zaidi ya jirani zao.
Wateja wanapoanza kukimbia mtu hufikiri anamkosi, wenzake wanamfitini au amerogwa! Lakini kumbe sivyo. Bei zako mbaya ndizo zinaweza kuwa chanzo cha kukimbiza wateja. Kwa hiyo unapopanga bei ni muhimu kuangalia mambo kama tafiti za jirani zako wanauzaje au uimara wa bidhaa zako.
5. Kubana matumizi.
Ili upate faida nzuri katika biashara yako, suala la kubana matumizi ni muhimu sana. Yako maeneo mengi ambayo mjasiriamali anaweza kubana matumizi bila kuathiri mwenendo wa biashara yake.
Katika kubana matumizi hakikisha unabana matumizi bila kuharibu ubora wa bidhaa ila jalli sana matumizi ambayo siyo ya lazima kwako kuyafanya katika biashara yako. Na pia biashara yako ifanye isije ikabeba matumizi yako mengi binafsi, badala yake jipangie mshahara.
6. Usafi.
Moja kati ya vivutio muhimu kwa wateja ni usafi. Wateja hupendelea kununua bidhaa au kupata huduma katika sehemu na wahudumu walio safi. Hivyo, inatakiwa mjasiriamali azingatie usafi katika maeneo kama eneo la biashara, usafi binafsi na bidhaa ziuzazwo au zizalishwazo.
Lakini kama eneo lako la biashara litakuwa linaendelea kubaki chafu hadi kusubiri eti Bibi afya aje akague, tayari utakuwa umeshapoteza wateja wengi. Tambua kuwa unapoimarisha usafi katika biashara yako ndivyo unavyoongeza idadi ya wateja wako.
Kwa kadri mjasiamali anavyojua siri hizo, ndivyo hujikuta katika nafasi nzuri ya kufanikiwa.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya ujasiriamli na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,




Aug 15, 2015

Njia 6 Muhimu Za Kukusaidia Kuitawala Hofu Inayokukabili Katika Maisha Yako.

No comments :
Habari za leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRAYA MAFANIKIO, ni matarajio yangu ya kuwa umzima na upo tayari  kwa siku nyingine tena kwa ajili ya kujifunza kitu kipya cha kuweza kubadili maisha yako. Katika makala yetu ya leo tutaangalia namna tunavyoweza kuzitawala hofu zetu  zinazotukabili mara kwa mara katika maisha.  
Mara nyingi katika maisha yetu hofu huwa inaonekana ni kama kitu cha kawaida kwa binadamu kwa sababu tu, kila mtu inampata. Wengi wetu bila kujijua huwa tuna hofu za aina mbalimbali ambazo huwa zinatukabili. Hofu hizi huwa zinatofautiana kulingana na mtu mmoja na mwingine. Hofu hizi kwa wengine huwa ni kubwa zaidi na kwa wengine  ni za kawaida tu.
Wapo ambao huwa ni watu wa kuogopa sana juu ya kesho yao wakiwa hawaelewi nini hatima ya maisha yao ya kesho, wapo ambao huhofia sana kazi zao wakiwa hawana uhakika wa ajira zao na wapo pia ambao huhofia juu ya kifo na mengineyo mengi. Ukichunguza utagundua hizi ni baadhi ya hofu chache, kati ya nyingi ambazo wengi huweza kuwa nazo katika maisha yao.
Lakini hata hivyo ikumbukwe pia hofu hizi mara nyingi huwa zinasababishwa ama kuzalishwa na jamii yetu tunamoishi. Kwenye jamii ukiangalia  zipo hofu nyingi ambazo huwa tunapewa kama ‘wewe hufai katika hili,’ huwezi kufanikiwa’ na nyingine chungu nzima na matokeo yake tunajikuta ni watu wa hofu kila kukicha.
Sasa tunawezaje kuzitawala hofu hizi na kuishi maisha ya amani?
1. Kuwa makini na mambo yanayokupa hofu.
Ni muhimu sana kuwa na makini na yale mambo yote yanayokupa hofu sana. Jaribu kufakari na kujiuliza ni kipi kinachokufanya wewe kuwa na hofu zaidi. Na pia jiulize tena ikiwa utaachana na hofu hizo nini ambacho utakipoteza? Kwa kifupi, utagundua hofu nyingi ulizonazo ni wewe mwenyewe umeamua kuzishikiria na zinakutesa bure.

SOMA; Mambo MuhimuYa kukusaidia Kukupa Furaha Katika Maisha Yako.



2. Tambua kila mtu ana hofu zake.
Unaweza ukawa unahofu kwa sababu ya kuogopa kushindwa kitu ulani . Hiyo inaweza ikawa ni sawa lakini kitu cha kutambua kwako ni kuwa kila mtu kwa namna moja ama nyingine huwa anashindwa kwa sehemu yake. Kama ni hivyo ni lazima kwako wewe kuweza kumudu hofu zako na kuacha kuogopa kila kitu bila sababu ya msingi.
3. Jifunze zaidi mambo chanya.
Hii ni njia mojawapo rahisi ya kuweza kukabiliana na hofu kwa urahisi. Unapojifunza vitu chanya utajikuta ule woga uliokuwa nao unapungua siku hadi siku. Unaweza kujifunza kupitia nukuu za mafanikio ama vitabu au blog nzuri zinazohamisisha kama DIRA YA MAFANIKIO na AMKA MTANZANIA. Kwa kufanya hivyo utajikuta hofu ulizonazo unakuwa sasa unauwezo wa kuzitawala. 

SOMA; Mambo 5 Unayoyapoteza Katika Maisha Yako Kwa Sababu Ya Kuwa Na Hofu.

4. Jaribu kufanya mambo mapya.
Inawezekana mfumo wa maisha unaoishi nao wa kufanya mambo yale siku hadi siku ndiyo unaokupa hofu. Jifunze kufanya mambo mengine mapya ambayo yataweza kukuongeza ujasiri na nguvu ya kuweza kuikabili hofu uliyonayo. Kwa kufanya hivyo utajikuta unaitawala hofu yako na kuwa na maisha ya tofauti na ambayo unayo sasa.
5. Sikiliza mziki unaokupa matumaini.
Ni vizuri kusikiliza muziki ambao unakupa matumaini na faraja katika maisha yako ya kesho. Acha kusikiliza mziki tu kwa sababu upo kwenye kifaa cha kusikilizia. Kwa kusikiliza miziki hii itakupa nguvu kubwa ya wewe kuweza kusonga mbele pale unapokuwa na hofu na kumudu kuzitawala hofu hizo kwa sehemu kubwa katika maisha yako.

SOMA; Hivi Ndivyo UnavyowezaKuongeza Thamani Zaidi Katika Maisha Yako.
6. Kuwa mtu wa matumaini.
Ishi maisha kwa kuamini kuwa hofu ulizonazo unaweza kuzishinda. Acha kuwa mwoga sana kupitiliza hiyo kwa vyovyote haitakuweza kukusaidia wewe zaidi ya kukupotezea kwenye njia ya mafanikio. Unapokuwa unaishi kwa matumaini inakuwa ni njia rahisi kwako ya kuweza kutawala hofu zinazokukabili.
Hizo ndizo njia muhimu unazoweza kuzitumia kuweza kuiondoa hofu inayokukabili katika maisha yako. Kwa makala nyingine zaidi endelea kufuatilia DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
dirayamafanikio@gmail.com

Aug 13, 2015

Jifunze Kilimo Bora Cha Vitunguu-2

No comments :
Habari rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO karibu tena katika siku nyingine ambapo tunapata nafasi ya kujifunza juu ya fursa ya uwekezaji katika kilimo cha vitunguu lakini ikiwa ni makala ambayo tuliianza wiki iliyopita.
Katika makala hiyo ya wiki iliyopita tuliweza kuangalia aina za kilimo cha vitunguu, mahitaji muhimu katika kutayarisha shamba, upandaji wa mbegu za vitunguu, matunzo ya vitunguu, namna ya kupata mbegu bora pamoja na aina za vitunguu vinavyolimwa nchini kwa wingi.
Leo katika makala yetu, tutaendelea na kuangalia katika maeneo mengine muhimu yanayohusika katika suala zima la uzalishaji wa vitunguu na kukupa faida inayotakiwa ikiwa wewe ni mkulima uliyepania kufanikiwa. Kwa kuanza makala yetu, tutaanza na kujifunza magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.

SOMA; Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu

Magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.
Wadudu waharibifu.
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao hili:
1.Viroboto wa vitunguu.
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.

Dalili za kugundua.
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.
Kuzuia.
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35, Parathion nk. Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako    liwe limekomaa.
Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi. Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.
2. Chawa wekundu. (Thrips)
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu(Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu.
Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
·                     Kuweka shamba katika hali ya usafi
·                     Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
·                     Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
3. Sota (cutworms)  
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya usafi.

SOMA; Kilimo Bora Cha Pilipili Hoho Na Faida Zake.

4. Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:-
·                     Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
·                     Kuteketeza masalia ya mazao
·                     Kutumia mzunguko wa mazao
5. Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
·        Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
·        Kuteketeza masalia ya mazao
·        Kutumia mzunguko wa mazao
Magugu.
Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
(Goal 2E).
Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au kubabua vitunguu.
Magonjwa ya vitunguu.
a)     Ukungu mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua Ugonjwa huu
·        Utaona unga wa rangi ya zambarau katika majani.
·        Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kunyauka.
·        Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia
·        Inashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa mwingi.

·        Tumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.
Dalili zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.

SOMA; Badili Maisha Yako Kwa Kuwekeza Kwenye Kilimo Hiki Cha Vitunguu Saumu.

Namna ya kuzuia
Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.
·        Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.
·        Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.
·        Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa kuchimba na jembe.
·        Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.
Kuzuia
·        Tumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi mwingine.
·        Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole.
Kumbuka tumejifunza kuanzia utayarishaji wa shamba na aina za mashamba, pili tukaangalia aina za mbegu na jinsi ya kuchagua mbegu bora yenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa, pia tukalenga kwenye maeneo na hali ya hewa, tukaangaza na katika Magonjwa yanayoweza kuathiri zao la kitunguu pamoja na kudhibiti wake.
Tunakutakia kila la kheri katika kilimo bora na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
Makala hii imeandikwa na  mtaalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com