google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Feb 27, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Muda Wako Vizuri Na Kukuletea Mafanikio Makubwa.

No comments :
Muda ni mali! Huu ni usemi maarufu sana kwa vijana na wazee. Unaonekana ni usemi wa kawaida na uliozoeleka kwa watu wengi, maskini na matajiri, wanawake na wanaume. Japokuwa watu wengi tunautumia usemi huu, lakini baadhi yetu hatuelewi maana yake na wengi wetu hatuutumii katika maisha yetu.

Muda ni mali maana yake kila kitu, vitu vyote vinavyoonekana vidogo na vikubwa ni matokeo ya matumizi ya muda. Hata mimi na wewe ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kila mafanikio yaliyowahi kutokea na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na matumizi ya muda,yaani muda ukitumika vizuri mafanikio yanapatikana na muda huo huo usipotumika vizuri hakuna mafanikio.

Hakuna haja ya kueleza na kufafanua maana ya muda, ila nataka ujue kuwa kuna aina za muda, ndiyo zipo aina mbili za muda. Aina ya kwanza ya muda ni MUDA WA SAA. Muda huu unaanzia sekunde hadi mwaka. Katika muda wa saa, tunaposema miaka miwili ni miaka miwili, haizidi wala haipungui.Tunaposema huyu ana miaka hamsini ina maana mtu ameishi vipindi hamsini ambapo kila kipindi kina jumla ya miezi kumi na mbili, haizidi wala haipungui.

Aina ya aili ya muda ni MUDA HALISI. Muda halisi unaundwa na muda wa saa na matukio. Katika aina hii ya muda tunaangalia matukio yaliyotokea katika muda wa saa husika.Tunalinganisha idadi ya miaka na miezi na matukio au mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika. Watu wanaweza kuwa sawa katika muda wa saa lakini wakawa tofauti katika muda halisi. Mtu anaweza kuwa na umri wa miaka sitini(katika muda wa saa) lakini akawa kwa mafanikio ni kama mtu aliyeishi miaka thelathini tu.

Na pia mtu mwingine anaweza kuwa na umri wa miaka thelathini, lakini akawa na mafanikio makubwa sana kimaisha kama mtu aliyeishi miaka mingi sana duniani, yawezekana hata miaka sabini. Usichanganyikiwe, nalinganisha muda wa saa na mafanikio. Muda halisi unatuambia kwamba kuna kuchelewa katika maisha. Muda halisi unatukumbusha kuwa kuna wakati tunaweza kupoteza miaka yetu bila kujua. Unatukumbusha kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi. 

Tumejifunza aina za muda na tofauti zake, sasa tuangalie  matumizi ya muda wa saa.Tunatumia  muda huu kufanya mambo matatu ambayo yanatuleta kwenye muda halisi, tukiwa tumewahi au tumechelewa  tunatumia muda katika kufikiri, kusema au kuzungumza na kufanya mambo mbalimbali katika maisha yetu.

Baada ya kuangalia matumizi ya muda wa saa, tumegundua kuwa tunautumia muda kama chombo kutusafirisha kutoka katika ulimwengu wa namba na mahesabu kwenda kwenye ulimwengu wa halisi,ulimwengu wa vitendo ambapo tunaweza kufanya tathmini na kuona kuwa tumewahi au tumechelewa, tuko nyuma au  tuko  mahali sahihi.

Sasa tuangalie mambo ya kufanya ili tuweze kuutumia muda wa saa na kufikia mafanikio ambayo yataweka uwiano sawa kati ya muda wa saa na muda halisi katika maisha yetu.Yapo mambo mengi ambayo unapaswa kuyafanya ili uweze kutumia muda wako vizuri, baadhi ya  mambo hayo ni haya yafuatayo:-

1. Weka kumbukumbu ya mambo unayofikiria, unayoyasema na kutenda.
Kumbukumbu ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kwa sababu ndizo zinazotusaidia kufanya tathmini. Jitahidi kuweka kumbukumbu za mambo unayofikiri, unayosema na kutenda japo kwa siku moja. Mwisho wa siku jitahidi kukukumbuka mambo uliyofikiria, uliyosema na kutenda yawe mazuri au Mabaya. Hii itakusaidia kufanya tathmini ya matumizi ya muda kwa siku hiyo.

Tathmini hiyo itakusaidia pia kujua umetumia muda vizuri au vibaya. Mara nyingi sana siyo rahisi kukukumbuka mambo yote uliyofikiria na kusema lakini ni rahisi kukukumbuka matukio na mara nyingi matukio hutokana na kufikiri na kusema,kwa hiyo kukumbuka matukio ni njia rahisi zaidi yakukuwezesha kufanya tathmini ya siku nzima.


2. Weka ratiba ya siku nzima.
Ratiba ni muhimu sana katika maisha ya kila siku.Usianze siku bila kujua utafanya nini siku hiyo. Unaweza kuweka na kupanga ratiba ya siku inayofuata kabla ya kulala au asubuhi kabla hujaanza jambo lolote. Watu wote waliofanikiwa, wamefanikiwa kwa sababu ya matumizi mazuri ya muda, wanafanya kazi zao kwa ratiba na wana nidhamu linapokuja swala la matumizi ya muda. Bila kuwa na ratiba muda hutumika bila mpangilio na wakati mwingine muda hupotea bure. Unapoweka ratiba hakikisha kila kitu ulichokiweka kina wakati na muda wake.  Kinaanza saa ngapi na kuisha saa ngapi. Ni vyema ratiba hii iwe na mambo ya msingi tu. Usisahau mapumziko. Mapumziko ni muhimu kwa utendajibora wa akili na mwili.

3. Epuka kuwa na mipango mingi.
Katika ratiba yako usiweke mambo mengi sana ambayo utekelezaji wake ni mgumu au yanachosha.Weka mambo machache  ambayo yanakupa nafasi ya kupumzika na kutafakari namna ya kuianza siku inayofuata. Ukiweka mambo mengi kuna hatari ya kuyatekeleza nusunusu na mengine yanaweza yasitekelezwe kabisa.

4. Usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia ratiba yako.
Mara unapoanza kutekeleza mipango ambayo iko kwenye ratiba yako, usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia na kuvuruga ratiba yako. Kuwa na nidhamu na heshimu ratiba yako. Zipo dharura lakini si dharura zote  zinahitaji kushughulikiwa papo .Kama dharura ni ya msingi na inahitaji kushughulikiwa papo hapo hamna tatizo.Jifunze kutambua na kutofautisha dharura zinazohitaji kushughulikiwa papo hapo na zile zinazoweza kushughulikiwa baada ya ratiba kukamilika.

Kuna watu ambao wako tayari kuvuruga ratiba zao na kuacha shughuli zao kwa sababu ya mambo yasiyo ya msingi kwa mfano kuangalia mechi na burudani zingine ambazo haziwasaidii katika maisha yao. Narudia tena,uwe na nidhamu heshimu ratiba yako.

5. Epuka kutumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo ya lazima na yasiyo na faida.
Epuka kutumia muda mrefu kufanya mambo yasiyo ya msingi na yasiyo na faida kwa mfano kuchati kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia mechi na burudani zingine wakati ambapo unatakiwa kufanya mambo ya msingi kwa ajili yako na jamii inayokuzunguka. Sina maana mitandao ya kijamii mibaya ila nasisitiza kuwa na kiasi na kuipa nafasi ndogo katika maisha ya kila siku. Kama utakuwa unawasiliana kwenye mtandao wa kijamii basi iwe kwa faida na si kupoteza muda.

Ninasema hivi kwa sababu hili limekuwa tatizo Kubwa  sana kwa kizazi cha sasa hasa vijana, tena wanafunzi ambao wanatakiwa wasome kwa bidii wasipoteze muda hata kidogo. Muda wa kufanya mambo ya msingi utumike kufanya mambo ya msingi na mambo mengine yapewe nafasi ya pili au ya mwisho.

5. Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo ya msingi.
Unashauriwa kutumia 75% hadi 80% ya muda wako kufanya mambo yenye tija kwako na kwa wanaokutegemea.Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo yatakayokujenga na kukuimarisha kiakili,kijamii na kiuchumi. Fanya kazi za kukuingizia kipato, soma vitabu, magazeti, na majarida yatakayokuongezea  maarifa na kupanua ufahamu wako.Ukiingia kwenye Internet soma vitu vinavyokujenga na siyo kufuatilia habari za watu maarufu huku hakuna cha maana unachopata.

Wengine wanaingia kwenye Internet  kuangalia ili kuangalia picha za ngono na utupu. Watanzania wengi watu wazima ukiwauliza walisoma vitabu lini, hawakumbuki, wengine wanakwambia shule ya msingi na wengine sekondari, inasikitisha. Wengine hata wanaponunua simu, hawasomi vile vitabu vinavyoelekeza namna ya kutumia hiyo simu. Watu walio wengi sana kama ni kusoma wanapenda kusoma vitu ambavyo haviwasaidii sana katika maisha yao kama magazeti ya udaku.

Nakutakia kila la kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

  • Makala hii imeandikwa na Deogratius Harold wa Mbeya- Tanzania.
  • Mawasiliano 0718 610 022







Feb 24, 2015

FEDHA: Sababu 7 Zinazokufanya Ushindwe Kuwa Na Pesa Zakutosha Katika Maisha Yako.

No comments :
Katika maisha kuna wakati unaweza ukawa unajiuliza na pengine kushangaa kwanini umekuwa ni mtu ambaye huna pesa za kutosha wakati ukija kuchunguza maisha ya wanaokuzunguka ni watu wenye pesa na maisha yao wanayaendesha vizuri tu. Inawezekana ukawa unafanya kazi ama biashara nzuri inayokuingizia kipato cha kutosha lakini kutokana na sababu usizozijua huwa ukijikuta ni mtu wa kuishiwa na kujikuta kuwa huna pesa. Kama umekuwa ukiishi hivi na kuwa mtu wa kuishiwa na kushindwa kuwa na pesa za kutosha , makala hii ni muhimu sana kwako. Je, unajua ni sababu zipi zinakufanya ushindwe kuwa na pesa ya kutosha katika maisha yako?

Hizi Ndizo Sababu 7 Zinazokufanya Ushindwe Kuwa Na Pesa Pesa Zakutosha Katika Maisha Yako.

1. Una tabia mbaya zinazokuzuia kupata pesa.
Kuwa na tabia mbaya zinazokuzuia kupata pesa, ni sababu mojawapo ambayo inasababisha wewe ushindwe kuwa na pesa za kutosha kukosha. Kama maisha yako yametawaliwa na tabia mbaya kama matumizi mabaya ya pesa, ulevi na kuangalia TV kwa muda mrefu, hali ambayo inakupelekea wewe kupoteza muda mwingi sana ambao ungekusaidia katika suala zima la uzalishaji, sahau kuwa na pesa. Hii inatokea ni kwa sababu tabia zako hizo zinakuwa hazikusaidii kukuzalishia zaidi ya kukufanya uzidi kuishiwa na kujikuta kukosa pesa katika maisha yako, mara kwa mara.


2. Unazungukwa na watu wengi ambao sio sahihi kwako.
Ili tuweze kufanikiwa na kuwa na mafanikio makubwa zaidi, tunahitaji kuwa na watu sahihi na waliofanikiwa zaidi yetu ili kuweza kutupa hamasa ya mafanikio. Katika maisha yako unapokuwa umezungukwa na watu wengi ambao ni hasi, hawaamini katika utajiri na mafanikio, ni lazima wewe utaanza kuwa kama wao kidogo kidogo na mwisho wa siku utajikuta umekuwa mtu ambaye na wewe unashindwa kuwa na pesa za kutosha kama wao. Kuzungukwa na watu wengi ambao sio sahihi kwako hii ni sababu mojawapo inayokusababisha wewe ushindwe kumudu kupata pesa.

3. Umekuwa mwongeaji sana bila kuchukua hatua.
Unapokuwa mwongeaji sana juu ya ndoto zako bila kuchukua hatua yoyote uwe na uhakika ni lazima mifuko yako iwe tupu, haina kitu. Watu wengi huwa ni waongeleaji wazuri sana wa ndoto na malengo waliyonayo, lakini linapokuja suala la vitendo inakuwa hakuna. Kama unatabia hii uwe na uhakika lazima pesa zitakupiga chenga, kwa sababu ndoto bila vitendo ni kazi bure. Wapo watu wengi sana hapa duniani ambao walikufa na kuzikwa na ndoto zao nzuri walizokuwa nazo bila kuzifanyia kazi. Jifunze kufanyia kazi ndoto zako, ili ubadili maisha yako.

4. Umekuwa hauna mipango maalumu.
Ni kitu ambacho unatakiwa ujiulize mara kwa mara katika maisha yako kuwa unataka kuwaje baada ya miaka michache kuanzia sasa? Unataka kuwa kama ulivyo sasa kwa kutegemea kazi ya aina moja? Ama una mipango gani mathubuti uliyojiwekea, ambayo itakusaidia uweze kuweza kuongeza kipato chako? Tatizo la watu wengi ambalo huwa lina sababisha moja kwa moja kuwa watu wa kushindwa kushindwa kupata pesa za kutosha katika maisha yao, linatokana na kuwa watu wakukosa mipango maalum itakayowaongoza kwenye uhuru wa kifedha.

5. Umekuwa ukikata tamaa mapema.
Kuwa na tabia ya kukata tamaa mapema kwa kile unachofanya, hiki ni kitu kingine ambacho kimekuwa kikikufanya uendelee kushindwa sana kupata pesa za kutosha katika maisha yako. Umekuwa ukikosa pesa kwa sababu, unakuwa unaachia fursa nyingi  ambazo zingeweza kukusaidia kukupatia kipato cha kutosha. Kwa sababu ya kukata tamaa mapema unajikuta ukiwa ni mtu ambaye unapoteza pesa nyingi, ambazo zingeweza kukusaidia katika maisha yako.

6. Umekuwa ni mtu wa kupoteza muda sana.
Kama unaishi na unaendelea kuishi maisha ya kupoteza muda katika maisha yako huwezi kufanikiwa kwa chochote, zaidi utaendelea kuwa maskini. Watu wengi bila kujijua huwa ni watu wa kupoteza muda sana katika mambo yasiyo ya msingi kama mitandao ya kijamii, TV na mengineyo. Kwa kupoteza muda huko hushindwa kupangilia mambo ya msingi ambayo yangeweza kuwasaidia kuingiza kipato na matokea yake husababisha kuwa ni watu wa kushindwa kupata pesa. Kama unaishi maisha haya ya kutumia muda hovyo, usilaumu kama utakuwa ni mtu wa kushindwa kupata pesa za kutosha katika maisha yako.  

7. Umekuwa huna tabia ya kujiwekea akiba.
Hili ni kosa ambalo umekuwa ukilifanya mara kwa mara, umekuwa ukitumia kiasi chote cha pesa na kujikuta huna akiba hata kidogo. Kama maisha yako yako hivi, suala la kushindwa kupata pesa nyingi kwako halitakiwa jambo la kushangaza. Unaposhindwa kuweka akiba hata kiasi kidogo basi maisha yako utazidi kuyafanya kuwa magumu siku hadi siku.

Unao uwezo wa kuishi maisha yoyote ya kimafanikio kama utaamua kuwa hivyo kweli katika maisha yako. Kuwa na fikra sahihi zitakazo kuongoza kwenye uhuru wa kifedha. Kwa kifupi, hizo ndizo sababu zinazokufanya ushindwe kuwa na pesa ya kutosha katika maisha yako.

Nakutakia kila kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku, kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
  
IMANI NGWANGWALU,




Feb 20, 2015

Haya Ndiyo Maradhi Ya Utajiri Wa Ghafla. Soma Hapa Kujua Zaidi.

No comments :
Siku hizi mazungumzo yanayohusu pesa, mali na utajiri kwa ujumla, yamekuwa ni jambo la msingi linalopewa kipaumbele na kila mtu katika jamii yetu. Ingawa, tamaa ya kutaka kujitajirisha kwa vyovyote vile, imejengeka na kujizatiti ndani ya mioyo ya watu kiasi cha kutufanya kuwa kama watumwa vile. Mwelekeo huu wa kupenda na kutamani sana utajiri, umewafanya baadhi ya watu wavuke mipaka ya maadili mema na kuutafuta utajiri huo kwa njia za mkato, zisizo halali.

Nakumbuka kuna jamaa yangu mmoja kipindi cha nyuma kidogo, baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya biashara katika chuo kimojawapo hapa nchini, aliweza kubahatika kuajiriwa na serikali katika idara moja iliyokuwa ikijihusisha na maduhuri ya serikali kutoka kwa wafanyabishara wadogo na hata kwa wale wakubwa. Katika muda wa miaka tu tokea aajiriwe, jamaa huyu aliweza kujitajirisha  kwa kiwango kikubwa na cha kutisha sana.

Njia alizotumia katika kujitajirisha kwake bado inabaki kuwa siri yake. Lakini kwawatu wenye kujua kiwango chake cha mshahara na muda aliofanya kazi, hawakusita kusema kwamba, utajiri huo ulipatikana kwa njia za mkato mkato, ikiwa ni pamoja na kuibia serikali. Mara baada ya kuona kwamba ametajirika kiasi cha kuogofya, akawa sasa hata mwenyewe anaonekana kutokuamini, kutokana na wingi wa pesa alizokuwa nazo. Hivyo kutokana na hali hiyo, alianza kushitakiwa na dhamira yake.

Matokeo yake ni kwamba , alianza kuingiwa na hofu ya kuja kukamatwa na mwajiri wake. Hali hiyo iliendelea kumsumbua kwa muda mrefu. Katika hali kama hii aliendelea kusumbuliwa na maumivu makubwa ya kiakili na kihisia. Hivyo, ikawa kwamba, katika harakati za jamaa huyu kuondokana na maumivu hayo, aliamua kutafuta mwavuli wa kumpa nafuu. Ilibidi aanze ufujaji wa pesa hizo kwa kulewa kupita kiasi na ngono za hovyo.

  
Ilifika hatua ambapo jamaa huyu akawa anashindana na mkewe katika kuzichota fedha hizo kutoka sehemu walikokuwa wakizihifadhi ndani ya nyumba yao. Migogoro ya ugomvi kwenye ndoa yake likawa ni jambo la kawaida. Vilevile jamaa huyu akawa anawaalika jamaa zake aliomaliza nao masomo ya chuo kikuu, wakanywa na kufurahia maisha.

Alifanya hivyo, bila yeye mwenyewe kujua kwamba, ilikuwa ni jitihada yake ya kutibu majeraha ya hisia zake, kutokana na kushtakiwa na dhamira zake, kwa vitendo  vyake vya ubadhirifu, rushwa na wizi wa fedhaza ofisi yake. Hata hivyo, tiba hiyo haikufua dafu kwani hatimaye jamaa huyu aliamua kuacha kazi yeye mwenyewe kwa hofu ya kudakwa na mwajiri wake.

Wataalamu wengi wa afya ya akili wanadai kwamba mtu anapopata utajiri wa ghafla huwa ni ngumu sana kwake kuweza kukabiliana nao huo utajiri wa ghafla. Wataalamu huweza kuongeza kuwa utajiri huo huweza kusababisha familia kuvunjika na kuharibu kabisa maisha yao. Na kwamba fedha hizo, zinakuwa haziwaletei tena amani, uraha na hata kuridhika kama walivyokuwa wakifikiri mwanzo.

Vilevile kulingana na maoni ya wataalamu mbalimbali wa masuala yahusuyo afya ya akili, wanaendelea kudai kuwa watu wengi ambao hupata utajiri huu wa ghafla na wa kupindukia mara nyingi huwa ni watu wa kuugua maradhi ambayo yamepewa jina la maradhi ya utajiri wa ghafla, ambayo huwa yana dalili kama hizi:-

Kushtuka moyo sana, hofu za ghafla na ya mara kwa mara, kukosa usingizi, kukosa amani na kuhisi kuwa na hatia kwa sababu ya kuwa na pesa nyingi kupindukia ambazo tena ukiangalia sio za halali. Pia, kuhisi kwamba hawastahili kuwa na pesa au utajiri mkubwa wa kiasi hicho. Watu wengi wenye utajiri mkubwa na wa ghafla ndivyo walivyo na wanaishi na maradhi ya utajiri wa ghafla, ingawa sio rahisi sana kubaini na hawawezi pia kukwambia.

Hivyo, ni vizuri tukawa na mtazamo chanya na unaofaa kuelekea kwenye utajiri tunaoutaka  na kuumiliki baada ya kufanya kazi halali tena pengine muda mrefu, ni sehemu tu ya jitihada za kujipatia mafanikio ya kweli. Kwani mafanikio haya yanatutaka tuutumie utajiri huo vizuri. Kutumia utajiri huo vizuri ni pamoja na kuutumia katika kuwatendea mema watu wengine, kuutumia katika kazi na miradi mbalimbali ya kijamii.

Kwa kufanya hivyo, ni wazi kabisa tutakuwa tumeigundua na kuipata siri au tiba itakayoweza kutusaidia katika kuepukana na mashtaka hata hukumu itokanayo na utajiri wa haraka haraka.

Nakutakia kila la kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kupata maarifa bora yatakayobadili maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,





Feb 19, 2015

Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.

No comments :
Habari ya leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nimatumaini yangu ya kuwa umzima wa afya na unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako ya kila siku. Ninakukaribisha sana katika siku nyingine tena, ambapo tunakutana kujadili maisha, lengo likiwa ni kuhakikisha tunapata maarifa bora yatakayoweza kutusaidia kuweza kuboresha maisha yetu na kuwa ya kiwango cha juu kabisa cha mafanikio kama tunavyotaka iwe.

Katika makala yetu ya leo tutaangalia hasa juu ya malengo na jinsi ambavyo tunaweza kufikia malengo tuliyojiwekea bila kizuiliwa na kitu chochote. Mara nyingi wengi wetu kuna wakati huwa ni watu wa kujiuliza, nitawezaje kufikia lengo hili ama lile katika maisha yangu. Ni maswali ambayo huwa yanakuja pengine kutokana  na mtu huyo kugundua kuwa kuna uwezekano wa yeye kutotimiza malengo yake kwa sababu anazozijua yeye, ikiwa ni pamoja na wasiwasi ama kushindwa kujiamini.

Wengine kutokana na wasiwasi ama kushindwa kujiamini kama nilivyosema, hujikuta ni watu wa kuamini kuwa labda wanaotimiza malengo ya aina fulani ni watu wenye vipaji, wamejaaliwa na pia ni watu wenye bahati sana katika maisha yao, kitu ambacho sio kweli hata kidogo. Kiukweli, unaouwezo mkubwa wa kutimiza malengo yoyote unayojiwekea katika maisha yako, kama utaamua iwe hivyo kwako. Hakuna kitu ama mtu mwenye uwezo wa kukuzuia wala huhitaji nguvu za ziada kufanikisha hilo.


Unaweza ukawa unaanza kujiuliza nifanye nini au ni kipi cha kufanya ili niweze kutimiza malengo yangu muhimu niliyojiwekea? Ni vizuri kujiuliza hivyo maana hiyo nayo ni hatua ya kuonyesha kuwa una nia na mafanikio unayoyataka na wala hutanii. Kipo kitu muhimu ambacho wewe unatakiwa ufanye ili kutimiza malengo yako, kitu hiki nikufatilia na kufanyia kazi hatua hizi tano za kufikia malengo yako na si vinginevyo.   Ukifanya hivyo uwe na uhakika utafikia malengo yako bila wasiwasi. Unajua hatua hizo ni zipi?

Hizi Ndizo Hatua Tano Muhimu Za Kufikia Malengo Uliyojiwekea.

1. Ni lazima uwe na hamasa ya kutaka kufanikiwa.
Hautaweza kufanikiwa kama huna njaa na kiu kubwa ya mafanikio ndani mwako. Ili uweze kufanikiwa hasa kwa malengo uliyojiwekea ni lazima uwe na hasira kubwa ya mafanikio. Ukiwa na hasira hii, itakusaidia wewe kupita eneo lolote, hata katikati vizuizi ama vikwazo ambavyo huwa tunakutana navyo katika safari ya mafanikio. Watu wengi wenye mafanikio makubwa duniani ni watu ambao walikuwa na hasira na malengo yao waliyojiwekea.



2. Anza kuchukua hatua mapema.
Kuongea sana juu ya mipango na malengo mazuri uliyonayo hakutakusaidia kitu, zaidi ya kuchukua hatua muhimu za kuelekea kwenye utekelezaji. Anza kuchukua hatua mapema za kutekeleza ndoto zako hata kwa kidogo kidogo ipo siku utafika. Ni bora ukafanya kwa kidogo hiyo itakusaidia sana tofauti na ambavyo ungekaa na kusubiri, hiyo ingekuwa inakupotezea muda sana katika maisha yako.

3. Unahitaji kujifunza zaidi.
Hii ni hatua muhimu pia ya kufikia malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Ni muhimu kujifunza na ukapata maarifa yanayoendana na malengo unayoyahitaji katika maisha yako. Hiyo itakusaidia kujua vitu vya msingi vinavyoendana na malengo uliyojiwekea. Kwa mfano, kama malengo yako ni kuwa millionea baada ya miaka 20 kuanzia sasa ni lazima uanze kujifunza kuishi maisha wanayoishi mamilionea kwa kujisomea kila siku.

4. Unahitaji kuwa na mitazamo chanya.
Mara nyingi kuna wakati huwa tunashindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea kutokana na mitazamo tuliyonayo juu ya malengo yetu. Kama unajiona huwezi kufikia malengo yako, huo ndio ukweli hutaweza kuyafikia. Jenga mitazamo chanya ambayo itakusaidia kufikia malengo muhimu uliyojiwekea. Achana na fikra ama imani za kuwa huwezi kufanikiwa kwa sababu hii na hii, jiwekee mitazamo chanya na utaweza kufikia malengo yako.

5. Jifunze kutokana na makosa.
Kuna wakati huwa tunafikia mafanikio kwa yale tunayoyahitaji baada ya kukosea sana hiki na kile. Hautaweza kufikia mafanikio au malengo yako kwa urahisi kama unavyofikiri, kuna wakati ni lazima ukosee. Unapokosea huo ndio huwa wakati muhimu kwako wa kujifunza kutokana na makosa uliyoyafanya.  Acha kusononeka wala kulia kama kuna sehemu umekosea, hiyo hatakusadia kitu. Badala yake, chukua hatua muhimu ya kunyanyuka pale ulipoanguka, jifunze na kisha songa mbele.

Mwisho, unaposhindwa kufikia malengo yako kwa namna yoyote ile acha kulaumu vitu ambavyo viko nje ya wewe kuwa ndiyo vimesababisha ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea. Mara nyingi sisi wenyewe huwa ndio huwa vizuizi wa malengo yetu. Jifunze hatua hizo tano muhimu zikusaidie kufikia malengo muhimu uliyojiwekea katika maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio. Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri yanayoendelea humu.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

  IMANI NGWANGWALU,




Feb 18, 2015

Mambo 5 Yanakuzuia Wewe Kuwa Tajiri.

No comments :
Watu wengi huwa ni watu wakijirudisha nyuma  katika maisha yao pasipo kujua hasa kutokana na vitendo, mienendo, hulka na hata tabia walizonazo kwa ujumla. Hayo ni mambo machache kati ya mengi ambayo yamekuwa yakisimamisha ndoto za watu wengi katika safari nzima ya kuelekea kwenye utajiri. Kiuhalisia, ili uweze kufikia ngazi kubwa ya mafanikio na hatimaye kuwa tajiri unahitaji kujifunza vitu vingi sana vitakavyoweza kukusaidia kusonga mbele, ikiwa na pamoja nakujua vitu vinavyokuzuia wewe kuwa tajiri. Leo katika makala hii tutazungumzia mambo yanayokuzuia wewe kuwa tajiri katika maisha yako.

Yafuatayo Ni Mambo 5 Yanakuzuia Wewe Kuwa Tajiri.

1. Umekuwa ukiathiriwa sana na mazingira uliyopo.
Hii ndiyo sababu kubwa mojawapo inayokufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa tajiri. Hili limekuwa likitokea kwako pasipo kujua na pengine umekuwa ukiona kama jambo la kawaida tu kwako, bila kugundua kitu. Inawezekana ukawa umekulia katika jamii maskini ambapo muda mwingi tokea unasoma shule na mpaka sasa uko mtaani umekuwa ukiona watu wengi wanaokuzunguka ni maskini. Picha utakayokuwa inakujia kichwani kwako ni kuwa haiwezekani kuwa tajiri. Unaamini hivyo ni kwa sababu ya mazingira yanayokuzunguka unaona wengi ni maskini na ni kitu ambacho kimekuwa kikikuathiri na kukuzuia wewe kuwa tajiri.


2. Hujaamua kuwa tajiri katika maisha yako.
Maamuzi ni kitu cha muhimu sana katika maisha yako. Hata kama utakuwa unasoma vitabu vya mafanikio kwa wingi, kuhudhuria warsha na semina mbalimbali za mafanikio, kama hujafanya maamuzi mazito ya kutaka kuwa tajiri katika maisha yako, huwezi kuwa tajiri. Mafanikio makubwa ya maisha yako yanategemea sana na maamuzi unayoyafanya leo kila siku. Ukiamua kuwa tajiri kisha ukajitoa kulipia gharama za kuwa tajiri, hilo linawezekana. Maamuzi utakayochukua yana nguvu ya kukutoa kwenye umaskini na kukufanya kuwa tajiri. Mpaka sasa hujawa tajiri moja ya kitu kinachokuzuia ni maamuzi yako mwenyewe.

 3. Umekuwa mtu wa kuahirisha sana mambo yako.
Unashindwa kufikia ndoto zao kubwa kwa sababu ya tabia yako hii ya kuahirisha mipango yako mara kwa mara, hali ambayo imekuwa ikisababisha uzidi kukosa fursa nyingi kila kukicha. Kama kuna jambo umeamua kulifanya na kulitekeleza ni vizuri ukalifanya leo ili uweze kufikia mafanikio yako unayoyataka. Kama ni kesho ambayo unasema kila siku utafanya hutaweza kuja kuipata mpaka unazeeka. Jifunze kufanya mambo yako leo leo na achana na kesho utapoteza muda wako bure kuisubiri na kesho haitafika.

4. Umekuwa ukitumia pesa zako vibaya.
Hili ndilo kosa kubwa ambalo umekuwa ukilifanya na limekuwa likikugharimu na kukuzuia kuwa tajiri. Mara nyingi umekuwa ukitumia nguvu nyingi kutafuta pesa zako, lakini unapozipata umekuwa ukizitumia hovyo sana hali inayosababisha ushindwe kuweka hata fedha kidogo kwa ajili ya akiba yako. Na umekuwa ukifanya hivi kwa sababu ya kukosa nidhamu binafsi juu ya pesa zako na umejikuta umekuwa mtumwa wa pesa. Kama unaendelea na maisha haya ya kutumia pesa zako bila ya utaratibu maalumu, tambua kabisa utabaki kuwa maskini siku zote na hili halina ubishi.

5. Umekuwa ni mtu wa kupoteza muda sana.
Ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema mara kwa mara kuwa, kama unaishi na unaendelea kuishi maisha ya kupoteza muda, elewa huna kabisa maisha ama kwa maneno rahisi huwezi kufanikiwa tena katika maisha yako. Muda ni kila kitu katika maisha yako unapocheza na muda, inakuwa ni sawa na kuchezea maisha yako mwenyewe. Ubaya wa muda ukiupoteza ndio haurudi tena hata ufanye nini. Jifunze kutumia muda wako vizuri, ili ukuzalishie na  ukuletee mafanikio makubwa.

Hayo ndiyo mambo yanayokuzuia wewe kuwa tajiri katika maisha yako, nakutakia kila kheri katika safari yako ya mafanikio. Nakusihi endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku. Usisite pia kuwashirikisha wengine ili tujifunze wote kwa pamoja mambo mazuri yatakayoboresha maisha yetu.

IMANI NGWANGWALU,








Feb 17, 2015

Mambo 6 Unayotakiwa Kujua, Ili Kuboresha Biashara Yako.

4 comments :
Kuwa na kiu ama shauku ya kufikia ngazi kubwa ya kimafanikio kibiashara, ni hitaji ambalo kila mjasiriamali na mfanyabiashara wa kweli  huwa nalo ndani ya moyo wake. Pamoja na kiu hii ya kutaka kufikia mafanikio hayo makubwa kibiashara, wajasiriamali  wengi hujikuta wakikwama na kushindwa  kutimiza malengo yao. Kwa kawaida, huwa yapo mambo mengi yanayochangia kutokea kwa hali hii, ikiwemo na kufanya biashara kwa mazoea na matokeo yake kushindwa kuboresha biashara.

Unaposhindwa kuboresha biashara yako, sio tu kwamba itapelekea wewe kukosa wateja, bali pia itakusababishia kushindwa kufikia mafanikio makubwa uliyojiwekea katika maisha yako. Kwa kujua hilo, ni muhimu sana kwako kuiangalia na kuichunguza biashara yako mara kwa mara na kufanya marekebisho muhimu na ya lazima, ili kupata matokeo chanya unayoyahitaji na si vinginevyo. Lakini, hautaweza kufanya chochote au marekebisho yoyote kama hujui mambo haya.

Haya Mambo 6 Unayotakiwa Kujua, Ili Kuboresha Biashara Yako.

1. Kubali Kuwa Kuna ushindani.
Ni muhimu kujua hili mapema kuwa biashara unayoifanya hauko peke yako, wapo watu pia wanaofanya biashara kama ya kwako. Kwa kujua hilo hutakiwi kubweteka, kujiachia ama kulala na kusubiri wateja waje, utakuwa unapoteza muda na hutapata mafanikio makubwa kama unayoyataka. Badala yake, fanya kazi kwa bidii kuweza kukabiliana na upinzani ulionao na usiogope  wala kutishwa na chochote, hapo utakuwa umefanya kitu cha kuboresha biashara yako.


2. Kuwa na malengo na biashara yako.
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayoyataka katika biashara yako, ni muhimu pia kujiwekea malengo maalum ya kibiashara. Malengo hayo yatakusaidia kujua ni wapi unapotakiwa kufika baada ya muda fulani na wapi ulipokwama. Unapokuwa na malengo juu ya biashara yako, ni lazima nidhamu yako itakuwa juu hasa katika mambo ya pesa na utahakikisha kufanya lolote ili biashara yako ikue. Biashara yoyote unayoifanya kama haina malengo maalumu haiwezi kukua na kufika mbali hata iweje.

3. Jitoe Kufanya kazi kwa bidii.
Kwa kuwa umeamua kuwa mjasiriamali, kitu pekee ambacho kinaweza kufanya biashara yako ing’ae ni kufanya kazi kwa bidii,  kwa ubunifu na maarifa makubwa. Nguvu nyingi, mawazo na mwelekeo mkubwa unatakiwa kuupeleka kwenye biashara yako ili ikuletee mafanikio makubwa na  si vinginevyo. Kumbuka, wewe ndiyo bosi na mkurugenzi wa biashara yako unayoifanya, ukilala au kusinzia ujue kabisa kila kitu kitaharibika na hutaweza kusonga mbele.


4Ishi na watu wenye mitazamo chanya.
Itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa kama utakuwa una watu wengi wanaokuzunguka ni wenye mitazamo hasi na biashara unayoifanya. Watu hawa watakukatisha tamaa kwa maneno na mienendo yao na utajikuta unashindwa kusonga mbele. Ili uweze kuboresha biashara yako na kufikia mafanikio makubwa, ni muhimu sana kuwa na watu chanya ambao wanauwezo wa kukusaidia kwa hali yoyote ile hata pale ambapo mambo yako yanakwenda hovyo. 

5. Badili jinsi unavyojitazama mara moja.
Kuwa na mtazamo chanya juu ya biashara yako ni kitu cha lazima sana kwako, ili iweze kuleta mabadiliko unayatarajia. Biashara yako haitafika popote kama utakuwa mtu wa kuitazama na kuona kuwa haitafanikiwa sana kama unavyoziona za wengine. Kutokana na mitazamo wako huo utaanza kufanya mambo kizembe hali itakayopelekea wewe kushindwa. Kama unataka kuboresha  biashara yako, badili jinsi unavyojitazama wewe na biashara kwa ujumla.

6. Jifunze zaidi kuhusu biashara.
Unatakiwa kujifunza na kuilewa vizuri biashara unayoifanya kila siku. Hiki ni kitu ambacho hutakiwi kukwepa kwani kitakusaidia kuiboresha biashara yako kwa sehemu kubwa sana. Kwa kadri jinsi utakavyozidi kujifunza juu ya biashara yako, utagundua mapungufu mengi ambayo ukija kufafanyia kazi, itakusaidia kuhama kutoka ngazi moja na kuelekea ngazi nyingine zaidi ya mafanikio kibiashara.

Kumbuka, ili tuweze kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa, tunalazimika kuboresha  biashara zetu kwa sehemu kubwa kila siku. Kama utashindwa kuboresha biashara yako, basi elewa tu hutafika mbali sana kimafanikio kama  unavyofikiri, kwani nguvu ya ushindani itakushinda na utajikuta umebaki pembeni na kuwa mtazamaji kwa wengine. Kwa kuanzia, hayo ndiyo mambo muhimu unayotakiwa kuyajua ili kuboresha biashara yako.

Nakutakia ushindi katika biashara yako iwe ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na kuhamasika, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,


Feb 13, 2015

Kama Unaendeshwa Na Kitu Hiki, Maisha Yako Ni Magumu Sana.

No comments :
Mtu mwenye hisia nyingi ambaye anaongozwa na hisia, ni yule ambaye huweza kuathiriwa au kutikiswa kwa urahisi zaidi na hisia. Ni jambo zuri kujijua sisi wenyewe na haiba zetu na hata kutambua hisia zetu. Ninapozungumzia hisia nikiwa na maana ya hali kama kuwa na furaha, huzuni, chuki na hata wakati mwingine kijicho hizo ni baadhi tu ya hisia.

Baadhi ya watu ni wenye kuongozwa sana na hisia wakati ambapo wengine hawako hivyo na kwa  kuutambua ukweli huu tutaweza kuzuia na kuepuka kuumiza vichwa vyetu na hata kupata maumivu mengine katika maisha yetu. Hata kama hatumo katika kundi la wale wenye hisia nyingi, bado kila mmoja wetu anazo hisia na yuko katika hatari ya kuongozwa na hisia hizo.

Tunaweza kuamka mapema sana asubuhi siku moja, huku tukiwa tumejazwa na hisia za huzuni na kwa siku hiyo nzima tukaongozwa na kufuata hisia hizo. Siku inayofuata tunaweza tukaamka pia tukiwa tumechukia, huku tukihisi au kutaka kuona kila mmoja wetu pale nyumbani kwetu aondoke machoni petu, hivyo tukajikuta tukaishia kufanya vituko vya ajabu tu.

Wakati mwingine tunaweza kuamka na hisia za kujisikitikia sisi wenyewe na kujuta sana na hata kuamua kukaa kwenye kona tukiugulia kwa siku nzima huku tukiwa tumeshika tama. Na kujiuliza maswali mengi ambayo hayana majibu na huku tukiwa hatutaki kabisa kuongea na mtu. Na inapotekea mtu akatuongelesha tunakuwa wakali sana kiasi cha kwamba tunaweza kumjibu vibaya kama sio sisi tuliozoeleka.


Hivyo basi, iwapo tutaamua kuziachia hisia zetu zifanye vile zinavyotaka, basi ni wazi kabisa hisia hizi zitachochea matatizo ambayo yatasababisha tutoke nje ya makusudio yetu mema na kutupeleka kwenye makusudio au matakwa ya kutuangusha. Hapa ndipo pale tunapoanza kusema, ‘ilikuwa ni ibilisi tu’. Ndio maana katika maisha yako, kama bado ni mtumwa na unaendelea kuendeshwa na hisia zako, maisha yako ni magumu sana. Ni magumu kwa sababu kila wakati utakuwa unaishi maisha yanayokuumiza wewe tu.


Nimetumia miaka mingi ya maisha yangu katika kufuata vile nilivyokuwa nikijihisi. Kama niliamka asubuhi nikiwa mwenye huzuni, basi nilihuzunika siku nzima. Kwa wakati huo sikuweza kujua kwamba, ningeweza kuzizuia hisia za aina hiyo. Sasa nimetambua kwamba, ninaweza kupambana kikamilifu na hisia zote mbaya na zilizo hasi ambazo zinatamani kuniongoza siku nzima.

Ni lazima tujifunze kuwa wenye tahadhari kuhusiana na hisia zetu mwenyewe na kuweza kuelewa jinsi tutakavyoweza kuziongoza na kuzisimamia kwa usahihi na uhakika zaidi. Njia mojawapo ya kufanya hivyo, ni kuzijua aina tofauti za haiba au tabia na kujua namna zinavyoitikia kwa njia tofauti, hali au mazingira yanayofanana.

Nimejifunza kwamba, ninapoamka asubuhi nikiwa na kisirani, sipaswi kuendelea kukilea kisirani hicho. Ninapaswa badala yake kuamua kuwa mimi, kuamua kuwa na mkabala tofauti wa kimaisha kwa siku hiyo. Ni mimi ninayepaswa kusema ninataka nijisikie vipi, siyo mazingira au hali inayonizunguka.

Ninapojikuta nimenyong’onyea, ni lazima nijiulize haraka kama ni lazima ninyong’onyee. Ni wazi wazi kwamba, huwa ninapata jibu la hapana. Kwa hiyo, kuanzia hapo hutafuta sababu ya kunyong’onyea kwangu. Nikishaipata hutafuta sababu iliyo kinyume na hiyo, ambapo hunisaidia kuondokewa na kunyong’onyea huko sana.

Nakutakia maisha mema yawe ya furaha kwako, endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku, karibu sana.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,


Feb 12, 2015

Kama Hujui, Mabilionea Wengi Duniani Wako Hivi.

1 comment :
Kila kundi la kipato lina tabia na mienendo yake. Pengine kunakuwa na ugumu wa kuikwepa mienendo hiyo kwa wahusika, baada ya kuingia humo au mienendo hiyo ndiyo imewasaidia kufika hapo walipofika. Tunasema, kama alivyo binadamu ambapo kila mmoja ana haiba yake, makundi ya kipato nayo yana haiba zake, ambazo zinaweza kuwa tofauti na makundi mengine.

Kwa mfano, ukitazama kundi la mabilionea walio wengi duniani, utabaini kuwa wana sifa ambazo zinajitokeza sana kwa watu hao. Kuna sifa ambazo wanakuwa nazo na wala hawazipangi, bali ni kwa sababu ya mazingira au saikolojia ya fedha, wao wanakuwa na tabia au mienendo hiyo zaidi kuliko watu wa makundi mengine. Kutokana na mienendo hiyo mara nyingi ndiyo inawafanikisha sana.

Ukikagua sana, utakuja kugundua kuwa mabilionea walio  wengi ni wale ambao wanafanya biashara zinazohusiana na fedha, kama benki ikiwa pamoja na uwekezaji wa hisa, kuna ambao wanasughulikia mawasiliano kama simu na mitandao ya intaneti na hata kujishughulisha na ujenzi katika kiwango cha kimataifa au kwenye maeneo mbalimbali kama sehemu muhimu ya biashara zao.

Unaweza ukajiuliza maswali mengi kidogo na kuanza kushangaa biashara zingine vipi? haziwezi kumpa mtu utajiri na hatimaye kuwa bilionea? Siyo hivyo, kuwa kwamba biashara zingine haziwezi kumpa mtu ubilionea, hapana. Hizi ndizo ambazo zimewapa wengi ubilionea zaidi. Ukitazama kwa makini utagundua ukweli huu kuwa mabilionea wengi wamezalishwa kutokana na biashara hizo.


Pia mabilionea walio wengi wanatabia za kuacha mali zao kwa taasisi za kusaidia au hata kwenye nyumba za ibada au mifuko mbalimbali ya misaada baada ya kufa kwao.Na huacha fedha kidogo sana kwa watoto wao. Hapa kwetu, watoto wakishakuwa na baba mwenye fedha, hawataenda shule wala kujifunza maisha. Wanasubiri baba afe ili warithi. Wakati mwingine hurithishwa hata kabla baba hajafa. Matokeo yake ni kutapanya mali na kubaki mikono mitupu.

Hata kuna kipindi Bill Gates alishawahi kusema kwamba, hata iacha fedha yake kwa watoto wake, bali ataitumia kusaidia kuondoa matatizo yenye kusumbua sana dunia. Kabla hajafa ameshaanza kufanya hivyo. Watoto wake nao wanahangaika kivyao kujua maana ya kutafuta. Ni kwa sababu, kuwa sisi, ikiwemo kutafuta mafanikio kwa bidii zote, ndicho hasa kilichotuleta duniani. Hujaumbwa uwe maskini.

Lakini lingine la kushangaza zaidi ni kwamba, mabilionea wengi hawana hata digrii ya kwanza. Inawezekana walipitia vyuo lakini wakapata cheti au stashahada au walimaliza tu elimu ya msingi au sekondari. Kwa hiyo utakuja kugundua kuwa, fedha au utajiri hausiani sana na kusoma sana na hii inaonyesha haviko karibu. Mawazo, yaani unachoamini kuhusu fedha na utajiri, ndilo jambo la awali kabisa.


Mabilionea wengi pia hawakupewa urithi au kupata bahati nasibu katika maisha yao. Walio wengi  wametafuta fedha kwa juhudi zao wenyewe kwa kuanzia chini kabisa. Wengine waliweza kusota hadi wakawa kama vituko, lakini wakaja kusimama katika njia ambayo watu wengine wameshangaa na kubakia kusimulia wasielewe ni kitu gani kilichofanyika.

Kuna tatizo moja kwa mabilionea waliowengi. Kwa kufuata au kuhangaika kupata mafanikio zaidi, hujikuta wakisahau kwamba, kuna burudani, kuna ‘hobi’ na muda wa kusahau masuala ya shughuli. Wao ni watu wa kazi tu na ubunifu ndivyo vyenye kuwaumiza kichwa na si vinginevyo. Kuna wakati huwa wanajikuta hata wakipunguza hata masaa ya kulala sababu ya kufanya kazi kwa bidii zote.

Hebu jaribu basi kujikagua ili uone kama ni kweli nawe unaweza kuwa na sifa kadhaa kama hizo za mabilionea. Huenda nawe unatamani kuwa bilionea ila hujajua au kuamua ni kwa njia gani. Jua sifa zao, labda utawea kupima kiwango cha ukaribu wako kwao. Siyo lazima uwe na fedha nyingi ili kuwa bilionea, anzia hapo ulipo ukiwa umepania kuwa, unataka kuwa bilionea, utafanikiwa.


Tunakutakia kila la kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na kuhamasika, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,






Feb 9, 2015

Maisha Ni Vitendo Na Si Ndoto Pekee, Ndoto Ni Mwanzo Tu Wa Maisha…

No comments :
Kwa kawaida, binadamu ana mambo matatu muhimu ambayo anaweza kuyaendesha au yakamwendesha kichwani kwake, moja ni fikra zake au mtazamo (thoughts you think), mbili ni taswira anazozijenga kichwani kwake (image you visualize) na tatu ni vitendo vyake (the actions you take). Sisi binadamu tunawajibu wakuhakikisha tunaleta maendeleo katika maeneo tunayoishi kwa juhudi zetu binafsi. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu mwenyewe.

Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake. Mambo yote tunayoyaona duniani, ugunduzi, vitabu, miziki, filamu na kila kitu kilichopo duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha, vipaji, talanta na habari njema ya maisha yako. Kutokana na upekee ulionao duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe. Historia ya dunia inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na makubwa kuhusu uwezo wao.

Toka enzi za wajasiriamali tunaowasoma katika historia akina Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na hata kutojiamini kabisa. Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo mengi kwa kutumia vipawa vyao.

Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wameshawishiwa na mifumo ya dunia na maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama nakala. Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo wao wa kipekee na kutumia upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao.


Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako yatapata maana. Unacho kipaji ndani yako. Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani, Mungu aliumba mwanadamu mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.

Unaweza usiwe na uwezo kuanzisha biashara ya mgahawa au ya daladala lakini ukawa na uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo za kila aina hivyo ukawa mjasiriamali  katika kanda ya mziki iwapo una uwezo wa kuchekesha basi fanya ujasiriamali katika kipengele cha ucheshi kama jamaa wa futuhi. Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa duniani ili  kuifanya dunia itembee, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ing'are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa hatujayajua bado lakini yamo ndani yako. Aidha wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia iwe na mitandao tunayoiona sasa hivi.

Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na mengine. Bila kujionea aibu mwenyewe, na kujitafuta na kujiuliza kasoro zako ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza, tafuta kujua mazuri ya kwako huku ukitafuta kuongeza mengine.

Ukiona Kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope kujaribu, jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi. Sikiliza sauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani? Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?

Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. Vipo vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya. Lakini ni uamuzi wako kukubali kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa vile ninavyotaka maishani.

Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali kumalizwa, vumilia, jiamini, Jipende, jiendeleze, jikaze, jionyeshe, jitafute mwenyewe, jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na nguvu zozote mbele yako. Kumbuka kuwa dunia hii itaendelea kuendeshwa na hata kutengenezwa na binadamu wenye uelewa mpana wa nguvu iliyo ndani yao na si wababaishaji na wenye maisha ya maridadi.Wanadamu wote walioweza kufanikiwa.

Kuna wakati tumekuwa tukilaumu watu wasiohusika katika maisha yetu magumu, kuwa wanaharakati wa mambo yasiyotuhusu, kutoa maoni yasiyo na maoni na kuchambua timu za ulaya na kuelezea mchezaji fulani analipwa kiasi gani cha mshahara. Ni lini umewahi kaa nyumbani kwako au kwenu na ukatumia muda wako kuchambua vipaji vyako? Ambavyo ungevitumia katika maisha yako na jamii inayokuzunguka?Kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajijua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe.

Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki, nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio atakayotengeneza na mwenyewe. Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa, kila mwanadamu anao uwezo wa kufanikiwa. Na zaidi ni kuwa kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake, lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna vichangizi vya mafanikio / success ingredients.

Unachopaswa kutambua ni kuwa, hali ya maisha uliyonayo sasa si kipimo cha mafanikio yako ya baadaye, unaweza kuwa vyovyote kimafanikio kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha Kwa kujua vipaji na vichagizi hivyo ni kama vifuatavyo: Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha.

Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni, maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo. Ukitaka kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa duniani.

Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe, ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza. Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini. Kila mwanadamu anayo zawadi ndani yake, zawadi hii huja kama kitu anachokipenda na kukiweza. Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio. Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta mafanikio.

Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk. Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio. Maisha ni vitendo na si ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupanga peke yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo.

Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza na kujifunaza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha bila maarifa hayatembei. Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu.

Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuaji kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako unakua zaidi. Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa mjasiriamali wa kipekee na yale ayatakayo maishani, Dunia ina mengi ya kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli.

Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili. Siri kubwa ya watu wenye mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha, wapo tayari kuumia kwa kuchagua maisha wayatakayo. Chagua kipengele mojawapo cha kijasiriamali unachotaka kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua kufanikiwa.

·        MAKALA HII IMEANDIKWA NA MESHACK MAGANGA – IRINGA

·        MASALIANO - 0713486636