google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jul 30, 2015

Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu

No comments :
Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo wa familia za kitanzania. Afrika Mashariki, na Dunia Nzima. 
Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini. Vitunguu hutumika katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia hutumika kutengeneza supu n.k

Aina Za kilimo Cha Vitunguu
Kilimo cha vitunguu kinaweza kufanyika kwa aina mbili
  •   Green House
  •  Shambani 

Kilimo cha kitunguu Green House

Kilimo cha vitunguu katika shamba la kawaida.

Mahitaji muhimu katika kuzalisha zao la vitunguu
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu.
Kutayarisha shamba
Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.
Upandaji wa mbegu za vitunguu
Mbegu zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi ya cm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari. Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota, matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada ya siku 7 hadi 10.
Matunzo ya bustani ya vitunguu
  • Umwagiliaji

 Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu. Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) Umwagiliaji ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba. Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua. 
Pia ni vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu. Kuthibiti magugu na kupandishia udongo Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu. Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa kutumia madawa ya kuua magugu.
Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya vitunguu ipo juu juu sana. Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu sana.
Hali ya hewa na maji
Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.
Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati
wa kukomaa na kuvuna vitunguu.
Aina za vitunguu
Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta. ikiwa kilimo bora kitazingatiwa. Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
  • Mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
  • Msimu wa kupanda
  • Uwezo wa kuzaa mazao mengi
  • Uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Mbegu bora

Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-


  • Uotaji zaidi ya 80%
  • Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
  • Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unyevu.
Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
  • Chanzo cha mbegu
  • Tarehe ya uzalishaji
  • Tarehe ya kuisha muda wa
  •  Kifungashio cha mbegu.
Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja
Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: 
  •  ALPHA Seed Co, Popvriend,
  • · Rotian Seed, 
  • ·  Kibo Seed, 
  • ·   East African Seed Company nk. 

 Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya pembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
Nikutakie siku njema na kilimo bora, katika makala ijayo tutaangalia magonjwa yanashambulia vitunguu na jinsi ya kuweza kuyazuia.
Makala hii imeandikwa na  mtaalamu wa masuala ya kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com









                                         ,
















Jul 28, 2015

Mambo Muhimu Ya kukusaidia Kukupa Furaha Katika Maisha Yako.

No comments :
Mara nyingi katika maisha yetu iwe kazini au katika jamii tunayoishi huwa ni watu wa kukutana na hali tofauti tofauti ambazo wakati mwingine huwa zinatupa furaha au huzuni katika maisha yetu. Lakini, pamoja na hali zote hizo kuweza kujitokeza katika maisha yetu suala la kuwa na furaha ama huzuni huwa linabaki mikononi kwetu sisi wenyewe.
Hii huwa iko hivyo kwa sababu, sisi ndiyo huwa ni watu wa mwisho wa kuamua maisha yetu tuyape furaha au huzuni. Kama tutakuwa ni watu wa kuchagua mambo ya kutupa furaha basi ni wazi maisha yetu yatajawa na furaha, lakini pia kama tutakuwa ni watu wa kuchagua mambo yakutupa huzuni pia maisha yetu yatakuwa ya huzuni hivyohivyo.
Hivyo, mpaka hapo unaweza ukawa unaona kuwa suala la kuwa na furaha au huzuni ni suala linalolenga uchaguzi zaidi katika maisha yetu. Kitu cha msingi na cha kuzingatia ili kuwa na furaha ni kuhakikisha wewe huathiriwi sana na mazingira ya nje katika kukupa furaha yako. Sasa je, ni mambo gani ambayo wewe unatakiwa kuyajua ili yakupe furaha ya kweli katika maisha yako?
1. Badili mtazamo wako jinsi unavyo yaangalia mambo.
Mtazamo ulinao juu ya maisha yako au jinsi unavyoyatazama mambo mara nyingi huo ndio unaokupa furaha au huzuni katika maisha yako. Watu wegi huwa wanatabia ya kuangalia mambo kwa mtazamo hasi sana. Kutokana na kuyaona mambo kwa mtazamo hasi ndivyo hujikuta wakipoteza furaha katika maisha yao.
Kama unataka kujenga furaha zaidi katika maisha yako kuwa na mtazamo chaya. Kama ulikuwa unahisi na kuona fulani ni mbaya sana kwako badili mtazamo wako na anza kumwangalia katika upande wa uzuri wake. Kwa jinsi unayozidi kuyaangalia mambo mengi kwa mtazamo chanya ndivyo utakavyoweza kujikuta unafurahia zaidi maisha na kuwa na furaha.

2. Fikiria majibu ya kile unachokitaka.
Wengi wetu huwa ni watu wa kufikiria sana matatizo waliyonayo badala yakufikiria njia za kutoka kwenye matatizo hayo. Hujikuta ni watu wa kuumia na kuwaza pengine kutokana na ugumu wa maisha walionao. Kwa kuendelea kufikiria matatizo badala ya kutafuta suluhu hivyo hupotezea wengi furaha.
Furaha ya kweli katika maisha yako haiji tu kwa kufikiria sana matatizo uliyonayo, inakuja kwa kutafuta suluhisho la matatizo hayo. Unaweza ukawa unajiona una mtatizo mengi sana yanakufanya ukose furaha, hiyo ni kweli lakini kitu cha msingi tafuta njia ya kuondokana na matazo hayo. Kwa kufanya hivyo utaijenga furaha siku hadi siku.
3. Angalia mambo uliyoyafanikisha.
Inawezekana ikawa unakosa furaha kutokana na malengo yako mengi kuona kama vile hayajatimia. Kwa kuangalia hivyo hiyo itakuumiza sana. Ili iweze kuondokana na hali hiyo jifunze sana katika maisha yako kuanglia mambo yale uliyoyafanikisha. Hata kama ni kidogo lakini kama ulifanikiwa kwa namna fulani jipongeze kwa hayo kwanza.
Kwa jinsi utakavyozidi kuangalia mambo uliyofanikiwa nakuyaweka katika orodha ndivyo itajikuta unaanza kupata nguvu ya kutenda zaidi na kuwa na furaha ambayo ulikuwa unahisi pengine umeipoteza kabisa. Siku zote kumbuka hili, jifunze kuyaangalia mambo uliyoyafanikisha. Mambo haya yatakusaidia kukupa furaha zaidi kuliko unavyofikiri.
4. Fanya mambo yatakayowapa furaha wengine.
Katika maisha yako kila siku fanya jambo, hata kama ni kidogo  litakaloweza kumpa mwingine furaha na siyo huzuni. Kama utamfanya mtu mwingne awe na furaha ni wazi kabisa lazima na wewe utajikuta unafuraha. Hiyo ni kanuni rahisi kabisa ambayo unaweza ukawa unaitumia kila siku katika maisha yako kukujengea furaha.
Watu wengi huwa wanategemea kupata furaha kwa wengine wakati wao huwa hawatoi hiyo furaha. Katika dunia hii mara nyingi unapata kile unachokitoa. Kama unatoa mafanikio, tegemea kupata mafaniko. Kama unatoa furaha, tegemea kupata furaha pia katika maisha yako. Hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda.
5. Ishi na watu wenye furaha.
Kama utakuwa ni mtu wa kutafuta marafiki ambao muda mwingi wao ni watu wa huzuni, usitegemee kuwa na furaha katika maisha yako. Furaha ya kweli utaipata katika maisha yako kama utakuwa unazungukwa na watu wenye furaha zaidi. Unaweza ukawa unaanza kushangaa kwa nini hii iko hivyo?
Mara nyingi watu hawa watakusaidia kukuambukiza furaha hiyo nawe utajikuta ni mwenye furaha kama wao. Lakini kama unaishi na watu hasi watu wa kuhuzunika mara kwa mara, tambua utakachovuna hapo ni huzuni hizohizo. Watu wanaotuzunguka wanaathari kubwa sana katika maisha yetu iwe katika suala la furaha au mafanikio kwa ujumla.
6. Kila siku fanya kitu unachokipenda.
Inaweza ikawa ni kitu kidogo tu na cha kawaida unachokipenda lakini kama unakipenda kifanye kila siku kitakuongezea furaha. Kama wewe ni mtu wa kupenda kusoma vitabu soma walau kurasa chache tu, utaweza kutimiza furaha yako. Kama umezoea kuimba na unapenda kuimba, halikadhalika fanya hivyo hiyo itakuongezea furaha pia.
Kwa kawaida yale mambo tunayoyapenda hayo ndiyo huwa yanatuongezea furaha. Haijalishi mambo hao ni madogo au mkubwa kiasi gani lakini ni muhimu sana kwetu kuyafanya kila mara kama tu yanatupa furaha katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunayapa maisha yetu vile tunavyovihitaji na kujikuta ni watu wa furaha.
Kwa vyovyote vile iwavyo maisha yako unayouwezo wa kuyapa furaha ukiamua iwe hivyo kwako. Kwa kutegemea na kuamini kila siku kuwa maisha yako ni lazima yawe ya furaha na kufanya mambo yatakayokupa furaha katika maisha yako, hivyo ndivyo iatakavyokuwa ni lazima utakuwa na furaha. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo muhimu ya kukusaidia kukupa furaha maisha yako.
Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, endelea kuwashirikisha wengine kujifunza zaidi kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,





Jul 23, 2015

Nguvu Kubwa 5 Za Mafanikio Ulizonazo Ndani Mwako.

No comments :
Habari za siku rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO Kwa nguvu zake Mungu naamini umzima na unaendelea na harakati nzima za kuhakikisha maisha yako yanakuwa imara kufikia viwango vya juu vya mafanikio.
Karibu tena katika siku nyingi nzuri ambapo tunakuwa katika darasa huru la kuweza kujadili mambo muhimu ya kimafanikio. Leo katika makala yetu ya leo tutaangalia nguvu kubwa za kimafanikio ambazo binadamu kama binadamu huwa anazo ndani yake na zinapotumiwa kikamilifu huwa zinaleta matokeo makubwa ya kimafanikio kwa maisha ya mtu.
Hizi ni nguvu ambazo kila binadamu aliye chini ya jua huwa anazo ingawa kwa wengi inakuwa ni ngumu kuweza kuzijua. Ni nguvu hizihizi ambazo zinapotumika katika maisha ya wengine huweza kuleta maajabu na kuonekana maisha yao kama vile ya ajabu hivi kumbe ni matokeo ya nguvu ambazo hata wewe unaweza ukazitumia na kufanikiwa.
Ni nguvu ambazo huwa ni zaidi ya bomu la nyukilia zinapotumika kikamilifu. Na ni nguvu ambazo nataka hata wewe uweze kuzijua ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri yamafanikio. Ikumbukwe kuwa mara nyingi binadamu anapoambiwa kuwa ana nguvu nyingi za ziada kwa wengi huonekana ni kichekesho na huwa hawaamini kitu kama hicho.
Kwa pamoja napenda nikushirikishe nguvu hizi muhimu kwako ambazo ukizitumia kwa namna yoyote ile lazima uwe mshindi na uachane na maisha ya kulalamika ambayo umekuwa nayo sasa kwa muda mrefu. Je, unajua ni nguvu zipi hasa ambazo unazo ndani yako zenye uwezo wa kukufikisha kwenye mafanikio makubwa?
1. Nguvu ya Uzingativu.
Hii ni moja kati ya nguvu kubwa sana uliyonayo ndani mwako lakini inapotumiwa huwa ina uwezo mkubwa wa kukupa mafanikio unayoyataka. Mara nyingi unapokuwa unaweka nguvu kubwa ya mawazo katika kitu kimoja na kuamua kuachana na vitu vingine kabisa visivyoendana na kile unachokitafuta hapo ndipo unapokuwa unatumia nguvu ya uzingativu kwa usahihi zaidi.
Nguvu hizi za uzingativu unapozidi kuziweka katika jambo moja iwe malengo yako au kitu chochote kile ni lazima uweze kufanikisha jambo hilo hata iweje. Itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kushindwa kutokufanikiwa kama kweli utakuwa umeweka nguvu yako ya uzingativu  sehemu moja tu na kutoisambaza sehemu nyingine. Hii ni siri mojawapo nzuri ya kimafanikio kama utaitumia.
Unaweza ukalijua hili zaidi kwa kuangalia mfano wa kioo ambacho kisayansi kinafahamika kama lensi. Hiki ni kioo ambacho wengi tumewahi kukutana nacho tukiwa shuleni. Kioo hiki huwa kinatabia na sifa moja kubwa ya kuweza kukusanya mwanga au miale ya jua na kuweza kuiweka sehemu moja. Kama ilivyo kwa kioo hicho ndivyo ambavyo nguvu ya uzingativu inavyofanya kazi kwetu na kuleta matokeo chanya ikiwa itatumiwa vizuri.

2. Nguvu ya maamuzi.
Hii pia ni moja kati ya nguvu kubwa iliyondani mwako lakini kwa wengi pia huwa haijulikani. Kama ilivyo kwa nguvu ya uzingativu na jinsi ambavyo inavyofanya kazi, nayo pia nguvu hii huwa ina matokeo yake ambayo yanaweza kuwa hasi ama chanya kulingana na jinsi ambavyo ilivyotumika kila siku katika maisha yako.
Kumbuka maisha yako, yapo hivyo kutokana na nguvu ya mamuzi ambayo uliweza kuifanya katika kipindi cha nyuma. Kama uliweza kufanya maamuzi sahihi basi upo kwenye njia sahihi ya kuelekea mafanikio, lakini kama maamuzi yako yalikuwa mabovu ndivyo ambavyo na maisha yako yalivyo kutokana na maamuzi uliyofanya.
Haijalishi unapitia kwenye utata au ugumu wa maamuzi kiasi gani, lakini kitu kikubwa ambacho unatakiwa kukijua ni lazima uwe na maamuzi sahihi ambayo yatakusaidia kukupa mafanikio unayoyahitaji katika maisha yako. Kinyume cha hapo utakuwa ni mtu wa kupoteza muda wako bure kwani hutoweza kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji katika maisha.
3. Nguvu ya ung’ang’anizi.
Katika maisha yetu kuna wakati huwa tunakutana na vikwazo vingi sana ambavyo huwa vina uwezo mkubwa wa kuturudisha nyuma. Vikwazo hivi huwa tunauwezo wa kuviweza kuviepuka kwa kufanya kitu kimoja ambacho nacho ni kuweza kung’ang’ania mpaka kuhakikisha kuona matokeo tunayoyataka katika maisha yetu.
Kwa kung’angania jambo ambalo tunataka kulifanya ndivyo ambavyo huwa  tunajikuta tunatumia nguvu hii ambayo huwa tunayo ndani mwetu. Kumbuka huwezi kung’ang’ania kitu mpaka kuweza kuwa na msukumo fulani ndani yako. Msukumo huo ambao unakuwa unauhisi unachemka ndani mwako huo ndio nguvu mojawapo ya kimafanikio ambayo unakuwa nayo bila kujua.
Watu wengi ambao unaweza ukawaona wanashindwa katika maisha yao kwa namna moja au nyingine huwa ni watu ambao mara nyingi wameshindwa kutumia nguvu hii ambayo ipo ndani mwao. Kwa kawaida unaposhindwa kutumia nguvu hii ya kung’ang’ania changamoto kidogo tu ikijitokeza katika maisha ni lazima kwako uweze kushindwa hata ufanyanye nini.
4. Nguvu ya kufikiri kile unachokitaka.
Ili uweze kupata kile unachokihitaji hii ndiyo nguvu pekee unayotakiwa kuitumia. Nguvu hii ni nguvu ambayo huweza kufanya kazi kwa kuweka picha kwenye ubongo au akili yako yale mambo unayoyata tu. Kwa mfano kama unataka kujenga nyumba nzuri, picha ipi inayokujia kichwani mwako? bila shaka ni aina ya nyumba tofauti tofauti zinakuja kichwani mwako.
Picha hizo unazoziona hizo ndizo nguvu ya kufikiri kile unachokitaka. Nguvu hii wakati mwingine kitaalamu hufahamika kama ‘Power of imagination’. Hivyo unaona kabisa hata wewe unaposema nataka gari nzuri, kichwani mwako hayaji maneno G-A-R-I N-Z-U-R-I. kinachokuja ni picha za hizo gari za aina tofauti.
Kufikiri kile unachokitaka ni nguvu mojawapo muhimu ambayo binadamu anayo ndani yake na inauwezo mkubwa wa kumsaidia kufikia mafanikio yoyote anayotaka. Kwa vyovyote vile iwavyo katika maisha yako, jizoeze kuujaza ubongo wako picha ambazo unataka zikutokee. Kwa kufanya hivyo ni lazima uweze kufanikiwa.
5. Nguvu ya hamasa.
Hii ni nguvu ambayo huwa tunayo ndani yetu ambayo mara nyingi huweza kuipata kutokana na kuona wengine ambavyo wananya vizuri katika mambo yao ama wakati mwingine huwa tunaweza kuipata kupitia vitabu, mitandao ya kuhamasisha na kuelimisha kama huu wa DIRA YA MAFANIKIO na semina au warsha mbalimbali.
Jaribu kufikiri kidogo, bila haka unaweza ukawa shahidi mzuri wa hili hasa pale ambapo huwa unajisomea vitabu vya mafanikio. Kuna msukumo au nguvu fulani ambayo huwa unaipata kutoka ndani mwako, pengine kutokana na kile kilichoelezwa kuweza kukugusa zaidi katika maisha yako. Nguvu hiyo mbayo huwa unaipata hiyo ndiyo nguvu ya hamasa, ambayo ipo ndani mwako.
Kwa kumalizia makala hii, tambua kuwa binadamu kama binadamu anazo nguvu nyingi sana ndani yake ambazo akiweza kuzitumia zinaweza kumfanyia mambo makubwa na kumfikisha kwenye kilele cha mafanikio. Hizo ni baadhi tu ya nguvu tulizonazo ndani mwetu.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza zaidi.
Kama una maoni, maswali au ushauri karibu sana.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,


   





Jul 21, 2015

Kipaji Chako Ni Ajira Namba Moja.

No comments :
Tunu muhimu za mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya kila mtu ni vipawa/talanta. Kwa bahati mbaya sana na pengine kutokujua umuhimu wa vipawa, watu wengi hawatilii maanani vipaji walivyonavyo. Wengi wanaishi kwa kuiga maisha ya watu wengine kana kwamba wao ni nakala ya wengine. Kipaji chako ni mtaji mkubwa kama utaamua kukitumia vizuri ipasavyo. Kipaji chako ni fursa ya kufanikiwa maishani. Ni daraja la maendeleo kwa binadamu yeyote yule.
Kipaji ni umahiri wa kipekee aliouweka Mungu ndani ya akili ya mtu unaongoza usadifu wa viungo na fikra zake kufanya jambo Fulani kwa upekee kabisa. Ni talanta ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni ujuzi wa kuzaliwa nao, elimu inakusaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake kwa ufanisi na kwa manufaa zaidi. Kwa mfano, michezo mbalimbali, sanaa kama mziki, kuchora, kucheza mpira, kuimba, kusanifu, kubuni program za kompyuta, mitandao, na wakati mwingine kuchonga. Wapo watu ambao wana vipaji katika eneo mojawapo wanachotakiwa kufanya ni kuvitumia vipaji vyao.
Watu mashuhuri na wale waliofanikiwa sana ni wale waliotumia vipaji vyao vizuri. Kuna mifano hai mingi kama Filbert Bayi wa Tanzania alitumia talanta yake ya kukimbia mbio, wanamuziki kama vile Michael Jackson, Rose Muhando walitumia sauti zao kufanikiwa. Na hata wachezaji maarufu wanatumia vipaji vyao kucheza mipira na wanafanikiwa kuliko hata wasomi wenye shahada lukuki.
Wasanii na wana michezo wengi ni miongoni mwa watu maarufu na matajri sana duniani, japokuwa walio wengi hawana elimu kubwa kiasi cha kushangaza , walichofanya ni kutumia vipawa vyao kama ipasavyo. Maana hata sukari iliyo katika chai bila kukorogwa chai inaonekana haina sukari. Vivyo hivyo vipaji tunavyo, ili vifanye kazi vizuri inabidi tuvikoroge.

Mungu alituumba na vipaji na talanta nyingi tofauti ili tuvitumie kufanikiwa maishani. Kila mtu ana talanta yake imejificha ndani ya umaizi wa akili yake. Tunahitaji kuweza kuziibua talanta hizo  kule ziliko fichika, na kuzitumia huku tukibadili mitazamo na kasumba. Huwa nasikitika sana kumsikia mtanzania anasimama kwenye chombo cha habari akisema yeye ni maskini anahitaji msaada. Wakati huo kafunika talanta zake kibindoni, na nyuma kaacha ardhi kubwa, misitu mingi na hata watoto wengi ambao ni nguvu kazi muhimu katika kuchangia maendeleo.
Wapo watanzania wanadiriki kusema kuwa “sisi tutaendelea kubaki maskini hivihivi” na wengine wanadai umaskini wao ni mpango wa Mungu. Huu ni uongo na ni dhambi. Mungu angetaka sisi tuwe maskini asingeweza kutupa ardhi kubwa, asingetupa mvua nyingi na maji mengi, asingetupa samaki wengi, asingetupa ndege na wanyama wengi wa mwituni. Asingutupa afya njema na nguvu. Mungu alitupatia vyote hivi ili tuwe matajiri tuwasaidie na wale wanaoishi nchi zisizo na ardhi (mawe tu), nchi zisizo na bahari, nchi zisizo na msitu, mto wala bwawa. Sisi siyo maskini kamwe.
Na kiongozi au mwanasiasa anayetamka Tanzania ni maskini(wakati yeye ni tajiri) huyo ni mpotoshaji. Tusiwafundishe watoto wetu mtazamo hasi hata kama tunachangamoto. Kuwa na matatizo ni sehemu ya changamoto za maisha, tunazipaswa kuzikabili. Maana hakuna mtu au nchi inayojitosheleza. Ndio maana hata wao walioendelea huko ulaya bado wanakuja kwetu kununua malighafi ili wakutumie huko kwao.
Tena nadhani hata walioita mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini(MKUKUTA) walikosea sana. Ingefaa ukaitwa “mkakati wa kukuza uchumi na ustawi wa maisha ya watu”. Kuutaja umaskini wakati tupo ndani ya utajiri mkubwa ni kujitafutia laana ya kudumu .Maana kama tunakubali sisi ni maskini kamwe hatuwezi kuweka mikakati ya maendeleo. Tunabaki na mikakati ya kimaskini.
Nafadhaishwa na mtazamo unaotaka kuzoeleka hapa Tanzania miongoni mwa vijana kuwa mtu yeyote akifanikiwa: kumiliki nyumba nzuri, shamba zuri lenye mavuno mengi, gari zuri, kiwanda na hata kuwa na elimu nzuri anaitwa fisadi, yaani mwizi. Unakuta vijana wenye nguvu wanapita makazi ya watu wenye nyumba nzuri wanasema “unayaona mahekalu ya mafisadi” wakimaanisha kuwa kila nyumba nzuri, kiwanda kikubwa, shamba kubwa ni la fisadi au mwizi. Kwao maendeleo ni wizi na siyo jitihada za kazi. Hawa wamepotoka sana.
Umaskini siyo mpango wa Mungu wala siyo ngozi ya kuzaliwa nayo isiyobadilika. Hata vitabu vitakatifu kama vile bibilia na msahafa vimesema wazi kwamba umaskini siyo mpango wa Mungu. Mungu anataka kila mtu aishi maisha mazuri yenye ustawi huku akimpenda na kutii mwongozo wake. Kila binadamu anahitaji maisha bora. Kila binadamu anahitaji kulala pazuri, kula vizuri, kusafri vizuri, afya bora, kupata elimu bora, mazingira safi, kucheza pazuri na kufurahia maisha kwa ujumla.
Watu wanakuwa kwenye shida kama vile kuishi katika nyumba mbovu, na kula chakula kibaya au kisichotosheleza siyo kwa sababu wao wanapenda, au kudhani kuwa maskini ndiyo sifa ya uadilifu. La hasha ni kwa sababu hawana. Fikra za kuyaona maendeleo yoyote ya mtu au kikundi cha watu ni ufisadi ni dalili kupoteza dira na kukosa matumaini kuelekea ufukara wa kudumu na dhiki kuu.
Na ukiona kijana mwenye nguvu anatamka kuwa hayo majumba ni ya mafisadi, fahamu kuwa familia yake na jamii inayomzunguka iko msibani. Si tetei wizi ama ufisadi na si sahihi kuwa mwizi au fisadi. Na ni dhambi hata kwa mungu wezi waadhibiwe tena vikali.
Lakini, pia sikubaliani na mtazamo kwamba kila anayefanikiwa ni mwizi au fisadi. Kuna watanzania wengi tu ambao wanakesha, wanafikiri na kubuni mbinu za kufanikiwa huku wakiongozwa na jitihada kubwa ya kufanya kazi na kuchangamkia fursa ndani na nje ya nchi na kutumia pesa kwa kwa makini katka uwekezaji binafsi bila ufujaji.
Hawatapanyi mapato kwa starehe na kuulimbukia utandawazi. Kila senti yao inatumika kwa tija na manufaa. Hawa wanastahili pongezi siyo kuitwa wezi. Kazi kubwa tliyonayo hasa vijana ni kutambua vipaji vyetu na kuvitumia ipasavyo.Tpunguze kulalamika tuongoze juhudi zetu katika ufanya kazi zaidi. Tutafanikiwa sana maishani.
§  MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTEMI ZOMBWE, DAR ES SALAAM.

§  MAWASILIANO 0713 000027 

Jul 3, 2015

Hatua Tano Muhimu Za Kuelekea Kwenye Mafanikio.

No comments :
Mara nyingi sana katika maisha yetu tumesikia maneno kama “nipe tano” “chukua tano” maneno hayo yamekuwa maarufu na katika mazingira tofauti, yamekuwa yakiashiria ushindi , au hali ya mafanikio au furaha baada ya hali fulani.
Vivyo hivyo katika maisha yetu ya kutafuta kufanikiwa katika yale yote tunayoyafanya kila siku viko vitu au hatua ambazo huwa zinatulazimu kuzijua au kuzipitia kama kweli tunamaanisha na tunadhamiria hayo mafanikio tunayoyatafuta.
Watu wengi hutamani mafanikio na kuyazungumzia sana katika maneno yao ya kila siku lakini hawajawahi kuyaishi mafanikio hayo kwa sababu ya kutokuwa na dhamira madhubuti katika kuyaelekea. Je, unajua ni hatua zipi muhimu za kuelekea kwenye maisha ya mafaniko?
1.Kuwa na uwezo binafsi wa kuvikagua vile ulivyo ndani yako.
katika maisha yetu ya kila siku hatuna budi namna ya kujifunza kujikagua sisi wenyewe, kuvikagua vile tulivyonavyo ndani yetu kwa sababu ni ukwelli kwamba pasipo kujikagua sisi wenyewe basi hatutaweza kuyatambua mapungufu tulionayo na kama hatutoyatambua mapungufu hayo hayatoweza kushughulikiwa na kuondelewa, maana yake ni kwamba tutazidi kushi na upungufu wetu na hivyo kuathiri ufanisi wetu na mwisho wake mafanikio yetu kwa ujumla yataathirika.
Labda nikupe mfano wa mtu mwenye duka , mara kwa mara huwa na muda wa kuvikagua vitu au mali aliyo nayo dukani kwake na hapa huweza kutambua nini kimepungua , nini hakipo kabisa na nini hakipo kwa wingi. Katika kujikagua sisi wenyewe sio tu tutapata uhakika  wa vile tusivyonavyo bali pia tutapata kufahamu vile tulivyonavyo kwa wingi. Jifunze kufanya tathmini ya maisha yako kila wakati, tathmini matendo yako ya kila siku, maneno yako ya kila siku, mitazamo yako ya kila siku, halafu angalia wapi kuna upungufu na wapi kuna fursa.

 2. Uwezo wa kuwa na msimamo.
Wengi wetu tumeshindwa kuyafikia malengo tuliyowahi kujiwekea kwa sababu tu hatuna msimamo katika vile tunavyoviamini kwa hiyo inakuwa ni rahisi kuyumbishwa na kupeperushwa na kila upepo unaokuja upande wetu. Ili kufikia mafanikio tunayoyatamani hatuna budi kuwa na misimamo fulani katika maisha. Naupenda msemo unaosema kama huwezi kuwa na msimamo na chochote basi utachukuliwa na chochote.
Kama wewe ni kijana na huna msimamo katika baadhi ya mambo basi ni rahisi kujikuta unabebwa na mengi kama vile rushwa na ubadhilifu. Ni vyema kufahamu kila wakati maishani kuwa kama huna msimamo katika ufanisi basi utaangukia katika uzembe na kutokuwajibika na kama hautakuwa na msimamo katika kuhakikisha unafanikiwa basi utaangukia katika umaskini.
3. Uwezo wa kupiga hatua.
Yamkini unatamani sana kufanikiwa na kila siku unaongelea sana mafanikio, ni vyema kujua kwamba mafanikio yetu hayaji kwa kuyatamani au kuyaongelea bali katika uwezo binafsi wa kuamua kupiga hatua. Yawezekana upo katika chombo kizuri tu cha usafiri lakini utajikuta unapitwa na kila mtu, hata wale wenye vyombo vibovu vya usafiri nao watakupita kama utakuwa umekaa tu kwenye chombo chako pasipo kuruhusu mwendo.
Chukua hatua kuelekea mustakabali wako, angalia mbele yako unaona nini? Niniambacho unakiona kwenye mustakabali wako? Nini  ungetamani ukipate kwenye mustakabali wako? Anza kufanya kila kinachohusika ili kuona hiyo ndoto yako ikiwa dhahiri.
Anza kupiga hatua ya kwanza na hatua nyingine zitakuwa ni rahisi kufuatia. Kamwe usitishike na umbali unaouona kuelekea mustakabali wako, jinsi unavyopiga hatua ujasiri wako unafunguka na kukua, kumbuka kuwa kila hatua unayoipiga hata kama ni ndogo kiasi gani inakusogeza karibu na mustakabali wako.

4. Uwezo wa kujitengenezea sura ya maisha yako.
Katika maisha yetu ya kila siku ni ama uamue kuitengeneza sura ya maisha yako au kuibomoa sura hiyo, wengine wetu maisha yetu hayajawahi kuwa na sura nzuri ya kuvutia.
Sisi wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kuamua kuitengeneza sura hiyo kuwa kama vile tunataka iwe, ukiamua kukaa tu pasipo kufanya chochote basi umekusudia kwa dhamiri halisi kuiharibu sura  ya maisha yako mwenyewe.
Ulimwengu wa leo unabadilika kwa kasi sana, ili kuweza kubakia kwenye maana na wenye umuhimu basi hatunabudi kuwezana na mabadiliko hayo. Kama hutoweza kuyaweza mabadiliko ya karne hii basi mabadiliko hayo yatatuweza.
 5. Uwezo wa kukikalia kiti na kuyaongoza maisha yako mwenyewe.
Ziko nyakati ambazo wengi wetu hatuwezi kufika tunapotamani kufika kwa sababu dereva anayeendesha chombo chako siyo wewe, wakati huohuo unafikiria kuelekea pale unapopatamani wewe.
Ni ngumu katika maisha kama unaifahamu ndoto yako na unaiona kesho yako na unaitamani sana kuifikia  basi amua kukaa kwenye kiti cha dereva wewe mwenyewe na kuendesha chombo kuelekea huko.
Watu wengi siyo kwamba tumewakabidhi wengine udereva wa safari yetu kwa kujua bali ni kwa kutokujua, mara unaona muelekeo wa safari siyo ule unaoutarajia, yamkini sasa dereva uliyemkabidhi kiti anakupeleka kwenye ndoto yake na siyo ya kwako tena.
Sasa amua kuingia kwenye kiti cha dereva wewe mwenyewe, hayo ni maisha yako na siyo mwingine. Kamwe usiache furaha ya mafanikio yako katika mikono ya mwingine. Kubali na kuwa tayari kubeba majukumu. Kama unatokea unafanya makosa basi usijitetee na kukwepa, chukua tano!
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTAALAMU WA SAIKOLOJIA,

CHRIS MAUKI WA GAZETI LA MWANANCHI.

Jul 1, 2015

Mawazo Yako Ndiyo Nguvu Uliyonayo.

No comments :
Upo uhusiano mkubwa sana baina ya namna unavyofikiri, na jinsi unavyoishi. Kushindwa kwako, hakutegemeani na nguvu yoyote ulivyonayo isipokuwa ufahamu wako. Kuanguka kwako hakutegemei maadui wengi ulionao, isipokuwa aina ya mtazamo ulionao. Kurudi nyuma kwako hakutegemei historia yoyote uliyowahi kuwa nayo, isipokuwa namna unavyoendekeza mawazo yako ya kushindwa.
Naelewa kwamba panahitaji mjadala wa kina kuhusu kipi kinachomtawala mwenzie: mawazo yetu ndiyo yanayotuongoza ama ni sisi ndio tunayaongoza mawazo. Hapo inapidi tushukie penye uelewa na namna mawazo yetu yanavyojengeka vichwani mwetu.
Kwa haraka haraka, nadhani, tuwaza vile tulivyoviingiza ubongoni iwe kwa hiari yetu wenyewe ama pasipo hiari hiyo. Kwa maneno mengine sisi ndio watawala wa mawazo yetu. 

Hiyo ni kusema kwamba unavyojiona, ndivyo ulivyo. Ukijidharau, hakuna mtu atakuja kukufanyia kazi ya kukuonyesha thamani uliyonayo. Ukianza leo kujiona masikini, ni wazi kuwa akili yako itakubaliana nawe na kusema kweli, utakuwa umeukaribisha umasikini wako kwa mikono yako miwili.
Ningependa kukuachia ujumbe huu mfupi na makini kwako utambue kuwa katika kila unalojaribu kulifanya, dhania kwamba haiwezekaniki jambo hilo likashindwa kwa namna yoyote. Kwa sababu, haiwezekani ukashindwa katika jambo lolote, isipokuwa kama utakubali akilini mwako kwamba umeshindwa.
Achana na mawazo ya kushindwa shindwa. Achana na watu ambao hawaishiwi stori za ubaya ubaya. Amua kuyaelekeza mawazo yako kwenye mafanikio. Kwa sababu mawazo yako ndiyo nguvu yako kuu uliyonayo! Itumie nguvu hiyo! Ikusaidie kufanikiwa zaidi.
Lakini pale utakapoweza kujiona huwezi na umeshindwa kutumia nguvu hiyo basi huo ndiyo utakuwa mwisho wa mafanikio yako wewe mwenyewe. Ni muhimu kulijua hili na kutumia nguvu hizi kikamilifu kwa ajili ya mafanikio zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
MAKALA HII IMEANDIKWA NA CHRISTIAN BWAYA WA JIELEWE BLOG


Huyu Ndiye Mtu Pekee Anayekufanya Ushindwe Katika Maisha Yako.

No comments :
Habari za siku ya leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Ni matarajio yetu ya kuwa umzima wa afya na karibu sana katika siku nyingie ambapo unapata nafasi ya kujifunza mambo muhimu ya kimafanikio. Katika makala ya leo tutaangalia jambo muhimu la kujifunza kupitia simulizi liliyotolewa na mwandishi nguli wa vitabu John Mason.
Katika kitabu chake cha ‘Limitation is Imitation’ mwandishi huyu anaelezea hadithi ya kijana mmoja ambaye siku moja aliweza kutoka na baba yake na kwenda kutalii katika eneo moja la mlimani ambapo wote kwa pamoja waliweza kupata nafasi ya kupanda juu ya mlima huo.
Wakiwa juu ya mlima ule kijana yule mdogo pengine kutokana na uchovu ilifika mahali alitaka kudondoka yaani nikiwa na maana aliteleza na kutaka kuanguka chini. Kutokana na hofu hiyo ya kutaka kudondoka chini kijana yule alijikuta akipiga kelele  ‘Yaaaa! Yaaaa!’. Kwa mshangao tena, kutokana na kelele hizo alizozipiga alishangaa tena kelele hizo hizo za kwake zinasikika upande mwingine.
Kijana yule kitu hicho kilimshangaza sana na kujikuta akimuuliza baba yake nini hicho alichokisikia ambacho kilitoa sauti kama yake. Lakini kabla hajajibiwa na baba yake swali lake, kijana huyu alishangaa tena maongezi hayohayo anayomuulizia baba yake yanasikika upande wa pili tena. Hali hiyo ilizidi kumtia hofu zaidi na wasiwasi mwingi na kuwa na kulikoni nyingi kwenye kichwa chake.
Baba yake baada ya kuona hivyo aliamua kumwambia mtoto wake kuwa kitu hicho anachokisikia kinafahamika kama mwangwi na kisha akamfafanuliwa jinsi inavyokuwa na kwa sababu gani huo mwangwi huo unatokea na kisha mwisho kabisa akasisitiza kwa kijana wake kuwa hivyo ndivyo maisha yetu huwa yako hivyo kama mwangwi.

Kijana alistaajabu na kushangaa, lakini aliambiwa na baba yake huo ndiyo ukweli anaotakiwa aujue kuwa maisha  yetu yanakuwa kama mwangwi ama sauti inayojirudiarudia kwa sababu yanatupa kila kitu kama tulivyokitoa. Kama utatoa upendo jiandae kupokea upendo, kama huwa unatoa mafanikio na kufanya kila kinachoendana na mafanikio jiandae kupokea mafanikio pia katika maisha yako. Kwa tafsiri hiyo maisha yako ni mrejesho wa vitendo vyetu tunavyovifanya katika maishayetu.
Maisha uliyonayo siyo ajali kama unavyofikiria, ni matokeo ya mrejesho wa yale mambo unayoyafanya. Jaribu kuangalia na kujichunguza kidogo utagundua ukweli wa hilo kuwa unavuna ulichokipanda huo ndiyo mrejesho ninao taka kukwambia. Hivyo kama unajiona maisha yako ni mabaya acha kulaumu watu wengine, mtu wa kwanza kumlaumu ni wewe mwenyewe kwani huyu ndiye mtu pekee anayekufanya ushindwe katika maisha yako.
Kuna wakati pia mwandishi  Stewart Johnson aliwahi kusema kuwa kitu kikubwa katika maisha yetu ni siyo kushindana na wengine ni bali kushindana sisi wenyewe na kuwa bora zaidi na zaidi siku hadi siku, hili ndilo jukumu na lengo kubwa ambalo tunatakiwa tuwe nalo katika maisha yetu. Na huu ndiyo ukweli usiopingika unaotakiwa uujue ili kuboresha maisha yako.
Katika maisha yako kama unataka mafanikio zaidi jifunze kutambua kwamba maisha yako ni kama mwangwi. Ukishajua hilo lipia gharama za mafanikio hayo kwa kufanya vitendo ambavyo vitakufanya lazima ufanikiwe. Acha kujidanganya wewe mwenyewe na kuamini kuwa yupo ‘mchawi’ anayeweza kukwamisha mipango na malengo yako.
Hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kukuharibia maisha yako ni wewe mwenyewe kutokana na vitendo vyako. Jifunze sasa kutokuwaangalia wengine kama chanzo cha matatizo yako, badala yake anza kujiangalia wewe kwanza kuwa ndiye unayesababisha ushindwe kufanikiwa. Hakuna mtu anayekufanya ushindwe zaidi ya wewe mwenyewe kujiaminisha kuwa huwezi na unajikuta umeshindwa kweli.
Kumbuka siku zote maisha yako yapo hivo kutokana na mambo yale uliyoyapanda, ama uliyoyatoa. Hakuna kujuta wala kulalamika kwa kuwa tunapata vitu vinavyotokana na sisi wenyewe ni matokeo ya matendo yetu ambayo tunayafanya mara kwa mara na kila siku. Hivyo ni rahisi kusema kuwa katika maisha yetu tunavuna kile tulichokipanda na siyo vinginevyo.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kwa kujifunza na kuelimika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,