google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Oct 3, 2019

Fedha Hutupa Furaha Tunapokuwa ‘Vijogoo’ Tu.

No comments :
Je, kuwa au kupata fedha nyingi ndiko kunakoweza kumfanya mtu awe na furaha ya kweli? Hili ni swali ambalo huenda kwa sasa, idadi ya watakaojibu kwa ndiyo, inaweza kuwa ya chini kuliko miaka kadhaa iliyopita.
 
Kwa kiasi fulani, watu wanaoamini kwamba, fedha ni kila kitu imepungua. Sababu ni nyingi, lakini ugunduzi wa matumizi ya akili ya kawaida umekuwa ukijitokeza siku hadi siku. Nchi zilizoendelea kwa fedha, watu wake wamekuwa wakiingia kwenye kukosa furaha kwa mapana makubwa zaidi.

Wamerekani, wajapani, waingereza na wengine wamekuwa wakisongeka na kujiua na kukata tamaa, zaidi kuliko muda mwingine wowote huko nyuma, kwa sababu ya pesa tu. 

Watafiti wamebaini hivi karibuni kwamba, fedha huweza kuongeza furaha kwa aliyenazo kama yeye ndiye ‘kijogoo’ kwenye eneo analoishi, ofisini au pale ambapo mtu huweza kubainishwa na wengine kuwa ndiyo ‘kijogoo’ kwa fedha nyingi kuliko wenzake. Lakini inayopatikana ni furaha kidogo na ya muda mfupi.
Wanasema, hapo suala siyo mtu ana kiasi gani, bali zaidi anamzidi nani. Kama mtu ana fedha, lakini akabaini kwamba, hapo mtaani kuna wanaomzidi, ni wazi hatafurahia kuwa na fedha hizo. Kwa nini hatafurahia?

Wamebaini watafiti hao kwamba, fedha huwa zina tatizo la kutafuta ushindi. Kama mtu hujui saikolojia ya fedha, ni dhahiri atajibainisha nazo. Akishafanya kosa hilo la kujibainisha nazo atataka au kujikuta akitaka awe ndiye mwenye nyingi zaidi. Katika kutafuta yeye awe ‘kijogoo’ ndipo furaha inapoondoka. Siku zote tunaposhindana maishani, furaha nayo hukimbia.

Furaha ya kweli kutoka kwenye fedha haiji kwa mtu kutaka kuwafikia wengine, hapana. Furaha ya kweli huja pale ambapo mtu yuko juu ya wengine na hao wengine wanajitahidi kupigana vikumbo kutaka kumfikia.

Kwa mfano, watafiti wamegundua kuwa, mtu analipwa au pato lake ni kiasi gani, siyo suala la maana sana, bali wenzake wanalipwa au pato lao ni kiasi gani, ndilo jambo la maana. Hii ina maana kwamba, kama mtu anapata 500,000 kwa mwezi na wenzake, wale wakaribu yake ambao ndiyo kipimo chake, wanapata kila mmoja kiasi kisichozidi 400,000, huyu mtu ni lazima atakuwa na furaha tu. Hata kama fedha hizo hazitoshi matumizi, ili mradi yeye ndiye mwenye kufukuzwa ili akutwe, atakuwa na furaha zaidi.

Umri unatajwa pia na wataalamu hawa. Wanasema, watu wakiwa kwenye umri unaolingana au kukaribiana, mwingine anapokuwa na fedha zaidi, hawa wanaomfukuza au wanaojilinganisha naye, hutaka kumpita, kukosa furaha zaidi, hata kama wana mamilioni zaidi.

Kwa hiyo, kinachowakosesha wengi furaha katika suala la pesa, siyo fedha yenyewe, hapana. Kinachowakosesha furaha ni kutaka kufika mahali ambapo wao ndiyo watakuwa kipimo cha juu cha wenye fedha zaidi. Bado hata hivyo furaha hiyo itakuwa siyo ya muda mrefu mwingine atakapoonesha dalili za kutaka kumfikia, kiwango cha furaha ni lazima kitapungua au kwisha. 

Kwa kuwa kila siku watu wanapitana kwa kipato, kutegemea furaha kupitia fedha ni upotezaji wa muda kwa sababu, furaha hiyo ni bandia sana na inakuwa siyo ya kudumu kwako.

Tunakutakia mafanikio mema endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

IMANI NGWANGWALU,



Oct 2, 2019

Hawa Ndio Watu Hatari Usiowajua, Wanaonyonya Nguvu Za Wengine.

3 comments :
Inaweza kuonekana kama ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu wanaonyonya nguvu za watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi anakufa bila kujua. Watu hawa hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine wakiwa ni watu wetu wa karibu sana, kama wazazi, wapenzi, watoto, jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi kunyonya nguvu zetu? Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda kweli.

Mtu anaweza kuuliza, inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo nguvu ni zipi? Kwa mfano, mimi ninapo kuwa nakukera kila siku, ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia, unaumia kihisia na kimwili. Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa athari kubwa kimwili na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi kukutokea umekerwa na mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu anayekukera unakuwa unajisikia vibaya.

Hebu pia tuchukue mfano wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa maringo, dharau, kulaumu bila kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na asiyejali kuhusu madhila ya wengine, ni wazi aliye chini  yake ataumia tu, kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye anaweza kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.

Ni vigumu kubaini mtu ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini na kuwabaini watu wa aina hiyo popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua nikuelekeze au kukutajia sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha wakiwa maganda matupu, huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha kufanya.

Hizi ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-

1. Kuna watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”

Hawa ni watu ambao muda wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku ambayo utakutana nao ukute wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia hali. Kila siku wao ni walalamikaji, wanaoamini kwamba, wanaonewa na kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au kukosoa tu, lakini bila kutoa pendekezo au kuonesha ni  njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia zipi zingetatua tatizo.

Wao wanaona kwamba, wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa. Hawa kwa kawaida hawana uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au walichobuni, hapana. Hata kama wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na mtu, watajikuta wakiingia kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze kujibu, kama basi watakuwa na uwezo wa kujibu.

Hawa ni wanyonya nguvu za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu wa aina hii anakujia na kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko au kukosoa kwake, huna budi kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye. Ni lazima ufanye hivyo, kwani akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu zako zote.


2. Kuna watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.

Hawa ni wanyonya nguvu pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi mtu anaweza kuamini kwamba ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni jambo dogo. Hawa wako maofisini na majumbani. Mtu anaumwa na mafua, lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa na kuacha kabisa wosia, kwamba anakufa.

Yeye mwenyewe huyu anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo, atapata huruma zaidi, ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali na kutaka kupima umuhimu wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza hata kusababisha hata wengine wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana kwenye maneno yao.

3. Kuna wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti

Hawa ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe  na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi nafasi. Mtu atazungumza yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa tatu mfululizo. Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza yeye. Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.

Hajali kama kuna mtu ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali, kama unamsikiliza unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha kutokujali. Kama ni nyumbani au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri aliomba kwako, yeye ndiye atakupa ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya kuzungumza katika kumshauri. Hawa ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.

4. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.

Kila wakati linapotoea jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya kulaumu ili wengine washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko wazi kabisa kwamba, hao anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa na kuona kwamba, anaowalaumu hawana tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.

Anaweza kuangalia mtu anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini atajaribu kwa kadiri awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala wakati mwingine hakihusiani moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’ lengo ni kumfanya mtu ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi nzuri ya sasa, anataka kukosoa ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa ni kuwapuuzia.

5. Kuna wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji ushauri.

Asubuhi atakuja kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni atakutafuta. Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni vizuri kumwonesha kwamba, unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati kumwonesha kwamba, huna jibu, siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu hujui. Ukikosa njia au jibu mara kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe jeuri au dharau ama kisirani.

6. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.

Badala ya kunyamaza, akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako na kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi kuwa mbaya’ bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka kuumiza hisia za mwingine.

Bila shaka umeshawahi kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa. Jitahidi wakati wote kuwa makini wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua namna ya kuwaondolea mbali kwenye maisha yako.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







                                                           

Oct 1, 2019

Kama Una Tabia Hizi, Mafanikio Kwako Yatabaki Kuwa Ndoto.

2 comments :
Adui wa kwanza wa mafanikio katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Wewe ndiye unayeamua,ufanikiwe au usifanikiwe. Ninaposema hivi nina maana kwamba ziko tabia ambazo ukiwa nazo unafanikiwa na zipo tabia  mbazo ukiwa nazo utaishia kuona wenzako wanafanikiwa wewe unabaki palepale.Tabia hizi ni adui mkubwa wa mafanikio yako. Kwa hiyo usianze kutafuta mchawi wa mafanikio yako,mchawi wa kwanza ni wewe. Wewe ndiye mwenye maamuzi ya mwisho juu ya maisha yako unataka yaweje.

Hizi ni tabia ambazo umekuwa nazo kwa muda mrefu na hutaki kuziachia. Kwa jinsi unavyoendelea kuwa nazo ndivyo ambapo unajikuta maisha yako yanazidi kuwa magumu na wakati huo huo mafanikio kwako yataishia kuwa ndoto ya saa sita mchana, ndoto ya alinacha na mara nyingi utajikuta ukiishi maisha ya wasiwasi huku ukiwa hauna uhuru katika maisha yako. Unapojifunza tabia hizi fanya mabadiliko, chukua hatua sahihi za kubadili maisha yako na utafanikiwa.

Hizi ndizo tabia ambazo ukiwa nazo, mafanikio kwako yataishia kuwa ndoto za mchana:-

1.Kutokuwa na malengo.
Ili mtu afanikiwe lazima awe na malengo. Malengo ndio chanzo cha mafanikio, mafanikio hayaji kwa bahatí mbaya. Watu wote waliofankiwa unaowafahamu na usiowafahamu walikuwa na malengo, wakayaweka katika vitendo na kufanikiwa. Kama wewe ni mwanafunzi weka lengo unataka kuwa nani baadaye, vinginevyo utaishia kusoma na kubaki huna kazi ya kufanya; unakuwa umepoteza muda bure katika maisha yako.

Kama wewe ni mfanyabiashara weka lengo la kuwa mfanyabiashara mkubwa. Zingatia kwamba malengo ndiyo yanakupa dira na muelekeo katika maisha yako. Kupitia malengo unajua unatakiwa uanzie wapi na uishie wapi kulingana na lengo ulilojiwekea kwa wakati huo. Kutokuwa na malengo katika maisha ni sawa sawa na kusafiri bila kujua unaenda wapi. Hii ni hatari sana kwako.



2 .Kutokuwa na malengo  maalum yanayoeleweka.
Kuwa na malengo haitoshi, ni lazima uwe na malengo yanayoeleweka na kufikika. Ni kosa Kubwa kuwa na malengo mengi Ambayo hayafikiki na kutaka kuyatekeleza kwa wakati mmoja. Kuwa na malengo mengi  humfanya mtu achanganyikiwe. Mtu mwenye malengo mengi ana hatari ya; Kuchanganyikiwa na kushindwa kuamua aanze na lipi, amalize na lipi,pia ana hatari ya kutekeleza mambo nusunusu na hatimaye kushindwa kuendelea kabisa na mipango hiyo.

Weka malengo machache ambayo una uwezo wa kuyatekeleza kwa muda uliopanga kisha anza kutekeleza mpango mmoja hadi mwingine. Ukishafanikiwa kutekeleza mipango hiyo weka lengo lingine na utazidi kupiga hatua moja hadi nyingine na kuzidi kufanikiwa siku hadi siku.

3. Kukosa uvumilivu.
Mafanikio ni safari ndefu sana katika maisha ya binadamu. Mafanikio ya kweli yanachukua muda mrefu kupatikana, hayachukui muda mfupi kama wengi tunavyotaka. Kutaka mafanikio kwa muda mfupi ni tatizo ambalo limetukumba wengi katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Watu wengi tunaiogopa safari ndefu ya mafanikio, tunataka mafanikio ya muda mfupi.

WatuWengi wanakata tamaa mapema kwa kwa sababu wanataka mafanikio kwa mnuda mfupi jambo ambalo haliwezekani. Matokeo yake wanaamua kupita njia za mkato ili kufikia malengo wanayojiwekea. Usiogope kuchukua muda mrefu hadi kufanikiwa,hayo ndiyo mafanikio ya kweli. Ikiwa unataka kufikia mafanikio, usiogope kupita jangwani.


 4. Kukosa nidhamu.
Nidhamu ndicho chanzo cha mafanikio. Ukitaka kufanikiwa ni lazima ujitambue wewe ni nani una lengo gani na unapaswa kufanya nini ili kufanikisha lengo lako. Si hivyo tu unapaswa kuwa na mipaka katika utendaji wako. Unapaswa kujua lipi la kufanya na lipi si la kufanya, LAZIMA UWE NA NIDHAMU. Nidhamu ni uwezo wa kujitawala na kujizuia, kujiwekea  mipaka ya utendaji wewe mwenyewe bila kusimamiwa.
Unaweza kuiga na kufanya karibú kila kitu unachokiona na kukisikia, lakini si lazima uige na kufanya, mambo mengine siyo ya kuiga. Jiheshimu mwenyewe, pia  heshimu na kazi yako.Usiache kazi na  kufanya mambo mengine yasiyo ya msingi ambayo hayakusaidii kufikia lengo lako.

5. Kukosa shukurani.
Hakuna mtu anayefanikiwa katika maisha yake kwa juhudi zake mwenyewe bila kuwategemea wengine kwa namana yeyote ile, hayupo dunia hii. Tambua mchango wa wengine katika mafanikio yako. Kuna njia  nyingi za kuonyesha kwamba unatambua mchango wa jamii inayokuzunguka katika mafanikio yako. Baadhi ya mashirika na taasisi huamua kuchangia huduma za jamii kama elimu na afya kwa kutoa vitendea kazi kwa shule au hospitali.

Baadhi ya watu huamua kuwasaidia wengine katika shughuli zao   kiuchumi. Yapomambo mengi unayoweza kufanya ili kuonyesha kwamba unatambua mchango wa wengine katika mafanikio yako. Si vyema kutokufanya jambo kwa ajili ya wengine ikiwa wapo ambao walifanya kitu fulani na wengine wanaendelea kufanya kwa ajili ya mafanikio yako. Kwa hakika kuna watu wamefanya kitu fulani kuchangia mafanikio yako, wewe unafanya nini kwa ajili ya wengine?

6. Kuwa na hofu sana.
Watu  wengi huwa wanaogopa kujaribu kufanya kazi fulani kwa sababu watachekwa au kujishushia hadhi mbele ya jamii. Baadhi ya watu wanaogopa kujaribu  kwa sababu wakishindwa watachekwa na kujisikia vibaya. Wengine wanaogopa kupoteza fedha baada ya kupata hasara. Ni bora kujaribu ukashindwa kuliko kutokujaribu    kabisa. Mafanikio huja kwa kujaribu na kushindwa bila kukata tamaa. Katika ugunduzi wa gropu,Thomas Edison alishindwa zaidi ya mara elfu moja, hatimaye alifanikiwa mpaka leo hii tunasimulia habarí zake na kujifunza kutoka kwake.

Thomas Edison anasema,Udhaifu wetu mkubwa upo kwenye kukata tamaa. Njia ya hakika ya kuweza kufanikiwa ni kujaribu mara nyingine  tena. Kupata matokeo Ambayo hukuyatarajia na huyataki katika jambo ulilolifanya, haina maana kwamba matokeo hayo hayana faida.Wakati umejaribu njia zote na kushindwa, kumbuka hili-HUJASHINDWA. Kumbuka, kujaribu na kushindwa ni sehemu ya mafanikio.


Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku, karibu sana.

  • Makala hii imeandikwa na DEOGRATIUS GUNJU WA MBEYA TANZANIA
  • Mawasiliano 0718 610022