google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Feb 28, 2017

Jenga Mafanikio Makubwa,.. Kwa Kupanda Mbegu Ya Mafanikio Yako Kila Siku.

No comments :
Inawezekana upo kwenye wakati mgumu sana kimaisha ukiwa huna pesa, mipango yako inakwenda hovyo na huna uhakika hata hiyo kesho yako itakuwa vipi yaani ni kipi utakula na kipi utavaa.
Kila njia unayowaza kwamba inaweza kukuingizia kipato bado unaona pia nayo kama vile haikusaidii sana. Ukiangalia kila mlango unaoufahamu wewe wa kukupa pesa kama haupo na hata wale wateja wako umewapoteza.
Hali kama hizi ni hali ambazo zinamkuta karibu kila mtu duniani. Kuna mahali katika maisha yako ni lazima itafika utajikuta upo njia panda kwa sababu ya mambo yako kwenda hovyo hovyo.

Inapotokea hali kama hiyo mifuko imechacha yaani huna mapesa, kitu kikubwa cha kufanya badala ya kusikitika, anza kupanda upya mbegu ya mafanikio yako tena. Ni wakati wa kuhakikisha unapanda mafanikio yako ili kesho uvune.
Kwa jinsi utakavyozidi kupanda mbegu nyingi za mafanikio leo ndivyo utajikuta unavuna sana kesho. Kama unalalamikia leo maisha yako ni magumu, hebu jiulize ulipanda nini unachotaka kuvuna leo.
Tukiangalia hakuna ulichokipanda. Kama hukupanda kitu, kaa kimya anza kuweka mikakati na mipango yako upya ya kimaisha itakayokupa mafanikio makubwa kesho. Kila kitu kinawezekana ukiamua.

Weka mipango, mikakati yako vizuri leo ili kesho yako iwe ya mafanikio makubwa na tabasamu. Tumia uwezo wako wote ulionao mpaka kufanikiwa. Ili usitumie njia ya mkato ya kung’ang’aniza kuvunja yai ili utoe kifaranga, nenda kwa taratibu na UTAFANIKIWA. Usivunje kanuni.

Feb 27, 2017

Malezi; Watoto Wasitumike Kama ‘Risasi’ Za Kushambuliana Sisi Wenyewe.

No comments :
Mfumo dume umekuwa na mwelekeo wa kuchochoea utoaji wa talaka kwa wana ndoa kirahisi sana. Utakuta wanaume huamua kuwapa talaka wake zao hata kwa makosa madogo madogo tu.
Na wanapofanya hivyo huhakikisha kuwa akina mama hao hawaondoki na kila kitu. Mara nyingi wamekuwa wakiondoka bila chochote, msaada wowote na hata bila watoto wao.
Wengi wetu tumekuwa hatushituki, tunapowaona wanandoa ambao walikuwa wakipendana wakipeana talaka. Na vile vile tukiwawekea utaratibu wa kuwasaidia wanandoa wanao achana, ili waweze kupona kihisia na kiakili.
Lakini, jambo la kukumbuka ni kwamba, unapompa talaka mwenzako, maana yake unamkana na kuondoa msamaha wako, upendo wako, na uaminifu wako kutoka kwake.

Pia, kuishi maisha ya useja ni jambo lililogumu hata zaidi. Iwapo wewe bado ni kijana na damu yako inachemka, kuishi maisha ya peke yako kunakufanya ukose usalama, uwe na hofu ya kukufanya upate maradhi yatokanayo na hisia. Lakini, pia upweke na kadhia zingine nyingine huwezi kuvikwepa.
Ni kweli kuwa, ndoa ni jambo jema na linalokubalika na jamii. Lakini iwapo ndoa itakuwa na matatizo au migogoro, wanandoa watapaswa wafanye nini? Ukweli ni kwamba, ni lazima pawepo na mlango wa nyuma wa kutokea. Tunapaswa tukumbuke kwamba, tunapoona kuna kitu kinachoitwa talaka, tujue tunapoelekea si pazuri.
Kuufahamu ukweli huu kutakusaidia tuepukana na matatizo, sisi na watoto wetu. Ingawa lengo si kutalakiana, lakini dunia yetu hii ni kubwa, na lolote lile linaweza kutokea.
Vilevile ukweli ni kwamba, wanandoa wanapotalikiana huendelea kubaki na maumivu au mateso kwa miaka mingine ipatayo kumi. Hali huwa mbaya zaidi kwa watoto.
Kwa mujibu wa kitabu kiitwacho Second chances kilichotungwa na kuandikwa na Sandra Blakeslee na Judith Wallerstein, ambao walifanya utafiti wa muda mrefu unaohusu madhara yanaotokana na talaka.
Katika utafiti wao wanasema kwamba, hata kama talaka itatolewa katika njia halali na ya haki, bado huo ni udanganyifu wa kihisia tu, kwani madhara yake huendelea kuwepo.
Pia wanasema kwamba, talaka ndiyo sehemu pekee katika maisha ambayo watoto hutumika kama risasi za kushambuliana sisi wenyewe, yaani mke na mume. Talaka ina maumivu makali kushinda matatizo  ambayo inajaribu kuyatatua.
Hata hivyo, jambo la kukumbuka ni kuwa, ndoa siyo kamilifu kwa sababu inaundwa na binadamu wasiokuwa wakamilifu. Licha ya ukweli huo, bado uwezekano upo kuboresha zetu. Na tutaweza kufanya hivyo, iwapo tutakuwa na uelewa wa kutosha unaohusu ndoa.
Ni Baraka ya aina yake ikiwa utaamua kusali na kujiandaa kwa ajili ya ndoa yako. Bila shaka kuna matatizo mbalimbali kwenye ndoa. Lakini iwapo kila mwanandoa atakubali kuwajibika kikamilifu, ndoa inaweza kuboreka kila mwaka, na kisha kuleta furaha, kuongeza na kukuza urafiki wa wanandoa.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Tunakutakia kila la kheri,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,


Feb 24, 2017

Linda Muda Na Mafanikio Yako Kwa Kusema HAPANA.

No comments :
Moja ya jambo muhimu unalotakiwa kulifanya ili kuweza kufanikiwa  ni kule kujenga uwezo wa kusema HAPANA hasa kwa mambo ambayo hayaendani kabisa na malengo ya maisha yako.
Wengi wetu mara nyingi ni watu wa kukubali karibu kila kitu katika maisha yetu, hasa pale tunapoambiwa na wengine kwamba tufanye kitu cha aina fulani. Huwa si watu wenye uwezo wa kusema hapana.
Kwa kawaida unaposhindwa kusema hapana kwa yale mambo ambayo hayaendani na malengo yako, unakuwa ni mtu kama ambaye unapoteza muda sana.
Sasa basi, kama usipoweza kusema hapana, ujue kabisa utapotezewa sana muda wako na watu wengi ambao watakuwa wanataka ufanye mambo yao. Hivyo, utake usitake hapa ndipo unalazimika kujifunza kusema HAPANA. 

Jifunze kusema hapana ujenge mafanikio yako.
Kila wakati linda muda na mafanikio yako kwa kusema HAPANA. Kama usipoweza kusema utapoteza muda wako na hata mafanikio yako kwa ujumla na hilo litakuwa halina ubishi.
Ili uweze kufanikiwa katika hili, zipo HAPANA kubwa za aina tatu ambazo unatakiwa uzijue na kuzizingatia  ili uweze kupata mafanikio.
Sema hapana kwako wewe mwenyewe.
Watu wasio na mafanikio ni wazito sana kusema hapana kwa mambo ambayo hayawasaidii. Angalia mambo unayoyafanya yanakusaidia kufanikiwa au la. Kama mambo hayo hayakusaidii kufanikiwa, sema hapana tena ya herefi kubwa.
Kwa mfano kama kuna jambo unataka kulifanya leo, halafu unajisikia uvivu uvivu unataka kulifanya kwa wakati mwingine, sema hapana nitafanya leo leo. Usikubali kitu chochote kikukwamishe katika hili, sema hapana.
Sema hapana kwa watu wengine.
Acha kuona aibu kama kuna jambo ambalo unaambiwa na huliwezi, sema hapana kwa jambo hilo. Jiulize ukimkubalia kila mtu kitu anachotaka kwako itakuwaje? Nafikiri utakuwa kama mtumwa wao.
Angalia hata matajiri wakubwa hawakubali kila kitu. Sema hapana kwa wengine pia. Mwanzo linaweza likawa zoezi gumu kidogo kwako lakini siku zinavyozidi kwenda utazoea na utamudu.
Sema hapana kwa dunia.
Ili uweze kufanikiwa unatakiwa uyajue makusudi yako vizuri yaliyokuleta duniani. Ukishajua hivyo, kataa kitu chochote ambacho unaona hakiendani na malengo yako hata kiwe kizuri sana.
Hapa inabidi ujue kusema hapana hata kwa fursa zote ambazo zipo nje ya makusudi yako. Ng’ang’ania kitu kile ambacho umekusudia kukifanya, acha kuyumbishwa na mtu au kitu.
Hivyo ndivyo unavyoweza kujifunza kusema hapana na kujenga misingi imara ya maisha unayotaka.
Badili maisha yako kwa kuwa na fikra sahihi, endelea kujifunza kupitia mtandao wako bora wa dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Chukua hatua na kila la kheri,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,


Feb 23, 2017

Kama Unabomoa Misingi Hii…Hutaweza Kufanikiwa Tena.

No comments :
Tumia kile ulichonacho kwa uhakika na vizuri kabisa. Acha kujidanganya kwamba unataka mafanikio makubwa wakati hata ile misingi ya kutengeneza mafanikio makubwa unaiharibu hovyo hovyo.
Haiwezekani eti unasema unataka mafanikio makubwa wakati unatumia muda, pesa na nguvu zako hovyo, ambapo vitu hivyo kwa pamoja vingekusaidia kufikia mafanikio makubwa kama ungevitumia vizuri na kwa busara.
Hata Pesa unazozipata hazijiamulii zenyewe kwamba ‘sasa mimi pesa ninakwenda kununua kitu hiki au kile.’ Wewe ndiye mwenye jukumu la kupanga pesa zako zitumike wapi na kwa sababu ipi.
Sasa kama hiyo iko hivyo, kwa nini unafanya maamuzi mabovu ambayo yanakupotezea pesa nyingi na kwa kiasi kikubwa? Kuwa makini sana na matendo yako ili yasikupotezee pesa ambayo ni moja rasilimali muhimu kukusaidia kufanikiwa.
Hapo ulipo najua una pesa za kiasi fulani hata kama ni ndogo, najua una muda na nguvu fulani, sasa kwa nini hivi vitu usivitumie kwa uangalifu ili viweze kukusaidia kukupa mafanikio makubwa na badala ya kuvipoteza tu kiholela.

Tumia kidogo ulichonacho, ili kufanikiwa.
Watu matajiri, wanajua namna ya kutunza pesa zao vizuri, kwa nini wewe usiwe miongoni mwao? Huna pesa za kutosha si kwa sababu pesa zinakukimbia bali ni kutokana na matendo yako yanayofukuza pesa.
Kitu cha kufanya jiulize, ni hatua zipi utaweza kuzichukua ili kuweza kulinda hata zile rasilimali zako za kukusaidia kufanikiwa ambazo ni pesa, muda na nguvu zako. Kama hujui tafuta watu wenye mafanikio kisha wafatilie na ujue nini cha kufanya.
Lakini kitu ambacho nataka uelewe hapa jifunze sana kutumia kile kidogo ulichonacho kikusaidie kufanikiwa. Najua unaelewa wapo watu ambao wanadharau sana hasa ikiwa wanacho kile kidogo.
Watu hawa mara nyingi hawajui thamani ya kutumia kile kidogo walichonacho. Iwe ni pesa kidogo watazitumia hovyo mpaka zitakwisha. Iwe ni muda kidogo pia watautumia hovyo hata bila kupata faida ya muda huo.
Kwa kuwa wewe umeshalijua hili leo, amua kutumia kiasi kidogo cha pesa ulichonacho kwa busara ili kikusaidie kutengeneza pesa nyingi. Pia amua kutumia muda, nguvu zako au chochote ulichonacho ambacho unaona ni kidogo kikusaidie kufanikiwa.
Hata Musa wakati anawaongoza wana wa Israeli kuvuka bahari ya shamu, alitumia fimbo aliyonayo kupiga bahari na ikagawanyika, hapo ndipo wana wa Israeli wakaokolewa.
Leo hii ni kipi ambacho huna. Najua una kidogo ulichonacho ila hujaona sana kama kinaweza kukusaidia. Sasa hebu anza leo kukiangalia kwa jicho la tofauti ili kikusaidie kujenga mafanikio makubwa.
Kabla sijaweka kalamu yangu chini pengine nikwambie hivi, kama unabomoa misingi hii ya kushindwa kutumia kile angalau kidogo ulichonacho kwa busara na vizuri…kufanikiwa kwako itabaki kuwa hadithi.
Hiyo iko hivyo kwa sababu, mafanikio yanajengwa na vitu vidogo vidogo sana ambavyo mwanzo huonekana si kitu wala si chochote, lakini vitu hivyo ndivyo hatimaye vinavyofanya mafanikio yakaonekana kwa nje.
Sasa wewe ni nani hadi ufanikiwe wakati unajiona kabisa unavunja sheria za asili za mafanikio? Huwezi kufanikiwa. Ila kikubwa utakachofanya ni kujidanganya tu kwamba ipo siku lazima nitafanikiwa.
Mpaka hapo ulipo jiulize je, hicho ulichonacho unakitumia kwa vizuri ili kikusaidie kupata kingine kikubwa? Lakini ikiwa unataka kufika katika ngazi fulani ya mafanikio, huku hapo ulipo hujiwekei misingi imara hutaweza kufika huko.
Kila wakati jitathimi katika kila eneo unalotaka kufika kwa kujiuliza je, kile kidogo ulichonacho unakitumia ili kukusaidie kufanikiwa? Ukiweza kupangilia vizuri matumizi ya kidogo ulichonacho na kuhakikishia UTAFANIKIWA.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

Feb 22, 2017

Maeneo Unayotakiwa Kuwajibika Sana Ili Kujenga Mafanikio Makubwa.

No comments :
Kati ya kitu ambacho unatakiwa uelewe katika safari yako ya mafanikio ni kwamba, mafanikio yoyote unayoyatafuta yanaanza na wewe. Hiyo ikiwa na maana, hakuna mtu mwenye hamasa kubwa ya kufikia  mafanikio yako zaidi ya wewe.
Kwa hivyo, hiyo inatuonyesha kwamba ili ufanikiwe, unatakiwa kuwajibika katika maisha yako kwa nguvu zote na kwa asilimia zote. Ikiwa hutafanya hivyo utajiangusha mwenyewe, maana hutaweza kufanikiwa.
Kupitia makala haya nataka nikupe dondoo za kukusaidia kujua maeneo ambayo unatakiwa uwajibike kwa uhakika ili upate mafanikio unayoyahitaji. Bila kupoteza muda tufuatane pamoja katika makala haya kujifunza;-
1. Wajibika kufanya maamuzi sahihi.
Kabla hujafanya kitu chochote ni lazima ufanye maamuzi. Na kufanya maamuzi ya kuweza kubadili maisha yako kuna wakati huonekana ni kitu kigumu sana.
Lakini hakuna namna nyingine zaidi ya kujua unatakiwa ufanye maamuzi yatakayobadilisha maisha yako. Pia  inatakiwa ujue bila kufanya maamuzi bora ya kukufanikisha itafika mahali utakwama.

Wajibika katika kila eneo la maisha yako kwa ukamilifu.
2. Wajibika kuweka mipaka ya maisha yako.
Ikiwa unataka kufika kule unakotaka kufika kimafanikio lazima ujue jinsi ya kuweka mipaka kwenye maisha yako. usiruhusu maisha ako yaingiliwe na kila mtu anavyotaka. Weka mipaka maeneo muhimu.
Jifunze kuweka mipaka kwenye matumizi ya pesa zako, nguvu na hata muda wako pia. Usiogope kuweka mipaka yoyote ile, ni muhimu kufanya hivyo ili kupata mafanikio. Kama hutajiwekea mipaka itakusumbua sana kufanikiwa.
3. Wajibika kukabiliana na mabadiliko.
Tunaishi katika dunia inayobadiilika sana. Ili kuweza kwenda sawa na dunia hii inatakiwa ifike mahali ukakubali kuwajibika ili ikusaidie kwenda sambamba na mwendo kasi wa dunia.
Kama hutaweza kukabiliana na ushindani, elewa  kabisa utashindwa. Njia bora ya kuweza kukabiliana na ushindani ni kujifunza kila siku na kujua maisha yanataka nini kwa sasa.
4. Wajibika kuwa mkarimu.
Ni rahisi kufika ngazi ya juu kimafanikio ikiwa wewe mwenyewe utakuwa mkarimu. Unapokuwa mkarimu unajenga uaminifu mkubwa kwa watu na hiyo inakusaidia kushirikiana katika mambo mengi ikiwa pamoja na biashara.
Kiuhalisia hakuna mafanikio ambayo unaweza kuyapata kiurahisi kama ikiwa hutaweza kuwajibika katika hayo maeneo. Kila wakati hakikisha unawajibika vizuri katika maeneo hayo ili ujenge mafanikio makubwa na ya uhakika.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,


Feb 21, 2017

Hii Ndiyo Sababu Kwa Nini Utangaze Biashara Yako.

No comments :
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mbalimbali ambayo yanahusiana na masuala ya kibiashara. Na miongoni mwa maswali ambayo wamekuwa wakiniuliza ni kuhusu ni nini faida ya kutangaza biashara kwa sehemu kubwa?
Swali hili ndilo limenifanya nishike kalamu yangu ili niweze kulijibu. Nakusihi twende sambamba ili niweze kueleza kwa kinagaubaga, kwa nini unapaswa kuitangaza biashara yako tena kwa nguvu zote.
Matangazo ni usambazaji wa taarifa  sahihi  kuhusu bidhaa au huduma kutoka kwa mfanyabiashara kwenda kwa mteja. Matangazo ndiyo roho ya biashara, kwani bila kufanya biashara yako bila matangazo ni sawa na bure.

Itangaze biashara yako kujenga wateja wapya.
Nafikiri pia utakubaliana nami ya kuwa ili uweze kufanya biashara  yenye tija ni lazima uitangaze biashara yako, kwani " biashara ni matangazo".  Matangazo ndiyo yatakuyokufanya uweze kuongeza mauzo ya kibiashara kila wakati.
Kwa kuzingatia hilo unaweza kuitangaza biashara yako kwa njia ambayo itakuwa ni rahisi kwako. Na sababu kubwa ya kuitangaza biashara yako ni kuongeza wateja wapya.
Leo na dhumuni kubwa la kutangaza biashara yako ni kukutana na na watu wapya,  ukiona umetangaza biashara yako na hakuna mteja mpya hata mmoja ujue fika kuna mahala ambapo umekosea.
Hivyo fanya tathimni upya na ujipange upya na kuona ni jinsi gani unaweza kuitangaza biashara hiyo. Vile vile katika upangaji wa malengo ya kibiashara hakikisha ya kwamba unapanga na mbinu za kukutana na watu wapya kila siku.
Nasisitiza juu ya kukutana na watu wapya, kwa sababu nimegundua ya biashara nyingi zimekuwa hazifanyi vizuri kwa sababu zimekuwa na watu ambao wanaizunguka biashara ile ni wale wale kila siku. Hivyo kila siku fanya tathimini juu wateja wapya ambao wamekuja katika biashara yako.
Asante kwa kutembelea mtandao huu wa dira ya mafanikio,  usisite kumshirikisha na mwingine ili aweze kujifunza.
Ndimi afisa Mipango Benson Chonya,
0757909942.

Feb 20, 2017

Chanzo Cha Hofu Nyingi Ulizonazo Na Zinazokuzuia Ushindwe Kufanikiwa.

No comments :
Wapo watu ambao ni waoga sana kuwajibika hasa linapokuja suala la kufanya kile kitu wanachotakiwa kufanya. Utakuta ni watu wa kusingizia sana hiki au kile, kwamba siwezi kufanya kwa sasa, kwa sababu hii au ile.
Kwa mfano, utakuta mtu anataka kuanzisha biashara ya aina fulani, ambapo ukiangalia kama ataanzisha biashara hiyo, itamsaidia sana mtu huyo kuweza kuingiza kipato kikubwa na cha ziada.
Hata hivyo, kitu cha kushangaza au cha ajabu kwa sababu ya hofu ama wasiwasi tu, mtu huyo atajikuta anatoa visingizio vingi sana mpaka kushindwa kuanza biashara hiyo, ambayo ilitakiwa ainze mara moja.
Kitu usichokijua, kisaikolojia unaposhindwa kufanya jambo fulani kwa sababu ya hofu za mara kwa mara, mawazo yako ya ndani, mawazo yanayoumba au kupelekea mambo hutokea, huchukua hofu hiyo na kuihifadhi na kuifanya kama ‘ulemavu’ wako.
Kwa hiyo kila unapojaribu kufanya jambo jipya utakuta wazo linashuka haraka sana ndani yako, ‘Je ukishindwa itakuwaje? Si unaona wengi sana huwa wanashindwa hapo,’? Utashangaa ubongo wako una hofu sana, hata pengine bila kujua kwa nini?.
Lakini ukiangalia, hiyo yote inatokana na hofu ndogo ndogo ambazo ulizibeba sasa zimekaa kwenye mawazo yako ya kina na imekuwa kama ndio ‘ulemavu’ wako wa kiakili yaani 'psychological disorders', sasa kila kitu ukitaka kukifanya unakuwa una hofu.
Kitu cha kujiuliza kwa nini watu wanakuwa na hofu sana hasa pale wanapotaka kuanza jambo fulani? Chanzo hasa huwa nini?
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazopelekea hofu moja kwa moja kwenye maisha yako na kushindwa kuchukua hatua sahihi za majukumu yako.
1. Kuogopa kukosea.
Utakuta hapa hofu inazalishwa sana kwa sababu ya kuogopa kukosea. Utakuta mtu anakuwa ana wasi wasi mwingi hivi jambo hili lisipokwenda sawa itakuwaje? Mwisho wa siku kila kitu hufika mahali kimekwama.
Soma; Aina Nne Za Hofu Zinazokukwamisha Kufikia Malengo Yako.

Zishinde hofu zako, ili ujenge mafanikio makubwa.
2. Kuogopa kushindwa.
Pia kuna watu ambao wanajawa na hofu kwa sababu ya kuogopa kushindwa. Kwa watu kama hawa kwao wanaona inakuwa ni bora wasifanye kabisa kuliko wakafanya halafu wakashindwa. Kwa lugha rahisi watu wenye hofu hii huwa hawafanikiwi.
.3. Kutokujiamini.
Unaposhindwa kujiamini, elewa kabisa huwezi kufanikiwa katika kitu chochote. Kujiamani mara nyingi ndio msingi wa mafanikio. Waangalie watu ambao wanajiamini utakuta ni  watu ambao wanamafanikio wakati wasiojiamini hawana kitu maishani mwao.
4. Kuogopa ushindani.
Mwingine utakuta anashindwa kuanza jambo analotakiwa afanye, inaweza kuwa biashara au kitu chochote eti kisa kwa sababu ya kuogopa ushindani. Kwa jinsi anavyoogopa ushindani anajikuta hawezi tena kufanya kitu.
5. Kukosa hamasa.
Pia ni rahisi sana kuanza kuingiwa na hofu kama umekosa hamasa ya kile unachokifanya. Ni muhimu sana kuwa na hamasa ili ikusaidie kukujaza ujasiri wa kufanya hicho unachokifaya kwenye maisha yako.
6. Mawazo hasi.
Kama una mawazo sana kama vile ‘aah mimi sina uwezo wa kufanikisha hili, huu mradi sio saizi yangu,’ uwe na uhakika hutaweza kufanya kwa ujasiri, hapo utakuwa unajijaza hofu mwenyewe zitakazo kufanya ushindwe tu.
Kimsingi, kuogopa kushindwa, kuogopa ushindani, kugopa kukosea, kukosa hamasa, mawazo hasi na kutokujiamini ni moja ya sababu zinazokufanya wewe uwe na hofu kubwa kwenye maisha yako.
Chukua hatua na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,
dirayamafanikio.blogspot.com  

Feb 17, 2017

Chimbuko La Umaskini Kwa Waajiriwa Wengi Ni Hili Hapa.

No comments :
Umaskini ndani ya kundi la wasomi unazidi kuingia kwa kasi ya ajabu kadili siku zinavyozidi kwenda. Kundi la watu ambao wako kwenye hatari kubwa zaidi ni hasa wale walioko kwenye “ajira”. Ukweli ni kwamba watu wengi walioko kwenye ajira, kitu pekee wanachouza ili kupata kipato ni nguvukazi” tena ambayo bado ni “ghafi”.  

Uzoefu unaotokana na tafiti zilizofanywa, unathibitisha kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha waajiriwa na hasa wasomi wengi kuwa maskini. Lakini kubwa zaidi ni utamaduni wa wasomi kuendelea kuuza nguvukazi ikiwa bado ni “ghafi” (nguvukazi ambayo haijachakatwa).

Katika ulimwengu wa “uwekezaji” nguvu kazi ghafi ni mtaji muhimu sana, ambao ukichanganywa na mitaji mingine kama vile mashine, una uwezo wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye thamani kubwa kwa watu wengine.

Ukiuza nguvukazi ghafi unakuwa umeuza “mtaji” wako: Waajiriwa wengi wanaendelea kukumbwa na adha kubwa ya umasikini kutokana na kushindwa kutambua ukweli kwamba mara nyingi kwenye maisha ya ajira wamekuwa wakifanya zaidi biashara ya kuuza mtaji walionao (nguvukazi) kwa matajiri wenye hitaji la mitaji.


Ikumbukwe kuwa, ili uweze kuzalisha bidhaa na huduma unahitaji mitaji ya aina mbalimbali ikiwemo nguvu kazi ghafi. Ndiyo maana matajiri wengi wanapendelea zaidi kununua mitaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma, ambazo huwapatia faida kubwa sana. 

Katika biashara yoyote duniani, kuuza mtaji ni kufirisika jumla. Kwahiyo, umasikini tulionao umetokana na kuuza mtaji wetu kila siku tunapotumikia ajira zetu. Kwa maana nyingine waajiriwa wengi wanafirisika kila siku ya pale wanapokwenda kazini.

Watu wanaouza zaidi nguvu kazi ghafi wanabaki kuwa maskini kutokana na ukweli kwamba thamani ya nguvu kazi ghafi huwa ni ndogo sana, kwasababu inapatikana kwa wingi na haina usumbufu kuipata. 

Kwa mfano: ukijifanya kutoza bei kubwa nguvu kazi yako; waajiri wengi watakukimbia na chapuchapu watapata watu wengine wenye kuuza nguvu kazi ile ile kwa bei nafuu sana.

Hivi ndivyo unavyouza nguvu kazi ghafi: Unauza nguvu kazi ghafi pale unapotumia nguvu yako kufanyakazi ya kuzalisha bidhaa na huduma ambazo siyo mali yako bali ni mali ya mtu aliyekuajiri (mwajiri).
Unahitaji kufahamu kuwa, mwajiri amekuajiri ili umpatie (umuuzie) nguvu kazi ambayo ni mtaji wa kuzalisha bidhaa na huduma ambazo ni mali yake binafsi. 

Kwakuwa bidhaa zinazozalishwa ni za thamani kwa watu wengine, basi ni wazi kwamba watu hao watampatia pesa mwajiri wako ili kupata bidhaa; LAKINI hawatakupatia pesa wewe, kwasababu wewe unayo nguvu kazi peke yake, ambayo siyo hitaji muhimu kwa wateja wenye pesa zao. 

Ukiuza nguvukazi ghafi unauza “muda” wako: Kwakuwa umeajiriwa kwa madhumuni ya kutoa nguvu kazi kwa mwajiri wako, basi thamani yako inapimwa kwa kuangalia muda unaoutumia kufanya kazi.

Ili uweze kulipwa ni lazima kila siku ufike kazini na kusajiri muda wako. Usipoonekana kazini hakuna malipo yoyote, kwasababu muda wako utakuwa hujauwekeza kwa mwajiri. 

Kwahiyo, unapouza nguvu kazi ghafi basi ujue umeuza “muda” na binadamu wa kawaida hawezi kufanya kazi zaidi ya masaa nane kwa siku. Masaa yote haya unafanya kazi bila kupumzika na kuzalisha vitu vyenye thamani kubwa kuliko mshahara unaolipwa na mwajiri wako. 

Haijalishi, thamani ya vitu vilivyozalishwa ni kubwa kiasi gani, mshahara wako unaolipwa unaendelea kubaki pale pale kila mwezi. Hali hii ndiyo inakufanya wewe mwajiriwa kukosa muda wa kufanya vitu vyenye kukuletea faida kubwa na mafanikio maishani, na hivyo kuzidi kuwa maskini kadiri umri wako unavyoongezeka.

Ukiuza nguvukazi ghafi huna cha kurithisha familia yako: Kama unauza nguvukazi ghafi siyo rahisi kuirithisha kwa watu wako wa karibu, kwasababu nguvukazi kama ilivyo haihamishiki kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama kitu hakihamishiki ni vigumu pia kukibadilisha kwa urahisi kuwa pesa.

Hali hii inazidi kutukumba wasomi na waajiriwa waliowengi kutokana na ukweli kwamba unakuta umeajiriwa kwenye kampuni kubwa na una cheo kikubwa lakini ukifukuzwa au kufariki, haitokei mke au mtoto wako akapewa nafasi kama uliyokuwa nayo na wala familia haiwezi kutumia vyeti vyako vya elimu kuomba kazi.

Lakini kama ungekuwa kwa mfano umeandika vitabu, hata ukifa hakimiliki ya kuendelea kuvichapisha na kuviuza inahamishiwa kwa warithi wako na wanaendelea kufaidi sawa na wewe ulivyokuwa ukifaidi.

Ukiuza nguvukazi ghafi unapata hasara: Hasara kubwa unayoipata kutokana na kuuza nguvu kazi ni pale unapoishia kuuza kitu kimoja tu! Nacho ni nguvu kazi.

Hali hii inakubana kiasi kwamba unajikuta unalazimika kumtegemea mteja mmoja ambaye ni “mwajiri” na inakuwa siyo rahisi kubadilisha mteja kadiri unavyotaka.

Endapo ukiamua kuchakata nguvukazi yako na hatimaye kuzalisha bidhaa na huduma za thamani ni rahisi kupata wateja wengi, ambao ndio huleta mapato makubwa.

Hasara nyingine unayopata pindi unapouza nguvu kazi ghafi ni kuendelea kubaki kwenye kundi la watu maskini ambao wanapata kipato hai (active income), yaani unapata pesa unapofanya kazi tu, ukiacha pesa hakuna. Endapo, ikitokea unaumwa au umesafiri basi ujue hakuna pesa itakayoingia.

Ndiyo maana unakuta mtu ni tajiri leo kwasababu anafanya kazi ya kibarua, lakini baada ya muda mfupi unakuta ni maskini na kwa waajiriwa ni hivyo hivyo wanakuwa na pesa wakiwa bado kazini LAKINI wanapostaafu ajira wanarudia kwenye hali ya umaskini jambo ambalo huwafanya watu wengi kufa miaka michache baada ya kustaafu.

Washindi dhidi ya umaskini ni wale walioamua kuchakata nguvu kazi yao: Ukweli ni kwamba kila mchakato wowote lazima utoe matokeo. Matokeo ya kuchakata nguvu kazi ghafi ni “bidhaa au huduma” zenye thamani kubwa kwa watu wengine.

Kitendo cha kuchakata nguvu kazi kinatokana na matumizi ya nguvu ya akiri pamoja na nguvu ya mwili kwenye rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k, kwa lengo la kupata mali au bidhaa kwaajili ya watu wengine. 

Ukishapata bidhaa zenye thamani (manufaa) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa ili kujipatia bidhaa na huduma muhimu kutoka kwako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi na zenye thamani kubwa ndivyo utakavyopata pesa nyingi ambayo haina kikomo. 

Ni wakati sasa tuamke na tujibidishe sana kwa kuandaa mazingira yatakayotuwezesha hasa sisi wataka mafanikio kuuza “matokeo” ya nguvu kazi badala ya utamaduni wa sasa wa kuuza nguvu kazi ghafi.

Ukweli ni kwamba, unapokuwa mtu wa kuuza matokeo ya nguvu kazi ambayo ni bidhaa na huduma mbalimbali, tayari unakuwa umemaliza kazi, kinachofuatia ni kuendelea kuuza bidhaa hizo na wakati huo huo unakwenda kuwekeza muda wako huo kwenye kuzalisha vitu vingine, huku akiendelea kufaidi matunda ya kazi aliyoifanya mwanzo.

Kwa watu wote na hasa waajiriwa tunaotaka mafanikio makubwa, ni lazima kila mmoja wetu ajiwekee tarehe ya mwisho ya kuacha kuuza nguvu kazi ghafi.

Kila mmoja akifikia tarehe yake ya mwisho kuuza nguvu kazi ghafi, mara moja aanze kujikita katika kubadili nguvu ya akiri na hisia kuwa bidhaa na huduma zenye kuwa suruhisho la kudumu kwa matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wengine.

Kwakuwa utazalisha bidhaa na huduma zenye kuwa na manufaa makubwa kwa watu wengine, basi na wao watakupatia zawadi ambayo ni pesa, ili kujipatia kila kilicho bora kutoka kwako. Tukiweza kufanikisha azima hii, basi tutatajirika kutokana na ukweli kwamba watu wengi kwasasa wanataka bidhaa na huduma ambazo ni suruhisho ya changamoto zao. 

Wateja ni wengi ambao wako tayari kununua kila kitu kitakachozalishwa ilimradi kina thamani kwao, kwa hiyo soko ni kubwa. Nchi yetu inapokaribia kuingia uchumi wa kati, mahitaji ya bidhaa na huduma zitokanazo na nguvu ya akiri/fikra zitazidi kuongezeka. 

Bidhaa zenyewe ni kama vile muziki, sanaa, vitabu, program za mafunzo ya ujasiriamali/biashara/afya/kilimo/majengo pamoja na machapisho juu miongozo mbalimbali ya uwekezaji katika mambo ya utalii, uwindaji, gasi, mafuta, madini, kilimo n.k.

Uchumi wa watanzania ukizidi kuongezeka na idadi ya wasomi ambao ndio wahitaji wakubwa itazidi kuongezeka huko tuendako ~ Kwa hiyo ewe mtanzania mwenzangu, anza kuchukua hatua leo, wakati ni sasa.

Imeandikwa na Cypridion Mushongi wa MAARIFA SHOP.










Feb 16, 2017

Sababu 15 Zinazopelekea Kushindwa Katika Maisha Yako Wakati Wote.

No comments :
Kama wewe ni msomaji mzuri wa vitabu sina shaka na wewe, naamini umeshawahi kusoma kitabu cha ‘Think and Grow rich’ kilichoandikwa na Napoleon Hill miaka mingi ya nyuma.
Katika kitabu hiki mwandishi ameandika mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kukusaidia na  kukutoa kutoa kwenye umaskini hadi kuweza kufikia ngazi ya utajiri.
Hiyo haitoshi, Napoleon hill pia kupitia kitabu hiki, ameweza kuandika kwa ufasaha sababu 30 ambazo zinapelekea watu wengi kushindwa katika maisha wakati wote.
Kupitia makala yetu haya ya leo nataka nikushirikishe kwa ufupi baadhi ya sababu hizo muhimu ambazo hufanya maisha ya watu wengi kushindwa kufanikiwa na kuishi kwenye umaskini.
Zifuatazo Ndizo Sababu 15 Zinazopelekea Kushidwa Katika Maisha Wote.
1. Kukosa malengo maalumu.
Kama unaishi bila ya kuwa na malengo maalumu, hujui unapokwenda kwenye maisha ni sababu tosha itakayokufanya ushindwe katika maisha yako. Ishi kwa malengo ujenge mafanikio yako.
2. Kukosa nidhamu.
Hakuna mafanikio ambayo unaweza ukayapata bila ya kuwa na nidhamu. Inatakiwa uwe una nidhamu karibu katika kila eneo la maisha yako. Wengi wanaoshindwa katika maisha kiukweli hawana nidhamu.

3. Kuahirisha mambo.
Pia kuahirisha mambo inatajwa kama sababu ya kukufanya ushindwe katika maisha. Kama kuna jambo unataka kulifanya,hebu lifanye wakati huo huo. Acha kusubiri kesho utapotea.
4. Kukosa nguvu ya kushikiria.
Wengi nao wanashindwa kwa sababu hawawezi kunga’ng’ania. Ikiwa unataka kufanikiwa lakini huna maamuzi ya kuwa mbishi sahau mafanikio. Hii ni dunia inayotaka uwe mbishi kweli mpaka ufanikiwe kimafanikio.
5. Mtazamo hasi.
Hiki pia ni kikwazo kikubwa cha mafanikio kwa watu wengi. Kama wewe una mtazamo hasi, hauwezi kufanikiwa. Mafanikio yanajengwa kwa mtazamo chanya.
6. Kukosa maamuzi sahihi.
Ikiwa kila wakati huna maamuzi sahihi, kwa mfano, maamuzi ya kukusaidia kufanikiwa, tambua upo pia kwenye eneo la kushindwa kila wakati. Maamuzi bora ni nguzo au njia sahihi ya kukufanya ukafanikiwa wakati wote.
7. Woga.
Pia mwandishi ameeleza kwamba maisha ya wengi yamejawa na hofu sana. Sasa hiki nacho ni kikwazo kikubwa cha kuweza kufika mafanikio makubwa. Ni lazima kuishinda hofu ili kufikia mafanikio yoyote katika maisha yako.
8. Kujiwekea tahadhari sana.
Kuna watu ambao wao hawataki kukosea kabisa. Ni watu wanaotaka kuwa wako kamili kila wakati. Ili ufanikiwe ni muhimu ukajua kukosea pia ni ngazi ya kukusaidia kuweza kufanikiwa. Kosea, jifunze na songa mbele.
9. Kukosa nguvu ya uzingativu.
Inatakiwa mawazo yako yawe kwenye kile unachokifanya mpaka ufanikiwe. Kama mawazo yako unayapeleka sehemu tofauti huwezi kufanikiwa. Kwa kila unachokifanya, zingatia hapo kwanza.
10. Kukosa uvumilivu.
Maisha yanaenda sambamba na kuwa mvumilivu. Kuna wakati unaweza kukutana na magumu sana, lakini ukishindwa kuvumilia ndio basi tena huwezi kufanikiwa.
11. Kukosa ushirikianao na wengine.
Huwezi kufanikiwa kama huna ushirikinao mzuri na watu wengine. Mafanikio ni kutegemeana, hasa katika suala la kushirikiana. Ni muhimu sana kushirikiana na wengine ili kuweza kufanikiwa.
12. Kukosa mtaji.
Watu wengine pia wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa mtaji. Ingawa katika hili sio sababu kubwa sana kwa sababu unaweza ukajipanga na kisha ukapata mtaji baada ya muda fulani.
13. Kuishi kwa kuhisi sana.
Pia kuna wengine wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kuishi kwa hisia. Utakuta badala ya kufanya jambo fulani kwa uhakika, mtu anawaza tu kwamba nitafanya kesho au hata nisipofanya hakuna shida.
14. Kuingia katika biashara isiyo sahihi.
Kama upo kwenye biashara ambayo haipo sahihi, pia ni rahisi kuweza kushindwa katika hilo jambo unalolifanya. Inatakiwa kuwa makini na kichagua biashara ambayo ni sahihi kwako na ambayo itakupa mafanikio.
15. Kuingia katika mahusianao mabovu.
Hakuna kitu kibaya kama kuingia katika mahusiano mabovu. Unapojiingiza katika mahusianao mabovu ni chanzo kingine kinachoweza kukufanya ukashindwa katika maisha yako.
Ukichunguza na kuangalia hizo ndizo sababu zinaweza kukufanya ukashindwa wakati wote, haijalishi unafanya nini kama una sababu hizo nyingi ni lazima utashindwa.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,