google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Nov 30, 2016

Sifa Kuu Za Mjasiliamali Ndizo Hizi.

No comments :
Naamini katika kujifunza, hii ndiyo kauli yangu ambayo inaongoza maisha yangu kila wakati. Kama na wewe unaamini katika kujifunza nakusihi twende sawa.

Somo letu la leo nililipenda sana, na nikaona na niweze kukushirikisha katika somo hili,  somo hili alinifindisha mwalimu wangu wa saikolojia, mtoa siri za mafanikio, au huwa napenda sana kumuita mzee wa nyundo kali huyu si mwingine ni Sharrif Kisuda.

Ambapo katika somo hilo alinifundisha kiundani kuhusu maana halisi ya mjasilimali. Mwalimu wangu huyu alianza kunieleza kwa kusema  maana ya
Ujasiliamali.

"Watu wengi tunapenda kutumia  jina hili la ujasiriamali  lakini wengi wetu hatujui maana yake.”  Aliendelea kueleza ya kwamba Ujasiriamali ni Fursa ya mafanikio ambayo mtu yeyote bila kujali elimu yake au hali yake anaweza kuanzisha biashara au mradi wowote mkubwa au mdogo na kumwingizia kipato bila kutumia nguvu kubwa hatimaye kupata faida.


Watu wengi pia tunashindwa kutofautisha kati ya mfanyabiashara na mjasiriamali. Hawa ni watu wawili tofauti kabisa.  Mjasiriamali ni mbunifu au mtoa wazo la Bbiashara linaloweza kuzalisha Bidhaa. Lakini mfanyabiashara ni mtu anaye uza bidhaa iliyokwisha zalishwa na mjasiriamali kwa lengo la kupata faida. Hapo ndipo utapogungua mfanyabiashara ni mtumwa wa mjasiriamali. 

Japokuwa wote wanategemeana ili mmoja asipokuwepo mwingine anaweza kupoteza kabisa mwelekeo wake. Kwahiyo mjasilimali lazima ashirikiane na mfanyabiashara  katika kutimiza lengo mahususi la muhusika.

Na kila wakati lazima utambue ya kwamba Ujasiriamali una kanuni ambazo unapaswa kuzijua ili kutengeneza au kuzalisha Kitu chenye ubora,  ila katika Biashara haina kanuni ni kuangalia uhitaji wa soko na idadi ya Wateja. 

Kuwa mjasiriamali sio lazima usome mpaka upate digrii ya ujasiriamali zaidi unahitaji kusoma na kuzingatia taratibu na kanuni sahihi. Msingi wa awali wa Mjasiriamali ni wazo lakini msingi wa kwanza wa mfanyabiashara ni Pesa ya mtaji.

Kila Mjasiriamali ni mfanyabiashara lakini si kila mfanyabiashara ni mjasiriamali. Mjasiriamali ni mtu mwenye imani katika kila jambo analofanya na pia mtu aliyetayari kufanya maamuzi bila ya kujali sana matokeo. 

Mjasiriamali ana tabia ya kufanya Kitu anachokipenda na ndio maana huwa vigumu kukata tamaa hata kama kukitokea changamoto kiasi gani. Ni mtu jasiri na anaethubutu kufanya vitu ambavyo wengine huviogopa kuvifanya.

Na zaidi mjasiriamali ana nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya muda pesa na mali zake. Tofauti na mfanyabiashara akipata pesa ya ziada ni lazima aongeze matumizi na starehe zisizo na ulazima.

 Ngoja tuangalie sifa za mjasiliamali.

1.Hufanya kazi kwa bidii.

Mara kadhaa hauna haja budi kuchukia kuwepo katika ulimwengu huu eti kwa sababu Maisha ni magumu, ugumu wa maisha una sababishwa na wewe mwenyewe.

Na hii yote inatokana na kuweza kufanya kazi kimazoe, Mara nyingi ukiwa na tabia ya kufanya kazi kimazoea hata kwa kile kidogo unachokifanya hautakiona thamani yake. Hivyo nakusihi kila wakati hakikisha unafanya kazi kwa bidii huku ukiondokana na dhana ya ya kufanya kazi kimazoea.

2. Lazima awe mbunifu na mvumbuzi.

Hii ni tabia kubwa muhimu ambayo kwa kila mjasiliamali yeyote yule lazima awe nayo, bila ubunifu kwa hicho unachokifanya Ni bure. Ubunifu si kutengeneza kitu awali/ au Ni kitendo cha kufanya maboresho.

Kwa mfano utaona kila siku kampuni fulani za utengenezaji simu, kila kukicha wanafanya ubunifu kwenye bidhaa zao, hufanya hivyo ili kuongeza wateja. Kama ilivyo katika utengenezaji wa simu tumia kanununi hiyo hiyo katika kuboresha vitu ambavyo unavitengeneza au kuvifanya. 

3. Yupo tayari kujifunza kila wakati.

Kama nilivyoeleza hapo awali ya kwamba ujasiriamali ni imani, hivyo mara kadhaa kuamini ya kwamba mafanikio yanakuja kwa kujifunza vitu ambavyo vitamfanya aweze kukua kwa kile akifanyacho. Na vilevile yupo tayari kwa chochote ambacho huwa anafanya.

Ukitaka kuwa mjasilimali wa kweli, hakikisha ya kwamba unayazingatia hayo, kwa umakini zaidi na kuyafanyia kazi.

Imeandikwa na Afisa mipango Benson Chonya.

Nov 29, 2016

Kanuni Ya Usumaku (Law Of Attraction).

No comments :
Na Apolinary Protas wa Jitambue sasa.

Kwa wengine hupenda kuita ni Law of Attraction, lakini kwa upande wangu naona sio lazima niipe jina kwa kuitafsiri moja kwa moja kwenye kiswahili kama ilivyo kwenye kingereza lakini napendelea kuipa jina la Sheria ya Sumaku kwani jina hilo inakuwa rahisi kuielewa vyema. 

Kama inavyofahamika kuwa Sumaku ni kifaa ambacho kinavuta Chuma. Kama una sumaku, ukiiweka karibu na chuma utaona inavuta vitu vyenye asili ya Chuma. Usumaku ni ile hali ya uwezo wa kuwa na nguvu kama za sumaku, uwezo wa kuvuta vitu vyenye hali ya chuma. Je usumaku ni nini?

Kanuni ya Usumaku ni nini?

Ni kanuni inayotazama kuwa Ufahamu wa mwanadamu una sifa ya Sumaku. Kile kilichopo kwenye ufahamu wako unakiumba na kukipelekea kuwepo katika dunia yako. Kila jambo unaloliona halipo kwenye ufahamu wako tu lakini linaweza likawa kwenye ufahamu wa mwingine hivyo lipo kwenye ufahamu (ufahamu fulani). Chukulia ulimwengu kama umeme. Umeme huo upo katika hali mbalimbali ya nguvu na kila hali ina upekee wake. Ufahamu ni umeme, na ndio maana kwenye Ubongo kuna neva, neva hupitisha umeme kutoka kwenye ubongo na kwenda kwenye sehemu nyingine za mwili kama vile msuli na milango ya ufahamu. 

UNA UWEZO WA KUUMBA MAISHA YAKO.
Ufahamu ni kiini kikuu cha Mwanadamu na kila kiumbe. Kila kiumbe kina ufahamu wake kulingana na hali iliyopo lakini mwanadamu ndiye mwenye ufahamu wa kujitambua yeye ni nani. Na kuutambua ufahamu wake, lakini aina nyingine za uhai haziwezi kufahamu ufahamu wake ni nini na umeumbwa na aina gani ya ufahamu. 

Ndani yako kuna sehemu kubwa sana iliyo na nguvu kubwa sana ambayo huijui. Unaweza ukajiuliza ulipokuwa mdogo nani alikuwa anahakikisha unakua vyema, nani anahakikisha sasa hivi mapafu yako yanasukuma hewa, nani anayehakikisha moyo wako unadunda, ni sehemu ambayo unayo akilini mwako lakini tangu uumbwe mpaka leo hujawahi kuitazama na kujifunza kuitawala. Simaanishi ujue kutawala mapigo yako ya mwili bali namaanisha kuwa ndani mwako kuna nguvu kubwa, ambayo ukiamua kuiamuru kufanya chochote inaweza kukusaidia na kukupa chochote. Nguvu hiyo inaungana na ufahamu wako. Unachokiamini, unachokitafakari, na unachokisema kinaungana na nguvu hiyo vyema na kupelekea kufanyika. Unaweza ukawa hujaona hilo lakini ukiwa makini utagundua hilo. 

Kanuni ya USUMAKU inatufunza kuwa, unaumba uhalisia wa maisha yako wewe mwenyewe. Wewe ni kama Sumaku, unavuta uhalisia wowote ule ambao unaushikilia akilini kwa muda mrefu. 

Ukiamini kuwa wewe ni mtesekaji utazidi kuwa mtesekaji, ukiamini umebarikiwa basi unapata baraka, na ukiamini unaweza kutimiza jambo fulani nawe utaweza kulitimia. 
Hata Yesu alisema; Ukiwa na imani kidogo kama vile Punje ya Haradani unaweza kuuamuru mlima kuhama na ukahama. Jitambue Sasa na yatengeneze maisha yako vyema. 

Ansante kwa kusoma makala haya na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kjifunza.




Nov 28, 2016

Tumia Mbinu Hizi Ili Uweze Kuishi Ndoto Yako.

No comments :
Tuanze kwa kujiuliza je hilo ambalo unalifanya ni la kwako au ni la mtu mwingine? Je kama si ndoto yako unahisi ni lini utaishi ndoto yako? hivi hupendi watu watu wajifunze kupitia kwako?.

Usinipe majibu, nimeona ni vyema tuanze na kujiuliza maswali hayo kwani ni ya msingi sana, na majibu yake yatadhihirisha kuwa umekuja duniani kwa lengo la kutimiza ndoto zako na si ndoto wengine, hata pale unaposema Mwenyezi Mungu bariki kazi mikono yangu baraka hizo zikujie moja kwa moja. 

Zifuatazo ndizo mbinu za kuzitumia ili kuishi Ndoto zako.

1. Usipoteze Muda kwa vitu visivyo vya msingi.

Mara kadhaa tumekuwa tukitumia muda mwingi kwa vitu ambavyo vimekuwa si lolote kwetu. Tumeshindwa kufanya tathimini ya kutosha juu ya ndoto zetu tulizonazo, tumekuwa tukiishi ndoto ambazo si zetu, tumekuwa tukiishi maisha ya wengine.

Mara nyingi tumekuwa tukilalama bila kutoa sauti ya kwamba maisha ni magumu, na muda mwingine tumekuwa tukidiliki hata kusema ya kwamba dunia hii haina usawa, yote hayo hutokea hasa pale tunaposhindwa kufanikiwa, huku tukisahau ya kwamba wengi wetu tunafanya vitu vya watu wengine.

Usipoteze muda kufanya vitu visivyo vya maana kwako, ishi kwenye ndoto zako.

Hivi hujawahi kuona ya kwamba mtu ndoto yake ilikuwa ni Kuwa muigizaji na leo hii ni fundi mjenzi? Unadhani nini ambacho kimesababisha hali hiyo kutokea? Usinipe majibu.

Ila nikusihi ya kwamba dunia hii inahitaji mtu ambaye anaishi ndoto zake, hivyo kila wakati unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unaishi ndoto zako kwa kuzingatia lile likusukumalo kutoka nafsini mwako, usibadili mwelekeo wa kutimiza ndoto zako eti kwa sababu maisha ni magumu, eti kwa sababu ya ndugu, jamaa na marafiki. 

Amini ya kwamba ndoto zako zinawezekana, na hivyo anza kuishi ndoto zako sasa kabla ya kuifikia ndoto hiyo, kama unataka kuwa mwalimu anza kuifundisha jamii ambayo inakuzunguka sasa,  ukifanya hivi hautautumia muda mwingi kufanya vitu visivyokuwa vya maana kwani utakuwa umeanza kuishi ndoto zako. Mafanikio hayana kesho anza leo.

2.Usikubali kukatishwa tamaa.

Kuishi ndoto zako ni moja ya kitu kikubwa ambacho naamini unakitafuta katika maisha yako. Lakini wengi wetu, hushindwa kufikia ndoto hizo hii Ni kutokana na mazingira ambayo yanamzungumka mtu huyo. Lakini ipo siri ambayo wengi hawaijui ni kwamba siku zote kuwa wewe, usiwe wao.

Inawezekana ukawa hujanielewa ni hivi wengi hukatishwa tamaa na watu wengine, na kwa kuwa wewe hupagawishwa zaidi na aina hiyo ya watu unajikuta unaliacha jambo unalolifanya na kuanza jambo jingine, lakini kabla sijaweka nukta katika muktadha huu nikwambie ya kwamba chagua fungu lililo bora acha kukatishwa tamaa na watu ambao hawana msaada wowote.

3. Uwe tayari kupokea ushauri na kuufanyia kazi.

Dunia hii imejaa watu wa aina tatu, wapo wale washauri, wapo wakatishaji tamaa, wapo wale ambao wanasubiri wewe uanze kufanya jambo fulani ili na wao waanze kujifunza kupitia kwako, wala usijali hii ndio dunia bwana, unachatakiwa kufanya ni kujifunza kutoka kwa aina hizo zote tatu.

Lakini kujifunza huko si kila jambo la kuchukua mambo mengine yaache kama yalivyo,  ila jifunze yale mambo ya muhimu kutoka kwa washauri sahihi hasa wale ambao wanafanya mambo ambayo yanafanana na ndoto zako.

Najua kila kitu katika kujifunza kina changamoto zake unachotakiwa kufanya si kukata tamaa bali ni kupambana mpaka mwisho ili ujue hatima ya maisha yako.

4. Jifunze kwa waliofanikiwa.

Maisha ni kujifunza, si kujifunza tu bali kujifunza kitu kipya, kujifunza kitu kipya pekee yake haitoshi bali unatakiwa kukiweka katika matendo, kama utaamua kujifunza pekee yake haitakusaidia kitu.

Ni vyema kila wakati ukajua thamani ya kufanyia kazi kile ulichojifunza. Mabadiliko ya kitu chochote yanatokana na wewe kujua kitu kipya, haitawezekana hata siku moja eti unataka kutimiza ndoto zako kama haupo tayari kujifunza.

Mara kwa Mara wanasema hakikisha unajifunza kwa watu ambao wamefanikiwa, watu hawa wawe ambao wana mfanano wa ndoto zako.

Mwisho afisa mipago niweke nukta kwa kusema ya kwamba kutimiza ndoto zako inawezekana kabisa endapo utaamua kuchukua maamuzi ya kuanza kuchukua hatua ndogondogo siku leo. Maana mafanikio ni Leo wala si kesho.

Ni wako rafiki katika Mafanikio;
Afisa mipango Benson Chonya

Nov 25, 2016

Siri Nyingine Ya Mafanikio Kwa Richard Branson Ni Hii Hapa.

No comments :
Kuna wakati mwandishi, mhamasishaji na mfanyabishara maarufu duniani Richard Branson alipoulizwa ni nini siri ya mafanikio yake alisema kwa kifupi tu kwamba, siri ya mafanikio yake ipo kwenye umakini.
Richard Branson alisema ‘kuanza siku yako, bila kuwa makini na vitu unavyotakiwa kuvifanya, ni sawa na kuipoteza siku hiyo kabisa’. Branson aliendelea kusema ‘bila umakini hakuna mafanikio wala uzalishaji wowote  wa maana utakaoupata.
Kwa mujibu wa maelezo ya Branson anadai kwamba unapokuwa makini, unakuwa unajitengenezea ndani yako msukumo wa mafanikio, msukumo unaokuongoza kufanikiwa zaidi.
Kwa chochote kile unachokifanya iwe biashara, uandishi au mpiganaji wa masumbwi ili uweze kufanikiwa kwa viwango vya juu sana, ni wazi kabisa unahitaji kujijengea tabia ya kuwa na umakini.
Tatizo la watu wengi hawapo makini sana katika mambo yao au mfumo mzima wa kuendesha maisha yao. Kama vile madereva wa magari walivyo makini wawapo barabarani, vivyo hivyo nawe unatakiwa kuwa makini sana kwenye maisha yako.

Umkini wako ndio utakaokupa mafanikio
Hebu piga picha kama dereva wa gari asipokuwa makini awapo barabarani ni nini ambacho huwa kinatokea? Bila shaka hakuna jibu jingine ambalo utanipa zaidi ya ajali.
Hata kwenye maisha yetu hivyo ndivyo tunavyosababisha ‘ajali’ za kushindwa sana wakati mwingine kwa sababu ya kupoteza ule umakini. Unatakiwa kujiwekea umakini katika kila eneo la maisha yako ili ufanikiwe.
Na ili uwe makini yapo mambo kadhaa mbayo unatakiwa kuyafanya na kuyazingatia sana kila siku kwenye safari yako ya mafanikio. Unaposhindwa kuzingatia mambo hayo, ni lazima umakini utapotea na utaanza kuishi maisha ya kushindwa.
1. Anza siku yako upya.
Haijalishi jana yako ilikuwaje, kilicho kikubwa kwako ni kuanza siku yako upya. Sahau changamoto zote ulizokutana nazo jana ambazo pengine zilikukatisha tamaa sana.
Kitu cha msingi kwako anza siku yako upya kwa kuzingatia kile unachotaka kukifanya. Ikiwa utakuwa unazingatia sana mambo ya jana, hapa ni lazima umakini utakutoka na utashindwa kufanikiwa.
2. Andika malengo yako ya siku.
Acha kuishi kiholela, ishi kwa mipango kwa kuandika malengo yako ya siku, Hiyo itakusaidia kukuongezea umakini na kujua hasa ni kipi ufanye au kipi usiweze kufanya.
3. Tumia muda wako vizuri.
Matumizi mazuri ya muda ni chanzo kingine kikubwa cha kukusaidia kuweza kuwa makini. Kama unatumia muda wako hovyo, ni wazi au dalili ya wewe kutokuwa makini, zingatia sana matumizi yako ya muda.
4. Jiwekee mipango yako ya mbele.
Unapokuwa na mipango yako ya mbeleni uliyojiwekea, kwa mfano kujua ni nini utakifanya mwezi ujao au mwaka kesho, hiyo inasaidia sana kuongeza nguvu ya umakini kwa kile unachokifanya.
Naomba utambue kwamba siri nyingine ya mafanikio yako ipo kwenye umakini ulionao. Umakini ulionao ndio unaonyesha kwamba upo na nia ya kufikia kwenye mafanikio yako.
Hata hivyo kumbuka huwezi kuwa makini mpaka ujijengee tabia ya kuanza siku yako upya, kutumia muda wako vizuri, kuandika malengo kila siku na kujiwekea mipango ya mbeleni.
Nikutakie siku njema na mafanikio mema.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Nov 24, 2016

Ijue Elimu Hii Muhimu Ya Fedha Na Mafanikio, Ili Uwe TAJIRI.

No comments :
Leo ngoja tuzungumze juu ya fedha na vitu vinavyoambatana na fedha(Assets au Liabilities) ambavyo ni chanzo kingine cha kupima mafanikio yako au hata kujua utapita njia ipi kufikia malengo yako.

Watu wengi wamedumaa na kushindwa kusonga mbele kwa kukosa maarifa sahihi juu ya neno FEDHA.  Na bahati mbaya ualisia wa somo hili kivitendo halielezwi kisahihi shuleni au vyuoni, hapa naomba usinielewe vibaya na wala usije sema najifanya mjuaji la hasha.

Labda nitoe mfano. Shuleni au vyuoni ukifeli wewe unaambiwa mjinga lakini kwenye usakaji wa fedha uhalisia wa kufeli ni hatua mojawapo kufikia malengo maana ukiogopa kufeli kamwe sahau kuhusu mafanikio, maana hutaweza kujaribu kitu.


Pili shuleni/chuo unafundishwa kila swali lina jibu moja tu sahihi (1+1=2) lakini kwenye uhalisia inawezekana kabisa 1+1=6 na bado likawa jibu sahihi.

Shuleni/vyuoni hauruhusiwi kuigilizia hasa wakati wa mtihani lakini kwenye uhalisia wa kusaka mafanikio kudesa unaruhusiwa-bila shaka umeona kwanini nilipinga hapo juu.

Kuza ufahamu wako wa fedha kila siku.

Elimu ya fedha ni muhimu sana kuijua kwa undani na hapa nisisitize usije ukaridhika kamwe na ‘material’ yako ya darasana na A+ zako halafu ukajiona unaweza ukatoboa kirahisi kwenye uhalisia, hizo zilikuwa nadharia tu, vitendo ndiyo mpango mzima.

Hakikisha unasaka elimu zaidi juu ya fedha na matumizi yake sahihi. Huwa nasikitika sana kumwona kijana kwanza amepata kazi na kitu cha kwanza anachowaza ni gari!! Eti kwa kuwa ana kamshahara kaa milioni moja na laki mbili.

Kijana huyu anakuwa anajisahau kuwa amechimba shimo la kuchoma pesa hata kabla hajaimalika kifedha. Gari, nyumba unayomiliki, flat screen, radio, smart phone na vinginevyo hizo ni ‘liabilities’ ambazo zitaendelea kukumalizia kamshahara kako na kukufanya usimame pale ulipo kwa miaka mingi.

Kuwa makini, ishi maisha ambayo yanaendana na malengo yako. Kidogo ulichonacho kina thamani kubwa kama utakitumia vizuri, acha kuishi ili watu wakuone ishi wewe na usiishi wao!!

Nunua ‘asset’ maana zitakufanya uzalishe fedha na si kukimbilia kununua mchwa wa kutafuna hata kile kidogo ulicho nacho! Mfano wewe unakimbilia kununua viti vya kutembelea na mwenzako akanunua bodaboda ya kuzungusha machoni pa wengi wewe wa viti  vyako utaonekana mjanja lakini kiuhalisia mwenye bodaboda ni bora mara 1000 zaidi yako!

Hebu nikuambie kitu leo, acha uoga wa kuanza kidogo kwa kamtaji kidogo ukidhani si chochote, na ukasubiria hadi upate mamilioni ndiyo uanze safari yako ya mafanikio.

Utakuwa unajidanganya maana njia ya mafanikio iliyobora na matajili wengi wameitumia ni kuanza kidogo lakini kuwa na malengo makubwa. Na hiyo inasaidia sana kuendelea kujifunza kadili unavyokua (Nyani mzee amekwepa mishale mingi).

Hata Dangote tajili wa Afrika anakushauri (start small dream big). Cha msingi hakikisha unajifunza kuhusu pesa kila iitwayo siku kupitia vitabu, machapisho, semina za ujasiliamali au warsha mbalimbali (Kama kweli unataka kubadilika lazima uwekeze huko). 


Jifunze kuwa mpya kila siku/mwaka kwa kuongeza marafiki wapya hasa wale ambao wanafanya vizuri katika nyanja unazopenda! Na si dhambi kuachana na marafiki ambao wanakukatisha tamaa kila uchwao.

Hamna lisilowezekana chini ya jua kama utakuwa na imani ya kumtumaini Mungu na kuamini ana mpango na uwepo wako hapa dunia. Fanya kwa moyo bila chembe ya shaka hakika utafika.

Waliofanikiwa wengi ukiwauliza walifikaje walipo watakuambia kwa kweli hawajui ila wanachojua walifanya kazi kwa moyo na imani kubwa kuelekea kwenye malengo yao na Mungu atimaye amewawezesha.

Sasa kwanini wewe usite!!? Kuwa mdadisi na mwenye kiu halisi ya kile ukitakacho hata kama kijiji/mtaa mzima watakucheka kuwa hutaweza wewe jisemee tena ukijiamini kuwa unaweza kwani Mungu akiwa upande wako hakuna linalo shindikana!!

Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.

MAKALA HII IMEANDIKWA NA SHARIFF KISUDA alimaarufu mzee wa nyundo.
Mawasiliano 0715 079 993

Nov 23, 2016

Tumia Mbinu Hizi Kupanga Malengo Yako Ya Kimafanikio.

No comments :
Umbali uliopo kati ya malengo yako na mafanikio ni mrefu sana, na una vikwazo vingi sana, nafahamu fika ya kwamba hilo unalitambua vizuri sana.

Umbali huo ambao upo baadhi ya watu ambao wana Mafanikio wameweka mikakati thabiti ambayo imewafanya wameweza kufanikiwa.

Pia kwa upande watu ambao hawajafanikiwa kwa kiwango juu na wao katika malengo yao wameweka mikakati, ila wengi wao hukata tamaa njiani katika utekelezaji wa mambo mbalimbali yatayowalete mafanikio.

Hali hiyo hutokea kwa sababu wengi wao hushidwa kuhimili changamoto ambazo hujitokeza katika safari hiyo ya kutoka katika malengo hadi Mafanikio.

Kama na wewe ni miongoni mwa watu ambao hukata tamaa katika safari yako ya kuelekea mafanikio, naomba nichukue nafasi hii kuweza kukaribisha katika makala haya ambapo tutazungumzia masuala ya kupanga malengo yako hadi kufikia mafanikio.

Wengi hujikuta wakishindwa wakiishia njiani katika safari yao ya mafanikio hii ni kutokana kutokujua namna ya kuzitambua mbinu za kukuza  malengo hadi mafanikio.

1. Malengo ni lazima yaandikwe.

Malengo lazima uyaandike sehemu ambayo inaonekana, hapa ni maana ya kwamba uandike sehemu ambayo inaonekana, kufanya hivi kutakuwa kuna kutakufanya malengo hayo uwe unayakumbuka na kujua namna ya kuayatekeleza.

Unaweza ukayaandika malengo hayo kuyaweka katika simu yako katika (screen saver), kioo ambacho unakitumia kujitazama asubuhi na sehemu nyingine ambayo utayaona malengo hayo.



2. Weka vipaumbele katika malengo yako.

Inawezekana fika ukawa na malengo mengi, yaandike malengo hayo katika makundi matatu.

Kundi la kwanza jua yapi ni malengo ya muhimu yapi si malengo ya muhimu, yapi ni malengo ya haraka na yapi sio malengo, na tatu andika malengo ambayo sio ya muhimu sana.

Endapo utagawa malengo hayo utajua ni kipi kinatakiwa kuanza na kipi kinatakiwa kufuata na kwa muda gani.

3. Anza kwa kuanza na hatua ndogo.

Siku zote kama ilivyo ukuaji Wa kiumbe chochote chenye uhai huanza ukuaji wake katika hali ya chini. Kama ilivyo kwa kiumbe yeyote katika ukuaji hata katika ukuaji wa mafanikio yako huanza katika ngazi za chini.

Kitu cha msingi ni kuweza kupanua wigo mpana kwa ajili ya kupata mafanikio zaidi kwa kila jambo ambalo unalifanya. Na kwa kuwa mafanikio hayana ukomo hakikisha ya kwamba kila iitwayo leo unapata kiu ya kutaka kufanikiwa zaidi.

4. Malengo ni lazima yawe chanya.

Mara kadha watu huwa na ndoto nzuri sana, na pia wengi wao hupanga mambo mazuri kwa ajili ya utekelezaji wa ndoto hizo, ila changamoto kubwa ambayo huwa inakuja ni pale ambapo linakuja suala la utekelezaji wa jambo hilo.

Hapo sasa ndipo utakapoanza kumsikia mtu anasema aaah hivi nitaweza kweli, inatakiwa uondokane na kukata tamaa, vinginevyo kufanikiwa utaendelea kusikia kwa akina  Donald Trump.

5.Malengo lazima yawe katika muda maalumu.

Ni lazima uweke muda kamili kwa ajili ya kutekeleza malengo yako, ifike mahali Malengo yako yafananishe na makampuni yanayohusika ujenzi kwani wao kabla ya kuanza kwa mradi huwa wanafanya mahesabu ili kujue mradi huo wa ujenzi utachukua muda gani mpaka ukamilike.

Ukiishi katika utaratibu Wa kuweka mbinu hiyo itakuwa ni rahisi kwako kutekeleza mambo ambayo unataka kutekeza. Kwa mfano lengo lako ni kujenga nyumba unaweza ukaandika katika lengo lako ya kwamba baada ya muda fulani inabidi uwe umekamilisha ujenzi huo.

Kupanga malengo bila kujua muda Wa kutekeleza malengo ni sawa na bure. Hivyo ni vyema ukajua ya kwamba muda ni mali katika kufanikisha malengo yako kwa wakati sahihi.

6. Malengo ni lazima yawe na mbinu za utekelezaji.

Watu wengi wana malengo ya kusema kwa mdomo tu. Lakini nikwambie ya kwamba ukitaka kufa maskini basi endelea na utaratibu huo Wa kuweka malengo mdomoni.

Kama kweli unataka kufanikiwa hakikisha ya kwamba malengo ambayo umejipangia umeyaandika na kuandika mbinu au njia kwa ajili ya utekelezaji wa malengo hayo.

Kufanya hivi kutakusaidia kujua jinsi ambavyo utayatekeleza malengo hayo ili  kupata mafanikio. Kwa mfano kama malengo yako ni kujenga nyumba basi huna budi kuandika mbinu ambazo zitakusaidia kutengeza nyumba hiyo, pia hapa huenda sambamba na bajeti ya utekelezaji wa malengo yako.

7. Malengo ni lazima yapimike.

Kila malengo ambayo umejipangia Ni lazima yaweze kupimika. Kama nilivyoeleza hapo awali ya kwamba malengo ni lazima yawe na muda maalum kwa ajili ya utekelezaji.

Hivyo ni lazima upime malengo yako ni wapi ambapo umefikia?  Katika muda ambao umepanga kuyatekeza malengo hayo je unahisi utafikia malengo hayo?

Pia uchunguzi yakinifu juu ya malengo yako ni lazima ufanyike ili kujua  fursa na changamoto ambazo zimejitokeza katika kuteleza malengo yako.

Mpaka kufikia hapa sina la ziada, tukutane siku nyingine.

Ndimi Afisa Mipango Benson Chonya
0757909942


Nov 21, 2016

Acha Kurudia Kufanya Kosa Hili, Wakati Unatafuta Mafanikio.

No comments :
Kati ya kitu muhimu sana ambacho kinaweza kukusaidia katika safari ya kuelekea mafanikio yako, ni yale makosa unayoyafanya. Mara nyingi makosa hayo ukiyatumia vizuri ni nguzo kubwa ya kukusaidia kufanikiwa.
Lakini pamoja na makosa hayo kuwa ni msingi wa kukufikisha kwenye mafanikio, naomba ieleweke kwamba si makosa yote, yanaweza kukusaidia kufanikiwa. Yapo makosa ambayo hutakiwi kurudia kuyafanya kwenye maisha yako kabisa.
Ikiwa utakuwa ni mtu wa kurudia rudia kufanya makosa hayo mara kwa mara ni lazima safari yako ya mafanikio itakwama. Moja ya kosa kubwa ambalo hulitakiwi kulifanya tena katika maisha yako ni kosa la kutokuchukua hatua ndogo ndogo.
Acha kufanya kosa la kutokuchukua hatua ndogo ndogo kwenye maisha yako. Hatua hizi ndogo ni muhimu sana katika kukufikisha wewe katika mafanikio makubwa, ingawa unaweza kaziona hazina maana.
Kila hatua ni mafanikio.
Wakati wote acha kabisa kujijengea dharau kwamba, hatua ndogo haziwezi kukufikisha popote, kwa chochote kile kidogo ulichonacho usikione eti hakiwezi kukusaidia katika safari yako ya mafanikio, hicho kina msaada mkubwa sana kuliko unavyofikiri.
Kwa mfano, kama unaona una muda kidogo, tumia muda huo kidogo kufanya jambo la maana, hata kujisomea ila usiupoteze. Kama unaona una pesa kidogo, hata kama ni shilingi elfu moja, iweke pesa hiyo na usiipoteze eti kwa sababu ni ndogo.
Pia kama unaona una mtaji kidogo, tumia mtaji huo uweze kuwekeza na kukusaidia kutoka hatua moja na kuelekea hatua nyingine. Chochote kile kidogo ulichonacho, chukua hatua ya kukitumia kwa manufaa ili uweze kufanikiwa.
Utapoteza fursa nyingi na mafanikio makubwa kwa sababu ya tabia ya kudharau mambo madogo. Pengine tu, naomba nikukumbushe mafanikio yanajengwa na kanuni au vitu vidogo vidogo sana ambavyo wengi wanavidharau na kuviona havina msaada kwao.
Unachotakiwa kuelewa ni kwamba kila wakati kwa wewe kuwa makini na kutambua mchango wa mambo madogo madogo katika suala zima la kukufanikisha. Ikiwa utaendeleza dharau au tabia ya kutokuzingatia mambo madogo na kuona hayafai, nakupa uhakika huwezi kufika mbali kimafanikio.
Jenga mafanikio yako leo kwa kuchukua hatua ndogo sana hata kama zinaitwa hatua za kutambaa. Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyoanza, yanaanza kidogo kidogo sana.
Najua ni shahidi mzuri wa hili, ukiangalia makuzi ya mtoto, baadhi ya miti mikubwa kama mibuyu, ilianza kidogo kidogo sana, lakini leo hii ukuaji wake ni mkubwa sana ambao hauna mfano.
Tafakari juu ya hili na chukua hatua za kufanya chochote kile hata kama ni kidogo, lakini tambua kina msaada mkubwa sana kwa mafanikio yako leo na kesho, isitoshe naweza kusema huo ndio msingi mkubwa wa kimafanikio unavyojengwa duniani kote.
Dira ya mafanikio inakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe upande wako.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku na pia endelea kuwashirikisha wengine makala nzuri zinazotolewa hapa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,




Nov 18, 2016

Ili Ufanikiwe zaidi, Unahitaji Kuishi Na Watu Hawa.

No comments :
Katika kufikia mafanikikio makubwa unayoyatafuta, ieleweke wazi wapo watu ambao ni lazima sana uwe nao kwa karibu ili uweze kujifunza kwao na hadi kufanikiwa.
Kumbuka, sisi ni matokeo ya watu watano wanaotunzunguka. Kama unazungukwa na watu watano ni maskini, basi ni wazi upo uwezekano hata wewe kuelekea kwenye njia hiyo ya umaskini.
Mpaka hapo unaona upo ulazima wa wewe kuwa na watu sahihi  kila wakati kwenye maisha yako ili ufanikiwe. Usipate shida sana kujiuliza ni watu gani hawa ambao na unatakiwa kuwa nao ili kufanikiwa?
Ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuishi na watu hawa.
1. ‘Mentors’/Washauri.
Kwa chochote kile unachokifanya, wapo watu ambao wamekutangulia na wanakifanya kitu hicho tena kwa mafanikio. Watu hawa, ikiwa utajifunza kwao na kuwafanya wakawa ndio taa yako ya mafanikio, utafanikiwa.
Hawa ndio watu wa kuishi nao karibu kwa kuwafanya kuwa ‘Mentors’ wako au washauri wako wa karibu wa mafanikio. Hiyo iko hivyo kwa sababu njia unayotaka kupita wao tayari wameshaipita. Hivyo ni rahisi sana kukuelekeza.
Inawezekana unakwama kwenye maisha kwa sababu huna ‘mentor’ au hata mlezi mmoja wa mafanikio ambaye unamfuata. Sasa kama unaishi hivyo, sio rahisi sana kufanikiwa. Ni lazima uwe na mtu anayekuongoza kufikia mafanikio yako.
Unaweza ukawa unajiuliza sasa nitawapata wapi? Kama ni watu wenye pesa mbona wako ‘bize’ sana? hilo lisikupe shida,  jifunze kupitia kazi zao wanazotoa kama vile vitabu. Hapo utapata mawazo yao yote na ushauri wao kwa karibu sana.
Pata mshauri wa kukuza kipaji chako.
2. Watu wenye uzoefu kwa kile unachokifanya.
Mara nyingi wengi wetu tunakuwa tunapotea na kukosea sana kwenye maisha kwa sababu ya kuishi au kuzungukwa  na watu ambao si wazoefu sana na kile tunachokifanya.
Kwa mfano utakuta mtu ana duka la vipodozi, lakini ana shauriwa sana na watu ambao muda wote ni wafanyabiashara wa nguo. Hiyo pekee tu ni kosa ambalo  linakufanya kufanikiwa kwako isiwe rahisi.
Ili uweze kutoka kimaisha, jifunze kuwa na watu ambao wana uzoefu na jambo unalolifanya.  Watu hao watakusaidia sana kukuonyesha njia sahihi ya kufikia mafanikio yako kwa haraka. Ili kufanikiwa kwa hili usijifanye mjuaje, kuwa mpole kubali kujifunza.
3. Watu wanaokufanya ufikiri zaidi.
Pia mbali na ‘mentors’ na watu wenye uzoefu, watu wengine ambao unahitaji kukaa nao karibu sana ili wakusaidie kufikia mafanikio ni watu wanaokufikirisha zaidi.
Ni hatari sana kukaa na watu ambao hawakupi changamoto za kimaisha. Ni lazima uishi na watu ambao kila kukicha ni kama wanawasha kichwa chako ‘moto’ kutokana na changamoto wanazokupa.
Unapokuwa na watu hawa watakutia hasira na utafanya kazi kwa mwehu ili kuhakikisha unafanikiwa zaidi na zaidi. Maisha yako kumbuka yanataka changamoto ili yaweze kufanikiwa. Hivyo ni lazima kuwa na watu hawa.
4. Watu wanaosikiliza.
Kuna watu ambao katika maisha ni wabishi karibu kwa kila kitu. Hawa ni watu ambao hata wakielekezwa kitu kidogo wao hukimbilia kwenye kubisha. Ikiwa hutawajua watu hawa watakupotezea muda sana.
Kitu cha kufanya, epuka watu hawa na ishi na watu ambao wanasikiliza. Ishi na watu ambao mnaendana. Ikiwa kila mtu anakuwa ni mbishi jiulize  hayo mafanikio yatapatikana vipi?
Kwa kuhitimisha makala haya, naomba ieleweke hivi, wapo watu ambao unatakiwa uwe nao karibu, unatakiwa uishi nao ili uweze kufanikiwa. Na hao ndio watu unaotakiwa kuishi nao kama tulivyowajadili kwenye makala haya.
Endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,