google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 30, 2015

Haya Ndiyo Maajabu Makubwa Yanayoweza Kufanywa Na Mawazo Yako.

No comments :
Kila dakika ambayo inapita imeshakwenda zake, hairudi tena na hii ina maana kwamba, siku zako za kuishi zimepungua tayari. Ni ajabu hata hivyo, kwamba kila mtu anasubiri siku moja, siku fulani atakapofanikiwa jambo fulani, ndiyo aanze kufurahia maisha. Siku hiyo haitafika, ni leo.

Kila dakika inayopita, sehemu Fulani ya mwili wako, nayo imeondoka, imeharibika, hairudi tena. Lakini inasikitisha kuona kwamba, kila siku watu wanajiambia kwamba, watafanya tu, wakiwa hawajui kwamba, wanachakaa na muda sio mrefu watakuwa wameachana na miili yao, na kuwa kitu kingine tofauti.

Kumbuka tu kwamba, kila dakika inayopita, seli za mwili zipitazo bilioni tatu zinazalishwa mwilini ili kuchukua nafasi ya nyingine za idadi kama hiyo ambazo zimekufa katika dakika hiyo moja. Hatua hizi za mabadilishano ya seli hufanyika bila wewe kujua, kwa sababu zinaongozwa na kusimamiwa na mawazo ya kina.

Unaweza bila shaka kuona ni kwa namna gani, mawazo yako ya kina yana nguvu. Kwa mfano, mawazo haya ya kina hupokea kiasi cha vitu au mambo 600,000 ya kiufahaumu kwa dakika moja. Hii ina maana kwamba, mawazo hayo yana uwezo mkubwa sana, kuliko unavyofikiri na yana uwezo wa kufanya chochote katika maisha yako.


Ni ukweli yana uwezo mkubwa wa kupindukia. Hadi siku za karibuni, kompyuta ambayo ilikuwa na nguvu kuliko nyingine duniani ile ya clay, ambayo  ina uwezo wa kufanya mikokoto milioni 400 kwa sekunde. Ili kuweza kufanya kazi inayoweza kufanywa na mawazo ya kina kwa dakika moja tu, kompyuta hii inatakiwa kufanya kazi kwa kiwango hicho kwa miaka 100.

Je, huoni kwamba, mawazo yako ya kina yana uwezo wa kuzalisha chochote, kufanya chochote, kubuni chochote na kubadili chochote na kubadili chochote, kutokana na uwezo wake mkubwa sana? Mawazo ya kina ndiye mjenzi wa maisha ya kila mmoja wetu, lakini yanaweza pia kuwa mbomoaji wa kila kitu kutegemea tu unayatumia vipi.

Mawazo ya kina ndiyo mratibu na mdhibiti wa mawazo yetu. Kama ilivyo nyuklia, huweza kutumika vizuri na kuzalisha makubwa au kutumika vibaya na kuangamiza mamilioni. Mawazo yakina yana nguvu kubwa kupindukia na kama kila mmoja angejua namna ya kutumia, dunia ingekuwa haiko hovyo kama ilivyo leo.

Katika hatua za kuanzia, mtu anatakiwa aamini kufikiri vizuri, kufikiri kwa njia ambayo itamsaidia, badala ya kufikiri kwa njia ambayo itamuumiza na kumkera. Kufikiri vizuri ni kuamini kwamba, mtu anaweza, kuamini kwamba, matatizo kwenye maisha ni changamoto na siyo mwisho wa dunia au kushindwa kwako kabisa kama wengi wanavyofikiri.

Kutumia vizuri mawazo yetu ya kina hakuwezi kuwepo kama kufikiri kwetu katika maisha ya kawaida ya kila siku kumeharibika. Tukiwa na hofu, wasiwasi, chuki, visasi, hisia za kushindwa, woga wa kutokea mabaya na kuvunjika nguvu kirahisi, inaweza kuwa vigumu kwetu kuyatumia mawazo ya kina kwa faida yetu.

Mawazo yako ya kina yanauwezo wa kufanya maajabu au chochote unachotaka katika maisha yako kama utaamua kuyatumia vizuri. Kama unataka utajiri au furaha ni jukumu lako kuanza kufikiria kwa vile vitu unavyovitaka na sio vinginevyo, hiyo ndiyo nguvu kubwa ya mawazo unayotakiwa kuitumia na ikakusaidia kukufanikisha katika maisha yako.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea mtandao huu wa DIRAYA MAFANIKIO kwa kujiendelea kujifunza vitu vizuri zaidi, karibu sana.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,



Kama Unataka Kuwa Mtaalamu Katika Shughuli Unayofanya? Soma Hapa.

No comments :
Si kila anayefanya shughuli fulani huwa na utaalamu nayo, wengine wanaifanya kwa kuwa tu nafasi ilitokea  ya kuifanya. Na hautachukua muda kumgundua mtu anayefanya kazi zake kwa utaalamu, na yule anayebangaiza njaa tu, kwa jinsi wanavyoenenda na tabia zao. Mara nyingi
waajiri na wateja hulalamika kuwa anayewafanyia kazi  hana utaalamu.

Yawezekana humalizi kazi vizuri, umemcheleweshea au hata kumzungusha kwa muda mrefu bila taarifa sahihi. Si mara moja tunasikia 
ni jinsi gani tunatakiwa kuwa wataalamu katika shughuli tunazofanya. Kama unataka kupata mafanikio, kuchukuliwa kama mtu makini, kuonekana una mchango kwa unaofanya nao shuguli zako, kuzifanya kitaalamu ndio njia pekee ya kukufikisha huko.

Lakini tujiulize waajiri ama wateja wanatafsiri gani juu ya utaalamu? Wengi wao watakuona mtaalamu ikiwa wewe: Unafika eneo la kazi katika muda unaotakiwa; Unaifanya kazi uliyopewa vizuri; Unamaliza kazi kwa wakati.
Unadhani kuna matukio mengine ambayo unahisi ukiyafanya yatakuonyesha wewe si mtaalamu? Kuna matukio ukiwa unayafanya yanakutafsiri moja kwa moja kuwa wewe si mtaalamu wa shughuli unayofanya.

Kwa mfano ukiwa:- Unachelewesha kazi za watu, unahudhuria vikao ukiwa haujajiandaa, unatumia muda mwingi kuongea umbea muda wa kazi, kuwavunjia heshima wenzako,  kuwasubirisha wateja muda mrefu bila sababu za msingi, kuiba mawazo ya watu wengine kufanyia shughuli zako bila kuwahusisha, na kuvunja ahadi zako mara kwa mara.

Hebu leo tuangalie njia kumi utakazoweza kutumia kuwa mtaalamu katika shughuli yoyote unayofanya. Jitahidi kufanya shughuli zako kitaalamu na watu waweze kukuamini, kukuheshimu, na kukuona una uwezo wa kipekee. Japo mazingira ya kila kazi yanatofautiana lakini linapokuja suala la utaalamu huwa na tafsiri moja dunia nzima.

Hebu tuangalie sifa za kuwa mtaalamu ni zipi:-

1. Umahiri.
Lazima uwe mahiri katika kile unachofanya, ukitumia ujuzi na maarifa ya kutosha katika kazi yako ni lazima utaonekana mtaalamu na watu. Ni muhimu kwako kujifunza hili ili kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa ufanisi ambapo itakupelekea wewe moja kwa moja kuwa mtaalamu katika kile unachokifanya. Na utakuwa mtaalamu kutokana kujifunza kwako mara kwa mara, hivyo ni muhimu kuwa mahiri.


2. Zingatia muda:
Watu watakuwa wanakutegemea wewe ufike katika muda unaotakiwa ili shughuli ziende na umalize kwa wakati. Sio kuendelea kufanya shughuli zako kwa mazoea tu bila kujali muda, kwani hakuna anayependa kumuamini na kumpa kazi mtu asiyemaliza kwa wakati. Kama utaendelea kuwa mtu ambaye sio wa kutunza muda na unajidanganya kuwa eti unataka kuwa mahiri kwa kile unachokifanya sahau katika maisha yako.

3. Uaminifu.
Unatakiwa kuwa muwazi wa shughuli zako, na wale unaofanya ama unaowafanyia kazi nao wajue nini kinachoendelea. Ukianza kujifanya mjanja mjanja, katika shughuli unayofanya huku huwaweki wazi watu wengine hakuna atakayekuona mtaalamu hata kidogo. Matokeo yake utajishushia heshima hasa pale itakapobainika kuwa mambo yako hayaendi sawa kiaminifu zaidi.

4. Uadilifu.
Utaonekana mtaalamu ikiwa utakuwa unasimamia kanuni za shughuli yako. Hakuna anayependa kumpa kazi mtu asiyejua kufuata kanuni za kazi yake. Jifunze kufuata kanuni za kazi yako ili uwe mtaalamu uliyebobea vinginevyo utajikuta unakuwa ni mtu wa kubabaisha katika eneo ulilopo. Zingatia pia misingi ya maadili kati yako na wafanyakazi wenzako hilo ni jambo la msingi.

5. Heshima.
Kama huna heshima kwa watu wengine unaofanya nao au unaowafanyia shughuli basi hautaonekana mtaalamu hata kidogo. Ni muhimu sana kwako kuchunga heshima kwa wafanyakazi wenzako hata kama umewazidi cheo ni lazima uwe na heshima kwao. Kuwa na heshima tambua kuwa hiyo ni nguzo kubwa wewe ya kuweza kukutambulisha kuwa wewe umebobea na ni mtaalamu katika kazi yako na wala si mbabaishaji.

6. Ongeza ujuzi.
Tafuta ujuzi wa ziada, usiendelee kung'ang'ania ujuzi ule ule kila siku. Toka nje ya yale unayoyafahamu ili kupata mengine mapya  kuongezea katika yale unayayafahamu ili kuboresha zaidi utendaji. Kama utaendelea kung’ang’ania kuwa na ujuzi ule ule bila ya wewe kutaka kubadilika na  kujifunza kitu kipya, elewa kabisa utakuwa unajipunguzia sifa za kuwa mtaalamu kwa kile unachokifanya.

7. Mtazamo chanya.
Kama wewe kila siku unaangalia makosa tu bila kuwa na mtazamo chanya juu ya shughuli unayofanya kuwa mtaalamu itakuwa ndoto kwako. Ni lazima uwe na mtazamo chanya ili ujue nini cha kufanya kuliko kuangalia makosa tu kila wakati ambapo hayo makosa yanaweza yakakupunguzia na kasi ya kufanya vitu vingine vitakavyoweza kubadili mwelekeo wako na pengine kukufanya kuwa mtaalamu zaidi.
8. Toa msaada:
Wasaidie wenzako unaofanya nao shughuli sio kwa kuwa wewe unafahamu kitu fulani basi hutaki wenzako wafahamu. Waonyeshe jinsi ya kufanya kazi vizuri pale unapoweza na wasikilize pale wanapokuuliza maswali. Unapowasaidia wenzako ambao unakuwa unafanya nao kazi hii inakufanya kila siku utajikuta unaongeza utaalamu wako katika maisha yako.

9. Tenganisha matukio.
Usihusishe matukio ya nyumbani au mtaani na kazi, ukiwa katika shughuli zako weka mawazo yako yote hapo. Utakuwa mtu wa ajabu kufika eneo la kazi na kuanza kushughulikia masuala ya nyumbani huku ukiacha kazi haziendi. Jifunze kufanya kazi  kwa uangalifu ili usije ukajikuta unaupoteza muda wako mwingi pasipo kujijua hiyo inaweza ikawa ni hatari sana na itapunguza utaalamu wako.

10. Kuwa msikivu.
Kila mtu ana hitaji la kusikilizwa pale anapokuwa na jambo la kusema,
Kwa hiyo wape watu nafasi ya kukuelezea yale wanayodhani yatasaidia katika utendaji wa kazi. Acha kuwa king’ang’azi wa kutaka mipango yako au mambo yako ndiyo yatekelezwe na kusahau usikivu unaotakiwa kuwa nao hata wewe ili kuleta ushirikiano utakaoleta ufanisi hata kwako na kukufanya kuwa mtaalamu zaidi.

Kila mmoja wetu anapenda kupata mafanikio katika shuguhuli ile anayofanya, basi tuanze sasa kufanya kazi kitaalamu ili tuweze kufikia yale tunayoyataka. Nakutakia mafanikio mema, karibu DIRA YA MAFANIKIO uendelee kujifunza na kuhamasika kila siku.

IMANI NGWANGWALU,







Jan 29, 2015

Kama Hupati Matokeo Mazuri Kwa Kile Unachokifanya, Soma Hapa Kujua Nini Cha Kufanya.

No comments :
Umewahi kuona ama kusikia kuhusu watu waliojaribu bidhaa au kufanya biashara hii na ile na kupata mafanikio makubwa lakini unapojaribu wewe hupati matokeo mazuri? Je, umekuwa mtu anayeona hakuna kitu kinachoweza kukusaidia kupata mafanikio makubwa katika maisha yako? Huenda umekuwa ukijaribu kutumia njia fulani za kuboresha maisha yako, inayoonekana  kuwa nzuri sana, lakini umechoshwa sana na kukwama kila wakati.

Mara kwa mara umekuwa ukijitahidi kufanya hiki na kile lakini umekuwa huoni matokeo hasa ya kile unachokitaka. Kuna wakati umekuwa ukijiuliza pengine una mkosi au nini shida? Na imekuwa ikifika wakati unaanza kujihisi kutaka kukata tamaa kwa kile unachokifanya na kuona kuwa maisha kwako tena basi hayawezekani. Hebu tutazame jinsi unavyoweza kuwa umefikia hatua hiyo uliyopo na sababu zinazoweza kupelekea mambo haya kukutokea.

Kwanza, huenda kuna wakati ulijaribu kitu ama kwa kufuata ushauri, ama maelezo uliyosoma, ama kwa kuona mafanikio ya mtu mwingine. Kimsingi, umejaribu njia hiyo kwa kufuata uzoefu mzuri wa mtu mwingine. Hata hivyo ulipojaribu, hukupata matokeo kama uliyotarajia, ukaamua kuamini kuwa haikukusaidia. Lakini mawazo haya ni kweli kiasi gani? Mara nyingi, tena mara nyingi sana, matokeo ya vitu vya aina moja kwa watu tofauti huwa tofauti na ni kosa kujihukumu na kujilinganisha na watu wengine. Pengine ulihitaji muda zaidi. Huenda mazingira yako ni tofauti kabisa.

Bila kujali hayo na jinsi ulivyofikia, ulijijengea ukweli ndani ya nafsi yako na ukweli huo ni kwamba ‘jambo hili halikukusaidia’ ingawa kwa ukweli wa ndani kabisa, ukweli wako huo uliegemea kwa juu kwenye ulinganifu wako na mtu mwingine na ambaye hauna uhusiano wowote wa moja kwa moja nawe na kile ambacho ni bora kwako. Ni vema ukafahamu pia kwamba matokeo na mafanikio yote hayo unayoyaona kuhusu mtu huyo mwingine, yalikuwa kwa wakati ule uliozungumziwa na hiyo haina maana kwamba sasa ni zamu yako kutumia njia ama ushauri huo na kwamba matokeo mazuri kama yale yatakutokea nawe.


Kuanzia hapo, kila kitu utakachokijaribu kitafananishwa na kuhusishwa na matokeo ya kile cha kwanza, huku ukiwa na ukweli ndani yako ambao mwangwi wake unazidi kuunguruma wa ‘hili halikunisadia mara ya kwanza ngoja tuone safari hii kama litaweza’ tayari unakuwa kama unajipiga vita. Inawezekana hukutarajia kushindwa kwa njia ya moja kwa moja, lakini tayari unauona uwezekano huo na uamuzi wako umeegemea kwenye matokeo mabaya ya mwanzo.

Kwa kadri unavyojaribu mambo mengi ukiwa na mawazo haya, ndivyo unavyozidi kuyajenga mawazo haya ndani yako. Hatimaye inakuwa ni dhana iliyojaa ‘hakuna kitu kitakachosaidia.’ Kabla ya kutambua hilo, hiyo ndiyo aina ya mtu utakayokuwa. Mtu unayejaribu kufikia malengo fulani maalumu ama kujaribu kitu hiki ama kile ama teknolojia ile na kuwa na kauli ndani yake kwamba, ‘wengine wanafanikiwa lakini si mimi’

Sasa nini cha kufanya kama hupati matokeo mazuri kwa kile unachokifanya ukilinganisha na wengine? Ni vipi utaweza kijitoa kutoka kwenye mzunguuko huu? Kwanza, fahamu jinsi ulivyofikia huko, kwa kuilinganisha nafsi yako na matokeo ya watu wengine walioko kwenye njia tofauti kabisa nawe, ingawa huenda walikuwa wakitafuta matokeo kama unayoyataka wewe hivi sasa.

Halafu ujijengee dhana yako. Iruhusu nafsi yako kupata mafanikio kimtindo wake, bila kuamua kwa kuangalia kile kilichowatokea watu wengine, au matakwa yaliyowekwa na watu wengine zaidi yako wewe. Na ni pale utakapoamini kwamba unayo haki ya kufanikiwa, na ni kwamba, na ni kwamba utafanikiwa, ndipo maisha yako yatakapobadilika. Kila utakachokijaribu, kitakusaidia kwa sababu, umefahamu kwamba kinatakiwa kukusaidia wewe na si mtu mwingine.

Subira yako ya ndani na kutokuwa na maamuzi ya kabla ya mafanikio unayotaka, yenye kuegemea nje ya nafsi yako, itafanya kazi kwako kwa nguvu kubwa na utarudiwa na uwezo wako na kuweza kudhibiti mwelekeo wa mambo yako. Lakini kikubwa, jiwekee na wewe malengo yako na kuwa tofauti na kufanya mabadiliko kwa kile unachokifanya ukilinganisha na wengine uliwaona, hii itakusaidia kukuletea matokeo tofatuti katika maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,

0713048035/dirayamafanikio@gmail.com






Jan 28, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuishi Katikati Ya Tufani Za Kimaisha.

No comments :
Ukijaribu kutafakari jinsi binadamu anavyokumbana na matatizo magumu ya aina mbalimbali ya kimaisha, huenda unaweza ukahisi hali fulani ya kukata tamaa na hata kujiuliza kwamba, ni kwa jinsi gani binadamu huyu anaweza kukabiliana na hata kujikwamua kutoka kwenye hali hizo zinazokatisha tamaa. Hebu jaribu kukumbuka matatizo ya kiuchumi, ugaidi, magonjwa mabaya ya kuambukiza, vita na migogoro mbalimbali ya kijamii, majanga ya asili na mengineyo.

Yote hayo kwa muda mrefu yamekuwa ndiyo changamoto kubwa kwa binadamu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, bado kuna uwezekano mkubwa kwa binadamu huyu kuendelea kustawi na kushamiri kimaisha pamoja na kuzungukwa na matatizo hayo. Mambo yafuatayo yanaweza kumsaidia mtu katika harakati zake za kuyaboresha na kuyaendeleza maisha yake katikati ya changamoto hizo.

1. Jifunze kuangalia mambo kwa mtazamo chanya.
Litazame kila jambo linalokujia au kukupata kwa jicho lenye mtazamo mzuri na chanya. Katika suala hili inapaswa kukumbuka  kwamba , kunapotokea hali fulani itakayosababisha watu kusongeka, ujue kwamba, siyo lazima kila mtu asongeke na kwamba kunapotokea maradhi mabaya ya kutisha na yanayosababisha vifo, siyo lazima kila mtu afe. Huu ndio ukweli wenyewe, na bila shaka huwa tunahuzunika na kujisikia vibaya, pale tunapoona wenzetu wanateseka. Lakini hata hivyo, mateso yasiyo ya lazima yanatokana na hofu wasiwasi wetu hayana faida kwetu zaidi ya kutuumiza na kutuacha tukiwa wagonjwa hoi vitandani mwetu.



2. Fanya yale unayoweza kuyatimiza, usiyoyaweza achana nayo.
Wakati wote unapaswa kujiandaa kama vile askari wanavyofanya. Ujifunze kuzitupilia mbali hofu zako. Kwa kufanya hivyo utajiongezea uwezo wako wa kustarehe na kuburudika na maisha yako. Kwa kawaida, hofu iliyofika katika kiwango kikubwa na cha kudumu ni nguvu za kukuondolea uwezo wako wa kukabiliana na kupambana na hali ngumu zozote zile zinazokujia. Hivyo, kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya hali hizo za kutisha na kukatisha tamaa, ni jambo muhimu na linalopaswa kuzingatiwa kwa makini ili tuweze kuishi maisha yasiyotuelemea.

3. Yasawazishe maisha yako.
Fanya kila uwezalo, ili uweze kuyasawazisha maisha yako kwa kufanya kazi zako za kila siku kwa bidii, maarifa na kwa kufuata utaratibu uliojiwekea. Pia unapaswa kujiwekea muda kwa ajili ya kufanya mambo yanayokuhusu wewe binafsi, familia yako, hata jamii yako kwa ujumla. Ukiwa unafanya hivi mara kwa mara utakuwa unajijengea uwezo mkubwa wa kupambana na kila hali ngumu inayojitokeza katika maisha yako.

4. Tafakari kwa kina, Sali na uwe mwenye shukrani.
Hebu tafakari, Sali au hata ufikirie kidogo kuhusu Baraka za namna mbalimbali unazozipata ambazo zinatokana na wewe kuwa hai. Unaweza pia ukatembea tembea kwenye maeneo yenye kuvutia na kujiburudisha, kama vile bustanini, kwenye ufukwe wa bahari, na mbali kwingine kotekote unakohisi kwamba, kuna mandhari ya asili. Kutafakari kwa kina ni njia ambayo imethibitika kuwa na nguvu ya kupunguza sononi, na vilevile kuzingatia kwa makini masuala ya kiroho huongeza kwa kiwango kikubwa ile hali ya kuwajali, kuwathamini na kuwahurumia watu wengine.

Ukweli ni kwamba jawabu kwa kila tatizo lipo, hata katikati ya matatizo na vurugu nyingi, bado unaweza kulipata. Hivyo unapoamua kuutumia ushauri huo hapo juu, unaweza kujiongezea amani yako ya akili na kuridhika na maisha yako, mambo ambayo ni muhimukutumika kwenye maandalizi yako ya kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha. Kumbuka tu kwamba, walioweza kuokoka wakati wa mauaji ya halaiki kwenye kambi dhalili za mauaji za Hitler, wengi ni wale waliokuwa na matumaini, wale ambao walikuwa wakijiambia kila wakati kwamba, kila penye vurugu, pana suluhu.

Nakutakia mafanikio makubwa na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







Jan 27, 2015

Sababu Sita Zinazokufanya Ushindwe Kufikia Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako unaweza ukajikuta unafanya kila kitu cha kukusaidia kukufanikisha, lakini ukawa unashangaa mambo yako hayaendi vizuri kama unavyofikiri au kutarajia . Mara nyingi hiki huwa ni kitu cha kuumiza ubongo na inabidi wewe mwenyewe binafsi utulie ili kujua nini chanzo au sababu hasa inayopelekea wewe ushindwe kufikia mafanikio unayoyata katika maisha yako.  Kiuhalisia, huo zipo sababu zinazopelekea ushindwe kufikia mafanikio makubwa, ingawa kwa wengi huwa sio rahisi kuweza kuzijua na kuzitambua kwa haraka. Kama unataka kufanikiwa, hakikisha unazijua sababu hizi zinazokuzuia wewe kufanikiwa.

1.Unatumia muda wako vibaya.
Mara nyingi umekuwa ukiishi maisha ya kupoteza muda wako hovyo. Haya ndiyo maisha ambayo umekuwa ukiishi kwa muda mrefu na umekuwa ukiiona ni kitu cha kawaida tu, kupoteza muda wako bila sababu. Kitu usichokijua ni kuwa muda ni kitu muhimu sana katika kutimiza malengo yako uliyojiwekea. Hakuna mipango wala malengo yoyote hapa duniani, ambayo utaweza kuyatimiza kama utakuwa ni mtu wa kupoteza muda kila mara katika maisha yako.

Ukijaribu kuchunguza kwa makini, utagundua kuwa watu wengi wasio na mafanikio hapa duniani ni wale ambao pia matumizi yao ya muda ni mabovu. Hawa ni watu ambao wanauwezo wakishinda wakipiga soga kutwa nzima wakiongea hili mara lile hata kwa yale yasiyo na maana, ni watu ambao wanauwezo wa kushinda kwenye mitandao ya kijamii karibu kutwa nzima na ni watu pia ambao usishangae ukakutana nao kila mahali wao wapo tu. Kama unaishi maisha haya ya kuchezea muda hivi, nakupa pole, uwe na uhakika utakufa maskini na ndio kitu ambacho kinakufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa.


2.Umekuwa ukiahirisha sana mipango na malengo yako.
Jaribu kujiuliza mwenyewe ni mara ngapi umekuwa ukisema nitafanya hik na hiki kesho na inapofika kesho hufanyi tena na imekuwa kwako sasa kama ni kawaida  na umezoea. Kama utakuwa wewe ni mtu wa kuahirisha mipango na malengo yako uliyojiwekea kaika maisha yako itakuwa ngumu sana kutimiza hayo malengo yako. Kwa sababu hiyo kesho unayoisubiri na kusema kuwa utafanya haitafika.

Kitakachobaki kwako ni kila siku itakuwa kesho kesho na utajikuta ndivyo unavyozidi kupoteza muda wako na fursa muhimu za kukupatia mafanikio katika maisha yako. Kama kweli umemua kufanya mambo yako yafanye sasa hata kama ni kwa kidogo wewe fanya tu. Achana na habari ya kesho, ambayo unaingoja kila mara, hiyo haitafika milele. Kama unataka kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio makubwa, acha kuahirisha mambo yako.

3.Umekuwa ukiishi maisha ya visingizio sana.
Hii ni sababu kubwa sana inayokufanya ushindwe kusonga mbele katika maisha yako kutokana na visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo. Umekuwa ukitoa visingizio mara kwa mara kila kukicha kwa nini hufanikiwi. Hebu angalia ni mara ngapi umekuwaukisema huwezi kuanzisha biashara kwa sababu huna mtaji, ni mara ngapi umekuwa ukisema unashindwa kutoka kwenye umaskini kwa sababu una wategemezi wengi na hujiwezi. Umekuwa una visingizio hivyo ambavyo vyote ni kama unajitetea tu.

Lakini, sababu kubwa inayokufanya ushindwe kufanikiwa katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Unao uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yako ukitaka na hakuna kitu cha kukuzuia. Kama ukiamua leo hii, ukaachana na visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo, elewa kabisa utabadili maisha yako kwa asehemu kubwa sana na utaanza kuishi maisha unayoyataka. Visingizio visiwe sababu yaw wewe kuzuia kufikia mafanikio yako, jifunze kuwajibika na chukua hatua juu ya maisha yako.

4.Umekuwa ukikata tamaa sana mapema.
Haijalishi umeshindwa au umekosea mara ngapi kwa kile unachokifanya, kitu ambacho hutakiwi kufanya katika maisha yako ni kukata tamaa. Unapokuwa unakata tamaa unakuwa una utangazia ulimwengu kuwa mafanikio kwako basi tena. Kukata tamaa ni sababu ya kwanza ambayo inapelekea wewe ushindwe kwa kila kitu unachofanya katika maisha yako. Kama umeshindwa jambo na unafikiria kuwa upo mwisho wa safari na huna sehemu nyingine ya kwenda, tambua unajidanganya nafsi yako.

Umejifunga jela mwenyewe na mawazo yako ya kujikatisha tamaa. Kwa kufikiria hivyo ni kujitengenezea nafasi ndogo ya kufanikiwa katika unalolifanya,na nafsi yako itaanza kuamini wewe ni mtu wa kushindwa. Tunaishi katika ulimwengu wenye njia nyingi za kufanikiwa katika yale tunayojishughulisha nayo. Kumbuka pia wakati mwingine ni lazima kushindwa mara nyingi ili ufanikiwe. Na ndio maana unaposhindwa mara moja sio mwisho wa kila kitu. Wazo lako lolote ambalo limeshindwa kazi,linafungua njia ya wazo litakaloshinda.


5. Umekuwa ukiishi maisha ya kuwa na mitazamo hasi sana.
Wewe ni matokeo ya kile unachokifikiri na kukiamini katika maisha yako. Kama unaamini utafanikiwa ni kweli utafanikiwa na kama uaamini maisha yako ni kushindwa ni ukweli usiopingika lazima ushindwe . Ni mara nyingi umekuwa ukishindwa kufanikiwa na kufikia malengo yako makuu kutokana na fikra hasi ambazo umekuwa ukizibeba sana kila siku. Mara ngapi umekuwa ukiamini ya kuwa mafanikio wamejaliwa wengine na wewe ukijitoa kabisa? Kama unataka kubadii historia ya maisha yako, jifunze kuyaangalia mambo kwa mtazamo chanya zaidi, utafanikiwa.

6. Umekuwa mwongeleaji sana juu ya ndoto zako.
Ili uweze kufanikiwa na kufikia malengo yako ni muhimu sana kwako wewe kuwa mtu wa kuchukua hatua kwa vitendo mapema sana. Kama utakuwa wewe ni wa kuongea na hauchukui hatua yoyote dhidi ya ndoto zako itachukua muda sana ama haitawezekana kabisa kufikia malengo yako. Watu wengi wamejikuta wakiwa ni waongeleaji sana juu ya ndoto zao. Kuongelea sana juu ya ndoto na mipango mizuri uliyonayo hakutakusaidia kitu na ndicho kitu ambacho kimekuwa kikikuzuia ushindwe kufikia malengo yako makubwa uliyojiwekea mara kwa mara.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio makubwa na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,




Jan 24, 2015

Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Mara Kwa Mara Katika Maisha Yako.

No comments :
Habari za leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, naamini umzima na unaendelea na jitihada za kuboresha maisha yako. Nakukaribisha tena kwa moyo mkunjufu katika makala hii ya leo ambayo ipo kwenye mfumo wa simulizi ambapo kupitia simulizi hii utajifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na  maisha yetu kwa ujumla ya mafanikio tunayotafuta kila siku. Kupitia simulizi hii utajifunza na kutambua mambo muhimu ambayo unatakiwa uyafanye na yatakayokuletea mabadiliko makubwa sana katika maisha yako.

Wakati fulani, mtu mmoja alinisimulia kisa ambacho kilinifundisha ukweli mkubwa zaidi kuhusu maisha. Mtu Yule alinisimulia kuwa kulikuwa na bwana mmoja ambaye alienda kwa kinyozi. Wakati anaendelea kunyolewa kulizuka mjadala wa masuala mbalimbali . Mjadala huo, hatimaye ulifika mahali ambapo kinyozi na mteja walijikuta wakijadili masuala ya Mungu. Kinyozi alisema, ‘mimi naamini kabisa hakuna Mungu.’ Yule mteja( Yaani Yule bwana anayenyolewa) alimuuliza, ‘ni kwa nini unaamini kwamba, hakuna Mungu?’

Kinyozi kwa kujiamini kabisa alisema, ‘naamini hivyo kwa sababu, ukienda hapo mtaani hata sasa hivi utathibitisha. Kuna mateso kibao utayaona. Naamini, kama Mungu angekuwepo kusingekuwa na watu wanaoumwa, watu maskini kila mahali, watu wanaouawa bila sababu na uovu ambao umejaa hivi sasa duniani.’ Yule mteja hakuwa anataka kubishana kuhusu masuala ya Mungu, hivyo aliamua kunyamaza. Kinyozi alimnyoa na kumaliza kazi yake, ambapo mteja alitoka nje.

Yule mteja alipofika nje alimwona mtu mmoja ambaye alikuwa na nywele chafu na ndevu nyingi zinazofanana na ukoka kwa uchafu. Kuona vile, Yule mteja alirudi hadi pale kwa kinyozi na alipoingia tu ndani alimwambia, ‘ naamini hakuna vinyozi’. Yule kinyozi alimtazama mteja wake kwa wasiwasi, kabla hajamwambia, ‘hakuna vinyozi wakati mimi unaniona hapa, na nimemaliza mara hii tu kukunyoa?’ Yule mteja alimwambia, ‘kama ingekuwa kuna vinyozi, kusingekuwa na watu wenye nywele ndefu na chafu huko mtaani.’


Yule kinyozi kwa kujiamini kabisa kwamba, ameshinda, alisema, ‘ sasa kama ni kunyolewa si hadi waje hapa ofisini, wanifuate, ndiyo watahudumiwa….’ Yule mteja alimwambia, ‘basi Mungu pia yupo, bali ni hadi wenye shida na matatizo wamfuate na kumjua na kumkubali, ndipo ambapo watapata ahueni kupitia kwake.’ Halafu alitoka nje na kuendelea na shughuli zake.

Ndivyo ilivyo, watu wengi huwa wanadhani kitu au jambo fulani halipo kwa sababu tu hawajui jambo au kitu hicho kinavyofanya kazi. Siyo lazima Mungu, kila kitu kina kanuni ya namna kinavyoweza kujidhihirisha katika hali halisi. Utakuta mtu anakwambia, haiwezekani kufanikiwa kama hujasoma, haiwezekani kufanikiwa kama huna refa, haiwezekani kufanikiwa kama huna au hujafanya kile na kile. Lakini, kati ya hao wanaosema, hakuna hata mmoja ambaye amefanya au amethibitisha nadharia yake.

Ni kwa kuona tu watu wakiwa na shida njiani, wanaamini kwamba ni majibu kwamba Mungu hayupo. Kwa kuona maskini wengi hawana hela wala mali, wanaamini kwamba, hiyo ni dalili ya kutokuwezekana. Kama ilivyo kwa Mungu, hata mafanikio yoyote yale ni lazima mtu ayafuate kule yaliko. Kwa kuyafuata mtu atakutana nayo, kwa kunyoosha miguu tu, ni kweli hatayapata. Kila kitu hapa chini ya jua kinakwenda kwa kanuni, tofauti na watu wengi wanavyofikiri na kudhani.

Kwa hiyo, kama mtu anataka kujua kitu fulani kipo au hapana, inabidi ajifunze kanuni zake. Ni hatari sana kusema haiwezekani kufanikiwa kwa kuwa wewe u maskini au umeshindwa kuyafikia mafanikio unayoyataka, haiwezekani kwa sababu njia zimezibwa. Ni hatari kwa sababu, anachokiona mtu mara nyingi ni umbumbumbu wake au udhaifu wake. Fumbua macho sasa! Ubadili maisha yako kabisa. Achana na fikra za kudhani haiwezekani, tafuta njia kwanini hufanikiwi na kisha songa mbele. Kama utakuwa mtu wa hivi tu, mtu wa kufikiria hufanikiwi kwa sababu zako binafsi zisizo na maana, basi utakuwa umeng’ang’ania kitu kinachozuia mafanikio yako na hiki ndicho kitu kinachokufanya ushindwe mara kwa mara katika maisha yako.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kupata maarifa bora, yakayokuwa msaada mkubwa kwa maisha yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,

0713 048 035/dirayamafanikio@gmail.com 






Jan 22, 2015

Kama Unataka Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa, Acha Kufanya Mambo Haya.

No comments :
Mara nyingi huwa sio kitu kigeni kwa mtu ambaye ni  mjasiriamli wakati mwingine kufanya maamuzi yasiyo sahihi, kukosea hapa na pale na hata wakati mwingine kufanya biashara na watu ambao sio sahihi ambao wanauwezo wa kukurudisha nyuma, hii huwa inatokea sana bila kujua. Hiyo yote inakuja kutuonyesha kuwa katika suala zima la ujasiriamali makosa huwa yapo na ni muhimu sana kuweza kutusaidia kusonga mbele pale tunapochukua jukumu la kujifunza kutokana na makosa. Hata hivyo huwa yapo makosa ambayo huwa tunaweza kuyaepuka ikiwa kweli tuna nia ya kuwa wajasiriamali wakubwa. Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, acha kufanya mambo haya:-

1. Acha kuogopa sana ushindani wa kibiashara.
Ili uwe mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, kitu pekee ambacho hutakiwi kuogopa sana ni ushindani wa kibiashara. Badala ya kuogopa ushindani kaa chini na kisha ujifunze ni kitu gani unachotakiwa ufanye katikati ya ushindani huo mkubwa unaouona. Kama una jiamini na bidhaa zako sokoni au biashara yako huna haja ya kuogopa sana upinzani. Wajasiamali wengi kuna wakati huwa ni waoga sana wa ushindani kiasi cha kwamba hutumia pesa na njia nyingine mbaya kukabiliana na upinzani. Badaa ya kuogopa upinzani, jifunze sana kutengeneza wateja wapya, kuboresha huduma zako na kila siku mafanikio utayaona katika biashara yako na utakuwa umefukia ushindani.



2. Acha kutaka kujihusisha na kila biashara.
Ni muhimu kuzingatia na kuweka nguvu zako zote hasa kwenye biashara yako hususani katika kipindi ambacho biashara yako haijakuwa sawasawa. Katika kipindi ambacho unaendeleza biashara yako ili ikue na kufikia viwangi vya juu unavyotaka acha kupenda kujihusisha na biashara nyingine ambazo zinaweza kukupunguzia nguvu kwenye biashara kubwa. Watu ama wajasiriamali ambao mara nyingi huwa ni watu wa tamaa kwa kutaka kila kinachopita mikononi mwao wakifanye. Hili ni jambo la hatari, kwa sababu mambo mengi hutaweza kufanikisha yote kwa pamoja.

3. Acha kuwa na malengo ya muda mrefu wakati wote katika biashara yako.
Katika biashara kuna wakati mambo huwa yanabadilika tena kwa kasi kubwa sana kuliko. Unapokuwa mjasiriamali  jukumu lako kubwa ni kuhakikisha unaifikisha biashara yako mahali ambapo ni salama hata kama kuna wakati mambo yanabadilika. Hii ikiwa na maana kuwa kuna wakati, inabidi ujifunze kutokufikiria sana biashara yako itakavyokuwa baadae na kujikuta umesahau majukumu yako ya sasa ya kuifanya biashara yako ili isimame na kusonga mbele. Kumbuka si maanishi usiwe na malengo ya muda mrefu katika biashara yako, ninacholenga hapa usifikirie muda wako wote kwa jisi biashara yako itakavyokuwa na kusahau sasa  hiyo ni hatari kwako.

4. Acha kuwa na makadirio makubwa ya faida.
Jukumu kubwa unalotakiwa kuwa nalo kama mjasiriamali ni kuhakikisha unakuza idadi ya wateja kwa jinsi unavyoweza hili ndilo jukumu lako kubwa. Acha kufikiria sana juu ya faida kubwa utakayopata kutokana na biashara hiyo unayoifanya. Kumbuka, kuwa huwezi ukapata faida yoyote ile kubwa kama una idadi ndogo ya wateja. Jifunze mbinu na namna jinsi ambavyo utakavyoweza kuwa na wateja wa kutosha katika biashara yako. Ukifanikiwa hili utaweza kupata faida kubwa sana ambayo unaifikiria uwe nayo katika biashara yako.

5. Acha kutegemea chanzo kimoja cha fedha.
Kama una lengo la kuwa mjasiriamali mkubwa katika maisha yako na hatimaye kuwa huru kifedha, acha kutegemea chanzo kimoja cha fedha. Kama utafanya biashara kwa kutegemea chanzo kimoja cha pesa elewa kabisa hutafika mbali sana kimafanikio kama unavyofikiri. Unapokuwa na vitega uchumi vingi hivi vitakusaidia kuongeza pato lako siku hadi siku na utajikuta mwisho wa siku una kiasi kikubwa cha pesa ulichokikusanya kwa matumizi ya leo na baadae. Wajasiriamali wote wenye mafanikio makubwa hawategemei chanzo kimoja cha pesa ni watu wenye vianzio vingi vya pesa. Kama na wewe unataka kuwa mjasiriamali wa mafanikio, jiwekee vyanzo vingi vya pesa.  


6. Acha kuwa na matumizi makubwa ya pesa.
Ni hatari sana kutaka kukua kibiashara huku ukiwa ni mtu wa matumizi makubwa ya pesa zako. Kama unataka kufika mbali kwenye safari yako ya ujasiriamali, futilia mbali matumizi mabovu ya pesa uliyonayo. Unapokuwa na matumizi mabovu ya pesa unakuwa kama hufanyi kitu, kwa sababu unakuwa unapoteza pesa nyingi sana ambayo ilikuwa haina sababu ya kupotea hata kidogo. Jifunze kutumia pesa zako vizuri na kwa utaratibu maalum unaoeleweka. Ili kufanikisha hili hakikisha unatengeneza bajeti yako,ambayo itakuwa inakuongoza.

Kwa kumaliza naomba niseme hivi, kuwa mjariamali mkubwa na mwenye mafanikio unahitaji kujitoa kikamilifu na wakati mwingine kujikana kabisa na kuachana na hofu yakukabiliana na mambo.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kibiashara na ujasiriamali kwa ujumla iwe ya mafanikio.

Kwa pamoja tunaweza, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi na karibu sana.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,





Jan 21, 2015

Tabia 8 Muhimu Unazotakiwa Kuwa Nazo, Ili Kujenga Maisha Ya Mafanikio Makubwa.

No comments :
Ni ukweli usiofichika ili uweze kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio ya kiwango cha juu ni lazima ubadili tabia zako ulizonazo sasa na kuwa na tabia ambazo zitakuongoza kufikia mafanikio mkubwa zaidi. Unaweza usilione hili mapema lakini huu ndio ukweli, linapokuja suala la kutafuta mafanikio vipo vitu vingi unavyotakiwa kuvifanya na kubadili kama vile matumizi mabaya ya muda na pesa, lakini likiwemo na suala la kubadili tabia ulizonazo ambazo zimekufikisha hapo ulipo. (Unaweza ukasoma pia Kama Unataka Kufanikiwa Na Kuwa Tajiri, Acha Tabia Hizi)

Unapobadili baadhi ya tabia zako unakuwa unajiweka kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako uliyojiwekea. Kumbuka, mafanikio yanajegwa na na tabia ulizonazo, kwa kadri unavyokuwa na tabia za aina fulani, ndivyo mafanikio yanakuwa upande wako na kwa jinsi unavyokuwa na tabia za aina fulani pia utajikuta ndivyo unavyofukuza mafanikio katika maisha yako bila ya wewe kujijua. Ili kujenga maisha ya mafanikio makubwa  unayohitaji, hakikisha  unakuwa na tabia hizi katika masha yako.

1. Tabia ya kuamka asubuhi na mapema.

Unapoamka asubuhi na mapema kabla ya muda uliojiwekea, kabla ya watu        wengine, unakuwa unapata muda wa kutuliza akili yako, kujisikiliza wewe mwenyewe na kupata nafasi ya kutafakari juu ya maisha yako kwa ujumla.  Pia kwa kuamka asubuhi na mapema sio tu itakusaidia kukupa muda wa ziada wa kutafakari juu ya maisha, hiyo itakusaidia pia kukujengea tabia muhimu ya kupangilia siku yako mapema, wapi uanzie na wapi uishie, ambapo tabia hii itakuongoza kwenye mafanikio. Watu wengi wenye mafanikio wana tabia hii muhimu ambayo inawafanya wazidi kufanikiwa. Ni tabia ambayo unaweza hata wewe kuwa nayo ili ikuletee mafanikio mkubwa.


2. Tabia ya kuilisha akili yako kila mara.
Mara nyingi maisha yetu kwa wengi huwa yametawaliwa na kula vyakula vya kila aina, hilo unalijua. Lakini kuna kitu muhimu ambacho huwa haukilishi na kukisahau mara kwa mara. Kitu hiki sio kingine ni akili yako. Kama ambavyo mwili wako unahitaji kula kila siku pia  hata akili yako inahitaji kulishwa tena sana kila siku. Unahitaji kuilisha akili yako kwa kujisomea kila siku na hili ndilo hitaji la msingi unalotakiwa kuwa nalo ili uweze kufanikiwa. Usiache siku ikapita bila kwako kujifunza kitu kitakachobadili maisha yako. Tumia muda wako vizuri jifunze hata kwa dakika 20 au 30 kwa siku, baada ya muda utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako. Hii ni tabia muhimu sana kwako ambayo hutakiwi kuiacha ili kujenga mafanikio ya kudumu.

3. Tabia ya kufanya mazoezi kila siku.

Hata kama ni kwa dakika kumi na tano tu, unahitajika kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kila siku. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa unayotaka, kumbuka unatakiwa kuwa na akili safi ndani ya mwili wenye afya ya kutosha. Unapojenga tabia ya kufanya mazoezi unakuwa unaifanya akili yako iwe nzuri kiafya na kujikuta ukifikiri vizuri zaidi. Isitoshe mazoezi yanakusaidia  wewe kupunguza magonjwa hususani ya moyo na mengineyo mengi ambayo ungeyaweza kuyapata kizembe, kama ungekaa tu bila kufanya mazoezi ya aina yoyote ile, hivyo ni kitu kizuri kwa mafanikio yako unayoyahitaji.

4. Tabia ya kutekeleza mipango yako mapema.

Kuweza kuifanya siku yako iwe ya mafanikio, ni muhimu sana kwako kujiwekea utaratibu wa kupanga mambo yako mapema ikiwezekana siku moja kabla ili kuepuka kuingiliana kwa mambo ambako kunaweza kukwamisha katika mipango yako uliyojiwekea. Utaweza kufanya hivi kwa kuwa na ratiba yako ndogo ambayo itakuonyesha kwa uzuri ni nini ufanye katika siku husika inayofuata. Kuwa na utaratibu huu wa kujipangia mambo yako mapema utakusaidia wewe kufanya mambo yako kwa ufanisi na utalaam zaidi. Ukiwa na tabia hii, itakusaidia sana kufanikisha mipango yako mingi uliyojiwekea.

5. Tabia ya kuzingatia mambo.

Haijalishi unakumbana na changamoto za aina gani sasa, kitu kikubwa unachotakiwa nacho wewe ni kujifunza kutenda kwa uzingativu mkubwa unapotenda mambo yako. Acha tabia ya kuairisha na kusema ngoja nitafanya kesho, hii ni tabia ambayo itakukwamisha na kukurudisha nyuma kila siku. Kama kuna jambo au kitu ambacho ulitakiwa kukamilisha leo leo hata kama ni kidogo ni vizuri ukakamilisha leo ili kesho uingie kwenye jukumu lingine tofauti. Ili uweze kujenga mafanikio, ni muhimu kwako kuwa na tabia ya kuzingatia kila jambo unalolifanya na unatakiwa ulifanye kwa ufanisi mkubwa.

6. Tabia ya kuangalia malengo yako upya.

Ni kweli unaweza ukawa una mipango na malengo mazuri uliyojiwekea, lakini ni muhimu sana kwako kuwa na tabia ya kuangalia au kukagua malengo yako mara kwa mara. Unapokuwa na tabia ya kukagua malengo yako mara kwa mara, nakuyapitia tena tena na kuangalia wapi ulipokosea na wapi ulipofikia inakuwa inakusaidia wewe kusonga mbele na  kuyafanya malengo yako yazidi kuwa hai. Hakikisha kila siku unatenga muda kidogo wa kuyapitia malengo yako upya. Hii ni tabia muhimu sana mbayo unatakiwa kujijngea ili kuweza kufikia mafanikio makubwa yaliyoko mbele yako.

7. Tabia ya kujiamini zaidi.

Hii ni tabia ambayo muhimu pia unayotakiwa kuwa nayo ili kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako. Kwa kawaida linapokuja suala zima la kujiamini kwa wengine huwa ni shida kidogo. Unaposhindwa kujiamini elewa kabisa kwako itakuwa ni ngumu kuweza kufikia kiwango cha mafanikio unachotaka. Kwa nini inakuwa ngumu kufikia mafanikio unayotaka? Hii ni kwa sababu kila kitu ambacho utakuwa unataka kufanya utakuwa unahisi au unajiona kama vile huwezi, matokeo yake utajikuta utakuwa ni mtu wa kushindwa katika mambo mengi hata kwa yale ambayo hukustahili.

8.Tabia ya kufanya kazi kwa bidii.

Kufanya kazi kwa bidii, kuwa king’ang’azi katika malengo yako ni nguzo muhimu sana ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa  katika maisha yako. Ikiwa utaamua kujitoa mhanga na kufanya kazi zako kwa bidii zote na kujifunza vitu muhimu kwa kile unachokifanya, elewa kabisa mafanikio makubwa ni yako. Kama una nia ya kweli ya kutaka mafanikio makubwa, chukua jukumu la kujibidiisha kwa shughuli zako zote unazozifanya. Matokeo na matunda makubwa utayaona upande wako kadiri siku zitakavyokuwa zinaenda mbele. Hata ikifika wakati huoni matokeo mazuri wewe weka bidii hupotezi kitu.

Kwa kawaida tabia zetu ndizo zina nguvu ya kujenga ama kubomoa maisha yetu ya kila siku. Kama unataka maisha ya mafanikio, hakikisha unajifunza kujenga tabia zitakazo kuongoza kwenye mafanikio ya kweli na sio kukwamisha. Chukua hatua muhimu za kubadili na kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,