google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Mar 28, 2015

Hii Ndiyo Sababu Inayowafanya wengi Wawe Na Kisirani Asubuhi.

No comments :
Mara nyingi imeshawahi kukutokea wewe binafsi ama kuona kwa watu wengine mara wanapoamka asubuhi huwa ni watu wa kisirani sana tofauti na muda mwingine. Umeshawahi kujiuliza nini chanzo au sababu yake hasa? Kwa nini asubuhi mtu anapotoka usingizini, kisirani kinaweza kuzuka kirahisi zaidi kuliko wakati mwingine? Huenda jibu hulifahamu. Lakini, wataalamu wasiolala, wakichunguza matukio ya kila siku ya maisha ya binadamu wana majibu.

Kwa kawaida, mtu anapokuwa ameamka kutoka usingizini, akili yake inakuwa ina mawenge na kushindwa kufikiri vizuri. Inahitaji muda kidogo, ili mtu ambaye ametoka usingizini karibuni, kuweza kumudu kufikiri vizuri kwa utaratibu ule wa kawaida. Inaelezwa kwamba, uwezo wa kufanya uamuzi wa hekima unajengwa baada ya mtu aliyetoka usingizini, kupata muda wa kutafakari kwanza.

Kama mtu anatakiwa kufanya uamuzi wa haraka, mara baada ya kushtuka au kuamka kutoka usingizini, inaweza kumwia vigumu sana. Mara nyingi, akili ya mtu ambaye ndiyo ametoka usingizini muda huohuo, inakuwa na aina ya ukungu unaomzuia kufikiri vizuri na kwa haraka.

Inaelezwa kwamba, akili ya mtu ambaye ndio kwanza ametoka usingizini, inakuwa na ukungu kuliko ile ya mtu aliyekosa usingizi kwa saa 26. Hii inakuonesha ni kwa kiwango gani, mtu anapotoka usingizini, anakuwa na hali mbaya katika kufikiri.


Hata hivyo, wataalamu walioshughulikia kujua ukweli unaohusiana na kisirani cha asubuhi kwamba, huchukua kiasi cha dakika kumi hadi ukungu kuondoka akilini, ambapo mtu anaweza kuanza kufikiri vizuri. Lakini hata hivyo, imebainika kwamba, kwa watu wengine huchukua hadi saa mbili tangu kuamka, kabla ukungu wa akili haujatoka.

Utafiti huo bado unaendelea katika kutaka kujua muda hasa ambao akili inachukua kujirudisha katika hali ya kawaida baada ya mtu kuamka. Lakini pia kuangalia athari za watu kama madaktari ambao huamshwa usingizini kwenda kufanya uamuzi mkubwa unaohusu maisha ya mtu. Je, hali hii haiwezi kuwafanya madaktari kufanya makosa ya wazi yanayoweza kusababisha maafa kwa wagonjwa?

Ni juu yako sasa kujua namna ya kuwasiliana na mtu ambaye ndiyo kwanza ametoka usingizini. Kama kuna jambo linaweza kusubiri angalau kwa dakika ishirini baada ya mtu kuamka, ndiyo likasemwa, ni hekima kwa mtu kufanya hivyo. Kuchokoza hisia za mtu ambaye ndiyo kwanza ametoka usingizini kunaweza kuzaa kisirani ambacho vinginevyo kisingeweza kuzuka.

Kwa watu wanaojua jambo hili, huwa hawazungumzi jambo lolote wanapokuwa wametoka usingizini, labda kama ni muhimu sana. Wako wale ambao pia, wanapokuwa na jambo mbalo ni muhimu hawaambii wahusika wahusika, kama ndiyo kwanza wametoka usingizini. Husubiri ‘wachangamke’ kama inavyofahamika.

Unapolazimisha kuzungumza na mtu ambaye katoka usingizi muda sio mrefu kinachotokea mara nyingi ukijibiwa vibaya  au usipojliwa usishangae pia hii ndio huwa hali inayotokea. Na ndio ukweli wenyewe akili inakuwa bado ina maluweluwe. Kwa mujibu wa wataalamu hawa wanadai kuwa mara nyingi unpotoka usingizini hiki ndio huwa kipindi ambacho akili yako yako haifanyi kazi vizuri sana, kwa sababu inakuwa haijachanga sana.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

IMANI NGWANGWALU,



Mar 26, 2015

Kiri Kosa, Jifunze, Jipe Nafasi Ya Kuanza Upya.

No comments :
Katika safari ya maisha, ni jambo la kawaida kabisa kukutana na vikwazo vinavyoweza kukatisha tamaa. Ukubwa wa vikwazo au changamoto hizo, zinaweza kukusababishia ukaiona dunia kama imegeuka, au wakati mwingine ukatamani ipasuke uingie ndani yake.
 
Yapo mambo mengi yanayoweza kukufanya ufikirie hivyo. Huenda yakawa ni makosa ya kibinadamu, matatizo, changamoto, kukatishwa tamaa na baadhi ya watu au kujiponza mwenyewe kutokana na hili au lile. Lakini ukikaa chini, ukatafakari utatambua kuwa hakuna binadamu asiyeteleza kwa kufanya makosa au kupitia changamoto kwenye safari ya maisha.

Hivyo wakati mwingine unapaswa kuelewa kuwa kwa kila linalokupata, bado unayo nafasi ya kufungua ukurasa mpya. Kupatwa na mitihani katika maisha, mara nyingi ni darasa mojawapo tunalotakiwa kuliangalia kwa umakini ili kupata somo au fundisho lililo ndani yake.

Ikiwa mtihani huo umekuja kutokana na kosa ulilofanya, ni vyema kukubali kama umekosea na kisha kujipa nafasi ya kusonga mbele. Tunaelewa kuwa maisha ya kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine yanaendeshwa na misimamo mbalimbali. Kuna wale wanaoamini kuwa wao hawawezi kufanya  jambo Fulani na wakati mwingine kuamini kuwa hawawezi kukosea kabisa.

Ni sawa lakini tukumbuke kwamba hakuna binadamu aliyekamilika kwa kila mmoja wetu anaweza kuteleza na kufanya kosa bila kukusudia . Hivyo basi kwa namna yoyote ile katika maisha yetu kutenda makosa ni sehemu ya maisha. Ni vyema kujifunza kukubali kama umekosea na kujirekebisha.
   
Pili, jifunze kutokana na lile kosa. Si dhani kama leo ukikosea jambo Fulani unaweza kulirudia kosa kama lile siku nyingine. Hata kama ikitokea labda kwa namna nyingine tena. Nakumbuka wakati nikiwa mdogo baba yangu aliniletea zawadi kama pongezi ya kufanya vizuri darasani.
 
Siku hiyo aliponiletea tulikuwa tumekaa na kaka zangu. Alinikaribisha tukiwa pamoja ili iwe chachu kwa wao kufanya vizuri pia. Au pengine kuwafanya waone wivu na wao waweze kufanya vizuri wakiwa shuleni. Basi alinipa ile zawadi. Wakati wa kupokea nilifanya kosa kwa kupokea na mkono wa kushoto. Kwa ukali aliniambia nirudishe ile zawadi akaondoka nayo.

Baada ya kutafakari kwa muda nikakumbuka kumbuka kuwa nilifanya kosa kupokea na mkono wa kushoto kitendo ambacho alishawahi kutusisitizia kuwa siyo cha heshima. Lile lilikuwa funzo kwangu kwani mpaka leo sikuwahi kufahamu ile zawadi ilikuwa ni ya aina gani, kwani ilikuwa imefungwa.

Baada ya kutokea kwa kadhia ile na kuweza kugundua kosa langu, moja kwa moja nilienda kuomba msamaha kwa baba. Tangu siku ile sikuwahi tena kumpa au kupokea kitu chochote na mkono wa kushoto. Hata ikitokea hivyo kama nimejisahau lazima nitaomba radhi.

Ninachoamini mimi ni kwamba kwa hali yoyote ile ni lazima tuyape nafasi maisha yaendelee. Hivyo hatuna haja ya kuangalia nyuma pale tunapojikwaa, kwani utakachoambulia hapo ni maumivu tena inawezekana ukaumia hapo kuliko awali. 

Wapo waliofikia kufanya maamuzi ya ajabu baada ya kukutwa na mtihani au kufanya makosa katika jamii. Wengine hata waliweza kutengwa kutokana na makosa yao. Lakini kushindwa kwao kukubali makosa waliyotenda, kulizaa matatizo mengine. Kwani utakuta ili kuondoa aibu iliyo mbele yao, waliamua kukimbia miji yao na hivyo kwenda kuanza maisha sehemu nyingine. 

Suluhisho pekee la jambo kama hili ni kuomba msamaha na kujipanga upya. Usikubali kukata tamaa kwa kuanguka mara moja, hata ukianguka mara tatu bado unayo nafasi ya kusimama na kuanza upya na kufanya vizuri hata pengine kuliko mwanzo. Kitu kikubwa jiamini kisha chukua jukumu la kusonga mbele kwa kujiamini zaidi, utabadili maisha yako na utafanikiwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha yako.  

  • Makala hii imeandikwa na Suzan Mwillo wa Gazeti la Mwananchi.
  • Mawasiliano suzanmwillo@gmail.com


Mar 24, 2015

Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.

No comments :
Ni jambo ambalo mara nyingi huwa linafahamika na liko wazi kuwa, ili kuweza kufanikiwa na kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa ni lazima suala la kufanya kazi kwa ubunifu, juhudi kubwa na maarifa pamoja na kuwa king’ang’anizi kwenye mipango na malengo yako huwa linahusika kwa sehemu kubwa sana. Hutaweza na huwezi kuwa mjasiriamali mkubwa na kufikia mafanikio makubwa kama utakuwa huzingatii mambo hayo.

Pamoja na kufanya kazi kwa ubunifu, juhudi kubwa na maarifa, kuwa ni nguzo muhimu sana kwako wewe mjasiriamali ili kuweza kufikia mafanikio makubwa, lakini pia huwa kuna kitu cha ziada ambacho ni lazima ukifanye na kukifuata ili kuweza kuona mafanikio hayo unayoyataka. Kitu hiki ni wewe kuweza kujua hatua muhimu za kufuata ili kuweza kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa.

kwa kadri unavyozidi kujua hatua hizi zinakuwa zinakupa nguvu na hamasa kubwa ya kuendelea kung’ang’ania na kushikilia ndoto zako mapaka kuona zinatimia. Hizi ni hatua muhimu sana kwako na kwa kila mjasiriamali mwenye nia na kiu ya kutaka kufanikiwa na kufika mbali hasa katika safari ya kibiashara na maisha kwa ujumla. Je, unajua ni hatua zipi unazotakiwa kuzifuata ili kuwa majsiriamali mwenye mafanikio?

Hizi Hatua 8 Za Kufuata Ili Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.

1. Fanya kile unachokipenda kwa moyo wote.
Watu wengi huwa wana kawaida ya kufanya mambo yale ambayo hawayapendi sana katika maisha yao. Hii huwa inatokea au wanafanya hivyo kwa lengo hasa la kuingiza kipato.  Kutokana na kufanya mambo kwa kutopenda iwe kazi au biashara  hii  mara nyingi husababisha kutokuwa na mafanikio makubwa kwa kile wanachofanya.

Mafanikio huwa hayawezi kupatikana kwa sababu unapokuwa unafanya kazi ambayo huipendi kikubwa kinachokutokea utajikuta unakuwa ni mtu wa kulalamika sana na pia unakuwa unakosa ubunifu kitu ambacho ni hatari na  kitakufanya ushindwe moja kwa moja kwa kile unachokifanya. Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa, chagua kitu kimoja unachokipenda na kifanye kwa moyo wote, mafanikio makubwa utayaona.


 

2. Anza kwa kidogo.
Ni ushauri ambao pengine umewahi kuusikia mara nyingi  kwa namna moja ama nyingine, lakini na mimi napenda kukumbushia leo kwa kile unachotaka kukifanya kwenye biashara yako hiyo anza kwa hatua ndogo kwanza. Unapokuwa unaanza kwa kidogo inakuwa inakusaidia wewe kuweza kupima kama utaweza kwenda kwa hatua nyingine zaidi.

Acha kuogopa wala kukatishwa tamaa na kitu chochote katika maisha yako kwa kuhofu kuwa pengine hayo malengo yako hayawezi kutimia. Kila kitu kinawezekana na hakuna kitu kinachoshindikana kwako hata kidogo. Anza kutekeleza malengo yako kidogo kidogo hata kama ni makubwa vipi, lakini tambua kuwa ni lazima uyafikie.

3. Jifunze kutoka kwa wengine.
Hautaweza kufanikiwa kama utakuwa tu unaendesha biashara yako wewe mwenyewe na kushindwa kujifunza kutoka kwa wengine. Unapojifunza kutoka kwa wengine inakuwa inakusaidia kukupa wewe kuweza kutambua mapungufu uliyonayo ambayo yanaweza kukukwamisha na kukusaidia kuweza kusonga mbele zaidi.

Hata hivyo unaweza pia ukajifunza mikakati na mbinu za ujasiriamali zaidi kwa kujisomea kutoka kwa wajasiriamali wengine wakubwa kupitia vitabu ambapo nako huko utapata maarifa  bora yatakayokutoa hapo ulipo. Kama una nia na shauku kubwa kweli ya kutaka kufanikiwa na kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa ni lazima ukubali kujifunza kutoka kwa wengine kila siku.

4. Chukua hatua mapema.
Kusoma sana hakutakusaidia kitu hata kama utasoma vipi hiyo itakuwa ni sawa na kazi bure kama tu utakuwa huchukui hatua kwa vitendo kufanyia kazi kile kidogo unachojifunza. Kuwa mtu wa vitendo ni hatua muhimu sana kwako wewe ya kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa katika safari yako ya ujasiriamali na biashara.

Watu wengi wenye mafanikio makubwa siku zote huwa ni watu wa vitendo tu. Ndani ya maisha yao huwa yametawaliwa na vitendo na huwa ni watu ambao hawajui kitu kinachoitwa kuahirisha mipango waliyojiwekea. Jifunze kuchukua mapema katika kila kitu unachokifanya katika maisha yako, hiyo itakusaidia kufika mbali sana katika maisha yako. 

5. Kuwa na mipango imara.
Kila kitu unachokijua wewe chenye mafanikio makubwa hapa duniani, huwa kinaanza na mipango tena mipango iliyoimara. Hata biashara yako inahitaji kuwa na mipango mathubuti na imara ili iweze kufanikiwa zaidi na kukuletea matunda unayoyataka. Kinyume cha hapo utabaki ukilaumu tu kuwa mambo magumu kama wengine wanavyofanya.

Jifunze kujiwekea mikakati na mipango endelevu kwa biashara yako. Hakikisha mipango utakayojiwekea iweze kukusaidia kuisimamisha biashara yako na kuwa imara zaidi kwa miaka mingi zaidi. Chukua muda wa kutafakari na kujiuliza baada ya miaka miwili, mitatu au mitano kuanzia leo utakuwa umefika wapi kibiashara? Kuwa na mipango imara ni nguzo muhimu ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyahitaji.

6. Tengeneza ‘timu’ imara itakayokusaidia.
Mara nyingi huwa hakuna jeshi la mtu mmoja au mafanikio makubwa yatakayoonekana kwa mtu mmoja pekee. Kuna wakati katika maisha yetu huwa tunalazimika kutafuta watu watakaotusaidia katika biashara zetu hilo ni lazima. Hii huwa ni muhimu sana kwa sababu sio kila kitu tutaweza kukifanya sisi wenyewe tunahitaji wasaidizi ambayo ndiyo timu yenyewe.

Katika zoezi zima la zima la kujenga timu hakikisha unatafuta watu ambao watakusaidia kupigania kile unachotaka kitimie katika maisha yako. Nikiwa na maana kuwa timu yako inatakiwa kuwa msaada na kuweza kufanya kazi na wewe bega kwa bega mpaka malengo yako uliyojiwekea yanatimia yanatimia. Kuwa na timu imara ni kitu muhimu sana katika safari yako ya ujasiriamali.

7. Acha kufikiria kuwa umechelewa.
Unaweza ukawa unakwama au kushindwa kuendelea mbele kama inavyotakiwa iwe katika biashara yako, kutokana na mawazo ambayo unayo ya kuhisi kwamba pengine umechelewa kwa kile unachotaka kukifanya. Kwa mawazo haya yamekuwa yakikupelekea wewe kushindwa kufanya mabadiliko makubwa  yako katika biashara.

Kitu usichokijua hakuna kitu kinachoitwa kuchelewa katika maisha yako. Wapo watu ambao mwanzoni walijihisi na kujiona wamechelewa katika maisha yao, lakini walipokuja kugundua ukweli huu walikuja kufanya mabadiliko makubwa sana. Kisikuzuie kitu chochote kufikia ndoto zako. Unaweza ukawa na maisha yoyote unayotaka ukiamua.

8. Kuwa na mitazamo chanya.
Hiki ni kitu muhimu sana kukufikisha katika ngazi ya juu ya mafanikio na hatimaye kuwa tajiri kama utaamua kuwa na mitazamo chanya. Unapokuwa na mitazamo chanya inakuwa inakusaidia kukupa hamasa na nguvu ya kuona mambo yako yanawezekana hata katika maeneo ambayo kweli yanakuwa yanachangamoto.

Ikumbukwe kuwa watu wengi huwa wanakosa kufikia mafanikio makubwa kibiashara kutokana na kuwa watu wa hasi sana katika maisha yao. Hali hii huwa inawapelekea wao kushindwa kukabiliana na changamoto hata zile ndogo ambazo walikuwa wanauwezo wa kuzivuka. Kuwa na mawazo chanya ni muhimu sana kwa mafanikio yako.

Kwa kumalizia, ukumbuke kuwa kiu ya mafanikio yako unayoitaka uitimize itafanikiwa tu endapo, utakuwa mtu wa kujifunza na kuchukua hatua muhimu zitakazoweza kubadili maisha yako. Chukua hatua leo na acha kusubiri kesho au kesho kutwa utakuwa umechelewa sana na hautabadili kitu. Hizo ndizo hatua muhimu za kufuata ili kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,




  

Mar 21, 2015

Sifa 15 Ambazo Matajiri Wa Kweli Huwa Nazo.

No comments :
Ni ukweli uliowazi kwamba ili uweze kuwa tajiri wa kweli katika maisha yako huwa kuna sifa zake muhimu ambazo zinamfanya tajiri huyu wa kweli aweze kutofautiana na tajiri Yule ambaye anaweza kuwa ametumia njia za mkato ama ujanjaujanja fulani ambao huweza hata kuwaumiza wengine kihisia au kimwili ilimradi tu kuweza kufikia utajiri huo anaoutaka. Sifa hizi ndizo huwa zinaleta upekee na kuwafanya matajiri wa kweli kuwa muhimu sana duniani.

Sifa za matajiri wa kweli ambazo tunazizungumzia katika makala hii, ni za wale matajiri  ambao wameamua kupigania maisha yao kutoka chini kabisa mpaka kufanikiwa, ni wale ambao wameamua kutumia nguvu ya kuamua na kuvikabili  vikwazo mpaka kufanikiwa. Swali ambalo unaweza ukawa umeshaanza kujiuliza ni sifa zipi ambazo matajiri wa kweli huwa nazo, ambazo hata wewe unaweza kuzitumia katika maisha yako na kukuwezesha kuwa tajiri?

Hizi Ndizo Sifa Ambazo Matajiri Wa Kweli Huwa Nazo.

1. Wamenuia.
Watu wenye mafanikio wanakuwa wamenuia kufanikiwa. Wanachapa kazi na kila mara wanajifunza mambo mapya. Wanafanya kila jambo ambalo litawawezesha angalau kufanikisha ndoto zao. Ndani ya nafsi zao wanakuwa na shauku kubwa ya kufanikiwa hali ambayo inapelekea wafanye kila linalowezekana hadi waweze kufanikisha hizo ndoto zao.



2. Wamedhamiria.
Ukiwa una dhamira kubwa, utasababisha mambo yako mengi, kusonga mbele. Watu wenye mafanikio huwa wepesi sana kujua mambo gani ni ya kuyafatilia na mambo gani ya kuyapuuza. Kwa mambo waliyodhamiria huamua kufanya kazi kwa nguvu kubwa hadi kufanikiwa katika malengo yao.


3. Hujitoa mhanga
Mara nyingi watu wenye mafanikio hujitoa mhanga lakini zaidi zaidi ni majasiri . Wako tayari kuwekeza na kufanya maamuzi yanayoonekana  kuwa ya HATARI kwa watu wa kawaida. Katika suala zima la kujitoa mhanga huwa hawaogopi kitu na hawajali nani atasema nini? Wanachoangalia ni matokeo ya mbele yatakayowasaidia.

4. Hawakati tamaa.
Hawana msamiati wa “kukata tamaa” kwenye kufikiri zao na hata kuzungumza kwao au hata kwenye hisia zao. Hakuna kitu kama hicho kwenye ubongo wa mtu mpenda mafanikio. Wanaendelea kusonga mbele hata kukiwa na vikwazo lukuki. Wanachojua ni kufanya kazi mpaka kuweza kutimiza kile wanachokihitaji katika maisha yao.

5.Wabunifu.
Kila mtu anapenda kufanya maamuzi ya ubunifu katika maisha yake kwa kiasi fulani. Lakini watu wenye mafanikio wamegundua kwamba kuzama kwenye mafanikio huku ukiwa ndani mwako una ubunifu ni kitu muhimu sana katika kupata mafanikio unayoyahitaji. Kwa hiyo watu wote wenye mafanikio, wamezama sana kwenye ubunifu ili kupata matokeo wanayoyataka.

6. Ni wenye ndoto.
Ili kuweza kuishi maisha yenye maana, binadamu hana budi kuishi maisha yenye ndoto katika mipango na malengo muhimu aliyojiwekea. Watu wengi wenye mafanikio, kwa kawaida wanakuwa wametumia muda mwingi wakifikiria ni aina gani ya ndoto waitimize katika maisha yao. Wanapokuwa wameipata huweza kuifanyia kazi kwa nguvu zote mpaka kuweza kufanikiwa kwa kile hasa ambacho wanakuwa wamelenga katika maisha yao.


7. Hupenda kujifunza.
Wat wenye mafanikio mara nyingi huwa wana sifa ambayo huwa ni ya pekee ambayo huwa inawatofautisha kabisa na watu ambao hawana mafanikio. Sifa hii muhimu ambayo huweza kuwa nayo ni sifa ya kupenda kujisomea. Watu wenye mafanikio mara nyingi huwa ni watu wa kujifunza siku zote na huwa hawaachi. Kutokana na kujifunza huku kupitia vitabu na semina mbalimbali hujikuta wana maarifa mengi sana ambayo huweza kuwasaidia na kuwafanikisha kwa kiasi kikubwa kusonga mbele.

8. Wana uwezo wa kubadilika.
Watu wapenda mafanikio huenda kufuatana na upepo. Kuwa king’ang’azi, bila kusoma hali za nyakati za upepo na maisha yanaendaje kwa wakati huo kuna wakati kunaweza kukupeleka kuzimu. Watu wenye mafanikio wanaweza kubadili mwelekeo muda wowote ule hata bila kutarajia, hii ni moja ya sifa muhimu ambayo hata wewe unatakiwa uwe nayo.

9. Hawaogopi kutoa maamuzi.
Wahenga walisema, uwe mwepesi kutoa maamuzi na nenda polepole katika kubadili maamuzi. Watu wenye mafanikio ndivyo walivyo. Wanafanya maamuzi ya haraka na kuangalia mbele zaidi katika maisha. Kuwa mtu wa kigugumizi sana huweza kupunguza nguvu ama mwendo wa kuelekea kwenye mafanikio yako.

10. Watulivu.
Ni ukweli usiopingika mafanikio huchukua muda kuweza kuyajenga. Matajiri huwa sio watu wa kupenda mafanikio ya haraka kama unavyofikiri bali huwa ni watu wa kujiwekea mipango na malengo hadi kufanikisha kile wanachokihitaji. Huwa ni watu ambao sio wa kulazimisha mambo katika maeneo ambayo hayawezekani hasa katika njia  za mkato huwa hawaamini hilo. Huwa ni watu wa subira kuhakikisha mambo yanaenda katika uhalisia wake.

11. Wanajifahamu.
Ili kuwa mtu mwenye mafanikio huna budi kujijua uwezo wako ulionao na hata mapungufu uliyonayo ili kama ni kujirekebisha uweze kujirekebisha na kuweza kusonga mbele. Watu wenye mafanikio mara nyingi hujijua undani mwao, wanataka nini na kitu hicho wakitakacho watakipataje. Wanajua viwango vyao na hawavipunguzi zaidi ya kuviboresha.

12. Wawazi.
Watu wenye mafanikio mara nyingi huwa wawazi katika mambo yao. Kile wanachoongea ndio huwa wanamaanisha na sio tofauti na hapo. Huwa hawaoko tayari kuuma maneno, kama jambo haliwezekani watakwambia haliwezekani tu. Lakini zaidi ya hapo watu hawa huwa wako tayari kupokea habari zozote ambazo zinaweza kusababisha kufanikisha ndoto zao zifanikiwe bila kinyongo.

13. Ni watu wa kawaida.
Watu matajiri ni watu wenye furaha sana katika maisha yao na huwa hawana makuu hata kidogo. Huwa ni watu ambao wapo karibu sana na familia zao na kupata muda wa kuburudika. Ni watu ambao unaweza kupishana nao mara kwa mara kadhaa kutwa usijue kwamba wanauwezo mkubwa ndani mwao. Ni watu wanaojua kujichanganya kirahisi na hawauoni utajiri wao kama kitu cha ajabu sana, hivyo hujikuta ni watu wa kujali sana wengine.

14. Watu wa kiroho.
Hawa mara nyingi huwa ni watu wenye mambo ya kiroho. Wanaamini kwamba maisha yao sio tu maumbile ya nje bali hata mambo ya ndani mwao. Wanaamini kuongozwa na roho. Kumbuka sizungumzii dini hapa, bali nazungumza maisha yaliyo juu ya uhitaji na utashi wa mwili, hisia na akili.

15. Ni watu pia wa kuburudika.
Kuishi maisha mazuri haina maana kuwa kwamba ni kazi..kazi..kazi.. haina maana hiyo hata kidogo. Matajiri wa kweli na wenye furaha mioyoni mwao huwa ni watu wenye furaha na ni watu wanaopata muda wa kupumzika, wakifurahia upande wa pili wa maisha yao.

Kwa kuishi maisha ya kuwa na sifa muhimu ambazo matajiri wa kweli wanazo ni njia bora kabisa itakayokufikisha kwenye mafanikio ya kweli ambayo dunia inayahitaji. Hizo ndizo sifa ambazo matajri wa kweli huwa nazo na kuweza kuzitumia katika maisha yao ya kila siku.

Kwa pamoja tunaweza kuyafikia mafanikio makubwa tuyoyahitaji katika maisha yetu, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maaarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,





Mar 19, 2015

Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako unaweza ukajikuta ama unatamani sana uwe katika ngazi fulani ya mafanikio, lakini ni kitu ambacho huwa hakitokei kwako. Wakati mwingine umekuwa ukidhamiria na kuamini kwamba, lazima itakuwa, lakini huwa haiwi kama unavyofikiria. Pamoja na juhudi nyingi ambazo umekuwa ukizifanya, zimekuwa ni kama kazi bure kwani mara nyingi umekuwa ukishindwa kupata hasa kile unachokihitaji katika maisha yako ambacho ni mafanikio.

Pengine umekuwa ukijitahidi hata kufanya sala au tahajudi(Meditation) ili kuweza kubadili mwelekeo na kuweza hata kufanikisha kile unachokihaji, lakini wapi mafanikio hayo umekuwa huyaoni. Ni kitu ambacho kumekuwa kikikuchanganya na kushindwa kuelewa unakosea wapi hasa na ufanye nini? Hali hii imekuwa kuna wakati inataka kukuvunja nguvu na kukufanya uamini kuwa, suala la kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako ni kitu ambacho hakiwezekani.

Katika hali ya kushangaza umekuwa ukiona wengine wakijaribu kuomba mara moja na kuweza kufanikisha jambo lile, wakati kwako inakuwa ni vigumu sana, ingawa kama ni kudhamiria, na kuamini kwamba itakuwa ni kulekule na pengine zaidi kwa hilo linaloshindikana. Hali ama matokeo kama hayo yamekuwa yakikutisha tamaa na kukupelekea wewe kutaka kuamini kuwa una kitu kama mkosi au laana fulani hivi inayokuzuia ushindwe kufanikiwa, kitu ambacho sio kweli hata kidogo.


Bila shaka kwa namna moja au nyingine unaweza ukawa umewahi kukutana na hali hii katika maisha yako ambayo pengine imekuwa ikikuumiza kichwa na kushindwa kuelewa kabisa ni kitu gani kinachopelekea wewe usiweze kupata matokeo mazuri kwa kile unachokihitaji katika maisha yako?

Ingawa ukweli ni kwamba, kuamini kwamba inawezekana na kudhamiria kumudu, huweza kuzaa au kutozaa matunda kwa sababu moja tu kubwa. Huwa kunakuwa na kusigishana au kupingana kati ya kile ambacho mtu anachoamini na kile ambacho anadhamiria au kupania kiwe katika maisha yake na hiki huwa ndicho kitu kinachokufanya usipate kile unachokihitaji katika maisha yako.


Kama mtu  kwa mfano, anadhamiria au anapania kwamba, anataka kuona uhusiano wake na mke wake au mume wake unakwenda vizuri, huku akiwa anaamini kwamba, wanawake hawaaminiki, au wanaume ni wakorofi, uhusiano huo hauwezi kuwa mzuri, hata kama amepania na kusali vipi kwake uhusiano mzuri hauwezi kutokea. Unajua ni kwa nini?


Iko hivi, mara nyingi kupania au kuamini kwetu kwamba, inawezekana na kutaka kwetu jambo liwe kama tunavyotaka, sala zetu na maombi yetu, vyote hivi huwa vinafanyiwa kazi na mawazo yetu ya kina. Sasa, kama kuna kitu kingine ambacho ni kinyume na kile tunachotaka au kupania kiwe, ni wazi tunakuwa tunayachanganya mawazo ya kina na inakuwa ni vigumu sana kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.

Kama kweli tunataka uhusiano wetu uwe mzuri na tunaamini kwamba, inawezekana, lakini huko kwenye mawazo yetu ya kina tunaamini kwamba, wanawake ni dhaifu, hatutaweza kupata tunachotaka kwa sababu, mawazo yanakuwa  yanapokea taarifa au imani mbili zenye kukinzana au kupingana.

Kwa kuamini kwamba, wanawake ni dhaifu, lile wazo la kwamba inawezekana kuwa na uhusiano mzuri na bora sana litatupwa nje na kufanyiwa kazi lile lililokuwa hapo awali. Ni hadi ile imani kwamba, wanawake ni dhaifu iondolewe, ndipo ambapo kudhamiria au maombi yatafanya kazi.


Utakuta mtu anasali kila siku na kuamini kwamba, atafanikiwa katika jambo fulani, lakini anakuwa ana imani kwamba, rangi yake itamponza kwa sababu, anashindana na watu wenye rangi nyingine. ‘Wenzetu wale wanajua namna mambo haya yanavyofanywa’, atawaza. Kwa hiyo, dhamira na sala yake vitatupwa nje na hili la ‘wenzetu’, ndilo litakalofanyiwa kazi.

Imani zetu, ambazo tuliwekewa kwenye mawazo yetu siku za nyuma kwenye malezi au mazingira tulimokulia, zinakwenda kwa kina kirefu hivyo zina nguvu zaidi. Tunapoleta imai mpya zenye kukinzana na zile za zamani, hizi mpya ni lazima zitupwe nje au tuseme haziwezi kufanyiwa kazi kabisa kwenye mawazo yetu ya kina na kujikuta hatuwezi kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.

Hebu jaribu leo kufikiria ama kutengeneza orodha ya mambo ambayo umekuwa ukiyaomba au ukitaka uyafanikishe katika maisha yako na umekuwa ukiamini kwamba yanawezekana na umekuwa ukifanya kwa kupania, lakini bado hayakubali. Kama utayapitia vizuri na kurudi nyuma, utabaini kwamba, huenda kile ulicholishwa utotoni kuhusu kutowezekana kwa mambo hayo, bado kina nguvu kubwa kwenye mawazo yako ya kina.

Ili sasa uweze kumudu kupata kile unachokihitaji katika maisha yako ni muhimu sana kwako, kusafisha kwanza mawazo yako kuhusu yale mabaya yaliyowekwa humo kuhusiana na jambo ambalo unataka kufanikiwa kwalo. Kila kitu utaweza kukifanikisha katika maisha yako kama hakuna kukinzana ndani yako. Kumbuka na tambua kuwa kukinzana ndani mwako ndicho kitu kinachopelekea ushindwe kupata kile unachokihitaji katika maisha yako.

Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kwa ajili ya kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,




Mar 17, 2015

Kama Unatafuta kitu Hiki Katika Maisha Yako, Utateseka sana.

No comments :
Hebu fikiria, jaribu kufikiria, halafu karibia kuamini au amini kabisa kwamba, una vitu vifuatavyo. Una magari ya kifahari kumi, nyumba za kifahari mbili kila mkoa kwa mikoa yote Tanzania, mashamba ya ekari elfu moja kila mkoa na fedha zipatazo shilingi bilioni kumi benki. Hebu fikiria.

Najua unaweza kujenga taswira, kama tunavyofanya wakati tunapoota ndoto za alinacha, hadi kufanya hali ionekane kuwa ni kweli. Hebu fikiria tena kwamba, kwa sababu ya mali hizo umekuwa maarufu katika nchi za afrika mashariki na kati. Hebu fikiria kwamba, unaandikwa na kutajwa magazetini, redioni na kwenye televisheni.

Jione kwenye hizo fikra zako kwamba, hayo ndiyo maisha yako, tajiri na maarufu. Halafu endelea kufikiria kuhusu maisha yako. watu wanakujua, wanakuogopa, wanakushangaa na kukunyenyekea. Kila unapoenda unajua watu wanakutazama na kutamani wangekuwa kama wewe labda.

Endelea kufikiria kwamba, umekuwa tajiri na maarufu tangu mwaka 1990 hadi leo. Hebu jaribu kufikiri kwa makini zaidi, baada ya kusifiwa, kuogopwa, kunyenyekewa na kufahamika kila kona , halafu kingefuata kitu gani? Ni kitu gani ungekuwa umekipata? Sawa, umesifiwa na kufahamika na ukajisikia vizuri. Halafu inakuwaje baada ya kujisikia vizuri kwa muda wote huo?

Katika kufikiri kwako, unadhani bado utaendelea kujali kusifiwa na kunyenyekewa? Hapana, haiwezekani. Baada ya muda fulani wa kusifiwa na kunyenyekewa, utagundua kwamba, hakuna chochote ndani ya sifa hizo na kunyenyekewa huko. Kwanini? Kwa sababu, wewe siyo kusifiwa na kunyenyekewa, wewe ni wewe hiki ndicho kitu hasa nataka ukijue vizuri hapa.



Lakini, hata kama utaendelea kusifiwa na kujisikia vizuri, halafu itakuwa ni kitu gani? Hebu fikiria kwamba, kila asubuhi ukiamka, magazeti yamendika kuhusu wewe kwa sifa zote, hata bei ya viatu vyako, televisheni zinakuonesha  ukipanda gari lako la kifahari na kwenda uendako na redio zinazungumzia juu ya fedha na utajiri wako sana tu. Hebu fikiria, unadhani itakusaidia kitu gani  hiyo?

Mwisho wa sifa hizo ni upi hasa? Unaposifiwa ni wapi panajisikia vizuri, ni sehemu gani  ya mwili inapata furaha au starehe? Lakini, gharama ya kulinda sifa na kunyenyekewa huko unaijua? Huwezi kuijua kwa sababu hujaingia kwenye sifa na kunyenyekewa na watu. Ukiingia na wale ambao tayari wameshaingia, wanataka kutoka, hawataki tena ‘balaa’ hilo.

Mcheza soka maarufu wa siku za nyuma kidogo, David beckam aliwahi kusema, maisha yake ni upuuzi mtupu kwa sababu ya umaarufu, Diana aliwahi kujuta kufahamika kwake. Unapotafuta mafanikio kaa chini ujiulize kweli unataka mafanikio hayo makubwa hasa au unatafuta sifa tu ili watu wakujue?

Halafu jiulize tena wakishakujua nini kinatokea? Tunawajua akina Bush, Tunawajua akina Neymer, hata pia tunawajua akina Tyson. Halafu kuwajua kwetu kunawapa kitu gani, kinatokea kitu gani? Wanaendelea kuwa watu walewale, wanaendelea kuwa binadamu na kama sisi, miili yao itapotea hivi pindi.

Kuna profesa mmoja kwa jina alipata kufahamika kama Yunus, ambaye ni raia wa Bangladesh. Huyu alikuwa ana Benki ambayo iliweza kukopesha na kubadili hali za maisha ya familia karibu millioni tatu(siyo watu, ni familia) nchini humo.

Lakini, pamoja na uwezo huo aliokuwa nao yeye alipata kuishi kwenye nyumba ya kawaida tena ya kupanga. Hiyo yote inaonyesha profesa huyu alikuwa hataki sifa wala kunyenyekewa na kuandikwa kila mahali kwenye magazeti hilo lilikuwa sio lake, kikubwa alichokuwa akitafuta ni mafanikio katika maisha yake na ambayo yatasaidia na wengine.

Tuna watu katika jamii yetu tunayoishi, huwa ni watu wa kupenda sifa sana kiasi cha kujiita waheshimiwa. Si ajabu huwezi kuwashangaa watu hawa wakilewa sana kwa lengo la kutaka kuonyesha jeuri ya pesa kiasi cha kwamba mpaka kuweza kusahau nyumbani kwao.

Inadaiwa kwamba kwa watu kama hawa, ili akupe stahili yako, hata kama ni madaraka kazini, lazima umnyenyekee. Kama ametoka ndani, ni lazima uhakikishe unamkimbilia, kupokea mkoba na kujidai hata kama kumfuta vumbi kidogo kwenye suti hata kama haina vumbi.

Halafu unajiuliza, ni ya nini yote hiyo? Ni huyuhuyu ambaye anakunywa pombe hadi anasaidiwa kuingia garini? Kwanini anywe kiasi hicho? Pesa na umaarufu aliodhani utampa nafuu, vimeshindwa kufanya kazi hiyo. Sasa ina maana gani, utajiri na umaarufu?

Labda utajiri kama ule wa Profesa Yunus ndiyo utajiri tunaoutaka. Utajiri unaoangukia mikononi mwa watu waliokamilika, kimwili, kihisia, kiakili na kiroho. Huu utajiri mwingine ni visu vyenye kuwachanja walionao na kuwakatia wanaozunguka. Umaarufu tunaoutaka, hauna kitu kwa sababu, hata kama ungekuwa maarufu vipi, polepole umaarufu utafifia na maisha yako ya mwili hayazidi miaka 120.

Sasa kusifiwa kwa miaka 120 tu, kuna maana gani, kunakusadia kitu gani, wakati hata dini yako haikwambii kuwa itaishi milele. Umebaini kwamba, hukuja duniani kutafuta sifa na umaarufu, bali umekuja kuishi ili ufurahie maisha yako. Mara nyingi tunamtaja Bill Gates kila siku unafikiri anajali hilo? Unafikri anajali kutajwa huko, ambao ni mtihani mgumu kuliko kutafuta mali na utajiri alionao.

Ndiyo maana unaweza kukuta mtu amenunua kagari na kujenga kajumba, halafu anamtukana na kumdharau kila mtu. Anakwenda kwa wanamziki wamtaje jina lake kwenye nyimbo zao, anakwenda kwenye televisheni kujidai anasaidia watoto yatima. Anatafuta sifa na kutaka watu wamjue. Halafu wakishamjua ndiyo iwe nini?

Akiishiwa, anajifungia ndani, anachanganyikiwa, anajenga uadui na kila mtu, anadai amelogwa. Anakuwa anababaika kwa sababu amepoteza kile alichodhani ndicho yeye, mali na umaarufu. Hajui kwamba, yeye yupo kama binadamu na ni kamili  bila chochote. Ni lini binadamu atainua macho na kuuona ukweli? Inaniuma sana.

Kutafuta kujulikana ni kutafuta kuinuliwa kutoka pale ambapo mtu anaamini yupo(Chini) ili ajisikievizuri. Mtu ambaye anajua yupo anapostahili hana haja ya kutaka ainuliwe kutoka hapo nakupelekwa mahali ambapo atahisi kustahili.
Kutaka sifa ni kutaka kuondolewa kwenye tope, kwenye uchafu, pasipo faa na kuwekwa mahali pengine. Kwa hiyo mpenda sifa, ni mnyonge kuliko mtu mwingine yeyote.

Wengi huwa hatujui kwamba, sisi ni sisi na hatuwezi kuwa kitu kingine, tupande ndege, tununue merikebu, tujulikane hadi uvunguni, tuimbwe na maredio na kuoneshwa na matelevisheni kutwa kucha, bado ni sisi tu. Thamani yetu inaendelea kuwa ileile.

Huko ndani mwetu kunaendelea kuwa kulekule. Ni kama kiti, hata ukikiwekea marembo gani, ukaweka miguu mitatu, ukakitandika na dhahabu na lulu, kazi yake ni ileile ya kukaliwa, haibadiliki. Ikishabadilika, kinakuwa siyo kiti tena.

Nasi hata tuwe vipi, ubinadamu wetu hauwezi kubadilika, uko palepale. Msingi wa binadamu haubadilishwi na chochote, kama ambavyo dhima ya kiti haibadilishwi na namna kilivyotengenezwa. Kila mtu anapaswa kujua kuwa, amekuja duniani kuishi kama yeye.

Kama ni furaha atajipa mwenyewe, kama ni kero atajipa mwenyewe, kama ni kujishusha atafanya hivyo mwenyewe, hali kadhalika kujipandisha. Lakini, hata kama itakuwa vipi, anabaki kuwa binadamu.

Kama nilivyoanza awali mwa makala haya. Nakuomba ujaribu kufikiri tena kwamba, tayari una kila kitu kinachokuhangaisha hivi sasa. Fedha kibao, magari, majumba, umaarufu, mke au mume mzuri kuliko wote duniani, watoto wenye akili kuliko wote. Halafu kitafuata kitu gani?

Nataka ujiulize baada ya hayo yote kutimia, ni kitu gani kitafuata? Kama umefikiri vizuri, utagundua kwamba, ni upuuzi mtupu mbele. Utagundua kuwa hukuhitaji hivyo vyote hivyo, bali ulihitaji ulivyohitaji wewe kuvihitaji.

Hivyo vingine siyo wewe uliyevihitaji. Ni nani sasa anayekusumbua na kuhangaika na kubabaika na maisha kuvitafuta hivyo? Nakuachia swali hilo.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

IMANI NGWANGWALU,



     



Mar 12, 2015

Iheshimu Leo Isije Kukugharimu Kesho.

No comments :
Hivi umewahi kufanya kitu fulani halafu miaka ikapita ukajiuliza kama ni wewe umefanya hilo jambo, mimi nimewahi. Kuna wakati katika maisha unaweza ukajikuta umefanya jambo fulani halafu baadaye ukaja kujuta, ukajiona ni mjinga au hata limbukeni. Wakati mwingine linaweza likawa fundisho kwako kiasi cha kwamba hata mtu akushawishi vipi huwezi kurudi kufanya jambo hilo tena.

Hata hivyo tikirudi nyuma huenda wakati unafanya hayo mambo ulikuwa unashauriwa, hivyo ukajikuta ukawa sikio la kufa lisilosikia dawa. Au huenda hukupata nafasi ya mtu kukwambia unachofanya siyo na kwamba kitakuja kukugharimu maishani. Tuachane na sisi ambao tumepitia huko, tukajifunza na tukamwomba Mungu hiyo historia isije kujirudia tena katika maisha yetu.

Leo, naongea na wale wenzangu na mimi ambao tunaingalia leo. Kesho ni kama hatuijui vile au kama haitakuwapo kutokana na mambo tunayoyafanya. Wengine husema ‘kesho itajijua’. Kama ingekuwa hivyo basi tusingekuwa tunaihangaikia kesho.

Inafahamika wazi kuwa kila mtu ana uhuru wa kufanya kile anachokisikia, lakini ukweli unabaki palepale kwamba hata uhuru wa mtu binafsi una mipaka yake. Huwezi kufanya kila kitu bila kuzingatia mambo muhimu hasa ya kimaadili. 


Unajua kwa sisi vijana kuna mambo mengi tunayafanya kwa sababu ndio wakati wake, ujana si maji ya moto bwana. Ni kweli wala siyo uongo lakini wengi wetu tunafanya kwa kufuata mkumbo. Kuiga sijui fulani kafanya hivi na mimi nifanye, mwingine kaenda huku na wewe huyo kama kumbikumbi vile. Sasa unavyofanya hivyo unajua mwenzako kwa nini anafanya?

Wengi hasa wasichana wanaona fahari kumuiga fulani kafanya hivi ama vile. Kapate kile yeye atafanya kile akiwezacho hata kama kitamgharimu maisha yake lakini bora tu awe kama fulani. Kumbuka kuna kesho katika maisha yako, Yule unayemuiga hufahamu alivyojipanga hadi akafanya yale unayoyaona. Mambo mengine ni siri ya mtu. Sasa wewe unaingia kichwa kichwa utaumia.

Mwingine anaweza kuona rafiki yake, kachora tattoo na yeye huyo. Hivi unafahamu kwamba unaweza kukatisha ndoto za kuwa na mafanikio kuliko uliyonayo kwa sababu ya kufuata mkumbo? Kuna vitu tunaweza kuviona ni vya kawaida lakini kuna watu hadi leo wakikumbuka jinsi vilivyowagharimu katika maisha yao inakuwa inauma. Kuwa mtu na msimamo wako, maisha yako ni yako. Mwisho wa siku utakuja kusimama wewe kama wewe kwenye mambo yako ya msingi.

Nakumbuka kuna jamaa mmoja alipata nafasi ya kazi serikalini lakini alikuwa amechora tattoo. Kila siku akawa mtu wa kuvaa mashati yenye mikono mirefu, hata kukiwa na joto la aina gani hata mikono hawezi kukunja.

Alipoona watu wanamuuliza sana na kuna baadhi ya watu walianza kuhisi kwamba kuna kitu anaficha, alilazimika kwenda india kufanyiwa upasuaji. Huko alichomwa sindano ile ngozi ya juu iliyokuwa imechorwa ikaamuka halafu ikakatwa. Baada ya hapo aliuguza kidonda na kurejea akiwa na kovu. Hadi leo anakovu kwenye mikono. Sasa shida zote za nini? Iheshimu leo, isije ikakugharimu kesho.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kupata elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.
  •      Makala hii imeandikwa na Suzan mwillo wa Gazeti La Mwananchi.
  •                Mawasiliano suzanmwillo@yahoo.com

Mar 10, 2015

Hivi Ndivyo Kufikiri Kimazoea Kunavyoweza Kuharibu Maisha Yako.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yetu huwa tunajikuta ni watu wa kutenda mambo yetu kwa mazoea zaidi na kudhani tupo sahihi, wakati tupo kwenye makosa matupu ambayo huwa yanatuumiza, badala ya kutusaidia kama tunavyofikiri. Makosa haya huwa tunayafanya kutokana na matendo ama mienendo ambayo tunakuwa nayo binafsi katika maisha yetu ya kila siku bila kujijua sisi wenyewe kuwa tunakosea.

Makosa haya mara nyingi huwa yanatokana na kufikiri kimazoea. Kufikiri huku kimazoea kwa kawaida huwa ni jambo baya sana ambalo huweza kuathiri  maisha yetu. Tunapoamua kufikiri kimazoea maana yake huwa tunalazimika kufikiria kwa mujibu wa kile tulichofundishwa utotoni katika malezi au mazingira tulimokulia, bila kujiuliza wala kuchukua hatua zozote muhimu zenye uwezo wa kuleta mabadiliko tofauti kwetu.

Hebu fikiria kuhusu kulalamika au kunung’unika. Watu wengi huwa hawajui kwamba, tunaponung’unika tunasema au kujiambia kwamba hili tatizo ambalo tunalinung’unikia hatuwezi kulikabili au kulitatua, bali kuna wengine wanaoweza kulitatua. Kulalamika, iwe tunajua au hatujui, lakini kuna maana ya sisi walalamikaji kukosa uwezo, kushindwa kumudu, hivyo kutegemea wengine kumudu au kufanya kwa niaba yetu.

Kwa kulalamika, tunaamini kwamba, kwa hizo kelele zetu tunawachochea wengine  ambao tunaowaamini kwamba wana uwezo wa kukabiliana na yale matatizo yanayotukabili kwa wakati huo. Badala ya kulalamika, tunatakiwa kupeleka nguvu zetu zote kwenye suluhu ya tatizo. Kulalamika kuna maana kwamba, nguvu zetu tumezipeleka kwenye kuamini kwamba tatizo ambalo linatukabili hatuliwezi na hatuoni suluhu yoyote.


Hebu fikiria juu ya kulaumu kwako. Hii ni tabia ambayo wote tunaiona ni sahihi kabisa kwa sababu ya mazoea tu. Tunapolaumu, bila kujua tunaiambia dunia pamoja na sisi wenyewe kwamba, hatuna nguvu, bali kuna wenye nguvu zaidi kuliko sisi ambao wameshindwa kutuwezesha au kutugawia. Fikiria tena tokea umeanza kulaumu katika maisha yako ni kati kikubwa ambacho umevuna, zaidi ya kuharibu maisha yako?

Kwa kulaumu, tunatupa nguvu na uwezo uwezo wetu wa kubaki watupu. Kwa kuwa kila binadamu anapaswa kuwajibika kwa maisha yake, kulaumu tuna maana kwamba tumeshindwa wajibu wetu. Tunaamua kwa kusudi kabisa kuwa wahanga wa maisha yetu, uamuzi ambao haupendezi. Badala ya kulaumu sana, jifunze kukaa chini na kuchukua hatua ambazo zitakusaidia kuelekea kwenye kubadili maisha yako.

Kuna kujilaumu au kujikosoa, tabia ambayo pia ni ya kimazoea. Kumbuka, kile kinachoenda ndani, kwenye kufikiri kwetu, ndicho chenye kujionesha nje. Kwa kuwa maisha hutupatia kile tunachokihitaji, kwa kujilaumu au kujikosoa, tunachopata ni maumivu ya jambo tunalojilaumu kwalo. Tunapojiambia kwamba, sisi ni wajinga kwa sababu tumeshindwa  biashara fulani, ni lazima tutakuwa wajinga kweli, kwani hicho ndicho tunachokitaka.

Badala ya kujikosoa tunapofanya jambo kinyume na matarajio yetu na tunakuta tunataka kujilaumu, inabidi tuchukue kalamu na karatasi na kuandika yale yote ambayo ni mazuri kwa upande wetu. Tunayo mazuri mengi, kila mtu ana mazuri mengi. Hivyo, hatuna haja ya kujikosoa kwa mabaya yetu, kwani hayo siyo tunayoyahitaji. Unachohitaji wewe ni kuachana na kujikosoa sana na kusonga mbele.

Kila tunapojikosoa, tunapaswa kujua kwamba, tunazuia nguvu nyingi chanya kuweza kutufikia na kutusaidia tunakotaka kwenda. Hii ni kwa sababu tunayaambia mawazo ya kina kwamba, hatustahili kupata mema au mazuri. Kumbuka, maishani huwa tunakipata kile tunachokitaka au kukitarajia. Kama utakuwa tu wewe ni wa kujikosoa sana, itakuwa ni sawa na kujiambia hutaki mafanikio makubwa maishani mwako.

Kunakuwakosoa wengine kimazoea. Kwa mazoea, tabia hii huwa tunaiona kuwa ni ya kawaida sana na haina madhara kwetu. Huwa tuaamini kwamba, tuna haki ya kukosoa wengine na jambo hilo haliwezi kutudhuru. Kwa kuwahukumu wengine vibaya au kuwakosoa , tunatengeneza vurugu na ukosefu wa amani kwenye mfumo wetu wa kufikiri na ufahamu. Hii ni kwa sababu, tunaupeleka uzingativu wetu kwenye jambo ambalo hatulitaki.

Kijicho ni tabia ambayo wengi tunadhani au kuamini kwamba, ni lazima tuwe nayo. Lakini kijicho ni dalili ya mtu kuamini kwamba yeye hawezi kama huyo anayemwonea kijicho na hatakuja kuweza. Kuwa na kijicho ni moja ya tabia ya kimazoea ambayo huwa inauwezo mkubwa wa kuharibu maisha yetu wenyewe bila kujijua.

Jaribu kufikiria au kutazama ule uzoefu mzuri kuhusu maisha na siyo usioutaka. Jaribu kuangalia yale tu unayoyapenda kwa watu kuhusu watu wengine.  Kisha jenga tabia nzuri ambazo zitakusadia katika maisha yako na achana na kufikiri kimazoea ambako hakuwezi kukusidia kitu zaidi ya kukupa maumivu tu. Hivyo ndivyo kufikiri kimazoea kunavyoweza kuharibu maisha yako.

Nakutakia mafanikio mema, ansante kwa kutembelea matandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri yanayoendelea hapa.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU,