google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Feb 29, 2016

Mbinu Za Kukabiliana Na Ushindani Katika Biashara.

2 comments :
Mara nyingi wote tunajua wakati mwingine ili kuendesha biashara hadi ikakuletea mafanikio makubwa, inahitaji uvumilivu na kujituma sana hasa kutokana na changamoto nyingi zinazojitokeza kila siku kwenye biashara tunazozifanya.

Bila shaka utakubaliana nami moja ya changamoto kubwa zinazojitokeza katika kuendesha biashara iwe ndogo au kubwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya kutosha, mfumko wa bei, ushindani wa kibiashara na changamoto nyinginezo, ambapo usipokuwa makini unaweza ukakwama.

Leo katika makala haya tutaangalia moja ya changamoto hizo kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi sana. Changamoto hii si nyingine ni changamoto ya upinzani au ushindani unaojitokeza kwa kasi katika biashara kila kukicha.

Naamini hakuna asiyejua kwamba, kwa sasa ushindani kibiashara uko juu. Kila siku kumekuwa na biashara nyingi zinazoanzishwa. Na imekuwa si kitu cha ajabu kujikuta watu ishirini mkifanya biashara ya aina moja na kwenye mtaa mmoja.

Kutokana na ushindani mkubwa, wapo wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanikiwa na wengine kukwama kwa sababu ya kushindwa na nguvu ya ushindani. Lakini kwa kusoma makala haya, itakusaidia kujua mbinu za kukabiliana na ushindani kwenye biashara yako. Karibu sana kujifunza.

1. Toa bidhaa bora.

Ili uweze kumudu kukabiliana na washindani wako vizuri, njia bora ya kukabiliana nao ni kutoa bidhaa bora. Hakikisha wateja wako wanaridhika kabisa na kile unacho wahudumia. Isije ikatokea au ukasikia eti wateja wako wanalalamika kwa kukosa bidhaa bora. Kama itatokea hivyo, jirekebishe na toa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Kwa mfano wewe una duka la kuuza vifaa vya umeme. Jitahidi dukani kwako uwauzie wateja wako vifaa hivyo 'orijino' na sio 'feki'. Hiyo itakupa sifa kwanza na pia itakusaidia kuwashinda kirahisi wale wanaotoa bidhaa zisizofaa ambazo zikitumika kwa muda mfupi zimekufa. Kumbuka hili, kila wakati, kila siku,  kutoa bidhaa bora ni njia nzuri ya kuwashinda washindani wako.

KUWA MBUNIFU
 2. Angalia udhaifu wa washindani wako.

Hata kama washindani wako unaona wana bidhaa bora sana pengine hata kuliko wewe hilo lisikutishe sana. Kitu cha kufanya wewe, boresha bidhaa zako na  kisha nenda hatua ya ziada kwa kujifunza udhaifu wao. Ukishagundua udhaifu wao ni nini, utumie udhaifu huo kukusaidia kukufanikisha.

Tuchukulie kwa mfano wote mna mgahawa na mnatoa huduma ya chakula. Halafu ukaja kugundua jirani yako na ambaye ni mshindani wako, kwanza hawakaribishi wateja vizuri na pia  wateja wanalalamika chakula ni kidogo. Kitu cha kufanya wewe, ni kuhakikisha unawakaribisha wateja wako vizuri sana na ikiwezekana kutoa chakula kingi kidogo ili kufanya wateja wako wasilalamike kama yeye. Kwa kufanya hivyo utaweza kujipatia  wateja wengi hata waliokuwa kwa mshindani wako.

3. Kuwa mbunifu.

Mpaka hapo umeshajifunza ili kuwashinda washindani wako ni lazima utoe bidhaa bora na kuangalia udhaifu wao. Lakini hiyo haitoshi, pia unalazimika kuwa mbunifu zaidi kwa wateja wako. Ni muhimu kujua wanataka nini kwa wakati, ni kitu gani ambacho ukiongeza watavutika au ni huduma ipi ambayo wataitaka zaidi ambayo kwa sasa huna. Huo ni ubunifu unaotakiwa ili kukabiliana na ushindani hasa kwa kipindi cha sasa.

Kwa biashara yoyote inayoendeshwa kwa ubunifu ni rahisi kushinda ushindani na kusonga mbele. Lakini kama unaendesha biashara kimazoea kufanikiwa itakuwa ngumu. Tafuta kitu ambacho huna, kiongeze kwenye biashara yako. Kama una biashara ya saluni na ukagundua pengine ukiweka televisheni huku ukionyesha baadhi ya mipira ya ulaya itavuta wateja, basi fanya hivyo ili upate wateja  kutosha. Kama nilivyosema ubunifu katika biashara yoyote unalipa sana na pia ni njia sahihi ya kukabiliana na ushindani.

4.  Toa punguzo la bei.

Biashara yako inaweza ikawa ina mvuto mkubwa sana ikiwa kuna wakati fulani kunakuwa kuna punguzo maalumu la bei. Punguzo hili unaweza ukalifanya katika kipindi maalumu mfano cha sikukuu au ukaamua kushusha bei bidhaa fulani fulani hivi ili kuweza kuwavuta wateja na kuushinda upinzani.

Kwa mfano unaweza ukawa unafanya biashara ya kuuza simu. Ni vyema kwa baadhi ya simu ukashusha bei na kuwatangazia wateja wako ofa hiyo ambayo uwe na uhakika wataipenda. Kwa kutoa ofa hizo siku hadi siku zitaifanya biashara yako ing'ae na kuzidi kwenda juu na kuushinda upinzani.

 5. Toa huduma bora kwa wateja wako.

Tatizo kubwa walilonalo wafanyabiashara wengi hasa wadogo ni kule kushindwa kutoa huduma bora. Wamekuwa ni wafanyabiashara wa kufanya biashara, bora liende na kusahau kutoa huduma bora. Kwa vyovyote vile unaposhindwa kutoa huduma bora unajiwekea mazingira ya kushindwa kukabiliana na ushindani. Huduma bora inahitajika sana ili kuifanye biashara yako iende na wakati na kuwashinda washindani wako.

Katika kutoa huduma bora jifunze kuwafurahia wateja wako, jifunze kuwasikiliza na pia jifunze kuomba msamaha kama kuna kosa linaweza likawa limetokea la kibiashara. Hiyo ni mifano michache ya kutoa huduma bora lakini lilokubwa kwako ni kuhakikisha kwa namna yoyote ile unatoa huduma bora kwa mteja wako itakayomfanya afurahie huduma hiyo na kesho kurudi kwako tena. Bila kufanya hivyo, utapoteza wateja na watakimbilia kule zinakotolewa huduma bora.

6. Toa matangazo ya biashara yako.

Kwa kawaida hakuna biashara ambayo inaweza ikajiendesha kwa mafanikio makubwa na kushinda ushindani bila kuwa na matangazo. Biashara yako inategemea sana matangazo kuliko unavyofikiri. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu biashara yako inatakiwa kujulikana kila eneo ilina kuwavutia wateja wengi.

Tunapozungumzia matangazo kama huna mtaji wa kutosha si lazima yawe ya redioni au kwenye televisheni. Unaweza ukatengeneza vipeperushi kwa gharama ya kawaida au unaweza ukatumia wateja wako hao hao kuitangaza biashara yako na kupanua soko kwa kiasi kikubwa na kuwashinda wapinzani wako.

Kwa  kufanya mambo haya, yatakusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ushindani mkubwa unaojitokeza katika biashara yako.

Tunakutakia kila la kheri katika biashara yako na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.

Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,

Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,




Feb 26, 2016

Ndoa Imara Huweza Kutibu Hata Kansa.

No comments :
Maradhi ya kansa yamekuwa yakiwasumbua watu wengi sana kwa nyakati za hivi karibuni. Hata hivyo kuna aina nyingi za kansa, mojawapo ni ile ya kibofu cha mkojo.
Kulingana na utafiti mmoja uliofanywa nchini marekani, imeonesha kwamba, msaada wa karibu unaotolewa na wanandoa kwa wanandoa wenzao ambao, wameathirika na gonjwa wa kansa  ya kibofu cha mkojo, ni aina mojawapo ya tiba inayoweza kuwafanya wagonjwa hao wajisikie vizuri na kuishi kwa muda mrefu.
Utafiti huo ulionyesha kwamba, watu wanaougua ugonjwa huo ambao wako kwenye ndoa, wana nafasi kubwa ya kuishi muda mrefu zaidi ukilinganisha na wenzao ambao hawajaoa au kuolewa. Hali hii haichagui umri, rangi au hata kiwango cha athari ya ugonjwwa wenyewe.
Vilevile, tafiti mbalimbali za huko nyuma ziliwahi kuonesha kwamba, ndoa bora na imara zina uwezo wa kuwaongezea ahueni wanandoa wanaougua maradhi ya kansa ya matiti na ile ya mkojo.

NDOA IMARA INATIBU MARADHI MENGI.
Watafiti hao walizidi kusema kwamba utafiti huo mpya unaweza ukawa na manufaa zaidi kwa aina nyingine ya kansa. Hali kadhalika utafiti huo ulionesha kwamba,wagonjwa wa kansa ambao walikuwa wamefiwa na wenzi wao wa ndoa na wale waliotengana ama kutalikiana, waliathirika na ugonjwa huo zaidi.
Ingawa umri mkubwa nao ulichangia kwa kiwango kikubwa kwenye hali hiyo, kutokuwa na mpenzi kulionesha wazi kuwa na madhara makubwa.
Sababu hasa, inayoyaofanya kuwa na tofauti hiyo, bado haijaulikani. Hata hivyo, yapo maelezo machache yanayoweza kutolewa  kuhusiana na hali hiyo. Kwa mfano, mume au mke anaweza kumshauri mwenzi wake amwone mapema daktari, wakati dalili za mwanzo kabisa za ugonjwa zinapojitokeza. Na pia anaweza kumshauri mwenzake abadili mwenendo wa tabia zinazoweza kuuongeza madhara yatokanayo na ugonjwa huu kwa mfano, kuacha kuvuta sigara, kwani tabia ya uvutaji wa sifara huzidisha kiwango cha ugonjwa huu.
Na pia msaada wa mume au mke, kwa njia moja au nyingine, huzipa nguvu chembechembe hai za mwili zinazohusika na mfumo mzima wa wa ulinzi. Uchunguzi huo ulionesha kuwa, wagonjwa wa kansa ya matiti waliokuwa wameolewa na ambao walihisi kuwa wana uhusiano mzuri na imara na wenzi wao wa ndoa na kuwa wanapewa kila msaada wanaouhitaji, chembechembe zao hai zinazolinda mwili, zilionekana kufanya kazi kwa kiwango cha juu kabisa na hata ziliweza kuua baadhi ya vijidudu vinavyosababisha ugonjwa huo.
Ndoa bora na imara imekuwa ikitajwa sana kama ni tiba inayoweza kutibu maradhi mengi ikiwemo kansa na pia imekuwa ikielezwa kwamba, huufanya mwili wa binadamu kuwa imara zaidi, watu wenye ndoa za mashaka na vurugu, wanapoingia katika maradhi, wameonekana kudhoofu na pengine kufa haraka, ukilinganisha na wale ambao wako kwenye ndoa imara.
Kwa hiyo hapa utajua, inaposisitizwa kwamba,wanandoa wajenge ukaribu ambao utawezesha ndoa zao kuwa bora na imara, siyo tu kwa sababu ya ya kufurahia mahaba, lakini pia ni kwa sababu ya kunusuru afya ya miili yao. Tafiti nyingi zimekuwa zikionesha kwamba, wanandoa ambao wako kwenye vurugu za kindoa hupata madhara mengi ya kimwili, wanawake wanaelezwa kwamba huathiriwa zaidi na jambo hilo.

Kumbuka huu ni utafiti tu uliofanya na wenzetu. Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO  kila siku, ili uweze kuboresha na kubadili maisha yako.  
Tupo pamoja,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,

Feb 25, 2016

Misingi (3) Ya Kuweka Juhudi Katika Safari Ya Mafanikio

No comments :
Nafahamu ya kwamba kila mmoja anafanya mambo mbalimbali kama vile kusoma, kufanya biashara, na kutoa huduma mbalimbali. Lakini yote hayo huleta  matokeo chanya  endapo utaweka juhudi za kweli katika endaji wako na kinyume cha hapo utakuwa unashindwa. Watu wengi huwa tunafanya vitu ili mradi tu, siyo kama tunapenda kufanya vitu hivyo ila kwa kulazimishwa tu au kwa kuiga kutoka kwa watu wengine mwisho wa siku tunajikuta hatufanyi tena vitu hivyo.
Hebu tuendelee kidogo tuone maana ya neno JUHUDI ni kile kitendo cha kufanya kitu  kwa kutumia bidii, maarifa, nguvu na umakini wa hali ya juu ili kupata matokeo sahihi. Pia juhudi ni maarifa, njia, nguvu ambayo unaipata hata pale wanaokusaidia kwa sasa wakikuucha  je, unauwezo wakusimama peke yako? 

Mfano wewe ni mwanafunzi wazazi au ndugu zako wanakusomesha kwa hali na mali, swali la kujiuliza wewe mwanafunzi je una uwezo wa kusimama peke yako endapo wanaokusaidia watakuacha? Je utatumia juhudi gani katika kutafuta njia zako binafsi za kukamilisha jambo fulani?
Ifuatayo ndiyo misingi ya kuweka juhudi katika safari yako ya mafanikio;
Kwanza, Kujitoa.
Ili kuona unapata mafanikio makubwa hakikisha ya kwamba unajitoa kwa moyo wote katika kupata kile unachokihitaji. Kwa kitu chochote unachofanya jitoe kukipenda kitu hicho. Kwa mfano wewe ni mfanyabiashara eneo fulani hakikisha unaipenda kazi yako kwa kujifunza kila siku vitu vipya juu ya jambo unalolifanya. Pia kwa jambo lolote unalolifanya weka juhudi zote na kuhakikisha utapata kile unachokihitaji.

WEKA JUHUDI KWENYE KAZI ZAKO BILA KUCHOKA.
Pili, uvumilivu.
Wengi wetu huwa hatuna chembe ya uvumilivu hata kidogo hasa pale changamoto zinapojitokeza katika mambo tunayofanya. Pia tukumbuke ya kuwa changamoto ni sehemu anayopitia mtu yeyote msaka mafanikio. Jambo la msingi la kuzingatia ni uvumilivu na siyo kukata tamaa. Kuna usemi wa wahenga unasema ‘mvulivu hula mbivu’ Hivyo tuishi usemi huu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzikubali changamoto na kujua jinsi gani ya kuziepuka ili tupate mafanikio tunayoyahitaji.
Tatu, kuwa mbunifu.
Hii ndio siri kubwa katika kutafuta mafanikio makubwa ambayo  yapo upande wako. Kuwa mbunifu katika mambo mbalimbali huku ukiyatendea kazi hayo uliyoyabuni kwa juhudi zote. Kama wewe ni mwanamziki basi fanya kazi hiyo kwa juhudi zote huku ukiamini ya kuwa kipaji hicho ndio sehemu ya maisha yako na kipato chako, usifanye kitu kwa kujaribu.
Katika suala la kuwa mbunifu kuna msomi mmoja amewahi kusema ya kuwa dunia ya leo haitaki kujua wewe una nini ila ioneshe dunia wewe una nini? Nafikiri kwa mfano huo utakuwa umenielewa vizuri zaidi. Pia tukumbuke ya kuwa ubunifu sio lazima kuvumbua kitu kipya bali hata kwa kukiongezea ubora kitu cha zamani pia ni ubunifu pia.
Wapo baadhi ya watu wana pesa  lakini hawana juhudi. Kama wewe ni miongoni mwa watu hao kumbuka pesa hizo zitakuwa ni za msimu na pindi zitakapoisha utabaki unashanga tu. Watalamu mbalimbali wamebaini ya  kuwa na pesa bila  juhudi sio kufikia malengo. Tenda mambo yako katika mtiririko unaoelewaka na ambao unaweza kuutimiza kwa muda muafaka , ukifanya hivyo kuwa tayari kuyapokea mafanikio makubwa
Ewe rafiki yangu wa DIRA YA MAFANIKIO, tukumbuke ya kuwa JUHUDI ndio msingi rasmi wa mafanikio ambayo unayahitaji. Swali la kujiuliza je, upo tayari kulifanya jambo hilo kwa juhudi dhabiti? Kama jibu lako ni ndio basi weka juhudi zako zote katika utendaji wa jambo fulani kwa kuzingatia muda. Ukifanya hivyo mafanikio makubwa yatakuwa upande wako siku zote.
Ansante kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku. Ombi letu kwetu kwako, endelea kuwashirikisha wengine waweze kujifunza zaidi kutokana na makala tunazozitoa hapa.
Kama una maswali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii Benson chonya mtalamu wa maendeleo na mipango.
Simu; +255 (0) 652 015 024
E-mail; bensonchonya23@gmail.com
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com

Feb 24, 2016

Mambo 8 Yatakayosaidia Kufikia Malengo Yako.

No comments :
Kila wakati wengi wetu katika maisha, ni watu wa kujiwekea malengo. Mara nyingi huwa tunaweka malengo haya,  kwani kwa kujiwekea  malengo hayo ndiyo hutuongeza na kutuhakikishia  kule tunakotaka kufika kimafanikio. Kwa kujua hili, karibu kila mtu msaka maendeleo, kwake malengo huwa ni kitu cha lazima sio cha kuuliza tena.
Lakini hata hivyo, pamoja na kujiwekea malengo mazuri,  kwa bahati mbaya sana tena wengi wetu huwa bado hatuyafikii malengo hayo. Hapo ndipo maswali mengi sana ya kwanini huanza kuibuka vichwani kwetu? Kama mambo ni hivyo usikate tamaa, Kwa kufatilia makala haya utajifunza juu ya mambo muhimu yatakayokusaidia kufikia malengo yako.
1. Yajue malengo yako vizuri.                                                                        
Huwezi kufanikiwa kama huyajui malengo yako vizuri. Ni lazima malengo yako yawe ya wazi kwako. Ikiwezekana yaandike vizuri kwenye karatasi nayaweke sehemu inayoonekana. Kwa mafano kama lengo lako ni kufanya biashara ya ‘stationary’ liandike lengo hilo mahali na lionekane.  Kama pia lengo lako ni kufungua duka weka wazi lengo lako kwa kuliandika.
Watu wengi mara nyingi wanashindwa kufikia malengo yao kwa sababu malengo yao yanakuwa sio wazi sana. Siku zote mawazo yetu ya ndani hutusaidia kufikia malengo yetu, kama malengo hayo yana eleweka. Kinyume cha hapo, utakaa sana kusubiri malengo yatimie lakini wapi. Hivyo siri ya kufikia mafanikio jitahidi kuweka malengo yako wazi.

HAKUNA CHA KUKUZUIA KWENYE MAFANIKIO UKIAMUA.
2. Jitoe kikamilifu.
Siri ya mafanikio ni kujitoa kikimalifu kwa kile unachokifanya. Hata malengo yako ambayo umeshajiwekea na yako wazi ili kuweza kuyafikia ni lazima ufanye juu chini kujitoa kikamilifu na wala sio nusunusu. Ikiwa utakuwa unayaendea malengo yako, huku ukiwa hujaamua kujitoa kikamilifu tambua ikatokea umeshindwa usishangae hapo kwa hilo.
Kwa kuwa unanajua malengo yako nini, kama kuna kazi unatakiwa kuifanya ifanye kweli kwa nguvu zako zote bila kuchoka. Weka juhudi na maarifa yako yote na kuhakikisha unajitoa kweli. mafanikio yako hayatakuja kirahisi eti kwa kufanya kazi kilegevu. Jitoe kwa kupiga kazi kwelikweli mpaka kieleweke.
3. Kamilisha majukumu yako kila siku.
Unaweza ukawa unayajua malengo yako na umejitoa kikamilifu, lakini huwezi kuyafikia malengo yako kama kila wakti unakuwa hukamilishi zile kazi zinazotakiwa  kukusaidi kuyafikia malengo yako. Hapa sasa ndipo unapotakiwa kujilazimisha na kuhakikisha kila jukumu ulilonalo  unalikamilisha  kwa siku husika.
Kwa mfano kama wewe ni mfnyabiashra ulitakiwa kupga mahesabu Fulani ya kukusidia, fanya hivyo bila kuacha. Halikadhalika akama wewe ni mwandishi na umejipangia kuandika kurasa mbili kwa siku, pia fanya hivyo bila kuacha wala kuahirisha. Kwa kukamilisha majukumu yako kila siku itakusaidia kufikia malengo yako kuliko ambavyo ungefanya mambo nusunusu.
4. Yagawanye malengo yako.
Malengo yoyote ulinayo yanaweza kufikika. Haijalishi malengo hayo ni makubwa kivipi lakini uwezo wa kuyafanikisha upo, ikiwa tu lakini utafuata hatua za kuyakamilisha malengo hayo. Pengine unajiuliza kivipi au nitawezaje kuyakamilisha malengo yangu makubwa? Ni rahisi tu na hata wewe unaweza.
Kulielewa hilo vizuri ngoja nikupe kisa kimoja moja ambacho kinaelezea siku moja fisi mkubwa alimkuta fisi mdogo akimla tembo. Fisi Yule alivyoona vile alicheka sana na kumuuliza utamaliza lini? Fisi Yule mdogo alimwambia nitamla kidogo kidogo mpaka ataisha. Kwa kutumia mfano huo hivyo, ndivyo unavyotakiwa na wewe kufanya kwa malengo yako makubwa. Unajiona una malengo mkubwa yagawe vipande vipande mpaka uyafikie..
5. Tafuta msaada.
Ni rahisi kuyafikia malengo yako, kama utatafuta msaada wa kukusaidia kuyafikia malengo hayo. Acha kung’ang’ania kukamilisha malengo hayo ukiwa peke yake. Yaangalie malengo yako yana husu nini kisha baada ya hapo jiulize je, ni mtu gani au watu gani  ambao wanaweza kunisaidia kukamilisha malengo haya.
Kwa kujua watu ambao watakusaidia kukamilisha malengo yako itakusaidia sana kushirikiana nao kwa ukamilifu na kwa ubora wa hali ya juu hadi kufikia mafanikio yako. Tambua na elewa sio kwa sababu malengo ni yako, hivyo unatakiwa kuyakamilisha mwenyewe, hapana. Tafuta kile unachokosa, kisha omba msaada.
6. Kuwa chanya wakati wote.
Kuna wakati tunapokuwa tunajiwekea malengo huwa tunakutana na changamoto nyingi sana ambazo zinatukatisha tamaa. Sasa hali hii inapokutokea ni vyema ukajitahidi ukawa chanya wakati wote. Acha kukataa wala kujiona hufai, endelea kusonga mbele kati kati ya changamoto hizo ulizonazo wewe.
Kuwa chanya wakati unatafuta mafanikio inalipa sana. Tuchukulie kwa mfano unafanya biashara halafu ukapata hasara, hapo unafanyaje? Utaacha au itakuaje? Jibu ni kuendelea  na safari ya mafanikio kwa kutambua kwamba hiyo nayo ni hatua ya mafanikio pia. Ndiyo maana tunasema ni muhimu na lazima kuwa chanya ili kuyafikia mafanikio yako.
 7. Kuwa tayari kuyapitia malengo yako kila wakati.
Pamoja na kwamba umejwekea malengo vizuri, umejitoa kabisa kwenye malengo hayo, lakini hutakiwi kusahau kabisa kuyapitia malengo yako. Ni muhimu kuyapitia tena na tena malengo kwa kutambua wapi ulipofikia, nini kinachokukwamisha na ufanye nini ili uweze kusogea hapo ulipo kwa kasi zaidi.
Watu wengi wenye mafanikio wanayapitia malengo yao. Wanapita malengo yao asubuhi, wanapitia malengo yao mchana, wanapitia malengo yao jioni. Picha kamili ya malengo yao inakuwa ipo kichwani mwao tayari. Hiki ndicho kitu ambacho unatakiwa ukifanye hata wewe. Pitia malengo yako kila wakati ili yaumbieke vizuri na itakusaidia kuyakamilisha.
8. Jifunze kufurahia mafanikio kila hatua unayopitia.
Pamoja na kujiwekea malengo yetu makubwa, lakini kumbuka kuna yale malengo yetu madogo madogo ambayo huwa tunayashinda. Inapotokea umefanisha jambo fulani, hata kama kwako ni dogo ni vyema ukajifunza kulifurahia. Furahia mafanikio yako siku hadi siku kwa jinsi unavyoyapata. Hiyo itakupa nguvu ya kufanikisha mambo mengine.
Kama kweli una nia njema ya kufikia mafanikio makubwa, basi hayo mambo ni ya msingi sana katika kukusaidia kufikia malengo yako makubwa uliyojiwekea. Jukumu lako kubwa ni kuhakikisha unayaweka kwenye vitendo mambo hayo.  Na kwa kufanya hivyo basi utaweza kufikia malengo yako na kutakuwa hakuna wa kukuzuia.

Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila wakati. Usikose kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia makala tunazozitoa hapa.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,

Feb 23, 2016

Siri Ya Kufanikiwa Katika Katika Kila Jambo.

No comments :
Haijalishi hapo ulipo unafanya kitu gani, lakini ninachotaka kukwambia hapa leo, tambua ipo siri ya kuweza kukusaidia kufanikiwa kwa asilimia zote mia moja, kwa lile jambo unalolifanya. Watu karibu wote wenye mafanikio makubwa wanaitumia siri hii kuweza kufanikiwa.
Kama watu hawa wenye mafanikio wamekuwa wakiitumia siri hii kuwafanikisha, basi hata wewe unaweza kuitumia siri hii kukufanikisha na kubadili maisha yako kabisa. Pengine umekuwa ukishindwa sana kwenye maisha yako miaka na miaka kwa sababu ndogo tu, ya kushindwa kuijua siri hii na kuitumia. 
Ninachotaka kusema na kukusisitiza ni kwamba kwa malengo yoyote uliyonayo, unao uwezo wa kuyafikia ikiwa tu utaamua kuitumia siri hii ya ushindi kukufanikisha. Kumbuka siku zote hakuna uchawi wala muujiza katika mafanikio. Hata wewe unaweza kufanikiwa kwa kishindo ikiwa utazingatia na kufanyia kazi siri hii.
Usijali sana kwa sehemu ulipo kimaisha kwa sasa. Hiyo itabaki kwako kuwa historia. Angalia mbele nakutumia siri hii kubwa ya mafanikio ambayo unakwenda kujifunza sasa. Siri ambayo unatakiwa ujifunze na kuilewa vizuri ni siri ya kutengeneza tabia za mafanikio.

TENGENEZA TABIA ZA MAFANIKIO.
Hautaweza kufanikiwa ikiwa wewe hutajitengenezea tabia za kuelekea kwenye mafanikio unayoyataka. Mara nyingi miili yetu inapenda sana tuendelee kukaa katika hali tulizozizoea. Sasa mafanikio hayawezi kuja kwa namna hiyo ya mazoea. Ni lazima kuna mambo utatakiwa kuyabadilisha au  kutengeneza tabia za mafanikio.
Jaribu kumuangalia Mohamed Ally katika kipindi chake alichokuwa akishinda mapambano mengi ya masumbwi, asingeweza kufika huko kama asingetumia muda mwingi kufanya mazoezi na kujitengenezea tabia za mafanikio. Kilichomfanya afanikiwe ni kujitengenezea tabia za mafanikio na kuwa mtii. Hiyo ndiyo ilikuwa siri ya mafanikio yake.
Lakini si hivyo tu, hata ukichunguza maisha ya watu waliofanikiwa sana, kikubwa kilichowafanikisha na kuwafikisha walipo ni kule kujitengenezea tabia za mafanikio kila siku. Hapa ndipo mafanikio makubwa yanapoweza kuanzia na sio kinyume chake.
Kuna wakati niliwahi kusoma maandiko ya mwanasaikolojia Julia Kristina Mah, amabapo alikuwa akiongelea thamani ya kutengeneza tabia za kukufanikisha. Alisema moja ya tabia inayowafanya watu washindwe kuafanikiwa ni kule kupenda kufanya mambo kwa kujisikia au kuongozwa na hisia sana.
Aliendelea kusema watu wengi wana tabia ya kufanya mambo kwa kujisikia, kama anaona kachoka kidogo basi hafanyi atasubiri mpaka atakapokuwa sawa, hiyo ni tabia inayowarudisha wengi nyuma. Hivyo, dawa ya kutoka hapo ni kutengeneza tabia za mafanikio na si kusubiri.
Kaa chini na ujiulize ni kitu gani unakitaka katika maisha yako? Ukishakijua kitu hicho tengeneza tabia itakayokusaidia kukufikia kitu hicho. Kwa mfano kama unataka kuwa msomaji mzuri, basi tenga muda wa kujisomea kila siku hata kwa dakika ishirini kwa siku, baada ya muda utafikia lengo lako.
Kwa chochote unachokitaka inawezekana kukipata ikiwa utajitengenezea tabia imara za kukufanikisha. Ikiwa lengo lako ni kutafuta mtaji ni sawa, jiwekee akiba kidogo kidogo kila wakati, utafanikisha lengo lako hilo. Hakuna tena nasema hakuna utakachoshindwa kukifanikisha ikiwa una tabia sahihi za mafanikio.
Ni vyema ukaitambua siri hii ukaitumia kukufanikisha. Kumbuka, tabia ni kitu ambacho hufikirii kukifanya bali kina kuwa kwenye damu. Hivyo ndivyo unavyotakiwa kujitengenezea tabia zako za mafanikio. Bila kuchoka kila siku. Kwa kufanya hivyo utajikuta zile kazi ulizokuwa ukizifanya kwa ugumu zinakuwa rahisi sana kwako na kukupa mafanikio.

Ansante sana kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila wakati. Endelea kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia makala tunazotoa hapa.
Ni wako rafiki katika kuyasaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,

Feb 22, 2016

Sababu Zinazoweza Kufanya Biashara Yako Ikafa, Hata Kama Ina Mtaji Mkubwa.

No comments :
Mara nyingi wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mara kwanza huamini sana mtaji ndio kila kitu. Kwa imani hiyo, hujikuta mara baada ya kuingia kwenye biashara wanakuwa hawaweki nguvu nyingi katika maeneo mengine muhimu ili kuboresha biashara zao. Na matokeo yake hupelekea biashara hizo kuanza kufa huku zikiwa zina mtaji mkubwa kabisa.
Kinaweza kuonekana ni kitu cha kushangaza lakini huo ndio ukweli. Unajua ni kwa nini ? Ni kwa sababu waliaminishwa toka siku nyingi kwamba ukiwa na mtaji mkubwa basi, kila kitu kimekwisha. Lakini, leo katika makala yetu tutaangalia sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa.  
Kwa kupitia makala haya itakuonyesha na kukupa ukweli wa wazi  kwamba, mtaji mkubwa peke yake sio ‘gerentii’ ya kukufanya wewe ukafanikiwa kibiashara.  Yapo mambo mengine ya ziada ambayo unatakiwa kuyazingatia na kuyatilia mkazo kila siku, ili biashara yako iweze kukupa yale matunda unayoyataka.
Kumbuka haijalishi biashara yako ina mtaji kiasi gani, lakini elewa ukweli huu inaweza ikafa usipozingatia mambo haya ya msingi. Sasa nataka twende pamoja kujifunza na kujua mambo au sababu zinazoweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa vipi.  Karibu sana tujifunze pamoja.
1. Kukosa usimamizi imara.
Kama unaona unataka kuanzisha biashara yako, halafu ukagundua huna usimamizi imara ni bora ukaachana na hiyo biashara. Na kama ungekuja kwangu leo na kunieleza hali hiyo ilivyo,  ningekushauri hivi ‘ Chukua pesa hizo kisha nenda mjini, katafute sehemu wanakochoma nyama nzuri kula pesa yote usibakize hata  Shilingi mia moja.’
Sikutanii. Kwa nini nakwambia hivyo, kufanya biashara yako huku ukiwa huna usimamizi wa kutosha ni sawa na kupoteza pesa hizo. Tena unazipoteza bila kufaidi hata tone. Hapa unaona hata kama ungekuwa na mtaji mkubwa vipi, kama huna usimamizi ni lazima biashara hiyo itakufa tu, hakuna ubishi.

KUKOSA USIMAMIZI BORA, NI SUMU YA BIASHARA.
2. Kukosa elimu ya biashara.
Najua umeshawahi kusikia sana fulani alipata mkopo wa  benki milioni sitini, lakini biashara zake zimekufa. Unajua chanzo chake kimojawapo ni nini? Ni kukosa elimu ya biashara. Wengi wanapokosa elimu hii huwekeza kiholela sana matokeo yake kupoteza pesa nyingi bila sababu ikiwa pamoja na mtaji.
Kwa hiyo ili kufanikiwa kibiashara ni lazima wewe kuwa na elimu ya kutosha kibiashara. Pengine unataka kujiuliza nitaipata wapi sasa? Sikiliza huhitaji gharama kubwa sana kuipata. Unaweza kujifunza kupitia semina, huwezi hilo unaweza kujifunza kupitia mitandao ya kuhamasisha au ukanunua vitabu vinavyohusu biashara ukajifunza polepole. Lakini kikubwa usiikose elimu hii, vinginevyo utapoteza mengi ikiwa pamoja na biashara yako.
3. Matumizi mabaya pesa.
Sio kwa sababu biashara yako ina mtaji mkubwa na inaingiza pesa nyingi kwa siku, basi na matumizi yako yanakuwa yako juu bila sababu. Kama unafanya hivyo kwenye biashara yako nikupe tu uhakika huu, huwezi kufika mbali. Ni lazima uwe na mpangilio mzuri wa matumizi yako ya pesa ili kuifanya biashara yako ikazidi kuendelea.
Acha kujidanganya kwa kuendelea kutumia pesa vibaya, utazipoteza zote mpaka utashanga. Kikubwa unajua jinsi huo mtaji ulivyoupata. Kama ni hivyo kwa nini uutumie hovyo? Kuwa makini na pesa zako. Tofauti na hapo biashara yako itakufa tu hata kama sio leo, lakini lazima itakufa.
4. Kukosa ubunifu.
Ili uweze kukabiliana na ushindani, ubunifu ni muhimu sana katika biashara yako. Bila kuwa mbunifu huwezi kufanikiwa katika hiyo biashara kutokana na mazingira ya ushindani mkubwa tulionao kwa sasa. Kwa hiyo ni lazima kuwa mbunifu na kuifanya biashara yako ikaonekana ya tofauti na kukupa wateja wa kutosha.
Wengi wanaoshindwa kwenye biashara ni wale walioingia kwa kiburi cha mtaji mkubwa na kusahau ubunifu. Haijalishi unafanya biashara ndogo au kubwa weka ubunifu. Kila wakati tafuta ni kitu gani biashara yako inakosa, kisha kiboreshe zaidi. Jitahidi sana kuweka ubunifu ili kuifanya biashara yako iwe hai siku zote, vinginevyo utaiua.  
5. Kukosa nidhamu.
Kama unaendesha biashara yako na ukakosa nidhamu ya kuiendesha biashara hiyo, elewa kabisa utakuwa na mchango mkubwa sana wa kuiua. Nidhamu ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote na sio biashara tu peke yake. Jaribu kuangalia watu wote wenye nidhamu ya kazi mafanikio yao yakoje? Bila shaka ni makubwa.
Biashara nyingi sana zinazokufa huku zikiwa na mtaji mkubwa mara nyingi hukosa nidhamu. Tuchukulie una duka la reja reja, huwezi kufanikiwa ikiwa unafungua na kufunga unavyotaka. Ni lazima uwe una nidhamu ya muda, nidhamu ya kuwajali wateja au nidhamu ya kauli nzuri. Kwa kukosa nidhamu hizi biashara itakufa tu hata iwe kubwa vipi.
 6. Kukosa wateja.
Kati ya kiungo muhimu sana kwenye biashara yako ni wateja. Bila wateja hakuna biashara inayoweza kufanyika. Sasa kama utakuwa huna wateja hiyo inamaanisha biashara yako kwa vyovyote vile itaenda kufa hata ufanye nini. Maana hao ndio wawezeshaji wakubwa kwenye biashara yako kuendelea.
Sasa huwa zipo sababu zinazopelekea biashara hii ikakosa wateja na nyingine ikawa na watej wengi. Hivyo ni vyema ukazijua sababu hizo ili zikusaidie kuweza kujenga biashara ya uhakika na yenye mafanikio makubwa.
7. Kukosa vipaumbele.
Biashara yoyote iwe inanza au inaendelea ni lazima iwe na vipaumbele vya msingi ambavyo vinatakiwa vifuatwe kila siku. Kama kipaumbele chako kimojawapo ni kutaka kukuza mtaji ni vyema ukawa makini kuhakikisha hilo linatimia na kutekelezeka kwa haraka sana.
Lakini kama pia vipaumbele vyako ni kuhakikisha unadumisha mahusianao mazuri na wateja wako, pia ni bora ukatekeleza. Unapokosa vipaumbele hata vile unavyoviona ni vidogo ni rahisi sana kwa biashara yako kuweza kufa na kushindwa kuendelea hata kama ina mtaji wa kutosha. Kwa sababu hapa tunasema biashara inakuwa inakosa dira maalumu.
8. Kukosa mgawanyo wa majukumu.
Pia biashara inaweza ikafa hata kama ina mtaji wake mkubwa, ikiwa itakosa mgawanyo wa majukumu.  Ni lazima biashara iwe na mgawanyo wa majukumu ili iweze kusonga mbele. Kama unaona unafanya biashara huku kila kitu umeshikilia wewe na hakuna wa kukusidia elewa upo kwenye hali mbaya.
Ni lazima utafute watu wa kukusaidia hata kama pale haupo mambo yaweze kwenda sawa kabisa. Siri mojawapo kubwa ya kufikiwa mafanikio makubwa kwenye biashara yako ni kutengeneza mgawanyo mzuri wa majukumu kwa wasaidizi wako. Kushindwa kufanya hivyo ni lazima utaua biashara yako.

Kama nilivyoanza kwa kusema zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea biashara yako ikafa, hata kama ina mtaji mkubwa. Kwa leo naomba niishie hapo. Tukutane wiki ijayo kwa makala nyingine nzuri ya biashara. Kumbuka kuchukua hatua. KILA LA KHERI.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 04 80 35,

Feb 19, 2016

Faida Kubwa Za Nidhamu Binafsi Katika Kuyafikia Mafanikio Yako Makubwa.

No comments :
Nidhamu maana yake ni utaratibu au sheria anayojiwekea mtu au kuwekewa mtu katika kufanya au kutofanya kitu ama jambo fulani katika maisha.

Mara nyingi nidhamu humwongoza mtu na kumwekea mipaka kwa baadhi ya vitu kuvifanya au kutokuvifanya ima kwa kupenda au kutopenda.

Nidhamu ziko za aina mbili  nidhamu binafsi anayojiwekea mtu binafsi kwa makusudi ya kutimiza malengo fulani aliyojiwekea katika maisha yake. Na kuna nidhamu inayowekwa na kikundi, taasisi, kampuni au serikali ya nchi kwa madhumuni maalumu.

Leo tunaangalia zaidi katika nidhamu binafsi. Nidhamu binafsi ndio imekufanya wewe uwepo hapo ulipo na uwe hivyo ulivyo. Ni kutokana na nidhamu binafsi ndiyo  imekufanya ufanikiwe au usifanikiwe katika maisha yako. Nidhamu binafsi ndiyo inayomwongoza mtu katika kufanya maamuzi sahihi au yasiyo sahihi katika maisha yake.

Zifuatazo ni faida za mtu kuwa na nidhamu binafsi;-

 1. Nidhamu binafasi humfanya mtu kujitambua yuko wapi, ni nini wajibu wake katika maisha yake na jamii inayomzunguka.

2. Humwongoza mtu katika kufanya maamuzi sahihi katika maisha yake kwani humfanya atafakari kwanza hasara na faida ya kile anataka, kabla ya kulifanya.

3. Humfanya atimize malengo yake kirahisi kwa sababu hufikiri kabla ya kufanya mambo.

KUWA NA NIDHAMU BINAFSI.
4. Nidhamu binafsi humfanya mtu kupendwa na watu kwa sababu ya kufanya vitu sahihi na mwenye uhakika navyo.

5. Humfanya mtu asikurupuke na kuiga vitu asivyo na uhakika navyo.

6. Humfanya mtu kutimiza majukumu yake kwa wakati.

7. Humfanya mtu kujiamini na kuondokana na hofu katika maisha.

8. Humafanya mtu kuwa na matumizi mazuri ya muda na pesa.

9. Humfanya mtu kufanya vitu kwa malengo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

10. Humfanya mtu kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

Mbali na faida hizo za nidhamu binafsi, Zifuatazo ni hasara za mtu kutokuwa na nidhamu binafsi katika maisha yake.

1. Huishi kwa kufuata Mkumbo hawi na utaratibu ktk maisha yake ni kama bendera fuata upepo.

2.  Mtu ambaye hana nidhamu binafsi anakuwa hana maamuzi sahihi katika maisha yake na kamwe huwezi kumwomba ushauri mtu asiye na nidhamu binafsi atakupoteza

3. Humfanya mtu kutokujiamini na hivyo kuwa na wasiwasi na hofu katika kufanya jambo lolote. Sijui nitaweza nimtafute nani anishauri ili nisikosee.

4. Humfanya mtu kutumia vibaya muda wake na pesa zake kwani hutumia bila umiliki wowote ule.

5. Ni mtu asiye na malengo huishi kwa kubahatisha na kudra za Mungu. Anasema tutafika tu, ipo sikunami nitafanikiwa tu Siku na miaka inaisha hadi kifo kinamfika hakuna alichofanya.

6. Humfanya mtu kuvunjika moyo haraka pindi anapoanguka au kutifanikiwa katika jambo analofanya. 

7. Humfanya mtu kutokuwa na msukumo wa ndani katika kile anachofanya katika maisha yake hufanya ilimradi tu amefanya bila malengo yeyote.

8. Hukushelewesha au kukunyima kabisa fursa ya mafanikio na kutimiza ndoto zako katika maisha.

9. Ni rahisi kubadilisha maamuzi uliyojipangia na kuanza kufanya kitu kingine ambacho hukukipanga kukifanya.

10. Kukosa nidhamu binafsi humfanya mtu kudharaulika na jamii inayomzunguka kwa kukosa busara na ueledi katika kusema kwake, kutembea kwake na hata kutenda kwake.

Ansante kwa kufatilia makala haya na endelea kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO.

Ni wako katika kupeana hamasa ya kuyafikia mafanikio na uhuru wa kipesa.

Shariff H. Kisuda alimaarufu mzee wa Nyundo Kali. 
 
Simu; 0715079993.
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com

Feb 18, 2016

Jifunze Kuendesha Kilimo Hiki Cha Kisasa, Ili Uweze Kutoka Kwenye Umaskini.

No comments :
Habari rafiki na mpenzi msomaji wa DIRA YA MAFANIKIO. Naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza ili kuboresha maisha yako. Katika makala yetu ya leo  tutaangalia namna unavyoweza kuendesha kilimo bora cha kisasa ili uweze kukabiliana na changamoto za maisha ikiwemo na kuutokomeza umaskini kabisa.

Ikumbukwe kwanza kuna aina mbili kubwa za kilimo. Aina ya  kwanza ni kilimo cha nje yaani ‘outdoor farming’. Hiki ni kilimo ambacho hutegemea mvua au  umwagiliaji, lakini mkulima hana uwezo wa kutawala kiasi cha maji au kiasi cha jua. Mazao huweza kuzalishwa nje kama ambavyo wakulima wengi tumezoea kuwaona.

Aina ya pili ni kilimo cha greenhouse/ kitalu nyumba
Kilimo hichi hufanyika ndani ya nyumba maalumu iliyotengenezwa kwa kutumia aina maalumu zinazoruhusu mwangaza kupenya ndani.
Pembeni huzungushiwa wavu maalumu unaoruhusu hewa kuingia na kutoka. Na chini huwekewa mipira maalumu kwa ajili ya kufanya umwagiliaji wa zao lako.


Faida za kulima kwenye kitalu nyumba/greenhouse.  Mkulima anaouwezo wa kudhibiti hali ya hawa mfano kiwango cha maji yanayohitajika, kiwango cha joto, kiwango cha unyevu angani/ humidity. Na hivyo kumruhusu mkulima kufanya uzalishaji hata wakati ambapo mvua kubwa zinaendelea kunyesha sehemu mbali mbali.

KILIMO HEMA/GREEN HOUSE.
Greenhouse’ inapunguza mashambulizi ya wadudu waharibifu kwakua nyumba huzungushiwa wavu maalumu hupata mavuno mengi zaidi kwenye eneo dogo kutokana na mazingira maalumu ya uzalishaji. Mfano kwenye greenhouse’ yenye ukubwa wa mita 8 kwa mita 15 ambapo huingia miche 500 ya nyanya mkulima huweza kuvuna kuanzia kilo 5000 (tani 5) za nyanya na kuendelea.

Cha muhimu kukumbuka, kuwa na greenhouse pekee sio uhakika wa asilimia zote kukupatia mazao mengi kwasababu ni lazima iendane na upandaji wa mbegu bora ambazo ni maalumu kwa kilimo cha greenhouse.
Lazima uandae shamba lako vema kwa kulima vizuri na kuweka mbolea samadi yakutosha. Lazima umwagilie kwa wakati. Lazima pia uzingatie udhibiti wa wadudu na magonjwa.


Wakulima wengi wanaolima kizamani wanalalamika kilimo hakilipi na kweli kilimo cha kizamani hakiwezi kukulipa kamwe yaani Kilimo cha zama za kwanza za mawe. Kwa mfano watu wanaolima kwa kuangalia angani walioapanda matikiti kwa kutumia mvua za mwezi wa 11 sasa hivi wamevuna na wamejaza matikiti sokoni hayana wateja.

NYANYA
Hiyo ni kwa sababu kila mtu anaweza kulima tikiti kirahisi wakati mvua ya vuli iliponyesha. Sio wote mnakutana sokoni muda huu. Vile vile wakulima wakizamani muda wa miezi ya kwanza au ya pili hawawezi kulima sana nyanya kwa kuwa mabonde yao yamejaa maji na pia wanaogopa kupambana na magonjwa ya aina mbalimbali.

Matokeo yake wanajikuta wakipishana na pesa ambapo mwezi wa pili au watatu nyanya bei yake inakuwa juu sana. Sasa basi kumbe muda huu ungekuwa na kitalu nyumba/greenhouse ndio ilikuwa muda wako wakuvuna pesa mpaka mwezi wa sita wakati wale wanaosubiri kilimo cha kuangalia juu watakapoenda shamba.

Kwa kawaida green house zipo za aina tofauti kulingana na mkulima  anavyotaka iwe. Huwa zipo ‘greenhouse’ za ukumbwa kama huu;

Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x15 ni shilingi milioni 4.5

Greenhouse ya ukubwa wa mita 8 x20 ni shilingi milioni 5.5

Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x30 ni shilingi milioni 7.5

Greenhouse ya ukubwa wa mita 8x40 ni shilingi milioni milioni 8.5.


Kwa mkulima yoyote anayehitaji huduma ya kutengenezewa Greenhouse atafuatwa popote pale alipo na kampuni yetu bila bei yoyote kubadilika. Mkulima atapewa somo la zao analotaka kuzalisha na utunzaji wake
mpaka atakapovuna.

Makala hii imeandaliwa na John Mabagala, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo na anahusika pia na usambazaji wa pembejeo za kilimo katika kampuni ya JM AGROCHEMICALS iliyopo Morogoro mjini.

Kama unataka kufahamu vizuri zaidi juu ya kilimo hiki au unahitaji huduma ya kufungiwa Greenhouse, popote ulipo wasiliana naye kwa email jmabagala@gmail.com au 0754 282 448 .