google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

DIRA YA MAFANIKIO

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Oct 3, 2019

Fedha Hutupa Furaha Tunapokuwa ‘Vijogoo’ Tu.

No comments :
Je, kuwa au kupata fedha nyingi ndiko kunakoweza kumfanya mtu awe na furaha ya kweli? Hili ni swali ambalo huenda kwa sasa, idadi ya watakaojibu kwa ndiyo, inaweza kuwa ya chini kuliko miaka kadhaa iliyopita.
 
Kwa kiasi fulani, watu wanaoamini kwamba, fedha ni kila kitu imepungua. Sababu ni nyingi, lakini ugunduzi wa matumizi ya akili ya kawaida umekuwa ukijitokeza siku hadi siku. Nchi zilizoendelea kwa fedha, watu wake wamekuwa wakiingia kwenye kukosa furaha kwa mapana makubwa zaidi.

Wamerekani, wajapani, waingereza na wengine wamekuwa wakisongeka na kujiua na kukata tamaa, zaidi kuliko muda mwingine wowote huko nyuma, kwa sababu ya pesa tu. 

Watafiti wamebaini hivi karibuni kwamba, fedha huweza kuongeza furaha kwa aliyenazo kama yeye ndiye ‘kijogoo’ kwenye eneo analoishi, ofisini au pale ambapo mtu huweza kubainishwa na wengine kuwa ndiyo ‘kijogoo’ kwa fedha nyingi kuliko wenzake. Lakini inayopatikana ni furaha kidogo na ya muda mfupi.
Wanasema, hapo suala siyo mtu ana kiasi gani, bali zaidi anamzidi nani. Kama mtu ana fedha, lakini akabaini kwamba, hapo mtaani kuna wanaomzidi, ni wazi hatafurahia kuwa na fedha hizo. Kwa nini hatafurahia?

Wamebaini watafiti hao kwamba, fedha huwa zina tatizo la kutafuta ushindi. Kama mtu hujui saikolojia ya fedha, ni dhahiri atajibainisha nazo. Akishafanya kosa hilo la kujibainisha nazo atataka au kujikuta akitaka awe ndiye mwenye nyingi zaidi. Katika kutafuta yeye awe ‘kijogoo’ ndipo furaha inapoondoka. Siku zote tunaposhindana maishani, furaha nayo hukimbia.

Furaha ya kweli kutoka kwenye fedha haiji kwa mtu kutaka kuwafikia wengine, hapana. Furaha ya kweli huja pale ambapo mtu yuko juu ya wengine na hao wengine wanajitahidi kupigana vikumbo kutaka kumfikia.

Kwa mfano, watafiti wamegundua kuwa, mtu analipwa au pato lake ni kiasi gani, siyo suala la maana sana, bali wenzake wanalipwa au pato lao ni kiasi gani, ndilo jambo la maana. Hii ina maana kwamba, kama mtu anapata 500,000 kwa mwezi na wenzake, wale wakaribu yake ambao ndiyo kipimo chake, wanapata kila mmoja kiasi kisichozidi 400,000, huyu mtu ni lazima atakuwa na furaha tu. Hata kama fedha hizo hazitoshi matumizi, ili mradi yeye ndiye mwenye kufukuzwa ili akutwe, atakuwa na furaha zaidi.

Umri unatajwa pia na wataalamu hawa. Wanasema, watu wakiwa kwenye umri unaolingana au kukaribiana, mwingine anapokuwa na fedha zaidi, hawa wanaomfukuza au wanaojilinganisha naye, hutaka kumpita, kukosa furaha zaidi, hata kama wana mamilioni zaidi.

Kwa hiyo, kinachowakosesha wengi furaha katika suala la pesa, siyo fedha yenyewe, hapana. Kinachowakosesha furaha ni kutaka kufika mahali ambapo wao ndiyo watakuwa kipimo cha juu cha wenye fedha zaidi. Bado hata hivyo furaha hiyo itakuwa siyo ya muda mrefu mwingine atakapoonesha dalili za kutaka kumfikia, kiwango cha furaha ni lazima kitapungua au kwisha. 

Kwa kuwa kila siku watu wanapitana kwa kipato, kutegemea furaha kupitia fedha ni upotezaji wa muda kwa sababu, furaha hiyo ni bandia sana na inakuwa siyo ya kudumu kwako.

Tunakutakia mafanikio mema endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

IMANI NGWANGWALU,



Oct 2, 2019

Hawa Ndio Watu Hatari Usiowajua, Wanaonyonya Nguvu Za Wengine.

3 comments :
Inaweza kuonekana kama ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu wanaonyonya nguvu za watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi anakufa bila kujua. Watu hawa hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine wakiwa ni watu wetu wa karibu sana, kama wazazi, wapenzi, watoto, jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi kunyonya nguvu zetu? Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda kweli.

Mtu anaweza kuuliza, inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo nguvu ni zipi? Kwa mfano, mimi ninapo kuwa nakukera kila siku, ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia, unaumia kihisia na kimwili. Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa athari kubwa kimwili na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi kukutokea umekerwa na mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu anayekukera unakuwa unajisikia vibaya.

Hebu pia tuchukue mfano wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa maringo, dharau, kulaumu bila kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na asiyejali kuhusu madhila ya wengine, ni wazi aliye chini  yake ataumia tu, kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye anaweza kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.

Ni vigumu kubaini mtu ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini na kuwabaini watu wa aina hiyo popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua nikuelekeze au kukutajia sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha wakiwa maganda matupu, huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha kufanya.

Hizi ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-

1. Kuna watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”

Hawa ni watu ambao muda wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku ambayo utakutana nao ukute wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia hali. Kila siku wao ni walalamikaji, wanaoamini kwamba, wanaonewa na kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au kukosoa tu, lakini bila kutoa pendekezo au kuonesha ni  njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia zipi zingetatua tatizo.

Wao wanaona kwamba, wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa. Hawa kwa kawaida hawana uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au walichobuni, hapana. Hata kama wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na mtu, watajikuta wakiingia kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze kujibu, kama basi watakuwa na uwezo wa kujibu.

Hawa ni wanyonya nguvu za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu wa aina hii anakujia na kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko au kukosoa kwake, huna budi kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye. Ni lazima ufanye hivyo, kwani akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu zako zote.


2. Kuna watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.

Hawa ni wanyonya nguvu pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi mtu anaweza kuamini kwamba ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni jambo dogo. Hawa wako maofisini na majumbani. Mtu anaumwa na mafua, lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa na kuacha kabisa wosia, kwamba anakufa.

Yeye mwenyewe huyu anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo, atapata huruma zaidi, ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali na kutaka kupima umuhimu wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza hata kusababisha hata wengine wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana kwenye maneno yao.

3. Kuna wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti

Hawa ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe  na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi nafasi. Mtu atazungumza yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa tatu mfululizo. Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza yeye. Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.

Hajali kama kuna mtu ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali, kama unamsikiliza unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha kutokujali. Kama ni nyumbani au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri aliomba kwako, yeye ndiye atakupa ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya kuzungumza katika kumshauri. Hawa ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.

4. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.

Kila wakati linapotoea jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya kulaumu ili wengine washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko wazi kabisa kwamba, hao anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa na kuona kwamba, anaowalaumu hawana tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.

Anaweza kuangalia mtu anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini atajaribu kwa kadiri awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala wakati mwingine hakihusiani moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’ lengo ni kumfanya mtu ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi nzuri ya sasa, anataka kukosoa ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa ni kuwapuuzia.

5. Kuna wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji ushauri.

Asubuhi atakuja kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni atakutafuta. Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni vizuri kumwonesha kwamba, unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati kumwonesha kwamba, huna jibu, siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu hujui. Ukikosa njia au jibu mara kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe jeuri au dharau ama kisirani.

6. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.

Badala ya kunyamaza, akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako na kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi kuwa mbaya’ bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka kuumiza hisia za mwingine.

Bila shaka umeshawahi kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa. Jitahidi wakati wote kuwa makini wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua namna ya kuwaondolea mbali kwenye maisha yako.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







                                                           

Oct 1, 2019

Kama Una Tabia Hizi, Mafanikio Kwako Yatabaki Kuwa Ndoto.

2 comments :
Adui wa kwanza wa mafanikio katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Wewe ndiye unayeamua,ufanikiwe au usifanikiwe. Ninaposema hivi nina maana kwamba ziko tabia ambazo ukiwa nazo unafanikiwa na zipo tabia  mbazo ukiwa nazo utaishia kuona wenzako wanafanikiwa wewe unabaki palepale.Tabia hizi ni adui mkubwa wa mafanikio yako. Kwa hiyo usianze kutafuta mchawi wa mafanikio yako,mchawi wa kwanza ni wewe. Wewe ndiye mwenye maamuzi ya mwisho juu ya maisha yako unataka yaweje.

Hizi ni tabia ambazo umekuwa nazo kwa muda mrefu na hutaki kuziachia. Kwa jinsi unavyoendelea kuwa nazo ndivyo ambapo unajikuta maisha yako yanazidi kuwa magumu na wakati huo huo mafanikio kwako yataishia kuwa ndoto ya saa sita mchana, ndoto ya alinacha na mara nyingi utajikuta ukiishi maisha ya wasiwasi huku ukiwa hauna uhuru katika maisha yako. Unapojifunza tabia hizi fanya mabadiliko, chukua hatua sahihi za kubadili maisha yako na utafanikiwa.

Hizi ndizo tabia ambazo ukiwa nazo, mafanikio kwako yataishia kuwa ndoto za mchana:-

1.Kutokuwa na malengo.
Ili mtu afanikiwe lazima awe na malengo. Malengo ndio chanzo cha mafanikio, mafanikio hayaji kwa bahatí mbaya. Watu wote waliofankiwa unaowafahamu na usiowafahamu walikuwa na malengo, wakayaweka katika vitendo na kufanikiwa. Kama wewe ni mwanafunzi weka lengo unataka kuwa nani baadaye, vinginevyo utaishia kusoma na kubaki huna kazi ya kufanya; unakuwa umepoteza muda bure katika maisha yako.

Kama wewe ni mfanyabiashara weka lengo la kuwa mfanyabiashara mkubwa. Zingatia kwamba malengo ndiyo yanakupa dira na muelekeo katika maisha yako. Kupitia malengo unajua unatakiwa uanzie wapi na uishie wapi kulingana na lengo ulilojiwekea kwa wakati huo. Kutokuwa na malengo katika maisha ni sawa sawa na kusafiri bila kujua unaenda wapi. Hii ni hatari sana kwako.



2 .Kutokuwa na malengo  maalum yanayoeleweka.
Kuwa na malengo haitoshi, ni lazima uwe na malengo yanayoeleweka na kufikika. Ni kosa Kubwa kuwa na malengo mengi Ambayo hayafikiki na kutaka kuyatekeleza kwa wakati mmoja. Kuwa na malengo mengi  humfanya mtu achanganyikiwe. Mtu mwenye malengo mengi ana hatari ya; Kuchanganyikiwa na kushindwa kuamua aanze na lipi, amalize na lipi,pia ana hatari ya kutekeleza mambo nusunusu na hatimaye kushindwa kuendelea kabisa na mipango hiyo.

Weka malengo machache ambayo una uwezo wa kuyatekeleza kwa muda uliopanga kisha anza kutekeleza mpango mmoja hadi mwingine. Ukishafanikiwa kutekeleza mipango hiyo weka lengo lingine na utazidi kupiga hatua moja hadi nyingine na kuzidi kufanikiwa siku hadi siku.

3. Kukosa uvumilivu.
Mafanikio ni safari ndefu sana katika maisha ya binadamu. Mafanikio ya kweli yanachukua muda mrefu kupatikana, hayachukui muda mfupi kama wengi tunavyotaka. Kutaka mafanikio kwa muda mfupi ni tatizo ambalo limetukumba wengi katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Watu wengi tunaiogopa safari ndefu ya mafanikio, tunataka mafanikio ya muda mfupi.

WatuWengi wanakata tamaa mapema kwa kwa sababu wanataka mafanikio kwa mnuda mfupi jambo ambalo haliwezekani. Matokeo yake wanaamua kupita njia za mkato ili kufikia malengo wanayojiwekea. Usiogope kuchukua muda mrefu hadi kufanikiwa,hayo ndiyo mafanikio ya kweli. Ikiwa unataka kufikia mafanikio, usiogope kupita jangwani.


 4. Kukosa nidhamu.
Nidhamu ndicho chanzo cha mafanikio. Ukitaka kufanikiwa ni lazima ujitambue wewe ni nani una lengo gani na unapaswa kufanya nini ili kufanikisha lengo lako. Si hivyo tu unapaswa kuwa na mipaka katika utendaji wako. Unapaswa kujua lipi la kufanya na lipi si la kufanya, LAZIMA UWE NA NIDHAMU. Nidhamu ni uwezo wa kujitawala na kujizuia, kujiwekea  mipaka ya utendaji wewe mwenyewe bila kusimamiwa.
Unaweza kuiga na kufanya karibú kila kitu unachokiona na kukisikia, lakini si lazima uige na kufanya, mambo mengine siyo ya kuiga. Jiheshimu mwenyewe, pia  heshimu na kazi yako.Usiache kazi na  kufanya mambo mengine yasiyo ya msingi ambayo hayakusaidii kufikia lengo lako.

5. Kukosa shukurani.
Hakuna mtu anayefanikiwa katika maisha yake kwa juhudi zake mwenyewe bila kuwategemea wengine kwa namana yeyote ile, hayupo dunia hii. Tambua mchango wa wengine katika mafanikio yako. Kuna njia  nyingi za kuonyesha kwamba unatambua mchango wa jamii inayokuzunguka katika mafanikio yako. Baadhi ya mashirika na taasisi huamua kuchangia huduma za jamii kama elimu na afya kwa kutoa vitendea kazi kwa shule au hospitali.

Baadhi ya watu huamua kuwasaidia wengine katika shughuli zao   kiuchumi. Yapomambo mengi unayoweza kufanya ili kuonyesha kwamba unatambua mchango wa wengine katika mafanikio yako. Si vyema kutokufanya jambo kwa ajili ya wengine ikiwa wapo ambao walifanya kitu fulani na wengine wanaendelea kufanya kwa ajili ya mafanikio yako. Kwa hakika kuna watu wamefanya kitu fulani kuchangia mafanikio yako, wewe unafanya nini kwa ajili ya wengine?

6. Kuwa na hofu sana.
Watu  wengi huwa wanaogopa kujaribu kufanya kazi fulani kwa sababu watachekwa au kujishushia hadhi mbele ya jamii. Baadhi ya watu wanaogopa kujaribu  kwa sababu wakishindwa watachekwa na kujisikia vibaya. Wengine wanaogopa kupoteza fedha baada ya kupata hasara. Ni bora kujaribu ukashindwa kuliko kutokujaribu    kabisa. Mafanikio huja kwa kujaribu na kushindwa bila kukata tamaa. Katika ugunduzi wa gropu,Thomas Edison alishindwa zaidi ya mara elfu moja, hatimaye alifanikiwa mpaka leo hii tunasimulia habarí zake na kujifunza kutoka kwake.

Thomas Edison anasema,Udhaifu wetu mkubwa upo kwenye kukata tamaa. Njia ya hakika ya kuweza kufanikiwa ni kujaribu mara nyingine  tena. Kupata matokeo Ambayo hukuyatarajia na huyataki katika jambo ulilolifanya, haina maana kwamba matokeo hayo hayana faida.Wakati umejaribu njia zote na kushindwa, kumbuka hili-HUJASHINDWA. Kumbuka, kujaribu na kushindwa ni sehemu ya mafanikio.


Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku, karibu sana.

  • Makala hii imeandikwa na DEOGRATIUS GUNJU WA MBEYA TANZANIA
  • Mawasiliano 0718 610022






Apr 24, 2019

Usipoteze Muda Wako, NI Utajiri Wa Kesho Yako.

No comments :
Muda ni mchache, maisha uliyonayo au maisha tuliyonayo ni mafupi, kwa hiyo kila muda na fursa unayoipata hata kama ni ndogo sana, tafadhari itumie vizuri na kwa uhakika mkubwa. Kutumia muda wako hovyo, hakuna tofauti na wewe kuamua kupoteza fursa za mafanikio yako tena kwa makusudi.
Ili kutumia muda wako vizuri, unatakiwa kufanya kile kinachotakiwa kufanyika kwa wakati ule  hata kama mwili wako uwe unataka au hutaki.  Moja ya kanuni ambayo inatumika na watu ambao hawafanyi kitu katika maisha, ni kutokuchukulia leo katika umuhimu wake. Kama leo yako unaiona ipo ipo tu, upo kwenye wakati wa kupoteza.
Maisha ya mafanikio yanatengemezwa na hatua ndogo ndogo sana za kila siku. Inapotokea wengine wanasita kuchukua hatua wewe unatakiwa kuchukua hatua na si kupoteza muda na kusema nitafanya siku nyingine. Muda ulionao ni wa dhahabu, ukipotea umepotea, kama ukijua thamani ya muda wako hutaweza kuupoteza tena.

Moja ya siri ya kufikia mafanikio yako ni kutumia kwa usahihi kila fursa ambayo unaipata. Muda unakwenda na kupaa, unatakiwa kuwa rubani kuendesha muda wako kwa usahihi. Jiulize,  usipotumia leo fursa za mafanikio unazozipata unataka kutumia fursa hizo lini au wakati gani, naamini unanipata vyema.
Mwanamafanikio William Ward moja katui ya maandiko anasema, “unatakiwa ujifunze kujiendeleza kwa kusoma wakati wengine wamelala, unatakiwa kuwekeza wakati wengine hawaoni fursa, unatakiwa kujiandaa kwa kila kitu wakati wengine wanacheza”. Acha kupoteza muda wa maisha yako kwa chochote, utumie vizuri.
Elewa hakuna muda bora kama huu ulionao kwa sasa. Kama utakuwa ni mtu kupoteza muda wako na kusubiri, hicho unachosubiri upo uwezekano hutaweza kukifanya tena au utakifanya kwa tabu. Wengi wanaoahirisha mambo ukumbuke huja kuyafanya tena mara nyingi huwa ni ngumu sana kwao kuweza kutokea.







Apr 23, 2019

Kama Utapoteza Jambo Hili, Hutalipata Tena Maishani Mwako.

No comments :
Katika kijiji kimoja kulikuwako na watu watatu ambao walikuwa na safari ndefu sana ya kuelekea mbali na mahali walipokuwa wanaishi, safari hii ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kujitafutia  riziki zao za kila siku ambazo zilipatikana katika msitu fulani uliokuwa  mkubwa sana.
Watu hawa walitembea kwa umbali mrefu sana ikafika mahala wakawa wapo  katikati ya pori ambapo walianza kuingia na hofu ndani mwao, watu hawa majina yao ni, mtu wa kwanza alikuwa akifahamika kama moto, mtu wa pili alikuwa akifahamika kama maji na mtu wa tatu alikuwa hajulikani ni nani.
Wakiwa katikati ya pori wakiwa wamejawa na  wasiwasi na wanakokwenda  huku wakiwa hawaelewi watafika lini na muda gani, mmoja wao  akawambia wenzake “ jamani eeh hebu tusimame tuelezane kitu kimoja,  huyu hakuwa mwingine bali alikuwa ni moto, huku tukokwenda  nahisi tunaweza tukapotea.

Kama tunaweza tukapotea inabidi tuambiane ishara mapesa kabisa kwamba je, kama ukipotea utawezaje kujulikana sehemu uliyopo? yeye moto akasema  ikitokea tumeenda mahali na tukagawana kila mtu njia yake na ikawa haileweki mtu mwingine yupo wapi,  mimi kama moto ikatokea nimepotea basi msisumbuke kunitafuta ninyi angalieni ishara ya moshi popote utakapouona moshi unapotokea basi  hapo ndipo nitakapokuwepo.
Wakati huo wote moto anazungumza maji na yule mwingine ambaye hajulikani wakasema sawa mkuu sisi tumekuelewa.
Ikafika zamu ya maji naye kuzungumza, maji akasema “ moto mimi nakubaliana na wewe hata mimi nahisi kabisa kuna kila dalili zote za kupotea katika msitu huu, hivyo kama ikitokeo tumegawanyika na mimi nikapotea, mimi ili niweze kuonekana wala usisumbuke wewe angalia ishara ya kijani, ukiona sehemu ya kijani hapo ndipo utakaponipata.
Baada ya moto na maji kuzungumza hayo ikafika zamu ya mtu wa tatu ambaye hajulikani  kuzungumza, yeye akasema “jamani mimi mwenzenu sitabiriki”  mimi nikipotea sielewi mtanipataje kwa kweli maana mimi sina ishara yeyote ile nitakayoifanya ili mnione.
Sasa mimi na wewe tujiulize huyo mtu wa tatu alikuwa ni nani? Ambaye alisema hana ishara yeyote ile endapo atakuwa apotea? Endele kutafakari kisha unipe jibu.
Ila kwa kuwa umekuwa mzembe wa kuumiza kichwa basi ngoja nikupe jibu, mtu wa tatu alikwa ni muda.
Fundisho la hadithi hii ni:
Katika maisha yako poteza vitu vyote utavipata lakini usije ukapoteza muda wako huwezi kuupata, tumeona kuwa moto ukipotea ishara yake huwa ni moshi,  pia tumeona maji yakipotea ishara unaweza kuona ni ukijani katika uoto lakini muda ukipotea basi andika umeumia kwasababu muda huo hauwezi kurudi tena.
Kwahiyo tunafundishwa poteza  vingine kwenye maisha ila usithubutu kuja hata siku moja kuja kupoteza  muda wako, kwani ukipoteza muda hakuna ishara itakayokuonesha namna ya kupata ule muda ulioupoteza.
Hivyo fundisho kubwa hapa ni kuhakikisha unatumia muda wako vizuri ila kwa baadae usije ukajuta kwamba ulikuwa mjinga kwa kupoteza muda wako kwa kiasi hicho.
Nikutakie kila la kheri na tafakari njema ya hadithi hii, byee.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA AFISA MIPANGO BENSON CHONYA.


Apr 22, 2019

Kama Utakosa Kitu Hiki Sahau Kuishi Maisha Ya Uhuru, Furaha Na Mafanikio.

No comments :
Kama upo kwenye chombo cha usafiri, halafu ni usiku  na tena unataka kusafiri mbali na kwa haraka zaidi, kitu cha kwanza unachotakiwa kuhakikisha chombo hicho inacho ni mwanga wa uhakika. Pasipo mwanga wa uhakika safari yako itakuwa ni ya shida kidogo, unaweza ukaenda lakini si kwa kasi na mwendo ule unaoutaka wewe.
Hata kwenye maisha yako ukitaka kufika mbali kimafanikio kitu kimojawapo unachotakiwa kuwa nacho ni kujifunza kuwa na msamaha. Unapokuwa na msamaha, inakusaidia kuondoa uchungu, hasira, visasi vyote unakuwa umeweka pembeni na matokeo yake unakuwa huru kufanya mambo mengine na kusonga mbele.
Kuishi maisha ya kutokuwa na msamaha, ni sawa na kuendesha gari huku ukiwa umeshikilia breki, kwani kwa kufanya hivyo mwendo wako hautakuwa mzuri, ni rahisi kukosa mwelekeo na hata kupotea kabisa. Unatakiwa kukumbuka unapokuwa na msamaha hiyo inakuweka huru sana wewe kuweza kufikia mafanikio yako.

Unapoamua kuishi maisha ya kutokuwa na msamaha kitu kitakachofatia hapo kwako ni kwa wewe kuishi maisha ya kisasi. Inapotokea ukaishi maisha ya kisasi mwanzo inaweza ikaonekana ni maisha mazuri, lakini nikwambie maisha hayo yanakuwa ni mabaya sana kwako kwani yatakuzuia wewe kuweza kuendelea mbele sana.
Unapokosa msamaha kabisa ujue unakuwa maisha ambayo yanakuwa ya uchungu karibu wakati wote. Unatakiwa kujua ufunguo mojawapo wa furaha ni wewe kujijengea tabia ya kuwa na msamaha. Kama hautakuwa na msamaha sahau kabisa kwa wewe kuweza kuishi maisha ya furaha au maisha ya uhuru.
Kwa mujibu wa wataalumu wa saikolojia na mafanikio, inasemekana moja ya siri muhimu ya kuishi maisha marefu na yenye faida kila siku ni kwamba kabla hujalala, jifunze kumsamehe kila mtu ambae amekukosea. Unapowasamehe watu hao ambao wamekukosea hiyo ni njia ya wewe kuendelea kufanikiwa kwenye mambo yako.
Ni bora ukasamehe na kusahau kuliko ukashindwa kusamehe na kukumbuka. Elewa, kusamehe kila wakati kunaendana na Baraka, lakini kutokusamehe kunakuumiza wewe na kunakupotezea sana milango mikubwa ya Baraka ambayo inatakiwa itokee kwako. Kwa hiyo ipo haja ya wewe kuweza kusamehe kwa namna yoyote ile.
Kabla hujamaliza  siku yako unatakiwa ujue ni watu gani ambao wanahitaji msamaha wako na wasamehe hata usipowaambia. Usichome daraja moto mara baada ya kuvuka mto. Nikwambie huwezi kujua utatumia daraja hilo mara ngapi tena kwa usafiri. Ipo faida ya kuishi maisha ya msamaha, hebu anza leo kuishi maisha hayo uone faida zake.
Jiulize ni wapi unakwama hadi ushindwe kutoa msamaha, je msamaha unaotaka kuutoa kwani unalipiwa? Kama msamaha unaotaka kuutoa ni bure, hebu samehe na kisha baki huru na maisha yako. Maisha yako hayatakuwa mabaya kisa umemeshindwa kusamehe, zaidi utajenga maisha ya mafanikio makubwa kwako.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,











Mar 11, 2019

Tabia Muhimu Zitakazokusaidia Kukupa Mafanikio Kwa Kiasi Kikubwa.

No comments :
Moja ya sheria ya msingi na ya muhimu katika mafanikio yoyote yale ni kuwa na tabia nzuri. Tabia ni moja ya kitu ambacho ni cha msingi sana katika kukupa mafanikio yale uyatakayo. Ukiangalia wengi wanaoshindwa, chanzo kinaanzia kwenye tabia zao.
Tuchukulie kwa mtu anayataka mafanikio, kuwa na malengo tu peke yake na kuyafanyia kazi haitoshi, lazima mtu huyu awe na tabia zinazoendana na malengo hayo, kama kuwa na matumizi mazuri ya pesa au utunzaji wa muda mzuri.
Unapokuwa na tabia mbaya na huku ukitaka mafaniko, ni wazi hutaweza kufanikiwa na utahangaika sana kufikia mafanikio hayo. Mpaka hapo unaona tabia ni kitu cha msingi sana katika kukufanikisha wewe kwenye maisha yako.
Unaweza ukawa na mafanikio makubwa sana, ikiwa utajenga tabia bora za kukusaidia kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kila wakati. Je, unataka kuzijua tabia hizi ni zipi za kukusaidia wewe kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa?

1. Tabia ya kutafuta msaada.
Hakuna mtu ambaye anaweza kufanikiwa akiwa peke yake. Kila mtu anahitaji msaada kwa mtu mwingine hata kama msaada huo ni kidogo sana lakini msaada huo unahitajika ili kuweza kujenga mafanikio ya kudumu.
Unapokuwa unawasiliana na wengine na wakajua changamoto zako, ni rahisi sana kwa wao kuweza kukusaidia wewe na kupiga hatua mbele za kimafanikio. Usijaribu kuishi kipeke yako yako, tafuta msaada kwa wengine na utafanikiwa pia.
2. Tabia ya kuchukua hatua.
Unayo nafasi kubwa sana ya kufikia mafanikio yoyote yale unayoyataka kwenye maisha, lakini kama huchukui hatua nikwambie tu, utakufa kwa msongo wa mawazo. Najua una mawazo mazuri lakini hayawezi kufanya kazi mpaka uchukue hatua.
Huhitaji kuwa na hamasa ili uchukue hatua, wewe chukua hatua kwa hali yoyote uliyonayo. Acha kuendelea kufikiria sana juu ya ndoto zako, chukua hatua. Soma vitu vya kukusaidia na kisha amua kuchukua hatua na ukijenga tabia hii itakusaidia sana.
3. Tabia ya kutokuishi kimazoea.
Maisha ya watu wengi yanakuwa mabaya kwa sababu ya kuishi sana kimazoea. Kuishi kimazoea ni sumu kubwa sana ya wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa. Unatakiwa ujue namna ya kuishi nje ya mazoea yako ili uweze kufanikiwa zaidi.
Kila wakati tafuta namna ambayo itakusaidia wewe kuweza kuishi nje ya mazoea yako. Ikiwa lakini kila wakati unaishi kwenye mazea hayo hayo itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kusonga mbele na kupigia hatua hasa za kimafanikio.
4. Tabia ya kusema hapana.
Hii ni moja ya tabia nzuri sana kwako wewe kuindeleza ili kufikia mafamikio. Unatakiwa kujifunza kusema hapana kwa mambo mengi sana. Unatakiwa ujue kusema hapana kwa wanaokupotezea muda wako au kwa yale mambo usiyoyahitaji.
Ikiwa wewe utakuwa ni mtu wa kukubali kila kitu, kwamba kitu hiki kiwe hivi au vile ni ngumu sana kuweza kupiga hatua sahihi za kimafanikioo husika. Jifunze kusema hapana kwa kila kitu ambacho hakina manufaa kwako wewe.
5. Tabia ya kuchukua majukumu yako.
Unatakiwa ujue kila mtu ana changamoto zake za kimaisha, lakini kama unashindwa kuwajibika na majukumu hayo na kila wakati kutaka kulaumu tu watu wengine, hilo tu nikwambie utakuwa ni miongoni mwa watu ambao watashindwa sana.
Nikwambie tu, kubali kuwajibika kwa kila jambo linalokuhusu wewe. Wajibika kwenye ndoto zako, wajibika kwenye maisha yako ya kila siku. Kila wakati ujue jinsi ya kuwajibika na hapo utaweza kupiga hatua za mafanikio sahihi kwako.
Hivi ndivyo unavyoweza ukatumia tabia hizo vizuri na zikakusaidia wewe kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kwenye maisha yako kama unavyotaka iwe. Ni jukumu lako wewe sasa kuchukua hatua na kuhakikisha unasonga mbele.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,






Mar 10, 2019

Ikiwa Unaishi Hivi, Maisha Yako Ni Mafupi Sana.

No comments :
Ni jambo ambalo watu hulisema  mara nyingi bila kujua maana yake. Unaweza kukuta mtu akisema, ‘ndio maana amekauka, ana roho mbaya sana’. Ukimuuliza ni kwa nini anahusisha kukauka au afya mbaya na roho mbaya au kukosa upendo alikonako mtu, hataweza kukupa jibu sahihi. Lakini, anajua kwamba, kukauka huwapata wenye roho mbaya. Kauli hiyo ina ukweli mkubwa wa kutosha. Watu wengi ambao wanatengeneza nguvu nyingi hasi, hatimaye nguvu hizo huwarudia na kuwadhuru.

Kwa sehemu kubwa, madhara ya nguvu  hizo huja kujitokeza kwenye miili yao. Mtu ambaye anaumwa mara kwa mara, anaweza kuwa anaumwa tu kwa sababu nyingine, lakini pia anaweza kuwa anaumwa kutokana na nguvu hasi anazotengeneza. Nikisema nguvu hasi, nina maana ya kufikiri na matendo ambayo yanamuumiza mwenye mawazo na matendo hayo, pia wale wanaomzunguka. Kwa mfano, mtu asiyeweza kusamehe, mwenye visasi, mwenye kijicho, mpenda makuu, mshindani na mengine ya aina hiyo.

 Kuna watu ambao hutengeneza sana nguvu hasi kwa kufikiri kwao na tabia zao. Kwa kawaida, nguvu hasi huwa zinadhuru hisia na mwili wa mhusika. Kwa vipi? Hebu tutazame kushindwa kusamehe na kijicho. Mtu ambaye hawezi kusamehe, anajiweka mahali ambapo muda wote anakuwa kwenye hasira, hisia chungu na mikakati ya kulipa kisasi. Hii ni sawa na mtu ambaye ana kijicho, kwa mfano. Huyu naye, muda mwingi wa maisha yake, atakuwa akiumia kwani, kila wengine wakifanikiwa kwa chochote, atajihisi vibaya tu. kwa hiyo, hisia zake zitakuwa zinachokozeka karibu muda wote.

Kwa kawaida, hisia zetu zinapochokozeka, tunaiiingiza miili yetu kwenye kuzalisha kemikali au homoni ambazo wakati huo hazihitajiwi. Kwa uzalishwaji huo wa kemikali zisizohitajika mwilini, tunaiumiza miili yetu kwa njia mbalimbali. Kemikali hizo, hatimaye huanza kutuumiza kwa kuteleta maradhi mvalimbali miilini mwetu. Hili ni jamba ambalo limethibitishwa kitaalamu.


Kuna maradhi zaidi ya kumi ambayo chanzo chake ni mihemko yetu, maradhi ambayo kitaalamu hufahamika kama Emotionally Induced Diseases. Haya ni pamoja na maumivu ya mwili, tumbo, kufunga choo na mengine. Ndiyo maana, wale watu wote wanaokwenda hospitalini wakiwa wanaumwa, ambao wanaambiwa vipimo havioneshi maradhi yoyote, ukiwachunguza, utagundua kwamba, wanakabiliwa na hofu, mashaka, visasi  na matatizo mengine ya kihisia.

Sisemi kwamba, wote wanaopimwa na kuonekana hawana maradhi ndivyo walivyo, hapana. Lakini wengi kati yao ndivyo walivyo. Hata wale wanaodaiwa kuwa na mapepo pia, utakuta baadhi ni wale wenye hisia chungu. Kwa sababu ya maumivu ya kimwili na yale ya kiakili, unakuta watu hawa wakiwa dhaifu. Kama walivyo wagonjwa wengine, suala la udhaifu wa kimwili hujitokeza sana kwa watu hawa, kwani pamoja na maradhi yanayoletwa na hisia chafu, kinga ya mwili hushuka sana pale miili inapohemkwa mara kwa mara.

Ni rahisi kwa hali hiyo, watu wenye roho mbaya kukauka au kukosa afya imara. Ingawa siyo kweli hata hivyo kuwa watu wote wenye afya mbovu, inatokana na roho mbaya, hapana. Lakini, kwa wale walio na roho mbaya, yaani kufikiri na tabia zenye kuzalisha nguvu hasi, ni rahisi zaidi kwao kukosa afya bora kama tulivyoona. Ndiyo maana tunasema hivi, kama unaishi maisha haya kuwa na roho mbaya tu, maisha yako ni mafupi kwa sababu utakuwa ni wa afya mbovu kitu ambacho ni hatari sana kwako.

Nakutakia kheri ya mwaka mpya, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,




Mar 9, 2019

Kama Mambo Yako Yako Hovyo, Yaweke Sawa Kwa Kufanya Hivi.

No comments :
Ikiwa kuna wakati unaona maisha yanakuchanganya hasa kutokana na changamoto unazokutana nazo, usije ukakubali ukafanya kosa la kuchanganywa huko, badala yake tuliza akili yako na tafuta mwelekeo sahihi wa maisha yako kwa kuweka mambo sawa.
Ikiwa unaona pia unaweka juhudi nyingi sana na juhudi hizo hazikupi matunda sahihi, hapa tena usikatishwe tamaa, endelea kuweka juhudi, lakini tafuta kuelewa kwa nini juhudi zako hazikufanikishi na anza kutafuta njia nyingine itakayokupa matokeo makubwa kwako na kuweka mambo sawa.
Upo wakati katika maisha yako ambapo kuna mtu au watu  watakurudisha nyuma hata bila ya wewe kutegemea. Inapotokea wakati kama huu, sio swala la kutupa lawana na kusikitika, bali ni kuuvaa ujasiri na ushujaa na kutafuta mwelekeo upya kwa kuweka mambo yako sawa.
Kuna wakati katika  maisha yako unajiona upo njia panda, huelewi hata ufanye nini, inapofika wakati huu , jifunze kuweka nguvu za uzingativu katika kitu kimoja na kutafuta mwelekeo sahihi utakaokusaidia kuweka mambo yako sawa na yakae katika mkao wa mafanikio.
Zipo nguvu nyingi na kubwa sana katika maisha yako, ambapo nguvu hizo zinauwezo wa kubali hali yoyote ambayo unayo na unaona ni  mbaya na nguvu hizo hadi kukupa mafanikio halisi kama vile unavyotaka iwe.
Ndio maana, badala ya kulalamika na kutoa kila aina ya visingizio, jitahidi sana kuweka mambo yako sawa, kila unapoweka juhudi ya kuweka mambo yako sawa, utajifunza na kugundua kwamba kumbe unaweza ukatawala maisha yako kwa jinsi unavyotaka.
Je, katika maisha yako kuna kipi ambacho unakiona ndio tena basi kimeharibika na hakiwezi kukusaidia hata kufanikiwa. Kama kipo kitu cha namna hiyo, anza kikiweka sawa na kutafuta njia ya itakayofanya kitu hicho kikupe matunda uyatakayo.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, fursa za mafanikio zinapopatikana, ajira pamoja na uwekezaji, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Pia kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, PURE KIENYEJI na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Mar 8, 2019

Kama Utaruhusu Kelele Hizi…Utashindwa Kufanikiwa.

No comments :

Usisikilize kila kitu
Zipo kelele nyingi sana katika dunia hii ya habari. Utasikia hiki mara utasikia kile, ilimradi kukicha tu zipo habari na taarifa nyingi ambazo zinatolewa ambazo lengo lake wewe uzisikie na pengine kuzifanyia kazi.
Usipokuwa makini utajikuta kila kitu unataka kufatilia. Sasa njia ya kuweza kujiokoa na kelele hizo na kuweza kufanikisha malengo yako ni kwa wewe kuweka nguvu zako za uzingativu kwa kile unachokifanya.
Angalia kipi unakifanya, kisha kifatilie kitu hicho kila siku. Kelele za huku mara kule acha kuzifatilia zitakupoteza. Kumbuka, mikwenzi mingi ilimpoteza mbwa mawindoni, usiwe miongoni mwa watu watakao potea kwa sababu ya kelele.
Simamia na fatilia mipango yako kwa kuweka nguvu za uzingativu kwa kile ukifanyacho na utafanikiwa. Kuendelea kusikiliza kelele au kila linalosemwa utakuwa ni sawa na mtu ambaye ameamua kujipoteza yeye mwenyewe.
Katika dunia ya sasa, ni rahisi sana kusikia fursa hii au ile, lakini kwa ukweli uliowazi wewe kama wewe huwezi kufanya kila kitu. Kama ni fursa ni lazima utafanya chache na si kila fursa itakuwa yako.
Hivyo unatakiwa kuwa makini na taarifa unazozipokea. Unatakiwa kuwa mtulivu na usiwe mtu ambaye unaendeshwa na mihemiko isiyo ya maana. Kelele za dunia zisikuyumbishe hata kidogo, fuata malengo yako.
Ikitokea umekubali kuyumbishwa na dunia au na kelele za dunia, basi utaishi kama bendera fuata upepo maana hutafika popote. Utagusa hiki mara kile na kila kitu utakuwa unakianza na kukiacha kila ukisikia kuna kingine kizuri kinalipa.
Kuanzia leo jifunze kuweka masikio yako pamba, jifunze kuweka nguvu zako za uzingativu eneo moja, mahali ambapo utafanya kitu na kitaonekana cha thamani. Ukiziba masikio usisikie kitu, utajenga uwezo mkubwa wa kufanikiwa.
Chukua hatua kwa kufanyia kazi hicho ulichojifunza na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza na kuhamasika zaidi kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com