google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Feb 27, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Muda Wako Vizuri Na Kukuletea Mafanikio Makubwa.

No comments :
Muda ni mali! Huu ni usemi maarufu sana kwa vijana na wazee. Unaonekana ni usemi wa kawaida na uliozoeleka kwa watu wengi, maskini na matajiri, wanawake na wanaume. Japokuwa watu wengi tunautumia usemi huu, lakini baadhi yetu hatuelewi maana yake na wengi wetu hatuutumii katika maisha yetu.

Muda ni mali maana yake kila kitu, vitu vyote vinavyoonekana vidogo na vikubwa ni matokeo ya matumizi ya muda. Hata mimi na wewe ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kila mafanikio yaliyowahi kutokea na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya matumizi mazuri ya muda. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na matumizi ya muda,yaani muda ukitumika vizuri mafanikio yanapatikana na muda huo huo usipotumika vizuri hakuna mafanikio.

Hakuna haja ya kueleza na kufafanua maana ya muda, ila nataka ujue kuwa kuna aina za muda, ndiyo zipo aina mbili za muda. Aina ya kwanza ya muda ni MUDA WA SAA. Muda huu unaanzia sekunde hadi mwaka. Katika muda wa saa, tunaposema miaka miwili ni miaka miwili, haizidi wala haipungui.Tunaposema huyu ana miaka hamsini ina maana mtu ameishi vipindi hamsini ambapo kila kipindi kina jumla ya miezi kumi na mbili, haizidi wala haipungui.

Aina ya aili ya muda ni MUDA HALISI. Muda halisi unaundwa na muda wa saa na matukio. Katika aina hii ya muda tunaangalia matukio yaliyotokea katika muda wa saa husika.Tunalinganisha idadi ya miaka na miezi na matukio au mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika. Watu wanaweza kuwa sawa katika muda wa saa lakini wakawa tofauti katika muda halisi. Mtu anaweza kuwa na umri wa miaka sitini(katika muda wa saa) lakini akawa kwa mafanikio ni kama mtu aliyeishi miaka thelathini tu.

Na pia mtu mwingine anaweza kuwa na umri wa miaka thelathini, lakini akawa na mafanikio makubwa sana kimaisha kama mtu aliyeishi miaka mingi sana duniani, yawezekana hata miaka sabini. Usichanganyikiwe, nalinganisha muda wa saa na mafanikio. Muda halisi unatuambia kwamba kuna kuchelewa katika maisha. Muda halisi unatukumbusha kuwa kuna wakati tunaweza kupoteza miaka yetu bila kujua. Unatukumbusha kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi. 

Tumejifunza aina za muda na tofauti zake, sasa tuangalie  matumizi ya muda wa saa.Tunatumia  muda huu kufanya mambo matatu ambayo yanatuleta kwenye muda halisi, tukiwa tumewahi au tumechelewa  tunatumia muda katika kufikiri, kusema au kuzungumza na kufanya mambo mbalimbali katika maisha yetu.

Baada ya kuangalia matumizi ya muda wa saa, tumegundua kuwa tunautumia muda kama chombo kutusafirisha kutoka katika ulimwengu wa namba na mahesabu kwenda kwenye ulimwengu wa halisi,ulimwengu wa vitendo ambapo tunaweza kufanya tathmini na kuona kuwa tumewahi au tumechelewa, tuko nyuma au  tuko  mahali sahihi.

Sasa tuangalie mambo ya kufanya ili tuweze kuutumia muda wa saa na kufikia mafanikio ambayo yataweka uwiano sawa kati ya muda wa saa na muda halisi katika maisha yetu.Yapo mambo mengi ambayo unapaswa kuyafanya ili uweze kutumia muda wako vizuri, baadhi ya  mambo hayo ni haya yafuatayo:-

1. Weka kumbukumbu ya mambo unayofikiria, unayoyasema na kutenda.
Kumbukumbu ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kwa sababu ndizo zinazotusaidia kufanya tathmini. Jitahidi kuweka kumbukumbu za mambo unayofikiri, unayosema na kutenda japo kwa siku moja. Mwisho wa siku jitahidi kukukumbuka mambo uliyofikiria, uliyosema na kutenda yawe mazuri au Mabaya. Hii itakusaidia kufanya tathmini ya matumizi ya muda kwa siku hiyo.

Tathmini hiyo itakusaidia pia kujua umetumia muda vizuri au vibaya. Mara nyingi sana siyo rahisi kukukumbuka mambo yote uliyofikiria na kusema lakini ni rahisi kukukumbuka matukio na mara nyingi matukio hutokana na kufikiri na kusema,kwa hiyo kukumbuka matukio ni njia rahisi zaidi yakukuwezesha kufanya tathmini ya siku nzima.


2. Weka ratiba ya siku nzima.
Ratiba ni muhimu sana katika maisha ya kila siku.Usianze siku bila kujua utafanya nini siku hiyo. Unaweza kuweka na kupanga ratiba ya siku inayofuata kabla ya kulala au asubuhi kabla hujaanza jambo lolote. Watu wote waliofanikiwa, wamefanikiwa kwa sababu ya matumizi mazuri ya muda, wanafanya kazi zao kwa ratiba na wana nidhamu linapokuja swala la matumizi ya muda. Bila kuwa na ratiba muda hutumika bila mpangilio na wakati mwingine muda hupotea bure. Unapoweka ratiba hakikisha kila kitu ulichokiweka kina wakati na muda wake.  Kinaanza saa ngapi na kuisha saa ngapi. Ni vyema ratiba hii iwe na mambo ya msingi tu. Usisahau mapumziko. Mapumziko ni muhimu kwa utendajibora wa akili na mwili.

3. Epuka kuwa na mipango mingi.
Katika ratiba yako usiweke mambo mengi sana ambayo utekelezaji wake ni mgumu au yanachosha.Weka mambo machache  ambayo yanakupa nafasi ya kupumzika na kutafakari namna ya kuianza siku inayofuata. Ukiweka mambo mengi kuna hatari ya kuyatekeleza nusunusu na mengine yanaweza yasitekelezwe kabisa.

4. Usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia ratiba yako.
Mara unapoanza kutekeleza mipango ambayo iko kwenye ratiba yako, usiruhusu mambo yasiyo ya msingi kuingilia na kuvuruga ratiba yako. Kuwa na nidhamu na heshimu ratiba yako. Zipo dharura lakini si dharura zote  zinahitaji kushughulikiwa papo .Kama dharura ni ya msingi na inahitaji kushughulikiwa papo hapo hamna tatizo.Jifunze kutambua na kutofautisha dharura zinazohitaji kushughulikiwa papo hapo na zile zinazoweza kushughulikiwa baada ya ratiba kukamilika.

Kuna watu ambao wako tayari kuvuruga ratiba zao na kuacha shughuli zao kwa sababu ya mambo yasiyo ya msingi kwa mfano kuangalia mechi na burudani zingine ambazo haziwasaidii katika maisha yao. Narudia tena,uwe na nidhamu heshimu ratiba yako.

5. Epuka kutumia muda mwingi kufanya mambo yasiyo ya lazima na yasiyo na faida.
Epuka kutumia muda mrefu kufanya mambo yasiyo ya msingi na yasiyo na faida kwa mfano kuchati kwenye mitandao ya kijamii, kuangalia mechi na burudani zingine wakati ambapo unatakiwa kufanya mambo ya msingi kwa ajili yako na jamii inayokuzunguka. Sina maana mitandao ya kijamii mibaya ila nasisitiza kuwa na kiasi na kuipa nafasi ndogo katika maisha ya kila siku. Kama utakuwa unawasiliana kwenye mtandao wa kijamii basi iwe kwa faida na si kupoteza muda.

Ninasema hivi kwa sababu hili limekuwa tatizo Kubwa  sana kwa kizazi cha sasa hasa vijana, tena wanafunzi ambao wanatakiwa wasome kwa bidii wasipoteze muda hata kidogo. Muda wa kufanya mambo ya msingi utumike kufanya mambo ya msingi na mambo mengine yapewe nafasi ya pili au ya mwisho.

5. Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo ya msingi.
Unashauriwa kutumia 75% hadi 80% ya muda wako kufanya mambo yenye tija kwako na kwa wanaokutegemea.Tumia sehemu Kubwa ya muda wako kufanya mambo yatakayokujenga na kukuimarisha kiakili,kijamii na kiuchumi. Fanya kazi za kukuingizia kipato, soma vitabu, magazeti, na majarida yatakayokuongezea  maarifa na kupanua ufahamu wako.Ukiingia kwenye Internet soma vitu vinavyokujenga na siyo kufuatilia habari za watu maarufu huku hakuna cha maana unachopata.

Wengine wanaingia kwenye Internet  kuangalia ili kuangalia picha za ngono na utupu. Watanzania wengi watu wazima ukiwauliza walisoma vitabu lini, hawakumbuki, wengine wanakwambia shule ya msingi na wengine sekondari, inasikitisha. Wengine hata wanaponunua simu, hawasomi vile vitabu vinavyoelekeza namna ya kutumia hiyo simu. Watu walio wengi sana kama ni kusoma wanapenda kusoma vitu ambavyo haviwasaidii sana katika maisha yao kama magazeti ya udaku.

Nakutakia kila la kheri, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

  • Makala hii imeandikwa na Deogratius Harold wa Mbeya- Tanzania.
  • Mawasiliano 0718 610 022







No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.