google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Mar 4, 2015

Acha kutumia Njia Hii Kutafuta Mafanikio, Itakukwamisha Tu.

No comments :
Kuwa na mafanikio makubwa ni ndoto ambayo karibu kila mmoja wetu anayo katika maisha yake. Umuhimu huu wa kutafuta mafanikio unakuja, kutokana na wengi wetu kuwa wamechoshwa na maisha ya kubahatisha ambayo wanayo kila siku. Hivyo, kwa sababu hiyo wengi hujikuta wakifanya kila linalowezekana ili kufikia mafanikio hayo wanayoyahitaji ili mradi tu wafanikiwe.

Hata hivyo wengi wengi wetu huamua kusaka mafanikio kwa kutumia njia tunazojua na kuziamini sisi kuwa zitatufikisha katika kilele cha mafanikio. Kwa bahati mbaya, wapo ambao hutumia njia ambazo siyo sahihi kutafuta mafanikio na siku ya mwisho hujikuta wamekwama na kuanza kulaumu. Kwa leo nataka nikuonyeshe njia moja tu, ambayo wengi wamekuwa wakiiamini kwamba wakiitumia watapata mafanikio kwa urahisi.

Hii ni njia ambayo hata wewe unaijua na pengine umeshawahi kuitumia, lakini ukiendelea kuing’angania ipo siku itakurudisha nyuma sana mpaka utashangaa. Njia hii ni njia ya mkato, ni njia ambayo inapendwa na wengi katika kutafuta mafanikio. Hapa wengi sana wanaamini kupata mafanikio kwa njia rahisi na za mkato na mwisho wa siku huishia wakipoteza hata kile kidogo walichonacho kwa sababu ya kutumia njia hii kutafuta mafanikio.

Mara nyingi nchini kumewahi kutokea michezo inayohusisha pesa ama upatu, ambapo watu walichukuliwa fedha kiujanja ujanja kwa mamilioni.  Ingekuwa ni mara moja, mtu angeweza kusema jambo hilo lilikuwa ni bahati mbaya. Lakini kutokea zaidi ya mara moja na katika mazingira ya wazi kabisa kwamba, ni wizi wa mchana na bado watu wakashiriki, inaonesha ni kwa kiasi gani, watu wengi wanapenda njia za mkato kufikia mafanikio.


Hii inaonekana kwenye Nyanja zote za maisha, kuanzia kusoma, ajira, biashara, malezi, michezo na hata uongozi. Mtu au watu wanatarajia mambo yaende na kujitengeneza yenyewe bila juhudi zao. Kila mmoja anatarajia alale na kuamka asubuhi, mambo yakiwa yamebadilika yenyewe na kuwa safi. Kitu ambacho ni ndoto na hakita kuja kutokea, ingawa ndio wengi wanataka maisha yawe hivyo, hata kama hawasemi vitendo vinasema.

Ndiyo maana waganga wengi wa asili ambao wanadai wanaweza kumfanya mtu kupendwa bila yeye kupenda, kupata pesa bila kazi, kupanda cheo bila juhudi, kufaulu mtihani bila kusoma, wamejaa na wanapata fedha nyingi sana kutokana na wajinga hawa wanaoamini katika njia za mkato. Waganga hawa wamebaini kuwa kuna kufikiri kulikopogoka ambapo wengi hawajiamini katika kujiletea mafanikio halisi.

Bila shaka, ipo idadi kubwa ya watu wanaomini sana kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato. Ni watu wanaoamini hadi sasa kwamba, mafanikio yanaweza kuja bila ya mtu kufanyia kazi. Umefika wakati sasa wa wewe kufundishwa, kubadilika na kujua kwamba, ni kwa juhudi na maarifa yako pekee, utaweza kujinasua kutoka kwenye ujinga, umaskini na vikwazo vingine vya kimaisha.

Ni vigumu sana kung’oa au hata kukwangua ukoko ulio vichwani mwa watu wengi, kwamba yapo mafanikio bila ya njia za mkato na pia zipo njia zinazoweza kuwatajirisha kuliko wanavyofikiri sasa. Ni vigumu kwa sababu ukoko huo sio wa jana au juzi, bali ni wa miaka mingi sana vichwani mwao, ambao unawakwamisha na wakati mwingine huweza kujiona kama vile wanamikosi kumbe siyo.

Lakini kwa juhudi za pamoja na hasa kutoka kwa wale ambao wanaamini katika nguvu alizonazo binadamu katika kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini, hilo linawezekana. Wenye ufahamu huu wanapaswa kujua kwamba, wakimsaidia mtu mmoja kujua hilo hasa, yapo mafanikio bila njia za mkato, watakuwa wamesaidia lundo la watu kujua ukweli huu ambao utaleta mafanikio kwa jamii.

Ili kufanikisha hilo, bila shaka utahitaji mambo ambayo yatakufundisha kitu kipya kuhusu maisha yako ya kipato, misukosuko ya maisha, imani na mikabala mingine mingi ya kimaisha ambayo itakupa nguvu ya kujiamini na kujua kuwa hata wewe unaweza kufanikiwa bila kutumia mkato wala kubahatisha. Ni wazi unahitaji kuyajua haya yote kwa uchambuzi wa kina, kutoka kwenye watu wenye ufahamu usio na shaka ndani.

Unatakiwa ukisoma jambo likujenge siku hadi siku na sio likubomoe, hivyo, unahitaji vilivyo bora zaidi. Sasa una nafasi ya kufanya hivyo kwa kuboresha maisha yako na wengine ikiwa tu kila siku utatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza. Mtandao huu upo kwa ajili yako, na washirikishe wengine kujifunza Mambo mazuri yanayoendelea.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.