Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, September 2, 2015

Siri Kubwa Ya Kufanya Mabadiliko Kwa Kitu Chochote.

No comments :
Kwa muda sasa, nimekuwa nikijifunza mambo mengi yanayohusiana hasa na mabadiliko ya tabia anayoweza kufanya binadamu hadi kufikia mafanikio makubwa. Kutokana na umuhimu wa hili pia nimekuwa nikiwafundisha wengine kuweza kumudu kubadili tabia zao mbaya zinazoweza kuwazuia kufikia mafanikio makubwa na kujijengea tabia bora za mafanikio katika maisha yao.
Pamoja na harakati zote hizo nzuri, lakini ugumu umekuwa ukijitokeza kwa wengi kushindwa kubadili tabia zile mbaya hasa zinazowasumbua kila siku. Tabia hizi mbaya ninazozizungumzia zinaweza zikawa matumizi mabaya ya pesa, ulevi, uasherati, uvivu, kutokujiwekea akiba, malengo na nyinginezo nyingi ambazo kwa vyovyote vile ni kikwazo kikubwa katika kufikia mafanikio makubwa.
Hata hivyo kutokana na kujifunza nilikuja kubaini kwamba tabia zote hizo mbaya kila mmoja wetu anauwezo wa kuzitawala.  Inaweza ikawa ngumu kidogo kueleweka kwako lakini uwezo huu wa kuzitawala unakuja kwako,  ikiwa tu utatambua siri kubwa iliyofichika katika mabadiliko yoyote unayohitaji katika maisha yako. Kwa kujua siri hii utaweza kubadili chochote unachokitaka katika maisha yako.
Kumbuka kila kitu duniani kina uwezo wa kubadilika. Kama mabadiliko yalikuwepo na yataendelea kuwepo. Amini maisha yako pia yanauwezo wa kubadilika na kuwa mazuri, hata kama kwa sasa upo kwenye hali ngumu kiasi gani. Kitu pengine ambacho unajiuliza utawazaje kuzitawala tabia zako zinazokutesa na kukusumbua kwa sasa?

Hiyo ni rahisi sana. Utaweza kumudu kubadili tabia zako ikiwa tu wewe utakuwa makini na tabia ile inayokusumbua. Kama unasumbuliwa na matumizi mabovu ya pesa kitu cha kufanya hapo ni kuwa makini na matumizi hayo unayoyafanya. Hapa ni lazima ujenge utaratibu wa kila shilingi unayoitumia kuiwekea kumbukumbu au kuandikia mahali.
Kama una tatatizo kubwa la kutokujiwekea malengo na kuyatimiza, hapa pia ni lazima uwajibike kuhakikisha malengo yako yanatimia kwa gharama yoyote ile. Malengo yako yataweza kutimia kwa kuyafatilia kila siku hatua kwa hatua. Kitendo cha wewe kufuatilia malengo yako hatua kwa hatua mpaka kutimia hiyo yote inaonyesha ni kwa jinsi gani uko makini na kile unachokifanya.
Kwa hiyo mpaka hapo unaona kuwa siri kubwa ya kufanya mabadiliko yoyote katika maisha yako ipo kwenye kuwa makini na kile kitu unachotaka kukibadili. Wengi wanashindwa kufikia malengo yao na kutofanikiwa kutokana na kutokuwa makini katika hili. Kwa tafsiri nyingine unapokuwa makini inamaanisha nguvu zote za uzingativu unakuwa unazielekeza hapo.
Unaweza ukaanza sasa kubadili maisha yako  na kuwa na maisha ya tofauti kwa kuwa makini kwa yale mambo ambayo hutaki yawe katika maisha yako. Hii itakusaidia kumudu kufikia ndoto zako ulizojiwekea. Bila shaka unajua ama umeshawahi kusikiwa kwamba watu wote makini mara nyingi kufanikiwa kwao ni rahisi. Na huo ndio ukweli.
Kwa kadri utakavyozidi kuongeza umakini kwa jambo ambalo hulitaki liwe sehemu ya maisha yako ndivyo utakavyojikuta unamudu kulitawala kwa sehemu kubwa tabia zako na hatimaye kufanikiwa. Hii ni siri muhimu kuijua na inanguvu ya kubadilisha maisha yako na chochote kile kinachokusumbua.
Tunakutakia safari njema katika kufikia mafanikio makubwa.
Kwa elimu na maarifa bora ya kuboresha maisha yako, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,No comments :

Post a Comment