google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 27, 2015

Sababu Sita Zinazokufanya Ushindwe Kufikia Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako unaweza ukajikuta unafanya kila kitu cha kukusaidia kukufanikisha, lakini ukawa unashangaa mambo yako hayaendi vizuri kama unavyofikiri au kutarajia . Mara nyingi hiki huwa ni kitu cha kuumiza ubongo na inabidi wewe mwenyewe binafsi utulie ili kujua nini chanzo au sababu hasa inayopelekea wewe ushindwe kufikia mafanikio unayoyata katika maisha yako.  Kiuhalisia, huo zipo sababu zinazopelekea ushindwe kufikia mafanikio makubwa, ingawa kwa wengi huwa sio rahisi kuweza kuzijua na kuzitambua kwa haraka. Kama unataka kufanikiwa, hakikisha unazijua sababu hizi zinazokuzuia wewe kufanikiwa.

1.Unatumia muda wako vibaya.
Mara nyingi umekuwa ukiishi maisha ya kupoteza muda wako hovyo. Haya ndiyo maisha ambayo umekuwa ukiishi kwa muda mrefu na umekuwa ukiiona ni kitu cha kawaida tu, kupoteza muda wako bila sababu. Kitu usichokijua ni kuwa muda ni kitu muhimu sana katika kutimiza malengo yako uliyojiwekea. Hakuna mipango wala malengo yoyote hapa duniani, ambayo utaweza kuyatimiza kama utakuwa ni mtu wa kupoteza muda kila mara katika maisha yako.

Ukijaribu kuchunguza kwa makini, utagundua kuwa watu wengi wasio na mafanikio hapa duniani ni wale ambao pia matumizi yao ya muda ni mabovu. Hawa ni watu ambao wanauwezo wakishinda wakipiga soga kutwa nzima wakiongea hili mara lile hata kwa yale yasiyo na maana, ni watu ambao wanauwezo wa kushinda kwenye mitandao ya kijamii karibu kutwa nzima na ni watu pia ambao usishangae ukakutana nao kila mahali wao wapo tu. Kama unaishi maisha haya ya kuchezea muda hivi, nakupa pole, uwe na uhakika utakufa maskini na ndio kitu ambacho kinakufanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa.


2.Umekuwa ukiahirisha sana mipango na malengo yako.
Jaribu kujiuliza mwenyewe ni mara ngapi umekuwa ukisema nitafanya hik na hiki kesho na inapofika kesho hufanyi tena na imekuwa kwako sasa kama ni kawaida  na umezoea. Kama utakuwa wewe ni mtu wa kuahirisha mipango na malengo yako uliyojiwekea kaika maisha yako itakuwa ngumu sana kutimiza hayo malengo yako. Kwa sababu hiyo kesho unayoisubiri na kusema kuwa utafanya haitafika.

Kitakachobaki kwako ni kila siku itakuwa kesho kesho na utajikuta ndivyo unavyozidi kupoteza muda wako na fursa muhimu za kukupatia mafanikio katika maisha yako. Kama kweli umemua kufanya mambo yako yafanye sasa hata kama ni kwa kidogo wewe fanya tu. Achana na habari ya kesho, ambayo unaingoja kila mara, hiyo haitafika milele. Kama unataka kubadili maisha yako na kuwa ya mafanikio makubwa, acha kuahirisha mambo yako.

3.Umekuwa ukiishi maisha ya visingizio sana.
Hii ni sababu kubwa sana inayokufanya ushindwe kusonga mbele katika maisha yako kutokana na visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo. Umekuwa ukitoa visingizio mara kwa mara kila kukicha kwa nini hufanikiwi. Hebu angalia ni mara ngapi umekuwaukisema huwezi kuanzisha biashara kwa sababu huna mtaji, ni mara ngapi umekuwa ukisema unashindwa kutoka kwenye umaskini kwa sababu una wategemezi wengi na hujiwezi. Umekuwa una visingizio hivyo ambavyo vyote ni kama unajitetea tu.

Lakini, sababu kubwa inayokufanya ushindwe kufanikiwa katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Unao uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yako ukitaka na hakuna kitu cha kukuzuia. Kama ukiamua leo hii, ukaachana na visingizio vingi ambavyo umekuwa navyo, elewa kabisa utabadili maisha yako kwa asehemu kubwa sana na utaanza kuishi maisha unayoyataka. Visingizio visiwe sababu yaw wewe kuzuia kufikia mafanikio yako, jifunze kuwajibika na chukua hatua juu ya maisha yako.

4.Umekuwa ukikata tamaa sana mapema.
Haijalishi umeshindwa au umekosea mara ngapi kwa kile unachokifanya, kitu ambacho hutakiwi kufanya katika maisha yako ni kukata tamaa. Unapokuwa unakata tamaa unakuwa una utangazia ulimwengu kuwa mafanikio kwako basi tena. Kukata tamaa ni sababu ya kwanza ambayo inapelekea wewe ushindwe kwa kila kitu unachofanya katika maisha yako. Kama umeshindwa jambo na unafikiria kuwa upo mwisho wa safari na huna sehemu nyingine ya kwenda, tambua unajidanganya nafsi yako.

Umejifunga jela mwenyewe na mawazo yako ya kujikatisha tamaa. Kwa kufikiria hivyo ni kujitengenezea nafasi ndogo ya kufanikiwa katika unalolifanya,na nafsi yako itaanza kuamini wewe ni mtu wa kushindwa. Tunaishi katika ulimwengu wenye njia nyingi za kufanikiwa katika yale tunayojishughulisha nayo. Kumbuka pia wakati mwingine ni lazima kushindwa mara nyingi ili ufanikiwe. Na ndio maana unaposhindwa mara moja sio mwisho wa kila kitu. Wazo lako lolote ambalo limeshindwa kazi,linafungua njia ya wazo litakaloshinda.


5. Umekuwa ukiishi maisha ya kuwa na mitazamo hasi sana.
Wewe ni matokeo ya kile unachokifikiri na kukiamini katika maisha yako. Kama unaamini utafanikiwa ni kweli utafanikiwa na kama uaamini maisha yako ni kushindwa ni ukweli usiopingika lazima ushindwe . Ni mara nyingi umekuwa ukishindwa kufanikiwa na kufikia malengo yako makuu kutokana na fikra hasi ambazo umekuwa ukizibeba sana kila siku. Mara ngapi umekuwa ukiamini ya kuwa mafanikio wamejaliwa wengine na wewe ukijitoa kabisa? Kama unataka kubadii historia ya maisha yako, jifunze kuyaangalia mambo kwa mtazamo chanya zaidi, utafanikiwa.

6. Umekuwa mwongeleaji sana juu ya ndoto zako.
Ili uweze kufanikiwa na kufikia malengo yako ni muhimu sana kwako wewe kuwa mtu wa kuchukua hatua kwa vitendo mapema sana. Kama utakuwa wewe ni wa kuongea na hauchukui hatua yoyote dhidi ya ndoto zako itachukua muda sana ama haitawezekana kabisa kufikia malengo yako. Watu wengi wamejikuta wakiwa ni waongeleaji sana juu ya ndoto zao. Kuongelea sana juu ya ndoto na mipango mizuri uliyonayo hakutakusaidia kitu na ndicho kitu ambacho kimekuwa kikikuzuia ushindwe kufikia malengo yako makubwa uliyojiwekea mara kwa mara.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio makubwa na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,




No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.