google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 28, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kumudu Kuishi Katikati Ya Tufani Za Kimaisha.

No comments :
Ukijaribu kutafakari jinsi binadamu anavyokumbana na matatizo magumu ya aina mbalimbali ya kimaisha, huenda unaweza ukahisi hali fulani ya kukata tamaa na hata kujiuliza kwamba, ni kwa jinsi gani binadamu huyu anaweza kukabiliana na hata kujikwamua kutoka kwenye hali hizo zinazokatisha tamaa. Hebu jaribu kukumbuka matatizo ya kiuchumi, ugaidi, magonjwa mabaya ya kuambukiza, vita na migogoro mbalimbali ya kijamii, majanga ya asili na mengineyo.

Yote hayo kwa muda mrefu yamekuwa ndiyo changamoto kubwa kwa binadamu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, bado kuna uwezekano mkubwa kwa binadamu huyu kuendelea kustawi na kushamiri kimaisha pamoja na kuzungukwa na matatizo hayo. Mambo yafuatayo yanaweza kumsaidia mtu katika harakati zake za kuyaboresha na kuyaendeleza maisha yake katikati ya changamoto hizo.

1. Jifunze kuangalia mambo kwa mtazamo chanya.
Litazame kila jambo linalokujia au kukupata kwa jicho lenye mtazamo mzuri na chanya. Katika suala hili inapaswa kukumbuka  kwamba , kunapotokea hali fulani itakayosababisha watu kusongeka, ujue kwamba, siyo lazima kila mtu asongeke na kwamba kunapotokea maradhi mabaya ya kutisha na yanayosababisha vifo, siyo lazima kila mtu afe. Huu ndio ukweli wenyewe, na bila shaka huwa tunahuzunika na kujisikia vibaya, pale tunapoona wenzetu wanateseka. Lakini hata hivyo, mateso yasiyo ya lazima yanatokana na hofu wasiwasi wetu hayana faida kwetu zaidi ya kutuumiza na kutuacha tukiwa wagonjwa hoi vitandani mwetu.



2. Fanya yale unayoweza kuyatimiza, usiyoyaweza achana nayo.
Wakati wote unapaswa kujiandaa kama vile askari wanavyofanya. Ujifunze kuzitupilia mbali hofu zako. Kwa kufanya hivyo utajiongezea uwezo wako wa kustarehe na kuburudika na maisha yako. Kwa kawaida, hofu iliyofika katika kiwango kikubwa na cha kudumu ni nguvu za kukuondolea uwezo wako wa kukabiliana na kupambana na hali ngumu zozote zile zinazokujia. Hivyo, kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya hali hizo za kutisha na kukatisha tamaa, ni jambo muhimu na linalopaswa kuzingatiwa kwa makini ili tuweze kuishi maisha yasiyotuelemea.

3. Yasawazishe maisha yako.
Fanya kila uwezalo, ili uweze kuyasawazisha maisha yako kwa kufanya kazi zako za kila siku kwa bidii, maarifa na kwa kufuata utaratibu uliojiwekea. Pia unapaswa kujiwekea muda kwa ajili ya kufanya mambo yanayokuhusu wewe binafsi, familia yako, hata jamii yako kwa ujumla. Ukiwa unafanya hivi mara kwa mara utakuwa unajijengea uwezo mkubwa wa kupambana na kila hali ngumu inayojitokeza katika maisha yako.

4. Tafakari kwa kina, Sali na uwe mwenye shukrani.
Hebu tafakari, Sali au hata ufikirie kidogo kuhusu Baraka za namna mbalimbali unazozipata ambazo zinatokana na wewe kuwa hai. Unaweza pia ukatembea tembea kwenye maeneo yenye kuvutia na kujiburudisha, kama vile bustanini, kwenye ufukwe wa bahari, na mbali kwingine kotekote unakohisi kwamba, kuna mandhari ya asili. Kutafakari kwa kina ni njia ambayo imethibitika kuwa na nguvu ya kupunguza sononi, na vilevile kuzingatia kwa makini masuala ya kiroho huongeza kwa kiwango kikubwa ile hali ya kuwajali, kuwathamini na kuwahurumia watu wengine.

Ukweli ni kwamba jawabu kwa kila tatizo lipo, hata katikati ya matatizo na vurugu nyingi, bado unaweza kulipata. Hivyo unapoamua kuutumia ushauri huo hapo juu, unaweza kujiongezea amani yako ya akili na kuridhika na maisha yako, mambo ambayo ni muhimukutumika kwenye maandalizi yako ya kupambana na changamoto mbalimbali za kimaisha. Kumbuka tu kwamba, walioweza kuokoka wakati wa mauaji ya halaiki kwenye kambi dhalili za mauaji za Hitler, wengi ni wale waliokuwa na matumaini, wale ambao walikuwa wakijiambia kila wakati kwamba, kila penye vurugu, pana suluhu.

Nakutakia mafanikio makubwa na endelea kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.