google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jan 30, 2015

Kama Unataka Kuwa Mtaalamu Katika Shughuli Unayofanya? Soma Hapa.

No comments :
Si kila anayefanya shughuli fulani huwa na utaalamu nayo, wengine wanaifanya kwa kuwa tu nafasi ilitokea  ya kuifanya. Na hautachukua muda kumgundua mtu anayefanya kazi zake kwa utaalamu, na yule anayebangaiza njaa tu, kwa jinsi wanavyoenenda na tabia zao. Mara nyingi
waajiri na wateja hulalamika kuwa anayewafanyia kazi  hana utaalamu.

Yawezekana humalizi kazi vizuri, umemcheleweshea au hata kumzungusha kwa muda mrefu bila taarifa sahihi. Si mara moja tunasikia 
ni jinsi gani tunatakiwa kuwa wataalamu katika shughuli tunazofanya. Kama unataka kupata mafanikio, kuchukuliwa kama mtu makini, kuonekana una mchango kwa unaofanya nao shuguli zako, kuzifanya kitaalamu ndio njia pekee ya kukufikisha huko.

Lakini tujiulize waajiri ama wateja wanatafsiri gani juu ya utaalamu? Wengi wao watakuona mtaalamu ikiwa wewe: Unafika eneo la kazi katika muda unaotakiwa; Unaifanya kazi uliyopewa vizuri; Unamaliza kazi kwa wakati.
Unadhani kuna matukio mengine ambayo unahisi ukiyafanya yatakuonyesha wewe si mtaalamu? Kuna matukio ukiwa unayafanya yanakutafsiri moja kwa moja kuwa wewe si mtaalamu wa shughuli unayofanya.

Kwa mfano ukiwa:- Unachelewesha kazi za watu, unahudhuria vikao ukiwa haujajiandaa, unatumia muda mwingi kuongea umbea muda wa kazi, kuwavunjia heshima wenzako,  kuwasubirisha wateja muda mrefu bila sababu za msingi, kuiba mawazo ya watu wengine kufanyia shughuli zako bila kuwahusisha, na kuvunja ahadi zako mara kwa mara.

Hebu leo tuangalie njia kumi utakazoweza kutumia kuwa mtaalamu katika shughuli yoyote unayofanya. Jitahidi kufanya shughuli zako kitaalamu na watu waweze kukuamini, kukuheshimu, na kukuona una uwezo wa kipekee. Japo mazingira ya kila kazi yanatofautiana lakini linapokuja suala la utaalamu huwa na tafsiri moja dunia nzima.

Hebu tuangalie sifa za kuwa mtaalamu ni zipi:-

1. Umahiri.
Lazima uwe mahiri katika kile unachofanya, ukitumia ujuzi na maarifa ya kutosha katika kazi yako ni lazima utaonekana mtaalamu na watu. Ni muhimu kwako kujifunza hili ili kuweza kujenga uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa ufanisi ambapo itakupelekea wewe moja kwa moja kuwa mtaalamu katika kile unachokifanya. Na utakuwa mtaalamu kutokana kujifunza kwako mara kwa mara, hivyo ni muhimu kuwa mahiri.


2. Zingatia muda:
Watu watakuwa wanakutegemea wewe ufike katika muda unaotakiwa ili shughuli ziende na umalize kwa wakati. Sio kuendelea kufanya shughuli zako kwa mazoea tu bila kujali muda, kwani hakuna anayependa kumuamini na kumpa kazi mtu asiyemaliza kwa wakati. Kama utaendelea kuwa mtu ambaye sio wa kutunza muda na unajidanganya kuwa eti unataka kuwa mahiri kwa kile unachokifanya sahau katika maisha yako.

3. Uaminifu.
Unatakiwa kuwa muwazi wa shughuli zako, na wale unaofanya ama unaowafanyia kazi nao wajue nini kinachoendelea. Ukianza kujifanya mjanja mjanja, katika shughuli unayofanya huku huwaweki wazi watu wengine hakuna atakayekuona mtaalamu hata kidogo. Matokeo yake utajishushia heshima hasa pale itakapobainika kuwa mambo yako hayaendi sawa kiaminifu zaidi.

4. Uadilifu.
Utaonekana mtaalamu ikiwa utakuwa unasimamia kanuni za shughuli yako. Hakuna anayependa kumpa kazi mtu asiyejua kufuata kanuni za kazi yake. Jifunze kufuata kanuni za kazi yako ili uwe mtaalamu uliyebobea vinginevyo utajikuta unakuwa ni mtu wa kubabaisha katika eneo ulilopo. Zingatia pia misingi ya maadili kati yako na wafanyakazi wenzako hilo ni jambo la msingi.

5. Heshima.
Kama huna heshima kwa watu wengine unaofanya nao au unaowafanyia shughuli basi hautaonekana mtaalamu hata kidogo. Ni muhimu sana kwako kuchunga heshima kwa wafanyakazi wenzako hata kama umewazidi cheo ni lazima uwe na heshima kwao. Kuwa na heshima tambua kuwa hiyo ni nguzo kubwa wewe ya kuweza kukutambulisha kuwa wewe umebobea na ni mtaalamu katika kazi yako na wala si mbabaishaji.

6. Ongeza ujuzi.
Tafuta ujuzi wa ziada, usiendelee kung'ang'ania ujuzi ule ule kila siku. Toka nje ya yale unayoyafahamu ili kupata mengine mapya  kuongezea katika yale unayayafahamu ili kuboresha zaidi utendaji. Kama utaendelea kung’ang’ania kuwa na ujuzi ule ule bila ya wewe kutaka kubadilika na  kujifunza kitu kipya, elewa kabisa utakuwa unajipunguzia sifa za kuwa mtaalamu kwa kile unachokifanya.

7. Mtazamo chanya.
Kama wewe kila siku unaangalia makosa tu bila kuwa na mtazamo chanya juu ya shughuli unayofanya kuwa mtaalamu itakuwa ndoto kwako. Ni lazima uwe na mtazamo chanya ili ujue nini cha kufanya kuliko kuangalia makosa tu kila wakati ambapo hayo makosa yanaweza yakakupunguzia na kasi ya kufanya vitu vingine vitakavyoweza kubadili mwelekeo wako na pengine kukufanya kuwa mtaalamu zaidi.
8. Toa msaada:
Wasaidie wenzako unaofanya nao shughuli sio kwa kuwa wewe unafahamu kitu fulani basi hutaki wenzako wafahamu. Waonyeshe jinsi ya kufanya kazi vizuri pale unapoweza na wasikilize pale wanapokuuliza maswali. Unapowasaidia wenzako ambao unakuwa unafanya nao kazi hii inakufanya kila siku utajikuta unaongeza utaalamu wako katika maisha yako.

9. Tenganisha matukio.
Usihusishe matukio ya nyumbani au mtaani na kazi, ukiwa katika shughuli zako weka mawazo yako yote hapo. Utakuwa mtu wa ajabu kufika eneo la kazi na kuanza kushughulikia masuala ya nyumbani huku ukiacha kazi haziendi. Jifunze kufanya kazi  kwa uangalifu ili usije ukajikuta unaupoteza muda wako mwingi pasipo kujijua hiyo inaweza ikawa ni hatari sana na itapunguza utaalamu wako.

10. Kuwa msikivu.
Kila mtu ana hitaji la kusikilizwa pale anapokuwa na jambo la kusema,
Kwa hiyo wape watu nafasi ya kukuelezea yale wanayodhani yatasaidia katika utendaji wa kazi. Acha kuwa king’ang’azi wa kutaka mipango yako au mambo yako ndiyo yatekelezwe na kusahau usikivu unaotakiwa kuwa nao hata wewe ili kuleta ushirikiano utakaoleta ufanisi hata kwako na kukufanya kuwa mtaalamu zaidi.

Kila mmoja wetu anapenda kupata mafanikio katika shuguhuli ile anayofanya, basi tuanze sasa kufanya kazi kitaalamu ili tuweze kufikia yale tunayoyataka. Nakutakia mafanikio mema, karibu DIRA YA MAFANIKIO uendelee kujifunza na kuhamasika kila siku.

IMANI NGWANGWALU,







No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.