Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, April 2, 2015

Hivi Ndivyo Nguvu Ya Mawazo Yako Inavyoweza kukuepusha Na Matatizo.

No comments :
Umewahi kupata  hisia ama mawazo fulani kuhusu jambo fulani, lakini usijue hisia hizo zina maana gani na wala zinatokana na nini? Basi hisia hizo ndiyo hasa nguvu ya ufahamu wako au ‘intuition’, kama wataalamu wanavyoita. Nguvu za ufahamu ni nini? Fikiria ufahamu kama mshauri wako aliye karibu nawe akitaka kukusaidia na kukuongoza katika kila jambo.
 
Tatizo kubwa la mshirika wako huyu ni kwamba huwa hazungumzi lugha uliyoizoea wewe. Hii ni kwamba si wakati wote mshirika huyu hutoa kauli na kutoa maelekezo katika lugha uliyoizoea kuisikia na kuielewa kirahisi. Ili kuweza kukuza nguvu za ufahamu wako, unawajibika kuielewa lugha yake na huu ndio mtihani mkubwa katika hilo.

Unaweza vipi kujua namna ufahamu ufanyavyo kazi, au jinsi ya kuilewa lugha yake? Ufahamu unatumia ujumbe katika miundo tofauti wakati wote, kila siku. Wakati mwingine ufahamu huenda ukawa ni hisia hiyo niliyoilezea hapo mwanzo, yaani wakati unajua jambo fulani, lakini huna njia ya kufafanua kile unachofahamu.

Kwa mfano, unaweza ukawa uko barabarani unaendesha gari, na mara gari lingine likakupita kwa kasi. Gari hilo baadaye linapunguza mwendo na kuonekana kukuziba usiendelee vema na safari yako. Unaamua kulipita, lakini unasita ghafla na kuamua kuliacha liendelee kuwa mbele yako, ingawa unaliona kama linakuchelewesha na safari yako uliyonayo.Muda mfupi baadaye, unalishuhudia gari hilo lililo mbele yako, likigonga gari lilolo mbele yake kwa kushindwa kusimama wakati lilipolikaribia. Unawaza akilini kwamba , kama ungeamua kulipita gari lile, bila shaka wewe ndiye ungekuwa umegongwa saa hizi. Hii yote inadhihirisha uwezo au nguvu kubwa ya ufahamu jinsi inavyoweza kufanya kazi kwako.


Mfano mwingine, tuchukulie unatembea kandokando ya barabara ukiwa unazungumza na mtu. Mazungumzo yenu yanakuwa ni ya wewe kuomba kitu Fulani kwake na kusisitiza. Ghafla mtu unayezungumza naye anabadilika na kuonekana kukasirika. Anaamua kukuacha na kuongeza mwendo.

Ukiwa katika hali ya kushangaa kwanini amekuacha kuna wazo linakujia kuwa umfuate ili uendelee kuzungumza naye, lakini ghafla wazo linakujia usifanye hivyo bila kukupa sababu, ni kwa nini usifanye hivyo. Mita chache baadaye, gari linalokuja kwa kasi linaacha njia na kumgonga Yule jamaa yako uliyekuwa ukizungumza naye aliye mbele yako.

Si hivyo tu, kuna wakati unaweza ukajikuta unataka kusafiri. Mipango ya safari unakuwa umeiweka sawa, kinachokuwa kimebakiwa ni wewe tu kuondoka. Lakini, kitu cha kushangaza unaanza kujihisi mzito, unajivuta mpaka lile gari linakuacha. Muda mfupi tokea uachwe na gari lile unakuja kupigiwa simu kuwa gari lile limepata ajali mbaya sana.

Akili mwako sasa unaanza kujiuliza nini kingetokea kama ningepanda lile gari. Bila shaka utaanza kuwaza ni lazima pengine ningekuwa nimepoteza maisha. Lakini ni nini kilichokuokoa basi hadi ukashindwa kupanda lile gari bila kujijua, wewe mwenyewe unashangaa na unashindwa kupata majibu hasa yaliyokamili kwako. 

Pamoja na kuwa unaweza ukawa hujui kitu kinachokuokoa, lakini ni ukweli kwamba kinachokusaidia ama kukuokoa ni nguvu zako za ufahamu ulizonazo. Nguvu hizi za ufahamu kuna wakati zinaweza kuokoa maisha yako ikiwa utasikiliza kile zinachosema. Watu wengi wamewahi kuokolewa na nguvu za ufahamu wao bila kujijua.

Kuna wakati katika maisha yako kabla ya jambo baya halijaweza kukutokea, nywele za nyuma ya kichwa huwa kama unahisi zinasimama. Hii yote ufahamu wako huwa unataka kukuonyesha kuwa mbele kuna hatari.  Ikiwa unataka kuvuka barabara kwa mfano, basi ujue zinakuonya usivuke, kama unataka kwenda mahali basi ujue zinakuonya usifanye hivyo.

Nguvu hizi za ufahamu pia  huweza kukuokoa pale ulipotaka kwenda mahali na kusita ghafla, halafu huko ambako ungeenda kukatokea ajali ama mtu kupoteza maisha. Hivyo, huwezi kulijua hilo kwa sababu hukwenda huko, lakini kikubwa kinachokuwa kimekuokoa ni uwezo wa nguvu zako hizi. Ni nguvu hizi za ufahamu ambazo hufanya kazi kwa njia ambayo ni ya kushangaza kidogo. 

Ufahamu huu huja kwa sura tofauti. Fikiria ufahamu kama mshirika wako, kuna wakati mshirika huyu atazungumza na wewe kwa hisia tu, kuna wakati atazungumza kwa maneno kupitia mtu mwingine, kuna wakati atakupa ishara, kuna wakati atajaribu kukuzuia kufanya jambo fulani ambalo sio zuri kwako. Uko umuhimu wa kujua namna anavyoweza kuzungumza na wewe.

Kwa mfano, kama nguvu hizi za hisia zitazungumza nawe kupitia hisia, zinaweza kuwa hisia nzito  zinazokutaka ufanye kitu fulani ama uache kitu na kufanya kile kwa nguvu zako zote.

Kuna wakati nguvu za ufahamu zaweza kuzungumza nawe kupitia mtu mwingine. Kwa mfano, unaweza kuwa unafikiria kununua nyumba mpya, lakini huna uhakika ununue eneo gani. Mtu wa kwanza unayezungumza naye anakutajia eneo fulani.
 
Mtu wa pili unayejaribu kuzungumza naye anakutajia eneo hilohilo, wa tatu naye anakutajia eneo hilohilo. Unatazama kwenye gazeti na kukuta makala inayolisifia eneo hilo ambalo marafiki zako walikutajia kuwa ni eneo bora na linalokufaa kwa kuishi. Hadi hapa, ni wazi nguvu za ufahamu wako zitakusaidia kulifikiria eneo hilo na huenda sasa ukaamua kwenda kuliona.

Kuna wakati nguvu za ufahamu wako zitakuongoza kwa kukupa ishara. Zitakuongoza kwa kukupa ishara kwa kuona kitu kinachofanana na kile unachokitafuta. Kwa kuona kitu ambacho kipo sawa na kile unachokitafutia jibu hiyo moja kwa moja ni ishara tosha kwako.

Kuna wakati nguvu za ufahamu wako zitajaribu kukuzuia kuchukua hatua fulani. Huenda unataka kununua nyumba kwenye eneo fulani, lakini unagundua kwamba si ya hadhi unayotaka ama ni ya bei ya juu sana. Hii ni ishara ya kutaka utafute eneo jingine, ama kuwa na subira mpaka utakapopata nyumba kwenye eneo sahihi, ama kufikiria eneo lingine.

Huenda unataka kazi mahali fulani, lakini unakuta hakuna mwelekeo hata wa namna ya kuifatilia kazi hiyo ama wapi pa kuanzia. Hapa huenda nguvu za ufahamu zinakuelekeza utafute kwingine na kutokuendelea kuifatilia kazi hiyo tena uliyoelekeza mawazo yako. Katika matukio yote, ujumbe sio utakuwa wazi kama unavyotaka uwe.

Namna nguvu za ufahamu zinavyozungumza nasi, si siku zote unaeleweka kiurahisi. Lakini ikiwa utaendelea kuupima na kuendelea kutafuta jibu, jibu litakuwa wazi. Hisia zitakuwa nzito. Ishara zitaendelea kurudiwa na kuwa wazi. Ujumbe kutoka kwa watu wengine utarudiwa tena na tena na hatimaye ujumbe utakuwa wazi.

Kuna wakati huenda usielewe ujumbe mpaka miaka kadhaa baadaye. Lakini kuna siku utaonesha maana itakayoonekana katika wakati mwafaka utakapotimia. Kwa kifupi hivyo ndivyo, nguvu ya ufahamu inavyofanya kazi kwako na kukuongoza katika mambo mengi ambayo kuna wakati hata wewe hujui.

Nakutakia mafanikio mema katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

IMANI NGWANGWALU,

No comments :

Post a Comment