google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Apr 1, 2015

Hawa Ndio Watu 5 Hatari Wanaoweza kuharibu Maisha Yako.

No comments :
Ni ukweli na imedhibitishwa katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya malezi na dini zetu, kwamba huwa tunaambukizwa tabia nzuri au mbaya na wale watu ambao kwa muda mrefu tuko nao na tunawaamini kwa kiasi fulani. Watu hao wanaweza kuwa wazazi, marafiki, wafanyakazi wenzetu, wanafunzi wenzetu, jirani zetu na wengine.
 
Nimeona siyo vibaya kwa hali hiyo, kukushauri kwamba, unapaswa kuwa makini sana na watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa hata kama tunawapenda vipi.  Hili si jambo la mzaha kama unavyoweza kulitazama kijuu-juu. Ni jambo la dhati. Kwa haraka haraka naomba nikutajie watu hawa, wanaoweza kuharibu maisha yako.

1. Watu wanaofikiri, kusema na kutenda hasi.
Hawa ni watu ambao siku zote huwa hawaoni suluhu ya jambo, bali kuona matatizo tu. Ni watu ambao huzingatia zaidi mambo yasiyopendeza na siyo yale yanayopendeza. Mtu anaweza kufanikiwa kupata zabuni ya shilingi milioni 20 na kukosa ile ya milioni 100. Badala ya kushukuru na kuangalia ile zabuni aliyoipata, atazingatia na kuumizwa kichwa na kile alichokikosa. 

Hawa huwa ni watu ambao hata wakifanikiwa kivipi kimapato,bado maisha yao yanakuwa yamezingwa na hofu zisizoisha, kutoridhika na kutamani tena na tena bila ukomo. Kwao kushindwa kupata wakitakacho, bila kujali ni kitu gani, ndilo jambo linalopewa uzito badala ya kile walichokipata.

Lakini kwa bahati mbaya, watu wa aina hii huwa ni vigumu pia kufanikiwa kimapato katika Nyanja waitakayo. Ni kwa sababu, kwao matatizo madogo kuyaongeza chumvi nyingi na kuonekana kuwa makubwa sana. Kwao kushindwa jambo wanakutazama kama msiba mkubwa ajabu. Hukata tamaa haraka kwenye matatizo na hivyo hawapati nafasi ya kujifunza kupitia katika matatizo yao.

Ukiwa karibu na watu wa namna hii, ni wazi utadhani maisha ni tahadhari na mashindano ambayo mshindwa hapaswi kuishi. Lakini hata kama nawe uko hivyo, inabidi ujue kwamba, una safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio kama kweli unayataka. Watu wa aina hii wana nguvu hasi za kuweza kuambukiza maradhi yao kirahisi kwa wengine.

  
2. Watu ambao ni wafujaji wa mali.
Bila shaka umewahi kusikia watu wakisema ‘ponda mali kufa kwaja’. Sina uhakika watu wanaoamini katika usemi huu wana maana gani? Inawezekana ukawa na ukweli kama mtu anaamini kwamba yeye ni huo mwili wake na maisha yake huisha pale mwili wake unapoachana na mawazo au roho yake. Lakini hata kama mtu anaamini hivyo, bado kuna swali la msingi kwamba, maisha ni yeye peke yake?

Kuna wengine wanaoamini hivyo ambao wamesomeshwa kwa fedha za mifuko ambayo waanzilishi wake walishakufa zamani. Ni watu waliohangaika kutafuta, wakapata na kuweka ili wateja waje wawasaidie wengine. Sasa unashindwa kujua inakuaje mtu huyu anayeamini katika kuponda mali kufa kwaja asijiulize mchango wake kwa wengine ambao atawaachia nyuma. 

Hatukuletwa duniani ili kula na kuvaa vizuri na kufanya mapenzi sana, halafu tufe. Tuliletwa kwa kusudi maalumu na kusudi hilo kwa sehemu kubwa ni mchango wetu kwetu na kwa wengine hapa duniani. Elewa tu, unapaswa kuwaepuka watu ambao hawaamini kwamba wanapaswa kuweka akiba ili kufanya mambo ambayo yatawasaidia wengine baadaye. Wengine wao wanaweza kuwa ni familia zao, ndugu au jamaa zao, ama jamii nzima kwa ujumla. Bila shaka huko ndiko kufanikiwa kwa juu kabisa, tunapokuzungumzia kufanikiwa kwa upana wake.

3. Watu wasiojua cha kufanya baadaye.
Kuna watu ambao ukweli ni kwamba hawajui cha kufanya muda ujao. Watu hawa hula chakula tu, kunywa pombe tu, kucheza bao au karata tu, lakini wafanye jambo gani la kuwasaidia wao au wengine inawawia vigumu. Ni afadhali mtu ambaye hana malengo lakini kuna jambo au mambo anafanya, hawa hawana wanachofanya kabisa.

Kazi yao ni kutafuta mtu wa kumlaumu kwa kushindwa kwao kuwajibika. Hata wakipewa shughuli, watashindwa na kurejea kwenye kuishi kama mawe au kuku wa kufugwa bandani. Wanajua sana watu hawa kusingizia serikali au viongozi wa nchi. ‘wanaiba sana, ndiyo maana wengine hatuna cha kufanya’. Ni hodari sana kulaumu ndugu, ama jamaa zao. 

Hawa ni watu ambao kwa kawaida ukiwaendekeza wanakufikisha mahali ambapo unaweza kuamini kwamba maisha yana kasoro na wanaweza kukufanya uamini kwamba hata wewe hutendi mema kufanya shughuli na kuingiza kipato kingi. Dawa ni kuwakwepa kwa mbali na wala usikubali ‘kuwafuga’, watakuharibia sana maisha yako. 

4. Watu wanaoharibu majina ya wengine.
Siyo rahisi kwa mtu kufanikiwa kama ana kijicho, dhidi ya watu waliofanikiwa. Kuna watu ambao ni maadui wa watu wote wanaofanya vizuri. Hutumia kila wanaloweza kuwaharibu ama kuwazuia ili wasiende mbali. Wanaweza kukuza majungu au sifa mbaya kwa watu ambao wanaonyesha kuelekea kwenye mafanikio au hata kufanya njama tu ili waanguke. Badala ya kuwa karibu na hao wanaoelekea kwenye mafanikio ili wajifunze kitu, hutaka kuwaona wameanguka, hivyo muda wao mwingi huupoteza katika kutafuta na kumharibia yule au huyu na sio katika kutafuta mafanikio.

Kufuatana au kuwa karibu na watu hawa ni sawa na kutaka kuambukizwa bure nguvu hizi hasi ambazo zinadhuru sana bila mhusika kujua. Kwa nini tusijaribu kuiga na kujifunza kupitia mafanikio ya wengine katika kutafuta mafanikio yetu, badala ya kuwachukia? Kwa nini tusiamini kwamba wengine wakifanikiwa, nasi bila kujua tumefanikiwa pia? Kama kweli tunataka mafanikio ni lazima tuwaepuke watu hawa wenye kijicho na chuki.

5. Watu wasipenda shida wala usumbufu.
Hawa huwa ni watu ambao idadi yao inazidi kuwa kubwa kila kuchao. Ni watu ambao mara nyingi wakishasoma basi kila kitu huishia hapo na hutamani ama hupenda zaidi kila kitu kiletwe miguuni mwao. Ni watu ambao hawana juhudi wala ubunifu kwa kile wanachokifanya katika maisha yao. Watu hawa huwa ni watu wa jua kucha, jua kuzama siyo zaidi ya hapo. Matokeo yake ni kupata shida katika maisha. Pia hawa ni watu hatari sana kwako unaotakiwa kuwaepuka sana.

Hao ndio watu hatari ambao usipokuwa nao makini wanaweza kuharibu maisha yako kwa sehemu kubwa sana. 

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila siku.

IMANI NGWANGWALU,


.

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.