Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, April 14, 2016

Maadui Wakubwa Wa Mafanikio Walio Ndani Yako.

No comments :
Wengi kulingana na uzoefu tumezoea kuona maadui wengi wa mafanikio yetu walio nje yetu. Mara nyingi tunakuwa hatuko tayari kukubali kuwa rafiki na mtu ambaye kwa namna moja au nyingine tumetambua ya kwamba yeye ni kikwazo au adui wa mafanikio yetu, naamini hili unalijua vizuri. Kwa hilo huwa tupo tayari kumweka kando mtu huyo kwa sababu ni  chanzo cha kutufanya tushindwe kufanikiwa.
Hata hivyo pamoja na kuwa makini na wale tunaomini ndio maadui wa mafanikio yetu, tumekuwa tukisahau kwamba wapo baadhi  ya maadui wakubwa wa mafanikio ambao wako ndani yetu. Kwa bahati mbaya sana maadui hawa tumekuwa hatupo makini nao sana lakini ndio wamekuwa wakituzuia kufanikiwa kuliko hata wale maadui wa nje tunaowajua. Je, unajua hawa ni maadui wapi ulionao na wanakufaya ushindwe kufanikiwa?
1. Woga.
Kati ya kitu ambacho kinamsumbua sana binadamu ni pamoja na woga. Binadamu kwa kawaida kimaumbile ni mtu wa kuogopa mambo mengi sana ikiwemo hata woga wa mafanikio yake. Woga huu mara nyingi hupatikana kutokana na kujifunza, uzoefu au kusikia lakini ukija kuungalia hata kile kinachoogopwa kinakuwa sio halisi ama kwa lugha nyingine tunaweza kusema hakipo.
Inapofika mahali ukawa una woga mkubwa ndani yako suala la kufanikiwa katika maisha linakuwa ni gumu. Hiyo yote inakuwa ni kwa sababu hakuna hatua ambayo utaweza kuichukua zaidi ya wewe kuogopa na kujihisi hutaweza. Kwa hiyo kama unaendekeza woga, tambua huyo ni adui mkubwa sana aliye ndani yako ambaye anakuzuia kufanikiwa. Waangalie watu wengi waoga maisha yao huwa ni ya kushindwa sana karibu siku zote.

Toa woga, utatengeneza mafanikio makubwa.
2. Wasiwasi.
Tukiachana na suala la woga pia adui mwingine ambaye binadamu anambeba ndani yake ni wasiwasi. Watu wengi wanakuwa ni watu wa kutilia wasiwasi au mashaka kwa mambo wanayoyafanya au wanayotaka kuyafanya. Utakuta mtu anataka kufanya kitu fulani lakini ndani yake kunakuwa kuna maswali mengi sana ndani yake anayojiuliza kama ‘hivi kweli hapa nitafanikiwa’ na je ikitokea nimeshindwa itakuwaje?’.
Kwa wasiwasi huu mwingi ambao wengi wanakuwa nao unakuwa unawafanya kushindwa kufanikiwa. Utakuta kweli mtu huyu amefanikiwa kuushinda woga na kujaribu kuchukua hatua. Lakini, kitendo cha kuthubutu huku ukiwa na wasiwasi mkubwa ndani yako wa ‘sijui nitafanikiwa au nitashindwa, huwafanya kushindwa moja kwa moja. Na hii huwa inatokea kwa sababu ya mawazo ya kina yanakuwa yanaamini kile unachokihofia ndicho unachokitaka mwisho wa siku unajikuta umeshindwa.
 3. Imani potofu.
Maisha yote ya mafanikio yanaongozwa na imani. Unaweza ukawa una mipango na malengo mazuri kabisa ya kukusaidia kufanikiwa, lakini kitu cha kujiuliza je una imani inayokusaidia kufikia mafanikio hayo? bila kuwa na imani sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio ni rahisi kushindwa. Watu wengi wanakuwa wanatafuta mafanikio lakini huku ndani mwao wakiwa na imani hasi, imani potofu ambazo zinawazuia kufanikiwa.
Kwa mfano utakuta mtu anatafuta mafanikio lakini wakati huo huo ndani yake anaamini watu wanaofanikiwa ni wezi, mafisadi au wanyonyaji kwa wengine. Kwa imani kama hizi kufanikiwa inakuwa ni ngumu kwa sababu ndani yako unakuwa na imani potofu inayokuzuia kufanikiwa huko. Ni lazima kujenga mtazamo chanya ambao utakupa mafanikio. Acha kuwaza hasi ama kujenga imani potofu utakwama kufikia mafanikio yako makubwa.
4. Maamuzi mabovu.
Kila mtu katika maisha yake ana maamuzi ya aina fulani ambayo anayatoa kila siku. Kwa maaumuzi hayohayo hupelekea maisha yako kuwa mabaya au mazuri. Kama ndani yako unabeba maamuzi mabaya kila wakati basi elewa una adui mkubwa anayekuzuia kufanikiwa. Kwani kwa kuwa na maamuzi hayo itasababisha maisha yako kuwa mabovu na ya ajabu sana.
Kwa mfano maisha yako yapo hivyo kwa sababu ya maamuzi ambayo ulishayafanya siku za nyuma. Kama ulifanya maamuzi mabovu ndivyo na maisha yako yalivyo sasa. Kuwa na maamuzi mabovu ni adui mkubwa sana aliye ndani yako ambapo usipokuwa makini anaharibu sana maisha yako pasipo wewe kujua. Kitu cha msingi kwako ni kuwa makini na kujifunza kuwa na maamuzi sahihi. Kinyume cha hapo utapotea.
5. Hamasa.
Ili ufanikiwe ni lazima uwe na hamasa kubwa sana ndani yako kila siku. Bila kuwa na hamasa hakuna mafanikio utakayoweza kuyafikia. Kwa bahati mbaya au nzuri hamasa huwa zinaanzia ndani mwetu. Kama ikitokea umekosa hamasa pole pole unakuwa umebeba adui wa kukuangusha bila kujijua. Kwa hiyo unahitaji kujijengea hamasa ili uweze kufikia mafanikio yako kwa kiasi kikbwa siku hadi siku.
Kwa vyovyote vile, ni lazima kupambana na maadui hao walio ndani yetu ili kufikia mafanikio makubwa. Chukua hatua mapema za kubadili maisha yako.
Nakutakia kila la kheri na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu;- 0713 04 80 35,
E-mail;- dirayamafanikio@gmail.com
Blog;- dirayamafanikio.blogspot.com

No comments :

Post a Comment