Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, April 15, 2016

Mambo Yanayokufanya Ukose Furaha Kwenye Maisha Yako.

No comments :
Kila kitu tunachokifanya katika maisha yetu kinalenga kupata furaha ya kweli. Tunatafuta pesa, tunajenga nyumba nzuri, tunanunua gari nzuri, tunaoa au kuolewa na wachumba wazuri kwa sababu ya furaha.
Furaha ya kweli inapokosekana katika maisha, kwa wengi kunakuwa hakuna maana ya kuishi tena ndio maana umeshawahi kusikia kuna wengine wamejiua lakini hiyo yote baada ya kuona furaha halisi wanaikosa kwenye maisha yao.
Lakini kwa mujibu wa tafiti nyingi zinaonyesha kwamba, pamoja na binadamu kuisaka furaha hiyo usiku na mchana lakini kuna wakati furaha hiyo huwa inakosekana kutokana na mambo mabalimbali yanajitokeza.
Ili kuijenga furaha hiyo tena na kwa muda mrefu kitu cha kufanya kwanza ni lazima ujue mambo hayo yanayoweza kukupotezea furaha.
Kwa kusoma makala haya utajua mambo ya msingi yanayokupotezea furaha kwenye maisha yako.

1. Watu wanaokurudisha nyuma.
Mara nyingi ni vigumu sana kukubali ukweli wa mambo hasa kama kuna watu wanaokuumiza. Watu hawa watakuumiza moyo na kuiona dunia yote chungu kwako.
Nini cha kufanya?
Kitu kimojawapo cha kufanya ili usiendelee kuumia acha kuwaweka watu hao kichwani mwako. Kama kuna sehemu walikurudisha nyuma basi hiyo imeisha, wafute kichwani mwako na anza maisha mapya.
Kumbuka, maisha yako unaweza ukayafanya upya na kuwa bora tena.


Toa mawazo hasi akilini mwako, uishi maisha ya furaha.
2. Mawazo hasi.
Kuwa na mawazo hasi kila wakati hukufanya ujione hufai na isitoshe unaweza kukonda kabisa.
Unapokuwa na mawazo hasi yanakufanya ujione wakati mwingine unashindwa kwenye karibu kwenye kila jambo.
Nini cha kufanya?
Toa mawazo yako hasi yaliyo kwenye kichwa chako. Muda wote jione mshindi na beba vitu vya kukusaidia ikiwemo pamoja na kujisomea vitu chanya.

3. Kujishusha sana.
Kujikosoa, kujishusha na kujitilia shaka, ni mambo ambayo yanaweza kukuumiza sana na kukukosesha furaha kama utaendelea na kujikosoa huko.
Kitu gani kinachotokea? Kwa mfano unapojikosoa unakuwa tena huwezi kufanya kitu chochote cha kukusaidia. Kwa sababu kila unachotaka kufanya umeshajiwekea mipaka tayari.
Nini cha kufanya?
Tambua maeneo bora kwako na yafanyie kazi. Pia jipongeze kwa mafanikio madogo uliyowahi kupata na weka malengo tena ya kukufanikisha.

4. Kuchukulia mambo kwa ujumla.
Kama kuna mtu amekufanyia kitu kibaya au hajakufanyia kama ulivyotaka, usichukulie kama mtu huyo ndivyo alivyo na ukaanza kuumia.
Chochote kinachokutokea kwenye maisha yako kiwe kizuri au kibaya usikichukulie kwa ujumla wake. Fikiri mara mbili kwanza kabla hujajitolea hukumu,  vinginevyo utaumia sana.
Nini cha kufanya?
Jifunze kuona mambo yanavyokwenda kwa uhalisia wake. Na usichukulie kwa ujumla sana. Hiyo itakusaidia kujenga furaha ya muda mrefu.

5. Kujiwekea kumbukumbu mbaya kwenye akili yako.
Chanzo kingine cha kukufanya uzidi kukosa furaha ni kuendelea kujiwekea kumbukumbu mbaya zilizotokea hasa kwa kipindi cha nyuma.
Kama kuna jambo baya lilikutokea kipindi cha nyuma liache kama lilivyo, lakini kwa kuling’ang’ania litakusababishia kuendelea kukosa furaha kwenye maisha yako.
Huna haja ya kuweka kumbukumbu sana na mambo yanayokuumiza akili mwako kwa muda mrefu.
Nini cha kufanya?
Kuanzia sasa jaza ubongo wako mambo mapya ili kutoa mambo ya zamani ambayo yameujaza ubongo wako kwa muda mrefu na yanakuumiza. Kwa kujaza ubongo wako utajenga furaha upya ya maisha yako.

Endelea kujifunza kupitia DIRA YAMAFANIKIO kila siku.  Ni wako rafiki Imani Ngwangwalu. Mawasiliano +255 713 048 035.No comments :

Post a Comment