Mar 10, 2015
Hivi Ndivyo Kufikiri Kimazoea Kunavyoweza Kuharibu Maisha Yako.
Kuna wakati katika maisha
yetu huwa tunajikuta ni watu wa kutenda mambo yetu kwa mazoea zaidi na kudhani
tupo sahihi, wakati tupo kwenye makosa matupu ambayo huwa yanatuumiza, badala
ya kutusaidia kama tunavyofikiri. Makosa haya huwa tunayafanya kutokana na
matendo ama mienendo ambayo tunakuwa nayo binafsi katika maisha yetu ya kila
siku bila kujijua sisi wenyewe kuwa tunakosea.
Makosa haya mara nyingi huwa
yanatokana na kufikiri kimazoea. Kufikiri huku kimazoea kwa kawaida huwa ni
jambo baya sana ambalo huweza kuathiri
maisha yetu. Tunapoamua kufikiri kimazoea maana yake huwa tunalazimika kufikiria
kwa mujibu wa kile tulichofundishwa utotoni katika malezi au mazingira
tulimokulia, bila kujiuliza wala kuchukua hatua zozote muhimu zenye uwezo wa
kuleta mabadiliko tofauti kwetu.
Hebu fikiria kuhusu
kulalamika au kunung’unika. Watu wengi huwa hawajui kwamba, tunaponung’unika
tunasema au kujiambia kwamba hili tatizo ambalo tunalinung’unikia hatuwezi
kulikabili au kulitatua, bali kuna wengine wanaoweza kulitatua. Kulalamika, iwe
tunajua au hatujui, lakini kuna maana ya sisi walalamikaji kukosa uwezo,
kushindwa kumudu, hivyo kutegemea wengine kumudu au kufanya kwa niaba yetu.
Kwa kulalamika, tunaamini
kwamba, kwa hizo kelele zetu tunawachochea wengine ambao tunaowaamini kwamba wana uwezo wa
kukabiliana na yale matatizo yanayotukabili kwa wakati huo. Badala ya
kulalamika, tunatakiwa kupeleka nguvu zetu zote kwenye suluhu ya tatizo.
Kulalamika kuna maana kwamba, nguvu zetu tumezipeleka kwenye kuamini kwamba
tatizo ambalo linatukabili hatuliwezi na hatuoni suluhu yoyote.
Hebu fikiria juu ya kulaumu
kwako. Hii ni tabia ambayo wote tunaiona ni sahihi kabisa kwa sababu ya mazoea
tu. Tunapolaumu, bila kujua tunaiambia dunia pamoja na sisi wenyewe kwamba,
hatuna nguvu, bali kuna wenye nguvu zaidi kuliko sisi ambao wameshindwa
kutuwezesha au kutugawia. Fikiria tena tokea umeanza kulaumu katika maisha yako
ni kati kikubwa ambacho umevuna, zaidi ya kuharibu maisha yako?
Kwa kulaumu, tunatupa nguvu
na uwezo uwezo wetu wa kubaki watupu. Kwa kuwa kila binadamu anapaswa
kuwajibika kwa maisha yake, kulaumu tuna maana kwamba tumeshindwa wajibu wetu.
Tunaamua kwa kusudi kabisa kuwa wahanga wa maisha yetu, uamuzi ambao
haupendezi. Badala ya kulaumu sana, jifunze kukaa chini na kuchukua hatua
ambazo zitakusaidia kuelekea kwenye kubadili maisha yako.
Kuna kujilaumu au kujikosoa,
tabia ambayo pia ni ya kimazoea. Kumbuka, kile kinachoenda ndani, kwenye
kufikiri kwetu, ndicho chenye kujionesha nje. Kwa kuwa maisha hutupatia kile
tunachokihitaji, kwa kujilaumu au kujikosoa, tunachopata ni maumivu ya jambo
tunalojilaumu kwalo. Tunapojiambia kwamba, sisi ni wajinga kwa sababu
tumeshindwa biashara fulani, ni lazima
tutakuwa wajinga kweli, kwani hicho ndicho tunachokitaka.
Badala ya kujikosoa
tunapofanya jambo kinyume na matarajio yetu na tunakuta tunataka kujilaumu,
inabidi tuchukue kalamu na karatasi na kuandika yale yote ambayo ni mazuri kwa
upande wetu. Tunayo mazuri mengi, kila mtu ana mazuri mengi. Hivyo, hatuna haja
ya kujikosoa kwa mabaya yetu, kwani hayo siyo tunayoyahitaji. Unachohitaji wewe
ni kuachana na kujikosoa sana na kusonga mbele.
Kila tunapojikosoa,
tunapaswa kujua kwamba, tunazuia nguvu nyingi chanya kuweza kutufikia na
kutusaidia tunakotaka kwenda. Hii ni kwa sababu tunayaambia mawazo ya kina
kwamba, hatustahili kupata mema au mazuri. Kumbuka, maishani huwa tunakipata
kile tunachokitaka au kukitarajia. Kama utakuwa tu wewe ni wa kujikosoa sana,
itakuwa ni sawa na kujiambia hutaki mafanikio makubwa maishani mwako.
Kunakuwakosoa wengine
kimazoea. Kwa mazoea, tabia hii huwa tunaiona kuwa ni ya kawaida sana na haina
madhara kwetu. Huwa tuaamini kwamba, tuna haki ya kukosoa wengine na jambo hilo
haliwezi kutudhuru. Kwa kuwahukumu wengine vibaya au kuwakosoa , tunatengeneza
vurugu na ukosefu wa amani kwenye mfumo wetu wa kufikiri na ufahamu. Hii ni kwa
sababu, tunaupeleka uzingativu wetu kwenye jambo ambalo hatulitaki.
Kijicho ni tabia ambayo
wengi tunadhani au kuamini kwamba, ni lazima tuwe nayo. Lakini kijicho ni
dalili ya mtu kuamini kwamba yeye hawezi kama huyo anayemwonea kijicho na
hatakuja kuweza. Kuwa na kijicho ni moja ya tabia ya kimazoea ambayo huwa
inauwezo mkubwa wa kuharibu maisha yetu wenyewe bila kujijua.
Jaribu kufikiria au kutazama
ule uzoefu mzuri kuhusu maisha na siyo usioutaka. Jaribu kuangalia yale tu
unayoyapenda kwa watu kuhusu watu wengine.
Kisha jenga tabia nzuri ambazo zitakusadia katika maisha yako na achana
na kufikiri kimazoea ambako hakuwezi kukusidia kitu zaidi ya kukupa maumivu tu.
Hivyo ndivyo kufikiri kimazoea kunavyoweza kuharibu maisha yako.
Nakutakia mafanikio mema,
ansante kwa kutembelea matandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea
kwashirikisha wengine kujifunza mambo mazuri yanayoendelea hapa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com
- dirayamafanikio.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.