google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Mar 19, 2015

Hiki Ndicho Kitu Kinachokufanya Ushindwe Kupata Kile Unachokihitaji Katika Maisha Yako.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yako unaweza ukajikuta ama unatamani sana uwe katika ngazi fulani ya mafanikio, lakini ni kitu ambacho huwa hakitokei kwako. Wakati mwingine umekuwa ukidhamiria na kuamini kwamba, lazima itakuwa, lakini huwa haiwi kama unavyofikiria. Pamoja na juhudi nyingi ambazo umekuwa ukizifanya, zimekuwa ni kama kazi bure kwani mara nyingi umekuwa ukishindwa kupata hasa kile unachokihitaji katika maisha yako ambacho ni mafanikio.

Pengine umekuwa ukijitahidi hata kufanya sala au tahajudi(Meditation) ili kuweza kubadili mwelekeo na kuweza hata kufanikisha kile unachokihaji, lakini wapi mafanikio hayo umekuwa huyaoni. Ni kitu ambacho kumekuwa kikikuchanganya na kushindwa kuelewa unakosea wapi hasa na ufanye nini? Hali hii imekuwa kuna wakati inataka kukuvunja nguvu na kukufanya uamini kuwa, suala la kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako ni kitu ambacho hakiwezekani.

Katika hali ya kushangaza umekuwa ukiona wengine wakijaribu kuomba mara moja na kuweza kufanikisha jambo lile, wakati kwako inakuwa ni vigumu sana, ingawa kama ni kudhamiria, na kuamini kwamba itakuwa ni kulekule na pengine zaidi kwa hilo linaloshindikana. Hali ama matokeo kama hayo yamekuwa yakikutisha tamaa na kukupelekea wewe kutaka kuamini kuwa una kitu kama mkosi au laana fulani hivi inayokuzuia ushindwe kufanikiwa, kitu ambacho sio kweli hata kidogo.


Bila shaka kwa namna moja au nyingine unaweza ukawa umewahi kukutana na hali hii katika maisha yako ambayo pengine imekuwa ikikuumiza kichwa na kushindwa kuelewa kabisa ni kitu gani kinachopelekea wewe usiweze kupata matokeo mazuri kwa kile unachokihitaji katika maisha yako?

Ingawa ukweli ni kwamba, kuamini kwamba inawezekana na kudhamiria kumudu, huweza kuzaa au kutozaa matunda kwa sababu moja tu kubwa. Huwa kunakuwa na kusigishana au kupingana kati ya kile ambacho mtu anachoamini na kile ambacho anadhamiria au kupania kiwe katika maisha yake na hiki huwa ndicho kitu kinachokufanya usipate kile unachokihitaji katika maisha yako.


Kama mtu  kwa mfano, anadhamiria au anapania kwamba, anataka kuona uhusiano wake na mke wake au mume wake unakwenda vizuri, huku akiwa anaamini kwamba, wanawake hawaaminiki, au wanaume ni wakorofi, uhusiano huo hauwezi kuwa mzuri, hata kama amepania na kusali vipi kwake uhusiano mzuri hauwezi kutokea. Unajua ni kwa nini?


Iko hivi, mara nyingi kupania au kuamini kwetu kwamba, inawezekana na kutaka kwetu jambo liwe kama tunavyotaka, sala zetu na maombi yetu, vyote hivi huwa vinafanyiwa kazi na mawazo yetu ya kina. Sasa, kama kuna kitu kingine ambacho ni kinyume na kile tunachotaka au kupania kiwe, ni wazi tunakuwa tunayachanganya mawazo ya kina na inakuwa ni vigumu sana kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.

Kama kweli tunataka uhusiano wetu uwe mzuri na tunaamini kwamba, inawezekana, lakini huko kwenye mawazo yetu ya kina tunaamini kwamba, wanawake ni dhaifu, hatutaweza kupata tunachotaka kwa sababu, mawazo yanakuwa  yanapokea taarifa au imani mbili zenye kukinzana au kupingana.

Kwa kuamini kwamba, wanawake ni dhaifu, lile wazo la kwamba inawezekana kuwa na uhusiano mzuri na bora sana litatupwa nje na kufanyiwa kazi lile lililokuwa hapo awali. Ni hadi ile imani kwamba, wanawake ni dhaifu iondolewe, ndipo ambapo kudhamiria au maombi yatafanya kazi.


Utakuta mtu anasali kila siku na kuamini kwamba, atafanikiwa katika jambo fulani, lakini anakuwa ana imani kwamba, rangi yake itamponza kwa sababu, anashindana na watu wenye rangi nyingine. ‘Wenzetu wale wanajua namna mambo haya yanavyofanywa’, atawaza. Kwa hiyo, dhamira na sala yake vitatupwa nje na hili la ‘wenzetu’, ndilo litakalofanyiwa kazi.

Imani zetu, ambazo tuliwekewa kwenye mawazo yetu siku za nyuma kwenye malezi au mazingira tulimokulia, zinakwenda kwa kina kirefu hivyo zina nguvu zaidi. Tunapoleta imai mpya zenye kukinzana na zile za zamani, hizi mpya ni lazima zitupwe nje au tuseme haziwezi kufanyiwa kazi kabisa kwenye mawazo yetu ya kina na kujikuta hatuwezi kupata kile tunachokihitaji katika maisha yetu.

Hebu jaribu leo kufikiria ama kutengeneza orodha ya mambo ambayo umekuwa ukiyaomba au ukitaka uyafanikishe katika maisha yako na umekuwa ukiamini kwamba yanawezekana na umekuwa ukifanya kwa kupania, lakini bado hayakubali. Kama utayapitia vizuri na kurudi nyuma, utabaini kwamba, huenda kile ulicholishwa utotoni kuhusu kutowezekana kwa mambo hayo, bado kina nguvu kubwa kwenye mawazo yako ya kina.

Ili sasa uweze kumudu kupata kile unachokihitaji katika maisha yako ni muhimu sana kwako, kusafisha kwanza mawazo yako kuhusu yale mabaya yaliyowekwa humo kuhusiana na jambo ambalo unataka kufanikiwa kwalo. Kila kitu utaweza kukifanikisha katika maisha yako kama hakuna kukinzana ndani yako. Kumbuka na tambua kuwa kukinzana ndani mwako ndicho kitu kinachopelekea ushindwe kupata kile unachokihitaji katika maisha yako.

Ansante kwa kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kwa ajili ya kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,




No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.