google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Mar 6, 2015

Kama Unafanya Kitu Hiki Kidogo Katika Kazi Unayoifanya, Ni lazima Ufanikiwe.

No comments :
Mara nyingi unapoamua kuipenda kazi yako kiukweli kutoka moyoni kitu pekee kitakachokutokea ni kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako. Unapokuwa unaipenda kazi yako, inakuwa inakupa nafasi ya kuweza kubuni na pia kuwavutia wengine na hata wale unaokuwa nao ukiwa hapo kazini kwako.

Mhudumu wa hoteli kwa mfano, anapokuwa anaipenda kazi yake, huweza kuwafanya wateja kuhisi kwamba, wanathaminiwa sana. Siku za nyuma kidogo, mimi binafsi na rafiki yangu wakati tupo Chuo tulikuwa tukitoka kwenda kula chakula cha jioni kila wikiendi katika mgahawa mmoja uliokuwa eneo la barabara ya sita, mjini Dodoma, ingawa sina uhakika kama bado upo au hapana.

Hapa kulikuwa na mhudumu ambaye alikuwa akiitwa Pendo. Huyu mhudumu alikuwa akiwafanya wateja wengi wajihisi vizuri, bila shaka. Alikuwa na upendo kweli kama jina lake lilivyo, alikuwa mcheshi na mvumilivu, yaani asiye na hasira. Kutokana na ucheshi wake huo kitu ambacho kilipelekea kuwa na wateja wengi zaidi katika eneo la kazi yake. Kwa kifupi, aliipenda kazi yake.

Pia ikafika wakati ambapo jamaa yangu mmoja alikuwa akitafuta mtu mwenye uwezo sana wa shughuli za mgahawa, mcheshi na mchapa kazi, ili aweze kusimamia hotel aliyokuwa anataka kuifungua. Alikuja kuniambia kuwa alikuwa ana wazo la kwenda kumchukua mhudumu Yule, lakini kwa bahati mbaya alienda na akawa amemkosa mhudumu Yule na aliambiwa amepata kazi sehemu nyingine nzuri zaidi.

  
Hivi karibuni pia huko Sweden, tukio linalokaribiana na hili langu ambalo nililipata kwa njia mtandao lilitokea. Mzee mmoja mteja katika mgahawa unaofahamika kama Njuraanger, kwenye mji wa Sundsvall, ulioko katikati ya nchi hiyo, alishangazwa na jinsi mhudumu mmoja msichana mdogo alivyokuwa akifanya kazi yake ya uhudumu kwa uadilifu mkubwa sana.

Mzee huyo ambaye alikuwa ni mfanyabiashara katika siku ya tukio alikuwa akila chakula cha jioni na wenzake. Baada ya kuhudumiwa na mhudumu msichana wa miaka 19, mzee huyu alifikiria na kuona kuwa, bakhshishi ya kawaida isingeweza kumfaa binti Yule zaidi ya kumpa gari moja iliyoko nyumbani kwake kama zawadi na hongera kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mzee huyu alitoa kutoka kwenye lundo la funguo zake, funguo za gari lile. Alimkabidhi funguo zile mhudumu Yule ambaye awali alidhani ni dhihaka. ‘Aliniuliza umri wangu na nilipomtajia alisema ananipa gari, alinipa funguo. Awali nilijua ilikuwa ni mzaha’ alisema binti Yule. Kesho yake alifatana na Yule mzee na kwenda kuichukua ile gari.

Mzee huyo alipoulizwa sababu ya kumpa msichana huyo bakshishi ya gari, alisema aliona umalaika Fulani kwa msichana huyo. Ni wazi uhudumiaji wake ulimvutia hadi akaona ni vyema kumpa bakshishi za kawaida haitoshi. Huyu mzee alisema aliona umalaika ndani ya mhudumu Yule. Umalaika tulionao hauwezi kuonekana kama tunafanya shughuli kwa kujilazimisha, siyo rahisi.

Ni wahudumu wangapi hapa nchini wanafanya kazi zao kwa kuzipenda? Lakini ni watumishi wangapi ambao kwa ujumla hufanya kazi au shughuli zao kwa kujilazimisha? Ni wengi sana. Matokeo yake ni nini? Ni maumivu yasiyoisha, majuto na kujenga uadui na watu wote tunaokutana nao hapo kwenye shughuli zetu.

Ni muhimu sana kwetu kuweza kujifunza kuzipenda shughuli tunazofanya. Kuzipenda kuna maana ya kuziheshimu na kuzikubali kwamba, kwa sasa, hizo ndizo shughuli zetu. Kwa kadri jinsi tutakavyozidi kupenda shughuli zetu ndivyo tutazidi tukijikuta tunavuta mafanikio makubwa upande wetu kwa sababu tunakuwa tunafanya kwa moyo wote bila kuchoka. Na kama unafanya kitu hiki kidogo katika kazi unayoifanya ni lazima ufanikiwe.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.

IMANI NGWANGWALU,

  • 0713 048 035,


No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.