Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, March 17, 2015

Kama Unatafuta kitu Hiki Katika Maisha Yako, Utateseka sana.

No comments :
Hebu fikiria, jaribu kufikiria, halafu karibia kuamini au amini kabisa kwamba, una vitu vifuatavyo. Una magari ya kifahari kumi, nyumba za kifahari mbili kila mkoa kwa mikoa yote Tanzania, mashamba ya ekari elfu moja kila mkoa na fedha zipatazo shilingi bilioni kumi benki. Hebu fikiria.

Najua unaweza kujenga taswira, kama tunavyofanya wakati tunapoota ndoto za alinacha, hadi kufanya hali ionekane kuwa ni kweli. Hebu fikiria tena kwamba, kwa sababu ya mali hizo umekuwa maarufu katika nchi za afrika mashariki na kati. Hebu fikiria kwamba, unaandikwa na kutajwa magazetini, redioni na kwenye televisheni.

Jione kwenye hizo fikra zako kwamba, hayo ndiyo maisha yako, tajiri na maarufu. Halafu endelea kufikiria kuhusu maisha yako. watu wanakujua, wanakuogopa, wanakushangaa na kukunyenyekea. Kila unapoenda unajua watu wanakutazama na kutamani wangekuwa kama wewe labda.

Endelea kufikiria kwamba, umekuwa tajiri na maarufu tangu mwaka 1990 hadi leo. Hebu jaribu kufikiri kwa makini zaidi, baada ya kusifiwa, kuogopwa, kunyenyekewa na kufahamika kila kona , halafu kingefuata kitu gani? Ni kitu gani ungekuwa umekipata? Sawa, umesifiwa na kufahamika na ukajisikia vizuri. Halafu inakuwaje baada ya kujisikia vizuri kwa muda wote huo?

Katika kufikiri kwako, unadhani bado utaendelea kujali kusifiwa na kunyenyekewa? Hapana, haiwezekani. Baada ya muda fulani wa kusifiwa na kunyenyekewa, utagundua kwamba, hakuna chochote ndani ya sifa hizo na kunyenyekewa huko. Kwanini? Kwa sababu, wewe siyo kusifiwa na kunyenyekewa, wewe ni wewe hiki ndicho kitu hasa nataka ukijue vizuri hapa.Lakini, hata kama utaendelea kusifiwa na kujisikia vizuri, halafu itakuwa ni kitu gani? Hebu fikiria kwamba, kila asubuhi ukiamka, magazeti yamendika kuhusu wewe kwa sifa zote, hata bei ya viatu vyako, televisheni zinakuonesha  ukipanda gari lako la kifahari na kwenda uendako na redio zinazungumzia juu ya fedha na utajiri wako sana tu. Hebu fikiria, unadhani itakusaidia kitu gani  hiyo?

Mwisho wa sifa hizo ni upi hasa? Unaposifiwa ni wapi panajisikia vizuri, ni sehemu gani  ya mwili inapata furaha au starehe? Lakini, gharama ya kulinda sifa na kunyenyekewa huko unaijua? Huwezi kuijua kwa sababu hujaingia kwenye sifa na kunyenyekewa na watu. Ukiingia na wale ambao tayari wameshaingia, wanataka kutoka, hawataki tena ‘balaa’ hilo.

Mcheza soka maarufu wa siku za nyuma kidogo, David beckam aliwahi kusema, maisha yake ni upuuzi mtupu kwa sababu ya umaarufu, Diana aliwahi kujuta kufahamika kwake. Unapotafuta mafanikio kaa chini ujiulize kweli unataka mafanikio hayo makubwa hasa au unatafuta sifa tu ili watu wakujue?

Halafu jiulize tena wakishakujua nini kinatokea? Tunawajua akina Bush, Tunawajua akina Neymer, hata pia tunawajua akina Tyson. Halafu kuwajua kwetu kunawapa kitu gani, kinatokea kitu gani? Wanaendelea kuwa watu walewale, wanaendelea kuwa binadamu na kama sisi, miili yao itapotea hivi pindi.

Kuna profesa mmoja kwa jina alipata kufahamika kama Yunus, ambaye ni raia wa Bangladesh. Huyu alikuwa ana Benki ambayo iliweza kukopesha na kubadili hali za maisha ya familia karibu millioni tatu(siyo watu, ni familia) nchini humo.

Lakini, pamoja na uwezo huo aliokuwa nao yeye alipata kuishi kwenye nyumba ya kawaida tena ya kupanga. Hiyo yote inaonyesha profesa huyu alikuwa hataki sifa wala kunyenyekewa na kuandikwa kila mahali kwenye magazeti hilo lilikuwa sio lake, kikubwa alichokuwa akitafuta ni mafanikio katika maisha yake na ambayo yatasaidia na wengine.

Tuna watu katika jamii yetu tunayoishi, huwa ni watu wa kupenda sifa sana kiasi cha kujiita waheshimiwa. Si ajabu huwezi kuwashangaa watu hawa wakilewa sana kwa lengo la kutaka kuonyesha jeuri ya pesa kiasi cha kwamba mpaka kuweza kusahau nyumbani kwao.

Inadaiwa kwamba kwa watu kama hawa, ili akupe stahili yako, hata kama ni madaraka kazini, lazima umnyenyekee. Kama ametoka ndani, ni lazima uhakikishe unamkimbilia, kupokea mkoba na kujidai hata kama kumfuta vumbi kidogo kwenye suti hata kama haina vumbi.

Halafu unajiuliza, ni ya nini yote hiyo? Ni huyuhuyu ambaye anakunywa pombe hadi anasaidiwa kuingia garini? Kwanini anywe kiasi hicho? Pesa na umaarufu aliodhani utampa nafuu, vimeshindwa kufanya kazi hiyo. Sasa ina maana gani, utajiri na umaarufu?

Labda utajiri kama ule wa Profesa Yunus ndiyo utajiri tunaoutaka. Utajiri unaoangukia mikononi mwa watu waliokamilika, kimwili, kihisia, kiakili na kiroho. Huu utajiri mwingine ni visu vyenye kuwachanja walionao na kuwakatia wanaozunguka. Umaarufu tunaoutaka, hauna kitu kwa sababu, hata kama ungekuwa maarufu vipi, polepole umaarufu utafifia na maisha yako ya mwili hayazidi miaka 120.

Sasa kusifiwa kwa miaka 120 tu, kuna maana gani, kunakusadia kitu gani, wakati hata dini yako haikwambii kuwa itaishi milele. Umebaini kwamba, hukuja duniani kutafuta sifa na umaarufu, bali umekuja kuishi ili ufurahie maisha yako. Mara nyingi tunamtaja Bill Gates kila siku unafikiri anajali hilo? Unafikri anajali kutajwa huko, ambao ni mtihani mgumu kuliko kutafuta mali na utajiri alionao.

Ndiyo maana unaweza kukuta mtu amenunua kagari na kujenga kajumba, halafu anamtukana na kumdharau kila mtu. Anakwenda kwa wanamziki wamtaje jina lake kwenye nyimbo zao, anakwenda kwenye televisheni kujidai anasaidia watoto yatima. Anatafuta sifa na kutaka watu wamjue. Halafu wakishamjua ndiyo iwe nini?

Akiishiwa, anajifungia ndani, anachanganyikiwa, anajenga uadui na kila mtu, anadai amelogwa. Anakuwa anababaika kwa sababu amepoteza kile alichodhani ndicho yeye, mali na umaarufu. Hajui kwamba, yeye yupo kama binadamu na ni kamili  bila chochote. Ni lini binadamu atainua macho na kuuona ukweli? Inaniuma sana.

Kutafuta kujulikana ni kutafuta kuinuliwa kutoka pale ambapo mtu anaamini yupo(Chini) ili ajisikievizuri. Mtu ambaye anajua yupo anapostahili hana haja ya kutaka ainuliwe kutoka hapo nakupelekwa mahali ambapo atahisi kustahili.
Kutaka sifa ni kutaka kuondolewa kwenye tope, kwenye uchafu, pasipo faa na kuwekwa mahali pengine. Kwa hiyo mpenda sifa, ni mnyonge kuliko mtu mwingine yeyote.

Wengi huwa hatujui kwamba, sisi ni sisi na hatuwezi kuwa kitu kingine, tupande ndege, tununue merikebu, tujulikane hadi uvunguni, tuimbwe na maredio na kuoneshwa na matelevisheni kutwa kucha, bado ni sisi tu. Thamani yetu inaendelea kuwa ileile.

Huko ndani mwetu kunaendelea kuwa kulekule. Ni kama kiti, hata ukikiwekea marembo gani, ukaweka miguu mitatu, ukakitandika na dhahabu na lulu, kazi yake ni ileile ya kukaliwa, haibadiliki. Ikishabadilika, kinakuwa siyo kiti tena.

Nasi hata tuwe vipi, ubinadamu wetu hauwezi kubadilika, uko palepale. Msingi wa binadamu haubadilishwi na chochote, kama ambavyo dhima ya kiti haibadilishwi na namna kilivyotengenezwa. Kila mtu anapaswa kujua kuwa, amekuja duniani kuishi kama yeye.

Kama ni furaha atajipa mwenyewe, kama ni kero atajipa mwenyewe, kama ni kujishusha atafanya hivyo mwenyewe, hali kadhalika kujipandisha. Lakini, hata kama itakuwa vipi, anabaki kuwa binadamu.

Kama nilivyoanza awali mwa makala haya. Nakuomba ujaribu kufikiri tena kwamba, tayari una kila kitu kinachokuhangaisha hivi sasa. Fedha kibao, magari, majumba, umaarufu, mke au mume mzuri kuliko wote duniani, watoto wenye akili kuliko wote. Halafu kitafuata kitu gani?

Nataka ujiulize baada ya hayo yote kutimia, ni kitu gani kitafuata? Kama umefikiri vizuri, utagundua kwamba, ni upuuzi mtupu mbele. Utagundua kuwa hukuhitaji hivyo vyote hivyo, bali ulihitaji ulivyohitaji wewe kuvihitaji.

Hivyo vingine siyo wewe uliyevihitaji. Ni nani sasa anayekusumbua na kuhangaika na kubabaika na maisha kuvitafuta hivyo? Nakuachia swali hilo.

NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa elimu na maarifa bora yatakayoboresha maisha yako.

IMANI NGWANGWALU,     No comments :

Post a Comment