Mar 11, 2016
Usipojiandaa Kwa Mabadiliko Haya, Hakuna Wa Kukusaidia Katika Maisha yako.
Dunia imekuwa ndogo sana,bila kujali utaiita kitu gani. Kama utaita utandawazi, sayansi na teknolojia, demokrasia zaidi, uchumi wa soko, teknolojia ya habari au chochote, ukweli unabaki kuwa huo. Ni jambo la kusikitisha sana kuona wasomi na wanasiasa ambao kwa bahati mbaya naweza kusema hawana jipya sana kwa jamii, wakilaumu serikali kwenye suala la utandawazi.
Nijuavyo mimi, mabadiliko ya
kijamii hayawezi kuzuiwa na mtu, hata kama angekuwa na uwezo wa kiwango gani,
labda anachoweza ni kufanya uharibifu wa kuwafuja watu na matokeo yake ya
kawaida hayapendezi sana. Hakuna mtu ambaye angeweza kuzuia mfumo wa maisha
holela ya binadamu wa awali ambapo mali ilikuwa ni kiwango cha nguvu za mwili
alizokuwa nazo binadamu. Yule aliyeweza kuua Tandala kwa jiwe ndiye aliyekuwa akiheshimiwa na kufikia mafanikio
kirahisi.
Hakuna ambaye angeweza
kuzuia mfumo huo kuupisha ule wa uchifu, ambapo mwenye kauli na uwezo wa karibu
kabisa kufanikiwa alikuwa ni mtu yeyote kutoka ukoo wa kichifu. Hata kama mtu alikuwa akidondokwa na kamasi kutwa
nzima, ili mradi tu anatoka ukoo wa kichifu, huyu ndiye aliyehesabiwa kuwa bora
na alikuwa na njia rahisi zaidi kufikia mafanikio.
Hakuna aliyeweza kuuzuia
baadaye mfumo wa mtaji kufuatia mapinduzi ya viwanda vya ulaya. Kipindi hicho
mtu mwenye uwezo na aliyeweza kufikia mafanikio ya kipato ni Yule ambaye
alikuwa na mtaji. Mfumo huu umeendelea na bado hadi sasa unavyo vijiukoko
vyake, ambavyo huenda vinaishiaishia.
Leo hii hakuna anayeweza
kuuzuia mfumo uliopo hivi sasa duniani, unaoitwa kwa majina mengi, ambao
umetawaliwa na maarifa. Mtu mwenye maarifa ndiye ambaye leo hii anaweza
kuzungumzia kufikia mafanikio kiurahisi kabisa. Kwa maarifa nina maana ya
ufahamu wa mambo mengi ya kila siku. Kuna njia nyingi za kupata taarifa ambazo
zinaweza kumfanya mtu kujaa maarifa yatakayowezesha kuishi vizuri katika
kipindi hiki.
Leo hii, mabadiliko
yanayotokea hapa duniani ni makubwa na ya kila siku, siyo kila mwezi, kila
mwaka au muongo(miaka kumi) bali ya kila siku kama siyo kila saa. Wengi tunajua
kwamba, kila mwaka kunakuwa na ugunduzi tofauti na wa kushangaza wa kompyuta,
vifaa vya viwandani na hata nguo. Dunia inakimbia sana kuliko ambavyo wengi
tunaweza kukabiliana na kasi yake.
Leo hii hapa kwetu Tanzania
tunalalamika kwamba, wanaoitwa ‘makaburu’ wamevamia Nchi, tunaogopa kuhusu
umoja wa Afrika mashariki kwamba tutazidiwa na nchi nyingine zilizo kwenye
umoja huo, tunahofia pia ubinafsishaji na uwekezaji. Hatuna haja ya kuogopa
vitu hivyo vidogo, kwani vikubwa vinakuja, ambapo tutajikuta tumerejea kuwa
waosha vyombo vya wenzetu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Tunapaswa kuwa na
dira sahihi ya mafanikio na kuamka haraka sana.
Wakati wenzetu wanasoma na
kutaka kujua mabadiliko ya dunia ili kukabiliana nayo, sisi tunasoma,
tunaangalia na kusikiliza, hadithi za habari za kuchochoea hisia zetu hasi.
Watanzania walio wengi wamekata tamaa bila kujijua.
Mwalimu nyerere aliwahi
kusema, ‘ tumechelewa, wakati wenzetu wanatembea inabidi tukimbie.’ Mimi
nasema, ‘tumekaa chini, wakati wenzetu wanakimbia, inabidi tuinuke na tupae
kabisa.’
Tatizo tulilonalo wengi
tulifundishwa na kulelewa na dhana ya kusaidiwa iwe na mjomba, ndugu ama
serikali na kusahau kuwa inatakiwa tujiandae kukabiliana na mabadiliko ya dunia
hii yenye kasi kubwa kupindukia. Ukweli ni kwamba, ili tuweze kujiandaa na
kukabiliana na mabadiliko haya ni lazima mabadiliko haya tuyafanya kwenye
ufahamu wetu. Ufahamu huu utatokana na utayari wako wa kupata maarifa ya mabadiliko ya dunia, bila kujali
umesoma hadi wapi au hukusoma kabisa.
Huwa inashangaza wakati
mwingine ninapokutana na watu ambao nilisoma nao Chuo kikuu au ambao nilifanya
nao kazi mahali fulani,wanaponiambia, ‘hayo mambo umejifunza lini, utapeli
huo.’ Huwa ninacheka kwa uchungu mwingi kwa sababu haipendezi kuona kwamba,
pamoja na silaha imara tuliyopewa yaani elimu ya chuo kikuu, tumeshindwa kuamua
kuitumia kuijua dunia kwa upana wake. Tunaamini yale masomo tuliyoyapata
chuoni, basi yametufanya kuwa machifu na tunaamini kabisa kwamba hakuna
kilichobaki na kujifunza kama kipo ni lazima kihusiane na masomo tuliyosoma
chuo kikuu.
Hili ni kosa na kasoro kubwa
sana. Kumaliza elimu ya chuo kikuu na kupata shahada ya kwanza, pili au tatu,
haina maana kwamba umepewa ‘waranti’ ya kuwa mtu finyu, kujua tu kile
ulichojifunza, basi. Hapana, dunia inaenda kasi sana na kile ulichojifunza
jana, leo hakina maana tena, kimebadilika sana. Bila kusoma, kujifunza na
kuyajua mengi mapya na makubwa zaidi utakwama, hata ndani ya taaluma yako.
Ni lazima tujifunze
kukabiliana na mabadiliko yoyote yale kwa kuwa na ufahamu wa kutosha. Isije
ikatokea kitu au chochote kitakachokuyumbisha. Kama ni kusoma tusome tukiwa na
malengo na sio kwa sababu tunataka stashahada au shahada , ambapo tunajikuta
tumekariri masomo badala ya kuyaelewa.
Tunafaulu kweli, lakini
tunakuwa finyu kuliko wale ambao hawakusoma kama sisi. Tunajikuta sio wabunifu,
hatuna jipya tunalochangia katika maeneo yetu ya kazi na kwa jamii. Tunajikuta
tumebaki kufanya kazi zilezile(Routine) kama kwamba ni madubwana (Robots).
Hatimaye hata wale wasiosoma hawaoni tofauti ya ufahamu kati yao na sisi na
tunapata dhambi kwa kufanya washindwe kuona faida ya kusoma.
Kuna wale wengine ambao
wamekata tamaa kwa sababu hawana elimu au hawana elimu ya kutosha. Ukweli ni
kwamba, dunia ya leo, elimu ni maarifa maalumu. Kwenda darasani ni muhimu,
lakini kutoenda darasini kama imetokea ikashindikana, haina maana kwamba mtu
hawezi kujifunza na kupata maarifa. Siyo kweli. Nasema siyo kweli kwa sababu
kama mtu hakwenda darasani anaweza kuwa na malengo na kufikia mafanikio makubwa
sana.
Kumbuka kwa sasa maisha ni
zaidi ya diploma au digrii, bali ufahamu wa mambo maalumu na malengo. Tunaweza
kuwa na digirii nyingi lakini tukashindwa kuona njia ya mahali tuendako kwa
sababu ya ugiligili, tukaanza kuwa walevi, tumekata tamaa. Tatizo hapo siyo
ubaya wa serikali au watu wanaotuzunguka, bali ni kushindwa kwetu kujua malengo
yetu maishani.
Kama umesomea au unasomea
ualimu kwa sababu ulikaa ‘kijiweni’ kwa muda mrefu ukaona huna la kufanya,
unapoteza muda wako bure. Kama ulisomea au unasomea kozi fulani kwa sababu
walioisoma wanapata fedha nyingi za rushwa huenda pia upo matatani. Kama
unasoma au ulisomea kozi fulani kwa sababu ya shinikizo la wazazi, ndugu au
jamaa, hujajitendea haki. Kikubwa jiandae kwa ajili ya mabadiliko yanayotekea
kila siku, usipojiandaa hakuna wa kukusadia zaidi utateseka sana katika maisha
yako.
Nakutakia mafanikio mema,
endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
- 0713 048 035,
- dirayamafanikio@gmail.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.