Aug 13, 2015
Jifunze Kilimo Bora Cha Vitunguu-2
Habari rafiki na mpenzi
msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO karibu tena katika siku nyingine
ambapo tunapata nafasi ya kujifunza juu ya fursa ya uwekezaji katika kilimo cha
vitunguu lakini ikiwa ni makala ambayo tuliianza wiki iliyopita.
Katika makala hiyo ya wiki
iliyopita tuliweza kuangalia aina za kilimo cha vitunguu, mahitaji muhimu
katika kutayarisha shamba, upandaji wa mbegu za vitunguu, matunzo ya vitunguu,
namna ya kupata mbegu bora pamoja na aina za vitunguu vinavyolimwa nchini kwa
wingi.
Leo katika makala yetu,
tutaendelea na kuangalia katika maeneo mengine muhimu yanayohusika katika suala
zima la uzalishaji wa vitunguu na kukupa faida inayotakiwa ikiwa wewe ni
mkulima uliyepania kufanikiwa. Kwa kuanza makala yetu, tutaanza na kujifunza
magonjwa na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
SOMA; Jifunze Kilimo Bora cha Vitunguu
Magonjwa
na wadudu waharibifu kwa vitunguu.
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu
mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili
kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua
za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.
Wadudu waharibifu.
Kuna aina tatu (3) za wadudu wanao haribu zao
hili:
1.Viroboto wa
vitunguu.
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la
vitunguu hapa nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno. Wadudu
hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.
Dalili za kugundua.
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa
na mabaka meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka
kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani hunyauka kabisa.
Kuzuia.
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile
thiodan-35, Parathion nk. Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa
vitunguu mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako liwe
limekomaa.
Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo
kuwa na mazao aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k. Wadudu
wengine waharibifu wa vitunguu ni funza anayekata miche na minyoo ya mizizi. Hawa
hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao bustanini.
2. Chawa wekundu.
(Thrips)
Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa
wekundu. (Thrips) ambao wanashambulia majani, Uharibifu uletwao na wadudu chawa,
unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha
mlipuko wa wadudu.
Wanashambulia majani kwa kukwarua kwarua na
kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya
fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
·
Kuweka shamba katika
hali ya usafi
·
Kuondoa magugu
shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
·
Kupulizia dawa ya
wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
3. Sota (cutworms)
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha
uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota
wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye
ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
unapunguza sana idadi ya mimea shambani na
kuleta upungufu wa mazao.
Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa
kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya
usafi.
SOMA; Kilimo Bora Cha Pilipili Hoho Na Faida Zake.
4. Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha
upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji kwenye majani na
kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea
unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Njia ya kudhibiti:-
·
Kupulizia dawa za
wadudu Karate na Selecron.
·
Kuteketeza masalia ya
mazao
·
Kutumia mzunguko wa
mazao
5. Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake
wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao
wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Njia ya dhibiti:
·
Kupulizia dawa ya wadudu
kama karate Selecron na Dursban
·
Kuteketeza masalia ya
mazao
·
Kutumia mzunguko wa
mazao
Magugu.
Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo
miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu
zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya dawa za magugu ni
madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
(Goal 2E).
Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua
magugu aina mbalimbali. Dawa Inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya
kupandikizwa miche shambani. Palizi baada ya kutumia dawa ya magugu ni muhimu
ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu. Wakati wa palizi, vitunguu
na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze mizizi au
kubabua vitunguu.
Magonjwa ya vitunguu.
a) Ukungu
mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi
iliyo ambatana na unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua
Ugonjwa huu
·
Utaona unga wa rangi
ya zambarau katika majani.
·
Majani hugeuka rangi
na kuwa njano na baadaye kunyauka.
·
Ugonjwa huu hupenya
hadi chini kwenye tunguu na kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia
·
Inashauriwa kubadili
aina ya zao katika shamba lako kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya
vitunguu. Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao upangwe kiasi kwamba
vitunguu visipandwe eneo moja mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa
mwingi.
·
Tumia dawa za kuzuia
ukungu. Hii ifanyike kabla ya kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga
dawa kama vile maneb, Dithane M45, zineb ya unga, n.k. Wakati unapoona hali ya
hewa inayo wezesha kuenea kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na
unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya siku
sita ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea
hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.
b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa
wakati vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.
Dalili
zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na
baadaye hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza
vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko katika jani zima au shina la
kitunguu. Baada ya wiki kama tatu hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani
yote huanguka na kukauka. Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna
kwa kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.
SOMA; Badili Maisha Yako Kwa
Kuwekeza Kwenye Kilimo Hiki Cha Vitunguu Saumu.
Namna ya kuzuia
Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za ugonjwa
huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili kuzuia au kupunguza kuenea kwa
ugonjwa.
·
Kwa kinga ya bustani,
piga dawa za Dithane M 45 na dawa zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa
hizi zitasaidia kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.
·
Tumia kilimo cha
kuzungusha au kubadilisha mazao katika eneo la bustani yako. Usipande mfululizo
jamii yoyote ya vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.
·
Wakati wa kuvuna,
epuka kukata au kusababisha vidonda katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea
na siyo kwa kuchimba na jembe.
·
Baada ya kuvuna anika
vitunguu juani kwa siku moja au mbili kabla ya kuviweka katika magunia au
ghala.
c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na
unasababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi
na kuwa njano na baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi
hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi ya njano na kisha shina au
mche mzima hunyauka.
Kuzuia
·
Tumia kilimo cha
kuzungusha mazao badala ya kupanda vitunguu katika eneo moja toka msimu moja
hadi mwingine.
·
Panda aina za vitunguu
zinazo vumilia ugonjwa huu kwa mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red
creole.
Kumbuka tumejifunza kuanzia utayarishaji wa
shamba na aina za mashamba, pili tukaangalia aina za mbegu na jinsi ya kuchagua
mbegu bora yenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa, pia tukalenga kwenye
maeneo na hali ya hewa, tukaangaza na katika Magonjwa yanayoweza kuathiri zao
la kitunguu pamoja na kudhibiti wake.
Tunakutakia kila la kheri katika kilimo bora
na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kujifunza zaidi.
Makala
hii imeandikwa na mtaalamu wa masuala ya
kilimo na ufugaji ndugu Mosses Shio Wa TANaGRI.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.