Aug 24, 2015
Jinsi Unavyoweza Kushinda Tatizo Ulilonalo Na Kuishi Maisha Ya Ushindi Na Furaha.
Kila mmoja wetu katika maisha yake huwa
anakabiliana na matatizo ya aina fulani, ambayo katika hali ya kawaida huwa
siyo rahisi kuyakwepa. Matatizo haya mara nyingi huwa yanajitokeza katika
biashara zetu, familia na wakati mwingine ni matatizo ya mtu binafsi ambayo
huwa nayo. Wakati mwingine matatizo haya, huwa yanaonekana ni makubwa sana
kwetu kama mlima kiasi kwamba tunaanza kufikiri tunashindwa kuyamudu.
Kutokana na matatizo haya wapo ambao hufikiri na
kujiona wanamkosi na wapo ambao hufikiri kuwa wamerithi kwa namna fulani
matatizo. Kila mtu huja na mtazamo wake kutokana na matatizo yanayomkabili.
Kitu wasichokijua kumbe ndani yao wanauwezo mkubwa wa kushinda matatizo waliyonayo
na kuishi kwa ushindi ili mradi tu waitambue siri hiyo na kuweza kuitumia
vizuri.
Katika makala hii utajifunza njia, mbinu na
mikakati ya kukusaidia kushinda tatizo ulilonalo na kuishi maisha ya ushindi.
Utatambua jinsi unavyoweza kuhamasika na kujiamini wewe mwenyewe binafsi kuwa
unaweza kutatua tatizo lako na kufanikiwa kusonga mbele bila shida yoyote.
Ieleweke kuwa kila tatizo ndani yake huwa lina njia ya kulitatua hata liwe
kubwa vipi.
Inaweza isiwe rahisi sana kwako kunielewa lakini, kwa
vyovyote vile iwavyo kama una tatizo linalokukabili huo si mwisho wa kufanikiwa
kwako. Bali ni dalili tosha ya kukupeleka kwenye mafanikio unayoyataka. Unaweza
ukajiuliza kwa nini hiyo iko hivyo? Ni kwa sababu matatizo yanakuwa yanakupa
ukomavu ambao hukuwa nao hapo mwanzo ikiwa utajifunza kupitia matatizo hayo.
Unawezaje kushinda matatizo uliyonayo na kuishi
maisha ya furaha na ushindi?
1.
Amini inawezekana kulitatua tatizo ulilonalo.
Siku zote ushindi wa mambo yote huwa unaanzia
kwenye kuamini. Kuamini ndiyo nguzo kuu ya mafanikio. Unapokuwa na imani inakusaidia
kuweza kutatua tatizo ulilonalo hata liwe kubwa vipi. Kitendo cha kuwa na imani
kinakupa ujasiri wa kukabiliana na tatizo lako bila woga. Watu wenye imani
kubwa mara nyingi huwa ni washindi katika mambo yao.
Hata ukiangalia dini nyingi duniani msingi wake
mkubwa umejikita kwenye imani. Watu mbalimbali waliopata matatizo kipindi hicho
walitumia imani kama nguzo kuu na kuamini kuwa wanaweza kufanikiwa kutoka
katika matatizo waliyonayo na ni kweli waliweza kutoka. Hivyo ili uweze kutoka
katika tatizo ulinalo ni muhimu kuwa na imani ya kukusaidia kutoka hapo.
2. Lijue
tatizo lako vizuri.
Kuamini tu peke yake hakutoshi, ili kuweza kutoka
kwenye tatizo ulinalo ni muhimu pia kulijua tatizo lako vizuri. Kwa nini
ninasema ni muhimu kulijua tatizo lako? Unapolijua tatizo lako hiyo inakusaidia
kuweza kulikabili vizuri bila woga na
hatimaye kulishinda. Kama tatizo lako hulijui vizuri itakuwa ngumu kulishinda.
Hata unapokwenda kwa daktari kwa ajili ya kutibiwa pamoja
na kuwa unajua kuwa unaumwa na umemweleza daktari kuwa pengine kichwa kinauma,
lakini daktari huyu atalazimika kukupima kabla ya kukupa dawa. Anachofanya daktari
hapa, nikuhakikisha anajua tatizo lako vizuri kabla hajakupa dawa ambazo hazihusiki.
Ili utoke kwenye tatizo ulinalo ni muhimu ulijue vizuri ili upate njia sahihi
za kulikabili.
3.
Acha kuchanganyikiwa na tatizo lako.
Hata kama ikitokea tatizo lako limekuwa kubwa kiasi
gani gani kitu cha msingi acha kuchanganyikiwa na tatizo lako. Unaweza ukasema ‘aah hili haliwezekani’, lakini ninachotaka kukwambia inawezekana. Unapokuwa unakuja
juu ama unajihisi kuchanganyikiwa mara nyingi kinachokutokea unakuwa hauna
uwezo wa kulikabili hilo tatizo na badala yake unalikuza.
Watu wengi huwa wanashindwa kukabili vizuri matatizo
yao kutokana na kuhisi kuchanganyikiwa. Linapotokea tatizo kaa chini kwanza
tulia kwa muda kisha tambua njia sahihi ya kulikabili. Mara nyingi huwa
linaonekana kubwa ni kutokana na jinsi tunavyolipokea. Tuchukulie kweli hata
kama ni kubwa hata ukija juu kiasi gani au uhisi kuchanganyikiwa utafanyaje?
ndio limeshatokea. Kitu cha msingi tuliza kwanza sana akili yako unapopata
tatizo, ili upate njia sahihi za kulitatua.
4. Acha
kufikiria sana juu ya tatizo hilo.
Usipoteze muda sana kufikiria juu ya tatizo lako. Si
maanishi hapo unakuwa unalipuuza hapana, ila badala ya kulifikiria tatizo hilo sana
weka nguvu zako nyingi katika kulitatua tatizo hilo na kulishinda. Kama utaendelea
kulifikiria tatizo hilo kwa muda mrefu usishangae kama itatokea hutapata
suluhisho la kulitatua.
Weka nguvu nyingi chanya katika kutatua tatizo lako.
Ikitokea umeshindwa kwa namna moja au nyingine tafuta msaada wa kukusaidia
kutoka kwenye tatizo hilo na acha kung’ang’ania kulifikiria. Inawezekana tatizo
linalokusumbua linaweza lisiwe kubwa sana kama unavyolifikiria, zaidi
unajiumiza bure kwa kulifikiria sana.
5.
Acha kuzungumzia kushindwa.
Inaweza ikawa inaonekana kweli upo katika hali
ngumu ambayo inapelekea kushindwa hiyo ni sawa, lakini acha kuzungumia juu ya
kushindwa kwenye tatizo lako. Kwa kadri unavyokuwa unazungumzia kushindwa
ndivyo ambavyo unakuwa unakosa ujasiri wa kukabiliana na tatizo ulinalo na
mwisho wa siku unajikuta unashindwa kabisa kulitatua.
Kumbuka tatizo lolote ulinalo unaweza kukabiliana
nalo. Haijalishi ukubwa uliopo kwenye hilo tatizo, kwa vyovyote vile iwavyo mwisho
wake upo. Jipe moyo inawezekana na hakuna marefu yasiyo ya ncha, kama ni hivyo
na tatizo lako litaisha hivyohivyo bila wasiwasi.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia
mafanikio makubwa. Karibu sana kwenye mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO
kujifunza na kuhamasika kila siku na endelea kuwashirikisha wengine kuweza
kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048 035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.