Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, August 20, 2015

HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUKABILIANA NA WATU WABAYA KATIKA MAISHA YAKO.

No comments :
Katika maisha yako kwa vyovyote vile huwezi kukosa watu ambao ni lazima wakuone wewe ni mbaya wao, hufai, huna maana wala lolote na pengine wanaokupinga kwa mambo mengi ambayo unayafanya hata kama yana msaada kwao. Unapokutana na watu hawa ambao kwako ni lazima wanakuwa wanakuumiza kwa namna moja au nyingine huwa unajisikiaje?
Inawezekana ukawa unajisikia vibaya sana kiasi cha kutaka kupambana nao, lakini ukija kuangalia hiyo kwako haikusaidii sana. Kitu cha kutambua ni kwamba hawa ndiyo watu wabaya kwako ambao huwezi kuwakwepa, lakini unao. Kama ni hivyo unawezaje kukabiliana na watu hawa ambapo wakati mwingine wanaweza kuwa ni jamaa zako wa karibu?
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukabiliana Na Watu Wabaya Katika Maisha Yako.
1. Weka mikakati ya kuongea nao.
Badala ya kuwapa nafasi ya kukuongelea wewe tu, fanya mpango wa kuweza kuongea nao. Usifanye kosa la kuwakimbia au kuwaongelea na wewe pembeni. Ukifanikiwa kuongea, hiyo itakusaidia kuweza kulewana nao vizuri kwa kujua nini hasa tatizo na kulitafutia majibu yanayotakiwa. Na huo ndiyo unaweza ukawa mwisho wa kukuongelea wewe tena vibaya katika maisha yako.

2. Tafuta marafiki chanya.
Inaweza kabisa kwako ikawa ngumu kuongea nao na kila kitu unaona kama kimeshindikana. Lakini kitu muhimu cha kufanya hapa fanya mpango wa kutafuta marafiki wengine chanya ambao utakuwa nao. Marafiki hawa watakusaidia kuona mambo kwa mtazamo chanya na  kukusahaulisha na wabaya wako ambao pengine wanakuumiza moyo.
3. Tafuta msaada zaidi.
Ni vizuri ukatafuta msaada wa kuweza kukusaidia kupata kile unachohitaji na ukaacha kulaumu kwa nini watu hao wanakusema vibaya. Tafuta ushauri kwa mtu makini ambaye anaweza kukupa ushauri mzuri wa namna gani utakavyokabiliana na wabaya wako. Kwa kubadilishana mawazo na mwingine inaweza kuwa kukupa majibu ya upesi ni nini kifanyike.
4. Acha kusikiliza sana maneno hayo.
Kama unaamini unasemwa kwa tabia ambayo kwako wewe uaona ni sahihi, endelea na tabia yako hiyo bila kusikiliza kitu chochote. Funga masikio na songa mbele kwa kile unachoona ni msaada kwako. Ukisikiliza kila kitu utajikuta ukiumia sana na mwisho hutafanya kitu chochote cha kuweza kukabiliana na tatizo lako la kukabiliana na wabaya wako.
5. Achana nao.
Inaweza ikawa ni uamuzi mgumu kwako, lakini kama mambo yote yameshindikana hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuachana nao. Haina haja ya kushikiria kitu ambacho kinakutesa. Kwa vyovyote vile watu hao hawana msaada kwako ni vyema ukafanya uamuzi mgumu wa kuwatoa kwenye ubongo wako na kuendelea na mambo mengine, vinginevyo utaumiza kichwa kufikiria mambo ambayo huna uwezo nayo.
Zipo namna nyingi ambazo unaweza ukakabiliana na watu wabaya maishani mwako, hizo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kuzitumia kulifanikisha hilo.
Kwa makala nyingine nzuri zaidi endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza kila siku na kuboresha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,No comments :

Post a Comment