google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Dec 15, 2016

Ifahamu Nguvu Ya Kufikiri Na Kushukuru Katika Maisha.

No comments :
Katika vitu ambavyo wanadamu tumekuwa hatuvitilii maanani ni vitu vikubwa viwili, vitu hivyo ni kufikiri na kushukuru. Nimesema hivyo nikiwa na ushahidi tosha kwa kile ambacho nakiamini, na pia ni sahihi kwa asilimia zote ambazo unazifahamu wewe.

Unashangaa kwanini nasema kwa kujiamini? Wala usishangae bali tuendelee kusonga mbele mwanzo mpaka mwisho wa makala haya ili tuweze kwenda sawa.

Ukweli ambao upo wazi ambao hauhitaji hata mwanga wa jua ili kuonekana kwa watu wake upo bayana kabisa, ni kwamba tumekuwa tukilalamika kwa kutoa sauti au hata kutotoa sauti ya kwamba maisha ni magumu.

Yote hiyo inaweza ikawa hivyo kwa sababu watu tumeshindwa kuwekeza muda wetu katika suala zima la kufikiri, huenda nikawa nimekuacha ila nataka tusemezane bila kuoneana haya. 

Ipo sababu kubwa leo kuweza kutenga muda kwa kila siku angalau masaa mawili kwa ajili ya kufikiri, si kufikiri tu bali kufikiri vitu vipya.


Kama unafanya biashara, kilimo au kitu chochote ni vyema ukatenga angalau masaa hayo mawili kwa ajili ya "kuwaza". Kufanya hivyo kutakufanya uweze kuwa bora hatimaye kuonesha utofauti na wengine.

Ifahamu Nguvu Ya Kufikiri Na Kushukuru Katika Maisha.
Itumie nguvu a kufikiri vizuri ikusaidie kufanikiwa.
Hakuna maisha bora kama utaamua kufanya kitu kile kile, kila wakati kwa njia ambazo umezizoea. Fanya kitu cha tofauti kwa kuwa wewe ni wa tofauti.

Na kama ilivyo kauli mbiu ya mtandao huu ni kwamba badili maisha yako kwa kuwa na fikra sahihi, hivyo fikiri sana kwani fikra chanya huleta mabadiliko ya kweli hakuna jambo lolote litafanikiwa kama litakuwa katika mtazamo hasi.

Lakini tukija katika upande wa pili ni kwamba katika vitu ambavyo havipo katika tamaduni zetu ni jambo zima la kutoa "Shukrani" kutoa shukrani ni jambo la faraja sana mbele za Mungu na mwanadamu ambaye amekusaidia wewe kwa namna moja ama nyingine kuweza kufika hapo ulipo.

Elewa na tambua ya kwamba usingefika hapo ulipo kama ungesimama peke yako. Mbele ya Mafanikio yako kuna mtu nyuma yake. Swali la kujiuliza ni shukrani gani ambazo umezitoa kwa mtu huyo?


Ukifikiri kwa umakini utagundua ya kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye umewahi kutoa shukrani kwake, hii ni kwa sababu shukrani zetu ni za mara moja kama mla ndizi.

Naendelea kujihoji pasipo kupata majibu ni maisha gani hayo ambayo umeyachagua? Kwanini uishi maisha hayo yasiyokuwa na faida na chukizo mbele za Mungu?

Unafikiri ya kwamba ukitoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu na mtu ambaye amekusaidia kuwa hapo utapungua uzito au utafirisika? La 
hasha binafsi naona kama ukiweka utaratibu wa kushukuru itakusaidia kuweza kufanikiwa zaidi. 

Huenda ninachokisema leo kikagusa moja kwa moja. Utajiuliza labda leo Afisa mipango kaamuka na mimi, la hasha kwa kuwa mawazo yangu hayana ukomo wa kuwaza wacha niseme tu, huenda yakagusa kwa namna moja ama nyingine na yakakusaidia.


Nguvu ya kushukuru huongeza baraka za kimafanikio kila wakati, haiwezekani wewe ukawa ni mtu kuomba tu kuliko kushukuru, kufanya hivyo ni sawa na bure hata vitabu vya dini havijakaa mbali nasi kwani vinatukumbusha ya kwamba "kila ajuaye kuomba lazima ajue na kushukuru".

Hivyo jiwekee utaratibu wa kufikiri na kushukuru ili uweze kupata amani ya moyo hatimaye kufikia ile ndoto kubwa uliyonayo. Kama umenielewa vizuri baada ya kumaliza kusoma makala hii chukua dakika chache kuwashukuru wote ambao wamekusaidia kufika hapo ulipo.

Lakini ikumbukwe kumshukuru mtu ni lazima umwambie mtu huyo. Pia utakuwa mchoyo wa fadhira kama utashindwa kujishukuru mwenyewe. Endapo nimekukwaza utanisamehe sana kwani wajibu wangu kukueleza ukweli kila nipatapo nafasi.

Ndimi :Afisa Mipango Benson Chonya,



No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.