Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, May 30, 2017

Fanyia Kazi Mambo Haya, Ili Kuendelea Kujenga Msingi Mkubwa Wa Mafanikio Yako.

No comments :
1. Zipo kelele nyingi sana katika dunia hii ya habari. Utasikia hiki mara utasikia kile. Usipokuwa makini utajikuta kila kitu unataka kufatilia. Sasa njia ya kuweza kujiokoa na kelele hizo na kuweza kufanikisha malengo yako ni kwa wewe kuweka nguvu zako za uzingativu kwa kile unachokifanya.
Angalia kipi unakifanya, kisha kifatilie kitu hicho kila siku. Kelele za huku mara kule acha kuzifatilia zitakupoteza. Kumbuka, mikwenzi mingi ilimpoteza mbwa mawindoni, usiwe miongoni mwa watu watakao potea kwa sababu ya kelele. Simamia na fatilia mipango yako kwa kuweka nguvu za uzingativu kwa kile ukifanyacho na utafanikiwa.
2. Maisha na mafanikio ya kweli yanakuja kwa wewe kuweka thamani na kutoa mchango mkubwa kwa wengine. Mafanikio hayaji kwa bahati nasibu au chochote kile ambacho kipo kwenye njia ya mkato. Mafanikio ya kweli yanatengenezwa sana na kwa wewe kuendelea kuweka thamani na kutoa michango kwa wengine.
3. Kila wakati tafuta mafanikio yako kwa kufanya kile unachokipenda. Unapofanya kile unachokipenda utake usitake ni lazima utajituma tu bila hata kusukumwa. Kupenda kile unachokifanya, kazi kwako itakuwa ni kama mchezo na kwa kifupi ni rahisi tu kuwa mlevi wa kazi yaani ‘workaholic’ hasa kama unafanya kile unachokipenda.
Mara nyingi unapoona watu wanasukumwa sana katika kazi zao, na ni watu ambao kama hawajitumi ni rahisi kujua watu hao wanafanya kazi ambazo hawazipendi na wala hazipo kwenye mioyo yao. Wanafanya ili mradi siku ziende. Timiza mipango uliyojiwekea, kwa kuchagua kile unachokipenda kwenye maisha yako na kifanye.

4. Wakati tukiwa vijana wadogo wengi wetu tulikuwa na ndoto nzuri sana kwamba nikikua nitafanya hiki au kile na ilikuwa rahisi kuweza kuona kama vile kila kitu kinawezekana na wala hakuna changamoto kubwa sana.
Lakini kwa kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda zile ndoto zetu zilianza kupotea hasa baada ya kukumbana na changamoto za kimaisha za hapa na pale. Kitu cha kujiuliza kwako kwa mfano je, ile ndoto yako ya utotoni unayo au imepotea?
Kwa vyovyote vile ilivyo ndoto yako ipo ila kikubwa ulichokifanya umeizika ndoto yako bila kujua.Umeshindwa kufanya namna nzuri ya kuweza kuifufua ndoto yako na kuiweka wazi hadi iweze kufanikiwa.
Sasa  jiulize hivi kama huna mpango na ndoto yako ambayo ulikuwa unapienda, kwa sasa unaishi maisha a aiana gani? Ni rahisi kukwama katika maisha na kupata ugumu fulani kama hufuati ndoto yako na hufanyi kile kitu unachokipenda maishani.
Kuanzia  sasa jipe muda wa kufikiri tena na anza kufatilia ndoto yako ile ambayo ulikuwa umeisahau. Kaa chini ujiulize una ndoto ipi ambayo unatakiwa kuifailia? Kisha anza kuifatilia ndoto yako na itakuwa kweli.
5. Kuna wakati tunajiambia sana ‘mwaka huu nahitaji kuongeza mtaji, mwaka huu nahitaji pia kufanya biashara ile, au mwaka huu nahitaji kufanya hiki au kile’. Hizi ni sentensi ambazo naamini umezisikia sana zikisemwa na kuna kipindi hata wewe umekuwa ukijisemea hivyo.
Katika ulimwengu wa mafanikio ipo hivi kile kinachokufanikisha si kile unachokihitaji, bali kile kinachokufanikisha ni kile unachokifanya au kukifanyia kazi, ndicho hicho kinachokufanikisha na kukupa mafanikio.
Hakuna atakayejali kwa kile unachohitaji au unakisema sana hata kiwe kizuri vipi, dunia inajali kile unachokichukulia hatua na kukifanya. Hicho unachokifanya kila siku, hicho ndicho kinachokusogeza kwenye mafanikio yako.
Unaweza ukahitaji mambo mengi sana lakini kama huchukui hatua uwe na uhakika huwezi kufanikisha kitu chochote katka maisha yako, zaidi yako utaishia kusema nahitaji hiki au kile na miaka inaenda na bado ukajikuta hupati kitu.
Kuna watu ambao ukiwachunguza karibu maisha yao yote ni watu wa kusema nitafanya hiki mwaka huu au kile na hawafanyi. Maisha ya mafanikio hayataki ‘blaa blaa’ yanataka ufanye kitu yaani uchukue hatua za kimafanikio.
Kumbuka unachokihitaji hakiwezi kukupa mafanikio unayoyataka kwa asilimia zote, acha kulinga na kujidai kwa kile tu unachokihitaji, badala yake uelewe kabisa kile unachokifanya hicho ndicho kitakachokupa maisha na mafanikio unayotaka.
6. Kipimo cha mafanikio yako  kipo kwako wewe mwenyewe na wala hakipo kwa mtu mwingine. Njia pekee itakayokufanya uweze kupima mafanikio yako ni kwa kwewe kuangalia hatua unazozipiga kulekea kwenye mafanikio hayo.
Mafanikio yako hayapimwi kwa kuangalia mafanikio ya mtu mwingine. Bali mafanikio yako yanakuja kwa sababu ya zile hatua zako mwenyewe unazotakiwa uzipige kila siku kuelekea kwenye mafanikio.
Unawezaje sasa kujua kama umefanikiwa ikiwa hujilinganisha sana na wengine? Hilo ni rahisi tu, ni kwa wewe kuangalia ni hatua gani umepiga ukijilinganisha na mwaka jana au wakati uliopita.
Kumbuka kila siku hili, chukua hatua kila siku za kuelekea kwenye kile unachokifanya. Usijali wala usiangalie ikiwa unachukua hatua kidogo, kitu cha msingi chukua hatua kwani hicho ni kipimo cha mafanikio yako.
7. Kuna wakati tunakutana na ugumu sana katika kufanya vile tunavyotaka kuvifanya. Kutokana na ugumu huo na kuna wakati huweza kujikuta hata tukitaka kuahirisha kufanya mambo yetu. Kwa hali yoyote unayokutana nayo hata kama ni ngumu vipi, hebu hicho unachotaka kukifanya kifanye.
Usiahirishe mambo yako kwa sababu ya ugumu, fanya hivyo hivyo, ‘just do it,’. Weka visingizio pembeni, usiwe kama mtoto mdogo ambaye kila kitu anasingizia. Tengeneza ukomavu wa kiakili kwa kuamua kufanya hata kama ipo shida na ugumu vipi wewe fanya kwa kusukuma na utaona mafanikio yakijitokeza kwako.
Nakutakia siku njema na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,

No comments :

Post a Comment