Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, May 18, 2017

Kile Kinachokufanikisha Sio Kile Unachokisema Sana, Bali Ni Hiki Hapa…

No comments :
Kuna wakati tunajiambia sana ‘mwaka huu nahitaji kuongeza mtaji, mwaka huu nahitaji pia kufanya biashara ile, au mwaka huu nahitaji kufanya hiki au kile’. Hizi ni sentensi ambazo naamini umezisikia sana zikisemwa na kuna kipindi hata wewe umekuwa ukijisemea hivyo.
Katika ulimwengu wa mafanikio ipo hivi kile kinachokufanikisha si kile unachokihitaji, bali kile kinachokufanikisha ni kile unachokifanya au kukifanyia kazi, ndicho hicho kinachokufanikisha na kukupa mafanikio.
Hakuna atakayejali kwa kile unachohitaji au unakisema sana hata kiwe kizuri vipi, dunia inajali kile unachokichukulia hatua na kukifanya. Hicho unachokifanya kila siku, hicho ndicho kinachokusogeza kwenye mafanikio yako.

Weka mipango yako katika vitendo.
Unaweza ukahitaji mambo mengi sana lakini kama huchukui hatua uwe na uhakika huwezi kufanikisha kitu chochote katika maisha yako, zaidi yako utaishia kusema nahitaji hiki au kile na miaka inaenda na bado ukajikuta hupati kitu.
Kuna watu ambao ukiwachunguza karibu maisha yao yote ni watu wa kusema nitafanya hiki mwaka huu au kile na hawafanyi. Maisha ya mafanikio hayataki ‘blaa blaa’ yanataka ufanye kitu yaani uchukue hatua za kimafanikio.
Kuanzia leo unatakiwa ujifunze na kutambua kwamba vitendo ndivyo vinavyosema kuliko maneno. Kama ni kusema kila mtu anaweza kusema na kuweka ndoto zake vizuri mpaka ukashindwa kuweza kuamini kama kweli anaweza akashindwa.
Lakini kinachokuja kuweza kutofautisha kati ya wale wanaoshindwa na wale wanaofanikiwa ni namna ya kuchukua hatua za kuelekea kwenye mafanikio. Kwa chochote ambacho unaamua kukifanya, chukua hatua.
Katika kuchukua hatua usijali, hatua hizo ziwe ni kidogo au unaona kama hausogei, kikubwa ni ile hali ya kwenda mbele. Hivi ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa na hivi ndivyo pia kile kinachokufanikisha jinsi kinavyokuja.
Kumbuka unachokihitaji hakiwezi kukupa mafanikio unayoyataka kwa asilimia zote, acha kulinga na kujidai kwa kile tu unachokihitaji, badala yake uelewe kabisa kile unachokifanya hicho ndicho kitakachokupa maisha na mafanikio unayotaka.
Je, unakipi unachokihitaji leo? Chukua hatua sasa kwa kukifanya.
Nakutakia siku njema na kila la kheri katika kuyafikia mafanikio yako makubwa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0628 92 98 16,

No comments :

Post a Comment