Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, May 19, 2017

Jifunze Kwanini Tunasema Hakuna Makosa Duniani.

No comments :
Mojawapo ya vitu ambavyo vinachukiwa sana na binadamu ni kitu kinachoitwa “makosa”. Jambo hili la makosa linaogopwa sana kutokana na ukweli kwamba, wengi wetu tumekulia na kulelewa katika mfumo ambao ni watu wachache kwa nafasi zao wanaamua na kushawishi juu ya nini kifanywe na wengine ambao ni wengi. 

Maana yake ni kwamba, watu wengi licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuamua juu la mustakabari wa maisha yao, bado wanaishi na kuendesha maisha yao kwa kufuata akili na maelekezo ya watu wengine ambao kimsingi ni wachache— siku hizi wanaitwa mabosi.

Mapokeo ya kitu kinachoitwa “makosa”, yanatokana na watu kuishi na kutegemea maelekezo ya watu wengine. Kila mara wengi wetu tunasubiri tupangiwe cha kufanya au tusikie wakubwa zetu wanataka tufanye nini. Matokeo yake watu wanaposhindwa kutekeleza majukumu waliyopangiwa, au wanaposhindwa kufuata maelekezo kama walivyopewa na wakubwa zao, moja kwa moja tunaambiwa tumefanya “makosa”.


Mifumo yetu ya kijamii imejengeka katika mazingira ambayo, kila mtu anataka akupe maelekezo yake moja kwa moja na uyafanyie kazi. Pia, kila aliyekuzunguka anapenda ufanye mambo yako kwa jinsi anavyopenda yeye, hata kama hicho unachofanya siyo cha kwake.

Hali hii kimsingi ndiyo imetujengea hisia kali juu ya kitu “makosa”. Kwa hiyo, wengi wanaona bora kukwepa kufanya makosa kuliko kujaribu kufanya vitu ambavyo vinakwenda kukuletea ukombozi na mafanikio katika Maisha.

Neno “makosa” ni la kawaida sana kama yalivyo maneno mengine;mfano: “mafanikio, juhudi, maarifa n.k. Makosa ni jambo ambalo linaonekana la tofauti kutokana na mazingira tuliyolelewa. Tangu ukiwa mdogo unafundishwa kutokufanya na ikiwezekana kuepuka makosa. Mara nyingi tendo la makosa tukiwa wadogo liliaambatana na adhabu au faini kali ikiwemo viboko.

Tukiwa shuleni, kitu cha kwanza tulichofundishwa ni kuogopa kufanya makosa. Leo hii, sisi kama watu wazima jamii yetu inatutegemea kuiongoza katika mapambano dhidi ya umaskini, lakini ukweli ni kwamba tuna utu uzima wa mwili tu basi! zaidi ya hapo tumejaa woga wa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha.

Kutokana na woga juu ya kitu “makosa” wengi wameshindwa kuishi Maisha ya kujiamini juu ya kile wanachokifanya. Kila wakitaka kufanya kitu fulani mara wanajawa na woga ambao unatokana na hulka ya kila wakati kukwepa kufanya makosa.

Ukweli ni kwamba hakuna makosa duniani, isipokuwa kuna masomo ambayo yanakusaidia wewe kuweza kukua na kuwa mtu wa hali na hadhi ya juu katika maisha. Ukiamua kukaa chini na kutafakari juu ya yale unayodhani yalikuwa ni makosa kuyafanya ni mengi. Lakini, pamoja ya kwamba ni mengi, bado utagundua kuwa kuna masomo ambayo ulijifunza kutokana na makosa hayo ambayo yamekuwa yakikusononesha kila kukicha.

Kutokana na kusononeshwa na yale unayodhani ni “makosa” umejikuta ukiwa siyo mtu mwenye furaha, na wakati mwingine umejikuta siku zako nyingi zinapotea bure. Makosa au shida zilizowahi kukupata hazina uhusiano na uwezo mkubwa ulionao ndani ya wewe. Kamwe usihusishe makosa ya zamani na uwezo wako. Kuna majibu sahihi ya changamoto zetu ambazo zinapatikana na kujulikana baada ya wewe kujaribu na kukosea

Kitu kinachoitwa “makosa” kinachochewa na ubinafsi, ambao ni hali ya watu wengi kujipendelea zaidi kuliko watu wengine. Ndiyo maana watu wengi wanaamini kwa dhati kwamba watu wanaoweza kufanya makosa ni wengine na siyo wao. Hapa utaona kila mara mtu akisababisha tatizo au kosa, wengi utafuta kila namna, ilimradi makosa yaonekane yamefanywa na mtu mwingine.

Katika ujasiriamali na biashara makosa ni kitu gani? 
Tunaweza kusema kwamba makosa ni ile tu hali ya kushindwa kufikia matarajio uliyokuwa nayo kabla ya kuchukua hatua. Katika kujaribu kufikia malengo na matarajio, kuna vitu vingi sana ambavyo havipo katika udhibiti wetu na hivyo kupelekea lolote kuweza kutokea kinyume na matarajio yako ya awali. Ukilifahamu hili, huwezi tena kushindwa kuwa na moyo wa kukubali makosa yaliyotokea chini ya mamlaka yako.

Kuna faida kubwa sana pale unapoamua kukubali makosa; kwanza unafungua akili yako kupokea somo jipya lililotokana na makosa. Pili, unapata fursa ya kufahamu ni kitu/mbinu gani ni ya mafanikio na ni ipi si ya mafanikio. Kwa maneno mengine ni kwamba kadiri unavyokosea mara nyingi ndivyo unazidi kugundua njia na mbinu ambazo hazifanyi kazi, na unapoamua kuanza tena, maana yake ni kwamba hutaweza kuzitumia tena, badala yake utabuni kitu kipya—chapa kazi usiogope! 

Kwahiyo, tangu sasa yachukulie makosa kama masomo ya kukuendeleza na kukuimarisha kiajira, kibiashara, kiujasiriamali, kimahusiano na kimaisha kwa ujumla. Hakikisha fikra juu ya makosa zisiwe kikwazo, wala kisingizio tena cha wewe kushindwa kufanya shughuli halali za kukuletea kipato kikubwa na mafanikio makubwa.

Natumaini kuwa kwa wewe kuweza kusoma Makala hii leo, kwa vyovyote vile, woga juu ya makosa umeanza kupungua. Endelea kujifunza kila mara kupitia mtandao wako wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku.


No comments :

Post a Comment