Sep 23, 2016
Fahamu Kwanini Kesho Si Rafiki Wa Mafanikio Yako.
Katika maisha yetu ya kila siku, neno "Kesho" linatumika
sana kama njia pekee ya kuahirisha mambo mengi, ambayo kimsingi yalitakiwa
yafanyike "leo" .
Kesho ni miongoni
mwa maneno yanayopendwa kutumiwa kama kinga ya kukataa kutimiza majukumu fulani
ya leo. Badala ya mtu Kusema "HAPANA" Kitu hiki, utakuta mtu
huyo anajibanza nyuma ya kesho, Huku akidhani Kuwa ataweza
kufanya au kutimiza majukumu ya leo siku ya Kesho.
Matokeo yake, kesho ikifika anasogeza
tena mbele kwa sababu kuna kesho nyingi mbele yake. Kwa maneno mengine ni
kwamba, tunahitaji kujiadhari sana na "kesho" kwani bila kufanya
hivyo, tutajikuta kwenye hali ya umaskini mkubwa sana bila kujua.
Ni Ukweli usiopingika kuwa neno baya
kuliko maneno mengine na linaloongoza kwa kuharibu maisha ya binadamu ni neno liitwalo "kesho".
Watu wengi hasa maskini, watu ambao
hawajafanikiwa, wasiokuwa na furaha, na wale wasiokuwa na afya njema ni kundi
la watu ambao upendelea sana kutumia neno " Kesho" .
Ndiyo maana watu wa namna hii, mara
nyingi hupendelea kusema maneno kama"nitaanza uwekezaji kesho au "
nitaanza kutumia lishe bora kesho " au nitaanza mazoezi
ya kupunguza uzito Kesho! Wengine husikika wakisema" nitaanza
kusoma labda kesho.
Anza siku yako leo, kama hakuna kesho. |
Ukichunguza kwa undani unagundua kuwa
neno "Kesho" linatumika sana kumaanisha kuwa jambo
fulani litaanza kufanyika siku ambayo siyo ya leo. Ndiyo maana utasikia
nitaanza hiki siku Ya kesho, wiki, mwezi, mwaka kesho au wakati ujao.
Kwanini
Watu hupendelea Kusema Kesho?
Sababu ni moja tu kwamba tunayo HULKA
ya kupenda kufanya Vitu vingi kwa mara moja na ambavyo haviko hata kwenye mpango
maalum.
Tunapenda sana kufanya kazi kwa
kufuata kasi ya matukio yanayoendelea kutokea. Kwahiyo, mambo au shughuli
za leo zinapozidi uwezo unaamua kuzipeleka siku ya kesho.
Kwa mfano unaweza kukuta kwamba kufika
saa sita mchana ya leo, Tayari umekwisha kuahirisha shughuli nyingi za leo na
kuzipeleka kesho. Lakini uzoefu unaonyesha kuwa unapoona kitu hujakifanya leo,
basi ujue siyo muhimu.
Kuhusu kitu gani muhimu ufanye leo,
hakiji hivi hivi, ni lazima shughuli zako nyingi za kila siku zifanyike kwa
kulenga ndoto yako ya maisha yaweza kuwa ni miaka mitano, kumi au na zaidi.
Bila kuwa na ndoto au maono juu ya maisha
unayotaka kuyaishi, Lazima utaendelea kufanya kazi zako nyingi kwa kufuata
matukio ya siku husika.
Mwisho wake kila utakapofanya
Tathmini ya miaka 5 au 10 iliyopita unajikuta umezidi kurudi nyuma, hapo ndipo
utaanza kutafuta wa kumlaumu. Kuchanganyikiwa kwa Watu Wengi ambako huambatana
na msongo mkubwa wa Mawazo, mara nyingi huja kwa njia hii.
Kwahiyo, ni muhimu sana kwetu
tunaotaka maisha huru ya mafanikio kutambua kuwa vitu vyote muhimu kwa maisha yetu
ni inatakiwa vinavyofanyika leo.
Maisha yako siyo kesho, wiki, mwezi,
mwaka au miaka kumi ijayo bali maisha halisi, ambayo una fursa ya kufanya kazi
itakayo kuletea mafanikio makubwa siku za mbeleni ni leo.
Ni muhimu tukafanya yale yote yaliyo
muhimu leo. Ukishatambua hilo, utakuwa wa kwanza kuona umuhimu wa kuianza
siku yako mapema Alfajiri.
Kushindwa katika maisha yako hakuji
siku moja bali ni matokeo ya kushindwa kidogo kidogo kila siku. Ukiona
umeshindwa au unakabiliwa na umaskini usifikiri ni jambo ambalo limetokea leo
bali ni kutokana Na wewe kuchezea yale masaa ya kuanzia unapoamka hadi
unapolala.
Kwa hiyo kwa maneno au lugha rahisi "LEO
Ndiyo Dili" kubwa ya kubadili maisha yako. Hii ikiwa na maana kwamba
tukifanya kazi sana leo tutapata ushindi au mafanikio kidogo na kesho tukifanya
kama au zaidi ya leo tutapata mafanikio Kidogo.
Yale mafanikio kidogo kidogo
tunayovuna kila siku ndiyo kwa ujumla wake yatatufanya kuwa na mafanikio makubwa
miaka 5 au 10 ijayo na hapo ndipo Wengi watakapoanza kukutambua kwamba na wewe
huwa upo!
Jitahidi kuipenda na kuikumbatia leo
na uachane kuwa na mpenzi wa kesho kwasababu, neno Hili linaharibu sana maisha
ya watu wengi kuliko maneno mengine.
Achana na neno "Kesho" kwasababu
haitatokea uione kesho. Kesho huwa haipo. Kesho huwa ipo tu kwenye
akili za watu waota ndoto bila vitendo na washindwaji.
Nimalizie kwa Kusema Kuwa sijawahi
kuiona "Kesho" Kitu tulichonacho Pekee ni "Leo". LEO
ni neno la washindi na Kesho ni neno la washindwa.
Endelea kujifunza kupitia
dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Makala hii imeandikwa na Cypridion Mushongi wa MAARIFA SHOP.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.