Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, September 27, 2016

Jinsi Ya Kupata Mafanikio Makubwa Kwa Kuboresha Mambo Haya Matatu.

No comments :
Kimsingi, mafanikio yoyote unayoyatafuta yanaongozwa na kanuni. Kanuni hizo ndizo huamua ufanikiwe au usifanikiwe kwa kiasi gani kulingana na jinsi unavyozitumia.
Bila kuzijua kanuni hizo na kuzifanyia kazi, ni kazi bure utahangaika sana kutafuta mafanikio na utaambulia patupu. Wengi wanaoingia kichwa kichwa kutafuta mafanikio bila kuzijua kanuni hizo, huwa si rahisi sana kufanikiwa.
Kama ambavyo umekuwa uijifunza mara kwa mara kupitia mtandao huu, zipo kanuni nyingi za mafanikio ambazo unatakiwa kuzitumia na kuziishi kila siku ili zikuletee manufaa makubwa kwako.
Moja ya kanuni hizo za mafanikio, ambayo leo kupitia makala haya nataka ujue ni kanuni ya kuboresha. Hii ni moja ya kanuni ambayo ni rahisi, ila itakupa mafanikio makubwa sana endapo utaamua kuifanya iwe sehemu ya maisha yako.
Kivipi? Ipo hivi. Kanuni hii inatueleza, kwa chochote unachokifanya, kadri siku zinavyokwenda lazima ukiboreshe na kuwa bora kuliko mwanzoni au ulivyokuwa ukianza. Ulazima wa kufanya hivyo upo kwa sababu ya mabadiliko yanayotokea kila siku.
Boresha mbinu na bidhaa zako, pesa utapata tu.
Na mabadiliko yanapotokea yakakuta hujaboresha mambo yako vizuri,  kwa vyovyote vile ni lazima utakwama. Hivyo ndio maana unatakiwa kuwa bora kila wakati.
Lakini hata hivyo ili kanuni hii iweze kufanya vizuri na kukupa matokeo ya haraka, yapo maeneo ya msingi amabayo unatakiwa kuyaboresha. Kwa kuboresha maeneo haya ni lazima ufanikiwe.
Hebu bila kupoteza muda, twende pamoja kuangalia maeneo ambayo unatakiwa kuyaboresgha ili kujitengenezea mafanikio makubwa maishani mwako.
Kwanza, boresha bidhaa zako. Kama wewe ni mzalishaji au muuzaji wa bidhaa za aina fulani, kitu cha kwanza ambacho unatakiwa kujua ni kuboresha hizo bidhaa zako kwa kiwango cha juu sana.
Hakuna mteja ambaye anapenda kuuziwa kitu ambacho si kizuri au ni feki. Hivyo ili umshawishi awe mteja wako wa kudumu katika kipindi hiki cha ushindani ni lazima ujifunze kwa kiasi kikubwa kuboresha bidhaa zako kwa viwango vya juu.
Hebu jaribu kuangalia kampuni nyingi kitu kikubwa ambacho zinafanya, utakuta karibu kila siku wanaboresha bidhaa zao. Kama ni kampuni ya usafirishaji, utawaona kila wakati wanajitahidi kama ni mabasi yao kuyafanya yawe bora zaidi.
Kila kitu chenye mafanikio makubwa katika hii dunia ili kifanikiwe ni lazima kwanza kiboreshwe. Bila kuboreshwa hakuna mafanikio ambayo yanaweza kupatikana ya maana.
Pili, boresha mbinu zako. Kama ilivyokuwa kwenye kuboresha bidhaa zako, pia unalazimika kutumia kanuni ya  kuboresha mbinu zako ili kupata kile unachokipata sasa kwa uhakika mkubwa.
Ili uweze kuboresha mbinu zako, kila wakati jaribu kuwa mbunifu na kujiuliza ni njia gani nyingine unaweza ukaitumia na ikakupa mafanikio makubwa. Ukishaipata njia hiyo itumie mara moja.
Kwa jinsi utakavyozidi kuwa mbunifu na kuwaza tena na kuwaza, namna ya kuboresha njia nyingine za mafanikio, ni uhakika mafanikio utaanza kuyaona bila tabu yoyote. Kikubwa boresha sana mbinu zako.
Tatu, chukua jukumu la kujiboresha wewe. Hakuna unachoweza kukibadili katika maisha yako, ikiwa kama wewe mwenyewe umegoma kuchukua hatua zitakazopelekea uwe bora katika maisha yako.
Oooh unajiuliza linawezekana vipi? Ni rahisi tu kwa kujifunza kwa wengine na kujisomea karibu kila siku, ndivyo unazidi kuwa bora na kupelekea mafanikio ya wazi kutokea kwenye maisha yako.
Kama kuna eneo unajiona ni mdhaifu au huwezi kwa namna moja au nyingine, lifanyie kazi eneo hilo mara moja. Kwa mfano, unataka kuwa mwimbaji bora, fanya mazoezi kila siku bila kuchoka.
Kumbuka, hakuna mafanikio ya kubahatisha hata siku moja. Kama unataka mafanikio ni rahisi tu, fuata kanuni za mafanikio kila siku na hakikisha unaboresha mbinu zako, unaboresha bidhaa zako bila kusahau ni lazima wewe ujiboreshe pia wakati wote.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili uweze kujifunza. Kujiunga tuma neno MAFANIKIO YANGU, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,


No comments :

Post a Comment