Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, September 26, 2016

Mambo Muhimu Ya Kuzingatia, Ili Kujenga Hamasa Ya Kudumu.

No comments :
Kuna wakati katika maisha unaweza ukajikuta una wazo la kufanya biashara au una wazo la kusoma kitabu au una wazo la kufanya kitu fulani kwa hamasa kubwa sana.
Lakini kitu cha kushangaza pale tu unapoanza kufanya jambo hilo, hamasa hiyo huanza kupungua kidogo kidogo na wakati mwingine hujikuta imeisha kabisa na wewe kujikuta huwezi tena kuendelea.
Wakati huo huo unakuwa unashangaa na kujiuliza sana, hamasa yote kubwa uliyokuwa nayo imekwenda wapi? Hapa kuna wakati unakuwa huelewi kabisa ni nini kilichopoteza hiyo hamasa?
Pia hata hivyo, unakuwa tena unashangaa kuwaona watu wengine wakifanya kitu hicho hicho, ambacho wewe umekishindwa. Tena unakuwa unajiuiza hamasa ya wao kufanya inatoka kwao wapi? Wakati wewe umeshindwa?
Kumbe, kitu usichokijua ni kwamba hamasa ni kitu ambacho huzaliwi nacho. Hakuna mtu ambaye anazaliwa akiwa na hamasa ya kufanya kila siku zaidi ya wewe kuamua kuitengeneza.
Inapofika mahali unajihisi kabisa umekosa hamasa, tambua kabisa ipo namna ambayo unaweza ukaiongeza hamasa hiyo. Lakini, kuongeza huko au kuchochea huko hamasa hakuji hivi hivi tu, mpaka uzingatie mambo muhimu ya kujenga hamasa.
Yafuatayo Ni Mambo Muhimu Ya Kuzingatia, Ili Kujenga Hamasa Ya Kudumu.
1. Anza kwa kidogo.
Kwa chochote kile unachotaka kukifanya hata kama unahamasa nacho kubwa vipi, anza kidogo. Hiyo itakusaidia kutokuta tamaa au kukupunguza hamasa, endapo itatokea umepata matokeo ya tofauti.
Kwa jinsi unavyoanza kwa kidogo inakuwa sio rahisi kwako, kukosa hamasa kwa urahisi. Inatokea hivyo kwa sababu kila siku unavyofanya kwa kidogo, unakuwa unajitengenezea nguvu ya mwendelezo wa kusonga mbele.

Tafuta sababu ya kufanya.
2. Fanya jambo hilo kwa sababu.
Chochote unachokifanya ili kikujengee hamasa ya kudumu ni lazima uwe na sababu ya kufanya. Kosa wanalofanya watu wengi, sababu zinakuwa sio nzito sana au hazijitoshelezi.
Je, unaweza ukajiuliza binafsi, hilo jambo unalolifanya sasa, ni sababu ipi inayokuongoza hadi ukalifanya? Je, ni kwa sababu ya pesa au kwa sababu unalipenda au kwa sababu unataka kusaidia jamii? 

Ukishajua sababu inakuwa sio rahisi kwako kukata tamaa, hata pale yanapotokea mazingira ya kukatisha tamaa.
3. Kuwa na maono.
Wakati wengi wetu hamasa inapungua kwa sababu ya kushindwa kuwa na maono maalumu ya kule tunakokwenda na kile tunachokifanya. Lakini ikiwa maono yako wazi, ni rahisi kudumisha hamasa yako wakati wote.
Jaribu kujiuliza kama hicho unachokifanya kitakupa faida kubwa sana na pesa nyingi huko unakokwenda, je unaweza ukakiacha kwa urahisi? Ukiwa na picha ya namna hiyo itakusaidia sana wakati wote kujijengea hamasa ya kudumu maishani mwako.
4. Tengeneza tabia ya mwendelezo.
Kuna siku  tunajikuta kweli tumechoka na hatuwezi kufanya lile jambo tunalolifanya na akili inakuwa inatuambia tulia, utafanya kesho. Ukikubali kuisikiliza hiyo sauti, utapotea.
Kuwa na tabia ya kukifanya kile unachokifanya kila siku hata kama ni kwa dakika kumi tu inatosha. Haijalishi umejisikia au haujisikii wewe fanya.  Tengeneza mwendelezo wa kufanya kila siku(Consintence). Ikiwa utafanya hata pale ambapo hujisikii kufanya ni lazima utajenga hamasa yako sana.
5. Tumia kushindwa kama chanzo cha hamasa kubwa.
Hata inapotokea pale unaona kama umeshindwa, tumia kushindwa huko kama sababu kubwa ya kuelekea kwenye mafanikio yako. hakuna mtu ambaye hashindwi kwenye safari ya mafanikio.
Achana na habari ya kulalamika pale unashindwa zaidi ya kujifunza. Ukishalijua hilo, jifunze sana kutokana na makosa yako na chukua hatua ya kuweza kuendelea mbele hatua kwa hatua.
Kwa kuzingatia mambo hayo machache, hivyo ndivyo unavyoweza ukajikuta umejenga hamasa ya kudumu wakati wote katika maisha yako.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili uweze kujifunza. Kujiunga tuma neno MAFANIKIO YANGU, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

No comments :

Post a Comment