Feb 17, 2017
Chimbuko La Umaskini Kwa Waajiriwa Wengi Ni Hili Hapa.
Umaskini ndani ya kundi la wasomi
unazidi kuingia kwa kasi ya ajabu kadili siku zinavyozidi kwenda. Kundi la watu
ambao wako kwenye hatari kubwa zaidi ni hasa wale walioko kwenye “ajira”. Ukweli
ni kwamba watu wengi walioko kwenye ajira, kitu pekee wanachouza ili kupata
kipato ni “nguvukazi” tena
ambayo bado ni “ghafi”.
Uzoefu unaotokana na tafiti
zilizofanywa, unathibitisha kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha waajiriwa
na hasa wasomi wengi kuwa maskini. Lakini kubwa zaidi ni utamaduni wa wasomi
kuendelea kuuza nguvukazi ikiwa bado ni “ghafi” (nguvukazi ambayo
haijachakatwa).
Katika ulimwengu wa “uwekezaji”
nguvu kazi ghafi ni mtaji muhimu sana, ambao ukichanganywa na mitaji mingine
kama vile mashine, una uwezo wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye thamani kubwa
kwa watu wengine.
Ukiuza nguvukazi ghafi unakuwa umeuza
“mtaji” wako: Waajiriwa wengi wanaendelea kukumbwa na adha kubwa ya
umasikini kutokana na kushindwa kutambua ukweli kwamba mara nyingi kwenye
maisha ya ajira wamekuwa wakifanya zaidi biashara ya kuuza mtaji walionao
(nguvukazi) kwa matajiri wenye hitaji la mitaji.
Ikumbukwe kuwa, ili uweze kuzalisha
bidhaa na huduma unahitaji mitaji ya aina mbalimbali ikiwemo nguvu kazi ghafi.
Ndiyo maana matajiri wengi wanapendelea zaidi kununua mitaji kwa ajili ya
kuzalisha bidhaa na huduma, ambazo huwapatia faida kubwa sana.
Katika biashara yoyote duniani, kuuza
mtaji ni kufirisika jumla. Kwahiyo, umasikini tulionao umetokana na
kuuza mtaji wetu kila siku tunapotumikia ajira zetu. Kwa maana nyingine
waajiriwa wengi wanafirisika kila siku ya pale wanapokwenda kazini.
Watu wanaouza zaidi nguvu kazi ghafi
wanabaki kuwa maskini kutokana na ukweli kwamba thamani ya nguvu kazi ghafi
huwa ni ndogo sana, kwasababu inapatikana kwa wingi na haina usumbufu kuipata.
Kwa mfano: ukijifanya
kutoza bei kubwa nguvu kazi yako; waajiri wengi watakukimbia na chapuchapu
watapata watu wengine wenye kuuza nguvu kazi ile ile kwa bei nafuu sana.
Hivi ndivyo unavyouza nguvu kazi ghafi: Unauza nguvu kazi
ghafi pale unapotumia nguvu yako kufanyakazi ya kuzalisha bidhaa na huduma
ambazo siyo mali yako bali ni mali ya mtu aliyekuajiri (mwajiri).
Unahitaji kufahamu kuwa, mwajiri
amekuajiri ili umpatie (umuuzie) nguvu kazi ambayo ni mtaji wa kuzalisha bidhaa
na huduma ambazo ni mali yake binafsi.
Kwakuwa bidhaa zinazozalishwa ni za
thamani kwa watu wengine, basi ni wazi kwamba watu hao watampatia pesa mwajiri
wako ili kupata bidhaa; LAKINI hawatakupatia pesa wewe, kwasababu wewe unayo
nguvu kazi peke yake, ambayo siyo hitaji muhimu kwa wateja wenye pesa
zao.
Ukiuza nguvukazi ghafi unauza “muda”
wako: Kwakuwa umeajiriwa kwa madhumuni ya kutoa nguvu kazi kwa
mwajiri wako, basi thamani yako inapimwa kwa kuangalia muda unaoutumia kufanya
kazi.
Ili uweze kulipwa ni lazima kila siku
ufike kazini na kusajiri muda wako. Usipoonekana kazini hakuna malipo yoyote,
kwasababu muda wako utakuwa hujauwekeza kwa mwajiri.
Kwahiyo, unapouza nguvu kazi ghafi
basi ujue umeuza “muda” na binadamu wa kawaida hawezi kufanya kazi zaidi ya
masaa nane kwa siku. Masaa yote haya unafanya kazi bila kupumzika na kuzalisha
vitu vyenye thamani kubwa kuliko mshahara unaolipwa na mwajiri wako.
Haijalishi, thamani ya vitu
vilivyozalishwa ni kubwa kiasi gani, mshahara wako unaolipwa unaendelea kubaki
pale pale kila mwezi. Hali hii ndiyo inakufanya wewe mwajiriwa kukosa muda wa
kufanya vitu vyenye kukuletea faida kubwa na mafanikio maishani, na hivyo
kuzidi kuwa maskini kadiri umri wako unavyoongezeka.
Ukiuza nguvukazi ghafi huna cha kurithisha
familia yako: Kama unauza nguvukazi ghafi siyo rahisi kuirithisha kwa
watu wako wa karibu, kwasababu nguvukazi kama ilivyo haihamishiki kutoka kwa
mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama kitu hakihamishiki ni vigumu pia
kukibadilisha kwa urahisi kuwa pesa.
Hali hii inazidi kutukumba wasomi na
waajiriwa waliowengi kutokana na ukweli kwamba unakuta umeajiriwa kwenye
kampuni kubwa na una cheo kikubwa lakini ukifukuzwa au kufariki, haitokei mke
au mtoto wako akapewa nafasi kama uliyokuwa nayo na wala familia haiwezi
kutumia vyeti vyako vya elimu kuomba kazi.
Lakini kama ungekuwa kwa mfano
umeandika vitabu, hata ukifa hakimiliki ya kuendelea kuvichapisha na kuviuza
inahamishiwa kwa warithi wako na wanaendelea kufaidi sawa na wewe ulivyokuwa
ukifaidi.
Ukiuza nguvukazi ghafi unapata hasara: Hasara kubwa
unayoipata kutokana na kuuza nguvu kazi ni pale unapoishia kuuza kitu kimoja
tu! Nacho ni nguvu kazi.
Hali hii inakubana kiasi kwamba
unajikuta unalazimika kumtegemea mteja mmoja ambaye ni “mwajiri” na
inakuwa siyo rahisi kubadilisha mteja kadiri unavyotaka.
Endapo ukiamua kuchakata nguvukazi
yako na hatimaye kuzalisha bidhaa na huduma za thamani ni rahisi kupata wateja
wengi, ambao ndio huleta mapato makubwa.
Hasara nyingine unayopata pindi
unapouza nguvu kazi ghafi ni kuendelea kubaki kwenye kundi la watu maskini
ambao wanapata kipato hai (active income), yaani unapata pesa unapofanya kazi
tu, ukiacha pesa hakuna. Endapo, ikitokea unaumwa au umesafiri basi ujue hakuna
pesa itakayoingia.
Ndiyo maana unakuta mtu ni tajiri leo
kwasababu anafanya kazi ya kibarua, lakini baada ya muda mfupi unakuta ni
maskini na kwa waajiriwa ni hivyo hivyo wanakuwa na pesa wakiwa bado kazini
LAKINI wanapostaafu ajira wanarudia kwenye hali ya umaskini jambo ambalo
huwafanya watu wengi kufa miaka michache baada ya kustaafu.
Washindi dhidi ya umaskini ni wale walioamua kuchakata nguvu kazi yao: Ukweli ni
kwamba kila mchakato wowote lazima utoe matokeo. Matokeo ya kuchakata nguvu kazi
ghafi ni “bidhaa au huduma” zenye thamani kubwa kwa watu wengine.
Kitendo cha kuchakata nguvu kazi
kinatokana na matumizi ya nguvu ya akiri pamoja na nguvu ya mwili kwenye
rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k, kwa lengo la kupata mali au
bidhaa kwaajili ya watu wengine.
Ukishapata bidhaa zenye thamani
(manufaa) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa ili kujipatia
bidhaa na huduma muhimu kutoka kwako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi na
zenye thamani kubwa ndivyo utakavyopata pesa nyingi ambayo haina kikomo.
Ni wakati sasa tuamke na tujibidishe
sana kwa kuandaa mazingira yatakayotuwezesha hasa sisi wataka mafanikio kuuza “matokeo”
ya nguvu kazi badala ya utamaduni wa sasa wa kuuza nguvu kazi ghafi.
Ukweli ni kwamba, unapokuwa mtu wa
kuuza matokeo ya nguvu kazi ambayo ni bidhaa na huduma mbalimbali, tayari
unakuwa umemaliza kazi, kinachofuatia ni kuendelea kuuza bidhaa hizo na wakati huo
huo unakwenda kuwekeza muda wako huo kwenye kuzalisha vitu vingine, huku
akiendelea kufaidi matunda ya kazi aliyoifanya mwanzo.
Kwa watu wote na hasa waajiriwa
tunaotaka mafanikio makubwa, ni lazima kila mmoja wetu ajiwekee tarehe ya
mwisho ya kuacha kuuza nguvu kazi ghafi.
Kila mmoja akifikia tarehe yake ya
mwisho kuuza nguvu kazi ghafi, mara moja aanze kujikita katika kubadili nguvu
ya akiri na hisia kuwa bidhaa na huduma zenye kuwa suruhisho la kudumu kwa
matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wengine.
Kwakuwa utazalisha bidhaa na huduma
zenye kuwa na manufaa makubwa kwa watu wengine, basi na wao watakupatia zawadi
ambayo ni pesa, ili kujipatia kila kilicho bora kutoka kwako. Tukiweza
kufanikisha azima hii, basi tutatajirika kutokana na ukweli kwamba watu wengi
kwasasa wanataka bidhaa na huduma ambazo ni suruhisho ya changamoto zao.
Wateja ni wengi ambao wako tayari
kununua kila kitu kitakachozalishwa ilimradi kina thamani kwao, kwa hiyo soko
ni kubwa. Nchi yetu inapokaribia kuingia uchumi wa kati, mahitaji ya bidhaa na
huduma zitokanazo na nguvu ya akiri/fikra zitazidi kuongezeka.
Bidhaa zenyewe ni kama vile muziki,
sanaa, vitabu, program za mafunzo ya ujasiriamali/biashara/afya/kilimo/majengo
pamoja na machapisho juu miongozo mbalimbali ya uwekezaji katika mambo ya
utalii, uwindaji, gasi, mafuta, madini, kilimo n.k.
Uchumi wa watanzania ukizidi
kuongezeka na idadi ya wasomi ambao ndio wahitaji wakubwa itazidi kuongezeka
huko tuendako ~ Kwa hiyo ewe mtanzania mwenzangu, anza kuchukua hatua leo,
wakati ni sasa.
Imeandikwa na Cypridion Mushongi wa MAARIFA SHOP.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.