Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, February 24, 2017

Linda Muda Na Mafanikio Yako Kwa Kusema HAPANA.

No comments :
Moja ya jambo muhimu unalotakiwa kulifanya ili kuweza kufanikiwa  ni kule kujenga uwezo wa kusema HAPANA hasa kwa mambo ambayo hayaendani kabisa na malengo ya maisha yako.
Wengi wetu mara nyingi ni watu wa kukubali karibu kila kitu katika maisha yetu, hasa pale tunapoambiwa na wengine kwamba tufanye kitu cha aina fulani. Huwa si watu wenye uwezo wa kusema hapana.
Kwa kawaida unaposhindwa kusema hapana kwa yale mambo ambayo hayaendani na malengo yako, unakuwa ni mtu kama ambaye unapoteza muda sana.
Sasa basi, kama usipoweza kusema hapana, ujue kabisa utapotezewa sana muda wako na watu wengi ambao watakuwa wanataka ufanye mambo yao. Hivyo, utake usitake hapa ndipo unalazimika kujifunza kusema HAPANA. 

Jifunze kusema hapana ujenge mafanikio yako.
Kila wakati linda muda na mafanikio yako kwa kusema HAPANA. Kama usipoweza kusema utapoteza muda wako na hata mafanikio yako kwa ujumla na hilo litakuwa halina ubishi.
Ili uweze kufanikiwa katika hili, zipo HAPANA kubwa za aina tatu ambazo unatakiwa uzijue na kuzizingatia  ili uweze kupata mafanikio.
Sema hapana kwako wewe mwenyewe.
Watu wasio na mafanikio ni wazito sana kusema hapana kwa mambo ambayo hayawasaidii. Angalia mambo unayoyafanya yanakusaidia kufanikiwa au la. Kama mambo hayo hayakusaidii kufanikiwa, sema hapana tena ya herefi kubwa.
Kwa mfano kama kuna jambo unataka kulifanya leo, halafu unajisikia uvivu uvivu unataka kulifanya kwa wakati mwingine, sema hapana nitafanya leo leo. Usikubali kitu chochote kikukwamishe katika hili, sema hapana.
Sema hapana kwa watu wengine.
Acha kuona aibu kama kuna jambo ambalo unaambiwa na huliwezi, sema hapana kwa jambo hilo. Jiulize ukimkubalia kila mtu kitu anachotaka kwako itakuwaje? Nafikiri utakuwa kama mtumwa wao.
Angalia hata matajiri wakubwa hawakubali kila kitu. Sema hapana kwa wengine pia. Mwanzo linaweza likawa zoezi gumu kidogo kwako lakini siku zinavyozidi kwenda utazoea na utamudu.
Sema hapana kwa dunia.
Ili uweze kufanikiwa unatakiwa uyajue makusudi yako vizuri yaliyokuleta duniani. Ukishajua hivyo, kataa kitu chochote ambacho unaona hakiendani na malengo yako hata kiwe kizuri sana.
Hapa inabidi ujue kusema hapana hata kwa fursa zote ambazo zipo nje ya makusudi yako. Ng’ang’ania kitu kile ambacho umekusudia kukifanya, acha kuyumbishwa na mtu au kitu.
Hivyo ndivyo unavyoweza kujifunza kusema hapana na kujenga misingi imara ya maisha unayotaka.
Badili maisha yako kwa kuwa na fikra sahihi, endelea kujifunza kupitia mtandao wako bora wa dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Chukua hatua na kila la kheri,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,


No comments :

Post a Comment