May 16, 2015
Huu Ndio Msingi Halisi Wa Mafanikio Unayoyatafuta.
Inaonekana tulio wengi tunadhani kwamba, watu wanaopata utajiri, ni wale ambao wanatengeneza fedha nyingi kwa mpigo au wale ambao wamerithi fedha kibao. Kuna ukweli ambao wengi hatuujui kuhusu jambo hili. Kwa kuangalia idadi ya watu ambao wametajirika kwa njia halali, tunaona wazi kwamba, wengi wamefikia hali hiyo kutokana na kuweka akiba kwa muda mrefu sana.
Mtaalamu mmoja wa uchumi wa
marekani, Ric Edelman, katika kitabu chake cha Ordinary people, Extraordinary Wealth anaonyesha kile kinachofanya
watu matajiri kuendelea kuwa matajiri. Anasema kitu hiki ni kule kuendelea kwa
watu hao kufanya mambo yaliyowafanya kuwa matajiri. Kinachowafanya watu maskini
nao kuendelea kuwa maskini ni kuendelea kufanya yale yaliyowafanya kuwa
maskini.
Huu ni ukweli mtupu, hasa
kama mtu hataangalia jambo hili kwa jicho la siasa. Kwenye siasa tunaambiwa
umaskini wetu ni matokeo ya wengine kupura raslimali, kujilimbikizia na
kutokujali. Huenda kuna ukweli, lakini mimi siyo mwanasiasa, hivyo sina vigezo
vya kuunga mkono au kukanusha nadharia hizo.
Ric Edelman anasema ,
umaskini ni dhana ya kwenye mawazo wakati kuishiwa ndiyo dhana ya mfukoni.
Unaweza kukabiliana na kuishiwa lakini ni vigumu kukabiliana na umaskini.
Kukabiliana na kuishiwa kunafanyika kwa njia moja tu, ya kufanya kazi kwa
bidii, kuweka akiba, kuweka tena akiba na tena na tena kwa muda mrefu. Baada ya
kufanya hivyo, itakuwa ni vigumu sana kwako kuweza kuishiwa.
SOMA; Kama Unafikiri Huna Akili Za Kutosha KupataMafanikio Katika Maisha Yako. Hakikisha Unasoma Hapa.
Lakini umaskini haukabiliki
kwa hivyo, kwani uko kwenye mawazo yako, ni hadi ukubali kutoka humo. Mtu ambaye
ana mawazo ya kimaskini hawezi kamwe kuweka akiba, kila anachopata, kiwe kidogo
au kikubwa, hukitumia chote. Anategemea kwamba, kuna siku itazuka kutoka pasipo
kujulikana bahati ya kupata fedha nyingi kwa mkupuo, ambapo atakuwa tajiri
mkubwa.
Kwa watanzania tulio wengi,
hayo ndiyo maradhi yetu, kuweka akiba kwa ajili ya kupata utajiri ni jambo
linaloonekana vituko mawazoni mwetu.
Hata wale waliofanikiwa wengi wao hawakuanza kuwekeza kwa mamilioni ya
fedha, bali fedha kidogo , wakawekeza tena mahali pengine na kupata kidogo na
baada ya miaka kumi hadi ishirini wakawa wamefanikiwa.
Hapa kwetu ukimwambia mtu
aweke akiba katika kile kidogo anachokipata ili baada ya miaka kumi au ishirini
awekeze mahali, atakutazama kuanzia juu hadi chini. Tumelelewa katika mfumo wa
kutaka leoleo, hatukujengewa msingi wa kujenga dhana thabiti ya kutunza kidogo
na kuwa na subira. Tunataka tupate hapohapo na kwa wingi.
Tumezoeshwa kuishi kwa njia
za mkato sana tangu tukiwa watoto
nyumbani, shuleni na ukubwani. Tunachofikiria ni nafsi ya kuiba, kupata rushwa
nzito au kudhulumu wengine ili tuwe matajiri kwa haraka sana.
Mtu ambaye anakushangaa
ukimwambia aweke akiba kidogokidogo ili baada ya miaka ishirini aje awekeze na
kuanza kuvuna, ukija kukutana naye baada ya hiyo miaka ishirini, utamhurumia.
Hali yake itakuwa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa hiyo miaka ishirini nyuma.
Kama utaweza kumkumbusha,
atajuta kwamba kama angejua angekusikia. Watu wa namna hii kazi yao ni kusema,
‘fulani tulikuwa naye juzijuzi hapa hapa,
analala chumba kimoja, lakini hivi sasa mambo yake mazuri sana.’ Miaka
ishirini kwake ni juzijuzi, lakini alishindwa kuutumia muda huo kwake kwa
kuuona ni milele.
Kuna wakati niliwahi
kukutana na kijana mmoja mfanyabiashara ya mikononi. Aliweza kunishawishi sana
hadi nikanunua kisagio(blender) alichokuwa akiuza. Nilivutiwa sana na uwezo
wake wa kushawishi. Nilimuuliza malengo yake ni nini hasa maishani? Alisema
anatamani sana kuja kuwa na duka kubwa la jumla.
Niliendelea kumuuliza tena
anachukua hatua zipi kuweza kufikia lengo lake na anatarajia ni baada ya muda
gani atakuwa amefanikiwa, alisema, ‘sijaanza
bado, nikipata fedha nyingi nitafungua, mwaka wowote mambo yakiwa safi, basi
nitafungua duka’.
Nilimhurumia sana lakini pia
niliwahurumia watanzania wenzangu wengi ambao naamini tunaishi kwa mkabala huo.
Nilimwambia kwamba, ni vizuri akawa na juhudi za makusudi za kuanza kuelekea
kwenye lengo lake na ni vizuri akajiwekea muda ambapo anaamini atakuwa amefikia
lengo lake.
Hebu fikiria kama wewe ndo
ungekuwa huyu kijana ama unafanya
biashara za mkononi, jiulize mwenyewe, una malengo gani, kutembea kutwa-kuchwa
kwa miaka mingapi? Lazima ulenge jambo, hata kama jambo hilo ni la kufanya biashara
ya mkononi maisha yako yote, basi uwe umelenga na kuamua, siyo ufanye tu kwa
sababu inabidi ufanye.
Namkubuka mwalimu wangu mmoja aliyenifundisha kipindi
cha nyuma wakati nikiwa shule ya msingi. Mwalimu huyu alikuwa akiandika kila
kitu ambachoangetarajia kukinunua kwa mwezi husika kabla ya mshahara. Nakumbuka
tulikuwa tukicheka sana tulipokuwa tukiziona karatasi zake za bajeti( tulikuwa
tunapata nafasi hiyo kwani tuliweza kuingia kwake tutakavyo, akiwa ni rafiki wa
familia yetu) . tulicheka kwa sababu tuliona ni kichekesho mtu kuandika hata
penseli ambayo atainunua na kuitumia mwezi ujayo.
Lakini nakumbuka pia nikiwa
kidato cha tano niliweza kuambiwa kuwa mwalimu yule kwa sasa amejenga nyumba
kubwa na ya kisasa kwao. Nilifurahi sana na kujifunza kwamba kuweka akiba ni
msingi halisi wa njia ya kuelekea kwenye kipato bila kujali unapato la kiwango
gani. Mwalimu wangu huyu aliweza kujenga kwa mshahara wa ualimu wa shule ya
msingi bila mkopo wa benki au taasisi yoyote ya fedha. Pamoja na kuwa ilichukua
zaidi ya miaka kumi, lakini lengo lake lilifikiwa.
Kuna walioko kwenye ualimu
kwa miaka thelathini ambao hawana viwanja, tena vijijini na pengine wansingizia
udogo wa mishahara wanayopata. Inawezekana, ikawa ni kweli kabisa mishahara
hairidhishi. Lakini kabla hatujakimbilia kwenye mishahara, tumewahi kujiuliza
kuhusu matumizi yetu na juhudi zetu katika kutaka kufanikiwa?
Mwalimu wangu yule hatajwi
tu kwa kuweka akiba, bali hata kwa kuamua kujifunza zaidi ili apande na pato
litune kidogo. Je, sisi tumefanya hivyo au tunatafuta ‘mchawi’ tu? Tusione
aibu. Hata kama tuko karibu na kustaafu, tukijiuliza kuhusu malengo yetu na
kuyabaini, tukaanza leo kuyafuata, tutamudu kufanikiwa. Kumbuka kufanikiwa ni
hatua isiyo na kikomo, siyo kituo.
Wengi mara tunatafuta
visingizio ni kwa nini inakuwa vigumu kwetu kuweka akiba. Tutasema matatizo ya
kifamilia, tutasema kulikuwa na mgonjwa, tutasema hatuna kipato cha kutosha,
tutasema mabadiliko ya kipato na mengine mengi tu. Lakini ukweli unabaki
palepale kwamba, kama tumeamua kuweka akiba, tutaweka tu, bila kujali ni
matukio yanatokea kwenye maisha yetu.
Kama tunaweza kuvaa, kupata
chakula, kulipa kodi ya nyumba na kumudu matumizi mengine , hata kama ni kwa
shida sana, tunaweza pia kuweka akiba kwa shida sana hivyohivyo, tukiamini
kwamba ni jambo muhimu kabisa. Lakini huwa tunashindwa kwa sababu akiba
tunaichukulia kama siyo kitu cha lazima sana katika maisha yetu. Kumbe kitu
pengine ambacho hujui, kuweka akiba huu
ndio msingi wa mafanikio halisi unayoyatafuta.
Kwa kuthibitisha hili kuna
akina mama hapa nchini ambao wamefungua biashara, kujenga nyumba kubwa,
kusomesha watoto na kufanya mengine ya maana kutokana na kuweka akiba kwenye michezo
yao inayofahamika kama ‘upatu’. Wameweza kufanya hivyo, kwa sababu akiba hii ni
ya lazima, ukishaingia itabidi ujinyime hata kula ili uweke, vinginevyo upate
matatizo hasa. Ukichukulia suala la akiba kama ni lazima, utamudu kuweka akiba
na kufanikiwa.
Nijuavyo mimi ni kwamba,
usingizie au usisingizie, bado kuweka akiba kutabaki kuwa muhimu sana katika
maisha yako. Ni wewe ambaye unatakiwa kuamua kuhusu hatma yako kimapato. Bila kujali
una kiasi gani cha kimapato au umri gani, naamini ili mradi unapata chochote
katika kutafuta kwako, unaweza kuweka akiba. Unachohitaji sio mamilioni, bali
uwezo wa kumudu kuwekeza kidogo mahali ili uzalishe na kupata nguvu ya kuweza
tena kuzalisha mahali pengine au kuongeza pale ulipowekeza kidogo.
Usidanganywe hata kidogo,
bila kuweka akiba ni kazi bure. Kuna watu ambao kazi yao ni kusema tu, fulani kapata
kwa sababu ya magendo au rushwa, kwa sababu hawajui ukweli. Mahali pasipo na
uwekaji wa akiba hakuna mavuno. Akiba ndio msingi pekee wa mafanikio yako hata
kama unaanzia chini kabisa.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, endelea kuwashirikisha wengine kutembelea
mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.