May 13, 2015
Kama Unafikiri Huna Akili Za Kutosha Kupata Mafanikio Katika Maisha Yako. Hakikisha Unasoma Hapa.
Kwa kawaida kila binadamu anapojaribu kufanya shughuli fulani akashindwa hutafuta sababu iliyomfanya ashindwe. Mara nyingine mtu huweza kuhisi kwa mawazo tu kuwa hawezi kufanya shughuli fulani kwa kuwa hana uwezo wa kutosha wa kiakili.
Je, wewe huwa unataka
kufanya shughuli fulani ya kuendeleza maisha yako lakini ukahisi kuwa huna
akili za kutosha kulifanya kwa usahihi hivyo ukaogopa na kuacha kulifanya?
Kama jibu lako ni ndiyo, sihisi
uko peke yako. Kuna watu wengi wanaokabiliwa na ugonjwa huu mkubwa ambao ni
sumu kubwa ya maendeleo ya binadamu na ambao kila mmoja wetu hana budi
kupambana nao.
Inakadiriwa kuwa karibu watu
asilimia 95 huwa wanafikiria kwa viwango mbalimbali kuwa wana upungufu wa akili
za kuwawezesha kufanikiwa katika maisha. Watu hawa mara nyingi huweza kujiona
ni wanyonge kwa kudhani hawawezi kitu tena katika maisha yao.
Kutokana na hisia hizi
potofu za kufikiri kuwa wana upungufu wa akili, kujiona hawawezi ama wanyonge
hii huweza kupelekea kudumaza uwezo wao kiakili na kufanya kushindwa
kukabiliana na mazingira ya maisha yenye changamoto nyingi.
Lakini mara nyingi huwa
wanashangaa wanapowaona watu wengine ambao wana hakika hawana uwezo wa kiakili
unaofikia ule wa kwao wanafanya kwa ufanisi shughuli ambazo wao walihisi
hawawezi kuzitenda hata kidogo.
Ni vyema tukumbuke kuwa
kilicho muhimu siyo kiwango gani cha akili ulichonacho bali ni jinsi
unavyozitumia akili ulizonazo. Fikra zinazoongoza akili yako ni muhimu zaidi
kuliko kiwango cha ubongo wako. Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kuulizwa na
mzazi, “Je, mwanangu anapaswa kuwa na
kiwango gani cha akili ili aweze kuwa mwanasayansi?”
Yule mtaalamu alimjibu mzazi
hivi, “ Mtoto wako hahitaji kuwa na akili za kupindukia, wala uwezo maalum wa
kukumbuka na wala sio lazima awe mtoto anayepata alama za juu sana masomoni.
Haya yote yanasaidia lakini lililo muhimu kuliko yote ni lazima awe na masafa
makubwa ya mvuto na upendo wahali ya juu katika sayansi.|”
Katika maisha mtu mwenye
imani, matumaini na hisia chanya katika uwezo wake wa kielimu na ambaye ana
kiwango cha akili cha IQ 100 ataweza kupata ajira bora, pesa nyingi, maisha
mazuri na hadhi ya juu katika jamii kuliko yule mwenye akili kiwango cha IQ 120
na mwenye hisia hasi katika uwezo wake wa akili na hulka ya kukata tamaa.
Nakumbuka mwaka fulani
nilikutana na rafiki yangu tuliyesoma naye zamani ambaye alikuwa na akili sana
na hata alifaulu vizuri kupindukia katika masomo yake chuo kikuu.
Nilikumbuka alipojiunga na
chuo kikuu aliamua kusomea shahada ya biashara kwa azima kuwa baada ya masomo
angefanya kazi kwa miaka michache na hatimaye kufungua kampuni ya biashara.
Wakati nilipokutana naye
ilikuwa imepita miaka zaidi ya kumi tokea alipomaliza chuo. Nilipomuuliza kama
alikuwa ameanza biashara alisikitika na kunieleza kwa unyonge kuwa aliogopa
kuingia katika biashara kwa kuwa aligundua uendeshaji wa biashara umebadilika
na kuwa mgumu sana.
Hivyo akahisi hana akili ya
kutosha kuendesha biashara, kwa ufanisi zaidi. Alitoa mfano wa changamoto
alizohisi zilihitaji uwezo mkubwa kuliko aliokuwa nao kama vile kuamua aina ya
biashara itakayofaa, jinsi ya kupata wateja, namna ya kupata mitaji kwa mikopo
ya benki yenye riba kubwa, makadirio ya faida na kodi ya mapato na vitu vingine
kadha wa kadha.
Aliendelea kunieleza kuwa
hata hivyo amestaajabu kuwa baadhi ya watu wengine aliosoma nao sekondari ambao
alijua hawana akili kama yeye, wameangia katika biashara na wamepata mafanikio
makubwa sana. Alisema kuwa wengine ni wale aliosoma nao chuo kikuu lakini
hawakuweza kufuzu.
Ni kitu ambacho hata wewe
unaweza ukajiuliza kwanini baadhi ya wasomi hawapati ufanisi katika maisha?
Ingawa sio rahisi pia kuamini kuwa baadhi ya wasomi hushindwa kupiga hatua ya kujipambanua
katika maisha utafiti ndivyo umethibitisha kuwa huu ni ukweli mtupu.
Unaweza ukakuta mtu ni msomo
mzuri tu kabisa, pengine mwenye ufaulu mzuri alioupata pindi akiwepo darasani.
Pamoja na akili zote hizo sio ajabu kumkuta mtu kama huyu akiwa na maisha
ambayo hayana maendeleo ya kutosha kulingana na elimu yake, hii yote inatokana
na mtu kujiona hana akili za kutosha kuambana na maisha mpaka kufanikiwa.
Ni muhimu sana kwako
kufikiria sasa kwa mtazamo chanya zaidi ili kuweza kuachana na hali uliyonayo
inayokufanya uweze kujiaminisha mwenyewe kuwa eti huwezi kufikia mafanikio kwa
sababu huna akili za kutosha kuweza kufanya hivyo. Kila mtu anauwezo wa kufanya
chochote kile akitakacho.
Jifunze na achana kujaza
ubongo wako vitu vingi visivyoweza kukusaidia. Tumia ubongo wako kufikiria vitu
vitakavyoweza kubadili maisha yako badala ya kuutumia ubongo wako kama ghala ya
kuhifadhi mambo mbalimbali. Na muhimu zaidi ni kuweza kuepukana na hisia kuwa
huna akili za kukwezesha kupata mafanikio makubwa kaika maisha yako.
Tunakutakia kila la kheri
katika safari yako ya mafanikio, ansante sana kwa kuwa msomaji mzuri wa mtandao
huu wa DIRA YA MAFANIKIO na karibu sana kujifunza zaidi.
DAIMA
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713 048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.